Tuesday, January 6, 2009
WANAUME KWA KUPENDA SIFA!
Kuna mambo madogo madogo yanayowahusu wanaume huwa watu wengi hawayaoni na kufanya tafakuri.
Katika makuzi yangu nimegundua udhaifu ambao wanaume wengi wanao lakini hausemwi kwa sababu ya mfumo dume kutawala.
Nimegundua kwamba sifa ndio inayowauwa wanaume wengi, kwa kutaka kwao, kuimarisha mfumo dume walionao (ego)
Nitajaribu kueleza kidogo kuhusu maana ya hili neno ego, kwa tafsiri yangu isiyo rasmi, naomba munirekebishe kama sitapatia.
Kwa mujibu wa nadharia za wanasaikolojia ego ni yale tuliyofundishwa na jamii kwa ujumla, yaani yale tuliyoambiwa kwamba ni mabaya au mazuri kwa mujibu wa jamii. Kwa mfano wanaume wamefundishwa kwamba wao ni kichwa cha nyumba, wao ndio wenye maamuzi sahihi, hawakosei, wana akili kuliko wanawake, wana mamlaka juu ya wanawake, wao ndio wanaotakiwa kuchumbia kulipa mahari na kuoa, na mambo mengine mengi tu unayoyafahamu.
Kwa hiyo ndio sababu utakuta wanaume wanapenda sana sifa, wanataka wanawake wawaone kwamba wao ndio bora kabisa na wasioshindwa na jambo lolote. Ukitaka mwanaume akuchukie basi mkosoe.
Wakati fulani wakati nafanya kazi kwa kwenye taasisi moja, aliwahi kuja kijana mmoja ambaye alivaa kihuni huni hivi akitaka kumuona mkurugenzi wa ile taasisi.
Kwa bahati mbaya mkurugenzi hakuwepo, nikamuuliza, Jina lake ili mkurugenzi akirudi niweze kumfahamisha.
Basi yule kijana akionekana kushangaa, aliniuliza, “Ina maana hunijui mimi?”
Nikamjibu, “Ndio Mimi sikujui!”
Mwenzake aliyefuatana naye akaniuliza kama naangalia TV, nikamjibu kuwa, huwa naangalia lakini sio vipindi vyote vya kwenye TV, ndipo akaniambia kuwa yule kijana ni mwanmuziki maarufu wa Bongo Fleva anayejulikana Afrika ya Mashariki na anaonekana sana kwenye TV, ndipo nikamwambia kwamba huwa sisikilizi hiyo miziki, kwa sababu siipendi.
Yule kijana alionekana kuishiwa na nguvu kwani hakutegemea jibu la aina ile kutoka kwangu kwa sababu aliniona mimi ni msichana na labda ni mshabiki wa muziki wa Bongo Fleva.
Alichotegemea kutoka kwangu ni kumsifia, na kumtetemekea na labda kujishaua na kujipendekeza kwake, kwa kuwa hiyo ndiyo tabia ya wasichana wengi wa umri wangu.
Sio kwamba naidharau hii miziki ya Bongo Fleva, lakini nadhani malezi yameniathiri, kwetu hatuna kawaida ya kusikilia hiyo miziki ya Bongo fleva.
Nyumbani kwetu tunasikiliza nyimbo za dini na labda Country music na R&B yaani miziki ya taratibu.
Ninayo mifano mingi sana maana huwa napambana na wanaume wengi sana wakware ambao nawaona wanavyopata taabu kujipendekeza wakiwaona wasichana warembo.
Nakumbuka siku moja nilikutana na kijana mmoja maeneo ya Mlimani City, huyu kijana niliwahi kusoma naye sekondari lakini yeye alinitangulia, baada ya kukumbushana habari za shule na vituko vyake aliniomba niungane naye kwenda kupata chakula cha mchana mjini ili tuweze kuzungumza zaidi.
kwa kuwa nilikuwa na safari ya mjini nilimkubalia.
Baada ya kufanya manunuzi tulitoka nje, basi yule kijana akataka kuita Taxi, nilimjulisha kwamba nimekuja na gari hivyo haina haja ya kuchukuwa Taxi.
