Monday, March 23, 2009

HIVI SISI TUMELISHWA NINI?

Tumegeuka taifa la wachuuzi

Nimesoma kwa makini mjadala uliowekwa na dada Yasinta uliokuwa na kichwa cha habari kisemacho MISHAHARA HAITOSHI TUACHE UZEMBE KAZINI Mjadala huo umezua maswali mengi kuliko majibu hasa kutokana na maoni ya mchangiaji wa kwanza mwanablog na mwanautambuzi Kamala kuja na hoja ya kupinga kile kilichosemwa na Yasinta, ambaye hata yeye amekiri kuwa mjadala huo aliutoa kwa Profesa Mbele aliyeuweka pale kibarazani kwake, baada ya kuwa umemvutia sana.

Mimi naamini kuwa kila mtu anayo haki ya kuzungumza kile anachokiamini ilimradi kusiwe na kuvunjiana heshima na kukashifiana, kama alivyowahi kusema kaka Bwaya wakati fulani kuwa kutofautiana ndio kujifunza. Kilichonishangaza ni kuona mjadala huu umeanza kupogoka na kupoteza mwelekeo kwa baadhi ya wachangiaji kushambuliana bila kujenga hoja.

Nimevutiwa sana na maoni ya kaka Mubelwa, kaka Bwaya na Profesa Mbele, Maoni yao yamedhihirisha kuwa ni watu waliokomaa hasa katika kujenga hoja na kuheshimu maoni ya wengine.

Hivi kuna tatizo gani kuiga yale ya wenzetu yanayoweza kutufaa kuharakisha ukuaji wa uchumi hapa nchini? Mimi siamini kuwa hilo ni tatizo.

Ikumbukwe kwamba sheria inayozungumziwa, inatekelezwa katika nchi ambazo zimeshaendelea na zimepiga hatua kubwa sana kimaendendeleo. Hizi ni nchi ambazo tunazipigia magoti kuomba misaada mbalimbali ya kijamii. Je kuna tatizo gani kuwaiga kwa ustawi wa maisha yetu wenyewe?

Nchi zote duniani ambazo watu wake wanamaisha bora, hazikupata mafanikio hayo kwa kutegemea wafadhili au kusubiri wawekezaji kutoka nje ili wananchi wake wageuzwe vibarua kwenye ardhi yao wenyewe.
Nchi hizo zimeweza kufika hapo zilipofikia kwa sababu wananchi wake waliamua kufanya kazi. Kila mtu alizalisha na mwisho wa siku kukawa na ziada.

Iwapo nguvu kazi katika jamii haitatumika ipasavyo, ina maana kwamba watu wachache watazalisha kwa ajili ya wale wavivu wasiozalisha. Ni vigumu nchi kujiletea maendeleo.
Inaonekana mawazo yetu wote yamefungiwa mahali, kiasi kwamba tumefika mwisho wa kufikiri kwetu. Hivi bado tunaendelea kujidanganya kuwa tutapiga hatua katika kujiletea maendeleo?

Maendeleo gani hayo tunayozungumzia, ikiwa tu kupendekeza kuhusu watu kukatwa mishahara wakichelewa makazini au kusingizia kuwa wanaumwa kunazua mjadala mkubwa mpaka watu kutishiana kutoana macho. Wanaotetea wananufaika na nini?
Hivi mnadhani ni kitu gani kilichopelekea yule mkuu wa wilaya kule Bukoba kuwacharaza waalimu bakora? Si haya yanayosemwa? Eti watu wanalipwa mishahara midogo. Sasa hiyo ndiyo ihalalishe watu kuwa wazembe?

Hata katika vitabu vya dini imesisitizwa sana kwamba kila mtu afanye kazi, katika Korani, kitabu cha kiislamu ipo aya inasema, “ Mkimaliza kuswali mtawanyike katika uso wa dunia ili kujitafutia ridhki” haikusemwa watu wakakae vijiweni na kupiga soga, na katika Biblia kuna andiko linasema “Asiyefanya kazi na asile chakula”

Kila mtu anapaswa kufanya kazi na kulipwa ujira kulingana na kazi yake, na kuna haja ya kutungwa sheria kali itakayomlazimu kila mtu kufanya kazi.
Kuna kundi kubwa la vijana limekaa bila kufanya kazi kutwa kwenye vituo vya mabasi wakivizia kuibia watu. Nguvu kazi inapotea bure, halafu tunapiga kelele kuwa kuwa nchi hii ni masikini. Mimi nasema umasikini uko vichwani mwetu, tukiweza kuuondoa, maendeleo ya uchumi yataonekana haraka sana.

