Thursday, April 9, 2009

AMADOU NA MARIAM: WAO WAMEWEZAJE?

Pamoja na kwamba ni walemavu wa kuona lakini wameweza.

Ni katika viunga vya Bamako nchini Mali ndipo historia ya wanamuziki hawa wawili vipofu, mtu na mkewe ilipoanzia na kusambaa, kuanzia kule nchini Burkina fasso, Ivory Coast, Asia, Ulaya na America.
Wanamuziki hawa ni Amadou na Mariam ambao ambao wanazidi kuishangaza dunia kutokana na umahiri wao kimuziki.
Historia inaonesha kwamba wanamuziki hawa, Amadou Bagayoko ambaye ni mpiga gita na mwimbaji, aliyezaliwa mwaka 1954, katika jiji la Bamako nchini Mali na
Mariam Doumbia ambaye ni mwimbaji mahiri aliyezaliwa mwaka 1958, walikutana katika chuo cha vijana wasioona, wakiwa wanafundishwa stadi mbalimbali za maisha ambapo walijikuta wote wakiwa na kipaji cha muziki.

Mnamo mwaka 1974, Amadou alianza kupiga muziki na bendi ya Les Ambassedous Du Hotel.

Kufikia mwaka 1980, Amadou alioana na Mariam na wakati huo huo walianzisha bendi yao wenyewe pamoja na chuo cha kufundishia muziki kwa wale wasioona.

Hadi kufikia mwaka 1985 wanandoa hawa walikuwa wamejijengea umaarufu mkubwa kwa muziki wao wa Blues wenye vionjo vya gitaa Rock, mirindimo ya Violin yenye asili ya Syria na vyombo mbali mbali vya muziki vyenye asili ya Cuba, Misri, Columbia na India. Vyombo vyote hivyo kwa ujumla wake vilileta ladha ya muziki wa Afro Blues.

Ziara yao ya kwanza, nje ya Mali ilikuwa ni ile ya kitembelea Burkina Fasso mwaka 1986, na baadae Ivory Coast ambapo walikaa kwa miaka 7 na kufanikiwa kurekodi kaseti zipatazo 5.

Kaseti hizo ziliuzwa sana na kuwajengea umaarufu Afrika Magharibi na hivyo kupata wafadhili ambao waliwapeleka nchini Ufaransa kurekodi santuri ambayo iliwatangaza dunia nzima na kuwafanya kupata mialiko ya kwenda kutumbuiza kwenye matamasha mbali mbali ya muziki duniani.

Mnamo mwaka 2003 wanamuziki hawa walikutana na mwanamuziki maarufu wa Kilatini Manu Chao ambaye aliwasaidia kutengeneza santuri yao maarufu ya Dinanche a Bamako ikiwa na maana ya Jumapili ndani ya Bamako ambayo nayo iliuzwa sana.

Wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani, wanamuziki hawa kwa kushirikiana na mwanmuziki wa Ujerumani Herbert Gronermeyer walirikodi wimbo maalum wa kombe la dunia ambao ulishika namba moja katika vituo vya Redio vya

Ujerumani na hivyo kuzidi kujijengea umaarufu mkubwa katika maisha yao ya muziki. Wanamuziki hawa wamefanikiwa kutoa santuri 7 ambazo zote zimewaletea mafanikio makubwa.

Ukweli nikwamba wamepitia katika mazingira magumu kwa kiasi fulani hadi kufikia katika kilele cha mafanikio waliyo nayo sasa. Kuna wakati iliwalazimu kuhamia Ivory Coast ili kutafuta soko la muziki wao.

Katika mahojiano waliofanyiwa hivi karibuni walikiri kwamba, chuo cha vijana wasioona walichosomea ndio chanzo cha wao kufahamiana na kuibua vipaji walivyonavyo katika muziki.

Walisema kwamba hiyo ndio iliyosababisha wao kuanzisha chuo chao cha kuwafundisha vijana wasioona muziki.

Hii inadhihirisha kwamba ni kwa kiasi gani wenzetu waliona umuhimu wa kuwawezesha watu wenye ulemavu, hasa wenye ulemavu wa kuona.

Sasa hivi kuna vijana wengi walemavu wanaozurura hovyo mitaani nchini kwetu na hata wengine kufikia kuwa ombaomba kwa sababu hawakufundishwa staidi za maisha na wala hawakuandaliwa mazingira mazuri ya kujiajiri.

Ukweli ni kwamba tunavyo vyuo vichache sana vinavyofundisha staidi za maisha kwa watu wenye ulemavu ambavyo vingi vinamilikiwa na taasisi za kidini, Idadi ya vyuo hivi hailingani na idadi ya walemavu walioko hapa nchini.

Katika karne hii ya sayansi na teknolojia ilitakiwa ile dhana ya kuona kwamba ni mkosi kuzaliwa mtoto mlemavu katika familia iwe imefutika, kwa sababu siku hizi kuna nyenzo nyingi zilizogunduliwa ambazo ni rahisi kutumiwa na walemavu katika kuzalisha mali na kuchangia pato la taifa, badala ya kuiacha nguvu kazi hii kupotea bure.

Amadou na Mariam licha ya kuwa ni walemavu wasioona wametoa ajira nyingi kwa vijana wa nchini Mali kupitia muziki wao.

Hata hapa nchini kwetu, iwapo serikali itafungua vyuo vingi kwa ajili ya walemavu ili wafundishwe staidi za maisha na kuandaliwa mazingira mazuri ya kujiajiri, kuna uwezekano mkubwa wa kuibua vipaji na kupunguza ukali wa maisha kwa ndugu zetu hawa wenye ulemavu.

Si vyema watu hawa wakipuuzwa kwani kila mtu ni mlemavu mtarajiwa, hujafa hujaumbika.

1 comment:

Mzee wa Changamoto said...

Swali zuri Da Koero. Walichofanya ni kutumia pale walipowezeshwa. Watu wenye ulmavu kama huu wa kuona huwa wanawekeza akili na mawazo yao katika kile wajuacho na ndio maana wakifunzwa huwa na matokeo mazuri ama niseme hufanya vema katika kile wafunzwacho. Kuhusu serikali na viongozi wa nyumbani naona suala moja. Kuwa wengi wao (na hapa nasema wengi na si wote) wanatumia matatizo ya wananchi kupata kura na kisha wanatumia nafasi zao kwa mambo makubwa mawili. Kujinufaisha na kuandaa mazingira mazuri ya kuchaguliwa tena. Lakini huu ndio ulitakiwa kuwa wakati wa kufanya kile wanachotakiwa kufanya ambacho ni kuwawezesha wenye uhitaji ambao hii ni haki yao (sio kusaidiwa).
Lakini na viongozi wa VYAMA hivi wanahitaji kuweka unazi pembeni na kuwatetea wanaowaongoza. Wanatakiwa kuhakikisha kabla ya uchaguzi wameainisha ni yapi mahitaji ya wanachama wao na kisha kuyawakilisha kwa kila mgombea kuona ni yupi mwenye majibu ya matatizo yao, kisha wahakikishe wanafuatilia baada ya kiongozi huyo kuingia madarakani