Mungu huwa analipa hapa hapa duniani, aliendele kusimulia Eliza miaka mitano baadae nilipata taarifa kuwa aliyekuwa mchumba wangu amelazwa katika Hospitali ya Mount Meru na hali yake ni mbaya sana. Aliyenipa taarifa hizo hakuniambia kuwa anaumwa ugonjwa gani.
Sikwenda kumuona wala sikujishughulisha kufuatilia habari zake, niliendelea na maisha yangu kama kawaida. Wiki mbili baadae nilikutana na rafikiye na alishtuka sana kuniona kwani tulipoteana kwa muda mrefu sana takribani miaka mitano kwani nilihama katika shule ile siku nyingi nikapangiwa kufundisha shule iliyoko jirani na ninapoishi kwa hiyo kuja maeneo ya katikati ya mji ilikuwa ni mara chache sana.
Yule rafiki wa aliyekuwa mpenzi wangu aliniomba tutafute mahali tukae ili tuongee kwani alikuwa akinitafuta kwa siku nyingi sana. Tulisogea katika Baa iliyoko jirani na tulipofika pale yule bwana aliniomba niagize kinywaji, niliagiza maji ya kunywa.
Yule bwana akaniomba niende Hospitalini nikamuone mpenzi wangu wa zamani kwani hali yake ni mbaya na amekuwa akinitajataja sana kuwa anahitaji kuniona kabla hajafa ili aniombe radhi, nilishangaa sana, aniombe radhi kwa lipi? Mbona mimi nilishamsamehe siku nyingi.
Nilikataa kwenda kumuona, lakini baada ya rafikiye huyo kunibembeleza sana nilikata shauri niende kumuona, ili kuondoa lawama.
Nakumbuka ilikuwa ni siku ya ijumaa, rafiki wa mpenzi wangu alinifuata shuleni mida ya jioni akiwa na gari lake na tukaondoka na kwenda Mount Meru hospitali kumuona yule bwana,
Tulipofika, tulielekea wodini moja kwa moja, kwa jinsi tulivyokuwa tukitembea kuelekea wodini na ndivyo mapigo ya moyo wagu yalivyozidi kuongezeka, nilikuwa napumua haraka haraka kama vile nilikuwa nakimbia mpaka shemeji angu akawa na wasi wasi.
“Vipi shemeji, unayo matatizo ya moyo?” aliniuliza….
“Hapana sina kabisa? Nilimjibu kwa sauti ya kutetemeka. Tulipo karibia Wodi aliyolazwa yule mpenzi wangu wazamani yule shemeji yangu aliniomba tupumzike pale nje kwanza kabla ya kuingia wodini, lengo lake ilikuwa ni kunipa nafasi nipumue na ku relax kidogo.
Tulipoingia wodini niliwakuta ndugu zake wengi, nadhani walikuwa wanafahamu ujio wangu kwani walisogea pembeni na kunipa nafasi ili niweze kumuona mgonjwa.
Nilisogea pale kitandani alipo, alikuwa amekonda sana kiasi kwamba hata ile sura yake niliyoizoea ilikuwa imetoweka, alinikazia macho kwa nukta kadhaa bila kusema neno, ndugu zake waliniambia kuwa alikuwa amekata kauli tangu jana.
Alinionesha ishara niiname kama vile alitaka kuniambia kitu, nilijongea karibu na yeye na kuinama, alinishika mkono kwa nukta kadhaa kisha akaongea kwa sauti ya chini sana,,, “Naomba unisamehe mpenzi wangu, nisamehe ili nikapumzike kwa amani”
Nilijikuta machozi yakinitoka na nilishindwa kusema kitu chochote nikabaki nikiwa nimemtumbulia macho..
“Nilishakusamehe mpenzi wangu, najua sio wewe bali ni shetani ndiye aliyesababisha yale yaliyotokea yatokee” Nilimwambia.
Tuliangaliana, nikamuona akitokwa na machozi, namimi sikuweza kujizuia nilijikuta nikilia nilitoa leso yangu na kujifuta machozi na kisha kumfuta na yeye.
Niliondoka pale na yule shemeji yangu, aliyenipeleka pale. Njiani alinisimulia mkasa uliompata mpenzi wangu yule wa zamani mpaka kuwa katika hali ile.
Kumbe yule mpenzi wangu wa zamani alihamishiwa Moshi, kwa hiyo ikabidi yeye na yule mkewe aliyenisaliti wahamie moshi. Miaka miwili baadae mkewe akiwa ni mjamzito wa miezi mitatu yule bwana akapata mkasa wa upotevu wa mamilioni ya pesa katika kitengo chake na yeye kama mkuu wa kitengo hicho na wenzake wakawekwa ndani. Kutokana na mshituko wa mumewe kuwekwa ndani, yule mkewe akapoteza ujauzito.
Baadae walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka, lakini walinyimwa dhamana kutokana na unyeti wa mashitaka yao.
