Monday, August 31, 2009

SERA YETU YA ELIMU HAPA NCHINI MBONA IMEPOGOKA HIVI!

Ni hivi karibuni niliandika juu ya habari ya vibaka wa pale Tandale kwa Mtogole na Manzese niliyoipa kichwa cha habari kisemacho “DAR ES SALAAM: TANDALE KWA MTOGOLE NA JARAMBA LA SASAMBUA SASAMBUA” . Niko Arusha kwa sasa na niko huku kutokana na shughuli za kifamilia.

Kwa hapa Arusha eneo ambalo unaweza kulifananisha na Tandale kwa Mtogole au Manzese ni Unga Limited, Ngarenaro, Kimandolu, na Sanawari eneo la Mbwa Chini.
Nimetolea mfano maeneo hayo kwa kuwa ndio maeneo ninayoyafahamu vizuri, lakini naamini mikoa yetu yote hapa nchini inayo maeneo fulani fulani ambayo ni korofi kwa uhalifu.

Lengo langu leo sio kuongelea uhalifu na hao vibaka, bali nataka kuzungumzia sera yetu ya elimu hapa nchini. Nilipokuwa Dar es salaam, kila nikipita katika vituo vya daladala nakuta kundi la vijana wanaopiga debe maarufu kama mateja, na hao hao ndio vibaka wanaopora watu hapo vituoni.

Katika utafiti niliofanya nimegundua kuwa kila mwaka idadi ya wapiga debe katika vituo vya daladala inazidi kuongezeka, hii ina maana gani, ni kwamba kila mwaka wanafunzi wanapomaliza darasa la saba lipo kundi kubwa la wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo ya sekondari hivyo huishia mitaani.

Je nini majaaliwa ya wanafunzi hawa? Je ni kwa nini nguvu kazi hii inaachwa ikipotea bure, hivi kupiga makelele ya kuita abiria na kujipatia shilingi mia au mia mbili ndio uzalishaji? Je kijana huyu anachangiaje pato la Taifa?

Ukweli ni kwamba sera yetu ya elimu hapa nchini imepogoka mno na haimuandai kijana kujiajiri ili kujiletea maendeleo na kuongeza pato la Taifa, na hili niliwahi kulijadili katika mada niliyoipa kichwa cha habari kisemacho “
HIVI MSOMI HASA NI NANI?

Nakumbuka wachangiaji wengi waliojitokeza kila mmoja alisema lakwake na mjadala ule uliisha bila kupata muafaka. Sina haja ya kurudia kile nilichokisema, bali leo ninayo maoni tofauti kidogo katika kulizungumzia hili.

Kuna siku nilikuwa naongea na mzee Mkundi, ambaye ni baba yangu, huyu mzee mie hupenda kumuita M-Conservative, kutokana na misimamo yake.
Siku hiyo nilimuuliza juu ya tofauti iliyopo kati ya mfumo wa elimu tulionao sasa na ule uliokuwa ukitumiwa na wakoloni, kabla ya kupata uhuru.

Baba alishangazwa na swali langu hilo, lakini hata hivyo alinijibu. Kwa mtazamo wake alisema kwamba pamoja na kwamba sera ya elimu ya mkoloni haikuwa na nia ya kutaka Muafrika ajitawale, lakini yalikuwepo maeneo ambayo sera hiyo ilifanikiwa sana.
Kwa mfano, wale wanafunzi ambao walikuwa hawana uwezo darasani lakini walionesha kuwa na vipaji, hao waliandaliwa kulingana na vipaji vyao huku wale wenye uwezo darasani waliendelea na masomo ya elimu ya juu.

Katika wale ambao walikuwa hawana uwezo darasani ndio waliokuja kuendelezwa katika fani mbalimbali kama vile utalamu wa kilimo, ufundi washi, useremala, makenika, ufundi mitambo, uhunzi na fani nyingine za michezo.
Yote hayo yalifanyika katika program maalum kwa hiyo hakuna mwanafunzi ambaye hakuwa na uwezo darasani ambaye alitelekezwa.

Tulipopata uhuru ndio kila kitu kilipoanza kuvurugwa taratibu, katika mfumo wa elimu.
Labda kulikuwa na nia nzuri ya kutaka kubadili ule mfumo wa elimu wa kikoloni uliokuwa umejikita zaidi katika kuwaandaa makarani wa kusimamia shughuli za wakoloni na kuweka mfumo wa kizalendo, lakini mabadilliko hayo hayakufanywa kwa umakini, kwani ilitakiwa tuache yale mabaya na kuchukua mazuri kama hayo ya kuwaandaa vijana katika nyanja mbali mbali kutokana na vipaji vyao. Lakini hata hivyo mzee Mkundi alibainisha kuwa, inawezekana ni kweli makosa yalifanyika kutokana na upeo finyu tuliokuwa nao wakati huo, lakini hivi mpaka leo bado tumeshindwa kutengeneza sera maridhawa ya kuwaandaa vijana wetu ili kujiajiri?

Hayo ndio majibu ya mzee Mkundi kwa mtazamo wake, hata hivyo niliamua kumshirikisha Profesa Matondo {bonyeza hapa kumsoma} katika mjadala huu, naye alikuwa na haya ya kusema:


Ukweli ni kwamba mfumo wa elimu yetu ni mbovu na kama ulivyosema haumwandai kijana kuweza kufanya lolote mbali na kuajiriwa baada ya shule. Tatizo ni kwamba hatuna ajira za kutosha na vijana wengi wanaishia kutelekezwa. (1) Kuna shule chache sana za sekondari na vijana wengi wanashindwa kukivuka hata kizingiti cha darasa la saba. Sijui hawa ni asilimia ngapi lakini nadhani ni wengi sana pengine karibia asilimia 75. Hakuna anayejua wala kujali hawa wanakwenda wapi baada ya kumaliza darasa la saba. Wengine wanajaribu umachinga, upiga debe na bila shaka kuwa vibaka na ujambazi. Halafu serikali inajaribu kupambana na tatizo hili kwa kuajiri mapolisi zaidi. Tazama maoni yangu niliyoweka katika blogu yako hapa:

(2) Hivi ulishawahi kujiuliza ni kwa nini watu wanaofeli mitihani ndiyo tunawatuma wakawe waalimu na waelimishaji wa taifa letu? Eti ukishindwa kwenda High School (division 3 na division 4) ndiyo unapelekwa ualimu. Unaweza kupata F zote na D mbili tu au tatu tu lakini bado taifa likakupa wajibu mzito wa kuandaa vijana wake. Huu nao ni muujiza. Literally kipofu anamwongoza kipofu mwenzake. Hapo unategemea nini? Kwa wenzetu huku kuanzia mwalimu wa chekechea ni lazima awe na digrii ya kwanza ya chuo kikuu, na awe "certified". Shule za msingi ndiko hasa tunapaswa kuweka misingi na kama mtoto anaanza na waalimu wetu hawa waliopata F zote na D mbili katika masomo yao ya kidato cha nne, unamtegemea mtoto huyo atakuwaje hata katika viwango vya juu vya elimu?

(3) Suala jingine ni lugha. Miaka saba ambayo ni ya muhimu sana kwa mtoto, mtoto anafundishwa kwa lugha nyingine na kimiujizaujiza tu anategemewa kwamba anapokwenda sekondari basi atakuwa amekifahamu Kiingereza sawasawa kiasi cha kukitumia ipasavyo katika masomo yake. Watoto wengi wanakwenda kidato cha kwanza hata hawajui kujitambulisha katika Kiingereza halafu wanategemewa eti waweze kuzifahamu Newton's Laws of Motion na maana zake pamoja na manufaa yake. Hapa ndipo elimu inakosa maana na kuwa zoezi la kukariri tu. Unakariri, unakopi kwenye mtihani, unapata A unasonga mbele ingawa hujui kitu. Na hili linaendelea mpaka pale Mlimani. Unapata digrii yako, unabahatika kuajiriwa, unaboronga na mambo yanaendelea. Japo leo kuna mfumuko mkubwa wa hizi "academy" zinazofundisha kwa Kiingereza tupu, tatizo ni kwamba nyingi zipo mjini wakati walengwa wake wako kijijini; na hata huko mjini ni wangapi wanaweza kumudu gharama zake?

Mzee Mkundi yuko sawa. Wakoloni hawakumtelekeza mtu kwani walihitaji sana watu wenye ujuzi fulani kuweza kuwasaidia katika shughuli zao nyingi. Walihitaji mafundi seremala, waachi, mafundi umeme, mafundi wa magari n.k. kwani wasingeendelea kuagiza watu hawa kutoka kwao Ulaya. Sijui tulishindwa nini kuendeleza sera nzuri kama hii. Siasa ya Kujitegemea mashuleni ilikuwa na lengo kama hili lakini bila vifaa na vitendea kazi, siasa hiyo iliishindwa. Badala yake ikawa wakati wa kujitegemea watoto mnakwenda kufagia na kumwagilia maua maji!Je wadau wengine mnasemaje juu ya hili?