Tusipotumia nguvu kazi yetu kwa kiwango chetu cha mwisho, tutakuwa tunapoteza muda bure, na tutaendelea kuwa watumwa wa wenzetu hadi mwisho.

4 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

koerooooooooooooooooooooo

natamani nikae kimya nisikilize wengine wanasemaje lakini natekenyeka kidogo na fikra mgando zetu kidogooo.

hivi maendeleo nini ni? magari, majengo, majumba, wake/waume, nguo au ninini hii maendleo mnaypitafuta na iko wapi? mbona manabii walikufa masikini kabisaaaa?

kwa nini tuige wazungu kwani wao wameishia wapi sasa na maendeleo yao? labda nisome kwenye blog yangu hapa;http://kamalaluta.blogspot.com/2009/03/dini-usomi-na-kupotea-kwa-binadamu-wa.html

kwani wazungu wanaisaidia afrika kweli?
kwani unadhani nchi hizo unazodhani zimeendelea zilifnaya tu kazi? au unafikiri umasikini wa afrika ni wa waafrika? kwani afrika illiwahi kuwa masikini?

hivyo vitabu vya dini sasa sivielewi lakini kumbuka viliandikwa na watu pia kama wewe, yasinta au mbele.

sina swali la ziada mheshimiwa koero

ERNEST B. MAKULILO said...

Habari Da Koero,
Nimekutana na mjadala huu kwa mara ya pili, ambapo debate ilikua hii hii ya masuala la mshahara kutosha au kutokutosha.Katika mada hiyo ndipo ilipoibuka hoja ya Kufanya kazi kwa bidii kama njia ya maendeleo, ambayo ni hoja yako ya msingi.

Naanza kwa kukubaliana na hoja za msingi na Ndugu Kamala na hoja yake ya kuwa "misaada" kutoka nchi zilizoendelea si misaada ya kweli, Afrika haisaidiwi.Nakubaliana naye kwa kuwa kinacholetwa Afrika madhara yake ni makubwa mno kwa sasa na baadaye.Ni sawa na mwanaume mwenye virusi vya UKIMWI amtongoze mwanamke ambaye ni mzima wa afya, hajaathirika..na kwa kwa kuwa huyo dada ana shida na hela, na kwa ukweli anatambua kuwa huyu mwanaume ana virusi vya ukimwi, basi mwanaume huyu anataka 'kumsaidia" dada huyu kwa kufanya naye ngono bila hata ya kondom na kumpatia milioni kumi za mtaji.Swali la kujiuliza, je kupewa milioni kumi na kuachiwa ukimwi ni kusaidiwa?Kama huku ni kusaidiwa kuachiwa janga kubwa la namna hii, basi Afrika inasaidiwa, na kama si kusaidiwa basi Afrika haisaidiwi.

Tukija katika hoja ya kufanya kazi kwa bidii.Nakubaliana na wewe kwa hoja kuwa unapofanya kazi kwa bidii inalipa, HARDWORK PAYS. Lakini nakuja kukubaliana tena na Ndugu Kamala kuwa si kazi bidii ndio kulipa kwa kitu.Maana yake ni nini, ukiondokana na theories za development ambazo ndio hizo nyingi zinasema watu wafanye kazi kwa bidii nk, ukija ktk practice, uhalisia wa ukweli ktk nchi zinzoendelea unaweza kufanya kazi kwa bidii na mateso yapo pale pale.Mfano, wanachuo wengi waliomaliza vyuo walipangiwa ualimu kufundisha...tangu wapangiwe mwaka jana mwezi wa nane, hadi leo hii hawajapewa hata senti tano na serikali kama malipo ya kuanza kazi yaani kujikimu, mshahara hata mmoja hawajalipwa.Sasa unaposema kazi kwa bidii tu ndio suluhisho unaangalia mambo mengine kama haya??Wakati mwalimu hajalipwa tangu mwaka jana mwezi wa nane hadi leo, huku marupurupu ya mbunge mmoja kwa siku akikaa bungeni ni sawa na mshahara wa mwalimu kwa mwezi mmoja., je Wabunge ndio wanaofanya kazi kwa bidii sana?Maana asiyefanya kazi asile, na anayefanya kazi kwa bidii sana analipwa kutokana na bidii yake, je wabunge wangapi umeshawahi kuwasikia wakiongea??Kwa miaka mitatu, Makamba kaisha ongea mara moja, nayo ni kusifikia Kikwete tu na hapo anakula marupurupu kibao.Kazi yake kwa bidii na juhudi iko wapi??

