Niliwahi kuandika makala nikizungumzia kuhusu kuzishitukia dini lakini nikapata changamoto kutoka kwa wazazi wangu.
Ilibidi nifunge mjadala ili nijipange upya kwani niligundua kwamba ile mada sikuiandika katika wakati muafaka.
Siku hizi kila kona ya hapa nchini kuna sauti nyingi zenye kumtaja Yesu, si kwa nia ya kumtukuza bali kwa kumkashifu na kumbeza.
Dini siku hizi zinatumika kama kitega uchumi, kama mwamvuli wa uovu, kama kimbilio la walioshindwa kujisaidia na kama kimbilio la waovu ambao wanataka kuonekana kama kondoo kwa ngozi wakati ni chui.
Imani ni nguvu na imani ni ukombozi, lakini ni utumwa na adhabu pia. Kila mtu mwenye imani kubwa juu ya kitu fulani ni lazima maisha yake kwa kiasi kikubwa yatafungwa na imani hiyo. Imani zetu ndizo zinazotufanya au kutuwezesha kuona kile tunachotaka maishani kinatutokea.
Imani zetu ndizo zinazotufanya kusali, kuomba kunyenyekea, kwa jina la mungu au chochote ambacho tunaamini kwamba ndicho kikubwa zaidi na kinachoratibu na kushikilia sehemu ya maisha ambayo sisi hatuna uwezo wa kuyadhibiti au kuyaratibu.
Kwa sababu hiyo kuna wenzetu ambao wamegeuza nguvu hiyo kuwa kifaa cha kujinufaisha wakati sisi tukiumia. Ni wengi hivi sasa ambao ni watumwa halisi wa hawa wachungaji na manabii. Kuna wachungaji na manabii wa uongo ambao hutumia nguvu za giza kufanikisha malengo yao.
Hali mbaya ya uchumi imewafanya wananchi walio wengi kugeukia dini kama suluhisho.
Kuna idadi kubwa kuliko wewe unavyojua ambayo huamini kwamba wanaweza kuondoa matatizo yao kupitia wachungaji.
Wanaamini pia kwamba matatizo yanayowakabili ni matokeo ya wachawi, mapepo au laana fulani.
Katika hali kama hiyo hawa wachungaji huwanasa kirahisi watu wenye imani za kishirikina kwanza halafu huwanasa wale wasiojua kwamba nao ni binadamu kama hao wachungaji. Hii ikiwa na maana kwamba nao wanaweza kujiombea na kujitafutia nafuu kwenye maisha.
Mawindo rahisi ya wachungaji na manabii matapeli ni wale watu wenye hofu, wasiojiamini, walio katika matatizo ambayo wameshindwa kuyapatia ufumbuzi, na wale ambao wanakabiliwa na hitilafu za kiakili, kama vile sononi, msongo, na fadhaa.
Kwa kuwa na hofu na shida zao wanakosa uwezo wa kujiuliza maswali na hivyo hutumika kama vitendea kazi vya wachungaji na manabii hawa ambao kati yao kuna wanotumia nguvu za giza kuwahujuma.
Mimi nimekulia katika dini ya Kikristo tena nilikuwa nasali katika dhehebu la wasabato, lakini siku hizi naomba nikiri wazi kwamba siendi tena kanisani.
Kwa nini?
Kwa sababu naamini kwamba naweza kuwa na imani yangu binafsi bila kuwa na dini na nikafika huko wanakopaita mbinguni.
Swala la msingi hapa ni uhusiano wangu na Mungu, je ni imara kiasi gani?
Kama uhusiano wangu na mungu ni imara, kwa maana ya kwamba namuamini na ninafanya yale yaliyo mema na sio lazima yawe ni yale yaliyoandikwa katika vitabu vya dini, basi hata dini haina maana kwangu.
Nasema haina maana kwangu kwa sababu siamini kwamba binadamu mwenzangu anaweza kuwa na uwezo wa kimungu na anaweza kubadili maisha yangu.