Tujadili kwa pamoja

Tuesday, August 25, 2009

UMRI WA UBARUBARU NA VIBWEKA VYAKE!!!


Ilikuwa ni mwaka 1998 na ninaukumbuka vizuri sana huo mwaka, kwani ndio mwaka niliovunja ungo, ni kipindi hicho ambapo nilianza kushangaa maumbile yangu jinsi yalivyobadilika na nilikuwa nahisi kuwa na mamlaka makubwa sana, sikutaka kuchuliwa kama mtoto tena ingawa nikuwa bado ni mtoto, kwa umbo na umri.
Nilikuwa nagombana na mama pamoja na dada zangu mara kwa mara pale nyumbani na sikusikia la mtu. Nilikuwa ni mbishi na mkorofi kwa kila mtu pale nyumbani, lakini mama yangu alikuwa ainichukulia kwa tahadhari sana, daima alizoea kusema kuwa hayo ni mapito tu. Kipindi hicho sikumuelewa juu ya kauli ile, lakini sasa nimemuelewa, tena vizuri sana.

Siku moja wakati naenda shule nilikutana na kijana mmoja mzuri na mtanashati hivi na kama bahati nzuri wote tulikuwa tunaelekea kituoni, kupanda basi, nilijikuta nikivutiwa na yeye na nilitamani sana kumsemesha lakini nilikuwa nawaonea aibu sana wanaume nikabaki nikimuangalia kwa jicho la kumuiba. Tulipofika kituoni nilijikuta kila saa nikimtazama, na kila akigeukia upande niliposimama na kugongana macho na mimi nilikuwa naangalia pembeni kwa aibu.

Nilitamani sana kumsemesha lakini sikuweza kufanya hivyo kutokana na aibu na pia nilikuwa nawaogopa wanaume. Nakumbuka wakati nilipokuwa mdogo, nilikuwa namsikia mama yangu akizungumza na dada zangu na kuwaeleza juu ya athari za kujenga mahusiano na wanaume katika umri mdogo, sikuwa nayasikiliza yale mazumgumzo kwa kuwa nilijua hayanihusu, jambo lingine ni juu ya tabia yangu sikuwa nawapenda sana wanaume na nilikuwa sina kawaida ya kuwazoea wavulana hata wale niliokuwa nikisoma nao.

Lakini tangu nimuone huyu kaka kwa jicho la kwanza, nilijikuta nikivutiwa naye ingawa sikujua kuwa navutiwa naye ili iweje, ila nilitamani sana kuwa naye karibu. Nikiwa katika lindi la mawazo huku nikiwa katika dunia ya peke yangu basi lilifika na yule kijana alipanda na kuondoka na kuniacha pale kituoni nikiwa nimeshikwa na butwaa huku nikijilaumu kwa kutomsemesha wala kumuuliza jina lake.

Sikuchukua muda nami nikapata basi na kupanda na kuelekea shuleni. Nilipofika shuleni ile sura ya yule kijana ilikuwa ikinijia mara kwa mara, na siku hiyo masomo hayakupanda kabisa mpaka mwalimu wangu mmoja akaniuliza kama nilikuwa naumwa, nikikataa kwa kumjibu kuwa siumwi, lakini nadhani aliona kuwa sikuwa katika hali ya kawaida siku hiyo. Niliporudi jioni nilikutana na kaka mmoja jirani yetu, ambaye nilikuwa nasoma na mdogo wake shule moja lakini madarasa tofauti, alinisimaisha na kuniuliza kama nimemuacha wapi mdogo wake, nilimjibu kwa kifupi kuwa nilimuacha kituoni, mara ghafla yule kijana akaja pale tulipo na kunisalimia kwa kunishika mkono, nilijikuta nikitetemeka na mapigo ya moyo wangu yakienda mbio, nilimjibu huku nikiangalia pembeni kwa aibu sikutaka kukutanisha macho na yeye, nadahani hata yeye alihisi jambo kwani aliniachia mkono wangu.

Yule kijana tunayeishi naye jirani alinitambulisha kwa yule kijana kuwa ni mjomba wake na yuko pale kwa muda akisubiri kujiunga na masomo ya kidato cha tano, ambapo alikuwa amepangiwa kwenda kusoma Tabora Boys. Kuanzia siku hiyo nilikuwa siishi kwenda kwa akina yule binti tuliyekuwa tunasoma naye lengo lilikuwa ni kutaka kumuona huyu kijana, ingawa sikuweza kuzungumza naye kutokana na kuwa muda mwingi alikuwa bize sana akijisomea.

Siku moja kama kawaida yangu nilikwenda pale nyumbani kwa rafiki yangu lengo langu kama kwaida lilikuwa ni kataka kumuona yule kijana na siku hiyo nilipania sana nizungumze naye, na kweli siku ile ilikuwa ni kama bahati kwangu nilimkuta yuko peke yake pale nyumbani na mtumishi wao wa pale nyumbani. Alianzisha mazungumzo na swali lake la kwanza alitaka kujua kuwa kama nimeokoka, nilimjibu kuwa sijaokoka, nilimrudishia swali lile kwa kumuuliza kama na yeye ameokoka. Jibu lake lilipenya moyoni mwangu kama mkuki moyoni. Alinijibu kwa upole kuwa ameokoka tangu akiwa darasa la tano, kutokana na kumtegemea yesu na ndio maana amekuwa akifaulu tangu darasa la saba mpaka sasa anatarajia kujiunga na kidato cha tano.

Jibu lake halikunifurahisha hata kidogo, lakini sikujua sababu ni nini?
Alitumia fursa ile kunishawishi niokoke na kumkubali yesu kuwa mwokozo wangu, nilimkatalia katukatu kuwa sikuwa tayari kuokoka, alinipa mifano mingi katika biblia, lakini hakuna hata moja lililoniingia katika mazungumzo yake bali nilikuwa najisikia furaha kwa jinsi alivyokuwa akizungumza kwa upole kama ananibembeleza, mawimbi ya sauti yake yalikuwa yakipenya katika masikio yangu kama vile aina fulani ya muziki mororo.

Nilikuwa natamani aendelee kuongea tena na tena. Lakini mara ghafla wenyeji walirudi na sikuwa na budi kuaga na kuondoka. Nilianza kuzoeana na yule kijana lakini mazungumzo yake ya kunishawisi niokoke sikuyapenda, hata hivyo ilibidi nikubali kuambatana naye kanisani anaposali ilimradi niwe naye karibu, kule nyumbani nilikuwa naaga kuwa nakwenda kwa rafiki yangu kujisomea.

Pale kanisani alinitambulisha kama mgeni wake ambaye amekubali kumpokea yesu kristo, nilishangiliwa sana na kupongezwa kwa uamuzi wangu ule, ingawa dhamira yangu ya kuwepo mahali pale haikuwa ni kwa ajili ya wokovu kama ilivyosemwa bali ilikuwa ni mapenzi niliyokuwa nayo kwa huyu kijana. Nilianza kujenga wivu, kila nikimuona anaongea na msichana mwingine pale kanisani kwao, roho ilikuwa inaniuma sana.

Siku moja wakati tunatoka kanisani alikuwa akinisindikiza kurudi nyumbani, mara tukakutana na kaka yangu mkubwa akaniuliza natoka wapi na yule niliyefuatana naye ni nani, nilimjibu kwa kiburi na jeuri kuwa haimuhusu, basi kaka alimfokea sana yule kijana kuwa anataka kuniharibia maisha na kumtishia kuwa atampiga. Yule kijana kwa uungwana aliondoka zake bila kusema chochote na kurudi kwao. Niliumia sana na niliporudi nyumbani nilijifungia chumbani kwangu na kulia sana.

Mama alikuja chumbani kwangu na kuniuliza sababu ya kulia, nilimueleza kila kitu, mama hakusema kitu aliondoka zake, lakini kaka alikuja huku nyuma na kunifokea sana.
Kesho yake nilisikia alikwenda pale alipofikia yule kijana na kumfokea sana yule kijana na kutoa onyo kuwa akimkuta na mimi atamfunga aozee jela. Ukweli ni kwamba kaka yangu huyu mkubwa alikuwa ni mkorofi sana, na alikuwa haelewani hata na dada zangu kwa kuwaingilia katika mambo yao wakati walipokuwa wanasoma.

Nilipopata taarifa juu ya yule kijana kufuatwa na kufokewa na kaka, iliniuma sana na niliamua kuchukuwa uamuzi hatari wa kutaka kujiua kwa kuhisi kudhalilishwa pale mtaani, nilikunywa idadi kubwa ya vidonge ambavyo hata sikujua kama vilikuwa ni vidonge gani na kujifungia chumbani kwangu, baadae nilianza kujiskia vibaya na hivyo nikaanza kuugulia, dada yangu alinisikia na alipoingia chumbani kwangu na kunikuta katka hali ile, nilimsikia akimuita mama kwa sauti kubwa “mama mwanao anakufa” nilipoteza fahamu na niliposituka nilijikuta nikiwa hospitalini nikiwa nimetundikiwa Dripu.

