Saturday, July 31, 2010

NIMEINGIA ARUSHA JANA KIMYA KIMYA!


Haya waungwana, nimeingia Arusha jana kimya kimya na safari hii nimesimama kilimo kwanza na nitajikita zaidi kwenye kampeni za nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha tunagawana kura za kishindo na muheshimiwa......

Naamini tunaweza iwapo nia na dhamira itakuwepo, kwani "Together change we can" Na Inshaallah Slaa ataingia mjengoni pale magogoni.

Thursday, July 29, 2010

WATANGAZA NIA WAMEANGUKIA PUA

Ni jambo la kufurahisha kwamba, kumbe wamezea mate tonge wako wengi, ni kama mchezo wa kuigiza vile au ile tamthiliya tamu ya Egoli. Kama mtakumbuka niliwahi kueleza kuhusu wale wakware wenye uchu anuai walioanza mchakato kabla ya kipyenga kupigwa.

Ni mada isemayo “Dalili hizi si za kweli” kama ungependa kujikumbusha mada hiyo, basi waweza kubofya hapa. Siku za karibuni wakaibuka tena wahafidhina tena kwa kasi wakitangaza nia, sijui ni baada ya kusikia kuwa Koero katangaza nia ya kugombea ubunge kule Arusha.

Wakionekana kuwa makini katika kuzicheza karata zao wakaibuka upya tena kwa kasi, nadhani walikuwa na ndoto za kufunga pingu za maisha na Mbunge…mweeeh Kalaghabahooo!! Yaani wanapiga honi kwa gari waliyopewa lifti??? . Maombi na Cv, zikatumwa, huku wengine wakijimwagia sifa lukuki, kwa tamaa ya kutaka kujimwayamwaya na kimwana…..safi hiyoooo…. Hebu Vuta pumzi msomaji

Nami nikaona huu ndio wakati wa kuweka mambo hadharani yaani HAPO SAWA…….jamanieeee waungwanaeeeeeee!!! Imekuwaje tenaaaaa!! Basi ipo hivi kuna maboksi matatu hapa, kulikoniiii….kaka zangu wakaibuka, lakini aliyeonekana kufuata nyayo za sheikh Wayaya wa kule Mwembe Chai ni kaka yangu mpenzi Markus Mpangala, lakini hata hivyo kaka yangu Chacha Ng’wanambiti na Fadhy Mtanga wakajaribu kuwa Nostradamus wa kudadavua mambo yajayo.

Si haba nikaweka angalizo tena……..Jamanieeee bado tu hamuhisi kitu kabisaaaaaa au mnayeyusha tuuuu!! Patamu hapo!!!….na hapo ndipo wakaibuka tena wadau na ndoto za alinacha……..wanguuuuu……wanguuuuu….nanunua bunduki mie…... najikokiiiii najikokiiii jamaniii salaaaaaleeeeee...…LOL

Kaazi kweli kweli,, na ndio maana nikasema kuwa kublog kuna raha zake, hasa pale unapowachezea shere wahafidhina………safi hiyoooo.

Nasema hivi, Mambo baaaado kabisa, kama ni siku, basi ndio kunapambazuka hata mawio haijafika waungwaaaaaa!!!, na lakini siwakatazi wadau kupiga jaramba maana hamuijui siku wala saa, kukaa benchi halafu ukaambiwa piga jaramba inatia matumaini mweeeeeh!!! kwa maana utukufu utawajia kama mwivi, na hapo ndipo mtakapokenua hadi jino la mwisho……chungu kapata kivunoooo!!! .Je ni nani ataangukiwa na utukufu huo, ni swala la kuvuta subira, lakini kwa kifupi ni kwamba, pamoja na wasifu wao maridhawa,.haikuwa tija kwangu, hivyo wameangukia pua…... wacheke wana mwanyaaaa!!.....LOL

Wera weraaaa, na sasa nawaomba tuelekeze fikra zetu katika kumpigia debe Dr. Slaa, ili kama mungu akipenda, Inshaallah….aingie pale mjengoni Magogoni…..... huku wanablog tukipiga jaramba pale Luthuli kwa mwendo wa kunyatia...... vijana wa mjini husema ..... mdomdo yaani kidogo kidogo.....….

Nasema hiviiiii kipenga bado kupulizwa, kwa hiyo watangaza nia vuteni subira……..... Vuteni Pumzi.......

Tuesday, July 27, 2010

BADO TU, HAMUHISI KITU?