Alionekana dhahiri kubabaika, na uso wake ulisawajika,
tulipoingia ndani ya gari,akaanza kujisemesha,
“Unajua gari langu limepata ajali juzi, kuna jamaa mmoja alinigionga kwa nyuma, hivyo liko gereji’
Nilimpa pole, lakini nilijua wazi kwamba anajihami, kwani sikumuuliza kama analo gari au la.
Yote hiyo ilikuwa ni kutaka sifa, alitaka nijue kwamba naye analo gari, kwa sababu kutokuwa na gari alijiona kama hajakamilika.
Kwa hiyo adui mkubwa kabisa wa mwanaume ni kukosolewa, lakini sio kwamba wanawake hufurahia kukosolewa, naomba nieleweke hapa, kwa kawaida mwanamke anapokosolewa haimpi shida, kama ilivyo kwa mwanaume, kwani kutokana na mfumo dume, wanawake wamekuwa wakikosolewa tangu miaka milioni iliyopita na kutupiwa lawama hata kama kosa ni la mwanaume.
Hebu soma Mwanzo 3 fungu la 11 mpaka la 13, naomba ninukuu:
“Akasema ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya nikala”. Mwisho wa kunukuu.
Kwa mujibu wa maandiko Eva alidanganywa na Nyoka ale tunda la mti wa katikati nae akamdanganya Adamu ili ale lile tunda, hivi hapo kosa ni la nani?
Yule aliyedanganywa au aliyedanganya?
Kwa nini Adamu asikatae kula lile tunda?
Si alikuwa anajua kabisa kwamba walikatazwa na Mungu kutokula hilo tunda la mti wa katikati?
Kwa nini asihoji sababu ya kutakiwa kula hilo tunda na Eva?
Ukichunguza sana utagundua kwamba yote hiyo ilikuwa ni kutaka sifa, alitaka awe na uwezo kama wa Mungu ili ajiridhishe, kwani alipewa kila kitu katika ile bustani ya Edeni lakini hakuridhika akautaka Umungu! Halafu leo analaumiwa mwanamke!
Mpaka hapo nadhani umeona ni kiasi gani wanawake wamekuwa wakikosolewa na kulaumiwa tangu enzi na enzi, na umeona hata Biblia imekiri hilo.
Ndio maana Mwanaume akikosolewa na mwanamke huumia sana, kwa sababu ya mazoea. Humfanya mwanaume kuona kama vile amenyang’anywa uanaume wake, hana thamani tena na hastahili.
Kama wewe ni mwanamke ukitaka kumuathiri mwanaume kisaikolojia basi mkosoe.
Kwa kawaida kukosolewa au kukosoa siyo jambo lenye kuweza kumpa mtu jazba. Lakini hivi sivyo ilivyo kwa mwanaume, kwani mfumo dume yaani ego ndiyo inayotawala kichwani mwake.
Tunashuhudia hata huko mashuleni tuliposoma, kama ukimzidi mwanaume kwa alama katika mitihani hasa kama anasifiwa kuwa ana akili sana, hiyo inaweza kumuathiri kisaikolojia, na anaweza kukosa raha au hata kujenga chuki.
Kwa upande wa sisi wanawake, nimejifunza jambo moja, kama umeolewa au uko kwenye uhusiano na mwanaume, basi kuwa makini sana unapomkosoa mwenzi wako.
Kwani unapomkosoa mumeo au mpenzi wako mara kwa mara unaweza kumfanya kukosa nguvu za kushiriki tendo la ndoa kwa sababu maumivu ya kukosolewa huendelea hadi kitandani.
Kwa bahati mbaya wanawake wengi hatujui na tunadhani wanaume ni kama sisi, kwa hiyo tunapowakosoa wanaume zetu tunaamini kwamba tunaweza kuwabadili kitabia kumbe ndio kwanza tunaelekeza uhusiano wetu au ndoa zetu shimoni.
