Alipofika hapa Arusha kwa mara ya kwanza ni mimi niliyempokea, nakumbuka ilikuwani mwaka 2000. Alikuwa ndio amemaliza chuo cha ualimu huko Ndala Tabora na alipangiwa kuja kufanya kazi hapa Arusha.
Akiwa ni mzaliwa wa huko Old Moshi mkoani Kilimanjaro, hakuwa na ndugu wala jamaa hapa Arusha, hivyo akiwa kama mwalimu mwenzangu nilimpokea na kukaa naye kama mdogo wangu. Hata hivyo uamuzi wa kumkaribisha binti huyu nyumbani ulifurahiwa na mpenzi wangu ambaye ni mchaga na alimuona yuele binti kama dada yake na mimi kuanzia siku hiyo tukawa tunaitana wifi na binti huyo.
Kwa kuwa nilikuwa na ugeni pale nyumbani ilibidi wakati mwingine niwe naenda kulala kwa mpenzi wangu kwa sababu pale nyumbani nafasi ilikuwa ni ndogo, kwani kutokana na mishahara ya waalimu kuwa midogo na kodi za nyumba hapa Arusha kuwa juu sikuwa na uwezo wa kulipia vyumba viwili.
Tulikuwa na kawaida ya kutoka jioni mara kwa mara mimi na mpenzi wangu kwenda kula nyama choma, nililazimika kumchukua wifi yangu na kutoka naye ili asijisikie mpweke.
Nakumbuka siku moja, wifi yangu huyo aliniuliza kama nina muda gani tangu niwe na uhusiano na kaka yake, nilimjibu kuwa tuna miaka minne tangu tuwe wachumba. Huku akionekana kushangaa alisema “Miaka minne hamfungi tu ndoa mnangoja nini?”
“Sijui kaka yako, kila nikimwambia tufunge ndoa anadai eti hajajiandaa, mpaka akamilishe mambo fulani”
“Mimi siwezi, miaka minne mko wachumba tu! Si umzalie mtoto labda ndio atachukua uamuzi? Alishauri wifi yangu,
“Siko tayari kulazimisha kuolewa kwa kumbebea mwanaume mimba kisa nataka kuolewa, kama anasubiri mpaka nibebe mimba, basi atasubiri sana,” nilimjibu
“Wifi wanaume wa siku hizi mwanzangu, wagumu kweli kuoa, usipowabebea mimba basi utabaki hapo, utashangaa kesho unasikia ana mtoto kwingine au anaoa mwanamke mwingine kisa kamjaza mimba” Alisema wifi yangu
Wifi kama imepangwa tuoane tutaoana lakini kama haijapangwa basi labda ni mipango ya mungu, nilimjibu.
Kuanzia siku hiyo nikashangaa kukawa na ukaribu sana kati mpenzi wangu na huyo wifi yangu, mara nyingi ilikuwa mpenzi wangu akija anatumia muda mwingi akiongea na huyo wifi yangu tena wakati mwingine wakiongea kikwao yaani kichaga, hata hivyo sikujali sana kwani nilikuwa namuamini sana mpenzi wangu.
Nilikaa na binti yule kwa takribani miezi sita na ndipo akapata chumba na kuhama.
Nilifurahi sana kwa binti huyo kuhama kwani nilijua kuwa sasa nitapata wasaa wa kujivinjari na mpenzi wangu, lakini mambo yalkuwa ni kinyume, kwani mpenzi wangu alibadilika na alikuwa haonekani kwangu kama ilivyokuwa kawaida yake, na nilipokuwa nikimuuliza alikuwa akisingizia kuwa yuko bize sana.
Mpenzi wangu alikuwa ni mtumishi wa Benki na kipindi ambacho anakuaga bize ni kipindi cha mwisho wa mwaka kutokana na kufunga hesabu za mwaka. Kwa hiyo kitendo cha mpenzi wangu kuwa bize katika kipindi kile kilinishangaza sana, hata hivyo hakupunguza upendo wake kwangu, aliendelea kunipenda na kunihudumia kama kawaida na tena aliongeza upendo sana kwangu kiasi kwamba sikuweza kumtilia mashaka kuwa huenda amepata mpenzi mwingine.
