Saturday, May 30, 2009

KOERO SAFARINI!!!!!

Kwa herini ya kuonana........
Kwa wanablog wenzangu na wasomaji wa blog hii ya VUKANI.

Kwa masikitiko makubwa napenda kuwafahamisha kuwa sitakuwepo mtandaoni kwa muda usiojulikana kutokana na kuwa safarini.

Ingawa ninapokwenda kuna mtandao lakini majukumua yanayonipeleka huko nadhani yatanichukulia muda mwingi, kwa hiyo ninayo matumaini hafifu ya kuonekana mtandaoni.

Kama nitapata nafasi basi naweza kupita japo siku moja moja hapa VUKANI kuwasalimia na kuwajulia hali pia nitakuwa nikiwatembelea wanablog wenzangu kama nitapata nafasi ili kupata habari, hekima na ujinga kidogo.

Nawatakia kila la heri na mungu akipenda tutaonana wakati ujaooooooo

Thursday, May 28, 2009

HEKAYA ZA BIBI KOERO!!!

UKISHANGAA YA MUSA

Hivi mnakijua kisa cha huu msemo wa “ukishangaa ya Musa utakutana na ya Firauni?
Basi leo ngoja niwasimulie kisa hiki ambacho nilisimuliwa na Bibi Koero nilipoenda kumsalimia mwaka juzi.

Kisa chenyewe sina uhakika kama ni kisa cha kweli au ni hadithi ya kusadikika na hekaya za bibi Koero katika kutoa mafundisho kwa wajukuu zake, si unajua jinsi bibi zetu walivyojaaliwa hekima kwa kutoa mafunzo kwa wajukuu zao kwa njia ya mafumbo misemo na hadithi za kufikirika ambazo zimejaa nahau na mafunzo.

Haya ungana na mimi katika simulizi za kisa hiki……

Hapo zamani sana enzi za himaya ya Firauni (Farao) kulikuwa na mivutano ya kimamlaka kati yake na Musa.(Yule Musa anyesimuliwa katika Biblia, aliyewatoa wana wa Israel kule utumwani Misri na kuwapeleka katika nchi ya ahadi)
Firauni alikuwa akishidana na Musa ambaye alikuwa akiongozwa na Mungu.
Basi ilikuwa ni kawaida watu kwenda kwa Firauni kupeleka mashauri yao inapotokea kutofautiana.
Firauni alikuwa akitolea maamuzi mashauri hayo, ambapo maamuzi yake mengi hayakuwa na haki na yalijaa utata mtupu. Lakini ikatokea baadhi ya watu wakawa hawaendi tena kwa Firauni kwa kuwa walipoteza imani kwake na badala yake wakawa wanaenda kwa Musa ambaye alikuwa akisifika sana kwa kutoa maamuzi ya haki na yaliyokubalika na pande mbili.

Basi ilitokea mtu mmoja alikuwa akisafiri kwa miguu, kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine, na kama unavyojua zamani kulikuwa hakuna usafiri wa magari au ndege, sana sana ilikuwa ni ngamia tu.
Wakati akiwa njiani akiendelea na safari yake alijisikia njaa na kwa mbali aliona shamba la mahindi, alipofika katika shamba hilo akakata mahindi mawili matatu na kukoka moto pale pale shambani na kuyachoma kisha akala na baada ya kushiba akaondoka zake na kuendela na safari yake…
Mara mwenye shamba akafika katika shamba lake na kukuta kuna mahindi yame katwa na kuchomwa pale pale shambani na kuliwa, akaamu kufuatilia nyayo za mwizi wake..

Yule mtu alikuwa akiendelea na safari yake bila kujua kuwa kuna mtu anamfuatilia nyuma.
Wakati akiendelea na safari yake mara akaona njiwa mzuri aliyenona yuko juu ya mti, akaokota jiwe na kumrushia yule njiwa na kumpiga sawia.
Akamchukua na na kumchinja, shida ikawa ni wapi atapata moto ili amchome njiwa wake na kumla.
Alipoangalia kwa mbali aliona kuna moshi unafuka, akaamua kuufuata ule moshi mpaka akatokea kwenye kijumba kimoja cha masikini mmoja na mkewe, alipobisha hodi akatoka mama moja mjamzito kwenye hiyo nyumba. Mama huyo alikuwa peke yake kwani mumewe alikuwa hayupo alikwenda kuhemea kijiji cha jirani.
Yule mama alikuwa amekoka moto nje ya nyumba kwa ajili ya kupikia, yule bwana akaomba ambanike njiwa wake, akaruhusiwa.

Wakati anambanika yule njiwa alikuwa akinukia ile mbaya, kiasi cha kumtamanisha yule mama mwenye mji,lakini kutokana na kutomjua yule bwana akaogopa kumuomba.
Basi yule bwana alipomaliza kubanika njiwa wake na kuiva akaaga zake na kuondoka huku akitafuna njiwa wake na kuendelea na safari.
Huku nyuma yule mama kutokana kutamani sana yule njiwa akapata uchungu sana kwa kitendo cha yule bwana kuondoka bila hata kumpa kipande cha nyama,na kutokana na kuwa na kisirani na hasira mimba ikatoka.
Mumewe aliporudi akamkuta mkewe amelala nje ya nyumba akiugulia kwa maumivu ya tumbo,alipomchunguza akagundua kuwa mimba imetoka.

Alipomdadisi, mkewe akamsimulia kisa cha yule mpita njia na njiwa wa kubanika kuwa ndio sababu ya mimba kutoka. Yule bwana akawa anamuhudumia mkewe, na mara yule bwana aliyeibiwa mahindi katika shamba lake akafika pale na kukuta yale matatizo, na baada ya kusimuliwa habari ya mpita njia na njiwa wa kubanika ndipo na yeye alipoeleza kisa cha kuibiwa na mahindi na kumtuhumu mpita njia na njiwa wa kubanika kuwa ndiye muhusika.

Ikabidi waungane muibiwa mahindi na yule, mkewe aliyepoteza ujauzito kumfuatilia yule mpita njia.
Hawakwenda umbali mrefu wakamkuta mpita njia amejipumzisha chini ya mti akipunga upepo, wakamkamata na kumweleza makosa yake, mpita njia akajitetea kuwa hakuiba mahindi bali alikata na kuchoma pale pale shambani kutokana na njaa na kuhusu mimba kutoka alikanusha kuhusika kwa sababu yeye alijichomea njiwa wake na kujiondokea zake baada ya kuruhusiwa na yule mama mwenye nyumba na wala hakujua lililotokea nyuma yake.

