Saturday, June 26, 2010

KINJEKITILE NGWALE NA HISTORIA YENYE UTATA!

Kulikuwa na mateso na kulimishwa kwa nguvu.

Leo katika kupekua kwangu mtandaoni, nimekutana na historia mbili tofauti zinazomzungumzia Kinjekitile. Kilichonivutia hadi kuamua kuwashirkikisha wasomaji wa kibaraza hiki ili tutafakari kwa pamoja ni kutokana na kupingana kwa historia hizo.

Wakati historia moja ikihoji kuwa Kinjekitile alikuwa shujaa au mshirikina? ambayo iliandikwa na mwandishi Aloyce Menda katika gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 21,2006, nyingine ilikuwa ikidai kuwa historia yake imepotoshwa, ambayo nayo iliandikwa na mwandishi Evaristy Masuha katika gazeti hilo hilo la Tanzania Daima la Alhamisi, Agosti 21, 2008.

Kwa historia hizo mbili kunaonekana kuwa na walakini na ni vyema historia hii ikawekwa sawa kwa manufaa ya vizazi vijavyo, la sivyo tutajikuta tukiwa tumepoteza kumbukumbu hii muhimu kwa vizazi vyetu.

Naomba tuwekane sawa katika swala hili, Je ni yupi yuko sahihi kati ya waandishi hawa wawili?

***************************************

KINJEKITILE - Jemedari shujaa kweli au mshirikina laghai tu?

Na Aloyce Menda

Ijumaa, Septemba 21,2006


'Wakoloni wa Kijerumani waliita Vita ya Majimaji kuwa ni uasi wa Majimaji au Majimaji Rebellion kwa Kiingereza. Kwa Wakoloni, Kinjekitile alikuwa mhaini aliyekuwa anapinga utawala halali. Kwa dhana hiyo, Kinjekitile alikuwa shujaa kwa kupigania uhuru wa watu waliokuwa chini ya ukoloni.

Lakini kwa kutazama kwa kina mbinu za ukombozi alizotumia kupigania huo uhuru, sioni ushujaa wake. Vitabu vya historia vilivyoandikwa na wakoloni na hata vya wazalendo vinaonyesha wazi kwamba Kinjekitile alilaghai mamilioni ya watu wasioelimika, kwamba risasi za moto kutoka katika magobore ya askari wa Kijerumani zinaweza kugeuzwa maji na kuishia kulowesha tu miili yao bila madhara yoyote.

Kinjekitile alilaghai watu kwamba yeye anafahamu sayansi ya kijadi itakayotumiwa na ‘watu wake’ katika vita dhidi ya Wajerumani na kushinda. Sayansi yenyewe aliifundisha yeye mwenyewe kilaghai na kuisambaza kutoka Kilwa hadi Songea.

Watu wengi wakapotoshwa na kuamini kwamba risasi za moto zitageuka maji katika vita, kasha wakahamasishwa kuanzisha vita bila kujiandaa kwa mbinu nyingine za ziada! Silaha zao za jadi zilikuwa ni mawe, marungu, mundu, pinde, mishale na mikuki butu. Hatari iliyoje hiyo!
Kinjekitile mwenyewe hakwenda mstari wa mbele katika vita halisi, wala hakudiriki kusitisha mapambano alipoona maelfu ya ‘watu wake’ wakiteketezwa kwa risasi. Badala yake, alikaa mafichoni huku akiendelea kutuma wasaidizi wake kushawishi watu waamini ulaghai wake, na kwamba waliokuwa wanakufa kwa risasi hizo ni wale tu ambao hawakutimiza vyema masharti ya ‘sayansi’ yake aliyowapa.

‘Shujaa’ Kinjekitile alikuwa tapeli hatari sana kiasi kwamba, hakuwa na himaya maalumu ya kuishi, tofauti na walivyokuwa kina Chifu Mkwawa, Mtemi Mirambo and Mangi Sina. Bila shaka alikuwa anafahamu fika kwamba siku moja ulaghai wake utafikia mwisho, ambapo watu wangemgeukia na kumtoa roho yake, hivyo alijihami kabla kwa kuishi mafichoni kama afanyavyo gaidi Osama bin Laden hivi sasa.

