Friday, April 12, 2013

KUMBE WAMAKONDE WANAOGOPA KUFA...!



Inaelezwa kwamba Maziko Wamakonde huwa na maombi tofauti na yale yanayofuatwa na madhehebu mengine. Badala ya Sheikh au Kasisi kusoma dua, Wamakonde wana desturi ya kuieleza maiti maombi na maonyo ili marehemu huyo asije patwa na madhara wala asiandamwe na mikasa katika safari yake huko aendako, na pia ndugu wanaobaki nyuma wasikabiliwe na mabalaa na mikosi ya aina yoyote. Wenyewe wanaamini kwamba mabalaa huongozana, yaani likitokea moja hufuata la pili, la tatu na kadhalika. Kwa mujibu wa simulizi zao, kuna madai kwamba pale mambo hayo ya mila yanapopuuzwa vifo mfululizo hutokea katika familia husika.

Mkuu wa mazishi Huieleza maiti wakati wa maziko:

“Ndugu umeacha jembe, mshale, shoka, nyumba na kazi kwa hiyari yako mwenyewe, hakuna aliyekulazimisha kufunga safari hii, ile wewe mwenyewe umeazimia. Umetuacha sisi huku nyuma kwa hiyari yako mwenyewe, Hivi, ufikapo kwenye ukomo wa safari yako, ukaeleze yanayokuhusu wewe binafsi. Wakikuuliza  ‘Wako wanadamu wengine waliobaki?’ ukawajibu, ‘hapana.’ Ujitahidi kuwathibitishia kwamba ni wewe tu peke yako, hakuna mtu mwingine aliyebaki.”

Kwa maneno hayo, inadhihirisha wazi kabisa kwamba waliobai nyuma wanaogopa kufa. Ingawa wanajua kuwa kufa kupo, ila kama kunaweza kukwepeka basi ombi lao lisikilizwe! 

Hata hivyo inadaiwa kwamba mila hii bado inafuatwa na Wamakonde wa Msumbiji, tofauti na Wamakonde wa Tanzania ambao mila kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa  muingiliano wa makabila na dini hizi za mapokeo

GAZETI LA VUKANI ....!!!!!


Aisee, hata sikujua kwamba kuna gazeti linaitwa VUKANI

Thursday, April 11, 2013

HILI NENO, "MWANAUME NI KICHWA CHA NYUMBA," HUWAPA KIBRI SANA HAWA VIUMBE




Kuna jambo moja ambalo hufundishwa na viongozi wa dini mbalimbali, ambalo pia waumini hulihubiri vizuri kila mahali wapatapo nafasi ya kufanya hivyo. Nalo si jingine ni lile la ‘mwanaume ni kichwa cha nyumba,’ ikiwa na maana kuwa mwanaume ndiye mkuu wa nyumba au familia. Suala hili linazungumzwa kama kwamba, mwanaume kuwa mkuu wa familia ni jambo la kimaumbile, lakini pia huzungumzwa kama vile, ukuu huo ni tiketi ya mwanaume kuikandamiza familia au mke. 

Nijuavyo mimi, wanaume wengi kuwa wakuu wa nyumba au familia ni suala la mazoea zaidi kuliko maumbile. Kwa miaka milioni kadhaa, mwanaume amejikuta akiwa ndiye mkuu wa familia. Kutokana na mazoea haya, jambo hili limekuwa kama vile ni la kimaumbile, yaani haliwezi kubadilika au kubadilishwa.

Lakini mbona kuna wanawake ambao ndiyo wakuu wa familia na familia hizo zinakwenda vizuri tu. Lakini vilevile kuna wanawake ambao hawana waume na wanaongoza vyema familia zao. Kwa bahati mbaya kwenye jambo hili, ni kwamba, kumekuwa na msisitizo kuwataka wanawake wawaheshimu waume na siyo wanandoa kuheshimiana. ‘mwanaume ni kichwa cha nyumba, ndiye msemaji wa mwisho. Inabidi aheshimiwe.’ Kuna watu ambao bila aibu huzungumza lugha hii.

Ni kweli wanaume wanahitaji au wanapaswa kuheshimiwa. Lakini siyo wanaume peke yao, bali binadamu wote wanapaswa kuheshimiwa bila kujali wanafanya nini au wakoje. Kwa hiyo siyo kwa sababu ni wasemaji wa mwisho, basi wao ndiyo wanaopaswa kuheshimiwa. Kwa kuamini hivyo wanaume wengi wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuwakandamiza wake zao na hata watoto. ‘Mimi ndiyo msemaji humu ndani, nimesema sitaki, basi.’ Mara nyingi matumizi ya mabavu kwa namna hiyo hutumika.

Kuna haja kwa wanaume kujua kwamba, kuwa kwao viongozi wa familia hakuwapi ubora wa ziada. Wanawake nao wanapaswa kujua kwamba, kutokuwa kwao wasemaji wa mwisho wa familia, hakupunguzi hata chembe ya thamani ya ubinadamu wao, kwani binadamu na wanandoa wanapaswa kuheshimiana. 

Friday, March 9, 2012

MIKOBA YA MANUNUZI INAPOKUWA NA VIJIDUDU GEMS





Utafiti uliofanywa na profesa Charles Gerba wa chuo kikuu cha Arizona nchini Marekani umebaini kwamba wengi wetu hususan sie kina mama hatusafishi mikoba yetu tunayotumia kufanyia manunuzi sokoni. Kuna hii mifuko maarufu kwa jina la mifuko ya Rambo au wakati mwingine tunayo mikoba maalum ya Canvas ambayo tunaitumia kufanyia manunuzi. Mikoba hii huwa tunaitumia na kisha kuihifadhi kwa matumizi wakati mwingine.


Je huwa tunaisafisha mikoba hiyo au tunaitumia mara kwa mara bila kuifanyia usafi kwa usalama wetu?


