Kabla sijaendelea kuandika kile ninachotaka kuandika humu, ningependa kuwaomba radhi wale wote ambao nitawakwaza kutokana na makala hii.
Naamini kila mtu anao uhuru wa kusema kile anachokiamini, hivyo nimeona na mimi nitumie uhuru wangu kusema kile ninachokiamini.
Ningependa kuchukuwa nafasi hii kuwaomba radhi, dada Yasinta, kaka Mpangala, kaka Kamala, kaka Mbilinyi, kaka Mtanga, kaka Mtwiba, kaka Bwaya, kaka Fita aka mzee wa Theolojia na wengine ambao sikuwataja lakini huenda habari hii ikawakera, kutokana na labda kugusa imani zao.
Hivi karibuni nimetofautiana sana na marafiki zangu kwa sababu eti siendi kanisani.
Kwani ni muda mrefu sasa nimekuwa siendi kanisani.
Kwa nini?
Ni kwa sababu nimepambazukiwa, nimeanza kutilia mashaka imani yangu ya kidini.
Familia yangu ni ya Kikristo wa dhehebu la Seventh Day Adventist (SDA) maarufu kama Wasabato, na tumekuwa tukihudhuria ibada tangu utoto wangu.
Nilivyozidi kukuwa ndivyo familia yetu ilivyozidi kutokuwa na mahudhurio mazuri kanisani. Kipindi hiki cha makuzi yangu akili yangu ilianza kujiuliza baadhi ya maswali yasiyokuwa na majibu.
Nilipofika kidato cha sita mahudhurio ya familia yangu kanisani yalipungua kabisa ikabaki kwenda mara moja au mbili kwa mwaka hasa labda kipindi cha Makambi.
Ni katika kipindi hiki ndipo nilipohudhuria ibada moja katika kanisa la Roman Catholic, nikiwa na rafiki zangu, niliamua kuungana nao ili kuwapa kampani.
Hili ni dhehebu la Kikriso kama la kwangu, lakini mbona lina taratibu nyingi tu ambazo ni tofauti na za kwetu sisi Wasabato?
Haya ndio maswali ambayo yalikuwa yakigonga katika kichwa changu kila wakati. Baada ya uzoefu na kuanza kukomaa nilianza kutafuta chimbuko la hii dhana ya dini. Nilianza kupata wasiwasi baada ya kugundua kwamba kila mtu amefuata dini ya wazazi wake na mababu zake.
Naamini ni watu wachache sana wanaoweza kusimama na kusema kwamba wamejichagulia wenyewe imani zao za kidini au hata madhehebu wanayokwenda kuabudia, nje ya dini au madhehebu ya wazazi wao.
Na kama walifanikiwa kufanya hivyo nadhani uhusiano na wazazi wao utakuwa una mashaka makubwa kama sio kuvunjika.
Kwa mfano mimi nilikuwa katika dhehebu la wasabato kwa sababu wazazi wangu ni Wasabato, kwa kuwa walinipeleka kanisani tangu nikiwa mdogo basi nikajikuta ni Msabato. Sikutakiwa kuhoji.
Jambo hili la kutokuwa na uhuru wa kuchagua dini lilianza kunitia wasiwasi kwa kiasi kikubwa.
Kwa jinsi nilivyozidi kukua ki umri na kimo ndivyo nilivyozidi kuyajua mambo kwa mapana zaidi, niligundua kwamba, kumbe dini zilikuwa zinatofautiana sana katika imani kiasi cha kufikia kurushiana maneno ya kejeli au wakati mwingine hata kupigana, hii iliendelea kunichanganya zaidi.
Hivi kwa mfano kama mimi ningezaliwa nikakuta wazazi wangu ni waislamu, kwa hiyo na mimi ningekuwa ni muislamu.
Na labda ningekuwa nawakejeli wakristo kwa kuwaona kama hawafuati dini ya kweli, bali dini yangu ndio ya kweli! Hii niliona haileti mantiki.
