Thursday, October 8, 2009

TUMESHINDWA KUANDIKA HISTORIA YETU WENYEWE?


Hivi karibuni niliomba msaada hapa katika kibarazani, nikiomba kuelekezwa mahali vinapopatikana vitabu mbalimbali vilivyokuwa vikitumika mashuleni miaka ya 1980.

Kutokana na ushirikiano mzuri wa wasomaji wa kibaraza hiki na wanablog wenzangu, nilielekezwa maeneo kadhaa ambapo niliambiwa nikajaribu huko, kwamba huenda nikavipata vitabu hivyo.

Ukweli ni kwamba sijavipata vitabu hivyo, lakini katika juhudi zangu za kutafuta vitabu hivyo nilipita katika taasisi ya kiswahili pale chuo kikuu mlimani {TUKI} na katika jengo la Quality Plaza lililoko Nyerere Road, pale kuna duka moja, nadhani linaitwa Mkuki na Nyota kama sikosei.
Nilikutana na vitabu vingi sana katika maeneo hayo, kwa mfano katika duka la vitabu lililopo pale Quality Plaza, nilikutana na vitabu vya elfu lela ulela, visa vya Sindbad baharia, na vingine vingi tu, hivyo hivyo pale Mlimani nilikutana na kazi nyingi za tafiti zinazozungumzia historia za makabila yetu, mila desturi na historia ya nchi yetu, bara la Afrika kwa ujumla na kadhalika na kadhalika.

Nilivutiwa na vitabu kadhaa ambavyo nilivinunua, lakini kilichonishangaza sana ni kukuta vitabu vingi vinavyoelezeza historia ya nchi yetu, makabila yetu na hata mila na desturi zetu vimetungwa na Wazungu.

Yaani nilishangaa sana kuona kwamba wazungu ndio wanaotufahamu zaidi kuliko sisi wenyewe. Pamoja na kuwa na wasomi wengi tena wa kutosha, lakini bado tumeshindwa kuandika historia ya nchi yetu, makabila yetu na mila na desturi zetu mpaka wazungu waje watuandikie?

Ina maana maisha ya mkazi wa pale Rufiji au Kipatimo kule Kilwa anayajua mzungiu kuliko Mtanzania mwenyewe? Au maisha ya mkazi wa kule Katerero Bukoba, Ruhuwiko Songea, Manyoni Singida, Mlima Kilimanjaro kule Moshi, Kyela kule Mbeya, au Kibaigwa kule Dodoma, wasomi wetu wameshindwa kufanya tafiti za makabila na mila na desturi za wakazi wa huko mpaka wazungu waje watusaidie kuandika?

Inashangaza kuona kuwa waliondika historia ya nchi yetu ni wazungu wengi sana ukilinganisha na sisi wenyewe.
Hata hivyo nilijaribu kumuuliza yule muuzaji wa vitabu na jibu lake lilikuwa ni rahisi sana, eti alidai kuwa wazungu wanazo fedha za kuendeshea tafiti mbalimbali ukilinganisha na sisi wenyewe. Ujinga gani huu..

Sina uhakika sana kama kilichoandikwa katika vitabu vyao kuwa ni sahihi kwani, habari zinazopendwa na hawa wenzetu ni zile zilizopotoshwa na kutiwa chumvi nyingi ili zivutie, hakuna habari inayohusu Bara la Afrika itakayoandikwa kwa usahihi kama ilivyo bila kutiwa chumvi. Lakini cha kushangaza huko mashuleni na vyuoni tunaambiwa tuvisome vitabu hivyo ili kuja kuvifanyia mitihani.
Hivi wasomi wetu wako wapi? Wanafanya nini? Na tafiti zao juu ya nchi yetu, makabila, mila na desturi zetu ziko wapi?

6 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Inasikitisha kusikia hili, Kama tulivyosema mara nyingi sisi waAfrika tunaamini sana wazungu wanaweza kila kitu kitu ambacho sio kweli. Lakini sasa ile imani imeshakolea vichwani mwetu. Naamini kabisa sisi pia tunaweza na inawezekana tunaweza kuliko wao kwani kumbuka zamani mila, desturi, hadithi walizokuwa wakisimulia wazee wetu unadhani hakuna mtu anaweza kuziandika wapo sana tu. Unafikiri hakuna awezaye kuandika kuhusu Bara la Afrika wapo sana lakini sasa naweza nikasema ni kutojiamini kuwa nasi tunaweza. Na huyu aliyesema pesa, sijui aliwaza nini. Naacha na wengine waseme pia, Ohh Koero pole kwa kutovipata vile vitabu hivi unataka kitabu kizima au sehemu zile za kurasa zilizoandikwa zile hadithi ulizozitaja. Naweza kuwa msaada.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Koero - inabidi tuangalie Historia kidogo. Ni ukweli ulio wazi kwamba (ukiachilia mbali Misri, Ethiopia na sehemu nyingine chache) wazungu ndiyo walituletea maandishi. Elimu yetu tuliyokuwa nayo haikuhitaji maandishi na jambo hili liliwashangaza wazungu mpaka wakaamua kutuita watu wa "bara la giza" kwani kwa mtazamo wao mtu asiye na maandishi pengine hana kitu cha kuandika, hana Historia!

