Saturday, March 6, 2010

UKOSAPO NENO JEMA, KHERI UJINYAMAZIE.

Nakuasa usikie, usemaji ni karama,
Maneno usirukie, sema mambo kwa kupima,
Utamkapo ujue, neno halirudi nyuma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Kheri ujinyamazie, ovu huleta khasama,
Majuto yasikujia, “Laiti nisingesema”,
Mtu baa azuae, Motowe utamchoma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Ni wengi wajiponzao, kwa zao mbovu kalima,
Heshima waitakao, waseme usemi mwema,
Wale waumbukanao, ni kwa ndimi kuparama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Watazame wakuao, dunia kuwatazama,
Ni wale wapimiao, kabla ya kuyasema,
Na kimya wanyamazao, wakosapo neno jema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Neno huenda likuwe,lizidi hata vilima,
Mambo mawi liyazue, akili zende mrama,
Au mema yatukie, liwapo neno la wema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Funzo walitufunzao, wazungupule wa zama
Zama za kale na leo, walokimcha Karima,
Yawe mema tusemao, tusije zusha zahama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Mola akubarikie, na ambaye akusoma,
Na furaha ututie, uwe ni diwani njema,
Mema utuhadithie, wana kwa watu wazima,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Shairi hili limetungwa na Mshairi maarufu Afrika Mashariki Bwana Amri Abedi, nami nimeona sio vibaya kulirejea ili tujifunze pamoja.................

6 comments:

Fadhy Mtanga said...

Ahsante sana kwa shairi zuri. Awali nilidhani nawe umekuwa mshairi.
Ni kweli chambilecho hayati Sheikh Amri Abeid Kaluta. Mwenyezi Mungu amrehemu.

Mzee wa Changamoto said...

Umenikumbusha ujumbe uliomo kwenye wimbo wa Hayati Lucky Dube katika albamu yake ya mwisho kutoka kabla hajafariki.
Wimbo wake wa pili (kwenye CD) una kiitikio kisemacho
" AND IF YOU CAN'T SAY SOMETHING GOOD ABOUT SOMEBODY, JUST SHUT UP"

Hebu usikilize wote hapa http://www.youtube.com/watch?v=aiT8RrIL9O8

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Wenzetu wa mwambao wangeingia na kibwagizo cha kiushikajishikaji kama Malika vile: "wape wape vidonge vyao, wakimeza wakitema shauri yao"

http://www.youtube.com/watch?v=uVQlqV1VkWM

Koero Mkundi said...

Prof. Matondo na kaka Mubelwa Nimesikliza, nyimbo zote mbili na nimeburudika nazo na nimejifunza kitu pia.

Natamani niziweke hapa kwangu lakini mwe, mtandao huku una nguvu ndogo , nimeshindwa kabisa.

Upepo Mwanana said...

Ningekuwa na uwezo wa kutunga mashairi, basi ningekuwa najimwaga kila siku na mashairi. Talanta yangu ni nyingine!!!

MARKUS MPANGALA said...

thamani mwanamke nini?
kivazi chenye kimini?

Raha ya tunda nini?
Ladha au kujilamba ulimi?

Utamu ukidi sana
sema bandu bandu.

Mwenyekiti ASANTE kwa shairin lako, ulilolitongoa kwa ABEID