Mchaga, anaishi Dar, umri miaka 34

Mmbulu, anaishi Arusha, Umri miaka 36

Mkinga, anaishi Dar, umri miaka 38

Unadhani huyu atakuwa ni nani?


Monday, July 26, 2010

Friday, July 23, 2010

MARKUS, HAYATI MWALIMU NYERERE ALIANDALIWA NA NANI?

Hayati Mwalimu wakati wa kudai uhuru

Nimesoma kwa masikitiko makubwa maoni ya kaka yangu, Paroko mstaafu Markus Mpangala, kuhusiana uamuzi wa vijana wengi kujiingiza katika siasa kwa wingi na kwa namna ya pekee tofauti na miaka ya nyuma.

Naomba niweke wazi kuwa uamuzi wangu wa kutangaza nia ilikuwa ni kutaka kuamsha ari kwa vijana ili wahamasike kugombea nafasi mbalimbali za uwakilishi hapa nchini. Binafsi naamini kuwa sisi vijana tuko timamu kabisa kuingia katika kinyang’nyiro hicho. Lakini kutokana na watu wenye maono yasiyo na tija kama ndugu yangu Markus, wanaanza kuwakatisha tamaa kwa maelezo kwamba hawajaandaliwa.

Lakini hata hivyo kuna jambo moja najiuliza, hivi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Rais wa kwanza wa nchi hii baada ya kujipatia uhuru kutoka kwa Waingereza aliandaliwa na nani?

Jambo moja muhimu linalopaswa watu kama Markus kulifahamu ni kwamba historia huwa haifutiki. Na ndio maana hata leo tunaweza kujua matukio muhimu yaliyoikumba nchi yetu kabla na baada ya uhuru.

Wakati ule tulipopata uhuru, tulikuwa na wasomi wachache sana ambao wengi wao walikuwa ni makarani wa wakoloni, lakini kutokana na vuguvugu la kutaka uhuru likiongozwa na wazee wa Dar es salaam ambao wengi wao hawakuwa na elimu ya kutosha wakati huo, lakini kwa kumtumia Mwalimu Nyerere walifanikiwa kwa kaisi kikubwa.

Baada ya uhuru wale waliokuwa wakiwatumikia wakoloni wengi wao wakiwa ni makarani ndio wakajikuta wakibebeshwa majukumu katika nafasi muhimu za uongozi ambapo walikuwa hawana hata uzoefu, wa kutosha katika uongozi wa juu serikalini hususana katika nafasi za uwaziri.

Leo hii kuna mabadiliko makubwa, vijana wengi ni wasomi waliobobea katika taaluma mbalimbali, na wana uwezo mkubwa wa kupambanua mambo kwa namna ya pekee, lakini kutokana na ufinyu wa kufikiri watu wanakaa na kudai kuwa vijana hawajaandaliwa. Je, kina Rashid Kawawa, Tewa Said Tewa, Mzee Opiyo, Mzee Kisumo, Bibi Titi Mohamed, Bi, Lucy Lameck, Bi, Thabidha Siwale na wengineo wengi waliandaliwa na nani?

Ikumbukwe kwamba wakati ule kulikuwa na changamoto nyingi, tofauti na sasa, lakini wenzetu hao walifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Leo hii vijana wanajitokeza kutaka kukushika nafasi za uongozi ili kuleta mapinduzi ya kifikra na kuleta tija hapa nchini, wengine wanaibuka na kusema kuwa hatujaandaliwa…….!

Bado nauliza, Je Hayati Mwalimu Nyerere aliandaliwa na nani?

Thursday, July 22, 2010

NIMETINGA JIJINI DAR KIMYA KIMYA!!!!!

Hii taswira ya Arusha nimeipenda sana

Hatimaye nimetinga jijini Dar kimya kimya, baada ya kurudisha fomu za kugombea ubunge kule Arusha. Kuna wadau wamedai kuwa, I am too young to be politician, lakini nasema hatishwi mtu hapa, kwani nani hapendi kusinzia mjengoni kule Dom….LOL.

Nitakuwa Dar kwa siku mbili tatu , lakini nitakuwa kifamilia zaidi, nikipata mibaraka ya wazazi katika kukabiliana na changamoto za kugombea kuteuliwa.

Naamini tuko pamoja……Je, hamjambo wasomaji na wanablog wenzangu?