Profesa Gerba ambaye ni mtaalamu wa masuala ya udongo, maji na mazingira, alichunguza na kupima zaidi ya mikoba 100 kwenye miji ya California na Arizona, na katika utafiti huo aligundua kwamba ni asilimia 3 tu ndio wanaosafisha mikoba yao. Katika utafiti huo aligundua mikoba mingi ikiwa na vijidudu hatari vya Coliform asilimia 50 na E. Coli asilimia 8

“Inashangaza kidogo kuona mtu anatumia mikoba hiyo kubebea nyama, mayai, mboga mboga ambazo hata hazijaoshwa vyema na makorokoro mengine ambapo yamesheheni vijidudu vya maradhi lakini haifanyii usafi mikoba hiyo, bali huiweka kwa matumizi wakati mwingine.” Alisema Mtaalamu huyo wa masuala ya udongo, maji na mazingira,

Profesa Gerba alishauri watu wawe wanaosha mifuko yao kwa sabuni na maji ya moto baada ya matumizi.



Saturday, March 3, 2012

SASA MIMI NI MKE WA MTU!




Asalaamu Aleikhum mabibi na mabwana – hii ni kwa ndugu zangu Waislamu

Shaloom – Hii ni kwa ndugu zangu Wakristo

Ni matumaini yangu nyote hamjambo na mnaendelea vyema na shughuli zenu za kila siku. Ni muda sasa sijaonekana humu Jamvini, na hiyo ilitokana na kutingwa na shughuli nyingi za kujiandaa na harusi yangu ambayo ilifanyika mwaka jana mwezi wa kumi.

Ni masikitiko yangu kwamba sikuweza kuwasiliana na wanablog wenzangu pamoja na wasomaji wa blog hii ya VUKANI, na hiyo ilitokana na kutingwa na mambo mengi yaliyojitokeza kwa kipindi hicho. Huyu mume wangu ni mtu anayependa usiri, hivyo hakutaka jambo hilo tulikuze saaana na kulifanya kwa mbwembwe. Tulifanya kasherehe kadogo sana ambako kaliwakutanisha ndugu wa pande mbili tu na baadhi ya marafiki wa karibu sana. Lakini pia ni vyema mkafahamu kwamba nimeolewa mkoani Kilimanjaro huko Marangu.

Baada ya harusi nilirejea kwenye pilika zangu za kusaka mkwanja, na kama mjuavyo kwamba biashara hapa nchini imebana sana, na watu wanakimbizana kutafuta masoko na hapo hapo tunapambana na TRA ilimradi shida mtindo mmoja.

Mume wangu alinishauri niache kublog, kitu ambacho sikuafiki, lakini baada ya kujadiliana kwa kina, tulikubaliana niendelee kublog, lakini nisimame kwa muda kwanza ili tuweze kusimama kibiashara na kuweka msingi wa maisha yetu kwani tulikuwa tunahitaji muda wa kuwa pamoja zaidi. Kwa sasa naitwa mama kijacho na niko mapumziko (Bed Rest) na ndio sababu nikapata muda wa kuandika na kuweka kitu hapa VUKANI.

Naomba mniwie radhi wote mliokwazika na kutowahabarisha juu ya harusi yangu, lakini nataka kuwahakikishia kwamba tupo pamoja.

Wednesday, November 30, 2011

WANAPOJIREMBA KUPITA KIASI INA MAANA GANI




Siku hizi, kuna ugumu wakati mwingine, kujua kama mtu ni mwanamke au ni mwanaume. Vijana na hata watu wazima wengi wanaume hujipamba sana kwa kutumia vipodozi, ambavyo kwa kawaida, vimekuwa vikitumiwa na wanawake. Kuna wanaume wanaopaka nyuso zao dawa za kung’arisha na kupambana kabisa na ndevu.


Hawa ukiwatazama nyuso zao ni kama za wanawake, kwani mwanaume mwenye uso mororo sana huonekana kama mwanamke kwa kiasi cha kutosha. Kuna wanaume wanaovaa hereni, bila hata kujua wazivae kwa namna gani. Uvaaji wa hereni kwa wanaume, ambapo inasemekana ulianzia kule Marekani, ulikuwa ukifanywa kwa sababu maalum na kwa namna maalum.


Kwa mfano kuna waliokuwa, au wanaovaa ili kuonesha upendeleo wao kimapenzi (kwa mfano ushoga) na wengine kwa sababu mbalimbali.Kwa kawaida mwanaume anapotoga sikio moja tu, hasa la upande wa kulia na kulivisha hereni, inamaanisha kwamba, mwanaume huyo ni shoga! Kwabahati mbaya hapa kwetu kuna vijana ambao hutoga sikio moja la kulia na bado wanaamini kwamba, wako salama. Ukweli ni kwamba siku akikutana na raia wa Marekani wanaotafuta mashoga, hawatasita kumwita na kumtongoza.


Ndio maana yake, kwani nyie mlidhani vipi?Kwa kawaida wanaume wamekuwa wakikataa kuvaa mapambo na kujipodoa kama wanawake katika kuonesha kwamba, mwili wao hauhitaji vitu hivyo kwani ni mwili wa kazi hususan za nguvu na hivyo mapambo hayawezi kuwa na maana kwao. Ndio maana najiuliza kujipodoa na kujipamba huku kwa wanaume na kuvaa hereni na makorokoro mengine yanaashiria jambo gani?




Friday, September 30, 2011

MABALAA HUMUANDAMA MTOTO WA KIKE TANGU AKIWA TUMBONI………!






Tatizo hili hufahamika kama Female Infanticide, yaani mauaji ya kukusudia yanayofanywa kwa mtoto wa kike. Achilia mbali kile kitendo cha mtoto kuuawa muda mfupi tu baada ya kuzaliwa, utelekezwaji wa mtoto wa kike mara tu anapozaliwa na kutoa mimba baada ya ugunduzi kwamba, ni mtoto wa kike, zote ni njia za kumuondoa mtoto wa kike duniani. Tatizo hili liko katika jamii zote zinazomchukulia mtoto wa kike kama balaa na yule wa kiume kama Baraka kwa familia.


