Monday, February 2, 2009

HAWA NDIO WATUMISHI DUNI ZAIDI-SEHEMU YA PILI

Hakuna wa kuwatetea!

Hivi karibuni shirika la Umoja wa kimataifa linaloshughulika na kuangalia ukiukwaji wa haki za binadamu (Human Right Watch) lilifanya uchunguzi kuhusiana na unyanyaswaji wa wafanyakazi wa kazi za nyumbani katika nchi za El-Salvado, Guantamala, Indonesia, Malasia, Morocco, na Togo.

Katika taarifa ya shirika hilo la Human Right Watch inaelezwa kwamba uchunguzi uliofanywa katika nchi nilizozitaja hapo juu umeonyesha kwamba unyanyasaji wa kimapenzi au kubakwa ndio tatizo kubwa linalowakabili wasichana wanaofanya kazi za ndani katika nchi hizo. Kwa bahati mbaya,wasichana hawa huogopa kutoa taarifa kwa kuhofia usalama wao,kwani wengi ni wahamiaji haramu kutoka nchi nyingine ambao husafiri kwa siri katika nchi hizo kwenda kufanya kazi za ndani kwa ajili ya kusaidia familia zao ambazo nyingi ni masikini.

Kwa mfano katika nchi ya El-Salvador asilimia 15.5 ya wasichana wanaofanya kazi za ndani waliobadili waajiri walikimbia unyanyasaji huu wa kijinsia au kubakwa.

Tatizo lingine linalo wakabili wasichana hawa ni kufanyishwa kazi nyingi kuliko kawaida bila kupata muda wala siku ya kupumzika. Binti mmoja aitwaye SARIHATI mwenye umri wa miaka 17 ambaye ni mhamiaji kutoka Indonesia aliyekwenda kufanya kazi Malaysia aliliambia shirika la Human Right Watch kwamba, alikua anaamshwa saa kumi alfajiri na kuanza kufanya kazi hadi saa moja jioni bila kupumzika. Aliendelea kusema, tangu alipoajiriwa na huyo mwajiri wake hakubahatika kutoka nje pale nyumbani na mwajiri wake huyo alikua na kawaida ya kumpiga mara kwa mara.

“Yule mama mwajiri wangu alikua na kawaida ya kunifokea na kunitukana bila sababu ya msingi na wakatia mwingine hunipiga sana. Nilikua natamani kutoka, lakini ameficha hati yangu ya kusafiria na nilikua naogopa serikali ya Malaysia kwamba angenikamata na kuniweka ndani kama mhamiaji haramu” alisema SIRHATI.

Taarifa hiyo ya Human Right Watch ilibainisha pia kwamba nchi ya Togo ndiyo inayoongoza kwa wasichana wengi kutoka nchini humo kusafiri katika nchi za Benin, Ghana, Nigeria na Niger kwenda kufanya kazi za ndani,wengiwao wakiwa wametoka kwenye familia za kimaskini.

Tatizo hilo la kusafirisha wasichana kutoka vijijini kwenda mjini kufanyishwa kazi za ndani halipo Togo peke yake, hata hapa nchini kwetu limekuwepo kwa mda mrefu. Lakini siku za hivi karibuni limekua kubwa kwani kumeibuka mawakala wanaosambaza vipeperushi maofisini hadi kwenye magazeti wanatafuta wafanya kazi wa ndani.

Mawakala hawa ndio wanao safiri mikoani na kwenda kuwahadaa wazazi wa wasichana hawa na kisha kuwaleta mjini na kuwauza na wengine kufanyishwa shughuli za ukahaba kwenye madanguro.

Tunapoelekea, mawakala hawa hawataishia kuwauza hawa wasichana nchini peke yake kwani kuna uwezekano mkubwa biashara hii kuvuka mipaka na kufanyika nje ya nchi za kiarabu ambapo kuna uhaba wa watumishi wa ndani.

Ninasema huenda itakua hivyo kwa maana ya taarifa rasmi. Lakini ukweli ni kwamba, kwa taarifa zisizo rasmi ni kwamba kuna wasichana wa Tanzania Uarabuni na hata kwenye baadhi ya nchi za Ulaya, ambao ni mayaya na watumishi wa ndani, ambao ni kama watumwa.

Ikumbukwe kwamba familia nyingi vijijini zinaishi katika lindi la umaskini na ndio sababu imekua rahisi kwao kuhadaiwa kirahisi na kuwaachisha mabinti zao shule na kuwakabidhi kwa mawakali hawa matapeli kwa ujira mdogo.

Shirika la kazi duniani (ILO) limeshatoa mwongozo kuhusiana na ajira hii ya watumishi wa ndani.