Wale watu hawakumuelewa na wakakata shauri wampeleke kwa Musa ili kumshitaki.
Walipofika kwa Musa, wote walisikilizwa kila mtu kwa nafasi yake na baadaa ya Musa kutafakari akatoa hukumu kuwa yule bwana aadhibiwe kwa kuchapwa bakora kisha aondoke zake….
Duh!! Ile hukumu haikuwaridhisha wale jamaa, ikabidi waende kwa Firauni, wakitegemea kupata haki zaidi kwani hukumu ya Musa waliiona kama imempendelea yule mpita njia.

Walipofika kwa Firauni, kama kawaida yake aliwasikiliza wote kila mtu kwa nafasi yake, kisha akatoa hukumu.

Hukumu nyenyewe inasemaje…soma hapa chini…

Firauni akasema yule mpita njia akabidhiwe shamba avune mazao yote kisha apande upya na kuyatunza mpaka yafikie katika hatua kama ile aliyoikuta ndipo amkabidhi mwenye shamba lake. Na kuhusu yule bwana ambaye mkewe alipoteza ujauzito, akasema yule mke akabidhiwe kwa mpita njia akakae nae mpaka apate ujauzito, ukishafikia miezi kama ile iliyotoka amrejeshe kwa mwenyewe….
Duh!!! Jamaa wakachanganyikiwa na ile hukumu wakaondoka pale kwa Firauni kimya kimya na wakamua kumsamehe mpita njia kwani hakuna aliyekuwa tayari kutekeleza ile hukumu.
Na hapo ndipo ulipozuka msemo wa
“Ukishangaa ya Musa utakutana na ya Firauni”

Nikipata nafasi nitawasimulia kisa kingine kizuri cha hekaya za bibi Koero…

Sunday, May 24, 2009

TUNATAKIWA KUZAANA KWA WINGI!

Tusingekuwa tunakufa tusingepata mahali pa kukanyaga




Nilipoandika kuhusu ongezeko la watu na uharibifu wa mazingira nilipata changamoto kadhaa kutoka kwa wasomaji wengi walinitumia email wakipinga au kuunga mkono hoja yangu.
Hata hivyo ni lazima nikiri kuwa maoni yaliyotolewa na msomaji wa kibaraza hiki aitwae Chacha aliyeko Musoma yalinivutia sana ikabidi niendelee kufanya utafiti juu ya jambo hili. Ili kujiridhisha ilibidi nizame katika makataba ya mzee mkundi huku nikisaidiwa na mtandao.
Katika utafiti wangu nimekuja kugundua kwamba kumbe idadi ya watu waliowahi kuishi hapa duniani ni kubwa ukilinganisha na idadi ya wale waliopo leo.
Kwa mujibu wa tafiti mbali mbali zilizowahi kufanywa imebainika kwamba ni asilimia 30 tu ya watu wote wamewahi kuishi hapa duniani.

Pamoja na ongezeko kubwa la idadi ya watu katika kipindi cha karne moja iliyopita, bado inaonekana kwamba watu waliowahi kuishi hapa duniani ambao sasa ni marehemu ni kubwa kuliko ile ya watu walio hai sasa hivi, hiyo ni kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa mwaka 2002, mojawapo tafiti hizo ni ile ya mtaalamu wa idadi ya watu aitwae Carl Haub alifanya.

Mtafiti huyo aliangalia mabadiliko ya idadi ya watu kutoka kizazi kimoja hadi kingine akizingatia mabadiliko ya mazingira, uchumi na matatizo ya uzazi na vifo.
Akifanya utafiti wake kwa kuanzia kipindi cha Adam na Eva, kilichoanza miaka 50,000 kabla ya kuzaliwa Bwana Yesu Kristo. Kumbe Adam na Eva walikuwepo hapa duniani miaka 50,000 kabla Yesu hajazaliwa.
Ingawa sina uhakika miaka hiyo ilipimwa kwa kalenda gani, lakini hilo tuachane nalo.

Kwa kuangalia tafiti nyingine zilizofanywa imebainika kwamba, tangu kuumbwa kwa binadamu wa kwanza, dunia imewahi kukaliwa na watu zaidi ya bilioni 105. Hii ina maana kwamba idadi ya watu walioko duniani hivi sasa ni asilimia 7 tu ya watu ambao waliwahi kuishi hapa duniani.

Hivi kama ingekuwa hatufi ingewezekana vipi watu kuishi hapa duniani hivi sasa? Je ni mpango wa Mungu ili kuepusha watu kufurika hapa duniani na kuhatarisha uwepo wake?
Kwa mujibu wa takwimu za umoja wa mataifa zilizotolewa hivi karibuni, kuna idadi ya watu wapatao Bilioni 7 hapa duniani .
Cha kushangaza Umoja huo wa mataifa unapiga kelele watu wapunguze kuzaa watoto wengi, ili kuepukana na uharibifu wa mazingira.
Hivi ingekuwa hatufi, ingewezekana vipi watu bilioni 105 hapa duniani ilhali watu bilioni 7 tu, wanatishia usalama wa dunia?

Hata hivyo kuna jambo moja ambalo Umoja wa Mataifa umeshindwa kulibaini. Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni zilizofanywa katika nchi za Ufaransa na Japani, imebainika kwamba nchi hizo nikama vile hawazaani, kwani idadi ya wanaozaliwa na wanaokufa iko karibu sawa (Zero Population) na wazee wanazidi kuongezeka katika nchi hizo, lakini bado Umoja huo wa Mataifa wanahimiza watu kutozaana kwa wingi.

Huko nyuma watu walizaana bila hofu na masharti, na ndio sababu idadi ya watu ilikuwa ikiongezeka kadiri miaka inavyokwenda, lakini siku hizi watu wanazaliwa kwa masharti.

Wakati omoja wa mataifa ukipiga kelele tupunguze kuzaana, na hapo ndipo tunaposhuhudia idadi ya vifo ikiongezeka kila uchao, utasikia mara tetemeko la ardhi limeua watu 3000, mara ajali ya ndege, mara ajali ya treni, mafuriko, magonjwa ya mlipuko, vimbunga, nakadhalika nakadhalika.
Na hapo tena tunasikia watu wakipiga kelele, jamaniee….. vifo vimezidi, watu wanakufa!!!????

Tunasahau kuwa ili dunia iendelee kuwepo ni lazima watu wazaane na nilazima watu wafe, huo ndio mfumo wa kuwepo dunia hii tunayoishi.