Inasemekana wakati mumewe akiwa bado yuko ndani, yule mkewe akawa anachapa umalaya akitembea na wanaume mbali mbali wakiwamo marafiki wa mume wake.
Ilichukua mwaka mmoja yule bwana kuachiwa kwa kufutiwa mashitaka kwa kuwa hakuhusika na ule upotevu. Alipotoka ndugu zake walimshauri amuache yule mwanamke kwa kuwa alikuwa na tabia mbaya za umalaya na alikuwa amemdhalilisha kwa ,arafiki zake, lakini yule bwana hakusikia aliwapuuza nduguzake na kumtetea mkewe kuwa hakuwa Malaya bali wanamsingizia.
Baadae yule mwanamke alipata ujauzito tena, lakini ujauzito huo ulikuwa na complicationa nyingi, na kumfanya kudhoofu sana, baadae ujauzito ule ulitoka tena na kuanzia hapo akawa ni mgonjwa wa kitandani, na alipopelekwa hospitali alikutwa na TB.
Hali ilizidi kuwa mbaya, mume alikuwa hana kazi na mke ndio alikuwa ni mgonjwa. Pamoja na juhudi za kumtibu mkewe kwa kushirikiana na ndugu zake lakini haikusaidia kwani alifariki.
Kutokana na kifo cha mkewe, yule bwana alipata mshtuko na hivyo kulazwa hospitali kwa matibabu, hata hivyo hali yake haikuonekana kutengemaa, ikabidi ndugu zake waishio Arusha wamchukue na kumhamishia Arusha kwa ajili ya kumhudumia.
Baada ya vipimo ilionekana kuwa yule bwana alikuwa ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.
Naambiwa kuwa kila siku alikuwa akinitaja taja na alikuwa anataka nitafutwe ili aniombe radhi kwani alinikosea sana.Ukweli ni kwamba mimi nilikwisha wasamehe wote na nilishasahau.
Yule rafikiye alinifikisha nyumbani kwangu, na tulipeana namba za simu na akaondoka zake. Siku iliyofuata yaani jumamosi, alifajiri alinipigia simu na kunijulisha kuwa yule bwana amefariki alifajiri ile na mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Moshi kwa mazishi inafanyika kwa kaka yake mkubwa maeneo Njiro. Nilikwenda Njiro na kuungana na ndugu wa marehemu. Nilikuwa ni miongoni watu waliosafiri kwenda Moshi kwa mazishi na ndugu wa marehemu walikuwa karibu na mimi utadhani nilikuwa ni mke wa marehemu.
Tulimzika mpenzi wangu wa zamani na kisha kurejea Arusha siku hiyo hiyo. Maisha yanaendela kama kawaida na nimeshasahau, ila tukio hili limenifundisha jambo, kuwa kama ukiona jambo haliwi kama unavyotaka au ulivyotarajia, huna haja ya kulazimisha, kwani huenda kuna kitu unaepushwa nacho. Namshukuru mungu kwa yote, kwani yeye ndiye mchungaji wangu.
Tuesday, August 18, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
4 comments:
Ninanukuu "Tulimzika mpenzi wangu wa zamani na kisha kurejea Arusha siku hiyo hiyo. Maisha yanaendela kama kawaida na nimeshasahau, ila tukio hili limenifundisha jambo, kuwa kama ukiona jambo haliwi kama unavyotaka au ulivyotarajia, huna haja ya kulazimisha, kwani huenda kuna kitu unaepushwa nacho. Namshukuru mungu kwa yote, kwani yeye ndiye mchungaji wangu." mwisho wa kunukuu.
Ni kweli kabisa hakuna haja ya kulazimisha hata hivyo namsifu dada Eliza kwa wema wake sijui kama ningekuwa mimi ningefanya alivyofanya. Hongera Eliza kwa kuwa na moyo ulio nao.Ni habari ya kusisimua sana asante Koero pia kwa mafundisho haya.
Dunia duara
Huyu jamaa H.I.V kugeuka AIDS iko kama ilichukuwa muda mchache sana!
Ningekuwa huyu dada ningeppima kucheki kwa kuwa kwa kawaida watu wenye H.I.V wanaweza kuishi na virusi muda mrefu kabla AIDS haijajitokeza.
Ni wazo tu kulingana na kufuatilia muda wa tukio mpaka Kifo!:-(
Simon, ukifuatilia kwa makini sana mikasa iliyomkuta huyo bwana, kutokuwa na kazi na kumuuguza mgonjwa. ni wazi kuwa lishe ilikuwa matatizo na msongo wa mawazo ulikuwa mkubwa pia. Hiyo inaweza kuchangia HIV kwenda kwenye AIDS kwa muda mfupi, Pia inawezekana alipata muda hata kabla ya kupata hiyo misukosuko. NIMESOMA KITU KWENYE HII HADITHI
Post a Comment