Kuna watoto wengi sana wa kike chini ya umri wa miaka kumi na nane wanaofanyishwa kazi za nyumbani, ukilinganisha na maeneo mengine yanayotuhumiwa kwa kutumikishwa watoto.
Eneo hili la utumikishwaji wa kazi za majumbani, ndilo linaloongoza kwa unyanyasaji wa aina mbalimbali kwa watoto hawa, japokuwa ni vigumu kufahamika kwa sababu vitendo hivyo hufanyika ndani ya majumba na kwa usiri mkubwa ambao si rahisi watu wa nje kufahamu.
Watoto hawa watumikishwao kazi za ndani hujikuta wakiwa ndani ya unyanyaswaji wa kijinsia ambao unaweza kufanywa kwa lugha ya matusi, kupapaswa kimapenzi bila hiyari yao, kubakwa na mwanaume aliyemwajiri au ndugu waishio kwenye familia husika, na wakati mwingine hupigwa bila sababu ya msingi.
Mara nyingi watoto hawa hufichwa ndani ya nyumba zenye kuta ndefu na hawaruhusiwi kutoka nje, wala kuwa na uhusiano na watu wa nje, hivyo hata wanapofanyiwa vitendo vya unyanyaswaji, huogopa kutoa siri kwa kuhofia vipigo kutoka kwa waajiri wao au kupoteza ajira.
Kama ukibahatika kusikiliza habari za wasichana waliookolewa kutoka katika ajira hizi za utumikishwaji majumbani, zitakusikitisha sana.
Binafsi niliwahi kufanya kazi kwa muda katika NGO moja ambayo inajishughulisha na kutetea haki za wanawake na watoto.
Ingawa nilikaa pale kwa muda mfupi lakini nilishuhudia matukio mengi yanayohusu unyanyaswaji wa watumishi wa ndani.
Nadhani kukaa kwangu pale kulinifundisha jambo moja muhimu katika maisha, kwani nilishuhudia kesi nyingine zikiwahusu watu wazito wenye madaraka makubwa kisiasa ambao huku nje wanaonekana kama watu waungwana kupindukia, kumbe ndani ya majumba yao ni mafisi wasio na hata chembe ya huruma.
Pia nilikuja kugundua kwamba NGO nyingi zinazojishughulisha na kutetea haki za wanawake na watoto huwa zinapokea vitisho vingi kutoka kwa watu hawa ikitokea habari za unyanyasaji wanazowafanyia watumishi wao wa ndani zimefikishwa huko.
Hii imesababisha NGO nyingi kuogopa kushughulikia kesi za watu wazito kwa kuhofia kudhibitiwa au hata kufungwa, na ndio sababu kesi nyingi tunazoona zikishughulikiwa na NGO hizi ni za watu wasio na majina makubwa.
Nilibahatika kuzungumza na binti mmoja ambaye aliokolewa na msamria mwema na kuletwa pale kituoni nilipokuwa nikifanya kazi.
Alifukuzwa na mwajiri wake kutokana na kuwa alikuwa ni mjamzito.
Kwa mujibu wa maelezo yake, ujauzito ule aliupata pale pale kwa mwajiri wake, na ukweli ni kwamba hajui ni nani hasa aliyempa ule ujauzito kwa kuwa alikuwa akiingiliwa na baba na wanae.
Kila mmoja kwa wakati wake. Baba akirudi kutoka kazini na kumkuta peke yake alikuwa akimbaka, huku akimtisha kwamba akimwambia mtu atamuua. Na watoto wawili wa kiume wa yule mwajiri wake hivyo hivyo wakirudi kutoka shule, maana walikuwa wakisoma Boarding, walikuwa wana kawaida ya kumbaka usiku kila mmoja kwa wakati wake.
Baadae alianza kuumwa umwa na akawa anatapika mara kwa mara. Kuona hivyo mke wa yule mzee ambaye alikuwa ni mtumishi serikalini alimtilia mashaka hivyo akampeleka hospitalini kwa ajili ya vipimo.
Majibu yalipotoka aligundulika kwamba ni mjamzito.
Walipofika nyumbani aliamriwa afungashe kila kilicho chake na aondoke, kwa madai kwamba hawezi kukaa na malaya.
Aliposema kwamba hawezi kuondoka kwa sababu ule ujauzito ameupata pale pale nyumbani kwake na wahusika ni mumewe pamoja na watoto wake, kwa sababu ndio waliokuwa wakimbaka mara kwa mara wakati yeye akiwa hayupo, aliambulia kipigo kutoka kwa yule mama huku akishirikiana na wale wanae.