Siku iliyofuata niliruhusiwa na kurudi nyumbani, mama yangu alichukuwa nafasi ile ya kuwepo kwangu nyumbani kwa mapumziko ya kuumwa kunipa darasa juu ya mabadiliko ya kimwili baada ya kuvunja ungo na hisia za kimapenzi, mama alikuwa wazi kwangu kwa kunieleza kila kitu juu ya mapenzi ya utotoni na athari zake na jinsi ya kuepuka vishawishi na namna ya kukabiliana na changamoto za usichana, na kikubwa zaidi aliniasa sana juu ya kuwaepuka wavulana wakware.

Naomba nikiri kuwa kwa swala langu yule kijana hakuwa na makosa na kamwe hakuwahi kunitamkia jambo lolole linalohusu na mapenzi wala kuonesha dalili za kunitamani licha ya kujipendekeza sana kwake, bali mimi ndiye niliyekuwa na kiherehere.

Baadae nilipata taarifa kuwa yule kijana aliamua kurudi kwao ili kuepusha shari. Ilinichukuwa takribani mwaka mzima yule kijana kufutika katika mawazo yangu kabisa, kwani pamoja na semina ya mama lakini nilikuwa najikuta tu natamani nikutane naye barabarani, jambo ambalo halikutokea na wala halitakuja kutokea.

Miaka miwili baadae nilipata habari ya kusikitisha, na ambayo iliniacha na majonzi hadi leo, yule kijana alifariki kwa ajali wakati akirudi nyumbani kwao baada ya kumaliza mitihani ya kidato cha sita. Ingawa nilishamsahau kutokana na kujitambua lakini habari za kifo cha yule kijana kilinisitua sana na kunikumbusha machungu ya siku ile niliyotaka kujimaliza kwa ajili yake. Najua ilikuwa ni utoto, lakini kwangu mimi lile lilikuwa ni darasa tosha.
Labda niwaulize wasomaji wa blog hii, hivi ni wazazi wangapi ambao wako wazi kwa mabinti zao kwa kuwaeleza ukweli juu ya mabadiliko ya miili yao pindi wanapovunja ungo?
Je ni wazazi wangapi ambao wako tayari kuwakabili mabinti zao na kuwaambia ukweli huu bila kuogopa mila na desturi ambazo nyingi zimepitwa na wakati?

Jamani umri wa ubarubaru una misukosuko na vitimbi vingi……….

Sikuandika habari hii ili kujidhalilisha bali kutaka wasomaji wa blog hii wajifunze kupitia uzoefu wangu huu. Naitwa Koero Japheti Mkundi

Saturday, August 22, 2009

DAR ES SALAAM: TANDALE KWA MTOGOLE NA JARAMBA LA SASAMBUA LA SASAMBUA

Niliamka alfajiri na mapema, ilikuwa ni kama saa 10:30, na kujiandaa, pamoja na kuandaa uji wa mgonjwa. Ni wiki sasa mama yangu amelazwa Hospitalini Muhimbili akisumbuliwa na Presha pamoja na kisukari.

Hivyo ndivyo alivyoanza rafiki yangu Zulfa, katika email yake aliyonitumia jana, akinisimulia masaibu aliyokutana nayo juzi jijini Dar es salaam.

Baada ya kujiandaa majira ya saa 11:00 nilitoka na kuelekea kituoni cha basi pale Magomeni Makanya, nilipofika pale nilikuta abiria kadhaa na nikajiunga nao kusubiri daladala, haikuchukua muda daladala moja aina ya Toyota Coster likafika na abiria wote tuliokuwa pale kituoni tukapanda, nilipata siti ya mbele karibu na dereva nikakaa na abiria wote walipoingia tuliondoka. Daladala letu lilikuwa likienda huku likipakia abiria wengine njiani.

Tulipofika maeneo ya Tandale kwa Mtogole basi letu likasimama ili kupakia abiria, na waliingia abiria saba, wanawake watatu waliokuwa wamevaa mahijabu yaliyofunika nyuso zao kama maninja na wanaume wanne waliokuwa wamevaa kanzu.

Walipoingia wote kabla basi halijaondoka, mwanamke mmoja miongoni mwa abiria wale alikwenda moja kwa moja kwa dereva na kuchomoa panga kutoka kibindoni na kumuwekea dereva shingoni na kisha kuzima gari na kuchukua funguo, wakati huo huo miongoni mwa wale abiria mwenye kanzu alimuamuru kondakta akae kwenye kiti huku akiwa amemshikia panga vile vile, wale abiria waliokuwa na mahijabu, tuliodhani kuwa ni wanawake, kumbe walikuwa ni wanaume. Walitandika kitambaa cheupe na kutuamuru abiria wote tuliokuwa ndani ya lile daladala kila mmoja aweke kila alicho nacho pale katika kitambaa akianza na simu. Walikuwa wakiimba ule wimbo maarufu huku Pwani unaotumika wakati wa kumtunza bi harusi kabla ya kuolewa uitwao sasambu sasambu, wakitaka kila mtu asasambue alicho nacho na kukiweka katika kile kitambaa.

Baada ya kuona kama vile tunachelewa walianza kutupiga kwa ubapa wa upanga na kutisha kuwa atakayekuwa mbishi au kujitia ujanja watamuua kwani hawana cha kupoteza, wanawake wote tulinyang'anywa mikoba yetu na cha kushangaza hata kile kikapu klichokuwa na uji wa mgonjwa walikibeba.

Kuna mzee mmoja hakuwa na simu na hiyo ilimgharimu, kwani walimpiga kwa ubapa wa upanga mpaka akajifanya amezirai ndio wakamuacha, wakati zoezi hilo likiendelea vibaka wengine walikuwa nje na kazi yao ilikuwa ni kutishia daladala nyingine zilizotaka kusimama katika eneo lile zisisimame.

Ilikuwa kila daladala likitaka kusimama wanapiga mapanga kwenye bodi ya daladala hilo na kutoa lugha ya vitisho hivyo hakuna daladala au gari lolote lililosimama katika eneo hilo kutokana na eneo hilo kuthibitiwa na vibaka hao.

Baada ya kuhakikisha wametupora kila kitu walitokomea kusikojulikana wakiwa na funguo za gari, na kutokana na juhudi za dereva wa basi lile na kondakta wake walifanikiwa kuliwasha basi letu na tukaenda moja kwa moja hadi kituo cha polisi pale Tandale.

Tulipofika na kutoa ripoti, askari wa zamu waliokuwepo pale kituoni walimshambulia dereva wa basi letu na kondakta wake kuwa ni wazembe kwa kuwa lile eneo linajulikana kuwa ni hatari kwa vibaka ambao hupora hata mchana kweupe inakuwaje yeye asimame kituoni hapo alifajiri yote hiyo? Walidai kuwa madereva wote wa mabasi yanayopita njia hiyo wanalifahamu eneo hilo ambalo wamelipachika jina la mahakama ya simu kutokamna uporaji wa simu uliokithiri katika eneo hilo la Kwa Mtogole.
Karibu abiria wote tuliokuwa pale kituoni ambao tumeporwa tulishikwa na mshangao, kumbe eneo linajulikana kuwa lina vibaka, sasa kwa nini hawathibitiwi na kituo cha polisi hakiko mbali na eneo hilo?

Tuliandikisha maelezo yetu kisha kila mtu akashika njia yake, mimi ilibidi nirudi nyumbani ili kutengeneza uji mwingine wa mgonjwa kwani uji niliokuwa niupeleke kwa mgonjwa umechukuliwa na vibaka.

Basi dada Koero huo ndio mkasa ulionipata mwenzio, na mama yangu sasa hivi ameruhiusiwa na anaendelea vizuri.

Huo ndio mkasa uliompata rafiki yangu Zulfa, na ndio akanitumia email hii ili niweke katika kibaraza cha VUKANI ili kuwahabarisha wasomaji wa kibaraza hiki waishio Dar Es Salaam wachukue tahadhari.

Hiyo ndiyo hali halisi iliyotamalaki katika eneo hilo na hata Manzese. Nakumbuka hivi karibuni nilipokuwa Dar Es Salaam mama mmoja rafiki wa mama yangu anayeishi Kimara, aliporwa hand bag yake akiwa ndani ya daladala wakati akienda kazini asubuhi, tena huyo kibaka aliingia kwenye daladala hilo kama abiria na alichukuwa hand bag ya mama huyo na kushuka bila wasiwasi kama ya kwake huku abiria wakimuangalia.

Pamoja na yule mama kupiga kelele za mwizi lakini hakuna hata abiria mmoja aliyejishughulisha kumkamata kibaka huyo na alitokomea zake bila wasiwasi, wale abiria walimlaumu yule mama eti ni uzembe wake kwani eneo hilo linajulikana kwa vibaka na ndio maana wanawake wanashauriwa kuweka hand bag zao chini ya miguu, na hairuhiusiwi kushika simu mkononi katika eneo hilo na kama ukipigiwa simu si vyema ukapokea kwani ukipokea hiyo simu itachukuliwa na wenyewe wenye simu yao, yaani vibaka.

