Neno VUKANI nimelitohowa kutoka katika lugha ya mama yangu ya kipare.
Neno hili lina maana ya AMKENI, nadhani kaka Mkodo Kitururu atakuwa anafahamu vizuri kwa kuwa ni lugha yake.
Nakumbuka wakati fulani nilikwenda likizo kijijini huko upareni kuwasalimia bibi na babu yangu wanaomzaa mama yangu, basi kila siku asubuhi bibi alikuwa na kawaida ya kutuamsha ili tusali pamoja na alikuwa akitumia neno Vukani.
Nilipouliza maana yake nikaambiwa ni Amkeni au kwa msisitizo wa kiingereza WAKE UP.
Basi kuanzia siku hiyo nikatokea kulipenda sana hili neno, sijui ni kwa nini lakini lilikuwa linanihamasisha sana kuamka kifikra badala ya kuamka asubuhi tu.
Wakati nilipokuwa nafungua Blog yangu nilikuwa tayari nimeshachagua jina hili, na cha kushangaza nilipoliingiza kwenye mtandao nikagundua kwamba neno hili linatumiwa na makabila mawili ya Ki Zulu na Ki-Xhosa ya nchini Afrika ya Kusini, likiwa na maana moja, yaani Amkeni.
Si hivyo tu bali pia lipo gazeti moja maarufu nchini humo, linaloitwa Vukani.
Kwa maelezo zaidi bofya hapa.
Amkeni nionavyo mimi sio kuamka kutoka usingizini tu bali ni kuamka kifikra na kuhoji kila tulichofundishwa au kuambiwa kama kina ukweli kiasi gani?
Si hivyo tu bali pia ni kuamka na kuachana na ile tabia ya kufikiri kwa mazoea na kutenda kwa mazoea.
Kila jambo unalolifanya ujue sababu ya kufanya hivyo, sio eti kwa sababu, mama, baba, bibi, babu, mjomba, shangazi, na jamii iliwahi kufanya hivyo.
Nakumbuka wakati fulani nilihudhuria semina ya mambo ya uongozi, basi yule mwezeshaji kutoka nchini Marekani alitutolea mfano mmoja wakati alipokuwa akitufundisha namna ya kuepuka kufanya mambo kwa mazoea.
Kisa chenyewe ni hiki:
Kulikuwa na mama mmoja alikuwa na tabia, kila akitaka kuoka samaki ni lazima amkate mkia kabla ya kumuweka kwenye kikaango, ndio amuweke kwenye oven. Hata kama samaki mwenyewe ni mdogo.
Siku moja binti yake aliyekuwa na umri wa miaka 10 akamuuliza mama yake sababu ya kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka, mama yake akamjibu kuwa mama yake alikuwa na kawaida ya kufanya hivyo.
Alipomuuliza kama aliwahi kumuuliza mama yake sababu ya kufanya hivyo, mama yake akajibu kwamba hakuwahi kuuliza.
Basi wakati fulani bibi yake alipokwenda kuwatembelea, kama bahati mama yake alikuwa akiandaa samaki ili amuoke kama ilivyo kawaida akamkata mkia,
binti akaona huo ndio wakti muafaka wa kuujua ukweli maada bibi yupo. Ndipo akamuuliza sababu ya mama yake kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka.
Si mnaona watoto wa wenzetu walivyo wadadisi?
Bibi akamwambia akamuulize mama yake sababu ya kufanya hivyo, yule binti akamjibu bibi yake kwamba, mama yake alimwambia kuwa yeye yaani bibi, ndiye aliyemfundisha kukata mkia wa samakai kabla ya kumuoka.
Yule bibi akafikiria kidogo, kisha akamjibu, kwamba alikuwa akikata mkia wa samaki kwa sababu kikaango chake kilikuwa ni kidogo, hivyo ili samaki aweze kuenea kwenye kikaango alikuwa analazimika kukata mkia.
Yule binti akamwambia bibi yake, “Mbona sisi kikaango chetu ni kikubwa na isitoshe tunavyo vikaango vingi tu vya saizi tofauti tofauti, je kuna ulazima gani mama aendelee kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka?
Bibi akamjibu kwamba hakuna ulazima wowote.
Basi kuanzia siku hiyo yule mama akawa hakati tena mkia wa samaki.