Thursday, May 14, 2009

MIAKA 30 BADO TUMEFUNGA MIKANDA!

Eti vita vya kumng'oa huyu jamaa ndio vinatutesa mpaka leo!

Juzi katika pekua pekua yangu katika maktaba ya Mzee Mkundi, nikakutana na Gazeti moja la Zamaani sana, ukilinganisha na umri wangu lakini, linaitwa Mzalendo.
Ni gazeti la mwaka 1979.
Kweli baba yangu alikuwa ni mtunzaji, maana gazeti lenyewe ukiliona bado lina hali nzuri tu na linavutia kulisoma.
Basi katika mojawapo ya habari iliyonivutia ni ile ya Aliyekuwa Rais wa kwanza wan chi hii Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aka Mzeee wa Mwitongo.
Ukweli ni kwamba nampenda sana huyu mzee. Huwa sikosi kusikiliza zile hotuba zake za alfajiri kupitia TBC1.

Hotuba hiyo ilikuwa ni ya kututaka sisi Watanzania tufunge mikanda kwa muda wa miezi 18, ili serikali iweze kurekebisha uchumi baada ya vile vita va Kagera.
Wakati wa Vita hivyo mimi nilikuwa sijazaliwa, na hata wakati hotuba hiyo ya kulihutubia taifa ikitolewa nilikuwa sijazaliwa pia, lakini kinachonifurahisha ni kwamba, kama kuna kitu ambacho kitakuja kutuhukumu basi ni maandishi, maana kauli inaweza kupingwa lakini maandishi, ni vigumu sana.

Haya Kiranja wa wakati huo Mwalimu nyerere kwa unyenyekevu kabisa akawaambia watanzania, “Jamaniee tunawaomba mfunge mikanda maana vita hii imetufilisi, na baada ya miezi 18, mutaifungua hiyo mikanda”
Ni kauli ambayo mzee yule aliitoa kwa unyeyekevu kabisa na kutokana na Imani waliokuwa nayo Watanzania kwake yeye watu, wakjifunga mikanda.

Lakini la kushngaza mpaka leo takribani miaka 30 tangu vita ile iishe bado asilimia kubwa ya Watanzania tumefunga mikanda huku wengine wakiwa wameilegeza na kuongeza Papi ili iwe kubwa zaidi.
Hali inazidi kuwa ngumu, kila kukicha, asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi katika ulitima wakishindia mlo mmoja kwa siku, na pengo kati ya mwenye nacho na asiye nacho linazidi kukua.

Juzi nimeenda kununua Dola kwenye duka la kubadilishia fedha pale Posta, nimekuta Dola inazidi kupaa, hadi jana dola moja imefikia kuuzwa kwa shilingi 1330! Sijui wachumi wetu hapa watatueleza nini?
Ukisikiliza Hotuba za kisiasa na takwimu zao zisizo na mshiko utacheka, utawasikia “Uchumi wetu unapanda kwa asilimia 0.0000001” sasa hii inamnufaisha nani?
Wakati tunapolilia kupunguziwa bei tunapofanya manunuzi, wengine wananunua bila hata kuuliza bei.

Mwalimu Nyerere alikuwa na vision, ingawa kuna wakati alifanya makosa, na hilo aliwahi kulikiri, pale aliposema, haiwezekani akae miaka 23 Ikuli halafu asifanye makosa, ni lazima atakuwa alifanya makosa kama binadamu kwani hakuw malaika. Lakini aliwalaumu viongozi wetu wa leo kuwa badala ya kuchukuwa yale mazuri aliyoyaacha wao wanachukuwa mabaya na kuyatupa mazuri, akili gani hii!

Wakati tunapata Uhuru Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, ili tuendelee, yaani tuondokane na umasikini , tunahitaji mambo makuu matatu,
1.Watu
3.Ardhi
4.Siasa safi na uongozi bora.


Kwa upande wa watu, wapo wa kutosha kabisa na tena ikiwezekana tuongezeke zaidi, kwa mujibu wa takwimu ya hivi karibuni tuko milioni 38,
Ardhi nayo iko ya kutosha, naambiwa kuwa karibu asilimia 60 ya ardhi ya nchi hii haijatumika inavyopaswa,
Kwenye siasa safi na uongozi bora, hapa ndio nina shaka napo, Mwalimu nyerere aliona kwamba ili tuwe na siasa safi ni lazima viongozi wawe waadilifu na hakutaka hilo liwe ni jambo la kupita, na ndio sababu mwaka 1967 wakakutana kule Arusha na kututangazia Azimio la Arusha.

Mwalimu alikuwa akililinda na kulitekeleza Azimio la Arusha kwa vitendo na ndio sababu alikufa akiwa ni mtu wa kawaida sana, akiwa amejikita kule Butiama Mwitongo akijilimia.
Alipong’atuka katika uongozi wa nchi hii, kama alivyowahi kusema mwenyewe, viongozi wetu wakutana kule Visiwani Zanzibar na kulivunja Azimio la Arusha, bila hata kuwatangazia Watanzania na waliporudi, kimya kimya wakaanza kujilimbikizia ukwasi kwa kufuru.

Kutokana na kuvunjwa kwa Azimio la arusha ndio maana sasa tunashuhuidia kashfa kama za EPA, Kiwira, Richmond, Dowans, Maliasili, TRA, na nyingine nyingi tu.

Mimi ni msomaji wa Biblia kidogo, katika Wagalatia kuna mahali Mtume Paul aliwambia wagalatia, nitanukuu “Enyi wagalatia, hivi ni nani aliyewaloga ninyi?, nami labda niulize, hivi sisi Watanzania ni nani aliyetuloga?
Nadhani Mchawi aliyetuloga alishakufa zamaaani….

Wednesday, May 13, 2009

SIJUI NDIE HUYU!

Hapa ni kwa bibi Koero, majira asubuhi, Binti huyu alikuwa ameandaliwa chai na Magimbi na bibi yake. Jamani maisha ya kijijini ni mazuri.
Hebu nisaidieni, hivi huyu ni nani?

Monday, May 11, 2009

ANA KILA SABABU YA KUJIVUNIA!

Nyumbani alikozaliwa Mama Namsifu Kiangi

Anaitwa Namsifu Kiangi, alizaliwa mwaka 1941 huko katika milima ya upareni, iliyoko wilaya ya Same Mkoani Kilimanyaro. Ni mtoto wa 5 kuzaliwa kati ya watoto 7 wa mzee Kiangi. Alizaliwa katika kijiji ambacho kinapakana na msitu wa Shengena
Huu ni msitu maarufu ambao ulikuwa ukitumiwa na wazee wa kipare enzi hizo katika kufanya matambiko, hiyo ilikuwa ni kabla ya ujio wa hizi dini za Kimagharibi.