Kama wewe ni muislamu unaamua kupigana na mkristo kwa sababu ya imani yake au Mkristo unaamua kupigana na Muislam kwa sababu ya imani yake, Je kama unapigana na mjomba, shangazi, au binamu yako?
Nilipokuwa kidato cha sita masomo niliyokuwa nikiyapenda sana yalikuwa ni ya Sayansi. Niliona kwamba baadhi ya mambo ambayo nilikuwa nikiyasoma katika sayansi yalikuwa yakipingana na mambo niliyojifunza kanisani. Niliamua nisiendelee kutilia mkazo sana maneno ya mchungaji, nikaona nichunguze mgongano huu wa dini kwa dini pamoja na ule mgongano wa dini na sayansi.
Ukweli ni kwamba sitaeleza mgongano wa dini na sayansi kwa sababu bwana Mtambuzi na kaka Bwaya waliwahi kulieleza hilo kwa kirefu, sidhani kama maelezo yangu yatatofautiana na ya kwao. Rejea makala zao kama unahitaji ufafanuzi zaidi.
Nilipoenda chuoni mahudhurio yangu kanisani yalikoma kabisa na tafakuri yangu kuhusu dunia ndiyo ikawa imepamba moto. Sasa nilikuwa nimeenda mbali zaidi, na kwamba, kumbe kulikuwa na watu ambao walikuwa wanaamini kwamba mungu hayupo, pia nikaangalia katika dini mbalimbali za mashriki ya kati, mambo niliyokutana nayo sikuwahi kuyasikia hapo kabla.
Kumbe migogoro kati ya dini na dini na kati ya dini na watu wasiomwamini Mungu ni kutokana na kila kundi kutokubaliana na nadharia ya mwenzake!
Kufikia hapo nilianza kuiangalia dini yangu kwa mtazamo tofauti, mimi sio mtoto tena.
Nilisoma habari za wale wanaoamini kwamba hakuna mungu mtandaoni, nikagundua sababu ya wao kuamini hivyo. Kitendo cha kusoma habari zao katika kuutafuta ukweli kumenisaidia kuelewa kwamba siasa ilihusika kwa kiasi kikubwa katika dini.
Niligundua kwamba vitabu vya Biblia viliunganishwa pamoja kutokana na maandiko ya awali ya viongozi wa serikali za wakati huo na kanisa kwa ajili ya malengo yao.
Nimegundua kwamba viongozi wengi wa dini hutumia vitisho vya moto wa milele wa mungu ili kuwafanya watu wanywee na kujiunga na dini zao, kwa hofu kuwa wasipofanya hivyo watakuja kuungua na huo moto wa milele!!!.
Mambo haya, pamoja na kukosekana ushahidi wa kuwepo mungu ilikuwa ni rahisi kwangu kukubaliana na nadharia ya watu wasioamini uwepo wa mungu.
Dini za Kimashariki zinaonekana kuleta mawazo mapya ya mtazamo wa kisasa. Kwani hazina mlolongo wa vitisho na msululu wa mambo magumu ya kufanya ili kuweza kufika mbinguni,. Dini hizi zinasisitiza mtu kujitambua.
Tatizo moja kubwa linalozikabili dini zetu nitabia ya dini moja kuihukumu dini nyingine kwamba haifai. Wengine wanadai wasioamini hata wale wenye mioyo safi na wadilifu hawafai na wataishia Jehanam. Lakini watu wenye roho mbaya, mradi tu ni waumini na wanatoa sadaka basi wataishi katika utukufu wa milele!
Kitu cha kushangaza ni kwamba katika biblia imeandikwa kwamba tusihukumiane, lakini wakristo wanawahukumu wasioamini, kwamba hawafai. Wasioamini nao wanatakiwa kumkubali kila mtu kwa imani yake, lakini utakuta wanadharau waumini wanaoamini uwepo wa mungu. Inabidi kila upande ukubali imani ya mwenzake, kwani kila upande una watu wengi tu wa kutosha.