Suala la mshahara mdogo ni kweli wandugu.Mshahara wa daktari mwenye degree aliyesoma miaka mitano unalingana na secretary au mfagizi wa TRA, kweli hapo kuna usawa?Mshahara wa mwalimu mwenye degree ukikata makato yake yote unabaki shilingi laki 270, je mtyu huyo ana mke, watoto wawili, na extended family lazima aisaidie, ndugu maisha yetu.Ataishi vipi kwa hela hiyo kwa mwezi??

Mambo mengine ni ya serikali na sera zake.Mfano ukiangalia gharama za internet Tanzania ni za juu mno, hivyo mtu unajikuta una kuwa limited in terms of opportunities.Maana kuna mambo mengine hutokea ktk internet pekee na sio magazeti ya bongo, sasa unadhani bidii itakuaje uweze kupata hiyo reward?/Mfano, Kigoma internet access ukienda cafe ni sh.500 kwa dakika 15 na iko very slow.Kusoma e-mails tu hutomaliza, muda huo nao umekwishia.Unadhani juhudi zitasaidia?Kuna mengi beyond juhudi.Juhudi inatakiwa tuizungumzie pale watu mpo ktk level of playing ground.Mfano Machenster Utd wakicheza na Liverpool., na sio Liverpool icheze na Ujiji United uanze kuleta mambo ya juhudi tena, watu hawako ktk level.Au ni sawa useme Chadema itoe ushindani thabiti kwa CCM...CCM ina resources kibao mno, za haki na wizi, hivyo hata juhudi zifanywaje bado ni ngumu.Angalia juhudi za Dr.Slaa, Dr.Rashid, Zitto nk huko bungeni...ikifika kupiga kura, CCM yote inasapoti sera ya chama chake.Kazi kwa bidii inategemeana na mazingira unayokutana nayo.

MAKULILO Jr,
www.makulilo.blogspot.com

Koero Mkundi said...

Kaka Makulilo.

Nakusalimia huko uliko.

Ahsante sana kwa kunitembelea na kutuelimisha.
nakubaliana na wewe kwa mtazamo wako na pia nakubaliana na Kamala kwa mtazamo wake.

Lengo langu lilikuwa ni kuweka ule mjadala katika hali ya kukosoana bila kujeruhiana kwa maneno ya kuzodoana.

Binafsi niliona kama mjadala ule unatoka nje ya mstari na ndio sababu nikaona nijaribu kuweka mtazamo wangu.

Nakubali kuwa kuna dhulma nyingi katika nchi hii, lakini hebu tujiulize mimi na wewe, Je hiyo inahalalisha uzembe na kutokufanya kazi?

Hivi ni nani anawachagua hawa viongozi tulio nao leo tena kwa kura za kishindo?

Kwangu mimi, naona hii ni changamoto kwa jamii, kukaa na kujiuliza, hali hii mapaka lini?

Je kuna haja ya kuendelea kukumbatia uozo huu ambao hauna manufaa kwetu na badala yake unatuumiza?

Bado nasisitiza kuwa kuna haja ya jamii kubadilika na kufanya kazi, tena kwa bidii, ili kujiletea maendeleo na kama ni swala la serikali kutokuweka sera zitakazolinda maslahi ya wananchi wake basi mwaka 2010 sio mbali, tuwaondoe.

Watu wa Musoma wametuonesha kuwa inawezekana, isiishie huko, kama wote tukiamua na kusema basi inatosha, hakika inawezekana.

Iko wapi ile serikali ya Mexico iliyotawala kwa miongo kadhaa, wanasiasa makini wa nchi ile waliona udhaifu huo wakaanzisha Operation Sangara yao na hatimaye kile chama kikang'olewa.

kama iliwezekana kule hata hapa inawezekana.
Lakini bado nasisitiza kuwa tufanye kazi na tuache uvivu na visingizio.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kazi kuilaumu serikali utafikiri wewe sio sehemu ya serikali. naomba majibu ya maswali ili mada inoge zaidi labda.

ukimtembelea yasinta, evarist kajibu vizuri kule!

makuliro kasaidia labda

ukiongelea uzembe, sijui nani mzembe. hivi uliwahi kumona tajiri kama mengi akiwa bize sehemu? kwani wanye mali wanafanyaga kazi? walaumuni pia