Sunday, January 25, 2009
NILISHINDWA KUMSAIDIA ZINDUNA!
Rafiki na ndugu yangu mpendwa.
Nilikuja nyumbani kwenu kama tulivyoahidiana ili nipate kukuaga lakini kwa bahati mbaya nimekukosa, nilikuja kukuaga kwa kuwa hutaniona tena kwani nasafiri safari ya mbali sana. Baada ya kusubiri sana nimeamua kurejea nyumbani na ilikufanikisha safari yangu, wakati nakuja kwenu nilipitia maduka kadhaa ya dawa na kununua vidonge vya klorokwini vipatavyo 40, naamini vidonge hivyo vitafanikisha safari yangu kwa amani, ili nipate kupumzika.
Naogopa na nahitaji mtu wa kuzungumza nae lakini simuoni, kwani nipo katika ulimwengu wa peke yangu na mbele yangu kuna giza nene, sijui msaada wangu utatoka wapi?Dada yangu mpendwa, wewe ndio rafiki yangu uliyekuwa karibu na mimi wakati wote, ukinipa moyo wa kuzikabili changamoto za maisha, lakini sasa naona imefikia tamati, sina budi kurejea kwa mola wangu.Najua ni dhambi kwa mwanaadamu kukatisha uhai wake kikatili namna hii, kama ulivyowahi kuniambia na kunisomea maandiko matakatifu katika biblia lakini kwa swala langu naamini hii ndio njia muafaka, naomba mungu anisamehe.
Naomba unisamehe kwa kukusababishia maumivu moyoni kwa kuondoka kwangu ghafla katika uso wa hii dunia, lakini sababu kubwa iliyosababisha hili litokee nadhani unaifahamu.Nasema unaifahamu kwa sababu umekuwa karibu na mimi kwa muda mrefu tangu tulipokutana sekondari tukiwa kidato cha kwanza mpaka tulipomaliza kidato cha nne.
Ulikuwa ni zaidi ya rafiki na ulitumia muda wako mwingi ukinifaariji na kunipa moyo hasa baada ya lile jaribio la kutaka kujiuwa la mwaka 2003 wakati tukiwa kidato cha tatu kushindikana.Ingawa naogopa lakini, nadhani hii ndio njia sahihi zaidi ili kuepuka haya maisha ninayoishi, maisha ya upweke yasiyo na hata chembe ya upendo, na hakuna hata mmoja zaidi yako wewe aliyejua upweke niliokuwa nao, hakuna hata mmoja miongoni mwa ndugu zangu aliyekuwa karibu yangu pale nilipohitaji masaada zaidi yako wewe, hakuna aliyewahi kunifuta machozi pale nilipokuwa nikilia kwa uchungu nikihitaji msaada zaidi yako wewe na kibaya zaidi hakuna hata aliyewahi kusikia kilio changu zaidi yako wewe.
Kwa muda mrefu nimekuwa nikipiga makelele ya kuomba msaada lakini sauti yangu imekuwa ikiishia mwituni, hakuna anayejali, na sasa nimeamua, ngoja niondoke labda watafurahi,maana wataishi kwa amani.Naamini hata kushindwa kwangu kuendelea na kidato cha tano ilichangiwa zaidi na matatizo ya kifamilia niliyokuwa nayo ambayo unayafahamu.
Dada yangu na rafiki yangu mpendwa tangu tulipoachana, mara baada ya kumaliza kidato cha nne na wewe kupangiwa kuendelea na kidato cha tano mkoani Morogoro, uliniacha na upweke mkubwa nisijue pa kukimbilia ili kupata faraja, kwani mateso yalizidi mno hapa nyumbani nilishindwa kujua mustakabali wa maisha yangu ya baadae na hakuna aliyeonesha kujali.