Dini ya kwanza kufika katika eneo hilo ilikuwa ni dini ya Kikristo ya dhehebu la Wasabato. Dhehebu hilo ndilo kubwa lenye wafuasi wengi katika eneo hilo la milima ya upareni kuliko dhehebu lolote lile,
Baada ya ujio wa dini hiyo wazee wengi wa kipare waliachana na mila na desturi zao na kuwa waumini wa dini hizi za kimagharaibi hususan Usabato.

Alizaliwa na kukulia katika dini hiyo ya kisabato, na lipofikisha umri wa kwenda shule wazaziwake walimpeleka shule, alifaulu vizuri darasa la nne na kuendelea na masomo katika shule ya Kimisionari ya Parane, ambapo aliendelea na masomo yake mpaka Middle School.

Alipomaliza middle school hapo mnamo mwaka 1964, aliajiriwa serikalini katika mojawapo ya wizara za serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Aliolewa mwaka 1965, na mzee Japhet Kisarika Mkundi ambaye naye alikuwa ni mtumishi katika taasisi za kigeni.
Mtoto wao wa kwanza wa kiume walimpata mwaka 1967, wa pili wa kike alizaliwa 1970, wa tatu wa kiume alizaliwa mwaka 1973 wa nne wa kike alizaliwa mwaka 1975, wa tano wa kike ambaye anaitwa Koero Japhet Mkundi alizaliwa mwaka 1985 na wa mwisho wa kiume anayeitwa Jarome alizaliwa mwaka 1988.

Akiwa ni Msabato mwenye kufuata maadili aliwalea wanae kwa umri na kimo katika maadili ya Kisabato, na kuna wakati alilazimika kuwalea wanae akiwa peke yake kwa muda wa takribani miaka 8 baada ya mumewe kwenda ughaibuni kikazi na masomo.

Kwa kushirikiana na mumewe wameweza kuwasomesha watoto wao wote na sasa wanajitegemea, baadhi wakiwa wameajiriwa na wengine wakiwa wamejiajiri.
Pia wapo ambao tayari wana familia zao na wameweza kuwaletea Mama Mkundi na Baba Mkundi wajukuu kadhaa

Mama huyu anayo kila sababu ya kujivunia, kwani kwa kushirikiana na mumewe wameweza kujenga familia yenye upendo na amani.

Jana Ilikuwa ni siku ya Mama Duniani (Mothers Day) sisi watoto wa mama Namsifu Japhet Mkundi Kiangi, tulimuandalia mama huyu kijisherehe kidogo cha kumpongeza kutokana na malezi yake kwetu. Niliporejeaa kutoka Morogoro majira ya jioni, niliungana na wenzangu katiaka sherehe hiyo fupi ya kumpongza mama yetu.
Sikuwahi kuandika makala hii jana kutokana na muda kuwa mwingi lakini hata hivyo sijachelewa.

Nawatakia Mama Namsifu na Baba Mkundi maisha marefu.
Ningekuwa na utaalamu kama wa Kaka Mubelwa Bandio ningemuwekea ule wimbo wa Tancut Almas ya Iringa usemao Sina cha kukupa mama.
Lakini naamini kaka Mubelwa ataniwekea wimbo huu wiki ijayo katika ile safu yake ya zilipendwa……..

Thursday, May 7, 2009

SUBIRA, UVUMILIVU NA UBUNIFU VIKALIPA: SEHEMU YA PILI

Hatimaye subira, uvumilivu na ubunifu vikalipa

Ndugu wasomaji wa bolg hii, kutokana na maombi ya wasomaji wengi nimelazimika kumalizia kisa hiki ambacho niliahidi kukimalizia wiki ijayo. Ukweli ni kwamba hiki kisa ni cha kweli na nilikipata kutoka kwa kaka wa rafiki yangu niliyewahi kusoma nae.
Sikutaja jina la mhusika na pia majina ya maeneo nimebadili ili kuficha utambulisho wa mhusika ili kuepuka usumbufu.
nakumbuka siku moja wakati tunapiga stori akanisimulia kwa kifupi juu ya maisha yake na jinsi alivyoweza kupambana na maisha mpaka akaweza kutimiza ndoto zake.
Nilivutiwa na stori yake nikamuomba niiweke hapa kibarazani ili wasomaji wa blog hii nao waweze kujifunza. Alikubali na kunipa stori yote juu ya maisha yake ingawa pia nimeifupisha ili nisiwachoshe, lakini naamini itakuwa imeeleweka.
Katika maisha sisi kama wanaadamu kila mtu anazo ndoto zake na kila mtu anatamani kufanikisha kile anachoamini kuwa kwake ni mafanikio, kwa hiyo misukosuko ya maisha isitukatishe tamaa kwani mlango mmoja ukifungwa mwingine pembeni yako uko wazi ni kiasi cha wewe kupepesa macho kuchunguza.
Haya ungana nami katika kumalizia kisa hiki chenye kufundisha.
Ingawa nilikuwa na kipato kidogo lakini nilikuwa na ndoto za kutaka watoto wangu wapate elimu bora tofauti na mimi baba yao. Nilikuwa ninaamini tu kuwa nitaweza na sikuwa na wasiwasi na hilo. Mara nyingi nilikuwa nikiwaambia wanangu kuwa lazima wasome mpaka chuo kikuu, lakini mke wangu alikuwa akiguna kila nikisema hivyo, alikuwa akinidharau wazi wazi na wakati mwingine alikuwa akinisema kwa mafunbo akidhani kuwa simuelewi.

Kusema ukweli kama ni kipaji mke wangu alikuwa nacho, alikuwa ni hodari wa kusema kwa mafumbo, kubeza na kushushua mpaka mtu akajisikia vibaya.
Unaweza ukasema jambo mbele ya mgeni akakushushua hivi hivi bila kujali kama kuna mgeni. Baada ya kutafakari sana niliamua nikubali yaishe, nimpe talaka halafu tugawane kile alichoita mali. Ulikuwa ni uamuzi mgumu lakini nilikuwa sina jinsi, niliona kuwa ile itakuwa ni njia sahihi ya kuepuka kero na kupoteza muda na pesa pasipo sababu.

Siku iliyofuata, asubuhi na mapema nilikwenda ukweni na talaka yangu ambayo niliiandika usiku ule ule.