Kwa hapa nchini mtoto wa kike huuawa kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Watoto wa kike hudharauliwa na kuachwa linapokuja swala la elimu katika familia. Ukichunguza hata wewe utabaini kwamba, katika familia nyingi, ambapo watoto wa kiume wamepata elimu bora, watoto wa kike katika familia hizo wamepuuzwa na hata kutopewa kabisa elimu.


Watoto wa kike, haswa wale wanaozaliwa nje ya ndoa wametelekezwa kirahisi, wamekataliwa na baba zao kirahisi, ukilinganisha na watoto wa kiume. Idadi ya watoto wa kike wanaokufa kutokana na kutelekezwa na kukataliwa na baba zao ni kubwa kuliko ya watoto wa kiume. Hata zile kesi nyingi za watoto kukataliwa na baba zao zinahusisha watoto wa kike zaidi.


Ni jambo la kushangaza kwamba ndoa ambayo ina watoto wa kike watupu hutazamwa kwa bezo na dharau ukilinganisha na ile yenye watoto wa kiume watupu. Hata wale wanawake wanaozaa watoto wa kike watupu hujihisi vibaya na kuamini kwamba walistahili kuzaa watoto wa kiume pia.


Kwa maeneo ua vijijini na katika familia masikini, watoto wa kike hutazamwa kama, ‘biashara ya kesho’ ambapo watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa hiyo thamani yao ni kuolewa, ni ile ya kibidhaa na sio kibinadamu. Na ndio maana mtoto wa kike anaposhindwa kuolewa huanza kuonekana kama mzigo usio na thamani, na hata kuzongwa hutokea.


Ili kujinasua na tatizo hili, msichana huenda kwa mwanaume yeyote kama kwa kujilazimisha. Kila mtu anajua kuhusu wazazi hapa nchini, ambao wamekuwa wakiwalazimisha binti zao kurudi kwenye ndoa za mateso kwa hofu ya kurejesha mahari. Kinachotokea ni binti hao kuuawa na waume zao. Ni wazi hii ni njia ya makusudi ya kuwapunguza wanawake, bila kujali mtu ataieleza vipi……………….


Chanzo........Jamii Forum


Monday, September 5, 2011

MCHUMBA ANGU YUKO FINLAND!

Naelekea Uzeeni sasa!




Ni miaka 16 sasa tangu nifahamiane naye, alikuwa ndio kwanza amemaliza kozi yake ya uhasibu na kuajiria katika ubalozi wa mmojawapo ya nchi za Ulaya hapa nchini.


Alipoanza kujitegemea, alipata nyumba iliyoko jirani na nyumbani kwetu, na huo ukawa ndio mwanzo wa kufahamiana naye. Alikuwa akijiheshimu sana na hakupenda kujichanganya na watu. Alitumia muda wake mwingi nyumbani kwake na kama akiamua kutoka mara nyingi alipenda kuwatembelea ndugu zake a marafiki zake waishio maeneo ya mbali.


Nilibahatika kufahamiana naye wakati fulani ilipotokea shida ya maji, na kwa kuwa, nyumbani kwetu kulikuwa na kisima, alikuja kuomba msaada wa maji na huo ukawa ndio mwanzo wa kufahamiana.


Naam, urafiki wetu ulimea na kukua, kiasi kwamba tulikuwa tukitembeleana mara kwa mara, alitokea kufahamiana na wazazi wangu pia na walimkubali sana, kutokana na jinsi alivyokuwa akijiheshimu.


Jambo moja lililonishangaza, ni kwamba sikuwahi kumsikia akizungumzia juu ya mahusiano yake, nilishikwa na udadisi na siku moja nikamuuliza kma anaye mchumba. Alinijulisha kuwa mchumba ake yuko Finland kwa masomo, nilimdadisi zaidi kama yuko huko kwa muda gani, akanijibu kuwa ni miaka miwili sasa. Alinijulisha kuwa mchumba ake huyo anasoma kule na itamchukua miaka 3 hadi kumaliza masomo yake na ndipo atarejea nchini na kuungana naye.


Ukweli ni kwamba rafiki yangu huyu alikuwa akifuatwa na wanaume wengi tu tena wa kutosha wakitaka kuwa na uhusiano naye, nadhani ni kwa sababu alikuwa ni mrembo sana, lakini alikuwa akiwakataa kwa maelezo kwamba, anaye mchumba tayari ambaye yuko nje ya nchi kwa masomo.


Nilimuheshimu sana kwa msimamo wake. Mwaka uliofuata binti yule alihama katika numba ile na kuhamia maeneo ya Sinza. Nilipoteana naye kwa takriban miaka 16. Ni hivi karibuni nimebahatika kukutana naye, alionekana dhahiri kuwa umri umekwenda.


Alinikaribisha nyumbani kwake maeneo ya Kimara, alinijulisha kuwa amebahatika kujenga nyumba yake mwenyewe. Wiki iliyofuata nilimtembelea nyumbani kwake. Alikuwa amejenga nyumba nzuri na alikuwa ameizungushia ukuta na kuweka geti. Alinikaribisha sebuleni kwake. Alinitambulisha kwa mdogo wake wa kike aliyekuwa akiishi naye ambaye alikuwa akisoma Chuo Kikuu Dodoma, na pia kwa msichana wake wa kazi.


Nilishikwa na udadisi wa kutaka kujua alipo mume wake, na labda kama ana mtoto. Alicheka sana na kisha akanishika mkono na kunipeleka chumbani kwake. Alikuwa na chumba kikubwa chenye nafasi ya kutosha na pia kulikuwa na meza kubwa ambayo ilikuwa imepambwa vizuri na vifaa vya ofisini pamoja na lap top, kwa ajili ya kazi zake.


Aliniacha kwa muda ili niridhishe macho yangu, kisha akaanzisha mazungumzo.