Naambiwa hali ni mbaya sana katika eneo hilo na tukio kama hilo lililompata rafiki yangu Zulfa sio la kwanza kutokea katika eneo hilo na hata Polisi wetu wanafahamu vizuri sana juu ya matukio ya uporaji yalivyokithiri katika maeneo hayo, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. Naamini hatua zisipochukuliwa na jinsi pengo la wenye nacho na wasio nacho linavyozidi kukua basi tutarajie vibaka hawa kupora mchana kweupe kwa staili ya kufunga mtaa.

Tuesday, August 18, 2009

DUH HATOKEI WA KUOANA NAYE!!!!! SEHEMU YA MWISHO

Mungu huwa analipa hapa hapa duniani, aliendele kusimulia Eliza miaka mitano baadae nilipata taarifa kuwa aliyekuwa mchumba wangu amelazwa katika Hospitali ya Mount Meru na hali yake ni mbaya sana. Aliyenipa taarifa hizo hakuniambia kuwa anaumwa ugonjwa gani.

Sikwenda kumuona wala sikujishughulisha kufuatilia habari zake, niliendelea na maisha yangu kama kawaida. Wiki mbili baadae nilikutana na rafikiye na alishtuka sana kuniona kwani tulipoteana kwa muda mrefu sana takribani miaka mitano kwani nilihama katika shule ile siku nyingi nikapangiwa kufundisha shule iliyoko jirani na ninapoishi kwa hiyo kuja maeneo ya katikati ya mji ilikuwa ni mara chache sana.

Yule rafiki wa aliyekuwa mpenzi wangu aliniomba tutafute mahali tukae ili tuongee kwani alikuwa akinitafuta kwa siku nyingi sana. Tulisogea katika Baa iliyoko jirani na tulipofika pale yule bwana aliniomba niagize kinywaji, niliagiza maji ya kunywa.

Yule bwana akaniomba niende Hospitalini nikamuone mpenzi wangu wa zamani kwani hali yake ni mbaya na amekuwa akinitajataja sana kuwa anahitaji kuniona kabla hajafa ili aniombe radhi, nilishangaa sana, aniombe radhi kwa lipi? Mbona mimi nilishamsamehe siku nyingi.

Nilikataa kwenda kumuona, lakini baada ya rafikiye huyo kunibembeleza sana nilikata shauri niende kumuona, ili kuondoa lawama.

Nakumbuka ilikuwa ni siku ya ijumaa, rafiki wa mpenzi wangu alinifuata shuleni mida ya jioni akiwa na gari lake na tukaondoka na kwenda Mount Meru hospitali kumuona yule bwana,

Tulipofika, tulielekea wodini moja kwa moja, kwa jinsi tulivyokuwa tukitembea kuelekea wodini na ndivyo mapigo ya moyo wagu yalivyozidi kuongezeka, nilikuwa napumua haraka haraka kama vile nilikuwa nakimbia mpaka shemeji angu akawa na wasi wasi.

“Vipi shemeji, unayo matatizo ya moyo?” aliniuliza….
“Hapana sina kabisa? Nilimjibu kwa sauti ya kutetemeka. Tulipo karibia Wodi aliyolazwa yule mpenzi wangu wazamani yule shemeji yangu aliniomba tupumzike pale nje kwanza kabla ya kuingia wodini, lengo lake ilikuwa ni kunipa nafasi nipumue na ku relax kidogo.

Tulipoingia wodini niliwakuta ndugu zake wengi, nadhani walikuwa wanafahamu ujio wangu kwani walisogea pembeni na kunipa nafasi ili niweze kumuona mgonjwa.

Nilisogea pale kitandani alipo, alikuwa amekonda sana kiasi kwamba hata ile sura yake niliyoizoea ilikuwa imetoweka, alinikazia macho kwa nukta kadhaa bila kusema neno, ndugu zake waliniambia kuwa alikuwa amekata kauli tangu jana.

Alinionesha ishara niiname kama vile alitaka kuniambia kitu, nilijongea karibu na yeye na kuinama, alinishika mkono kwa nukta kadhaa kisha akaongea kwa sauti ya chini sana,,, “Naomba unisamehe mpenzi wangu, nisamehe ili nikapumzike kwa amani”

Nilijikuta machozi yakinitoka na nilishindwa kusema kitu chochote nikabaki nikiwa nimemtumbulia macho..
“Nilishakusamehe mpenzi wangu, najua sio wewe bali ni shetani ndiye aliyesababisha yale yaliyotokea yatokee” Nilimwambia.
Tuliangaliana, nikamuona akitokwa na machozi, namimi sikuweza kujizuia nilijikuta nikilia nilitoa leso yangu na kujifuta machozi na kisha kumfuta na yeye.

Niliondoka pale na yule shemeji yangu, aliyenipeleka pale. Njiani alinisimulia mkasa uliompata mpenzi wangu yule wa zamani mpaka kuwa katika hali ile.

Kumbe yule mpenzi wangu wa zamani alihamishiwa Moshi, kwa hiyo ikabidi yeye na yule mkewe aliyenisaliti wahamie moshi. Miaka miwili baadae mkewe akiwa ni mjamzito wa miezi mitatu yule bwana akapata mkasa wa upotevu wa mamilioni ya pesa katika kitengo chake na yeye kama mkuu wa kitengo hicho na wenzake wakawekwa ndani. Kutokana na mshituko wa mumewe kuwekwa ndani, yule mkewe akapoteza ujauzito.

Baadae walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka, lakini walinyimwa dhamana kutokana na unyeti wa mashitaka yao.
Inasemekana wakati mumewe akiwa bado yuko ndani, yule mkewe akawa anachapa umalaya akitembea na wanaume mbali mbali wakiwamo marafiki wa mume wake.

Ilichukua mwaka mmoja yule bwana kuachiwa kwa kufutiwa mashitaka kwa kuwa hakuhusika na ule upotevu. Alipotoka ndugu zake walimshauri amuache yule mwanamke kwa kuwa alikuwa na tabia mbaya za umalaya na alikuwa amemdhalilisha kwa ,arafiki zake, lakini yule bwana hakusikia aliwapuuza nduguzake na kumtetea mkewe kuwa hakuwa Malaya bali wanamsingizia.

Baadae yule mwanamke alipata ujauzito tena, lakini ujauzito huo ulikuwa na complicationa nyingi, na kumfanya kudhoofu sana, baadae ujauzito ule ulitoka tena na kuanzia hapo akawa ni mgonjwa wa kitandani, na alipopelekwa hospitali alikutwa na TB.

Hali ilizidi kuwa mbaya, mume alikuwa hana kazi na mke ndio alikuwa ni mgonjwa. Pamoja na juhudi za kumtibu mkewe kwa kushirikiana na ndugu zake lakini haikusaidia kwani alifariki.

Kutokana na kifo cha mkewe, yule bwana alipata mshtuko na hivyo kulazwa hospitali kwa matibabu, hata hivyo hali yake haikuonekana kutengemaa, ikabidi ndugu zake waishio Arusha wamchukue na kumhamishia Arusha kwa ajili ya kumhudumia.
Baada ya vipimo ilionekana kuwa yule bwana alikuwa ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.

Naambiwa kuwa kila siku alikuwa akinitaja taja na alikuwa anataka nitafutwe ili aniombe radhi kwani alinikosea sana.Ukweli ni kwamba mimi nilikwisha wasamehe wote na nilishasahau.

Yule rafikiye alinifikisha nyumbani kwangu, na tulipeana namba za simu na akaondoka zake. Siku iliyofuata yaani jumamosi, alifajiri alinipigia simu na kunijulisha kuwa yule bwana amefariki alifajiri ile na mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Moshi kwa mazishi inafanyika kwa kaka yake mkubwa maeneo Njiro. Nilikwenda Njiro na kuungana na ndugu wa marehemu. Nilikuwa ni miongoni watu waliosafiri kwenda Moshi kwa mazishi na ndugu wa marehemu walikuwa karibu na mimi utadhani nilikuwa ni mke wa marehemu.

Tulimzika mpenzi wangu wa zamani na kisha kurejea Arusha siku hiyo hiyo. Maisha yanaendela kama kawaida na nimeshasahau, ila tukio hili limenifundisha jambo, kuwa kama ukiona jambo haliwi kama unavyotaka au ulivyotarajia, huna haja ya kulazimisha, kwani huenda kuna kitu unaepushwa nacho. Namshukuru mungu kwa yote, kwani yeye ndiye mchungaji wangu.

Sunday, August 16, 2009

HIVI HATUWEZI KUBADILIKA?

Wasomaji wapendwa, katika pitapita zangu leo nimekutana na hii makala, pale katika kibaraza cha Utambuzi na Kujitambua, na kama kawaida yangu nimeona nifanye Mdeso kwa msisistizo. Jamani haya mambo si yapo? Nimeona ni vyema tukiyasema kwa nguvu zetu zote ili hawa wanasiasa wetu matapeli ambao wako katika harakati za kunoa vinywa vyao ili kutudanganya hapo 2010, wajue kwamba kazi ipo.