Vita ilipokaribia mwisho wake kwa wazalendo wengi kufa kama sisimizi, Kinjekitile alitokomea pasipojulikana na hadi leo haifahamiki ‘shujaa’ huyo alizikwa wapi.

Mamilioni ya wazalendo kusini mwa Tanzania walikufa kwa njaa, maradhi na kukosa makazi baada ya vita hii. Wakoloni wa Kijerumani waliteketeza mashamba yao, mifugo na nyumba na kuhakikisha wanavunja misingi yote ya kiuchumi kama mbinu ya kujihami dhidi ya ‘maasi’ mengine.’

Unaweza kubofya hapa ili kuisoma historia hii kwa undani

Vita ya Majimaji: Historia iliyopotoshwa

Na Evaristy Masuha

Alhamisi, Agost 21, 2008


‘Leo napenda kuchimba zaidi ukweli huo huku nikijarijbu kutoa ukweli mwingine ambao utathibitisha historia hii huku nikiendelea kuwakumbusha Watanzania ambao watakuwa aidha wamesahau au hawakupata nafasi nzuri ya kuijua vita hiyo iliyokuja kujulikana kama “Vita ya Majimaji”.


Vita hiyo ilianza Julai mwaka 1905. Pigano la mwisho lilifanyika katika maeneo ya mpaka wa Tunduru na Masasi katika Kijiji cha Lusesule.

Mwaka 1907 wakati vita hiyo iliyokuwa kati ya serikali ya Wajerumani na Waafrika waliochoshwa na utawala wa suluba ikiendelea, Waafrika ambao walikuwa ni muungano wa makabila ya kusini hadi pwani ya Tanganyika, walikuwa wakipiga mishale na mikuki yao huku wakitamka neno ‘mashe’.

Neno hilo lipo kwenye lugha ya Kimatumbi ambalo tafsiri ya Kiswahili, ni ‘maji’, kama walivyoelekezwa na kiongozi wao hayati Kinjekitile Ngwale. Hiyo ndiyo iliyokuja kuzaa jina la ‘majimaji’.

Mwisho wa vita, Waafrika walishindwa vibaya na wengi wao kuuawa. Hapo ndipo historia ikaja kumtambua Kinjekitile kama kiongozi wa vita aliyewaahidi askari wake ushindi kutoka kwenye dawa aliyoamini ingeweza kubadilisha risasi kuwa maji, kitu ambacho hakikuwa kweli.

Historia hiyo tuliipokea na ndiyo tunayowafundisha vijana wetu na inatamka wazi kwamba dawa haikuwa kweli, kwani hakuna risasi hata moja iliyogeuka kuwa maji na matokeo yake Waafrika wengi walipoteza uhai wao.

Hapo ndipo nakosoa historia hiyo kulingana na mlolongo wa matukio yaliyofuatia hadi mwisho wa vita hiyo ambayo mwanzo ilikuwa ya ushindi mkubwa kwa Waafrika.

Historia hii ina tuambia kuwa Vita ya Majimaji ilianza mwaka 1905 Julai na mwezi mmoja baadaye yaani Agosti 24, mwaka 1905 Kinjekitile alinyongwa katika Kijiji cha Mhoro, Rufiji.
Tangu hapo wapiganaji wa Kiafrika wakaendelea kupigana bila kiongozi wao hadi Januari 1907.

Kwa mtazamo kama huo, tunaweza kupata picha ambayo itatufikisha katika ukweli wa historia ambayo walio kuwa na jukumu au uwezo wa kuhifadhi historia hiyo walilifanya makusudi kabisa ili tuamini kile walichokitaka wao.

Mwanzo wa Vita ya Majimaji huko Umatumbini ilikuwa ni mwendelezo wa vita ya muda mrefu kati ya utawala wa Wajerumani na Wamatumbi ambao walikuwa wamechoka kabisa kutawaliwa.

Hiyo ilitokana na Wajerumani walioingia kama marafiki, kugeuka kuwa wakatiili. Waafrika walichukizwa na kitendo cha kufanyishwa kazi katika mashamba ya Wajerumani kutwa nzima bila malipo.


