Tuesday, August 25, 2009

UMRI WA UBARUBARU NA VIBWEKA VYAKE!!!


Ilikuwa ni mwaka 1998 na ninaukumbuka vizuri sana huo mwaka, kwani ndio mwaka niliovunja ungo, ni kipindi hicho ambapo nilianza kushangaa maumbile yangu jinsi yalivyobadilika na nilikuwa nahisi kuwa na mamlaka makubwa sana, sikutaka kuchuliwa kama mtoto tena ingawa nikuwa bado ni mtoto, kwa umbo na umri.
Nilikuwa nagombana na mama pamoja na dada zangu mara kwa mara pale nyumbani na sikusikia la mtu. Nilikuwa ni mbishi na mkorofi kwa kila mtu pale nyumbani, lakini mama yangu alikuwa ainichukulia kwa tahadhari sana, daima alizoea kusema kuwa hayo ni mapito tu. Kipindi hicho sikumuelewa juu ya kauli ile, lakini sasa nimemuelewa, tena vizuri sana.

Siku moja wakati naenda shule nilikutana na kijana mmoja mzuri na mtanashati hivi na kama bahati nzuri wote tulikuwa tunaelekea kituoni, kupanda basi, nilijikuta nikivutiwa na yeye na nilitamani sana kumsemesha lakini nilikuwa nawaonea aibu sana wanaume nikabaki nikimuangalia kwa jicho la kumuiba. Tulipofika kituoni nilijikuta kila saa nikimtazama, na kila akigeukia upande niliposimama na kugongana macho na mimi nilikuwa naangalia pembeni kwa aibu.

Nilitamani sana kumsemesha lakini sikuweza kufanya hivyo kutokana na aibu na pia nilikuwa nawaogopa wanaume. Nakumbuka wakati nilipokuwa mdogo, nilikuwa namsikia mama yangu akizungumza na dada zangu na kuwaeleza juu ya athari za kujenga mahusiano na wanaume katika umri mdogo, sikuwa nayasikiliza yale mazumgumzo kwa kuwa nilijua hayanihusu, jambo lingine ni juu ya tabia yangu sikuwa nawapenda sana wanaume na nilikuwa sina kawaida ya kuwazoea wavulana hata wale niliokuwa nikisoma nao.

Lakini tangu nimuone huyu kaka kwa jicho la kwanza, nilijikuta nikivutiwa naye ingawa sikujua kuwa navutiwa naye ili iweje, ila nilitamani sana kuwa naye karibu. Nikiwa katika lindi la mawazo huku nikiwa katika dunia ya peke yangu basi lilifika na yule kijana alipanda na kuondoka na kuniacha pale kituoni nikiwa nimeshikwa na butwaa huku nikijilaumu kwa kutomsemesha wala kumuuliza jina lake.

Sikuchukua muda nami nikapata basi na kupanda na kuelekea shuleni. Nilipofika shuleni ile sura ya yule kijana ilikuwa ikinijia mara kwa mara, na siku hiyo masomo hayakupanda kabisa mpaka mwalimu wangu mmoja akaniuliza kama nilikuwa naumwa, nikikataa kwa kumjibu kuwa siumwi, lakini nadhani aliona kuwa sikuwa katika hali ya kawaida siku hiyo. Niliporudi jioni nilikutana na kaka mmoja jirani yetu, ambaye nilikuwa nasoma na mdogo wake shule moja lakini madarasa tofauti, alinisimaisha na kuniuliza kama nimemuacha wapi mdogo wake, nilimjibu kwa kifupi kuwa nilimuacha kituoni, mara ghafla yule kijana akaja pale tulipo na kunisalimia kwa kunishika mkono, nilijikuta nikitetemeka na mapigo ya moyo wangu yakienda mbio, nilimjibu huku nikiangalia pembeni kwa aibu sikutaka kukutanisha macho na yeye, nadahani hata yeye alihisi jambo kwani aliniachia mkono wangu.

Yule kijana tunayeishi naye jirani alinitambulisha kwa yule kijana kuwa ni mjomba wake na yuko pale kwa muda akisubiri kujiunga na masomo ya kidato cha tano, ambapo alikuwa amepangiwa kwenda kusoma Tabora Boys. Kuanzia siku hiyo nilikuwa siishi kwenda kwa akina yule binti tuliyekuwa tunasoma naye lengo lilikuwa ni kutaka kumuona huyu kijana, ingawa sikuweza kuzungumza naye kutokana na kuwa muda mwingi alikuwa bize sana akijisomea.