Friday, July 16, 2010

FULANA YANGU

Muafrika halisi

Jana katika pita pita zangu katika viunga vya hapa Arusha nikakutana na hii fulana na ikanivutia hasa. Ilibidi nijisachi na kuinunua kwani ilinipa taswira ya Mwanamke wa Kiafrika halisi.
pamoja na mtandao kuwa Kimeo siku za hivi karibuni, lakini nimemudu kuiweka picha hii kibarazani kwangu ili niweze kushea na wanablog na wasomaji wa kibaraza hiki kisichoisha visa na mikasa. Labda niwaulize wasomaji wa kibaraza hiki, kama nimependeza au?

Wednesday, July 7, 2010

MTANDAO UNAPOKUWA KIMEO!


Ni Siku ya tatu leo mtandao umekuwa Kimeo hapa Arusha kiasi kwamba mawasiliano na wanablog wenzangu na wasomaji wa kibaraza cha Vukani yamekuwa adimu kweli.
Sina taarifa za masaibu yaliyoikumba TTCL mpaka kufikia kutunyima haki yetu ya msingi ya kuwasiliana na wapendwa wetu.

Naomba mwenye taarifa zaidi anijuze maana leo imenibidi nipate mawasiliano kwa jirani mwenye kutumia Satellite ili niwasabahi wasomaji wa kibaraza hiki.
Jamani msione kimya bado ningalipo, na kwa sasa niko kwenye mchakato wa KUTANGAZA NIA kupitia Viti maalum vya CHADEMA huku Arusha.
Naomba wahafidhina msije nitoa roho……….NATANIA TU….!!!!

Sunday, July 4, 2010

TAFAKARI YA LEO: WALIPOKUTANA WANABLOG HAWA, JE WALIPANGA AU ILIKUWA NI NASIBU TU?

Walipanga au ilikuwa ni nasibu tu?

Ilikuwa ni siku ya Jumamosi May 15, 2010, pale katika Hoteli ya Kimataifa ya nyota tano iitwayo Movenpick Royal Palm, ndipo mahali ambapo wanablog hawa walikutana.
Kusema kweli sijui hata mpango wa kukutana kwao uliandaliwa vipi, ila katika hali ya kustukiza kupitia kibaraza cha kaka Fadhy tukajulishwa kwamba wanablog wamekutana pale Movenpick. Unaweza kubofya hapa kujikumbusha

Ulikuwa ni mwanzo mzuri na nilidhani kwamba milango itakuwa imefunguliwa kwa wanablog kukutana na kubalishana uzoefu hasa pale itakapotokea wale walioko Ughaibuni wanaporejea nyumbani.

Siku za hivi karibuni nikapata habari kuwa wanablog wenzetu walioko huko ughaibuni wako hapa nchini. Habari ambazo sijadhibitisha kwa kuwa hazina vyanzo maalum ni kwamba, Profesa Mbele alikuwepo au bado yupo hapa nchini, na pia Godwin Meghji naye yupo hapa nchini, vile vile Profesa Matondo naye nasikia yupo hapa nchini na inasemekana baada ya kukaa hapa Arusha kwa siku kadhaa ameelekea Shinyanga kuwaona wazazi wake. Sina uhakika kama bado yupo au kesharejea huko ughaibuni.

Ni bahati mbaya kwangu kuwa sikupata bahati ya kukutana naye alipokuwa hapa Arusha kwa kuwa nilikuwa huko milimani upareni nilipokwenda kumuona bibi yangu Koero ambaye alikuwa ni mgonjwa.

Niliporudi Arusha nikawa kila siku najaribu kusoma mitandao mbali mbali hususana vibaraza vya kaka Fadhi Mtanga, Chacha o’Wambura Ng’wanambiti na kaka Chib bila kusahau kibaraza cha kaka yangu Shabani Kaluse, nikitarajia kuziona sura za wanablog hawa pamoja na ugeni huu wa wanablog wenzetu kutoka ughaibuni, lakini mpaka leo sijapata taarifa rasmi kama wanablog hawa walikutana ama la.

Ni jana usku nilipokuwa nimejipumzisha nikitafakari juu ya ukimya wa blog zetu hizi hasa katika kipindi huki muhimu cha kuelekea uchaguzi mkuu, na ndipo nikawa najiuliza hivi kukutana kwa wanablog hawa pale Movenpick lilikuwa ni jambo la kupangwa au ilikuwa ni nasibu (Coincidence) tu?

Bado natafakari………..