Niliwahi kusoma kitabu kimoja cha mtaalamu mmoja maarufu wa uhusiano Mmarekani John Gray kiitwacho “Men are from Mars, Women are from Venus.
Kitabu hiki kimeeleza mambo mengi sana juu ya tofauti za kawaida kati ya wanawake na wanaume ambazo wengi hatuzifahamu, na huwa tunakosea na kutafsiri mambo ndivyo sivyo.
Naomba habari hii isichukuliwe kama nawashambulia wanaume, bali huu ni mtizamo wangu tu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
10 comments:
Duuuh Koero hii topiki imenishinda! ngoja kwanza hebu nifikirie kidogo au nianze wapi aaaaaa imenishinda sababu jana tu nimekosolewa, nimenyamaza kama maji mtunguni, najipa muda kujifunza, lakini sijui kwanini mungu alikataza ule mti matunda yake yasiliwe, sijui kwanini nyoka aliongea kwa uwezo wa mwenyezi mungu halagu wengine hadi leo wasiongee? nawaza tu, huyu aliyevaa kihuni hata mie ningemtoa ndugu siyo suala la Bongofleva kwani lazima kuwa na idhamu. LAKINI kweli sifa tunazo kwa uwongo ha ha ha ha ha ha ha nicheke kwanza halafu nikuambie kitu? SOMA PALE KWA KAKA SIMON KITURURU- kuna mada yake ameandika JIFUNIKE BASI TUSIKUTAMANI. kuna mabo lakini nakubaliana nawe dada Koero sijui wengine.
Ama kweli kuna mitazamo mingi katika kila jambo. Na kila upande waweza kujenga hoja ikakubalika. Nami nakubaliana nawe kuwa mengi ya yaliyosemwa yanaweza kuwa kweli. Lakini narejea tena niliyoandika kwa Kaka Bwaya juu ya akukosoaye na akusifiaye. Hapa kuna mambo mawili. Moja ni kile kinachokosolewa na pili ni namna unavyokosolewa. Mtu anapodhani anajua kitu nawe ukawa na uhakika kuwa hajui kisha ukamkosoa kuna uwezekano akawa mwelewa ama mwathirika wa ukosoaji huo kulingana na "tone" utakayotumia. Hapa tatizo kubwa ni "tone" na sio "point of view". Ukimwambia mtu "mambo ya hivyo yapo ila hili ni tofauti kidogo japo lafanana na hilo" atakuelewa na kukuchukulia tofauti na atakayemwambia "sio kila kitu kiko hivyo. Hiki ni tofauti, unajianya unajua kila kitu!!" Kwa hiyo wakati mwingine wanawake kwa kuwa nao wanasubiri "opportunities" za ku-show up pale wapatapo nafasi, basi huitumia nafasi waipatayo ku-downpress wenzao ili kwa hiyo nafasi ama kwa hilo jambo ama kwa wakati huo nao waonekane wako juu ya dunia. Hii si wote na ndio maana si wakati na kwa mambo yote watu huchukia kukosolewa. Na pia si wanaume pekee wanaochukia kukosolewa na si wanawake wote wasio na tatizo katika kukosolewa. Ni kwa yeyote, popote na vyovyote kwani hii ni juu ya "tone" na sio point of view kwa jinsia yoyote.
Asante kwa kufikirisha Dada
Lakini pia ni mtazamo wangu juu ya tatizo, pengine ndio tatizo lenyewe.
usitoe mfano wa bible kwani bible iliandikwa na wanaume na hivyo ni bonge la mfumo dume. sasa huyu msanii angekuwa wa kike harafu wewe ukawa wa kiume ingekuwaje?
kumbuka hakuna kitu kinaitwa mfumo dume bali tuna mfumo babe tu bila kujali jenda.
Nakubaliana na wewe kwamba wanaume wengi (kama sio wote) wanapenda kuonekana juu. Kumshushua, ni kutafuta kesi mchana kweupe. Hilo liko wazi.
Uliposimulia kisa cha Adam na Hawa, ulinifanya nifikirie; yupi dhaifu kati ya mwanamke na mwanamme?