Siku moja majira ya jioni nikiwa ndio nimerudi kutoka kazini nilipokea simu kutoka Singida kuwa mama yangu ni mgonjwa na kama nikimkuta hai ni bahati. Miaka mitatu iliyopita ndio nilimpoteza baba yangu kutokana na ugonjwa wa Kansa na sasa ni mama yangu sijui amepatwa na nini masikini. Kwa kuwa nilikuwa ni katikati ya mwezi na sikuwa na akiba ya kutosha nyumbani nilikata shauri kumpigia simu mpenzi wangu ili anipe msaada wa kifedha ili siku inayofuata nisafiri kwenda nyumbani kumuona mama yangu ambaye mpaka wakati huo sikujua kama yuko hai au ameshafariki, lakini nilipompiga simu mpenzi wangu, simu yake ilikuwa imezimwa. Huku nikiwa nimechanganyikiwa niliamua kwenda kazini kwake na nilipofika nikaambiwa ametoka.
Ilibidi niende nyumbani kwake maeneo ya Kaloleni na nilipofika huko napo sikumkuta. Nilikaa pale nje nikiwa nimechanganyikiwa kabisa nisijue cha kufanya, niliamua kumpigia simu yule wifi yangu niliyempokea na kukaa naye pale kwangu, siku hiyo ya ijumaa hakuja kazini alituma ujumbe kuwa anaumwa na asingeweza kuja kazini, na yeye nilipopiga simu iliita sana bila kupokelewa, na nilipojaribu kupiga tena simu ilikuwa imezimwa, niliamua kwenda nyumbani kwake maeneo ya Sanawari, na nilipofika nilikuta mlango wake umefungwa lakini nilisikia sauti ya redio ikiimba nyimbo za dini. Niliona viatu vinavyofanana kabisa na vya mpenzi wangu pale nje, nilihisi labda atakuwa ameamua kumtembelea dada yake.
Nilibisha hodi mara kadhaa, mara mlango ukafunguliwa, yule wifi yangu aliponiona alistuka sana na akafunga mlango haraka na kuniambia nisubiri. Mara alitoka na kufunga mlango kwa nje na huku akiwa amekunja sura akaniuliza nina shida gani, nilishangaa jinsi alivyoonekana kukerwa na ujio wangu, nilimuuliza kama anaendeleaje na kuumwa
“Yaani umetoka kwako kuja kutaka kujua tu kama ninaendeleaje, si ungepiga tu simu, sasa usumbufu wote wa nini?”
Nilimjibu kuwa nilipiga simu sana lakini haikupokelewa, nikadhani labda amezidiwa.
Kama nikutaka kujua hali yangu, basi mimi ni mzima wa afya, samahani nina mgeni ananisubiri ndani, alisema vile na kugeuka kuelekea ndani. Nilishangazwa na majibu yale, lakini nilijua labda ni kwa kuwa anaumwa, unajua sisi wanawake tuna vipindi tunakuwa na visirani kutokana na matatizo yetu mzunguko wa mwezi.
“Samahani Gau, nina matatizo na ndio nikaja kukuona, nimepigiwa simu kutoka nyumabni mama yangu ni mgonjwa mahututi, naomba kama una akiba ya shilini elfu hamsini unisaidie kisha nitakurudishia, nimejaribu kumpigia simu kaka yako lakini simu yake imefungwa” nilimwambia..
Aligeuka kwa dharau na kuniambia, “ hivi kumbe hukuja kuniona bali umeletwa na shida zako, kama ni pesa sina mtafute sijui mpenzi wako au mume mtarajiwa akusaidie” alisema vile na kuondoka zake akiniacha pale nje.
Nilisimama pale nje kwa nukta kadhaa nikiwa nimeduwaa, nilikuwa siamini kile kilichotokea, ama kweli fanya wema wende zako usingoje shukurani walisema waswahili, nilikaa na binti huyu kwa upendo. Miezi yote sita niliyokaa naye hakuwa akipokea mshahara kutokana na kuwa nje ya bajeti ya mshahara, nilimsaidia kwa kila kitu na hata alipopata malimbikizo ya mshahara alitaka kunirudishia kiasi cha fedha nilizokuwa nikimpa lakini nilikataa na ndipo akamudu kutafuta chumba na kuhama, sasa leo nakuja kumuomba anikopeshe pesa kidogo ananijibu kama anamjibu mtu asiyemfahamu!