Wamishenari, Wanaisimu, Wanahistoria, Wanaanthropolojia na "wataalamu" wengine kutoka Ulaya walifanya kazi nzuri sana ya (mbali na kutafsiri Biblia) kuandika sarufi za mwanzo, vitabu vya Historia pamoja na mila na desturi za makabila yetu. Baadhi ya vitabu hivi vina matatizo makubwa kwani wengi wao hawakuzifahamu vizuri tamaduni zetu na pengine kwa makusudi mazima na mitazamo yao potofu walipotosha mambo na kumdhalilisha Mwafrika. Na kwa bahati mbaya, kama ulivyosema tatizo hili bado lingalipo.

Huyo muuzaji aliyekwambia kwamba tatizo ni pesa yuko sahihi. Ni nani atakupa pesa pale Tanzania eti ukafanye utafiti kuhusu mila na desturi za Wasukuma? Hii itaonekana kama "ufisadi" fulani hivi kwani hatuna mwamko wo wote kuhusu kuendeleza utamaduni wetu na kwa wengi hii itaonekana kama kupoteza pesa za serikali bure. Ukitaka kufanya utafiti wa namna hii ni lazima utafute pesa pengine kutoka Ulaya na Marekani ambako serikali zake kupitia mashirika mbalimbali zimetenga pesa maalumu kwa tafiti za kila aina. Ndiyo maana hata mradi muhimu kama ule wa Lugha za Tanzania unafadhiliwa na Waswideni. Tunahitaji wafadhili watupe pesa kwa kila kitu.

Jambo jingine ni wasomaji. Ni nani atasoma kitabu cha Mila na desturi za Wasukuma hasa katika zama hizi za utandawazi? Hata Wasukuma wenyewe sidhani kama wana mwamko wo wote katika jambo hili. Kumbuka hizi ni zama za "usasa" na huu ni ulimwengu wa Britney Spears na 50 Cent. Nani anataka/anajali eti mila na desturi za Wapare? Zama ambazo hata Kiswahili - lugha kubwa kabisa na yenye kila kitu - tunaipiga dafrau isitumike tena katika shule za msingi baada ya kupoteza muda wa miongo karibu sita. Kwa hivyo waandishi wengi wanaona kwamba pengine "it is not worth it" kuhangaika kufanya utafiti, kuandika kitabu, kukichapisha (hapa napo ni kasheshe tupu) na halafu kisisomwe. Sana sana upate bahati kitabu hicho kichaguliwe na kutumiwa mashuleni lakini hata hapa napo naambiwa hata kitabu kiwe kizuri namna gani ni lazima uwe na mtu kule maamuzi yanakofanyikia akukingie kifua. Kwa ujumla ninachotaka kusema hapa ni kwamba sekta nzima ya utafiti na vitabu ina matatizo makubwa na mimi siwezi kuwalaumu wasomi na watafiti wetu hapa. Wapo waliojaribu kuandika vitabu vizuri sana na ukivisoma mpaka unashangaa lakini vitabu hivyo huwezi kuviona wala kuvisikia. Tafuta, kwa mfano, riwaya ya Rais wa Kesho ya Marehemu Munga Tehenan (Baba wa elimu ya Utambuzi Tanzania) usome uone. Hapo unaweza kujiuliza ni kwa nini kitabu kama kile kisisomwe na wanafunzi wa kidato cha sita/chuo kikuu? Sijui tunakoelekea!

Mzee wa Changamoto said...

Asante Da Koero. Umenifanya nionegeze jingine kwenye list yangu ya maombi. KINACHONIUMA ni kuwa wana pesa ya kufanya mengi lakini si yale yaliyo na manufaa kwa jamii.
Ni kweli kama alivyosema Kaka Matondo kuwa HAWAKUPI PESA lakini hii haimaanishi kuwa HAWASTAHILI KUKUPA PESA.
Kuna mengi wanayotenda ambayo yangeweza kusubiri. Kaka Bwaya alimnukuu Mzee mmoja aliyekuwa naye kwenye basi akisema siasa zetu ni za "miaka mitano" na ni lazima zijioneshe. Yaani hakuna anayetaka kuwekeza kwenye tafiti, bali kuzindua mavitabu ya uongo ya watu. Hakuna anayetaka kujenga mifumo ya majitaka, bali maghorofa lukuki juu yake (yasiyo na mfumo wa majitaka). Hakuna anayetaka kupeleka wanafunzi wengi shule za tiba na ualimu kwa elimu bora, wanafungua majengo ya zahanati na majengo ya shule.
Labda niseme tatizo kubwa ni kuwa hakuna anayetaka ku-pioritize mambo. Wanajali "mng'ao" wa ngozi yako hata kama umeipaka mafuta bila kuoga. Kwao kilicho ndani hawakifikirii, wanajali nje.
Tanzania yetu ni ya kujenga ENEMY na sio INNER-ME.
Blessings

Unknown said...

