Thursday, May 14, 2009

MIAKA 30 BADO TUMEFUNGA MIKANDA!

Eti vita vya kumng'oa huyu jamaa ndio vinatutesa mpaka leo!

Juzi katika pekua pekua yangu katika maktaba ya Mzee Mkundi, nikakutana na Gazeti moja la Zamaani sana, ukilinganisha na umri wangu lakini, linaitwa Mzalendo.
Ni gazeti la mwaka 1979.
Kweli baba yangu alikuwa ni mtunzaji, maana gazeti lenyewe ukiliona bado lina hali nzuri tu na linavutia kulisoma.
Basi katika mojawapo ya habari iliyonivutia ni ile ya Aliyekuwa Rais wa kwanza wan chi hii Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aka Mzeee wa Mwitongo.
Ukweli ni kwamba nampenda sana huyu mzee. Huwa sikosi kusikiliza zile hotuba zake za alfajiri kupitia TBC1.

Hotuba hiyo ilikuwa ni ya kututaka sisi Watanzania tufunge mikanda kwa muda wa miezi 18, ili serikali iweze kurekebisha uchumi baada ya vile vita va Kagera.
Wakati wa Vita hivyo mimi nilikuwa sijazaliwa, na hata wakati hotuba hiyo ya kulihutubia taifa ikitolewa nilikuwa sijazaliwa pia, lakini kinachonifurahisha ni kwamba, kama kuna kitu ambacho kitakuja kutuhukumu basi ni maandishi, maana kauli inaweza kupingwa lakini maandishi, ni vigumu sana.

Haya Kiranja wa wakati huo Mwalimu nyerere kwa unyenyekevu kabisa akawaambia watanzania, “Jamaniee tunawaomba mfunge mikanda maana vita hii imetufilisi, na baada ya miezi 18, mutaifungua hiyo mikanda”
Ni kauli ambayo mzee yule aliitoa kwa unyeyekevu kabisa na kutokana na Imani waliokuwa nayo Watanzania kwake yeye watu, wakjifunga mikanda.

Lakini la kushngaza mpaka leo takribani miaka 30 tangu vita ile iishe bado asilimia kubwa ya Watanzania tumefunga mikanda huku wengine wakiwa wameilegeza na kuongeza Papi ili iwe kubwa zaidi.
Hali inazidi kuwa ngumu, kila kukicha, asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi katika ulitima wakishindia mlo mmoja kwa siku, na pengo kati ya mwenye nacho na asiye nacho linazidi kukua.

Juzi nimeenda kununua Dola kwenye duka la kubadilishia fedha pale Posta, nimekuta Dola inazidi kupaa, hadi jana dola moja imefikia kuuzwa kwa shilingi 1330! Sijui wachumi wetu hapa watatueleza nini?
Ukisikiliza Hotuba za kisiasa na takwimu zao zisizo na mshiko utacheka, utawasikia “Uchumi wetu unapanda kwa asilimia 0.0000001” sasa hii inamnufaisha nani?
Wakati tunapolilia kupunguziwa bei tunapofanya manunuzi, wengine wananunua bila hata kuuliza bei.

Mwalimu Nyerere alikuwa na vision, ingawa kuna wakati alifanya makosa, na hilo aliwahi kulikiri, pale aliposema, haiwezekani akae miaka 23 Ikuli halafu asifanye makosa, ni lazima atakuwa alifanya makosa kama binadamu kwani hakuw malaika. Lakini aliwalaumu viongozi wetu wa leo kuwa badala ya kuchukuwa yale mazuri aliyoyaacha wao wanachukuwa mabaya na kuyatupa mazuri, akili gani hii!

Wakati tunapata Uhuru Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, ili tuendelee, yaani tuondokane na umasikini , tunahitaji mambo makuu matatu,
1.Watu
3.Ardhi
4.Siasa safi na uongozi bora.


Kwa upande wa watu, wapo wa kutosha kabisa na tena ikiwezekana tuongezeke zaidi, kwa mujibu wa takwimu ya hivi karibuni tuko milioni 38,
Ardhi nayo iko ya kutosha, naambiwa kuwa karibu asilimia 60 ya ardhi ya nchi hii haijatumika inavyopaswa,
Kwenye siasa safi na uongozi bora, hapa ndio nina shaka napo, Mwalimu nyerere aliona kwamba ili tuwe na siasa safi ni lazima viongozi wawe waadilifu na hakutaka hilo liwe ni jambo la kupita, na ndio sababu mwaka 1967 wakakutana kule Arusha na kututangazia Azimio la Arusha.

Mwalimu alikuwa akililinda na kulitekeleza Azimio la Arusha kwa vitendo na ndio sababu alikufa akiwa ni mtu wa kawaida sana, akiwa amejikita kule Butiama Mwitongo akijilimia.
Alipong’atuka katika uongozi wa nchi hii, kama alivyowahi kusema mwenyewe, viongozi wetu wakutana kule Visiwani Zanzibar na kulivunja Azimio la Arusha, bila hata kuwatangazia Watanzania na waliporudi, kimya kimya wakaanza kujilimbikizia ukwasi kwa kufuru.

Kutokana na kuvunjwa kwa Azimio la arusha ndio maana sasa tunashuhuidia kashfa kama za EPA, Kiwira, Richmond, Dowans, Maliasili, TRA, na nyingine nyingi tu.

Mimi ni msomaji wa Biblia kidogo, katika Wagalatia kuna mahali Mtume Paul aliwambia wagalatia, nitanukuu “Enyi wagalatia, hivi ni nani aliyewaloga ninyi?, nami labda niulize, hivi sisi Watanzania ni nani aliyetuloga?
Nadhani Mchawi aliyetuloga alishakufa zamaaani….