Nilipofika na kumueleza baba mkwe juu ya uamuzi wangu wa kuridhia kutoa talaka, baba mkwe alistuka, kwani hakutegemea uamuzi wangu ule.
Baada ya majadiliano tulikubaliana kiwanja kiuzwe na hela itakayopatikana pamoja na ile hela ya mafao ya kupunguzwa kazi tugawane sawa kwa sawa na hata vitu vya ndani pia vigawanywe kila mtu akaanze maisha kivyake. Iliniuma sana lakini sikuwa na jinsi.

Ndani ya wiki moja tuliuza kiwanja na tukagawane fedha pamoja na vitu vya ndani, nikawa nimeutuwa mzigo.
Nikaanza maisha mapya nikiwa peke yangu.
Niliamua kusafiri na kwenda nyumbani kuwaona wazazi na kupumzisha akili.

Nilirudi Dare s salaam baada ya wiki moja, hiyo ni baada ya kukaa na wazazi wangu kwa muda wa wiki moja nikipata ushauri kutoka kwa wazazi wangu namna nitakavyoweza kupambana na maisha baada ya kutengana na mke wangu.

Nilipofika tu nilitafuta kiwanja maeneo ya kule kule Segerea na nilibahatika kupata eneo la eka moja na haraka haraka nilisimamisha kibanda changu chenye chumba na sebule.
Niliamua kujikita zaidi kwenye kazi ya kupiga picha na niliamua kununua kamera mpya ya kisasa, kama masihara nilianza kuzururra mitaani maeneo ya Tabata kutwa nikipiga picha kwenye mabaa na mitaani na ghafla nikawa maarufu.

Nilianza kupata tenda za kupiga picha kwenye sherehe mbali mbali, misibani na kwenye matukio mbali mbali mitaani, na kijipatia fedha za kutosha.
Baadae nilipata wazo la kununua video kamera, hiyo ni baada ya kuwa naulizwa sana na wateja wangu.
Ili niweze kuitumia vizuri nikajiunga na chuo kimoja pale mjini ili kusomea mambo ya Video Production pamoja na Masomo International Technology ili niweze kufanya kazi zangu kwa ufanisi.

Ilinichukuwa miaka miwili kupata cheti changu cha diploma.

Nilikuwa napata kazi mbali mbali mpaka za mikoani na mpaka kufikia mwaka 2005 nilikuwa nimejenga nyumba yangu ya kubwa na kufungua studio yangu pale pale nyumbani ambapo nilikuwa nikifanya shughuli zangu mwenyewe.

Mke wangu tuliyeachana alikuwa akiendelea kujirusha na wanaume kwenye kumbi za starehe, niliamua kuwachukuwa wanangu na kuwapeleka nchini Uganda wakasomee huko.
Mwaka 2006 aliyekuwa mke wangu alifariki kwa kile wazazi wake walichoita TB, lakini dalili zote zilikuwa ni za kuugua ukimwi.
Sikusikitika sana kwani hayo yalikuwa ndio majaaliwa yake, alikuwa amevuna kile alichopanda.

Mnamo mwaka 2007 nilifunga ndoa na mchumba wangu baada ya kuwa wachumba kwa takribani miaka miwili.
Mchumba wangu huyu ambaye ni mwenyeji wa Mkoani Kilimanjaro, Mchaga ni mtumishi katika kampuni moja binafsi.

Ni mwanamke makini ambaye anajiheshimu na kuwathamini watoto wangu na amekuwa ni mshauri wangu katika mambo mengi na hata wazo la kuwapeleka watoto wangu Uganda kwa ajili ya kusoma ni yeye aliyelitoa.

Mpaka sasa tumejaaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume ambaye ana umri wa mwaka mmoja.
Ili kuimarisha kazi yangu hii nimenunua mitambo yangu ya kusafishia picha na vyombo vya kupigishia muziki Katika sherehe mbalimbali.

Kutokana na kazi yangu kuwa nzuri na yenye ufanisi nimekuwa nikipata kazi mbalimbali za mikoani.

Nimeweza kujenga nyumba zangu nyingine mbili, moja ikiwa Tabata Kimanga na nyingine ikiwa maeneo ya Kimara na zote nimezipangisha.

Matarajio yangu ni kumpeleka mke wangu nje akajifunze mambo ya upambaji ili tufungue kampuni kubwa itakayojishughulisha na upambaji katika sherehe mbalimbali.

Maisha ninayoishi sasa ni ndoto nilizokuwa nazo miaka 15 iliyopita kwani baada ya subira, pamoja na misukosuko mingi hatimaye nimeweza.
Subira, Uvumilivu na ubunifu vikalipa, hata wewe ukiamua unaweza.

Wednesday, May 6, 2009

SUBIRA,UVUMILIVU NA UBUNIFU VIKALIPA!

Kamwe sikukata tamaa

Ilikuwa ni mwaka 1999 baada ya kuwa nimetumikia shirika la umma kwa takribani miaka 20 nilijikuta nikiwa miongoni mwa wafanyakazi 70 wa shirika hilo tuliotupwa nje ya ajira kwa kile kilichoitwa ridandansi, ili kulinusuru shirika hilo ambalo lilianza kuyumba kutokana na ushindani wa kibiashara baada ya serikali kufungua milango kwa wawekezaji kutoka nje.

Baada ya kupata mafao ambayo hata hivyo hayakulingana na muda niliotumikia shirika hilo, nilikaa chini na kuanza kutafakari mustakabali wa maisha yangu ya baadae na familia yangu.

Nilikuwa bado naishi nyumba ya kupanga nikiwaa na mke na watoto wawili, wa kwanza wa kike aliyekuwa na miaka 5 na wa pili wa kiume aliyekuwa na miaka 2. Nilikuwa na jukumu zito la kuhakikisha watoto wangu wanapata elimu bora, Je hilo litawezekana baada ya kupoteza ajira? Nilijiuliza.

Katika kipindi cha miaka hiyo ishirini niliyofanya kazi katika shirika hilo, sikubahatika kujenga, ingawa nilifanikiwa kununua kiwanja maeneo ya Tabata Segerea, ambapo palikuwa ni kama porini wakati huo, tena kiwanja chenyewe kilikuwa ni cha mkopo ambao niliumaliza mwezi mmoja kabla sijapewa ridandansi.

Ukweli ni kwamba sikubahatika kujenga kutokana na maslahi kuwa madogo, kwani tulikuwa tukilipwa mshahara mdogo na kulikuwa hakuna marupurupu ya kutosha na hivyo nikajikuta nikiwa na maisha magumu.