Nakushukuru sana kwa misaada uliyonipa wewe binafsi na ile niliyowahi kupewa na wazazi wako, naomba ufikishe shukrani zangu kwao, na waambie kwamba nawapenda sana.Naomba usinililie, na amini kuwa naondoka hapa duniani nikiwa nakupenda sana, na kwangu mimi utaendelea kubaki ndugu na rafiki yangu mpendwa.Nakutakia maisha mema hapa duniani na baki salama.
Ni mimi rafiki yako, ndugu yako na mdogo wako
Zinduna.(Sio jina lake halisi)
Jana tarehe 24/01/2009, imetimia miaka mitatu tangu rafiki yangu huyu roho yake iachane na mwili, baada ya kuamau kukatisha maisha yake. Alikuwa bado ni binti mbichi ambapo ndio kwanza alikuwa ametimiza miaka 20, lakini kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa mama yake wa kambo akishirikiana na baba yake mzazi aliamua kukatisha maisha yake.
Kwangu mimi huu ulikuwa ni msiba mkubwa kwani alikuwa ni zaidi ya rafiki.
Nakumbuka ndio nilikuwa nimerudi Dar es salaam, nikitokea Morogoro kuja kufanikisha mipango ya kuhamia katika shule moja ya binafsi iliyoko hapa jijini Dar es salaam.Siku mbili kabla ya rafiki yangu huyu kuutoa uhai wake, kama bahati nilikutana nae Kariakoo, lakini akiwa anaonekana kuwa mnyonge na asiye na furaha, alikuwa amefuatana na binti mmoja ambaye alinitambulisha kuwa ni mdogo wake.
Alinivuta pembeni na kuniambia kuwa ni bora tumeonana kwani anayo mazungumzo marefu na mimi hivyo alitaka kujua ratiba yangu ili aje nyumbani tuongee.Nilimwalika aje nyumbani siku mbili baadae yaani Jumanne ya tarehe 24/01/2006, ambayo ndio nitakuwa na nafasi ili tuongee, lakini kwa bahati mbaya siku hiyo nilikwenda Morogoro kupeleka fomu fulani kule shuleni nilikokuwa nasoma na ilikuwa nirudi siku hiyo hiyo.
Hivyo ilipofika siku hiyo kabla sijaondoka kuelekea Ubungo kupanda basi kuelekea Morogoro niliacha maagizo kwa mama kuwa rafiki yangu huyo akija anisubiri.Ni kweli alifika pale nyumbani majira ya saa nne asubuni hivi na baada ya kuambiwa nimeenda Morogoro, alikosa raha, hata hivyo mama alimshauri anisubiri kwa kuwa nitarudi siku hiyo hiyo. Kwa mujibu wa maelezo ya mama yangu, alikuwa akiuliza mara kwa mara kama nitarudi saa ngapi, mpaka mama yangu akawa na wasiwasi, ikabidi amuulize kama ana shida kubwa na mimi, ndipo akamjibu mama yangu kuwa amekuja kuaga kwani anasafiri kwa hivyo ameona ni vyema aje kuniaga mimi rafiki yake.
Mama yangu akamthibitishia kwamba ningerudi mapema,siku hiyo hiyo.Mpaka kufikia saa nane mchana nilikuwa bado sijarudi, akaomba apewe karatasi na kalamu ili aniachie ujumbe. Alipoletewa ndipo akaniachia huo ujumbe niliouandika hapo juu.Nakumbuka nilirudi Dar es salaam majira ya saa kumi na mbili jioni kwani siki hiyo usafiri wa kutoka huko Shuleni nilikokuwa nikisoma mpaka Morogoro mjini ulikuwa ni mgumu kidogo.
Nilipofika nyumbani mama alinipa ile barua aliyoacha rafiki yangu, na nilipoifungua na kuisoma sikuamini kile kilichoandikwa katika ile barua, nilishitukia napiga yowe kubwa, hadi mama akashituka.Niliongozana na mama hadi Temeke Mikoroshini alipokuwa akiishi huyo rafiki yangu, tulifika pale majira ya saa mbili usiku, na tulikuta umati mkubwa wa watu. Ni kweli rafiki yangu amekufa! Nilishikwa na butwaa.