Niliondoka nikiwa nimechanganyikiwa, kwanza nilijiuliza juu ya vile viatu vinavyofanana na vya mpenzi wangu nilivyovikuta pale nje kwa yule binti, halafu kile kitendo cha kustuka aliponiona, na mbona alitoka na kufunga mlango kwa nje, au alikuwa hataki nimuone huyo mgeni wake, atakuwa ni nani? Nilijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu. Niliamua kumpigia simu rafiki wa mpenzi wangu wanaefanya nae kazi, alinielekeza mahali alipo, alikuwa kwenye Baa na rafiki zake wakinywa pombe na nyama choma, nilipofika alinikaribisha na kuniagizia bia, lakini nilikataa na sikupoteza muda nilimsimulia matatizo niliyo nayo, na yeye alijaribu kumpigia simu mpenzi wangu lakini simu yake haikupatikana.
Alinipa kiasi cha shilingi laki moja na kuniambia atamalizana na mpenzi wangu.
Nilikwenda kutoa taarifa kwa mwalimu mkuu na alinipa ruhusa ya siku tatu. Siku iliyofuata niliondoka asubuhi na mapema kwenda singida na hata asubuhi wakati naondoka nilipojaribu kumpigia simu mpenzi wangu simu yake haikupatikana vile vile.
Nilipofika nilikuta watu ni wengi pale nyumbani, nikajua kuwa, mama yangu ameshafariki. Ni kweli alikuwa amefariki siku ile ile niliyopigiwa simu, na kilichomuua ni shinikizo la damu.
Tumezaliwa watoto watano wanaume wanne na mimi mwanamke peke yangu, na ni wa mwisho kuzaliwa, tangu baba afariki kaka zangu wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara wakigombea urithi wa mali alizoacha baba ambazo ni nyumba mbili na mifugo kadhaa, yaani ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku.
Ugomvi huo ndio chanzo cha mama kupata shinikizo la damu na kufariki kutokana na ugomvi wa kaka zangu usioisha kutokana na kugombea mali za mzee.
Katika familia yetu mimi peke yangu ndiye niliyebahatika kuendelea na masomo hadi kuwa mwalimu lakini kaka zangu walikataa kusoma na kukimbilia kuwa wachuuzi wa biashara ndogo ndogo.
Tulimzika mama na baadae ndugu wa baba waliweka kikao na kupitisha uamuzi kuwa mifugo igawanywe na kisha nyumba ziuzwe na kila mtoto apewe chake ili kukata mzizi wa fitina.
Kila kitu kilifanyika kama maamuzi ya baraza la wazee walivyoamua, nilikabidhiwa ng’ombe zangu kumi na mbuzi nane na kondoo sita na nyumba ziliwekwa chini ya wazee wa familia ili zitakapouzwa kila mtu apate mgao wake, huo ndio ukawa mwanzo wa familia kusambaratika.
Nilikabidhi ile mifugo kwa mjomba wangu kaka yake mama na kuondoka kurudi Arusha kuendelea na kazi.
Kipindi chote nilipokuwa msibani Singida nilijitahidi kumtafuta mpenzi wangu lakini simu yake hauikupatikana.
Niliripoti kazini na kupokelewa na walimu wenzangu, na kuanza kazi, sikumkuta yule wifi yangu kazini niliambiwa kuwa aliaga kwenda kwao Moshi kuhudhuria matatizo ya kifamilia.
Baadae nilianza kusikia minong’ono kwa kaenda kwao kumtambulisha mchumba wake, sikufuatilia habari hizo, niliendelena na kazi zangu.
Siku iliyofuata nilipokwenda nyumbani kwa mpenzi wangu niliambiwa kuwa amesafiri kaenda kwao Moshi.
Siku tatu baadae nikiwa nyumbani kwangu uani nimetulia nikiwa bado nina majonzi ya kufiwa na mama yangu, mchumba wangu alikuja kwangu lakini hali aliyokuja nayo ilinishtua, hakuwa mchangamfu kama nilivyomzoea. Nilimkaribisha ndani, alisita kidogo kisha akaingia ndani, kabla hajakaa alianza kunishambulia kwa maneno makali eti nimemdhalilisha sana kwa marafiki zake kwa kitendo changu cha kukopa pesa kwa rafiki yake badala ya kumtafuta, aliongea kwa sauti ya juu na hakunipa nafasi ya kujieleza.
Aliniambia kuwa kuanzia wakati huo mimi na yeye tusijuane niende kwa huyo huyo aliyenipa nauli ya kwenda Singida. Aliondoka bila ya kunisikiliza na kutoweka.
