Ndugu wasomaji na wanablog wenzangu, bado niko Dar, na kutokana na pilika pilika zilizonileta hapa kutokamilika, nitalazimika kukaa hapa kwa wiki moja zaidi.
Leo naomba nizungumzie wajane.
Nilipokuwa Arusha, nilishuhudia tukio ambalo mpaka leo limenikaa sana akilini, na linaniumiza roho sana.
Nilishuhudia mama mmoja mjane akinyang’anywa kila kitu na ndugu wa mumewe mara bada ya kutoka kumzika mumewe. Tukio hili la kuisikitisha lilitokea wiki moja baada ya mazishi ya mumewe mpendwa.
Nilisimuliwa kuwa mama huyu alikuwa akiishi na bwana huyo kinyumba, hawakuwahi kufunga ndoa kutokana na sababu za kidini, mume muislamu na mke mkiristo, lakini waliishi pamoja kwa takribani miaka sita na kujaaliwa kupata watoto wawili.
Inasemekana upande wa mume hawakumpenda yule mwanamke, kisa alikataa kubadili dini, na kuwa muislamu ili wafunge ndoa, hiyo ikawa ndio sababu ya kukataa asiolewe na ndugu yao. hata hivyo waliendelea kuishi pamoja na kwa mapenzi kama mume na mke hadi wakapata watoto wawili, wa kike na wa kiume.
Mara yule bwana akaanza kuugua ghafla, alipopelekwa hospitali haukuonekana ugonjwa na baaada ya siku tatu akafariki dunia.
Kasheshe lilianzia hapo ndugu wa marehemu wakadai kuwa yule mwanamke alimpa sumu ndugu yao ili arithi mali.
Kisa yule bwana alikuwa anamiliki miradi kadhaa na pia alikuwa na nyumba mbili hapo Arusha, moja akiwa ameipangisha na nyingine akiishi yeye na familia yake.
Mara baada ya mazishi yule mwanamke aliamriwa aondoke, mara moja na nyumba na miradi ya mumewe ikawa chini ya himaya ya ndugu wa mume.
Sina uhakika kama yule mwanamke anaweza kupata msaada wa kisheria kwani hakuwa ana ndoa na yule mume.
Sina uhakika hatima na yule mwanamke na wale watoto kwani wamenyang’anywa kila kitu.
Ndugu wasomaji na wanablog wenzangu, naamini kuwa hili sio jambo geni masikioni mwenu, inawezekana mliwahi kusikia au kushuhudia unyama wa aina hii.
Swali ninalijiuliza mpaka sasa, ni je hivi unyama huu wanaofanyiwa wajane, utaisha lini?
Jana nilikuwa nilikuwa nasoma Biblia na katika kusoma kwangu nikakutana na fungu moja la biblia lililonikumbusha tukio hili la Arusha na ndipo nikaona niwashirikishe wasomaji na wanablog wenzangu tutafakari kwa pamoja.
Fungu lenyewe ni Kutoka 22: 22-24, linasema:
Nitanukuu, “Usimtese mjane yeyote aliyefiwa na mumewe wala mtoto yatima, ukiwatesa watu hao katika neno lolote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto nami nitawauwa ninyi kwa upanga na wake wenu watakuwa wajane na watoto wenu mayatima”
Mwisho wa kunukuu.
KARATU YAFIKIWA NA ELIMU YA FEDHA
-
Na. Saidina Msangi, WF, Karatu, Arusha
Wananchi wa Wilaya ya Karatu jijini Arusha, wametakiwa kuhakikisha kuwa
wanatumia Taasisi za fedha zilizosajiliwa am...
2 hours ago
3 comments:
Kwa kweli mimi mila nyingine bado sizielewi. Yaani watu wanaona mali ni kitu muhimu sana. Inawezekana huyo bwana wakati yupo hai hata hawakumjali na pengine walikuwa wanamchukia. Ndio maana tunasema mpende mtu akiwa hai na sio akifa kutaka tu mali zake. Kwa nini watu wanapenda sana vitu vya wenzao hasa wakifa. Kwani hata kama hajafunga ndoa lakini si walikuwa na watoto wawili je wale watoto nani atawasaidia?
Na kwa nini nao wasifanye kazi na kupata mali zao. Nimekumbuka nilisimuliwa na mtu kuna familia moja walifiwa na mama yao mpendwa na baadhi ya watoto wakawa wanamdai babayao wagawane vifaa ambavyo mama yao alikuwa amenunua kwani haitakuwa vizuri mke mpya wa babao atumie vile vyombo alivyonunua mamayao. Babao akawajibu ya kwamba yeye bado yupo hai na yule mama alikuwa mke wake. Yaani hapo ndipo nilipokuja jiuliza je mtu na mali kipi ni bara?
Sina hakika na sheria zilivyo hapo nyumbani lakini kama mali ilikuwa kwenye jina la Mume na watoto wanajulikana kuwa wa-mume, nina imani kuna namna ya kuhusisha hivyo viwili na kumpatia msaada huyo Mama. Ninalomaanisha ni kuwa ni lazima mali za wazazi zitumike kuwasaidia watoto na kama ni kweli kuwa hakuna msaada anaoweza kupata kisheria (jambo ambalo licha ya kunisikitisha halitanishangaza kutokana na siasa za hapo nyumbani) basi kunahitajika mabadiliko mengi sana.
Pengine KUBINAFSISHA SERIKALI KUU
Nafikiri kuna chama cha wanasheria wanawake,wanawasaidia watu wenye matatizo kama hayo,lakini sina uhakika,ila kwa sheria za nchi yetu bado kuna kazi kubwa sana ya kumkomboa mwanamke na watoto,sheria zinazotumika bado ni za mwaka 47 za ukandamizwaji.
Matatizo kama haya humkuta hata mwanamke aliyefunga ndoa,akifiwa na mume hana thamani tena ananyang'anywa kila kitu kisha anafukuzwa yeye na watoto wake,kuna unyanyaswaji wa hali ya juu sana na wanawake wengi hawajui wapeleke wapi malalamiko yao au vilio vyao ili wapatiwe msaada wa kisheria hii huwa inanisikitisha sana.
Post a Comment