Huwezi kuamini, kuna watu hawajiamini kabisa na wamekuwa dhalili kwa hawa wachungaji kiasi kwamba wanaamini kuwa hawawezi kubadili maisha yao wenyewe isipokuwa hawa wachungaji.
Kumbuka kwamba sisi tumeumbwa na mwenye enzi mungu kwa mfano wake, sio kwa sura bali kwa uwezo wake, kama yeye aliumba basi na sisi tunaweza kuumba, ni kiasi cha kutumia akili tu katika kufikiri kwatu. Kama ukiiweka rehani akili yako kwa mchungaji utaumba nini?
Kwa hiyo kama bado unategemea mchungaji akuamulie kuhusu maisha yako, basi ujue kwamba unayo matatizo makubwa ya kiakili na labda unahitajika upelekwe Mirembe kwenye hospitali ya wendawazimu.
Kama unawashangaa na kuwacheka wale wanaoamini waganga na uchawi basi ujue kwamba huna tofauti nao, kwa hiyo huna sababu ya kuwacheka.
Siku hizi kuna wachungaji hewa wanoibuka kila uchao na mazingaombwe yao, mtu anajifunza viini macho na uchawi halafu anaingia nao katika nyumba ya ibada na kuuonesha halafu anaita ni muujiza wa mwenye enzi mungu! Ama kweli wajinga ndio waliwao.
Kuibuka na kuongezeka kwa wachungaji hawa matapeli, inaonesha ni kwa kiasi gani watu wasiotaka kutumia akili zao wanavyoongezeka hapa duniani.
Ukweli ambao haukanushiki ni kwamba miujiza mingi inayofanywa na hawa wanojiita wachungaji au manabii iwe ni kwenye nyumba za ibada au hata huko mitaani ni miongoni mwa nguvu ambazo binadamu anazo au amejifunza na kufuzu kuwa nazo.
Wanaodanganywa na miujiza hii ni wale ambao bado wako kwenye giza la ujinga.
Hivi kweli tunahitaji miujiza ili tuweze kuomba na kusikilizwa na mungu?
Binafsi sidhani kama tunahitaji hiyo miujiza ili maombi yetu yasikilizwe na mungu, kwani miujiza haina maana yoyote kwa mungu.
Kama swala ni miujiza mbona hata shetani alifanya na anendelea kufanya miujiza.
Kwangu mimi miujiza ni mbinu inayotumiwa na watu hawa ili kunasa akili zetu, ili tuwaamini na tusionae uovu wao.
Kuongezeka kwa umasikini, kukata tamaa, watu kutojua malengo yao katika maisha, migogoro ya ndoa na familia, na kadhalika, ndio chimbuko la kuongezeka kwa wachungaji hawa na manabii matapeli, kwani hayo ndiyo mawindo rahisi kwao.
Binafsi naamini kwamba mchungaji, kiongozi wa dini au nabii ni yule anayemsaidia muumini au mwanaadamu kujua malengo yake ya kuwepo hapa duniani, kumsaidia muumini kuondoka katika hofu, na kuwaonesha namna bora ya kutenda mambo mema katika maisha, na hawawafungi na kuwafanya waone kwamba bila wao, yaani wachungaji, basi maisha yao hapa duniani hayana maana.
Kwa bahati mbaya viongozi wa dini wa aina hii ni adimu sana kupatikana.
Wachungaji na viongozi wa dini hatari wa kuogopwa ni wale ambao wanatumia nguvu ambazo sio za mungu bali za giza,
Kundi hili ni kubwa na linatawala katika nyumba za ibada, na linazaa viongozi na waumini kwa kasi ya ajabu.
Utakuta nyumba ya ibada inaanzishwa leo kesho imefurika waumini wengi mpaka unajiuliza watu hawa wamelishwa nini?
Na cha kushangaza miongoni mwa waumini hao, wapo wanaopoteza kazi, wanaopoteza ndoa zao, na wanaopoteza uwezo wa kufikiri na hatimaye wanakuwa mandondocha wasio na akili
Kumbuka kwamba wewe unaweza kusali na mungu akakusikia, unachotakiwa kufanya ni kuomba mungu na kuamini kwamba yupo na maombi yako yatakubaliwa, huhitaji kiongozi wa dini akusemee au akuombee kwa mungu kwani yeye ni binaadamu tu kama ulivyo wewe.