Si mnaona jinsi mtoto huyu alivyokataa kulishwa kitu bila ya kijua sababu?
Naamini kwamba wote mtakubaliana na mimi kwamba sisi tumelelewa hivi, tunaambiwa tukate mikia ya samaki kabla ya kuwaoka na tunafuata, na wala hatuulizi sababu.
Kwa hiyo ninaposema VUKANI ninamaanisha AMKENI, ili muweze kuhoji baadhi ya mambo tunayofundishwa au kuambiwa ambayo hayana mantiki.
Wednesday, January 21, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
9 comments:
Pengine hukupata mail yangu lakini niliuliza. Niliuliza nilipokuwa naandaa salamu kwa wana-blog na nilitaka kujua maana halisi kabla sijaiweka mle. Nilipoona kimya nikajua yaweza kuwa "personal" lakini sikuacha kuwaza. Sasa siku moja wakati natwanga muziki kwenye ZUNE yangu nikawa namsikiliza Miriam Makeba nako nikakutana na wimbo VUKANI.
Kilichotokea hapo ni kuwa hata wimbo wenyewe sikuuelewa lakini nikabaki naendelea kuunganisha moja na moja kuona kama ntapata mbili.
Sasa nimeelewa.
Asante kwa kutu-vukani-sha
Kaka Bandio na wewe kwa kukesha mtandaoni!!
Yaani hata bado nilikuwa sijahariri makala yangu mara naona maoni yako.
Haya Nimerekebisha kidogo nilisahau kuweka hiyo linki ya VUKANI, unaweza kurejea tena na kusoma hiyo Link.
Pole na shughuli za kila siku.
VUKANI-AMKENI enyi mlioko kondeni, mdhaniao blogu ni upepo wa kupita. AMKENI eni watu mliofumbwa macho na kuona utupu wa mfalme wenu. ANGALIENI msije mkaleta najsi katika ufalme wake. AMKENI enyi mlioko mlimani mdhaniao kuwa kukariri nadharia ni sawa na kuishi kawaida, AMKENI mpokeao milingula na kudhani mwajinufaisha. AMKENI enyi mpokeao kanga na shati nyakati za kampeni, amkeni kwani mlichobakiwa ni kipande cha nchi amkeni jamani.
TANGAZO: ILE MAKALA YA 'DINI INAPOTUMIWA KAMA KITEGA UCHUMI IMETOKA JANA JUMANNE JANUARI 20/2009 itafute isome. AMKENI
vukani, amkeni, imukamu, mukamo, jangu, oimuke, nk
Markus, Imetoka katika gazeti gani?
Mbona watoa taarifa nusu nusu, au ni siri?
Hebu weka mambo hadharani kaka.....
Kamala, Jamani mimi Kihaya sikijui, hebu nijuze basi una maana gani?
Asante sana Dada nilikuwa sijajua kwamba wenzangu huku mmekaa kwa amani na kujifunza mammbo mazuri, nashukuru nimepita na nitakuwa napita kila mara.
Dada kazi nzuri sana endelea kutuelimisha.
Lazarus Mbilinyi
Ni habari njema,namshukuru aliyehoji kuhusu maana ya hili neno,dada Koero ulikuwa na lengo zuri sana toka awali la kutuelimisha kuhusu kuamka,hata kama tulishaamka kwa kiasi fulani,sijisifii kwamba nilikwisha amka,bali naamini hakuna mtu ambaye yuko empty kabisa! Kidogo ambacho ninaweza kumshirikisha mtu kwa maendeleo yake ni ishara wazi kwamba nimekwisha amka.
Hii ni changamoto ya kufahamu kwamba tunatakiwa kuamka mapema zaidi !
Aya sasa, kwa pamoja wote tuamke,tusiseme kiswahili hakitumiki,ni sisi wenyewe hatukitumii,tuamke jamani,msomi anayeongea kiswahili fasaha lakini kimombo kinampiga chenga,hudharaulika na kuonekana usomi wake hauna maana eti kisa tu hajui kiingereza. Ati msomi ni yule ambaye akiambiwa aonyeshe "jembe" ashindwe kulionyesha na abaki anababaika, akiambiwa aonyeshe "hoe" alionyeshe kwa haraka bila kubabaika.Hima hima jamani Vukani! Tuamke.
Ni hayo tu!
Falsafa nzuri. Asante kwa kutuhabarisha.
Post a Comment