Basi hivyo ndivyo alivyojitoa uhai rafiki yangu huyo. Msiba huo ulibaki kuwa kumbukumbu katika maisha yangu, kwa binti mdogo kiasi kile kujitoa uhai mapema namna ile.Kwa kifupi,nilifahamiana na Zinduna nilipojiunga na kidato cha kwanza, baada ya kufaulu darasa la saba.Tulitokea kuwa marafiki na nilimpeleka nyumbani na kumtambulisha kwa wazazi wangu, na kutokana nna kuniamini ndipo akanisimulia madhila aliyokuwa nayo.
Mama yake alifariki akiwa na umri wa miaka mitano na inasemekana mama yake alifariki kutokan na Depression (Naomba wataalamu munisaidia kutafsiri neno hili kwa Kiswahili) baada kuwa ameteswa sana na mumewe yaani baba yake.
Mara baada ya mama yake kufariki, baba yake akaoa mke mwingine ambaye inasemekana kuwa ndiye aliyekuwa akimzuzua baba mpaka kufikia kumtesa mama yake. Huyo mama yake wa kambo alikuwa akimtesa sana kwani aligeuzwa kuwa mtumishi wa ndani pale nyumbani kwao na baba yake hakuonekana kujali sana kwani kwa kushirikiana na baba yake walikuwa wakimtesa na kumsimanga kuwa atakuwa Malaya kama mama yake, kitu ambacho si kweli, kwani hakuwahi kuwa na uhusiano na wanaume kama walivyokuwa wakimtuhumu.
Pamoja na mateso yote hayo lakini alijibidisha na masomo hadi akafaulu na kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule ya serikali, kitu ambacho hakikumfurahisha mama yake wa kambo.Kuanzia hapo mateso yalizidi na baba yake kama kawaida hakuonekana kujali.
Nakumbuka nilimsaidia sana katika kumfariji na kumpa moyo na hata pale baba yake alipokataa kumpa pesa za matumizi ya shule na mahitaji mengine, mama yangu alimpatia, hiyo ni baada ya kuwa nimemsimulia mama yangu juu ya mateso anayopata rafiki yangu huyo.
Hata nilipokuwa nikienda kwao kumtembelea mama yake hakuonekana kufurahia na muda mwingi alionekana kufoka foka bila sababu ya msingi.Kuna wakati mama yangu alimshauri ahamie kwetu ili kuepukajna na mateso yale lakini alikataa kata kata kwa madai kuwa baba yake atamuua.Habari za huyu binti ni ndefu sana na nikisema nisimulie nadhani nitawachosha.Hata hivyo bado ninayo maswali mengi sana juu ya lile tukio.
Hivi kama ningewahi kurudi si labda ningeweza kuokoa maisha ya rafiki yangu huyu?
Au kuchelewa kwangu kulikuwa ni kusudi maalum ili hilo tukio la rafiki yangu kujiua litokee?
Apumzike kwa amani na mwanga wa milele umwangazie.....................Aaaamen.
Habari hii itaendelea wiki ijayo......
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
7 comments:
Inasikitisha sana!:-(R.I.P mpendwa!
Sina hakika na nini kingetokea kama ungewahi kurejea nyumbani. Sina hakika kama kungempa nafasi ya pili kuendelea kuishi ama kungeishia kumumiza zaidi. Labda angeishi lakini akiwa na mawazo na akaishia kugongwa na magari barabarani kwa kutembea bila kufikiria kutokana na msongo wa mawazo. Ama ungeweza kumshawishi ahamie kwenu na kisha wazazi wake wakawapangia "dili" la kuwafanyizia na matokeo yake nyote mkawa wahanga. Ama angebadilika tu na kuwa binti mwema na kuanza kuishi maisha mema na kuwa msaada kwa jamii. Kaka Kitururu aliwahi kusema kuwa siri ya maisha wanaijua waliokufa na hawatarejea hivyo hakuna namna ya kuijua tukiwa hai.
