Friday, November 26, 2010

CHAI YA MKANDAA NA MUHESHIMIWA!

Siku hiyo ikifika!

Ijumaa ya leo nimeamka alfajiri na mapema, niliamka majira ya saa kumi na moja alfajiri, nje kulikuwa na dalili ya mvua kwani kulikuwa na wingu zito ajabu. Naam kitambo kidogo nikiwa nimesimama dirishani nikiwa bado nimevaa gauni langu jepesi la kulalia nikaona manyunyu ya mvua yakidondoka katika ardhi hii ya mwenyezi mungu. Yale manyunyu yalikuwa yakidondokea juu ya maua yaliyopandwa upenuni mwa nyumba yetu na yalikuwa yakichirizika taratiibu na kudondoka chini na kupotelea ardhini. Kwa kuwa ardhi ilikuwa kavu sana yale matone ya manyunyu yalikuwa yakimezwa na ardhi sawia.


Nikiwa pale dirishani nikiwa nimetumbua macho yangu nje, naam, nikaanza kuwaza, na kuwaza huko kulikuwa kama masihara hivi, ni jambo ambalo sidhani kama linawezekana lakini nilijikuta tu nawaza. Niliwahi kusoma katika blog ya kaka yangu Mtambuzi Shaban kuwa sisi wanaadamu huwa tunapitiwa na mawazo kati ya 5000 mpaka 6000 kwa siku, na ndio maana sikushangaa sana kujikuta nawaza juu ya jambo hilo.


Nilikuwa najiuliza, hivi itakuwaje siku moja itokee Muheshimiwa Rais anialike Ikulu ili kupata naye chai japo ya mkandaa? Sijui ni kwanini niliwaza hivyo, lakini nilijikuta tu nawaza juu ya jambo hilo. Lakini kama itatokea siku nikipata mwaliko huo…….kwanza sidhani kama nitalala, kwani nitakuwa nikiwaza jambo la kumweleza muheshimiwa, najua yapo madhila mengi sana yanayotukabili, lakini je nianze na lipi?


Je nianze kwa kumweleza madhila yanayowakabili wanawake na watoto? Lakini anaweza kunikata kalma na kunipa ushahidi kuhusiana na jinsi anavyojitahidi kuwawezesha na kuwapa vyeo wanawake na ninajua hatasita kumtaja Spika mpya wa Bunge mama Anna Makinda. Hapo nitaonekana sina jipya, Je kuhusu huduma za Afya? Hapo anaweza kunikumbusha kuwa katika kampeni zake ameahidi kujenga hospitali za rufaa kila mkoa.


Ebo! Sasa nitamweleza jambo gani….Niliendelea kuwaza……… Eheeeee… nimekumbuka Kilimo, nitamweleza kuwa siku hizi mtu kuitwa mkulima ni kama kumtusi, kwani kilimo kimepuuzwa sana na serikali, lakini hilo nalo anaweza kunishangaa, anaweza kuniuliza, hivi sijawahi kusikia kampeni za Kilimo Kwanza ambapo serikali imeelekeza nguvu nyingi katika sekta hiyo ili kuhakikisha kuwa tunafanya mapinduzi ya kijani? Pia anaweza kuniambia kuwa hata waziri wa wizara hiyo amemteua mjomba wangu Jumanne Maghembe.


Mweh! Sasa nizungumzie nini? Ok, hapa naona nitakuwa nimepatia, nitamuuliza kama atawachukulia hatua wale wote waliotuhumiwa kwa ufisadi bila kujali kuwa ni marafiki zake……… lakini hili nalo anaweza kuniruka kimanga, ‘ we huwaoni kina Basili Mramba, Yona na Mgonja wana kesi mahakamani?’ anaweza kusema hivyo..…….


Nadhani nitakuwa nimeishiwa na hoja……..Hebu nisaidieni wasomaji na wanablog wenzangu, hivi siku kama jambo hilo likitokea nizungumzie nini?

Thursday, November 25, 2010

MHESHIMIWA RAIS ALITUAHIDI HAYA, NI VYEMA KUWEKA KUMBUKUMBU

Ahadi za Muheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa mwaka 2010-2015:

1. Kulinda amani nchini kwa kuzuia chokochoko za kidini, kikabila na kisiasa.
2. Wananchi kutoondolewa kwenye Ranchi ya Misenyi
3. Kujenga Uwanja wa Ndege Misenyi
4. Kupanua Uwanja wa Ndege Bukoba
5. Kujenga uwanja wa ndege mkubwa Kigoma
6. Mtukula kupatiwa umeme kutoka Uganda
7. Mikoa ya Kagera, Kigoma, Lindi, Rukwa na Ruvuma kuunganishwa katika gridi ya taifa
8. Kuimarisha Takukuru kwa miaka mitatu
9. Hukumu kwa waliopatikana na hati ya kuua albino
10. Kununua meli kubwa kuliko MV Bukoba
11. Kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali
12. Serikali kulisaidia vyama vya ushirika
13. Kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa
kupeleka kikosi maalum chenye vifaa kupambana na wahalifu
14. Wilaya ya Geita kuwa hadhi ya mkoa Januari mwakani
15. Kulinda muungano kwa nguvu zote
16. Kuwajengea nyumba waathirika wa mafuriko Kilosa
17.Kununua meli mpya kubwa Ziwa Nyasa
18.Kujenga bandari Kasanga mkoani Rukwa
19.Kumaliza tatizo la walimu miaka mitano ijayo
20.Kufufua mgodi wa makaa ya mawe Kiwira
21.Kuzuia hatari za kisiwa cha Pangani kuzama
22.Kununua bajaji 400 kwa ajili ya kubeba wajawazito hasa vijijini


Chanzo Gazeti la Mwananchi