Hivi inawezekana watu wote hao wakawa ni wajinga?
Mimi kwa upande wangu naamini kila upande unategemeana na wa mwenzake, kama ukichunguza kwa makini imani ya kila mmoja.
Ingawa nimegundua kasoro ya dini yangu lakini sijawahi hata siku moja kuiponda. Ni moja ya urithi wangu, na imehusika kwa kiasi kikubwa katika malezi yangu.
Huu ni mtazamo wangu tu, naomba msinijengee chuki!!!!!!
MITAALA IZINGATIE MABADILIKO YA KIUCHUMI NA TEKNOLOJI-MAJALIWA
-
*WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kuwa mitaala inayoandaliwa ihakikishe
inazingatia mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya kiteknoloji...
3 minutes ago
5 comments:
Mhhh...dada yangu hapo umeibua mjadala mzito na wenye manufaa kwa jamii.Mie ni Mkatoliki japo si mhudhuriaji wa kanisani (nasali nyumbani).Rafiki zangu wengi ni Waislam kuliko Wakristo,na hilo lilinisaidia kuujua Uislam kidogo.Kitabu nacho kimenifanya niuelewe kwa undani zaidi.Kwa kifupi,dini ni dhana complicated na contradictory mno.Lakini ninachoamini hadi sasa ni kwamba ili mtu awe muumini analazimika kuitazama dini yake kiteolojia zaidi kuliko kisayansi.Kwa vile msingi mkubwa wa dini ni imani (ambayo kimsingi ni kitu cha kufikirika zaidi kuliko uhalisia),uthibitisho (proof) katika dini ni mgogoro (eg Mungu yuko wapi?Mbinguni ndio mahala gani?nk)
Dini zetu za asili (ATMs) kwa kiasi kikubwa zilikuwa tofauti na hizi za kimapokeo (Ukristo,Uislamu,etc) kwa vile ziliyapa mazingira uzito mkubwa (eg mizimu katika milima au misitu inayoonekana) na pia nafasi ya mwanadamu katika u-mungu ilikuwa kubwa pia (eg nafasi ya mzimu wa babu ktk ukoo au kabila).
Kufupisha hoja yangu,naafikiana nawe kwamba dini za mapokeo zimetawaliwa na mambo kadhaa ambayo licha ya kukinzana na mafundisho ya dini hizo pia yanachochea mgawanyiko badala ya umoja.Ikumbukwe kuwa ni dini hizi ndizo zilizopigana vikumbo kupora waumini wa dini zetu za asili (japo hazijafanikiwa 100% kwani nafasi ya dini hizo bado ni muhimu kwa baadhi ya wakristo na waislam eg mambo ya mila,matambiko,nk).
Mjadala mzuri na unasaidia kupanua mawazo vya kutosha.Ni vema ukiuendeleza mwakani (well,kesho).
HERI YA MWAKA MPYA
mmh...! nimeshusha pumzi kwa nguvu baada ya kuisoma hii ambayo mi nimependa kuiita funga mwaka. ahsante da koero kwa kuleta changamoto. naomba usiache, kazi imesimama. ngoja nifanye tafakuri ya kufa mtu baada ya kusoma hapa.
Kuyajadili haya mambo ya dini ni jambo la msingi. Profesa Shayo aliwahi kusema dini ni ajali ya kijiografia. Mara nyingi mtu haamui ni dini gani awe nayo. Anarithi dini ya wazazi wake. Na inapotokea kuwa mtu anaongoka ukubwani, mara nyingi hufanya hivyo si kwa sababu ya uchambuzi wa kina wa dini husika. Lakini ajabu ni kwamba kila mwamini huamini kuwa dini yake haina matatizo, na kwamba dini nyinginezo zote zina mapungufu makubwa kiasi cha kustahili moto wa milele.