Saturday, January 10, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
7 comments:
Dah! Japo nina ka-upeo fulani hivi kuhusu masuala ya imani, bado natambua kuwa si mjuzi saana na wala si mchambuzi mzuri hasa wa Imani za watu. Najua kuwa naamini na nadhani naweza kuizungumza na kuifuata vema imani yangu ila ntakaa pembeni kidogo ili wenye utambuzi wa maana waingie zaidi. Lakini kuhusu "mradi-dini" hilo halina ubishi. Kuhusu kuwa na wachungaji wasio na wito naamini linaonekana. Nilishawahi kuhudhuria kanisa ambalo tuliambiwa "sasa naanza kuombea wale wenye shukrani ya dola 50, kisha ntaongeza maombi kwa wenye 100 na ntakuwa naongeza maombi kwa alie na kiasi zaidi ya hapo". Hiyo ilinichosha. Lakini pia Mchungaji (ama Askofu kama alivyoamua kujiita siku za mwisho za uwepo wangu pale) alisimulia mambo mengi kuhusu uponyaji na kuwaombea watu mpaka waanguke (ambavyo wengine ndio huona kama kigezo cha upako) na alisema kuna kipindi walilazimika kulazimisha mambo kama kusukuma mtu aanguke ama ujinga mwingine katika maombi anayosema alikaribishwa kusaidia na kwa wakati huo hakuwa na karama kamili ya uponyaji.
Pia ni kweli kuwa tumeona watu wakiambia watoe VITO vyote walivyonavyo na kuviacha kanisani kwani si vya thamani na ni ushetani japo sielewi kwanini waambiwe waache Dhabau na Almasi zao kanisani na si kuvitupa kwenye dampo kama havina thamani. Ama wale ambao waliambiwa "wawekeze" dola 1000 kisha wataona malipo yake katika mwaka huohuo. Yaani unahimizwa hata ukakope ili uwekeze na watu wanafanya hivyo kwa spidi ya ajabu. Lakini yote ni IMANI ambayo kwa tafsiri ni KUWA NA HAKIKA NA MAMBO YATARAJIWAYO. NI BAYANA YA MAMBO YASIYOONEKANA) kwa hiyo ni suala la kuamini kijacho na ambacho hakionekani wala kuhakikisha mafanikio sasa na ndio maana nasema kwa kuwa ni IMANI, basi kwa tafsiri ya Imani mtenda na mtendewa wako sahihi maana wanabayanisha yasiyoonekana. Ila Nia ya kufanya hivyo ndio iletayo shida. Binafsi niko kama nilivyo na nakumbuka Ziggy Marley alisema LOVE IS MY RELIGION.
Nimesema si mjuzi wa masuala ya Imani za watu. Nimesema nionacho na nijuacho na naamini kuna wenye uchambuzi wa maana na ziada ambao watafanya hivyo.
Blessings
Koero: hii makala inatakiwa isomwe nchi nzima kwa niia nyinge ikiwemo gazeti, sina hakika kama utaafiki hilo lakini unao uwezo mkubwa wa kuandika makala. lakini najua wengin tumeacha kusoma magazeti sababu ya blogu maana zinatulisha kilichobora daiama.
Koero: usiponiruhusu basi tumia mwenyewe hakika ni CHANGAMOTO nzuri hiyo
Hii ni habari kubwa.
Jana nilipopitia blog ya kaka Bwaya nilikutanana na maoni yako ukitoa taarifa kwamba leo ungejilipua.
Nilikuwa nangojea kwa hamu nione huo mlipuko, na kweli nimeuona.
dada Koero mimi naogopa kusema mengi lakini msikilize kaka Mpangala katoa ombi maalum.
maana hii habari inapaswa isomwe na watanzania wote ili wafumbuke macho.