Kwanza limeagiza kwamba watumishi wote wa ndani wasiwe chini ya miaka 15 na wasiwe wameachishwa shule au wasiwe wamenyimwa furusa ya kwenda shule, na pia ihakikishe kwamba gharama za elimu, yaani ada haziwi kikwazo kwa watoto wa maskini kutopata elimu.

Pili zitungwe sheria mahususi za kuwalinda wafanya kazi hawa wa ndani kwa kuhakikisha wanalipwa mishahara mizuri, wanalipwa saa za ziada ya kazi yaani (over times) mapumziko ya siku moja kwa wiki, na mafao mengine stahili pindi wanapoachishwa kazi.

Tatu kuanzishwe namba ya simu ya bure (Tollfree) kama ilivyo kwa polisi kwa ajili ya kuwawezesha wasichana hawa wakifanyiwa vitendo vya unyanyasaji kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama. Namba hizo zitangazwe kwenye vyombo vya habari mbalimbali kama vile magazetini, redioni, na kwenye runinga.

Nne kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakao kamatwa na kukutwa na hatia ya kuwatesa na kuwanyanyasa kijinsia na kuwabaka watumishi wa ndani.

Tano kuwaokoa na kawatoa wasichana hawa mikononi mwa waajiri watesaji na kawapa hifadhi kabla ya kurejeshwa makwao, na kama watakua wameumizwa wameathirika kisaikolojia wapate tiba, kabla ya kurejeshwa makwao.

Iwapo serikali yetu itazingatia mwongozo huu, naamini unyanyasaji kwa watumishi wa ndani utapungua kama sio kuisha kabisa.

Hata hivyo ni vyema pia mawakala wanaotafutia watu, watumishi wa ndani wadhibitiwe wasiwe wanawaachisha watoto shule, na umri wa watumishi wa ndani pia uzingatiwe kulingana na mwongozo wa shirika la kazi duniani(ILO).

Hivi karibuni serikali imetoa muongozo juu ya mishahara ya watumishi hawa, Je mpaka sasa utekelezaji umefanyika kwa kiasi gani?
Je watumishi hawa wanafahamu mahali pa kufikisha kilio chao kama utekelezaji huo haufanyiki?
Je wameelimishwa kwa kiasi gani juu ya haki zao za msingi?

Tunaogopa na kusubiri kitu gani katika kutetea masilahi ya watumishi hawa au ni kwa sababu kila nyumba watumishi hawa wapo, na nyumba za wakubwa zinawatumishi zaidi ya watano. Hivyo kuchokoza ili walipwe vizuri kwa mujibu wa sheria ni kuharibu ‘dili’ zao?


Inabidi tukubali kwamba watumishi wa majumbani ndio watumishi duni na wanaonyanyaswa kuliko wengine hapa nchini. Bahati mbaya hakuna anayewatetea!!!!!!!

5 comments:

Fita Lutonja said...

Dada nimefurahia sana maandikoyako yaani yanavutia ni jamobo jema sana mimi nimetoka Dar nimesafiri kidogo kuelekea masomoni kusoma tena.

MARKUS MPANGALA said...

inashindwa kluanika zaidi ila hata kama ILO limetoa mapendkezo, sijui tunamwelekeo gani iwapo albino tu wanatutoa machozi ya unafiki na ngebe.
Koero:) nashindwa kuandika zaidi, naumia sana

Mzee wa Changamoto said...

"Hivi karibuni serikali imetoa muongozo juu ya mishahara ya watumishi hawa, Je mpaka sasa utekelezaji umefanyika kwa kiasi gani?
Je watumishi hawa wanafahamu mahali pa kufikisha kilio chao kama utekelezaji huo haufanyiki?
Je wameelimishwa kwa kiasi gani juu ya haki zao za msingi?"

Pengine hiyo ni nukuu nzuri ambayo inaweza kutoa picha ya kilichopo nyuma ya pazia. Ukweli ni kuwa wawekao sheria ndio wenye dhamana ya kuhakikisha utekelezaji NA NDIO WENYE HATIA.
Nahitaji kujieleza zaidi?

Koero Mkundi said...

Ahsanteni kwa mitazamo yenu,

kaka Fita nakutakia safari njema na masomo mema, kaka Markus, nipe muda naandaa makala juu ya mauaji ya Albino.
kaka Mubelwa nashukurui kwa mtazamo wako pia, nadhani mjadala huu unaweza kuupanua kwa kadiri uwezavyo,
Bado nahitaji maoni yenu kwa kuwa hii vita ni yetu sote.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

usisime hakuna chombo cha kuwatetea wakati blog yako ndo hivyo imeshaanza. always be hero, kuwa sauti yao usijirudishe nyuma kwa sababu blogu yako ni kubwa na inaweza kuleta mabadiliko!!!