******************************************

Ni nani atakaye kuja siku moja kuliona jambo hili, kuuona ukweli huu, kwamba nchi hii haina umaskini wa rasilimali, wala umasikini wa nguvu kazi, bali ina umasikini mkubwa wenye kutisha na kukera wa namna nzuri ya kufikiri.

Kuna kukomboka kwingi katika kufikiri kiasi kwamba watu wa nchi hii wanaonekana kama kituko katika mitindo yao mingi ya kimaisha.Ni kweli kwamba wananchi wengi wa nchi hii ni wapole, wanapenda amani na uaminifu, lakini ndani ya sura hiyo kumelala ujinga, kutojiamini, na hofu kuu iliyoambatana na kushindwa kwao kujijua.

Wananchi wengi wakiwapo pia viongozi wamekuwa wanaishi kwa kufuata utaratibu maalumu ambao tunauita mazoea ya namna ya kufikiri.Kuna kila kitu katika nchi hii, ambacho binadamu anakihitaji ili aweze kuishi katika ubora unaopimika. Kuna ardhi, maji ya kutosha, wanyama, madini, na nguvu kazi ya kutosha lakini kila siku hali ya mtanzania inazidi kudidimia, malalamiko yanazidi, kutoaminiana kunaongezeka na ulaghai unashamiri.

Kila kunapokucha kinachoboreka ni njia bora za udanganyifu, ulaji rushwa na ubabaishaji. Kila jinsi umri unavyosogea ndivyo jinsi kufikiri vizuri kunavyo didimia kwenye tope la ufahamu.Tunapenda sana kuishi katika dunia ambayo haipo tunapenda kuyatazama mambo au masuala mengi yanayotuhusu kimakengeza kana kwamba hayatuhusu sisi.

Hali hii bila shaka ni matokeo ya kufikiri vibaya tuna maana ya kuyatazama mambo au kila hali kwa imani ya kushindwa, kuharibu na machungu. kuyatazama mambo ya kila hali katika majaribio kwamba yatajiendesha yenyewe na kufikia mafanikio bila juhudi wala maarifa yetu.

Ndiyo maana yanaibuka masuala kama ya RICHMOND na EPA kama ilivyokuwa NET GROUP. Kila mmoja anajitahidi kujaribu kujidanganya kwa kudhani kuwa kuna miujiza ambayo huja tu tukiwa tumelala na mambo kuwa sawa na hakuna haja kwetu kuutazama ukweli na kuufanyia kazi. Mambo yanapobadilika, kwa sababu tuna asili ya ubishi, bila kujali tunabisha, na kujikuta tukiingia kwenye kulumbana kwa kuhemkwa bila kutafakari kwa kina.

Hebu tujiulize kuhusu Air Tanzania (ATCL) ni kweli serikali ina haki ya kudai kwamba shirika hilo limeshindwa kazi? Hivi Serikali imeshindwa kuwatumia wataalamu wetu hapa nchini kulinusuru hili shirika?Ukweli ni kwamba hali mbaya inayoyakabili haya mashirika yetu ya umma na mahali pengine ikiwemo kwenye shughuli zetu za binafsi hazitokani na uwezo wa kimapato uliomo humo au tulio nao bali zaidi kwa namna tuvyofikiri.

Mazoea yalisha tujengea kufikiri kwa namna fulani kuhusu kazi na uwajibikaji. Tulishajengewa kufikiri ambako kunatusukuma kudhani kwamba kila wakati na katika kila kitu tunadanganywa na kuonewa bila kutazama ukweli.Kikubwa ambacho serikali na wananchi wanapaswa kukifahamu ni kwamba tumeshatoka kwenye maisha ya miaka ya 1970 na tuko mahali pengine kabisa. Dunia imebadilika sana na inaanza kuingia mahali ambapo wale waliofikiri vizuri ndiyo pekee wenye nafasi ya kufikia mafanikio wanayoyataka.

Kujidanganya kwa kudhani kwamba kutafuta huruma, kuviringa maneno kwa njia tamu kutasaidia katika kufikia mafanikio ni kupoteza muda wetu bure. Kama hatuwezi kutimiza wajibu wetu ni ujinga mkubwa kutarajia kupata haki zetu, na kutumia mabavu kutatua matatizo yetu hutuingiza kwenye kiza kikubwa zaidi cha utambuzi ufahamu na hatima yake siku zote ni kukwama.

Ni vizuri kujiuliza kila wakati kama tunachodai ni haki yetu kweli au tunachowanyima wengine siyo haki yao kweli. Tukishindwa kujiuliza maswali ya namna hii tutakuwa hatujitendei haki kwasababu kila wakati tutahisi kuwa tumeibeba dunia na pia tutaweza kuhisi kwamba hatupendwi na kuheshimiwa. Muda wa kujidanganya umeshapita siku nyingi, hali halisi ndiyo muongozo wa maisha kwa sasa.

Friday, August 14, 2009

HUYU NDIYE YASINTA NGONYANI!!!

Yasinta Ngonyani, Picha kwa hisani ya Maisha Blog

Ni binti halisi wa kitanzania, ingawa anaishi ughaibuni lakini hujivunia asili yake na utaifa wake, ni binti pekee aliyejitolea muda wake kuwaelemisha watu wa rika zote bila kujali rangi, kabila, itikadi, taifa wala jinsia.

Binti huyu si mjivuni na hupenda kubadilishana mawazo na watu mbali mbali, na pia hupenda kufuatilia habari za nyumbani kwao alikotoka na haoni tahayari kuongea lugha ya kwao. Daima hujitambulisha kwa jina la asili ya kwao na huona fahari kutumia jina hilo.

Binti huyu hakuona ajizi kuwajuza wanae asili ya kwao japo wamezaliwa ughaibuni, amekuwa msitari wa mbele katika malezi ya wanae ili kuhakikisha wanae hao hawajitengi na asili ya aliotoka yeye.

Si mchoyo wa ushauri na kupitia makala zake aziwekazo kibarazani kwake amekuwa ni msaada kwa wengi, amekuwa mstari wa mbele katika kuilemisha jamii bila kujali rika. Amejitolea kufundisha kile akijuacho juu ya malezi na matatizo mbali mbali yanayowakabili wanandoa na malezi ya watoto.

Kibaraza chake kimekuwa ni kitovu chenye kukutanisha wadau mbali mbali wenye fikra pevu, na kuibua mijadala yenye kuelimisha, kufundisha, kuburudisha na kuhuzunisha pia.

Binafsi napenda kumuita dada na kwangu mimi ni zaidi ya dada, kwani amekuwa ni mwalimu mzuri kwangu nikijifunza mambo mengi kupitia kibaraza chake nimekuwa nikijifunza mengi, na sisiti kukiri kwamba chimbuko la kibaraza cha VUKANI ni kutokana na kile nilichojifuza kwake.

Ni mkweli na muwazi, na hasiti kusema wazi hisia zake, lakini huwa makini sana ili kuepuka kumuumiza mtu mwingine kihisia, na kama kwa kusema huko kutamkera mtu mwingine, ni mwepesi kuweka sawa maelezo yake ili kuondoa msigishano wa mawazo.

Nakumbuka wakati fulani nlipopata msongo wa mawazo kutokana na tofauti zangu na wazazi wangu, alikuwa ni mtu wa kwanza kunitumia email binafsi akijaribu kuniliwaza na kunitaka nisichukue hatua yoyote kujidhuru, naomba nikiri kwamba email ile ilinisaidia sana kurudi katika hali yangu ya kawaida na nilijisikia fahari kuona kwamba kuna mtu ananipenda na kunijali japo sijawahi kuonana naye uso kwa uso.

Huu kwangu ulikuwa kama muujiza, inakuwaje, mtu kusoma mawazo yangu kupitia blog tu halafu awe karibu nami kiasi hiki, ni kitu gani kimemvuta? Kusema kweli tangu siku hiyo niliamni kuwa maandishi yana nguvu sana na kupitia maandishi yawezekana mtu mwingine kukufahamu vizuri sana.

Nimekuwa karibu sana na binti huyu, na amekuwa ni mwema sana kwangu na mshauri wangu pia, na kupitia vibaraza vyetu, tumekuwa tukibadilishana mawazo na kupeana ushauri mbali mbali ili kuboresha ustawi wetu na wa familia zetu.

Huyu ndiye Yasinta Ngonyani, kwa kumsoma zaidi bofya hapa

Sunday, August 9, 2009

DUH HATOKEI WA KUONA NAYE!!!

Alipofika hapa Arusha kwa mara ya kwanza ni mimi niliyempokea, nakumbuka ilikuwani mwaka 2000. Alikuwa ndio amemaliza chuo cha ualimu huko Ndala Tabora na alipangiwa kuja kufanya kazi hapa Arusha.
Akiwa ni mzaliwa wa huko Old Moshi mkoani Kilimanjaro, hakuwa na ndugu wala jamaa hapa Arusha, hivyo akiwa kama mwalimu mwenzangu nilimpokea na kukaa naye kama mdogo wangu. Hata hivyo uamuzi wa kumkaribisha binti huyu nyumbani ulifurahiwa na mpenzi wangu ambaye ni mchaga na alimuona yuele binti kama dada yake na mimi kuanzia siku hiyo tukawa tunaitana wifi na binti huyo.