Nililia sana kwa uchungu. “Sijui nina mkosi gani mie,” nilijisemea
Niliamua kumtafuta rafiki yake aliyenipa nauli ya kwenda nyumbani, Singida, nilimpata na baada ya kumweleza yaliyonipata, alishanga sana na alipompigia simu ili kujua sababu ya kuninyanyasa alimjibu kuwa hayamuhusu na kukata simu.
Yule shemeji aliniambia kuwa nirudi nyumbani na atajaribu kutusuluhisha. Yule wifi yangu alirudi kutoka kwao, na kuripoti kazini, lakini hakunichangamkia wala kunipa pole, nilishangaa sana, kwani sikuwahi kugombana naye.
Nilikuwa sina mawasiliano na mpenzi wangu kabisa na hata namba yake ilikuwa haipatikani, baadae nilikuja kugundua kuwa amebadilisha namba, hiyo ni baada ya kumpigia rafiki yake mmoja na ndio akaniambia kuwa amebadilisha namba.
Siku moja jumamosi nikiwa zangu sokoni nilikokwenda kununua mahitaji nilikutana na mpangaji mwenzie na mpenzi wangu tulisalimiana, na kuanza kupiga stori za hapa na pale, aliniuliza kwa nini sionekani tena pale kwa mpenzi wangu, sikutaka kumweleza juu ya tofauti zetu, nilijua tu kuwa lile lilikuwa ni tatizo la kawaida ambalo lingeisha, kwani kutofautiana kwa watu wawili wapendanao ni jambo la kawaida tu. Nilimjibu kwa kifupi tu kuwa niko bize na masomo, nilimdanganya kuwa ninasoma chuo kikuu huria. Alionekana kutoridhika na jibu langu, nilimuaga na kuanza kuondoka, lakini wakati naondoka, aliniita kwa nyuma “Eliza” nilisimama ili kumsikiliza.
“Nina mazungumzo na wewe unaweza kunipa nafasi tukae mahali tuongee kidogo, ni kwa faida yako” aliniambia kwa kuonesha msisitizo.
Nilimkubalia, tukasogea hadi kwenye baa moja iliyokuwa jirani, aliniomba niagize kinywaji, nikaagiza maji na yeye akaagiza soda.
“Hivi ni kweli umeachana na mpenzi wako” Alianza mazungumzo kwa kuniuliza swali
Nilishikwa na mshangao, kwa swali lile, nikamuuliza sababu ya kuniuliza lile swali.
Mbona tunamuona yule binti uliyekuwa ukija naye pale kwa mpenzi wako, ndiye ameshikana uchumba na mpenzi wako na hivi karibuni alipekeka posa huko uchagani,
Hayo maneno ya mwisho niliyasikia kama mwangwi, na mwili wote umekufa ganzi, nilibaki kimya kwa nukta kadhaa, nilibabaika kidogo…
Yule mwanamke alionekana kushangaa, ina maana ulikuwa hujui?
Nilimjibu kuwa nilikuwa sijui, nilimshukuru na kuondoka zangu kuelekea nyumbani,nilipofika niliweka mizigo yangu ndani, nikatoka kuelelekea kwa yule binti Sanawari, nilipofika niliingia ndani moja kwa moja bila kubisha hodi, nilibaki nimesimama huku nikitetemeka, nilimkuta mpenzi wangu na yule binti wakilishana chakula kwa mahaba….
Sikuamini macho yangu, na hata wao walibaki wameduwaa, niliondoka mahali pale bila kusema lolote, hata majirani ambao walikuwa uani wakati huo walijua kuwa kuna jambo kwani niliwapita bila kuwasemesha na niliondoka bila kuwaaga.
Nilikwenda kwa mwalimu mwenzangu mmoja ambaye ni rafiki yangu, na kumweleza kila kitu. Kwa mujibu wa maelezo yake ni kwamba kumbe kipindi kile niliposafiri kwenda kumzika mama yangu ndio akachukua likizo ya wiki moja kwa madai kuwa amepata mchumba lakini alikuwa akitamba kuwa atatushangaza pale kazini. Hakuna aliyejali maneno yake.
Siku iliyofuata nilifika kazini na niliamua kuchukua likizo ya wiki mbili ili kupumzisha akili kwani nilihisi kuchanganyikiwa, nilimueleza mwalimu mkuu kila kitu naye alitaka kutukutanisha ili kujaribu kuondoa tofauti zetu lakini nilikataa, na alikubali kunipa likizo.