Hata hivyo ilibidi nianzishe mradi mdogo wa kupiga picha mitaani na hata kazini ili kujiongezea kipato, ingawa sikuwa napata hela za kutosha lakini si haba, fedha nilizokuwa napata zilikuwa zikinisaidia kupunguza ukali wa maisha.

Kwa upande wa mke wangu, naomba nikiri kuwa hakuwa na msaada sana kwangu. Alikuwa ni mama wa nyumbani, lakini hakupenda kujishughulisha kama wanawake wengine. Alikuwa ni mtu wa kushinda nyumbani kutwa akijiremba na kushindana na wanawake wenzie kwa mavazi, ilikuwa kila Khanga au Vitenge vipya vikiingia hakutaka vimpite na hata mtindo mpya wa mavazi ukiingia pia hakutaka umpite, nilikuwa na wakati mgumu kumridhisha kutokana na tamaa aliyokuwa nayo.

Tofauti na wenzangu niliokuwa nikifanya nao kazi, wake zao walikuwa ni wachapa kazi, hawakubweteka, na baadhi yao walifanikiwa hata kujenga nyumba zao baada ya kuunganisha nguvu kati yao.

Waliosema, nyuma ya mafanikio ya mume kuna mke na nyuma ya anguko la mume kuna mke hawakukosea .
Hii ina maana gani? Ina maana kuwa kufanikiwa kwa mwanaume au kutofanikiwa, kunategemea na aina ya mke aliyeoa.

Nakumbauka nilishauriwa sana na baba yangu nikaoe kijijini kwetu lakini nilikataa kwa madai kwamba siwezi kuoa kijijini, kwa kuwa wanawake wa kule ni washamba, kwa hiyo nikaamua kuoa hapa hapa jijini Dar es salaam, binti wa kingindo aliyezaliwa na kukulia mjini.

Tulikuwa tukiishi Magomeni wakati huo, eneo lililojaa uswahili, ushindani na na ushabiki wa kishagingi.
Hata kwao na mke wangu kulikuwa na uswahili mtupu, dada zake wote watatu walikuwa wameolewa na kuachika na wote wako nyumbani kwa wazazi wao, sijui ni kwa nini sikuliona hilo.

Katika kipindi ambacho nilikuwa nyumbani baada ya ridandansi nilikiona kigumu hasa, kwani baada ya mke wangu kujua kuwa nimepata mafao ya kuachishwa kazi alianza kutamba kuwa wanawake pale mtaani watamkoma, alikuwa na mahesabu ya kuvaa vito vya thamani na mavazi ya gharama ili wajue kuwa na yeye anazo.

Akili yake ilikuwa ni tofauti kabisa na ya kwangu, mimi nilikuwa na mipango tofauti kabisa .
Nilikuwa na mpango wa kupandisha vyumba viwili haraka haraka kule katika kiwanja chetu kisha tuhame ili kuepuka gharama za kulipa kodi ya pango, halafu nianzishe biashara ili niweze kumudu kupambana na ugumu wa maisha.

Siku moja nikiwa nimetulia chumbani usiku nilimuita mke wangu ambaye alikuwa nje akipiga soga na wanawake wenzie, alipofika nilianza kumueleza juu ya mipango yangu, lengo likiwa ni kumshirikisha katika mipango yangu niliyokuwa nimeiratibu tangu nilipopewa ridandansi.

Mke wangu alipinga kwa nguvu zote mipango yangu niliyopanga na hakutaka kunisikiliza, kwa maoni yake alitaka eti tugawane yale mafao ili kila mtu afe na chake kwani hakuwa tayari kwenda kuishi huko porini Segerea. baada ya kumweleza kuwa nilikuwa nimedhamiria kufanya kile nilichokisema na nilikuwa sitanii, alianza kuzungumza kwa sauti kubwa na kutukana.

Nilihisi hasira zikinipanda nikaamua kuondoka na kwenda kuzurura kidogo ili kupoteza mawazo, Nilirudi majira ya saa tano usiku, nilipofika nyumbani nilipokelewa na matusi na kashfa kutoka kwa mke wangu, kwani alinituhumu kuwa nilikwenda kwa wanawake wengine kwa kuwa sasa nina fedha.

Nilijikuta nikimpiga kwa hasira na kama si wapangaji kuamka kutokana na kelele za mke wangu na watoto labda ningeua, kwani nilipandwa na hasira kupita kiasi, na tangu nimuoe mke wangu siwahi hata kumfinya, hatua ya mimi kumpiga ilimshangaza hata yeye. Ndio tulikuwa tunatofautiana lakini haijawahi kufikia hatua ya kupigana.

Wapangaji wenzangu walipofika pale waliamua ugomvi wetu halafu wakinitoa nje ili nisije nikaendelea kumpiga mke wangu kwani alikuwa akiendelea kunitukana na kunikashifu hadharani bila ya aibu.

Aliondoka usiku ule ule na taxi kwenda kwao akiwa na watoto wetu maeneo ya mwananyamala ambapo ndipo wazazi wake walipokuwa wakiishi.
Baba wa mke wangu alikuwa ni mfanyakazi Bandarini na alifanikiwa kujenga nyumba nne hapa jijini Dar es salaam mbili zikiwa Mwananyamala na nyingine mbili zikiwa Kinondoni, na hiyo ndiyo iliyokuwa ikimpa mke wangu kiburi.

Niliingia ndani na kujifungia na kujitupa kitandani, na kuanza kutafakari juu ya lile tukio. Sikupata usingizi kabisa kutokana na mawazo niliyokuwa nayo, na nilijilaumu sana kwa kile kitendo nichokifanya cha kumpiga mke wangu. Nilijiona mjinga kwa kitendo kile.

Siku iliyofuata nilikwenda ukweni kwangu asubuhi na mapema ili kusuluhishwa. Nilipofika nilipokelewa na baba mkwe wangu na baada kusalimiana waliitwa wazee kadhaa wa pale jirani ili kuweza kusuluhishwa.
Katika kikao hicho mke wangu alidai talaka na alitaka fedha za mafao nilizopata baada ya kupewa ridandansi kazini tugawane na pia kile kiwanja chetu kilichokuwa segerea kiuzwe na fedha tugawane vile vile ili kila mtu afe na chake, nilipinga wazo lile kwa nguvu zote kwani sikuwa tayari kutoa talaka, nilikuwa nawahurumia wanangu kukosa malezi ya wazazi wote wawili.