Siku moja kama kawaida yangu nilikwenda pale nyumbani kwa rafiki yangu lengo langu kama kwaida lilikuwa ni kataka kumuona yule kijana na siku hiyo nilipania sana nizungumze naye, na kweli siku ile ilikuwa ni kama bahati kwangu nilimkuta yuko peke yake pale nyumbani na mtumishi wao wa pale nyumbani. Alianzisha mazungumzo na swali lake la kwanza alitaka kujua kuwa kama nimeokoka, nilimjibu kuwa sijaokoka, nilimrudishia swali lile kwa kumuuliza kama na yeye ameokoka. Jibu lake lilipenya moyoni mwangu kama mkuki moyoni. Alinijibu kwa upole kuwa ameokoka tangu akiwa darasa la tano, kutokana na kumtegemea yesu na ndio maana amekuwa akifaulu tangu darasa la saba mpaka sasa anatarajia kujiunga na kidato cha tano.

Jibu lake halikunifurahisha hata kidogo, lakini sikujua sababu ni nini?
Alitumia fursa ile kunishawishi niokoke na kumkubali yesu kuwa mwokozo wangu, nilimkatalia katukatu kuwa sikuwa tayari kuokoka, alinipa mifano mingi katika biblia, lakini hakuna hata moja lililoniingia katika mazungumzo yake bali nilikuwa najisikia furaha kwa jinsi alivyokuwa akizungumza kwa upole kama ananibembeleza, mawimbi ya sauti yake yalikuwa yakipenya katika masikio yangu kama vile aina fulani ya muziki mororo.

Nilikuwa natamani aendelee kuongea tena na tena. Lakini mara ghafla wenyeji walirudi na sikuwa na budi kuaga na kuondoka. Nilianza kuzoeana na yule kijana lakini mazungumzo yake ya kunishawisi niokoke sikuyapenda, hata hivyo ilibidi nikubali kuambatana naye kanisani anaposali ilimradi niwe naye karibu, kule nyumbani nilikuwa naaga kuwa nakwenda kwa rafiki yangu kujisomea.

Pale kanisani alinitambulisha kama mgeni wake ambaye amekubali kumpokea yesu kristo, nilishangiliwa sana na kupongezwa kwa uamuzi wangu ule, ingawa dhamira yangu ya kuwepo mahali pale haikuwa ni kwa ajili ya wokovu kama ilivyosemwa bali ilikuwa ni mapenzi niliyokuwa nayo kwa huyu kijana. Nilianza kujenga wivu, kila nikimuona anaongea na msichana mwingine pale kanisani kwao, roho ilikuwa inaniuma sana.

Siku moja wakati tunatoka kanisani alikuwa akinisindikiza kurudi nyumbani, mara tukakutana na kaka yangu mkubwa akaniuliza natoka wapi na yule niliyefuatana naye ni nani, nilimjibu kwa kiburi na jeuri kuwa haimuhusu, basi kaka alimfokea sana yule kijana kuwa anataka kuniharibia maisha na kumtishia kuwa atampiga. Yule kijana kwa uungwana aliondoka zake bila kusema chochote na kurudi kwao. Niliumia sana na niliporudi nyumbani nilijifungia chumbani kwangu na kulia sana.

Mama alikuja chumbani kwangu na kuniuliza sababu ya kulia, nilimueleza kila kitu, mama hakusema kitu aliondoka zake, lakini kaka alikuja huku nyuma na kunifokea sana.
Kesho yake nilisikia alikwenda pale alipofikia yule kijana na kumfokea sana yule kijana na kutoa onyo kuwa akimkuta na mimi atamfunga aozee jela. Ukweli ni kwamba kaka yangu huyu mkubwa alikuwa ni mkorofi sana, na alikuwa haelewani hata na dada zangu kwa kuwaingilia katika mambo yao wakati walipokuwa wanasoma.

Nilipopata taarifa juu ya yule kijana kufuatwa na kufokewa na kaka, iliniuma sana na niliamua kuchukuwa uamuzi hatari wa kutaka kujiua kwa kuhisi kudhalilishwa pale mtaani, nilikunywa idadi kubwa ya vidonge ambavyo hata sikujua kama vilikuwa ni vidonge gani na kujifungia chumbani kwangu, baadae nilianza kujiskia vibaya na hivyo nikaanza kuugulia, dada yangu alinisikia na alipoingia chumbani kwangu na kunikuta katka hali ile, nilimsikia akimuita mama kwa sauti kubwa “mama mwanao anakufa” nilipoteza fahamu na niliposituka nilijikuta nikiwa hospitalini nikiwa nimetundikiwa Dripu.

Siku iliyofuata niliruhusiwa na kurudi nyumbani, mama yangu alichukuwa nafasi ile ya kuwepo kwangu nyumbani kwa mapumziko ya kuumwa kunipa darasa juu ya mabadiliko ya kimwili baada ya kuvunja ungo na hisia za kimapenzi, mama alikuwa wazi kwangu kwa kunieleza kila kitu juu ya mapenzi ya utotoni na athari zake na jinsi ya kuepuka vishawishi na namna ya kukabiliana na changamoto za usichana, na kikubwa zaidi aliniasa sana juu ya kuwaepuka wavulana wakware.