Nilikaa nyumbani siku zote nilikuwa nilishinda ndani nikilia. Kwa muda mfupi nilikonda sana. Kumbe huku nyuma wakati nikiwa likizo yule binti aliomba uhamisho wa haraka na kwa kutumia pesa alifanikiwa kuhamishiwa shule nyingine.
Baada ya wiki mbili nilirudi kazini, lakini nilikuwa na aibu sana kwa kuhisi kufedheka, ilikuwa hata waalimu wenzagu wakicheka nahisi wananicheka mimi, pale nilipokuwa nikikaa napo mambo yaligeuka, baadhi ya wapangaji wenzangu ambao tulikuwa hatuelewani walitumia nafasi hiyo kunikejeli na kunisengenya waziwazi, nilikosa amani.
Niliamua kuhama, na baada ya wiki mbili nilihamia maeneo ya Sakina. Miezi mitatu baadae nakumbuka ilikuwa ni mwanzoni kwa mwaka 2001 yule mchumba wangu alifunga ndoa na yule binti, tena ilikuwa ni ndoa kubwa hasa iliyosheheni mbwembwe kibao. Siku hiyo niliamua kwenda Moshi kwa mwanafunzi mwenzangu niliyesoma naye chuo cha ualimu Patandi.
Siku zilipita na maisha yaliendelea, niliamua kusahau yote na kikubwa zaidi niliwasamehe yule mchumba wangu na yule binti, nikaendelea na maisha kama kawida.
Tangu wakati huo sijapata mwanaume wa kunioa, nimekuwa na uhusiano na wanaume kadhaa ambao waliniahidi kunioa lakini baada ya kuwa nao kwa miezi kadhaa waliniacha bila sababu.
Ninaumia sana mpaka sasa sijabahatika kupata mtu wa kunioa achilia mbali kupata mtoto, nimefikia mahali natamani sana kuwa na mtoto lakini nitamzaa na nani? Wanaume walivyojaa ulaghai. Ingawa nimebahatika kujenga nyumba yangu huko maeneo ya Kwa Moromboo baada ya kupata fedha za mgao wa mauzo ya nyumba zetu za urithi, lakini nahisi nina deni kubwa sana, nahitaji sana kuwa na mtoto.
Jana jumamosi siku ya Sabato nilishinda nyumbani nikitafakari majukumu yaliyonileta hapa Arusha, sikuwa na kazi nyingi za kufanya zaidi nilitumia muda wangu kupitia mtandao ili kusoma mawazo ya wenzangu katika blog mbali mbali.
Mara akatokea mgeni, naye si mwingine bali Rafiki wa wenyeji wangu, anayeitwa Elizabeth. Tangu nimefika hapa Arusha kwa mjomba nilitokea kufahamiana na dada Eliza na ametokea kuwa rafiki yangu wa karibu kiasi cha kuwa tunashauriana juu ya maisha na mambo mengine ya kitaaluma.
Dada Eliza ambaye ni Mwalimu ndio ametimiza umri wa miaka 38 lakini ukimuona umbo lake utadhani ni binti wa miaka 25 hivi, ukweli ni kwamba ana mwili mzuri.
Kwa udadisi wangu katika mazungumzo yetu ya jana nilitaka kujua kwa nini mpaka leo hajaolewa na wala hana mtoto? Na hiyo ndiyo ilikuwa simulizi yake.
Simulizi ya dada Eliza inasikitisha na kuhuzunisha sana. Ukweli ni kwamba wapo wanawake wengi wanatamani kuolewa lakini wamejikuta wakikabiliwa na mazingira kama ya dada Eliza, kusalitiwa, kudanganywa na kutapeliwa kimapenzi.
Kuna kusigishana sana linapokuja swala la kuoa au kuolewa, jamii imetufundisha kuwa mwanaume ndiye mwenye mamlaka ya kuamua kuoa na mwanamke anasubiri kuolewa, kwa maana ya kusubiri tamko la mwanaume kuwa yuko tayari kumuoa, na sio yeye aamue.
Tumekuta tayari utaratibu huo upo na umepewa nguvu na mila na desturi pamoja na hizi dini zetu za mapokeo, tumefika mahali wanaume wanawachezea wasichana watakavyo kwa kigezo cha kuwadanganya kuwa watawaoa, wakati hilo halina ukweli kabisa.