Baba yangu mkwe alikuwa ni mtu mwenye busara sana hakuafiki wazo la mwanae na aljitahidi sana kumuelewesha mwanae kuwa kile ninachotaka kukifanya sio kwa ajili yangu peke yangu bali ni kwa ajili yake na watoto, kwani si vyema kukaa katika nyumba za kupanga, na watoto wanakua. Lakini mke wangu kwa kushirikiana na mama yake pamoja na dada zake walishupalia talaka itolewe na mali igawanywe .

Wale wazee waliokuwepo katika kile kikao walijitahidi kutoa hekima zao ili kuinusuru ndoa yangu lakini haikusaidia.
Mwishowe ikaamuliwa shauri lile lipelekwe BAKWATA, baraza la kiislamu ili tuweze kusuluhishwa.

Nilirudi nyumbani nikiwa nimechanganyikiwa kabisa, sikulala usiku kucha nilikuwa nikiwaza juu ya mustakabali wa watoto wangu. Je maisha yao yatakuwaje baada ya sisi wazazi kutengana? Je watapata elimu kama nilivyokusudia?
Nilijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu.

Ungana nami wiki ijayo kumalizia kisa hiki chenye kufundisha….

Saturday, May 2, 2009

SHIRANGA LA UGONJWA WA MALARIA: BORA TUFE KULIKO KUATHIRI MAZINGIRA!

Hawa ndio waathirika
Nimerejea jijini Dar Es Salaam jana, nikitokea Arusha, nilikokwenda kufanya shughuli maalum ya kifamilia.

Kilichonipeleka sikuweza hata kukifanya kwani tangu nilipofika Arusha nilipatwa na Malaria kali iliyopelekea hadi kulazwa hospitalini na kutundikiwa drip kadhaa za kwinini.

Namshuru Mungu nilipata nafuu na hatimaye kupona kabisa. Nadhani kuugua kwangu kulikuwa na kusudi maalum, kwani niliugua katika wiki ambayo kulikuwa na maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa malaria na kama kawaida wanasiasa na wataalamu wetu walitoa matamko mbali mbali ili kuonesha kuwa ni kwa kiasi gani serikali yetu inachukua hatua madhubuti katika kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huu ambao unapoteza maisha ya watu wengi hapa nchini kuliko hata huu ugonjwa wa ukimwi unaopigiwa mbiu kila siku.

Ukweli ni kwamba nina mashaka sana na juhudi za serikali katika kutokomeza ugonjwa huu wa malaria kufanikiwa.

Kwa nini nasema nina mashaka na juhudi za serikali?

Ni kwa sababu tangu kuzaliwa kwangu mpaka leo hii nimeshuhudia mabadiliko kadhaa ya dawa za kutibu maleria zikiidhinishwa lakini hazikufanikiwa katika kutibu ugonjwa huo zaidi ya kuwasababishia watumiaji madhara na hata vifo.
Pamoja na juhudi hizo zinazochukuliwani na serikali nadhani sasa ni wakati muafaka wa serikali yetu kuangalia upya uwezekano wa kurudisha matumizi ya dawa ya kuulia wadudu ya
Dichloro-Diphenyl-Trichloroethane maarufu kama DDT, ili isaidie kuuwa mazalia ya mbu na kuwatokomeza kabisa kwani tutakuwa tunahangaika kutibu malaria na kila dawa huku mbu wakiendelea kuzaliana bila kuthibitiwa.

Naona huu ni wakati muafaka wa serikali yetu kuachana na kelele za hawa watu wanaojiita wana mazingira wanaotegemea misaada ya kifedha kutoka kwa wafadhili ambao wanafanya hivyo makusudi ili kuvilinda viwanda vyao vya madawa na ajira kwa wanachi wao.

Siku moja nilikuwa nikiangalia Luninga, mara nikamsikia mtaalamu mmoja wa mazingira, akizungumzia madhara ya DDT kwenye mazingira yetu kwamba kuna baadhi ya wadudu na mimea itatoweka, ujinga gani huu!
Yaani ni bora tufe kuliko mazingira na viumbe fulani kutoweka hapa duniani?

Kingine wanachodai wataalamu wetu hao, eti dawa hiyo ya DDT inasababisha Kansa na kuzaliwa watoto wenye mtindio wa ubongo.
Hivi watoto wote wanaozaliwa wakiwa na mtindio wa ubongo na wale wagonjwa wote wanaolazwa pale taasisi ya ugonjwa wa Kansa pale Ocean Road ni kutokana na DDT?

Mbona hawazungumzii huo mlundikano wa madawa feki hapa nchini ambayo huenda ndio yana madhara kuliko hata hiyo DDT.
Juzi hapa mama Margareth Ndomondo Singoda Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ametutangazia kupiga marufuku dawa za malaria aina ya Metakelfine, eti ni feki!
Miaka yote hiyo watu wamekuwa akitumia dawa hii katika kujitibu malaria sasa leo ghafla zinatangazwa kuwa ni feki.
Je ni watu wangapi watakuwa wameathirika na dawa hiyo?

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na waziri wa Afya Profesa David Mwakyusa ambazo hata hivyo zinatofautiana na takwimu zilizotolewa na na Daktari bingwa wa Malaria Muhimbili Profesa Zul Premji, katika mchakato wa kuelekea katika maadhimisho hayo ya siku ya malaria, alibanisha kuwa, takwimu rasmi kutoka katika vituo vya afya idadi ya watu wapatao 20,000 hupoteza maisha kila mwaka hapa nchini kutokana na ugojwa huu wa malaria, na wengi wao wakiwa ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na mama wajawazito.
Hata hivyo alikiri kuwa asilimia 60 ya vifo vinavyotokea majumbani kabla ya wagonjwa kufikishwa katika vituo vya afya ni kutokana na ugonjwa huo wa malaria.
Kwa muktadha huo basi, idadi halisi ya wagonjwa wanaofariki kutokana na ugonjwa wa malaria hapa nchini ni zaidi ya watu 80,000 kila mwaka.

Takwimu hizo zinatofautiana kwa kiasi kikubwa na takwimu zilizotolewa na Profesa premji aliyedai kuwa zaidi ya watu milioni moja hufa kila mwaka hapa nchini kutokana na ugonjwa huu wa malaria.
Hata hivyo kwangu mimi tofauti ya kitakwimu sio mada, bali ninalotaka kulizungumzia hapa ni juu ya serikali kurejesha matumizi ya DDT, hili naomba liwe ni mjadala wa kitaifa ili kunusuru roho za watu, jamani watu wanakufa sio mchezo!