Mwenzangu, alianza simulizi yake, …….. unadhani kipindi kile wakati nakwambia kuwa ninaye mchumba na yuko masomoni Finland ilikuwa ni kweli, la hasha, haikuwa kweli, bali nilikuwa nadanganya tu kwa sababu sikutaka kusumbuliwa na wanaume. Si unajua wanaume wa siku hizi wanapenda kuwachezea wanawake!, sasa mimi kwa kuliepuka hilo nikaona nitumie mbinu hiyo ili kuepuka usumbufu. Nilibaki mdomo wazi….


Basi bi dada………… aliendelea…….. nilipohama pale Mikocheni, na kuhamia Sinza, niliendelea na msimamo mwangu, sikuwapa wanaume nafasi, nilikuwa na malengo yangu na nilitaka nihakikishe yanatimia.


Ni malengo gani hayo…… nilimdadisi……


Kwanza, nilitaka nijenge nyumba yangu mwenyewe, na pia ninunue gari na kuanzisha biashara zangu na sasa nimetimiza malengo yangu, sasa tatizo linakuja.


Tatizo gani tena………..nilimuuliza.


Sitongozwi na wanaume……… na wananiogopa!..............haki ya Mungu Koero, yaani nina wakati mgumu kweli.


Mh! Niliguna…… wewe unadhani tatizo ni nini? Nilimuuliza,


Sijui sababu, lakini, naona kama vile hakuna anayevutiwa na mimi, najitahidi kuongea na wanaume lakini tunaishia kupiga stori tu, na wengine wananitongoza lakini ni waume za watu. Mwenzio naogopa kweli, mpaka nimejenga wasiwasi kuwa labda nimelogwa.


Mh……….Nilishusha pumzi……….Vumilia dada Jane, utampata atakayekufaa, muombe sana Mungu, atakupa mume aliye mwema, nilimpa moyo.


Mh, Koero, umri huu? Unajua mwakani natimiza miaka 39, mwenzio nazeheka hivyo, atanioa nani…. Nimekuwa nikibadilisha makanisa kama nini, katika kuombewa na kote huko naona maombi yangu hayajibiwi.


Marafiki zangu karibu wote wameolewa na wanaishi na waume zao, mimi tu, sijui nina mkosi gani…. Nilimuona Dhahiri machozi yakimlengalenga….


Nilimpa moyo na kumshauri asikate tamaa. Nilimwambia arudi kwenye kanisa lake la awali na ajiunge na kwaya ikiwezekana ashiriki kwenye kamati mbalimbali za kanisa na zitakazomfanya akutane na watu mbalimbali. Nilimwonya awe makini sana na wanaume walaghai kwani wapo wengine wanawezakutumia mwanya huo kummimbisha na kumtelekeza.


Alikubaliana na mimi na tukamaliza mazungumzo yetu kisha nikaondoka kurejea nyumbani…….. mweh dunia hii……. Habari ya dada Jane si kwamba tu ilinishangaza, bali pia ilinisikitisha. Yaani zaidi ya miaka 16 aliishi kwa kusema uongo ili kuwakwepa wanaume! Alichokuwa akikiogopa kwa wanaume ni kitu gani hasa?


Nilibaki nikijiuliza maswali chungu mzima na sikupata majibu. Ndio maana mie nasema wazi, jamaniee sijaolewa na wala sina mchumba Mbeya, Lundu Nyasa, Marekani wala Ulaya, niko Single, ready to mingle….leteni maombi na sifa zenu mtajibiwa…………LOL


Friday, September 2, 2011

WANAUME BWANA, HIVI MKIONA UCHI WA MWANAMKE MNAPATA NINI?

Wanaume wengine hata wakiona hivi huchanganyikiwa!



Kuna wakati huko Berlin, nchini Ujerumani, kulikuwa na unesho ambapo wanawake walikuwa wakionesha maungo yao kwa malipo. Wanawake hao walikuwa wakionesha maungo hayo kwa wanaume ambao wanaamini kwamba, kuona sehemu uchi wa mwanamke ndicho kilichowaleta hapa duniani.


Hebu sikia ujinga huo zaidi. Waandaaji wa onesho hilo ambalo lilihusisha wanawake wapatao 100 wa umri wa miaka 19 hadi 65 walilazimika kuwaita Polisi ili kudhibiti midume iliyokuwa ikifanya fujo wakati wa kukata tiketi kila mmoja akitaka awe wa kwanza kuingia kwenye onesho hilo.


Kila mmoja alikuwa akitaka awahi yeye kuona sehemu za siri ambazo bila shaka mkewe na watu wengine wa jinsia ya kike wanaomzunguka wanazo!


Mwandaaji wa onesho hilo, Vanessa Beecroft, ambaye ndiye mgunduzi wa njia hii ya kujipatia fedha kirahisi kutoka kwa wanaume hao wasio na haya, hufanya maonesho haya kwa jina la VB55 kwa nyakati na miji tofauti Ulaya.


Msije mkashangaa siku akija na huku Afrika kujichotea mamilioni ya dola, au akajitokeza mjanja mwingine huku Afrika na kuanzisha hayo maonesho, naamini wanaume watauana wallahi.

Monday, August 29, 2011

HATIMAYE MTUHUMIWA AJISALIMISHA!!!!



Haya jamani kilio cheni nimekisikia, jana ndio nimefika Dar nikitokea Tanga, Nilikuwa Tanga, kwa dada yangu ambaye alifanikiwa kuongeza idadi ya watu hapa duniani mwezi uliopita. kwa kuwa hakuwa na mtu wa kumsaidia, nililazimika kwenda kule kumpikia uji na mtori.

Nimerudi na tupo pamoja.


Monday, June 20, 2011

NIMEULIZWA TENA HILI SWALI: KWA NINI NILIAMUA KUITA BLOG YANGU VUKANI?

Vukani


Blog hii itakuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo. Pamoja na yote naamini pia italeta changamoto na migongano ya mawazo, ndio maana nikasema VUKANI.




KWA NINI NILIAMUA KUIITA BLOG YANGU, VUKANI?


Neno VUKANI nimelitohowa kutoka katika lugha ya mama yangu ya kipare.
Neno hili lina maana ya AMKENI, nadhani kaka Mkodo Kitururu atakuwa anafahamu vizuri kwa kuwa ni lugha yake.