Kwa kuwa nilikuwa na ugeni pale nyumbani ilibidi wakati mwingine niwe naenda kulala kwa mpenzi wangu kwa sababu pale nyumbani nafasi ilikuwa ni ndogo, kwani kutokana na mishahara ya waalimu kuwa midogo na kodi za nyumba hapa Arusha kuwa juu sikuwa na uwezo wa kulipia vyumba viwili.

Tulikuwa na kawaida ya kutoka jioni mara kwa mara mimi na mpenzi wangu kwenda kula nyama choma, nililazimika kumchukua wifi yangu na kutoka naye ili asijisikie mpweke.

Nakumbuka siku moja, wifi yangu huyo aliniuliza kama nina muda gani tangu niwe na uhusiano na kaka yake, nilimjibu kuwa tuna miaka minne tangu tuwe wachumba. Huku akionekana kushangaa alisema “Miaka minne hamfungi tu ndoa mnangoja nini?”
“Sijui kaka yako, kila nikimwambia tufunge ndoa anadai eti hajajiandaa, mpaka akamilishe mambo fulani”

“Mimi siwezi, miaka minne mko wachumba tu! Si umzalie mtoto labda ndio atachukua uamuzi? Alishauri wifi yangu,
“Siko tayari kulazimisha kuolewa kwa kumbebea mwanaume mimba kisa nataka kuolewa, kama anasubiri mpaka nibebe mimba, basi atasubiri sana,” nilimjibu
“Wifi wanaume wa siku hizi mwanzangu, wagumu kweli kuoa, usipowabebea mimba basi utabaki hapo, utashangaa kesho unasikia ana mtoto kwingine au anaoa mwanamke mwingine kisa kamjaza mimba” Alisema wifi yangu

Wifi kama imepangwa tuoane tutaoana lakini kama haijapangwa basi labda ni mipango ya mungu, nilimjibu.

Kuanzia siku hiyo nikashangaa kukawa na ukaribu sana kati mpenzi wangu na huyo wifi yangu, mara nyingi ilikuwa mpenzi wangu akija anatumia muda mwingi akiongea na huyo wifi yangu tena wakati mwingine wakiongea kikwao yaani kichaga, hata hivyo sikujali sana kwani nilikuwa namuamini sana mpenzi wangu.
Nilikaa na binti yule kwa takribani miezi sita na ndipo akapata chumba na kuhama.
Nilifurahi sana kwa binti huyo kuhama kwani nilijua kuwa sasa nitapata wasaa wa kujivinjari na mpenzi wangu, lakini mambo yalkuwa ni kinyume, kwani mpenzi wangu alibadilika na alikuwa haonekani kwangu kama ilivyokuwa kawaida yake, na nilipokuwa nikimuuliza alikuwa akisingizia kuwa yuko bize sana.

Mpenzi wangu alikuwa ni mtumishi wa Benki na kipindi ambacho anakuaga bize ni kipindi cha mwisho wa mwaka kutokana na kufunga hesabu za mwaka. Kwa hiyo kitendo cha mpenzi wangu kuwa bize katika kipindi kile kilinishangaza sana, hata hivyo hakupunguza upendo wake kwangu, aliendelea kunipenda na kunihudumia kama kawaida na tena aliongeza upendo sana kwangu kiasi kwamba sikuweza kumtilia mashaka kuwa huenda amepata mpenzi mwingine.

Siku moja majira ya jioni nikiwa ndio nimerudi kutoka kazini nilipokea simu kutoka Singida kuwa mama yangu ni mgonjwa na kama nikimkuta hai ni bahati. Miaka mitatu iliyopita ndio nilimpoteza baba yangu kutokana na ugonjwa wa Kansa na sasa ni mama yangu sijui amepatwa na nini masikini. Kwa kuwa nilikuwa ni katikati ya mwezi na sikuwa na akiba ya kutosha nyumbani nilikata shauri kumpigia simu mpenzi wangu ili anipe msaada wa kifedha ili siku inayofuata nisafiri kwenda nyumbani kumuona mama yangu ambaye mpaka wakati huo sikujua kama yuko hai au ameshafariki, lakini nilipompiga simu mpenzi wangu, simu yake ilikuwa imezimwa. Huku nikiwa nimechanganyikiwa niliamua kwenda kazini kwake na nilipofika nikaambiwa ametoka.

Ilibidi niende nyumbani kwake maeneo ya Kaloleni na nilipofika huko napo sikumkuta. Nilikaa pale nje nikiwa nimechanganyikiwa kabisa nisijue cha kufanya, niliamua kumpigia simu yule wifi yangu niliyempokea na kukaa naye pale kwangu, siku hiyo ya ijumaa hakuja kazini alituma ujumbe kuwa anaumwa na asingeweza kuja kazini, na yeye nilipopiga simu iliita sana bila kupokelewa, na nilipojaribu kupiga tena simu ilikuwa imezimwa, niliamua kwenda nyumbani kwake maeneo ya Sanawari, na nilipofika nilikuta mlango wake umefungwa lakini nilisikia sauti ya redio ikiimba nyimbo za dini. Niliona viatu vinavyofanana kabisa na vya mpenzi wangu pale nje, nilihisi labda atakuwa ameamua kumtembelea dada yake.
Nilibisha hodi mara kadhaa, mara mlango ukafunguliwa, yule wifi yangu aliponiona alistuka sana na akafunga mlango haraka na kuniambia nisubiri. Mara alitoka na kufunga mlango kwa nje na huku akiwa amekunja sura akaniuliza nina shida gani, nilishangaa jinsi alivyoonekana kukerwa na ujio wangu, nilimuuliza kama anaendeleaje na kuumwa
“Yaani umetoka kwako kuja kutaka kujua tu kama ninaendeleaje, si ungepiga tu simu, sasa usumbufu wote wa nini?”
Nilimjibu kuwa nilipiga simu sana lakini haikupokelewa, nikadhani labda amezidiwa.
Kama nikutaka kujua hali yangu, basi mimi ni mzima wa afya, samahani nina mgeni ananisubiri ndani, alisema vile na kugeuka kuelekea ndani. Nilishangazwa na majibu yale, lakini nilijua labda ni kwa kuwa anaumwa, unajua sisi wanawake tuna vipindi tunakuwa na visirani kutokana na matatizo yetu mzunguko wa mwezi.
“Samahani Gau, nina matatizo na ndio nikaja kukuona, nimepigiwa simu kutoka nyumabni mama yangu ni mgonjwa mahututi, naomba kama una akiba ya shilini elfu hamsini unisaidie kisha nitakurudishia, nimejaribu kumpigia simu kaka yako lakini simu yake imefungwa” nilimwambia..
Aligeuka kwa dharau na kuniambia, “ hivi kumbe hukuja kuniona bali umeletwa na shida zako, kama ni pesa sina mtafute sijui mpenzi wako au mume mtarajiwa akusaidie” alisema vile na kuondoka zake akiniacha pale nje.

Nilisimama pale nje kwa nukta kadhaa nikiwa nimeduwaa, nilikuwa siamini kile kilichotokea, ama kweli fanya wema wende zako usingoje shukurani walisema waswahili, nilikaa na binti huyu kwa upendo. Miezi yote sita niliyokaa naye hakuwa akipokea mshahara kutokana na kuwa nje ya bajeti ya mshahara, nilimsaidia kwa kila kitu na hata alipopata malimbikizo ya mshahara alitaka kunirudishia kiasi cha fedha nilizokuwa nikimpa lakini nilikataa na ndipo akamudu kutafuta chumba na kuhama, sasa leo nakuja kumuomba anikopeshe pesa kidogo ananijibu kama anamjibu mtu asiyemfahamu!

Niliondoka nikiwa nimechanganyikiwa, kwanza nilijiuliza juu ya vile viatu vinavyofanana na vya mpenzi wangu nilivyovikuta pale nje kwa yule binti, halafu kile kitendo cha kustuka aliponiona, na mbona alitoka na kufunga mlango kwa nje, au alikuwa hataki nimuone huyo mgeni wake, atakuwa ni nani? Nilijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu. Niliamua kumpigia simu rafiki wa mpenzi wangu wanaefanya nae kazi, alinielekeza mahali alipo, alikuwa kwenye Baa na rafiki zake wakinywa pombe na nyama choma, nilipofika alinikaribisha na kuniagizia bia, lakini nilikataa na sikupoteza muda nilimsimulia matatizo niliyo nayo, na yeye alijaribu kumpigia simu mpenzi wangu lakini simu yake haikupatikana.
Alinipa kiasi cha shilingi laki moja na kuniambia atamalizana na mpenzi wangu.