Nadhani, tunazo sababu nyingi kuzichunguza dini hizi. Tuzichunguze si kwa lengo la kuona ipi ni sahihi kuliko nyinginezo. Bali kujaribu kuona ikiwa nadharia za dini husika zina mantiki zinazoingia akilini ama la. Tuzichunguze kuona ikiwa kuna uhusiano wa namna fulani baina ya dini hizi (kama kuna namna fulani zinafanana hata kama zinajidai kukosoana) ama kuona ikiwa kila dini inaamini kitu chake tofauti na dini nyinginezo.
Kazi hii hatuna budi kuifanya. Kwa sababu tusipofanya hivyo tutaendelea kukaa katika kifungo cha fikra. Ni furaha yangu kuona kuwa Koero umejitosa katika mjadala wenye mwelekeo huu. Nitakuwa msatari wa mbele kukuunga mkono.
Katika kukuunga mkono, tuanze na SDA uliko sasa kinadharia: Unadhani kuna mapungufu gani ya msingi ya kiimani yanayokufanya ufikirie upya mahudhurio yako huko?
Mchango wa Evarist umeongeza ladha nzuri. Michango ya watu kama hawa inahitajika sana kwenye mijadala kama hii.
Evarest: Kulikoni, mbona safu ya Raia mwema ughaibuni hainokani siku hizi?
Dada koero, kama unavyosema huu ni mtizamo wako na uko huru kusema chochote. Sio wakati wa kilichodhniwa kuwa ni ukweli kuwa na nguvu za hata juuwawa endapo utatofautiana nacho!
Kuna watu wachache wanaomiliki dini hizi kwa malengo yao. Kumbuka maandiko yanayoitwa matakatifu au matukufu, ni mitizamo ya watu na jamii Fulani. Kwa mfano biblia ni documentary ya maisha ya waislaer.
Kama ulivyosema tulichaguliwa kila kitu zikiwemo dini na ibada, shule nakadhalika. Dini zinatawaliwa sana na Ego kwamba kila dini mungu wake ni bora kuliko wa mwingine. Hata hivyo Mungu huyu anaonekana kutisha kuliko kuwa kimbilio letu. Cku ya mwisho yeye anamoto, majoka, nge, viboko nakadhalika.
Imegundulika kwamba binadamu ndiye anaye muumba Mungu na sio mungu kumuumba mwanadamu katika makanisa yetu. Kwamba ubongo ndio unaotengeneza kumbukumbu na kuzitunza na hivyo kumbu kumbu za mungu ziko kwenye Bongo za wanaomwamini!
Ukiangalia kwa kina mafundisho ya baadhi ya mitume kama Kristo yamepotoshwa kwa makusudi na yote yafyanywayo makanisani sio maagizo ya kristo bali ya wanadamu. Ulishawahi kusoma vitabu vya Lenin na mashoshalisti wengine juu ya ukristo na utumwa/ukoloni? Wizi mtupu
Umeongelea hawa majamaa wa mashariki. Kwa kweli dini zao zinaeleweka na zinaingia akilini kwa kiasi Fulani. kuna kitu wanakiita “science of the soul” wanasema hii ni sayansi pekee ya kumjua mungu(kama unamwita hivyo) kwani huwezi kumjua Mungu kwa kufanya scientific experiments za kawaida na ndio maana wanasayansi wetu wanakataa kwamba hakuna mumgu ila wanadai kuna nguvu
Wanasema huwezi kumuona Mungu kwa macho yako ya kawaida ila kwa njia nyingine ambayo wanajaribu kuiita jicho la tatu. Wanatumia sana kitu kinachoitwa ‘meditation’ na kinasaidia sana katika maisha yetu ya kila siku.,
Labda nikukaribishe sana kwenye madarasa yetu ya utambuzi.
Natamani ningekuwa wa kwanza labda ningewasaidia wenzangu kufupisha maandishi. Lakini wamenitangulia na wamenisaidia mimi. Nashukuru kwa mtazamo wenu nyote na nimejifunza mengi. Kaka Fadhy, funga mwaka ya 08 naiona inanoga pande zte. Kila la kheri
Post a Comment