Hali hiyo ilijenga chuki kati ya Waafrika na Wajerumani, hivyo Wamatumbi walianzisha vita iliyokuwa ya Mzungu na Mwafrika popote pale walipokuwa wakikutana.
Hali hiyo ilishtukiwa na Wajerumani na hivyo wakaamuru Wamatumbi wote kuepukana na asili yao ambayo ilikuwa ni kutembea na fimbo au mkongojo kwani ilikuja kugundulika kwamba, mikongoja hiyo ndiyo ilikuwa ikigeuka silaha dhidi ya Wajerumani.

Hiyo ilikuwa mwaka 1896, baada ya serikali ya kikoloni kuweka mkazo na sheria kali dhidi ya Mmatumbi yeyote anayepatikana akitembea na aina yoyote ya mti. Mwaka 1898, Wamatumbi wakagundua mbinu nyingine ambapo sasa maboga waliyokuwa wakilima zaidi kugeuka kuwa silaha.

Wamatumbi ambao kwa asili walikuwa watu jasiri sana, walianza kupambana na kila Mzungu waliyekutana naye kwa kumponda kwa boga. Vita hiyo ambayo inajulikana kwa Kimatumbi kama ‘Ngondo ya Mayawa’, yaani vita ya maboga.

Staili hiyo iliwashitua Wajerumani ambao sasa walianza kupambana na Wamatumbi kwa mtutu wa bunduki pamoja na sheria za kufungwa na wengine kuhukumiwa kunyongwa. Hapo tena Mmatumbi akawa amekubali kushindwa.

Kwa mtiririko wa matukio kama hayo ambayo sasa yalielekea kuwakatisha tamaa Wamatumbi, ndipo mzee hodari na mganga maarufu sana kwa ukanda huo, mganga aliyekuwa na mifugo mbalimbali nyumbani kwake, ikiwamo nyoka na samba, alisimama na kuwaahidi Wamatumbi kuingia katika vita aliyoiita vita ya ushindi.

Mzee huyu ambaye vitabu vya historia vinamtambua kama Kinjekitile, ukweli halisi wa jina lake aliitwa Kinjeketile, yaani kimeniitikia kwa lugha ya Kimatumbi.


Kwa mjibu wa imani ya Wamatumbi, mzee Kinjekitile aliyewarejesha Wamatumbi katika roho ya ujasiri kutoka katika roho ya kukata tamaa, alizama ndani ya Mto Rufiji na kuibuka baada ya siku mbili, akiwa na mizizi ya dawa hiyo. Hiyo ilikuwa mwaka 1903.’

Unaweza kubofya hapa ili kuisoma historia hii kwa undani.

Saturday, June 19, 2010

KWA NINI KUWE NA ADIMIKO?

Nimejichimbia huku

Ni jambo la kusikitisha kuwa linatokea adimiko katika kipindi kibaya. Kipindi ambacho jamii inahitaji sana kuelimishwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Nimesema ni kipindi kibaya kwa sababu kwa kutumia maandishi yetu katika blog zetu hizi zisizoisha visa na mikasa tumekuwa tukiibua mijadala mbali mbali yenye kuelimisha kufundisha na kuchangamsha na kwa kupitia chagamoto hizo, wengi wamejifunza mambo mbalimbali yahusuyo jamii yetu hii, katika Nyanja ya kisiasa na kijamii kwa ujumla.

Adimiko langu halikuwa rasmi, lakini niliwahi kupita humu na kukiri huo udhaifu wa kuadimika pasipo taarifa. Lakini katika hali ya kushangaza nimeshangazwa na adimiko la baadhi ya wadau wenzangu katika vibaraza vyao kimya kimya na tusijue walipoelekea.

Hongera kwako kaka yangu Mubelwa Bandio kw akuliweka Adimiko lako hadharani na hivyo kuwatoa jakamoyo wadau waliozoea changamoto zako hapo kibarazani kwao.

Pia ningependa kuwapa pongezi wale wadau wanaoendelea kutupasha kwa habari motomoto za hapa na pale na kuifanya tasnia hii ya Blog kutodorora.