Nilikwenda kutoa taarifa kwa mwalimu mkuu na alinipa ruhusa ya siku tatu. Siku iliyofuata niliondoka asubuhi na mapema kwenda singida na hata asubuhi wakati naondoka nilipojaribu kumpigia simu mpenzi wangu simu yake haikupatikana vile vile.

Nilipofika nilikuta watu ni wengi pale nyumbani, nikajua kuwa, mama yangu ameshafariki. Ni kweli alikuwa amefariki siku ile ile niliyopigiwa simu, na kilichomuua ni shinikizo la damu.
Tumezaliwa watoto watano wanaume wanne na mimi mwanamke peke yangu, na ni wa mwisho kuzaliwa, tangu baba afariki kaka zangu wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara wakigombea urithi wa mali alizoacha baba ambazo ni nyumba mbili na mifugo kadhaa, yaani ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku.

Ugomvi huo ndio chanzo cha mama kupata shinikizo la damu na kufariki kutokana na ugomvi wa kaka zangu usioisha kutokana na kugombea mali za mzee.
Katika familia yetu mimi peke yangu ndiye niliyebahatika kuendelea na masomo hadi kuwa mwalimu lakini kaka zangu walikataa kusoma na kukimbilia kuwa wachuuzi wa biashara ndogo ndogo.

Tulimzika mama na baadae ndugu wa baba waliweka kikao na kupitisha uamuzi kuwa mifugo igawanywe na kisha nyumba ziuzwe na kila mtoto apewe chake ili kukata mzizi wa fitina.

Kila kitu kilifanyika kama maamuzi ya baraza la wazee walivyoamua, nilikabidhiwa ng’ombe zangu kumi na mbuzi nane na kondoo sita na nyumba ziliwekwa chini ya wazee wa familia ili zitakapouzwa kila mtu apate mgao wake, huo ndio ukawa mwanzo wa familia kusambaratika.
Nilikabidhi ile mifugo kwa mjomba wangu kaka yake mama na kuondoka kurudi Arusha kuendelea na kazi.
Kipindi chote nilipokuwa msibani Singida nilijitahidi kumtafuta mpenzi wangu lakini simu yake hauikupatikana.

Niliripoti kazini na kupokelewa na walimu wenzangu, na kuanza kazi, sikumkuta yule wifi yangu kazini niliambiwa kuwa aliaga kwenda kwao Moshi kuhudhuria matatizo ya kifamilia.

Baadae nilianza kusikia minong’ono kwa kaenda kwao kumtambulisha mchumba wake, sikufuatilia habari hizo, niliendelena na kazi zangu.
Siku iliyofuata nilipokwenda nyumbani kwa mpenzi wangu niliambiwa kuwa amesafiri kaenda kwao Moshi.

Siku tatu baadae nikiwa nyumbani kwangu uani nimetulia nikiwa bado nina majonzi ya kufiwa na mama yangu, mchumba wangu alikuja kwangu lakini hali aliyokuja nayo ilinishtua, hakuwa mchangamfu kama nilivyomzoea. Nilimkaribisha ndani, alisita kidogo kisha akaingia ndani, kabla hajakaa alianza kunishambulia kwa maneno makali eti nimemdhalilisha sana kwa marafiki zake kwa kitendo changu cha kukopa pesa kwa rafiki yake badala ya kumtafuta, aliongea kwa sauti ya juu na hakunipa nafasi ya kujieleza.
Aliniambia kuwa kuanzia wakati huo mimi na yeye tusijuane niende kwa huyo huyo aliyenipa nauli ya kwenda Singida. Aliondoka bila ya kunisikiliza na kutoweka.
Nililia sana kwa uchungu. “Sijui nina mkosi gani mie,” nilijisemea

Niliamua kumtafuta rafiki yake aliyenipa nauli ya kwenda nyumbani, Singida, nilimpata na baada ya kumweleza yaliyonipata, alishanga sana na alipompigia simu ili kujua sababu ya kuninyanyasa alimjibu kuwa hayamuhusu na kukata simu.

Yule shemeji aliniambia kuwa nirudi nyumbani na atajaribu kutusuluhisha. Yule wifi yangu alirudi kutoka kwao, na kuripoti kazini, lakini hakunichangamkia wala kunipa pole, nilishangaa sana, kwani sikuwahi kugombana naye.

Nilikuwa sina mawasiliano na mpenzi wangu kabisa na hata namba yake ilikuwa haipatikani, baadae nilikuja kugundua kuwa amebadilisha namba, hiyo ni baada ya kumpigia rafiki yake mmoja na ndio akaniambia kuwa amebadilisha namba.

Siku moja jumamosi nikiwa zangu sokoni nilikokwenda kununua mahitaji nilikutana na mpangaji mwenzie na mpenzi wangu tulisalimiana, na kuanza kupiga stori za hapa na pale, aliniuliza kwa nini sionekani tena pale kwa mpenzi wangu, sikutaka kumweleza juu ya tofauti zetu, nilijua tu kuwa lile lilikuwa ni tatizo la kawaida ambalo lingeisha, kwani kutofautiana kwa watu wawili wapendanao ni jambo la kawaida tu. Nilimjibu kwa kifupi tu kuwa niko bize na masomo, nilimdanganya kuwa ninasoma chuo kikuu huria. Alionekana kutoridhika na jibu langu, nilimuaga na kuanza kuondoka, lakini wakati naondoka, aliniita kwa nyuma “Eliza” nilisimama ili kumsikiliza.
“Nina mazungumzo na wewe unaweza kunipa nafasi tukae mahali tuongee kidogo, ni kwa faida yako” aliniambia kwa kuonesha msisitizo.
Nilimkubalia, tukasogea hadi kwenye baa moja iliyokuwa jirani, aliniomba niagize kinywaji, nikaagiza maji na yeye akaagiza soda.
“Hivi ni kweli umeachana na mpenzi wako” Alianza mazungumzo kwa kuniuliza swali
Nilishikwa na mshangao, kwa swali lile, nikamuuliza sababu ya kuniuliza lile swali.

Mbona tunamuona yule binti uliyekuwa ukija naye pale kwa mpenzi wako, ndiye ameshikana uchumba na mpenzi wako na hivi karibuni alipekeka posa huko uchagani,

Hayo maneno ya mwisho niliyasikia kama mwangwi, na mwili wote umekufa ganzi, nilibaki kimya kwa nukta kadhaa, nilibabaika kidogo…

Yule mwanamke alionekana kushangaa, ina maana ulikuwa hujui?
Nilimjibu kuwa nilikuwa sijui, nilimshukuru na kuondoka zangu kuelekea nyumbani,nilipofika niliweka mizigo yangu ndani, nikatoka kuelelekea kwa yule binti Sanawari, nilipofika niliingia ndani moja kwa moja bila kubisha hodi, nilibaki nimesimama huku nikitetemeka, nilimkuta mpenzi wangu na yule binti wakilishana chakula kwa mahaba….
Sikuamini macho yangu, na hata wao walibaki wameduwaa, niliondoka mahali pale bila kusema lolote, hata majirani ambao walikuwa uani wakati huo walijua kuwa kuna jambo kwani niliwapita bila kuwasemesha na niliondoka bila kuwaaga.

Nilikwenda kwa mwalimu mwenzangu mmoja ambaye ni rafiki yangu, na kumweleza kila kitu. Kwa mujibu wa maelezo yake ni kwamba kumbe kipindi kile niliposafiri kwenda kumzika mama yangu ndio akachukua likizo ya wiki moja kwa madai kuwa amepata mchumba lakini alikuwa akitamba kuwa atatushangaza pale kazini. Hakuna aliyejali maneno yake.

Siku iliyofuata nilifika kazini na niliamua kuchukua likizo ya wiki mbili ili kupumzisha akili kwani nilihisi kuchanganyikiwa, nilimueleza mwalimu mkuu kila kitu naye alitaka kutukutanisha ili kujaribu kuondoa tofauti zetu lakini nilikataa, na alikubali kunipa likizo.

Nilikaa nyumbani siku zote nilikuwa nilishinda ndani nikilia. Kwa muda mfupi nilikonda sana. Kumbe huku nyuma wakati nikiwa likizo yule binti aliomba uhamisho wa haraka na kwa kutumia pesa alifanikiwa kuhamishiwa shule nyingine.

Baada ya wiki mbili nilirudi kazini, lakini nilikuwa na aibu sana kwa kuhisi kufedheka, ilikuwa hata waalimu wenzagu wakicheka nahisi wananicheka mimi, pale nilipokuwa nikikaa napo mambo yaligeuka, baadhi ya wapangaji wenzangu ambao tulikuwa hatuelewani walitumia nafasi hiyo kunikejeli na kunisengenya waziwazi, nilikosa amani.

Niliamua kuhama, na baada ya wiki mbili nilihamia maeneo ya Sakina. Miezi mitatu baadae nakumbuka ilikuwa ni mwanzoni kwa mwaka 2001 yule mchumba wangu alifunga ndoa na yule binti, tena ilikuwa ni ndoa kubwa hasa iliyosheheni mbwembwe kibao. Siku hiyo niliamua kwenda Moshi kwa mwanafunzi mwenzangu niliyesoma naye chuo cha ualimu Patandi.