Baada ya kipigo alifukuzwa kwa kuondolewa kwa nguvu pale nyumbani, huku akiwa anadai mshahara wa miaka miwili. Hivyo aliondoka kama alivyokuja.
Baada ya kuhangaika mitaani ndipo alipopata mfadhili ambaye alimpa hifadhi na kumleta pale ili apate msaada wa kisheria.
Akieleza namna alivyokuja mjini, binti huyo alisema kwamba yuko mama mmoja alikuwa na kawaida ya kwenda kijijini kwao na kuchukuwa wasichana wadogo ambao walikuwa hawaendi shule kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwasomesha au kwa sababu nyingine.
Mama huyo huwahadaa wazazi wa wasichana husika kwamba anawapeleka mjini kuwatafutia kazi na pia huzipa familia hizo fedha kidogo ili kupata ridhaa za wazazi hao na kisha huja na wasichana hao huku mjini na kuwauza kwa watu wanaotafuta watumishi wa ndani, maarufu kama House Girl.
Kwa mujibu wa maelezo ya binti huyu, nilikuja kugundua kwamba wapo mawakala wengi wanaofanya kazi ya kuleta wasichana kutoka mikoani na kuwatafutia kazi za majumbani kwa makubaliano maalum.
Wakati mwingine mawakala hawa huwaachisha wasichana hawa shule kwa kuwadanganya kwamba watakuja kuwasomesha huku mjini kitu ambacho si kweli.
Ingawa tukio hili ni la siku nyingi, lakini nimelikumbuka, ndio nikaona niliweke humu ili wasomaji na wanablog wenzangu, muweze kuchangia na kutoa maoni yenu.
Lakini isije ikawa mada hii inawagusa baadhi yenu, maana naamini miongoni mwetu tunao watumishi majumbani, na huenda nao wanaishi ndani ya unyayasaji unaofanana na huu niliouelezea hapa.
Naomba tuwe wakweli kwa nafsi zetu. Je watumishi wetu wa ndani wako salama?
Mniwie radhi kama nimewakwaza.
Monday, January 5, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
8 comments:
Miongoni mwa makundi yanayokabiliwa na unyanyasaji mkubwa ni watumishi wa ndani.Na katika hilo,haichagua kati ya wasichana au wavulana,japo wengi wa watumishi wa ndani ni wasichana.
Mifano ni mingi,nami nimepata kusikia habari za kuhuzunisha kuhusu mateso yanayowakabili watumishi hao,lakini nalopenda kugusia hapa ni miongoni mwa vyanzo na labda nini kifanyike.
Kwa ujumla sekta ya ajira binafsi ni moja ya maeneo ambayo yanapuuzwa mno na watunga sera na sheria wetu licha ya umuhimu wake mkubwa katika jamii.Pengine kabla ya kuangalia namna watumishi wa ndani wanavyonyanyaswa,tuangalie jinsi waajiriwa katika nyanja nyingi za sekta binafsi wanavyotumikishwa sio kwa mujibu wa sheria bali matakwa ya wanaowaajiri.Look at bar maids,for instance,au vibarua mashambani,nk.Wengi wao hutumikishwa mithili ya watumwa huku excuse kubwa ikiwa "ugumu na ushindani wa ajira",yaani "usipotaka wewe kuna wenzio kibao wanahitaji."
Laiti kungekuwapo sheria kali (na zinazofuatwa na kusimamiwa) kuhusiana na ajira "binafsi" (au zisizo rasmi,sijui lipi ni jina sahihi) ni dhahiri ingekuwa rahisi kwa waajiriwa kudai haki zao na waajiri kutekeleza wajibu wao.Siku zote haki na wajibu ni shurti zifungamane.
Kwa akinadada wanaoajiriwa kama housegirls,just like barmaids,mara nyingi wanajikuta kwenye choice ngumu kati ya kudai haki zao (ambazo hawana uhakika wa kuzipata hata wakidai,and if they know them at all)na "kumtumikia kafiri ili upate mtaji wako." Wengi wao wanalazimika kuvumilia manyanyaso "ili mkono uende kinywani."
Imagine binti ameletwa kutoka Iringa,kwa mfano,anafika Dar hajua A wala B,anakumbana na unyanyasaji kutoka kwa mwajiri wake,hajui wapi pa kulalamika,na wakati mwingine hapewi hata uhuru wa kutembelea marafiki au ndugu,au pengine hana hata ndugu mmoja,hana namna ya kuwasiliana na wanaoweza kumsikiliza kilio chake...katika mazingira ya aina hiyo ni rahisi kwa mtumishi huyo kuamua kwamba hiyo ndio destiny yake...avumilie ipo siku yatakwisha.Unfortunately,mwisho wake unaweza kuwa mimba,kuambukizwa ukimwi au hata kusingiziwa wizi na kubambikiziwa kesi asiyostahili.