Naomba nami niseme...
Kuna wakati nikiyatazama mambo yanavyokwenda huwa nachoka. Kijijini kwetu kuna bwana alianzisha kanisa. Akasema matajiri hawatauona ufalme wa Mungu. Akahubiri kwa karama (ndivyo tunavyoita?) kubwa. Watu wakamwelewa. Wakapeleka utajiri wao kanisani. Leo niandikapo jamvini humu, askofu huyo (maana wakianzisha makanisa wao huwa maaskofu, sijui wito wao na elimu yao ya uaskofu) ni milionea. Anaishi maisha ya kifahari. Anamiliki magari ya kubeba abiria. Anamiliki NGO pia. Hali ya waumini wake, najisikia huruma.
Mfano mwingine, niacheni niseme leo. Mkoani Mbeya, nadhani ndiko kwaongoza kwa makanisa nchimu humu. Nani anabisha? Basi, mjini Tunduma kuna makanisa chungu mbovu. Viongozi wa makanisa wakizinguana kidogo basi wanajitenga na kanisa jipya linazaliwa. Makanisa ni mali binafsi za wao. Wao ndo wasemaji wa mwisho.
Ntasahau jambo hasa nnalotaka kutoa mfano. Mwaka 2006 katika kanisa moja huko mkoani Mbeya, mmiliki wa kanisa aka askofu mkuu aka mtumishi mbarikiwa wa Mungu aka mteule (ndivyo hujiita) alizawadiwa gari na waumini wake. Gari lilikuwa ni Escudo. Mteule alipopewa gari hiyo aligeuka mbogo. Akawaka akisema hawezi pewa gari la bei ndogo ambalo hata masikini anaweza kumiliki. Akadai haiwezekani waumini watembelee magari ya kifahari ilhali yeye anatembelea gari la kilofa.
Hivi ndivyo tunavyoyaona makanisa mamboleo. Ndivyo yanavyojionesha kwetu. Nadhani tumepata ajali kiimani. Sifahamu ni wapi, lakini kuna mushkeri. Achilia mbali matendo ya wateule hao kutoshabihiana na nafasi zao.
Kuna wakati huwa nawatafakari sana wakomunisti. Nadhani wanayo lojiki.
Ni hayo tu!
Karibu Kaka Mtanga. Naona umerejea kwa kishindo kikuu. Asante kwa yote
MADA hii kwa kweli ina changanya ila kwa upande wangu nitachangia kama mimi na imani yangu ya kwamba kweli wapo watu wanaotumia dini ili kujikomboa na umasikini lakini watu hawa ole wao ile siku ikifika pale tukapomuona mwana adamu anakuja hakika siku hiyo itakuwa chungu na maomborezo makali.
Ila kama mtu anafanya kazi ya Mungu kama inavyotakiwa huyu naye mungu ndiye ajuaye yote haya lakini imeandikwa ole wake ahukumaye kwa upanga naye atahukumiwa kwa upanga pia yatupasa kuangalia sana maadiko matakatifu.
Na inasemekana kuwa kila mtu anaishi kwa imani kama haamini Mungu basi anaamini kitu kingine kama pesa, mti, ng'ombe dume, mbuzi, makaburi nk.
Hakuna binadamu ambaye hana imani kwani tunaishi kwa kutegemea kitu tunachokiamini.Nina mengi ya kusema lakini naona nikomee hapo.
Mada nzuri nimeifurahi kwa sababu imetufahamisha ya kwamba katika dunia hii kuna watu ambao wanatumia kivuli cha dini kujinufaisha.
toka lini dini zikawa na lengo tofauti na biashara na kutawala watu kiroho? nani kakwambia ukristo wa leo una maana halisi ya ukristo? nani kwa kwambia upuuzi mnaoufanya makanisani kwenu una harufu ya ukristo?
acheni ujinga, tafuteni ukweli na kweli imo ndani mwenu sio kanisania na nyie ndio kweli yenyewe. mwapotola mkiitegemea kutoka kwa matapeli wa kiroho na kimwili
Post a Comment