Mimi mpaka leo najiuliza hivi kwa nini watu wanaoana, ni ili iweje? Je watu wanaoana kwa sababu wanapendana au ili wapate watoto?
Na kama watu wanaoana kwa sababu wanapendana, sasa mbona kuna talaka nyingi, kwa nini watu wanaachana? Talaka siku hizi zimekuwa kama jambo la kawaida kabisa.
Kama watu huona ili wapate watoto, Je haiwezekani mtu kupata watoto bila kuoa au kuolewa?
Hivi Mungu alisema muende mkazaane na kuijaza dunia au mkaoane na kuijaza dunia?
Sasa ndio hatokei wa kuoa au kukuoa, ndio hutazaa mpaka uoe au kuolewa?
Hili linahitaji tafakuri………….
ITAENDELEA………….
Sunday, August 9, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
4 comments:
Mmhhhh!!! Ndio nimezaliwa sijajua kuandika saana, Nikijua (by baadae) ntarejea. Lol
Blessings
Wakati huyo mtoto Mubelwa analialia ili anyonye, wacha t'wendelee.
Da Koero, ni simulizi inayosikitisha mno. Ndivyo mara nyingi mambo huwa. Nimpe pole nyingi sana da Eliza. Kwake maisha yamekuwa na tafsiri ya kusambaratika kwa familia, usaliti katika urafiki na mapenzi na mambo mengine mabaya.
Uwifi huu, usio na udugu wa damu, mara nyingi huacha madhara. Nasema hivyo kwani naifahamu stori ya ndugu yangu ambaye naye alikuwa na wifi kwa kigezo cha kabila moja na mumewe. Kwa bahati mbaya, kwa huruma zake akampa hifadhi nyumbani kwake, kisa wifiye huyo wa bandia ndo ameanza kazi. Hivyo akampa hifadhi ili ajipange sawasawa. Kilichojiri? Akapigwa bao na wifiye.
Tuache hayo. Da Eliza amefanyiwa jambo baya. Jambo ambalo limeacha makovu makubwa maishani mwake. Nampa pole sana. Namwombea faraja katika maisha. Namwombea kujaaliwa kupata mtoto. Namwombea kunusurika na laghai zetu wanaume.
Nirudi kwako da Koero. Suala la kuoa/olewa na kuzaa lina muktadha wake. Kwa jamii, hutegemeana na jamii fulani inavyolichukulia. Lakini kwa jamii zetu, huonekana ni heshima kwa ndoa kwanza kisha watoto. Kwa dini, huonekana ni sheria, ndoa kwanza.
Kwa Wakristo, ndoa inapewa msisitizo. Kwa maneno ya Biblia, ukisoma Mwanzo 2:24
"Kwa hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja."
Kwa tafsiri hiyo, hawa wawili kuwa mwili mmoja ni ndoa.
Lakini maagizo ya awali kwa mwanaume na mwanamke ni, "Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi."
Mwanzo 1:28
Ni hayo tu.
Nitanukuu "Nilisimama pale nje kwa nukta kadhaa nikiwa nimeduwaa, nilikuwa siamini kile kilichotokea, ama kweli fanya wema wende zako usingoje shukurani walisema waswahili, nilikaa na binti huyu kwa upendo. Miezi yote sita niliyokaa naye hakuwa akipokea mshahara kutokana na kuwa nje ya bajeti ya mshahara, nilimsaidia kwa kila kitu na hata alipopata malimbikizo ya mshahara alitaka kunirudishia kiasi cha fedha nilizokuwa nikimpa lakini nilikataa na ndipo akamudu kutafuta chumba na kuhama, sasa leo nakuja kumuomba anikopeshe pesa kidogo ananijibu kama anamjibu mtu asiyemfahamu!" mwisho wa kunuuu. Kwa kweli inasikitisha sana kama walivyosema wahenga wetu kikulacho ki nguoni mwako. Kwa kweli alivyotendewa huyo dada ni kitendo cha kusikitiasha sana. Lakini natumani Mwenyezi Mungu atamsaidia na atapata mchumba mwema na wale wawili maisha yao sijui kama yatakuwa ya furaha.Kwani wote wamemzurumu mtu waliyempenda na aliyewaamini. Kila la kheri.
Tupo pamoja ndugu yangu..kazi nzuri sana
Post a Comment