Kwa sababu haiwezekani mwenzako kafanya blanda na weye washiriki bila hata swali!
Nionavyo, kama ni mwanamme angeanza kula hilo tunda, sidhani kama angeweza kumrubuni mwanamke kulila. Ingekuwa ngoma nzito.
Kumbuka simulizi za wanaume kama akina Samson. Pamoja na mijiguvu yote ile, mtu mzima ilibidi atoboe siri kuruhusu wembe uvipitie vile vishungi. Huenda biblia haijaandika vyote kuhusu hili.
Maana yangu: Huenda mwanamme hupenda sifa kwa sababu anajijua kuwa ni duni kuliko mwanamke! Sijahitimisha...! Nani mwenye self esteem kubwa kuliko wmenzie?...huenda ndio maana anapenda sifa.
Kila siku mimi kichwa, wapi bwana ungegeuka bila shingo (mwanamke)? She has the influence.
Ebwanaee haya mawe noma.Ni kweli wanaume tunapenda sifa au tunapenda sifa kwa wasichana?
Zamani mdada akinikosoa ilikuwa ugomvi lakini sasa natafuta wa kunikosoa.
Haaaaaaa nimerudi tena. haya ya KALAMA niliwahi kutofautiana na TGNP kwamba hakuna mfumo dume bali saikolojia hizo ni propaganda za kushindwa kujua tatizo. Upoooo! unaona bwana! nikasema ukisema mfumo dume inamaana maadui zenu wanaume? sawasawa? sasa mbona tulizaliwa huru sote? ndiyo maana katika majadala wa dini nilihoji kwanini Injili ya Bikira mariailiachwa? duuuh mbona biblia yote akina BWAYA, MARKUS, EGI, na wengine kibao? mmm nasemaje kwani, labda utambuzi kweli kuna sifa na wanaume kupenda sifa. Pengine ni mazoea kwamba wanaume ni wapenda sifa, je sote tupo hivyo? Duu au wanawake wanaamini siye ndiyo baba ndiyo kichwa? eeeeeeh nina usongo sijui wa nini kwaheri halafu nacheka basi kidogo ha ha ha ha ha ha ha ha blogu raha sana. dada Koero tupe mada motomoto yaani unanikuna kinoma ila samahani sirudi ng'oooooooo mlimani kwenu KWAERIIII
Mungu mwenye uwezo ajuaye mwanzo mpaka mwisho wa yote, Kwanini aliweka tunda bustanini kama hakutaka liliwe? Kwanini hakuumba binadamu wote wawe dume jike, ili ukiniringia nijipe miba mwenyewe?:-(
Binafsi,nadhani kupenda sifa ni silika ya MTU na haina mahusiano na jinsia yake.Katika mifano miwili ya mwanzo,ya mwana-bongofleva na huyo jamaa aliyetaka kuchukua taxi,hakuna uthibitisho wowote kwamba laiti wahusika wangekuwa wanawake basi ingekuwa kinyume na ilivyotokea.
Lakini tunaweza kufanya utafiti usio rasmi ambao hauhitaji muda mwingi kupata matokeo yake.Soma habari kwenye magazeti ya udaku,then jaribu kuangalia "UTAFUTAJI SIFA/UMAARUFU" Kijinsia kati akina Kanumbas na akina Irene Uwoyas,Wema Sepetus,Sintas,Aisha Madindas,nk.