Nakumbuka wakati fulani nilikwenda likizo kijijini huko upareni kuwasalimia bibi na babu yangu wanaomzaa mama yangu, basi kila siku asubuhi bibi alikuwa na kawaida ya kutuamsha ili tusali pamoja na alikuwa akitumia neno Vukani. Nilipouliza maana yake nikaambiwa ni Amkeni au kwa msisitizo wa kiingereza WAKE UP. Basi kuanzia siku hiyo nikatokea kulipenda sana hili neno, sijui ni kwa nini lakini lilikuwa linanihamasisha sana kuamka kifikra badala ya kuamka asubuhi tu.

Wakati nilipokuwa nafungua Blog yangu nilikuwa tayari nimeshachagua jina hili, na cha kushangaza nilipoliingiza kwenye mtandao nikagundua kwamba neno hili linatumiwa na makabila mawili ya Ki Zulu na Ki-Xhosa ya nchini Afrika ya Kusini, likiwa na maana moja, yaani Amkeni.

Si hivyo tu bali pia lipo gazeti moja maarufu nchini humo, linaloitwa Vukani.

Kwa maelezo zaidi bofya hapa.

Amkeni nionavyo mimi sio kuamka kutoka usingizini tu bali ni kuamka kifikra na kuhoji kila tulichofundishwa au kuambiwa kama kina ukweli kiasi gani? Si hivyo tu bali pia ni kuamka na kuachana na ile tabia ya kufikiri kwa mazoea na kutenda kwa mazoea. Kila jambo unalolifanya ujue sababu ya kufanya hivyo, sio eti kwa sababu, mama, baba, bibi, babu, mjomba, shangazi, na jamii iliwahi kufanya hivyo.

Nakumbuka wakati fulani nilihudhuria semina ya mambo ya uongozi, basi yule mwezeshaji kutoka nchini Marekani alitutolea mfano mmoja wakati alipokuwa akitufundisha namna ya kuepuka kufanya mambo kwa mazoea.

Kisa chenyewe ni hiki:

Kulikuwa na mama mmoja alikuwa na tabia, kila akitaka kuoka samaki ni lazima amkate mkia kabla ya kumuweka kwenye kikaango, ndipo amuoke. Hata kama samaki mwenyewe ni mdogo.


Siku moja binti yake aliyekuwa na umri wa miaka 10 akamuuliza mama yake sababu ya kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka, mama yake akamjibu kuwa mama yake alikuwa na kawaida ya kufanya hivyo. Alipomuuliza kama aliwahi kumuuliza mama yake sababu ya kufanya hivyo, mama yake akajibu kwamba hakuwahi kuuliza.

Basi wakati fulani bibi yake alipokwenda kuwatembelea, kama bahati mama yake alikuwa akiandaa samaki ili amuoke kama ilivyo kawaida akamkata mkia, binti akaona huo ndio wakati muafaka wa kuujua ukweli maana bibi yupo. Ndipo akamuuliza sababu ya mama yake kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka.

Si mnaona watoto wa wenzetu walivyo wadadisi?

Bibi akamwambia akamuulize mama yake sababu ya kufanya hivyo, yule binti akamjibu bibi yake kwamba, mama yake alimwambia kuwa yeye yaani bibi, ndiye aliyemfundisha kukata mkia wa samakai kabla ya kumuoka. Yule bibi akafikiria kidogo, kisha akamjibu, kwamba alikuwa akikata mkia wa samaki kwa sababu kikaango chake kilikuwa ni kidogo, hivyo ili samaki aweze kuenea kwenye kikaango alikuwa analazimika kukata mkia.

Yule binti akamwambia bibi yake, “Mbona sisi kikaango chetu ni kikubwa na isitoshe tunavyo vikaango vingi tu vya saizi tofauti tofauti, je kuna ulazima gani mama aendelee kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka?

Bibi akamjibu kwamba hakuna ulazima wowote.
Basi kuanzia siku hiyo yule mama akawa hakati tena mkia wa samaki.

Si mnaona jinsi mtoto huyu alivyokataa kulishwa kitu bila ya kijua sababu?
Naamini kwamba wote mtakubaliana na mimi kwamba sisi tumelelewa hivi, tunaambiwa tukate mikia ya samaki kabla ya kuwaoka na tunafuata, na wala hatuulizi sababu.

Kwa hiyo ninaposema VUKANI ninamaanisha AMKENI, ili muweze kuhoji baadhi ya mambo tunayofundishwa au kuambiwa ambayo hayana mantiki.


Monday, June 6, 2011

AKATUPA KILE KIATU!

Akakitupa hapa!




Alikuwa yuko Bar moja maarufu iliyoko maeneo ya Kinondoni hapa jijini Dar na hawara yake ambaye ndio nyumba yake ndogo pamoja na marafiki zake kadhaa wakikata maji (Pombe), Bwana Tesha (sio jina lake halisi) alikuwa na furaha siku hiyo kwani alikuwa amefanikiwa kupata tenda moja ya bajeti kubwa ambayo ilimhakikishia kupata faida ya kutosha.




Bwana Tesha anamiliki kampuni yake ya Ujenzi hapa jijini na alikuwa bado ni kijana mdogo, lakini kwa muda mfupi tangu amalize masomo yake ya Chuo Kikuu pale Mlimani alimudu kujiajiri katika sekta ya ujenzi na kupata mafanikio makubwa katika sekta hiyo.



Akiwa bado anakata maji na marafiki zake pamoja na hawara yake alipigiwa simu na mkewe. Kwa kuwa kulikuwa na kelele za walevi katika Bar hiyo aliamua kwenda kupokelea simu ile ndani ya gari lake. Simu ile haikuwa na taarifa nzuri, alijulishwa na mkewe kuwa mama mkwe wake yaani mama wa mkewe amefariki ghafla kwa presha huko Moshi mkoani Kilimanjaro.