Nini kifanyike?Itachukua muda mrefu kubadilisha jambo linaloonekana kama sehemu ya utamaduni wetu.Lakini hiyo sio excuse ya kuacha jambo baya ati kwa vile tu "ni la kawaida."NGOs zinazojihusisha na eneo hilo zina role kubwa ya ku-play.Na zipo zinazofanya vizuri katika eneo hilo japo ni chache.Tatizo kubwa la civil society katika nchi zetu za dunia ya tatu,ni its failure to act as a bridge between the state and society.NGOs nyingi zimekuwa vyanzo vya mapato binafsi huku vikitumia legitimate causes such as hiv,poverty,child labour,sexual harassment,etc kuhalalisha existance zao pasipo kutekeleza wajibu wao.
Policy and law makers wetu nao wana nafasi muhimu ya kusimamia sheria zilizopo na kuziboresha ili kuhakikisha zinakuwa na manufaa kwa walengwa.Na hapo tena civil society ina role nyingine ya ku-act as pressure groups kuwakumbusha wahusika kuhusu mapungufu mbalimbali katika sheria husika.
Wahanga (victims) nao wana nafasi yao,no matter how difficult it is,nayo ni kuweka wazi madhila wanayokumbana nayo.Ni ngumu kwa vile inamaanisha kuhatarisha ajira zao.Na hapo tena civil society (kwa maana ya taasisi zinazojihusisha na eneo hilo) pamoja na policy and law makers wetu (isomeke serikali,wabunge,etc) wana jukumu la kuhamasisha waajiri kuzingatia sheria na waajiriwa kutambua haki zao na namna wanavyoweza kuwasilisha malalamiko yao kuhusu waajiri wao.
Ni ngumu,lakini inawezekana.Matokeo yanaweza kuchukua muda mrefu kupatikana,lakini la muhimu ni yapatikane.
mhhhhh, unyanyasaji wa kijinsia. je wale wanaolazimika kuvaanguo za kubana, wanaovaa nywele bandia, wanaolazimika kujikondesha, wanaojichubua, wanaobadili sauti zao, wanaolazimika kukodoa nk, hawanyanyasiki kijinsia?
wanaume wanaonekana kuwa viumbe wa hajabu kuliko wote duniani, japo wanawake hawaonekani kugoma kuolewa nao.
Inasikitisha!:-(
Inafikirisha.
Inahuzunisha.
Kujirekebisha.
Wao hawapo tayari.
Pengine wana kiburi.
Ahsante sana kaka Evarist kwa mchango wako maridhawa,
Maoni yako yamepanua wigo wa hii mada, nimetafakari kwa kina mchango wako nimeona nisifunge hii mada ili watu wengine waweze kuchangia, maana naona huu mjadala ni mzito na ni mpana sana kwa sababu unagusa maeneo mengi.
Ukweli ni kwamba umeeleza mambo mengi sana na umenifumbua macho kwa kiasi kikubwa sana.
Na wewe kaka Kitururu ulikuwa wapi? ni siku nyingi sijakuona kibarazani kwako.
kaka Fadhy ni kweli inahuzunisha na kufikirisha.
kuna jamaa pale maskani anajinafasi sana, duuh naogopa kusema mengi
Watumwa bado tunao majumbani kwetu. Hima tuupige vita utumwa huu.
Pamoja na kwamba mabadiliko ya mfumo wa maisha siku hizi unaowalazimu wanawake kuwaacha watoto wao kwa ajili ya kazi, nadhani kuna haja ya kuangalia suala hili kwa makini zaidi.
Uzuri wa kwanza wa blogu hii ni kuwa ni ya mwanamke wa Kitanzania. Pili, ni ya mwanamke anayeandika moja ya masuala muhimu sana ya unyanyasaji wa wanawake hasa wale wasiosoma (toka vijijini) ambao ni hawa watumishi wa ndani( zamani wakiitwa "maboi" wanawake kwa wanaume).
Mwaka jana hili suala lilizungumziwa katika vyombo vya habari baada ya yule mtumishi aliyempeleka Mdosi mmoja mahakamani kusaidiwa na chama cha wanawake cha TAWA London.
(soma http://kitoto.wordpress.com)
Wapo wasichana wanaonyanyaswa ugenini si tu kikazi bali pia wanabakwa na kupigwa (na Wadosi na Vigogo wa Kibongo) ughaibuni ( na TZ kwenyewe).
Ni vizuri wote tukipiga madebe; ila kelele zitasikika zaidi ikiwa waandishi wa kike kama dada Mkundi wakiendelea kuwika na kuimba hewani.
Post a Comment