Sunday, May 2, 2010

UCHAWI DHANA INAYOSUMBUA MAISHA YA KAWAIDA YA BINADAMU

Mganga akipiga Ramli
Kuna maelezo mengi sana ya uchawi. Lakini uchawi ambao umekuja kujulikana duniani kwa jinsi dunia yenyewe ilivyo,umekuwa ukibadilika kimwelekeo lakini kimsingi sayansi hii ambayo kwa miaka mingi hufundishwa kwa siri na wanaojua kwa wanaotaka kuijua na wakati mwingine kurithisha, ni ada ya wanadamu wengi hasa katika Bara la Afrika.

Wale wasomi hukataa na kukana uwapo wake, wanaikataa dhana yenyewe na wanasema kwamba si kitu kujadili na mgeuko wake ni fikra za dini tulizonazo za Kiislamu na Kikristo ambazo zinatambua uwapo wake na kusema ni kazi ya shetani na matumizi mabaya ya maarifa ambayo ni nadra kila mtu kuyajua.

Unaweza kujua vitu au kitu kinachoitwa uchawi kutokana na mambo kadhaa hasa yaliyoandikwa au kufanyiwa masimulizi katika vitabu mbalimbali vikiwamo vya Kurani na Biblia. Kila mwaka wenzetu wa Haiti,vitukuu na vilembwe vya waliofikishwa utumwani hufanya tamasha kubwa la wachawi, wao wana dini yao ambayo ni ya kuabudu kitu wanachoita voodoo.

Watu hawa wanachofanya kwa wengine ni uchawi lakini kwao ni imani kali ya kujisalimisha kwa roho mbalimbali zisizoonekana ambazo ndizo wanazodai kuwatawala. Nadharia na suala zima la uchawi limezungumziwa na kujadiliwa tena na tena na watu mbalimbali na kwa namna mbalimbali. Lakini taabu kubwa ni tafsiri ya uchawi.

Hivi unawezaje kuuzungumzia uchawi ukasahau wanga na uganga, upo wakati uchawi , uganga na wanga huwa ni kitu kimoja kwa wengi wetu. Uchawi umewekwa katika dhana kwamba watumiaji na waathirika ni washenzi lakini kama utakuwa umesikiliza gumzo la Ng'wanamalundi ipo tafsiri ndani ya waungwana kuhusiana na shauri hili na kusema kwamba uchawi unawahusu watu washenzi, kidogo inapoteza ukweli wa mambo.

Katika filamu ya Ng'wanamalundi, mchawi aliyewakilisha kundi la wachawi alisema yale ni maarifa na ufundi wa kufanya mambo, sasa kama washenzi wanayapata maarifa haya sijui inakuwaje hasa. Lakini tafsiri ya karibu kabisa ya watu kuhusu uchawi na hata katika makamusi yetu ni matumizi mabaya ya maarifa aliyonayo mtu kudhuru mtu mwingine au mali zake. Kamusi ya Kiswahili sanifu inasema kwamba uchawi ni ufundi wa kutumia dawa, aghalabu mitishamba na vitabu maalumu vya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe.

Katika hili ni wazi siri ndio jawabu la maana la maana ya uchawi , ufundi wa kuleta madhara. Mwanga kwa upande wake ni mcheza mahepe afanyaye mazingaombwe ya kichawi usiku. Ni tatizo sana kuzungumzia uchawi kama sihiri lakini shauri la kusema watu washenzi yaani wasiostaarabika ni kasheshe kubwa kwani wapo wachawi wanaoendelea na matajiri wakubwa wakiabudu uchawi kama chanzo kikuu cha utajiri wao, sasa nini hasa kipimo cha uchawi? Uchawi huu ambao huathiri viumbe kuna wakati hutumika kwa manufaa makubwa, ikiwa ni pamoja na kuzuia uharibifu mkubwa wa madhara ya uchawi katika jamii kwa kuwapo na mtu anayedhibiti wachawi wadogo na kuwaumbua.

Zipo nadharia zinazozungumza shauri zima la uchawi na Profesa Haward Safari katika mada yake ya uchawi katika Riwaya za Kiswahili mwaka 1993, alizungumzia shauri zima la uchawi na ushahidi wake. Alikuwa anazungumza katika mkeka mkubwa na waandishi wa vitabu, UWAVITA, na mfano wake wa bomu na nyutroni unaweza kukuweka hoi.

Ni kweli kuwa utaalamu wa kutengeneza bomu hili ni siri kubwa na wataalamu wake wanalindwa sana, kwa hiyo kama shauri hili la ufundi na usiri ni uchawi basi nyutroni ni uchawi na umetengenezwa kwa minajili ya kudhuru binadamu. Imani za kiuchawi ambazo zimekumba nchi yetu kwa kasi, ipo pia katika Bara la Afrika na Ulaya ambako ndiko inakoaminika imeanzia katika karne za kati.