Alirudi kwenye meza aliyokuwa amekaa ma wenzie na kuwajulisha juu ya taarifa ile, wenzie walimpa pole na kumshauri arudi nyumbani ili kumfariji mkewe. Hata hivyo alilazimika kwanza kumpeleka hawara yake nyumbani kwake maeneo ya Mwenge ndipo aende nyumban kwake maeneo ya Mbezi ya Kimara.



Wakati huo hawara yake alikuwa amelewa chakari na alikuwa hajitambui, hivyo ilimlazimu kumbeba na kumuingiza ndani ya gari yake aina ya Toyota RAV 4. Aliondoka hadi kwa hawara, aliteremka na kufungua mlango wa nyumba kisha akambeba hawara yake ambaye alikuwa hajitambui hadi ndani na kumlaza kitandani. Kwa kuwa alikuwa na funguo za akiba, alifunga mlango na kuondoka zake kuwahi nyumbani kwake.



Alifika nyumbani kwake majira ya saa nne usiku, na kukuta baadhi ya ndugu zake na ndugu wa mkewe. Baada ya mashauriano, walikubaliana yeye na mkewe waondoke kesho alfajiri, kwa kuwa yeye hahitaji kuomba ruhusa kazini.


Baadhi ya ndugu zake na ndugu wa mkewe alipanga kuondoka baadae na mabasi baada ya kuomba ruhusa kazini kwao. Walifungasha haraka haraka usiku huo huo kisha wakalala. Ilipofika alifajiri ya saa kumi za usiku waliondoka kuelekea Moshi. Ndani ya gari walikuwa wanne, mwanae wa kwanza wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 12 alikaa kiti cha mbele, mkewe pamoja na mwanae mwingine wa pili wa kike aliyekuwa na miaka 7 walikaa kiti cha nyuma. Kwa kuwa bado walikuwa na usingizi, wote walilala, na kutokana na ufinyu wa nafasi mama aliweka miguu yake katikati ya viti vya mbele na kujiegemeza kwa nyuma akimuacha mwanae wa kike amlalie mapajani mwake.



Mzee Tesha aliendesha gari kwa tahadhari sana ili kuepuka ajali. Wakati kunapambazuka alikuwa amekaribia maeneo ya mto Wami, na alijisikia kubanwa haja ndogo. Alilazimika kusimama na kuteremka ili kuchimba dawa. Alimaliza kuchimba dawa na kurejea ndani ya gari, lakini kabla ya kuondoa gari akashangaa kuona kiatu kinachofanana na kile alichovaa hawara yake usiku wa jana kikiwa chini ya kiti cha mbele cha abiria. Bwana Tesha akashtuka, akajua kile ni kiatu cha hawara yake ambaye atakuwa amekiacha mle katika gari kwa kuwa alikuwa amelewa chakari. Akageuka na kumwangalia mkewe aliyekuwa amelala kiti cha nyuma.



Aliwakagua wote ili kutaka kujua kama wamelala, na alipohakikisha kuwa wote wamelala, alikichukua kile kiatu na kukitupilia mbali, kisha akaondoa gari, akiwa amefarijika kuwa kiatu kile hakijaonwa na mkewe ambaye wanaaminiana sana tangu waoane miaka kumi iliyopita.


Aliendesha gari kwa mwendo wa wastani na ilipofika saa nne asubuhi walikuwa wako Segera, walisimama pale ili kupata staftahi. Baada ya kupaki gari aliteremka na wanae wawili na kutangulia mghahawani na kumwacha mkewe nyuma akijiweka sawa kabla ya kuteremka ndani ya gari.



Akiwa ndani ya mghahawa mkewe alimpigia simu na kumtaka aende kwenye gari kuna dharura, alitoka mghahawani na kumfuata mkewe kule kwenye gari, ili kujua kulikoni. Alipofika, alishtuka kumkuta mkewe kashikilia kiatu kimoja kinachofanana na kile alichokuwa amevaa hawara yake usiku wa jana walipokuwa kule Bar, akajua siri imefichuka, lakini akawahi kuficha mshtuko wake, na kumuuliza mkewe, “Vipi kuna nini mke wangu?”


Mkewe akamwambia kuwa ameshangaa haoni kiatu chake kimoja. Bwana Tesha akajua kiatu kisichoonekana ni kile alichokitupa kule mto Wami. Lakini alikuwa mwerevu….




“Mke wangu ana uhakika ulivaa viatu vyote viwili?” Alimuuliza mkewe akiwa na mshangao.



“Mume wangu pamoja na kuwa nimefiwa na nina uchungu sana lakini sijapoteza fahamu zangu kiasi cha kujisahau na kuvaa kiatu kimoja.” Mkewe alimjibu kwa upole.


Bwana Tesha alijifaragua akijifanya anakitafuta kiatu cha mkewe kwa bidii hasa, baada ya kupekua sana alikuja na ushauri mwingine, ambapo alimshauri mkewe wanunue kandambili avae kwa muda kwa madai kuwa wakifika Moshi watakitafuta kwa umakini.



Mkewe alikubali, lakini bado alikuwa na mashaka kidogo juu ya tukio lile. Walinunua kandambili na baada ya kupata kiamsha kinywa waliondoka. Walipofika Korogwe, Bwana Tesha alisimama na kwenda dukani ambapo alimnunulia mkewe Viatu vingine kisha wakaondoka kuwahi Mazishi.




Baada ya kufika Moshi habari ya upotevu wa kiatu kimoja ilisimuliwa na cha kushangaza tukio lile likahusishwa na mambo ya kishirikiana sambamba na msiba ule. Na hiyo ndio ikawa ndio salama ya Bwana Tesha kuepukana na fedheha ile ya kutupa kiatu cha mkewe baada ya kukifananisha na kiatu cha hawara yake.



Wednesday, June 1, 2011

AKANIAMBIA NIKIZEEKA NA KUWA BIBI KIZEE NISIJE NIKAMUOMBA UGORO!