Ingawa Mwananchi mimi kaamua kutupa yanayojiri kule Afrika ya Kusini kunakochezwa Kombe la Dunia, na ninadhani alisoma alama za nyakati akajua kuwa, kama ataweka longolongo za Politics hatapata msomaji kwa sababu macho na akili za watu wote karibu dunia nzima yako huko Bondeni kwa Mzee Madiba Mandela wakifuatilia kinyang’anyiro hicho.

Mzee wa Mataranyirato yeye akamua kumuandikia mkewe barua ya wazi huku Kamala akijiuliza huyu Mungu ni nani jamani. Mzee wa Nyasa, inasemekana kajitwisha mshipi na sasa anavua dagaa huko ziwa Nyasa, lakini si haba anatupasha mawili matatu.

Kaka yangu Matondo naye nasikia yupo nchini na kajichimbia huko Arusha, nasikitika kwamba niko huku Milima ya upareni kumuona bibi yangu mwenye jina lake Koero na hivyo kukosa nafasi hii adimu ya kukutana naye na kupata Kahawa pale chini ya mti maeneo ya Sanawari kwenye Hoteli ya Naura.

Dada yangu Subi naye yupo analiendeleza libeneke lake pale Wavuti na kama kawaida yake hakosi kutupasha habari motomoto bila kukosa za kisiasa. Bila kumsahau dada yangu kwa mama mwingine Yasinta Ngonyani, naona na yeye kaanza mwendo wa kunyatanyata katika kublog. Sio kawaida kijiwe chake kudororra, lakini safari hii, mweh! amelala doro.....sijui ndio majukumu au ni kupisha kombe la Dunia!

Kaka yangu Bwaya, nakumiss sana, hivi ziko wapi zile fikra zako pevu zenye kutekenya ubongo? Kwa nini lakini uadimike kiasi hiki jamani? Please, Please I beg you, come back Bro! We miss you so much……………..

Ningependa kuchukua nafasi hii kuwaomba wadau wenzangu kuwa, chonde chonde tusipotee mtandaoni kwani tunahitajika sana na jamii kwa ajili ya kutoa elimu ya uchaguzi. Sisi pia ni sehemu muhimu katika kuleta mabadiliko ya uongozi hapa nchini.

Saturday, June 12, 2010

TAFAKARI YA LEO: TAFAKARI NA CHUKUA HATUA!

Hatukuafuata kanuni


JE HIVI UNAJUA:

Kwamba tofauti kati ya nchi masikini na nchi tajiri haitokani na umri ambao nchi inayo. Na hilo tunaweza kulitambua kwa kuangalia nchi kama India na Misri; ambazo zina zaidi ya miaka 2000 tangu kuwepo kwake hapa duniani lakini bado ni nchi masikini!

Kwa upande mwingine nchi kama Canada, Australia na New Zealand ambazo miaka 150 iliyopita zilikuwa ni nchi masikini na zisizohesabiwa kama nchi zenye uchumi imara, lakini leo hii ni nchi zenye maendeleo makubwa na tajiri sana.

Tofauti ya nchi tajiri na masikini haitokani na nchi kuwa na maliasili na rasilimali za kutosha.

Japan, ni visiwa vidogo ambavyo karibu asilimia 80 vimezungukwa na milima na haina ardhi ya kutosha kwa kilimo na ufugaji, lakini ni nchi yenye uchumi imara sana.

Ni nchi ambayo inaagiza malighafi kutoka nje na kuzalisha bidhaa mbalimbali na kuziuza karibu ulimwenguni kote.

Mfano mwingine ni nchi kama Switzerland ambayo hailimi zao la Cocoa, lakini ni nchi ambayo inazalisha bidhaa ya chocolate yenye ubora hapa duniani. Ni nchi ambayo inalo eneo dogo kufaa kwa ufugaji lakini wameweza kuwa wazalishaji wazuri wa mazao ya mifugo yenye ubora wa hali ya juu kama vile Jibini. Ni nchi ndogo ambayo ina usalama, sheria nzuri na hali njema ya kazi unaoifanya iwe nchi salama zaidi kuliko nyingine duniani.