For the sake ya kutetea nafasi yangu kama mwanaume,naomba tujiulize: Hivi kati yetu (wanaume) na wanawake,ni kundi lipi linalohangaika sana katika suala zima la muonekano (looks)?Naomba nisisitize kwamba by muonekano simaanishi unadhifu bali namna mavazi au mitindo itakavyomwezesha mvaaji ku-stand out of the crowd.Waonekane vizuri ili iweje kama sio kusifiwa?JHivi when was the last time you heard mwanaume flani anahangaika na dieting ili awe na shepu ya kupendeza?Sanasana tunasifika sana kwa kula na sio kujinyima mlo ili tuwe na shepu...Na mara ya mwisho kusikia kundi kubwa la vijana wa kiume wakija Dar kutoka mikoani kusaka MISTA TANZANIA ilikuwa lini?Niweke pembeni "chuki" yangu dhidi ya ishu nzima za u-miss,lakini whole idea naiona kama kuji-commodify kwa jinsia ya kike...na kwa mtizamo wangu,hiyo inahusiana na kusaka sifa.Hata majumbani,ndugu zetu wa kike wanatumia muda mwingi zaidi kujiremba (na pengine kuishia kuchelewa which could lead them into kukosa sifa inayosakwa in the first place...umependeza sana lakini umewasili ukumbini late,hakuna wa kukona unavyong'aa...).Note:kupendeza kwa mwanaume ni ishu inayohitaji umakini katika jamii yetu ya kiafrika.Watu hawakawii kumhisi mtu vibaya...
Dada Koero,filosofia isiyo rasmi huko mtaani ni kwamba mwanaume anayependa SANA sifa hufananishwa na mwanamke,implying kwamba wanawake ni mahiri zaidi katika kupenda sifa kuliko wanaume.
Anyway,nimalizie kwa kusema kwamba kwa mtizamo wangu,kupenda au kuchukia sifa ni suala la mtu binafsi zaidi kuliko jinsia yake,na kama tutalifanya suala la kijinsia mifano hiyo juu inatosha kutueleza jinsia gani iko more obsessed na SIFA. Lakini tunaweza kwenda mbali zaidi na kuiangalia SIFA kisosholijia.As a positive sanction,sifa inaweza kudumisha yaliyo mazuri kwa mtizamo wa jamii husika eg kusifia tabia njema,mafaniko,juhudi,heshima,etc.Sifa pia inaweza kuwa motivational factor,kwa mfano kwenye taasisi za elimu ambapo SIFA zinazoambatana na ku-perform vizuri huwapa changamoto wale walio-perform kawaida au vibaya.Katika hilo,yaani sifa as a positive sanction,sioni ubaya wa yeyote,awe mwanaume au mwanamke,kutafuta sifa.
Pengine ni muhimu pia kukumbuka kwamba ni nadra kwa sifa ya kujipa,as opposed to sifa ya kupewa (au sifa "halisi" as opposed to sifa "feki")kumletea mlengwa matokeo chanya,at least kwa muda mrefu.Hoja hapa ni sustainability ya sifa anayopewa mtu kwa vile anastahili,tofauti na ile anayopewa ili kumridhisha au kwa malengo ya kupata kitu flani kutoka kwa msifiwa.Nadhani hata kwenye maandiko kuna kitu kama those who exalt themselves will be humbeled,and those who humble themselves will be exalted (nukuu isiyo rasmi).
Asante Kaka Evarist.
Naiona mada imefikia patamu.
Kama kumbukumbu zangu ziko sahihi, nakumbuka niliseam kwamba huo ulikuwa ni mtazamo wangu, naomba msinirushie mawe.
Kwa bahati mbaya nilikuwa nimeangalia upande mmoja wa shilingi zaidi ya mwingine.
Kaka Evarist umenipa chancgamoto. Hivi kumbe mwanamke kujiremba ni kupenda sifa?
Ahsante kwa kunijuza.
Wakati naandika mada hii nilihofia sana kushambuliwa na wadau wa blog hii hasa wanaume lakini haikuwa hivyo.
Ahsanteni sana kwa kuonesha ukomavu, kumbe naweza kuchokoza mada tofauti tofauti na kupata changamoto nyingi zenye kueleimisha.
Ahsanteni sana kaka Mpangala, kwa kurudi mara mbili, kaka Kamala , kaka Bwaya, mzee wa changamoto Mubelwa Bandio, na kaka uliyefunga kazi Evarist.
Nawashukuru sana kwa mitazamo yenu ambayo imenifungua macho kwa kiasi kikubwa.
naomba msichoke kusoma ujinga wangu maana huenda kuna mawili matatu mnajifunza ndani ya huu ujinga.
Post a Comment