Lakini msongo wa mawazo (depression) ni kitu cha hatari sana na kama usingefanikiwa kukitoa kingemuua kwa namna moja ama nyingine. Iwe kwa pressure, stroke ama maradhi mengine mengi yaendanayo na huo ugonjwa.
Nimesikitishwa saana na kisa hiki na naamini wazazi wanastahili kubeba lawama, laana na mzigo wooote wa kilichotokea.
Pole kwako na kwake pia.
Blessings
Dada Koero kisa hiki kinasikitisha sana!
Pengine asingekuwa karibu na wewe toka awali kuna uwezekano mkubwa maisha yake yangalikwisha potea mda mrefu sana hata kabla hamjakutana.
Kuna watu wengi walio ktk hali hizi za kunyanyaswa na hatimaye kuwa na misongo ya mawazo ya aina hii. Mwenye tatizo kukubaliana na hali na kuiona ni ya kawaida,ni vigumu sana. Msaada wa kifikra,vitu na hata wa kisheria inapobidi lazima tuvitoe pale tunapokutana na watu wenye matatizo kama haya na tusiishie kuona ni hali za kawaida.Nasema hivi kwani kuna wengine hukutana na hali hizi na kuzidharau bila kufikiri matokeo yake.
Shukrani za pekee kwa Dada Koero na familia yake.Kwa kweli mlionyesha moyo wa upendo.Mungu awazidishie.Ninyi ni mfano mzuri wa kuigwa.
kuna misongo mingi inayosababishwa na sayansi na teknolojia. mwaweza kuwalalamikia wazaziwake lakini sio wao na labda tatitizo ni binti mwenyewe japo kufa sio tatizo, sio mkosi na wala sio jambo la ajabu. kufa nikuuacha mwili, kuvua mwili hna kuendelea na maisha mengine bila mwili au kuvaa mwili mwingine na kuishi vinginevyo mapaka lengo lako la kuubwa likamililike.
hata wewe ukijisikia kuchoshwa na mwili, waweza uvua na kutimka. wengi hujiuwa bila sisi na hata wao kujua kwa sababu sisi tunasubili wanywe sumu wajitwange risasi ya kichwa nk. kukna njia nyingi sana za kufa na kujiuwa. lakini mimi naona kama alifanya busara kwani kama kukaa ndani ya mwili (kuishi) aliona ni tatizo kwa nini asiuvue mwili (kufa) unaomletea matatizo? hata wewe usione soo, usinganganie maisha kama yamekuchosha au umeridhika na maisha haya! MWAWEZA MSINIELEWE EHE!!
nasema kuna kitu kingekuwepo na kingetokea iwapo Koero ungekuwepo. Lakini hakikutokea kwasababu hukuwepo ndiyo maana mzee wa changamoto kasema, sijui ingekuwaje ungekuwepo.
Mungu awe naye Daima! Umenikumbusha kisa rafiki yangu Alfred Liponda alikuwa akiishi na mama mmoja wa Malawi aliyeolewa TZ, yule mamingawa hakumzaa alfred alimpenda sana tena sana, ajabu baba yake mdogo alfred hakumpenda mtoto wa kaka yake. Duh! msongo wa mawazo, siku moja ghafla akasema kichwa kinamuuma, tena tukiwa shule, siku ya pili alituacha akaaga dunia. Nilikuwa nalala naye kitanda kimoja tukiwa hosteli za shule. Inanikumbusha mbali Koero.
Kifo sio kibaya, lakini kwa mazingira ya kifo cha huyo binti, kwa kweli inasikitisha sana.
Nawashukuruni sana wote mliotoa maoni yenu na kwakunipa pole.
habari hii itaendelea wiki ijayo nitakapozungumzia sababu za vijana wngi kujinyonga wakiwa na umri mdogo kwa undani zaidi.
Hata hivyo nakaribisha maoni zaidi.
ahsanteni kwa kunitembelea.
Kamala: Kaaazi kweli kweli!!!!!!!
Post a Comment