Wakuu kutoka nchi zilizoendelea wanaowasiliana na wakuu wenzao wa nchi masikini wanaonesha kuwa hakuna tofauti kiakili.

Tukisema Rangi, Kabila au dini kuwa ndio kipimo cha tofauti ya nchi tajiri na msikini ni kujidanganya bure.

Wale wahamiaji kutoka nchi masikini ambao katika nchi zao walikozaliwa walionekana kuwa wavivu kupindukia ndio wazalishaji wakubwa katika nchi hizo tajiri.

Je tofauti yake ni nini hasa?

Tofauti ni mtazamo wa watu katika nchi hizo masikini, ambapo unachagizwa na elimu na utamaduni usio na tija ambao umekuwepo kwa miaka mingi.

Kwa kuangalia tabia na mienendo ya watu wa nchi zenye maendeleo na tajiri utagundua kwamba asilimia kubwa ya watu hao inafuata kanuni zifuatazo katika maisha yao.

Kanuni hizo ni hizi zifuatazo:

· Maadili
· Uadilifu
· Uwajibikaji
· Kuheshimu sheria na taratibu
· Kuheshimiana na hasa kuheshimu uhuru wa mtu mwingine
· Kupenda kazi
· Kujinyima na kuweka akiba na hatimaye kuwekeza katika biashara.
· Kujituma
· Kujali muda

Ni watu wachache sana katika nchi masikini wanaofuata kanuni hizo katika maisha yao ya kila siku.

Sisi sio masikini kwa sababu eti tuna uhaba wa maliasili/rasilimali au mazingira yaliyotuzunguka ni magumu.

Sisi ni masikini kwa sababu tuna tatizo la mtazamo na namna ya kufikiri.

Kama unaitakia mema nchi yako, basi sambaza huu ujumbe kwa watu wengi nchini kwako ili waujue ukweli huu:

Makala hii nimeitafsiri kutoka katika mtandao.
Chanzo hiki hapa:
http://www.mikebonnel.com/

Nakiri kuwa tafsiri ni yangu kama kutakuwa na mapungufu naomba mnivumilie
.

Monday, June 7, 2010

ETI MKUKUTA NI DAWA YA TUMBO NA UKIMWI!

Bado watu ni mbumbumbu kabisa!

Kwanza naomba radhi kwa kutoonekana mtandaoni kwa takribani wiki mbili sasa. Najua wale kondoo wangu waliozoea kupata neno kila Jumamosi watakuwa wamesononeka kutokana na mchungaji wao kutoweka neno la wiki juzi Jumamosi kama ilivyo ada.

Niko Arusha kwa sasa nikiendelea na juhudi za kifamilia za Kilimo Kwanza nikiwa nimejikita zaidi katika maeneo ya Karatu, kuliko na mashamba ya Mzee Mkundi.

Leo niko hapa Arusha mjini, nikiwa nimeamua kujipumzisha na kabla ya kurejea Karatu kesho kuendelea na shughuli za kilimo.

Ukweli ni kwamba sikupanga kublog kabisa, lakini nimelazimika kublog, baada ya kuangalia kipindi cha Uswazi kinachorushwa na TV ya East Africa yaani Channel 5.

Kilichonisukuma zaidi ni kutaka kujadili kile nilichokiona na kukisikia katika kupindi hicho ambacho kwa kweli kimeniacha mdomo wazi hadi hivi sasa.

Mtangazaji wa kipindi hicho Bwana Musa alikuwa akiwahoji vijana fulani katika maeneo ya Kinondoni ambao walikuwa kwenye maskani yao maarufu kama Camp.

Katika mahojiano hayo Musa aliwauliza vijana wale kama wanaelewa nini juu ya neno MKUKUTA.

Hapo ndipo nilipobaki hoi kutokana na majibu yaliyotoka kwa vijana wale.

Kijana wa kwanza alidai kuwa MKUKUTA ni mpango wa Elimu ya watu wazima, Musa alimuuliza maswali kadhaa kijana yule lakini alionekana kutokuwa na uhakika na majibu yake.