Hapa nchini vipo vitabu vingi vinazungumzia dhana hiyo katika mifumo mbalimbali ingawa vinavyoeleza kwa lugha ya kukua sana ni kama Mirathi ya Hatari kwa upande wa hadithi za kubuni, hadithi za dini hasa hadithi ya taaluma ya uchawi , Maalim Kisisina na ile ya Mussa na Wachawi wa Farao katika Biblia.

Katika simulizi la Maalim Kisisina, inaelezwa kulizuka matatizo makubwa wakati wa kunyang'anyana kitabu cha uchawi kati ya Jibril na maalim huyo na mwishoni Jibril alimwachia maalim huyo kitabu na ndio uchawi uliopo sasa duniani. Hadithi ya maalim huyu ipo katika Kurani na Biblia, kwa namna yake imezungumzia shauri la Musa na wachawi wa Farao ambao nao waliweza kugeuza fimbo zao kuwa kama nyoka kwa jinsi Musa alivyoweza. Kama kwa Jibril, Musa naye alionyesha ukuu wa uchawi dhidi ya shauri la Mungu na Mungu kuonekana kuwa mkubwa wa yote, fimbo ya Musa iliwalamba nyoka wale wa Farao.

Mashauri ya uchawi yapo hata Ulaya. Nchi kama Uingereza na Ujerumani ndizo zinazoongozwa kwa masimulizi ya uchawi kwa kuungama kwa wahusika. Kimsingi uchawi ni sanaa ambayo ipo katika kila mahali na ina vitisho vikubwa.

Siku za karibuni kumezuka mganga anayejulikana kwa jina la Manyaunyau ambaye anatoa vitu vinavyoitwa vya kichawi na watu wanashukuru kwa kufanyiwa hivyo. Watu katika hekaheka hizo wanaokumbwa na mikasa ya kunaswa katika anga za mganga Manyaunyau, wanazungumzia ndege zao wanazosafiria nyingine zikiwa na uwezo wa kubeba hadi abiria 16 (sawa na Cessna), kitu kinachoitwa mwanga chenye jicho moja kama kilichodaiwa kudakwa huko Kimara King'ongo ambacho kilifanyiwa hila ya kunaswa.

Si Kimara tu maeneo mengi ya Dar es Salaam yana matatizo hayo kukiwa na historia ya kitaifa ya uganga na ulozi. Mathalani watu wengi hawatasahau Mandondo wa Korogwe, Tekelo wa Dar es salaam, Kabwere wa Tanga, hao walikuwa waganga maarufu wa kufichua wachawi bila kumsahau mganga Kalembwana wa Malinyi.

Katika mtafaruku huo kuna mafuvu, vyungu vya kupikia nyama za watu, mikono ya biashara ya watu waliokufa ilipatikana. Kuna sababu nyingi za uchawi lakini nyingi ni za kiuchumi zaidi hasa kupata msukule, mifugo, mavuno na kimantiki majina haya ya msukule, ndondocha na kizuu yanaashiria mambo yaliyopo katika jamii na yote haya ni mashauri ya kiuchumi. Kuna mauaji yanafanyika katika Nyanda za Juu na Kanda ya Ziwa, siri kubwa ni uchumi watu wanataka kupatiwa utajiri kwa kuchanganya dawa na sehemu za mtu aliyeuawa.

Maiti zinazokatwa sehemu za siri zinadaiwa kufanywa hivyo kuvutia biashara, kwa hiyo shauri la kiuchumi husababisha kukomaa kwa imani hizi za kishirikina. Sifa na ujasiri ni sababu nyingine ya kichawi huku starehe ikiwa ni ya mwisho.

Yapo maelezo kwamba wachawi wanatumia uchawi kuwafanyia fidhuli watu, kula nyama zao, kucheza uchi usiku na watu huwapora wake wenzao kwa kuthubutu kuua waume zao. Uchawi ni sehemu ya utamaduni na inaonekana wazi uchawi hustawi zaidi katika umasikini.

Kinjeketile alitumia uchawi kuhamasisha watu kupambana na Wakoloni je kwanini leo wachawi wasitumie kuleta maendeleo kwa jamii? Hii taaluma yao ya kuingia maeneo bila kujulikana, kuruka na taaluma nyingine nyingi walizonazo, ni kwa nini wasiwafundishe watu bila kificho?

Chanzo hiki hapa:
http://www.habarileo.co.tz/biasharaFedha/index.php?id=10036

6 comments:

Jacob Malihoja said...