Naomba nikiri kuwa kwa swala langu yule kijana hakuwa na makosa na kamwe hakuwahi kunitamkia jambo lolole linalohusu na mapenzi wala kuonesha dalili za kunitamani licha ya kujipendekeza sana kwake, bali mimi ndiye niliyekuwa na kiherehere.

Baadae nilipata taarifa kuwa yule kijana aliamua kurudi kwao ili kuepusha shari. Ilinichukuwa takribani mwaka mzima yule kijana kufutika katika mawazo yangu kabisa, kwani pamoja na semina ya mama lakini nilikuwa najikuta tu natamani nikutane naye barabarani, jambo ambalo halikutokea na wala halitakuja kutokea.

Miaka miwili baadae nilipata habari ya kusikitisha, na ambayo iliniacha na majonzi hadi leo, yule kijana alifariki kwa ajali wakati akirudi nyumbani kwao baada ya kumaliza mitihani ya kidato cha sita. Ingawa nilishamsahau kutokana na kujitambua lakini habari za kifo cha yule kijana kilinisitua sana na kunikumbusha machungu ya siku ile niliyotaka kujimaliza kwa ajili yake. Najua ilikuwa ni utoto, lakini kwangu mimi lile lilikuwa ni darasa tosha.
Labda niwaulize wasomaji wa blog hii, hivi ni wazazi wangapi ambao wako wazi kwa mabinti zao kwa kuwaeleza ukweli juu ya mabadiliko ya miili yao pindi wanapovunja ungo?
Je ni wazazi wangapi ambao wako tayari kuwakabili mabinti zao na kuwaambia ukweli huu bila kuogopa mila na desturi ambazo nyingi zimepitwa na wakati?

Jamani umri wa ubarubaru una misukosuko na vitimbi vingi……….

Sikuandika habari hii ili kujidhalilisha bali kutaka wasomaji wa blog hii wajifunze kupitia uzoefu wangu huu. Naitwa Koero Japheti Mkundi

6 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Mmhhhhhh!!

Unknown said...

Ni uzoefu mzuri, na nimejifunza kitu hapo, ahsante kwa darasa lako...

Yasinta Ngonyani said...

Koero Ahsante sana kwa hili kwa sababu umenipa mafunzo nini mama anatakiwa kumweleza binti yake na mimi ninao huo mzigo na nimekuwa nikiwaza kila siku. Pia nakusifu sana kwa ushujaa wako wa kujieleza jinsi ulivyofanya sio wengi wanaweza kufanya hivyo. Pia napenda kukupa pole kwa kifo cha huyo kijana. Nikisema hivi najua, nina maana penzi la utotoni la kwanza ni kitu ambacho mtu huwezi kusahau. Hata kama wewe umesema ulimsahau lakini naamini kamwe hutamsahau atakuwa moyoni mwako milele niamini mimi. Asante Koero, Pia nami umenikumbusha kitu mmmmmh maisha haya kazi kwelikweli. Na mwisho napenda kumpongeza mama Namsifu kwa malezi yake bora. Mpe hizi salamu.

Yasinta Ngonyani said...

Nimerudi tena kuna kitu nilisahau:- Ni hivi napenda kumshukuru dada alipokustukia umekula vile vidonge. pia ndugu, mama Namsifu na nawashukuru pia waganga na waauguzi wate waliookoa maisha yako. kupenda ni kitu cha ajabu sana. Nimewashukuru hao waliokoa maisha yako kwa sababu leo hii sisi au mimi nisingekuona na hatungejuana. Na tungekosa haya mafunzo yote unayotoa hapa kibarazani kwako. NAJIVUNA SANA KUWA MA MDOGO KAMA WEWE. Ni hayo tu.

MARKUS MPANGALA said...

Nipo fasta sana kwahiyo nimeshindwa kuingia katika kibaraza changu lakini.......... Koero hii kitu ni tamu sana, tena sana nimefurahi kuwa unaweza kuongelea haya mambo maana watu tunadhani mifano lazima iwe ya wengine wakati nasi tunayo

BRAVO.
NB: mama yangu huwa anauliza swali moja anapotunda kuhusu ukimwi na mahusiano; MARA NGAPI UMESAHAU KUTUMIA KONDOMU?

HILO NDILO SWALI LA MAMA YANGU anapomwaga darasa lake lenye ucheshi

Markus Mpngala a.k.a mnyasa / paroko

PASSION4FASHION.TZ said...

Mmmh! Koero mpenzi nimesoma hii habari kwa msisitizo,ni nzuri na inamafunzo kwa vijana na wazazi pia,nimependa ulivyo muwazi,hicho kipindi kila kijana anakipitia kwa wasichana na wavulana pia.

Mara nyingi nimekuwa napitia hapa kibarazani kwako,kila habari unayoandika hapa huwa inanivutia sana,nazani ni mwandishi mzuri unafaa kuwa mwandishi wa vitabu.

Asante sana kwa kutupa darasa.