Kijana wa pili yeye alikuja na jibu kama la kijana aliyemtangulia lakini alikuwa na hadithi ndeeefu akijaribu kujenga hoja ya kutetea jibu lake kuwa MKUKUTA ni mpango wa Elimu ya watu wazima.

Aliyeniacha hoi kabisa kiasi cha kutamani kuzima TV ni kijana aliyejitambulisha kuwa anatokea kule Tabora ambaye alikuja hapa mjini mnamo mwaka 2005. Kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la King’walu alidai kuwa MKUKUTA ni dawa ya kienyeji ya kutibu tumbo.

Alipoulizwa na mtangazaji wa kipindi hicho kuwa aliambiwa na nani kuwa MKUKUTA ni dawa ya kutibu tumbo, alijibu kuwa kuna wakati aliwahi kuumwa na tumba na ndipo alipoletewa dawa hiyo na baba yake mdogo ambapo ilimtibu ugonjwa huo wa tumbo.

Awali nilidhani anafanya masihara, lakini kwa jinsi alivyokuwa kiulizwa ndiyo alizidi kunitia kichefuchefu.

Kwa mujibu wa maelezo yake alidai kuwa dawa hiyo inapatikana hapa mjini na hata huko Tabora na Shinyanga. Alizidi kubainisha kuwa dawa hiyo ni ya mizizi na inachemshwa na kisha kunywewa na mgonjwa wa tumbo.

Kijana huyo alizidi kupiga taralila zake kwa kudai kuwa dawa hiyo ya MKUKUTA pia inatibu UKIMWI na ugonjwa wa macho ambao umesambaa hapa nchini siku za hivi karibuni.

Bila shaka wewe unayesoma hapa unaweza kudhani kuwa napiga porojo lakini iwapo kama yupo mtu ambaye alikiona kipindi hicho cha uswazi usiku wa jana na ambacho kimerudiwa mchana wa leo atakubaliana na mimi.

Hata hivyo wapo vijana wawili ambao walijitahidi kujibu swali hilo. Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Dismas alijibu kwa kifupi tu kuwa ni mpango wa kuondoa umasikini na mwenzie aliyejitambulisha kwa jina la Mkude alijibu kuwa ni Mkakati wa Kupunguza Umasikini Tanzania yaani kwa kifupi ni MKUKUTA.

Kijana huyo alikiri kuwa hana maelezo ya ziada zaidi ya hivyo alivyojibu kutokana na uelewa wake baada ya kusikia maana ya neno hilo kupitia Redio, Magazeti na TV.

Kusema ukweli tunapoelekea ni pabaya mno. Iwapo kizazi hiki tulicho nacho ambacho ndicho tunachokikiita kuwa ni Taifa la kesho lakini kinakuwa na watu ambao hata hawafahamu kinachoendelea hapa nchini ni aibu.

Nasema ni aibu kwa sababu inavyoonekana tunapoelekea huko mbeleni tutakuwa na taifa la wajinga kabisa. Tunao vijana wengi sana huko mitaani ambao hata ukiwauliza leo hii waziri mkuu wetu anaitwa nani wanaweza kukujibu kuwa anaitwa Edward Lowasa, na hiyo inatokana na sisi vijana kutopenda kujisomea na hasa kusoma magazeti na vitabu vya maarifa.

Ukikutana na wanafunzi wa siku hizi kama hatakuwa na Gazeti la udaku basi atakuwa na Gazeti la Michezo, na kama ni kuangalia TV basi vipindi wanavyovipenda ni vile vya Miziki ya Bongo Fleva au vya miziki ya Kimagharibi, na Tamthilia za kimapenzi za kimagharibi, lakini Vipindi vya maarifa hawavipendi kabisa.

Leo hii nimepitia Blog ya dada yangu Yasinta, na hapo nikakutana na habari ya Balozi wa Sweden alipoiasa Serikali yetu. Habari hiyo dada Yasinta aliitoa katika Gazeti maarufu la Mwananchi.

Mwandishi wa habari hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Mwandishi wetu, naye alikuwa na yake. Nadhani kaka Mwaipopo aliweza kuonesha hiyo dosari vizuri sana, na kama ungependa kujua alichokosoa kaka mwaipopo, basi unaweza kubofya hapa.