Ni jana majira ya jioni nikikatiza mitaa ya Msasani, nikakutana na mateja wako wachafu wamekaa kijiweni wakipiga soga. Mara akaijitokeza teja mmoja na kuanza kuniita kwa sauti ya mlegezo (sauti ya mlegezo ni voice tone inayotumiwa na mateja), “Oyaa sister eee..hebu nisubiri basi nikuulize” mie sikumjibu wala kugeuka, niliendelea kuchapa mwendo.



Oyaa sister unajifanya uso wa mbuzi sio (hata sikumwelewa ana maana gani), niliendelea kuchapa mwendo bila kugeuka, na mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio kwa woga maana niliona dhahiri anaweza kunikaba, kwani nilipita vichochoroni.


Baada ya kuona simjibu wala kugeuka, akaanza kumwaga maneno ya kifedhuli…….


Unajifanya mzuuuri kumbe huna lolote, uzuri wenyewe uko wapi? Sana sana unatumia mgorogo tu, we nini bwana ….. unadhani tuna shobokea mademu sisi,…… shika time yako, huna lolote mshamba tu wewe……


Tena sikiliza…. Ukizeeka na kuwa bibi kizee usije ukaniomba ugoro, maana hamkawii nyie, ukizeeka na kimkongojo chako……(akainama kuonesha mfano wa bibi kizee na mkongojo) lazima utakuja tu …. Kisha akaanza kuigiza sauti ya bibi kizee na kusema, “Mzee naomba kaugoro hapo nitulize kiu yangu”


Sitakupa ng’oooo…….. Ishia huko………


Mie na watu waliokuwa karibu tulivunjika mbavu kwa kicheko, maana ilikuwa kama mchezo wa kuigiza vile.




Wednesday, May 25, 2011

NI MIAKA 26 SASA TANGU AZALIWE, LAKINI MIKASA, VISA NA VIJIMAMBO, VIMEENDELEA KUMTIA NGUVU.




Ilikuwa ni siku ya Jumamosi ya Sabato ya May 25, 1985, majira ya saa nne usiku ndipo binti huyu alipozaliwa. Alizaliwa akiwa na afya njema na uzito wa kuridhisha, ambapo siku iliyofuata mama wa binti huyu aliruhusiwa kutoka na kurejea nyumbani na kichanga chake.


Kalikuwa ni katoto kazuri ka kike ambako kalileta faraja katika familia ile ambayo tayari ilikuwa na watoto watatu wa kike na wawili wa kiume na hivyo kakawa kameongeza idadi ya watoto wa kike na kuwa wanne na kufanya idadi ya watoto katika familia hiyo kuwa na watoto sita.


Naambiwa kuwa binti huyu alikuwa na kipaji cha ajabu, hadi kiliwatisha wazazi wake, zile hatua za makuzi ya mtoto alizipitia lakini akiwa amewahi zaidi, kwa maana ya kuwahi kukaa, kusimama, kutembea na hata kuongea.


Akiwa na umri wa miaka miwili, tayari alikuwa amemudu kuwasha luninga na kubadilisha channel atakavyo, na si hivyo tu, alikuwa ni mdadisi na alikuwa ni mtoto anayependa kujifunza kila jambo.


Binti yule aliendelea kukua kwa umri na kimo huku akiwa na afya njema. Ni pale alipofikisha umri wa miaka mitano ndipo jambo lisilo la kawaida lilipomtokea binti huyu na kubadilisha kabisa historia ya maisha yake.


Inasimuliwa kuwa ilikuwa ni majira ya usiku ndipo binti huyu alipopatwa na homa kali sana, ambayo iliambatana na kile kinachoitwa degedege.


Kuumwa ghafla kwa binti yule kuliistua familia ile, na katika jitihada za kutaka kuokoa maisha yake alikimbizwa hospitali ya binafsi iliyopo jirani na pale kwao.


Alipofikishwa Hospitalini mama wa binti huyu alishauriwa na Daktari amkande na maji ya baridi ili kushusha joto la mwili ambalo lilikuwa limepanda kiwango cha kutisha. Daktari yule alitoa ushauri kuwa itakuwa ni jambo la hatari kuanza matibabu huku mgonjwa akiwa na joto kali kiasi kile.


Kwa kuwa Daktari alikuwa amemaliza zamu yake aliondoka nakuacha maagizo kwa Daktari na Muuguzi waliokuwa zamu akiwaelekeza hatua za kuchukua kulingana na maelekezo aliyoyaandika kwenye cheti.


Baada ya joto la mwili kupungua mama alimwita yule Muuguzi wa zamu na kumjulisha kuwa joto la mwil limepungua. Yule Muuguzi akiwa bado ana hali ya kuonesha kuwa katoka usingizini alisoma cheti na kisha akaenda kuchukua dawa.


Alirejea akiwa na vichupa vya dawa na sindano, na kumchoma sindano binti yule. Ile sindano ilisababisha binti kupoteza fahamu. Kuona hivyo alikimbia kumwita Daktari wa zamu.


Daktari wa zamu alipofika alimpima binti yule na kutoa maelekezo achomwe sindano nyingine haraka na kisha atundikiwe Drip. Maelekezo ya daktari yalifanyiwa kazi lakini binti yule hakuzinduka, ilibidi zifanyike Juhudi za kumhamishia Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ambapo alipelekwa moja kwa moja chumba maalum kwa wagonjwa mahututi (ICU). Alikaa kule kwa siku tano, na alipopata nafuu, akarudishwa kwenye wodi ya watoto na kuendelea na matibabu.



Binti aliendelea kupata nafuu, lakini kulikuja kugundulika kuwa amepatwa na tatizo lingine, nalo ni la kupoteza uwezo wa kusikia. Juhudi za Madaktari wa masikio kumtibu binti huyo zilishindikana, lakini mwishowe wakasema kuwa lile ni tatizo la muda tu, na limetokana na sindano ya kwinini aliyochomwa katika zahanati aliyotibiwa awali, hivyo ikiisha nguvu atarudisha uwezo wake wa kusikia.