Naona waliotangulia kutoa maoni yao wamemaliza kila kitu, pongezi kwako dada Yasinta, kaka Mubelwa na kaka yangu Matondo kwa maoni yenu murua… Niseme nini sasa, maana mmeliza kile kitu.

Kuna jambo moja hapa amelisema kaka Matondo, ambalo ni kubwa kabisa, nalo ni la watanzania kutopenda kujisomea na hasa kutopenda kusoma vitabu vya maarifa na vinavyozungumzia mambo ya nyumbani, maana hii ndio inakatisha tamaa hasa..Ni kweli kuwa serikali haitoi fungu kwa ajili ya watafiti wa ndani, yaani wasomi wetu, lakini kama watanzania wangekuwa ni wasomaji wazuri wa vitabu, hilo lisingekuwa ni tatizo, kwani kwa kujinyima na kutafuta udhamini wa hapa na pale wasomi wetu wangeweza kutunga vitabu vingi tu, kwani soko si lipo na kurudisha gharama na faida ingekuwa ni rahisi mno, lakini hali haiko hivyo, utajinyima na kuomba misaada ya udhamini wa hapa na pale na ukishachapisha kitabu chako utasoma peke yako, labda na familia yako.

Hayati Munga Tehenan aliwahi kulisema hili mara nyingi, na alishajaribu mara kadhaa kutunga vitabu vyenye maarifa haya na yale, tena aliviuza kwa bei nafuu sana, lakini wasomaji wako wapi.
Nakumbuka alipotoa kitabu chake kinachozungumzia saikolojia ya ujasiriamali, kinachoitwa, “Namna ya kupata fedha au bahati”.. ambacho kinamuandaa mtu yeyote kuzijua kanuni za maumbile na mvuto na kuvumbua kipaji chake na kukitumia ili kujitoa katika lindi la umasikini. Aliona ni busara kushirikiana na vyama vya kuweka na kukopa, yaani Saccos ili ikiwezekana wavisambaze kwa wanachama wao lakini kuwe na asilimia Fulani inayoingia katika chama, kwa ajili ya kustawisha mtaji wa saccos husika,. Hakupata ushirikiano kabisa, kwani walipuuza wazo lake na ubinafsi na ufisadi uliwekwa mbele….”Sasa sisi viongozi tutapana nini?” lilikuwa ndio swali aliloambulia.
Hayati Munga alikuwa ni muadilifu, na hakupenda kujiingiza katika hilo,,, akaona ni bora atafute namna nyingine ya kuviuza vitabu vyake, alifanikiwa kwa kiasi Fulani, ingawa haikuwa kwa kadri ya ndoto zake.

Watanzania tunapenda habari za udaku, majungu na fitina, lakini sio maarifa, hayana nafasi kabisa kwetu, hebu ona magazeti ya udaku yalivyo na soko, utashangaa….

Naacha, niwapishe na wengine…

Ramson said...

Jamani mmaliza yote....sasa niseme nini?

Kusema kweli kuna vitabu vingi ambavyo vingefaa sana kuingizwa katika mtaala wa elimu hapa nchini, hebu angalia kitabu kama kuwadi wa soko huria cha hayati Chachage, ni mfano wa vitabu ambavyo havitendewi haki kabisa na serikali yetu.

Markus Mpangala. said...

Kaka Ramson, kitau cha MAKUADI WA SOKO HURIA viongozi wetu wanakichukia sana, na kwakuwa kililenga upungwani wa serikali ya Mkapa basi chuki imeendelea. kwa taarifa nilizonazo kitabu kingine cha Chachage kinakuja. CHACHAGE: UCHAMBUZI WA SERA NA MASLAHI YA WATANZANIA. hii ni kwa mujibu wa dada Weshi Lema pale Afrikasana.

Suala la kusoma vitabu limenipa taabu kidogo kwani nimejikuta nikibishi vitu vingi na nimetayarisha makala za uchambuzi kuhusu uwongo wa wanahistoria wa kizungu kuhusu historia a mtu mweusi pale Misri. Tunasoma mambo mengi ya uwongo waliyoandika ingawa nakubali baadhi yake yanaukweli......lakini suala la ustaaarbu wa Misri tumedanganywa sana, wanahistoria toka ujerumani na kwingineko, TATIZO nilipotoa wazo la kitabu nilidokezwa kuhusu faida yaani PESA, nikafunga mafaili yangu na kuyarejesha nyumbani yametulia.

Ndiyo maana katika blogu yangu ya karibuni nyasa nimeweka UKURASA WA HISTORIA YA AFRIKA someni pale kwa umakini, na uwongo huo upo hata kwenye likitabu la wakristo wanaomhusudu jamaa mvaa misalaba wa Nazareti......samahani Mwenyekiti dada Koero kama sentesi hii inautelezi. Historai ya Rais aliyekufa karibu huko Gabon imeandikwa na wazungu, ajabu yaani hata watoto wake wanashindwa. Nashukuru HAKIELIMU kwa kuandika mkusanyiko wa mwalimu Nyerere.

asanteni kaka zangu mliotangulia kwa kutoa maoni poa.