Mbona Zanzibar wanatumia? Wao wamewezaje, na kwa nini isiwe huku kwetu Bara?
Hapa tunahitaji ufafanuzi kutoka serikalini, watueleze sababu ya kusita kuidhinisha matumizi ya DDT.

Historia inaonesha kwamba DDT iligunduliwa na mkemia mmoja wa Ki-Swiss aitwae Paul Muller hapo mnamo mwaka 1934, ambapo ilitumika kwa mara ya kwanza nchini humo mwaka 1939 kuuwa vijidudu vilivyokuwa vikishambulia viazi mbatata na kupata mafanikio makubwa.

Mnamo mwaka 1943 dawa hii ya DDT iliingia sokoni rasmi ikianzia katika nchi za Ulaya, ikitumiaka katika kuuwa wadudu watambaao na warukao wanaosababisha maradhi mbali mbali na kupata mafanikio makubwa.

Dawa hii ilitumika pia wakati wa vita vya pili vya dunia katika maeneo ya tropiki yaliyoathirika na maradhi mbali mbali yaletwayo na mbu na wadudu wengine ambayo yaliwasumbua na kuwatia hofu askari walikuwa vitani zaidi ya makombora na risasi.

DDT ilionekana kama muarobani wakati huo na iliheshimika sana kiasi cha kupelekea mgunduzi wake kutunukiwa nishani ya Nobel hapo mnamo mwaka 1948 kutokana na ugunduzi wake huo.

Zipo nchi ambazo zilizofanikiwa sana katika kupambana na ugonjwa huu wa malaria wakati huo miongoni mwa nchi iliyopigiwa mfano ni nchi ya Sri Lanka.
Mwanzoni mwa miaka ya 1950, zaidi ya watu milioni 2 walikuwa wakiripotiwa kuugua ugonjwa huo wa malaria kila mwaka nchini humo. Baada ya nchi hiyo kutumia dawa ya DDT kuteketeza mazalia ya mbu na wadudu wengine hapo mnamo mwaka 1954, idadi ya wagonjwa walioripotiwa katika vituo vituo vya afya ilipungua na hatimaye kwisha kabisa

Hata hivyo inaonekana mafanikio hayo hayakuwafurahisha matajiri na wamiliki wa viwanda vya madawa na kwa hila huku wakitumia fedha nyingi waliwashawishi wanamazingira ili kuipiga vita dawa hii ya DDT, wakilenga zaidi nchi za dunia ya tatu ambazo hazijajitambua na zinazotegemea misaada kutoka nchi wahisani.

Hawa watu ni wajanja sana, hawa ndio walioanzisha shirika la afya duniani WHO, shirika ambalo wanalifadhili kwa mapesa yao wanayochuma kwa kuuza madawa yao, kwa kuwa shirika hilo linatekeleza maelekezo kutoka kwa mabwana hao wakubwa wakatangaza kuwa ni marufuku dawa hiyo kutumika.
Ikumbukwe kwamba hawa wenzetu walifanikiwa kuwatokomeza mbu katika nchi zao kwanza na ndipo matumizi ya DDT yakaharamishwa.

Huku wakitumia njia ya kutoa misaada ya madawa na vyandaru, kwa staili ya kupiga kofi shavu la kulia na kisha busu shavu la kushoto.
Wanajua misaada yao haitawafikia waathirika wote na kwa upande mwingine wataendelea kuuza madawa yao kwa wingi na kujiingizia fedha lukuki, wajinga ndio waliwao!

Lakini ili ujue kuwa shirika hilo lina ubaguzi, ili kuzilinda baadhi ya nchi zao, wakaweka kipengele kuwa itatoa kibali kwa nchi ambayo itakuwa imeathiriwa sana na ugonjwa wa malaria na maradhi mengine yatokanayo na vijidudu viambukizi kutumia DDT, na itakuwa ni kwa muda maalum. Ebo ina maana mpaka watu wafe kwa wingi na ndipo idhini ya kutumika kwa dawa hiyo itolewe?
Huu ni uwenda wazimu, huyu WHO ni nani hasa? Kwani ndio wizara ya afya ya dunia?

Ukisoma takwimu zao, utashangaa, eti wanadai kwa mwaka watu wapatao 20,000 hupoteza maisha kwa maradhi ambayo yana viashiria vya madawa ya kunyunyizia wadudu. Kwangu mimi hiki ni kichekesho, Afrika peke yake inapoteza watu milioni 5 kwa mwaka kutokana na ugonjwa wa malaria, watu 20,000, ni kitu gani.
Tena kwa mujibu wa takwimu zao wamesema maradhi yenye viashiria, sio yaliyotokana na madawa ya kunyunyizioa wadudu, huu ni upuuzi mtupu.

Serikali ya Sri Lanka ni miongoni mwa nchi zilizotekeleza amri hiyo, lakini mara baada ya matumizi ya DDT kusitishwa nchini humo, Malaria ilirudi kwa kasi na kwa muda wa miaka mitatu ya mwanzo zaidi ya wagonjwa milioni moja waliripotiwa kwa mwaka.

Hata hivyo Serikali ya Nchi hiyo ikaamua kurejesha matumizi ya dawa hiyo ya DDT mnamo mwaka 1968 na kupuuza kelele za hawa wanafiki wanaojiita wanamazingira.

Nchi hiyo imekiri kuwa kwa kiasi kikubwa imepunguza maradhi kama malaria, homa ya malale, kichocho, upofu, matende, taifodi maradhi mengine yatokanayo na bakeria.

Sri Lanka imeangalia madhara yatokanayo na mbu na wadudu wengine, na huo uharibifu wa mazingira na athari nyingine za kiafya zinazotajwa kusababishwa na DDT, wakaona, hata hayo madhara ya kiafya yanayosemwa sio makubwa kwa kiwango kinachosemwa bali kimekuzwa tu na wataalamu hao, kwao muhimu ni maisha ya watu.

Mtaalmu mmoja wa Afya nchini humo aliwahi kuuliza ‘Iwapo mtu unakabiliwa na uchaguzi wa kukubali kuwa kipofu kabla ya kutimiza umri wa miaka 30 kutokana na vijidudu waambukizao maradhi hayo ya upofu au uwezekano mdogo sana wa kupata Maradhi ya Kansa kutokana na matumizi ya DDT kama utafanikiwa kuishi zaidi ya miaka 50 au 60, utachagua kipi?’

Haihitaji mtu kutumia akili ya wataalamu wa kutengeneza Roketi kupata jibu.