Habari ile haikuwafurahisha wazazi wa binti, lakini wafanye nini, na limeshatokea. Walisubiri kwa taktiban mwaka mzima, lakini hapakuonekana dalili yoyote ya kupona wala kupata nafuu. Ni dhahiri sasa walizidi kupata wasiwasi, kwani binti yao kipenzi alikuwa hana uwezo wa kusikia na ule uchangamfu, udadisi, na utundu aliokuwa nao, ulitoweka. Hali hiyo iliwanyima usingizi.


Hawakukata tamaa, wakageukia kwenye maombi, lakini maombi yao hayakujibiwa haraka kama ambavyo watu wengi wangependa. Wakakata shauri kwenda nchini Afrika ya Kusini, kwa matibabu zaidi. Walipofika kule, Daktari aliyewapokea, alimfanyia binti vipimo na kwa kushirikiana na Madaktari wenzie walitoa pendekezo wamfanyie binti upasuaji, ili kurekebisha ile hali.


Lakini siku iliyofuata, ambapo ilikuwa afanyiwe vipimo zaidi kabla ya upasuaji, yule Daktari alibadilisha uamuzi na badala yake akatoa pendekezo binti anunuliwe vifaa vya kumuwezesha kusikia, (Hiring aid) halafu baada ya mwaka mmoja warudi kwa ajili ya vipimo zaidi.


Kwa kifupi walisema kuwa ni mapema mno kukimbilia upasuaji kwa kuwa waliamini kwamba kuna uwezekano mkubwa binti akapata uwezo wa kusikia baada ya dawa aliyochomwa kuisha nguvu.


Walirudi nchini, na kuendelea na maisha, na baada ya mwaka mmoja hali haikuonekana kutengemaa, waliporudi Afrika Kusini maelezo yalikuwa ni yaleyale. Waliambiwa warudi Tanzania na kama kutakuwa na tatizo basi waende Muhimbili, kwani tatizo la binti linaweza kutatuliwa hapo. Juhudi mbalimbali za kitabibu zimefanyika lakini bado hazijazaa matunda.


Hali hiyo imemfanya Binti huyo kuwa mbali na mawasiliano ya simu hususan za mkononi akitumia zaidi Ujumbe wa badala ya kuongea, kutokana na tatizo hilo. Mawasiliano mengine anayopendelea anapotaka kuwasiliana na ndugu jamaa, wanablog, wasomaji wa blog na marafiki ni kwa kutumia barua pepe, kwani hiyo imemjengea marafiki wengi na amekuwa akiwasiliana nao kiurahisi zaidi.


Leo hii ni miaka 26 kamili tangu alipozaliwa binti huyu, na ni miaka 21, tangu alipopatwa na tatizo hilo ambalo ki-ukweli bado linaaminika kuwa lilisababishwa na muuguzi ambaye alimchoma sindano ya kwinini, badala ya kumtundikia Drip, kama alivyoandikiwa na Daktari aliyempokea binti huyo.


Bado anawaza ni wangapi baada ya mkasa wake wamepata matatizo kama haya? Ni wangapi wamesababishiwa maumivu, ulemavu na hata kifo kwa maamuzi finyu ya kutofuata maelezo ya Madaktari?


Anawaza ni wauguzi ama Madaktari wangapi ambao wametenda makosa kama haya na kuonywa ama kuwajibishwa kwa namna yoyote ile ili matatizo wanayosababisha kwa jamii yasiwe kitu kinachotokea kila mara?


Anawaza ni wangapi ambao tofauti na yeye hawawezi kuendelea na masomo kwa kuwa hawawezi kupata HEARING AID kulingana na gharama zake? Na hivyo kushindwa kuonyesha vipaji vyao halisi kwa matumizi ya nchi na dunia?


ANAWAZA namna ambavyo mimi nawe tunaweza kuwa suluhisho la matatizo haya ambayo YANAUMIZA SANA. ..........


Hata hivyo hali hiyo haikumkatisha tamaa kwani alimudu kusoma katika shule mbalimbali za kawaida huku akitumia vifaa maalum vya kusikia, ambapo alimudu kufika hadi kidato cha sita. Binti huyu hakutaka kuendela na elimu ya juu, na badala yake aliamua kujiingiza katika biashara akiwa ni mjasiriamali mchanga lakini mwenye matarajio makubwa.


Si hivyo tu, bali pia amekuwa ni mwelimishaji katika tasnia ya Blog akiwa anamiliki Blog yake ambayo imekuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo, lakini pia pamoja na yote anaamini kuwa blog hiyo imeleta changamoto na migongano ya mawazo, jambo lililowa “amsha” wengi na ndio maana akaiita VUKANI.


Hata hivyo hawezi kujivunia hapo aliopofikia katika tasnia ya Blog bila kuwataja wanablog wote wenye kumiliki blog za kiswahili, wasomaji wa blog, wazazi wake, marafiki na wale ambao kwa njia moja ama nyingine walifanikisha uwepo wa blog hiyo ya VUKANI. Hata hivyo HASITI kuwataja Kaka Markus Mpangala, kaka Mubelwa Bandio, na Dada Yasinta Ngonyani, hawa amekuwa akiwasumbua sana pale anapohitaji ushauri kabla ya kuweka bandiko katika kibaraza chake.


Asingependa kuwasahau Mzee wa Mataranyirato Chacha o'Wambura, Ngw'anambiti, Kamala Lutatinisibwa, Fadhy Mtanga, Christian Bwaya, Simon Mkodo Kitururu, Godwin Meghji, Evarist Chahali, Dada Subi, Faith Sabrina Hilary, Shaban Kaluse, Mwanamke wa Shoka Mija Sayi, Mariam Yazawa, Emuthree, Ramadhan Msangi, Salehe Msanda, Ma-Annonymacy............. na wengineo wengi, ambao kwa kweli wamekuwa mstari wa mbele katika kuifanya blog hiyo ya VUKANI kufikia hapo ilipo


WAKATABAHU


NI MIMI KOERO JAPHETI MKUNDI