Siku zilipita na maisha yaliendelea, niliamua kusahau yote na kikubwa zaidi niliwasamehe yule mchumba wangu na yule binti, nikaendelea na maisha kama kawida.

Tangu wakati huo sijapata mwanaume wa kunioa, nimekuwa na uhusiano na wanaume kadhaa ambao waliniahidi kunioa lakini baada ya kuwa nao kwa miezi kadhaa waliniacha bila sababu.

Ninaumia sana mpaka sasa sijabahatika kupata mtu wa kunioa achilia mbali kupata mtoto, nimefikia mahali natamani sana kuwa na mtoto lakini nitamzaa na nani? Wanaume walivyojaa ulaghai. Ingawa nimebahatika kujenga nyumba yangu huko maeneo ya Kwa Moromboo baada ya kupata fedha za mgao wa mauzo ya nyumba zetu za urithi, lakini nahisi nina deni kubwa sana, nahitaji sana kuwa na mtoto.

Jana jumamosi siku ya Sabato nilishinda nyumbani nikitafakari majukumu yaliyonileta hapa Arusha, sikuwa na kazi nyingi za kufanya zaidi nilitumia muda wangu kupitia mtandao ili kusoma mawazo ya wenzangu katika blog mbali mbali.

Mara akatokea mgeni, naye si mwingine bali Rafiki wa wenyeji wangu, anayeitwa Elizabeth. Tangu nimefika hapa Arusha kwa mjomba nilitokea kufahamiana na dada Eliza na ametokea kuwa rafiki yangu wa karibu kiasi cha kuwa tunashauriana juu ya maisha na mambo mengine ya kitaaluma.

Dada Eliza ambaye ni Mwalimu ndio ametimiza umri wa miaka 38 lakini ukimuona umbo lake utadhani ni binti wa miaka 25 hivi, ukweli ni kwamba ana mwili mzuri.

Kwa udadisi wangu katika mazungumzo yetu ya jana nilitaka kujua kwa nini mpaka leo hajaolewa na wala hana mtoto? Na hiyo ndiyo ilikuwa simulizi yake.

Simulizi ya dada Eliza inasikitisha na kuhuzunisha sana. Ukweli ni kwamba wapo wanawake wengi wanatamani kuolewa lakini wamejikuta wakikabiliwa na mazingira kama ya dada Eliza, kusalitiwa, kudanganywa na kutapeliwa kimapenzi.

Kuna kusigishana sana linapokuja swala la kuoa au kuolewa, jamii imetufundisha kuwa mwanaume ndiye mwenye mamlaka ya kuamua kuoa na mwanamke anasubiri kuolewa, kwa maana ya kusubiri tamko la mwanaume kuwa yuko tayari kumuoa, na sio yeye aamue.

Tumekuta tayari utaratibu huo upo na umepewa nguvu na mila na desturi pamoja na hizi dini zetu za mapokeo, tumefika mahali wanaume wanawachezea wasichana watakavyo kwa kigezo cha kuwadanganya kuwa watawaoa, wakati hilo halina ukweli kabisa.

Mimi mpaka leo najiuliza hivi kwa nini watu wanaoana, ni ili iweje? Je watu wanaoana kwa sababu wanapendana au ili wapate watoto?
Na kama watu wanaoana kwa sababu wanapendana, sasa mbona kuna talaka nyingi, kwa nini watu wanaachana? Talaka siku hizi zimekuwa kama jambo la kawaida kabisa.
Kama watu huona ili wapate watoto, Je haiwezekani mtu kupata watoto bila kuoa au kuolewa?

Hivi Mungu alisema muende mkazaane na kuijaza dunia au mkaoane na kuijaza dunia?

Sasa ndio hatokei wa kuoa au kukuoa, ndio hutazaa mpaka uoe au kuolewa?

Hili linahitaji tafakuri………….

ITAENDELEA………….

Friday, August 7, 2009

TANZANIA NA SIASA ZA KINYUMENYUME

Wasomaji wapendwa wa blog hii ya VUKANI, naona nimekuwa mtu wa kudesa siku hizi.
Hii nayo nilikutana nayo katika mtandao wa Jamii Forum, kama kawaida yangu nimeona si vibaya wasomaji wa blog hii nao wakitoa mtazamo wao..................


Badala ya kijenga barabara ili ziweze kupitika, Wananunua magari makubwa (heavy duty vehicles) ili kuwawezesha kupita katika barabara hizo mbovu. Bila kuangalia kuwa kuhudumia magari hayo ni inagharimu kiasi kikubwa sana cha pesa ya wapiga kula. Mfano chukulia gari aina ya Toyota Land Cruiser 4000cc or above, kiasi cha mafuta ambacho gari hili linatumia chukulia mfano kutoka Dar es Salaam mpaka Arusha (One way), kwa safari hiyohiyo mtu atakaye tumia Toyota RAV4 atakwenda na kurudi (round Trip) kwa kiasi kile kile cha mafuta na pengine kubakia na kiasi kidogo cha kuzungukia kilomita kadhaa akishafika. ukiachilia mbali na huduma nyingine kama services za kila mwezi /mwaka za magari haya ambazo nazo zinakwenda kwa karibia uwiano ule ule na gari kama RAV4.

Badala ya kusimamia vizuri vyanzo mbali mbali vya mapato na kuhakikisha kuwa zinatumika ipasavyo na katika uwiano unaeleweka, mfano kuboresha huduma za afya, elimu na mishahara na kuhakikisha kunakuwa na uwiano unaokubalika. Hii itasaidia kuboresha maisha ya raia na utawala wa kuheshimu sheria na kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza uhalifu.

Badala yake njia ya kupunguza uhalifu hasa ujambazi, serikali inaona ni kutoa mafunzo na kuajili askari zaidi. Hata uwiano ukiwa askari 1 kwa raia 1 hii kitu haitafanikiwa kupigana dhidi ya uhalifu kama hali ya maisha ya wananchi itandelea kuwa kama ilivyo kwani hata hao askari ni sehemu ya jamii hii pia na machungu ya maisha na wao yanawapata na uozo unaendela wa viongozi na wao wanaona pia. Sana sana itakuwa ni kufunza majambazi zaidi kwani katika matukio ya ujambazi yanatotokea hivi sasa wahusika wakuu ni askari, ukichukua matukio 5 ya uhalifu/ujambazi wa kutumia silaha matukio 3 kati ya hayo askari (ama askari wastaafu) wamehusika moja kwa moja na matukio.

Badala ya kurekebisha maisha ya vijijini na kupeleka huduma muhumu ili kupunguza tatizo la vijana wazururaji mijini na wengine kuishia kwenye umachinga badala yake wanaajili mgambo kwa ajili yakukabiliana na wachuuzi hao wa bidhaa ndogondogo na Mama lishe.

Badala ya kupima viwanja vingi na kuuza kwa bei ya kawaida kwa raia wote na hatimae watu waweze kununua viwanja hivyo na wajenge kutokana na mipango miji badala yake wanapima vichache na kuviuza kwa bei ya kulinganisha na ile wanayouza watu binafsi. Wanasahau kuwa wao ndio wanatakakiwa wasimamie na kutetea haki ya kila mmoja ya makazi bora yaliyokatika mpangilio badala ya watu wachache tu kusimamia soko hili na kutuwekea bei za ajabu ambazo hauwezi kuziangalia hata mara mbili. Matokea yake kila siku watu wanavamia misitu na kuendelea kujipimia bila mpangilio.

Badala ya manispaa kutumia kodi vizuri za wananchi na kubuni namna gani wanaweza kuweka mazingira safi hasa yale ya ufukweni badala yake wanapiga marufuku watu wasitumie maeneo hayo kwa kisingizio kuwa wanayachafua, kuzuia kuogolea ufukweni (beach), ama kuwa maeneo hayo kwa ajili kupunga upepo.

Badala ya kusikiliza malalamiko ya wanafunzi hasa wale wa vyuo vya elimu ya juu na kuyafanyia kazi wanapuuzia na wanafunzi wakigoma kudai maslahi hayo, wanaishia kuitiwa polisi na kufukuzwa vyuoni na kisha kupewa masharti ya ajabu ajabu kama kuandika barua ya kujieleza na kuorodhesha majina ya waanzilishi wa mgomo wanasahau madai ya mgomo huo ambao ndio mzizi.

Badala ya kufidia wananchi wanaoathirika kutokana na afya zao na maeneo yao kuharibiwa vibaya hasa yale yaliyo katika migodi na wengine kupoteza kazi zao ama kutolipwa mishahara yao kwa muda mrefu, badala yake wanafikiria namna ya kuwalipa fidia watu wachache mabilioni ya shilingi (wawekezaji feki wa migodi hiyo. Mfano KIWIRA).
Kuna mambo mengi sana hawa jamaa wanafanya kinyume na hali halisi.. mnaweza kutoa michango yenu na kuendeleza hiyo list ya REVERSE GOVERNANCE ya serikali yetu...