Nitaisoma vizuri Makala hii baadae niona naweza kuandika nini, lakini kwakweli Imani hizi za Uchawi ndio chanzo kikuu cha mabalaa mengi hapa Duniani hususani nchini, ndio Chanzo cha Wenye Ulemavu wa Ngozi kukatiliwa, na matukio mengine ya kutatanisha ya mauaji. kMfano eneo la mbagala mwishoni mwa mwaka jana kichaa mmoja maarufu eneo la zakhem alikutwa amekufa hana nyeti na ulimi.. sasa hebu angalia.. unaweza alikufa mchwa wamechukua nyeti na ulimi?

Jacob Malihoja said...

Nimeisona hii mada vizuri, nachoweza kusema, uchawi ni matokea ya Uvivu, wivu, tamaa, Ubinafsi, kukosa ubinadmu na roho ya dhuluma. Masuala yoyote ya kichawi iwe ni kwa ajili ya kuleta maendeleo au mafanikio mahali fulani ni lazima nyuma yake pataambatana na dhuluma fulani kwa mwanadamu mwingine. Sayansi hizi za kisiri zinachangia kwa kiasi kikubwa sana katika kugombanisha na kudhulu wanadamu.

Nimekuwepo kule Rujewa, Mbarali, Mbeya Kata anakotoka Blogger Majid Mjengwa anayetoka Kijiji cha Nyeregete, kwa takribani mwaka mmoja hivi, Kata yenye watu Elfu 30, kati ya Februari 2009 na August 2009 walikufa watu takriban 9 katika mazingira ya kutatanisha, wengi wao wakikutwa katika mfereji unaopeleka maji mashamba ya Mpunga. Kibaya zaidi wananchi wa eneo hilo wanaona ni jambo la kawaida na wanaonekana kulidhika nalo kwani hakuna juhudi za kueleweka kukabili hali hiyo.

Anayeingia katika sayansi ya kinyutroni kutengeneza mabomu hawezi kutakiwa kuuwa ndugu yake ili apate elimu hiyo, wala hawezi kutakiwa kuchinja kuku mweupe, wala hawezi kuambiwa akaoge njia panda. Wala hawezi kuambiwa akamkae motto wa miaka mitatu, wala hawezi kuambiwa apelike nyeti za Kichaa, wala hawezi kuambia apelike mkono wa albino. Ni dhahiri atatakiwa kulipa ada ya mamilioni ya shilingi ama dola kupata elimu hiyo. Mtu huyu anafichwa na kulindwa kwa ajili ya ushindani tu wa kibiashara wa kidunia na hofu ya teknolojia kuangukia mikononi mwa watu wasio na mjadala kama kina Osama bin Laden.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Kuna msemo kuwa 'kila mtu ni kichaa, kinachotofautisha ni kiwango cha ukichaa alokuwa nao mtu'!

Na kwa mantiki hii, KILA MTU hata wewe uloandika hapa na wewe unayesoma hapo ni mchawi.

Kinachogomba ni kiwango cha uchawi wako ukikitofautisha na wenzako. Na pia kiwango hicho chaweza kuwa HASI ama Chanya.

Hichokilichoelezewa katika mada ni HASI lakini uchawi ni uchawi tu, uwe hasi ama uwe chanya.

Hasi-wenyewe mnaipeleka kwenye Ushetwani
Chanya-mnaipeleka kwenye Umungu ama utakatifu :-(

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ni nguvu tu

Anonymous said...

Huwezi amini mimi niliwahi kuitwa mchawi tena nilikuwa msichana mdogo ambaye bado nasoma shule, ni kisa kirefu nikikisimulia chote nitakuwa nimeiba nafasi yote kwenye blogu. Lakini hii ilinifanya niamini kuwa mtu yeyote aweza kuitwa mchawi hata kama hana uchawi, hajui wala hafuatilii. Kitu kilichonifanya nionekane mchawi wakati huo ni kufaulu kwangu shule, kufanya vizuri na kutodhurika na nguvu hasi zilizokuwa zinaelekezwa kwangu. Kwa hiyo mimi nilionekana ni mchawi mkubwa kuwashinda wao maana kila walipokuwa wanakwenda kwa waganga kuroga na kuomba mabaya yanikute, mimi kwangu yalikuwa yanatokea mema au tofauti na walivyokuwa wakiomba wao. Ni hadithi ndefu lakini mpaka leo hii bado wapo wanaoamini kuwa nina nguvu za ziada ama za kichawi au sijui wenyewe wanavyoona.

Niko njiani kuandika kitabu kuhusu masaibu hayo yaweza kuwasaidia wengine wasikate tamaa maishani na kujiamini.

Unknown said...

Usiye na jina wa 6 May hapo juu, naomba uwasiliane na mimi kwa email hii:

kaluse2008@gmail.com