8 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Kufa kwa mchawi si tatizo Dada. Tatizo ni kwamba alikufa a waliohudhuria mazishi wpte wamepoteza kumbukumbu. Kwa hiyo hata kaburi la kutambikia na kufanyizia madubwana ya kuturejeshea uhalali wetu hatulijui.
Ntarejea

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

yes binti.

tatizo ni nyerere au sisi? wewe unauliza nani aliyetulogo? mimi sijalogwa wala kujiloga na waliojaribu kuniloga woote nimewashinda na wanajuuuuuta kunifahaaamu!.

unaweza kushangaa kwa nini nyerere alitumia pesa lukuki kumng'oa amini aliyekuwa akidai eneo dogo ambalo wakazi wake woote wanaongea kiganda.

hivi kama amini angechukua eneo lile, tungeapata hara gani? wengine hudai angetaka zaidi na zaidi, ndio sisi tungepoteza nini? hata idd amini angedai tanzania nzima,wewe nami tungepoteza nini? si tungeenndelea kuishi tu na kuwepo? ila nyerere angeupoteza 'unyerere' (urais) wake na hivyo tulipigana ili kulinda urais wa nyerere! kwani Tanzania ililumbwa na Mungu? hapana na wakoloni tu, kwa hiyo nyyerere aliheshimu mipaka ya wakoloni isitenguliwe, alikuwa tayari kuuwa hata watu wa mwenyezi mungu lakini mipaka ya wakoloni iwe vilevile. kwani wakoloni walimshirikisha nyerere kutenga mipaka hiyo? hapana.

tatizo letu ni unyerere wake

chib said...

Mchawi wa Tanzania ni watanzania wenyewe!

Hi from Kigali, Rwanda

Unknown said...

Dada Koero, pole sana kwa machungu ulokuwa nayo. Kumbuka unahusika na hayo yanayotokea. Ulishiriki kwa namna moja ama nyingine katika kuyasababisha hay. Hata kama Kamala hauoni ukweli huo na kuendelea kulaumu unyerere ambao uko kwako pia (si umesema kuwa unazizimia hotuba zake?).

Nakubaliana na Chib kuwa wachawi ni siye wenyewe Nadhani unajua kuwa hapa duniani ikiwamo Tanzania watu wengi wanapigia kelele kuwa UMALAYA ni kitu kibaya sana. Wajua vema kuwa malaya anayeuza mwili wake hahongwi chini ya 1000 hata kule kwenye madanguro ya Uwanja wa fisi na mwananyamala kwani bao moja ni alfu. Sasa WaTz wengi zaidi ya asilimia 99 ni wabaya kuliko malaya. wanakubali kuhongwa fulana, kanga, vitenge, sukari, chumvi, na kofia ambavyo thamani yake ni kama sh 12,500. Ukiigawa kwa muda wa miaka mitano mheshimiwa atakapokuwa madarakani yaani siku 1825 utaona kuwa Koero wewe umehongwa sh 7 kwa siku!!!!! Je wewe si mbaya kuliko Malaya?

Nimalizie kwa usemi wa mwanafalsafa mmoja alosema...'kiongozi ni kioo cha jamii. Kama kiongozi ni mbaya basi wale walomchagua ni wabaya zaidi kuliko yeye kwani waliona yeye ni afadhali afadhali kuliko wao'. Kwa hiyo hata wananchi wa kawaida wanaopiga kelele kuhusu ufisadi wakati nawaona wamevaa t-sheti za maisha bora kwa kila mTz nawashangaa saana. Kama hukulamba sukari walau umevaa tisheti, si ndio Koero?

Halafu mwambie Kamala akome kumbugudhi babu yake Nyerere, amwache apumzike kwa amani!!!

Samahani kwa kuhubiri japo upadre ulinishindaga!!!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

sijui kama nauzimikia ule mz*ga wa butiama ila napingana nao sana. nkubali mzee umelonga kweli

Mwanasosholojia said...

Jamani makamarade! Kulikoni ndugu zangu? Mnaanza cheza rede, Kusawili nchi yangu,
Mpaka Nyerere Kamarade, Mwamchamba babu yangu!
Aah jamani wapendwa, punguzeni uchambaji!

Matatizo ya Tanzania, ni ya kihistoria sikia
Kabla ya ukolonia, Maisha yalikuwa sawia
Watu walijivunia, Kuishi kwa usawa
Aah jamani wapendwa, punguzeni uchambaji!

Walipoingia wakoloni, wakavuruga kinoma
Wakanyonya bila soni, huku wakijinoma
Hawakuondoka nchini, wapita mlango wa nyuma
Aah jamani wapendwa, punguzeni uchambaji!

Nyerere hana kosa, alifanya aloweza
Wenzake walimtosa, huku wakimbeza
Akaona jitakasa, kuacha ngoma kucheza
Aah jamani wapendwa, punguzeni uchambaji!

Walopewa usukani,wakaanza kuvuruga
Wakabanwa na wakoloni, nchi kuivuruga
Wakaweka vibindoni,katika wetu uga
Aah jamani wapendwa, punguzeni uchambaji!

Dawa yake ni moja,kuuvunja mfumo
Lawezekana kwa umoja, na pia msukumo
Hamasisha kila mmoja,tumia mungurumo
Ipo siku iso jina,walala hoi tutashinda!

Christian Bwaya said...

Tatizo la nchi yetu linasababishwa na wewe unayesoma sentensi hizi sasa hivi. Hakuna mwingine. Ukitaka kuamini, anza sasa.

mzee wa matukiodaima habari bila uoga said...

Hapa sina neno