Saturday, January 31, 2009

NIMEZISHITUKIA OFA ZA WANAUME!!!!!!!

Tumezishitukia ofa zao

Kwa huku kwetu ni wanaume wachache sana wanaomsaidia mwanamke bila lengo la kumpata mwanamke huyo, na akimtaka, mwanamke anaweza kujisikia vibaya wakati mwingine kwa kudhani kwamba misaada hiyo itakoma haraka kwa sababu hakuna jambo lenye kuwashika, yaani tendo la ndoa, hivyo hulazimika kukubali kutoa tendo la ndoa ili misaada isikome.

Hata hivyo sio wanawake wengi wanaokubali kulipa fadhila kwa njia hiyo, lakini wanaume wengi hutumia misaada au ofa kama chambo cha kuwanasia wanawake.

Kwa wanawake kusaidiwa ni kusaidiwa tu huwa hakufungwi na kutakiwa kimapenzi, lakini kwa wanaume kusaidia huwa kunafungwa pamoja na mapenzi.

Je sababu ni nini?

Wanaume wamelelewa na kufanywa kuamini kwamba wanatakiwa kuonesha sifa fulani kwa wanawake kabla hawajawatongoza.

Kwa hiyo mwanaume kabla hajatongoza huanza kujisifu kwanza, ili mwanamke amuone kama mtu anayeweza, hivyo mwanaume anapotoa msaada kwa mwanamke kuna mawili kama sio matatu, ama anataka kusifiwa au anamtaka mwanamke huyo, au vyote.

Lakini pia wanaume wengi huamini kwamba kwa kutoa ofa, mwanamke atajua kwamba anamtaka, hivyo kwa wanaume hao ofa ndio kutongoza kwenyewe. Kwa hiyo mwanume kama huyu anapotoa msaada kwa mwanamke anatarajia kumpata kimapenzi mwanamke huyo.

Kwa mijini kwa mfano mwanamke anayepewa lifti ni yule mzuri kwa sura na umbo, ukweli nikwamba hakuna msaada hapo bali mwanaume anaanza kununua penzi ambalo hajalipata.
Mwanaume akimpa lifti mwanamke na kumtongoza, na mwanamke huyo akakataa, basi huo msaada unafutwa mara moja.

Kwenye baa, mwanaume anaweza kumtuma mhudumu ampe pombe mwanamke fulani. Hajui mwanamke huyo kaja hapo baa na nani na anafanya kitu gani. hiyo ofa sio ya urafiki bali ni ombi la mwili wa mwanamke huyo, kwani hiyo ni hatua ya awali ya kuwa karibu nae.

Kuna idadi kubwa ya wanaume ambao hujitolea kuwasomesha, kuwapa au kuwatafutia ajira wanawake, lakini nyuma ya kujitolea huko, kuna agenda ya kuutaka mwili wa huyo mwanamke.
Mara nyingi mwanamke anakuwa hajui kwamba misaada mingi ya wanaume imefungwa pamoja na mapenzi. Ni wanaume wachache sana waliolelewa tofauti wasiofanya hivyo.

Ukweli ni kwamba wanawake wengi wamekuwa wahanga wa misaada .
Utakuta mwanaume anamsaidia mwanamke, mwanamke anapokea misaada hiyo akijua ni ya kibinadamu, kumbe akilini mwa mwanaume ni kwamba amewekeza. kwa hiyo anapokuja kumtongoza mwanamke huyo akakataa basi vita huanza.

Mwanaume anaweza kukumbushia misaada aliyotoa. na katika hali ya kushangaza mwanamke huyo hushikwa na butwaa. kwani hakujua kwamba alikuwa anapewa misaada ili atoe mwili wake.

Kuna wanaume wengi tu ambao wanaweza kumpa mwanamke soda kama taarifa kwamba amempenda, na mwanamke anaweza kupokea soda hiyo akijua kwamba ni ofa ya kawaida, lakini baadae hushangaa akija kutongozwa, na akikataa, anadaiwa soda aliyokunywa.

Nawasihi wanawake wenzangu wawe makini na ofa za wanaume kwani nyingi zimejaa utata mkubwa.



Habari ndiyo hiyo..........









Tuesday, January 27, 2009

NDOA ZIMEGEUKA KUWA MSAMIATI MGUMU KWA WANAUME?

Siku hizi zimegeuka kuwa msamiati mgumu kwa wanaume
Kumekuwa na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa jamii kwamba imekuaje vijana wa kiume wamekuwa ni waongo sana hasa linapokuja swala la kuoa?

Kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo idadi ya wanaume wanaoogopa kuoa inazidi kuongezeka. Utakuta wapenzi wanaambiana kwamba wanapendana na kuahidiana kuwa wataoana, lakini kitakachotokea baada ya hapo ni mwanaume kuanza kupiga chenga kwa visingizio lukuki.

Kwa nini hali hiyo hutokea?

Ukweli ni kwamba hakuna jibu la moja kwa moja juu ya tatizo hilo, lakini lipo jibu ambalo linaweza kutupa angalau tafakuri.

Siku hizi hakuna shinikizo kubwa kutoka kwa wazazi au walezi la kuwataka vijana kuoa tofauti na zamani. Labda inawezekana ni kutokana na ugumu wa maisha au kulegalega kwa maadili, ndiko kunakopelekea jambo hilo kutokuwa na msukumo mkubwa.

Kwani maisha yamekuwa magumu kiasi kwamba mzazi au jamaa wa kijana anaweza kuhisi ugumu wa kumshinikiza kijana wake kuoa. Sababu nyingine ambayo labda hii ndiyo inayochangia kwa kiasi kikubwa ni ile tabia ya wasichana kukubali kirahisi kuishi na wanaume bila ndoa, au kuwa wapenzi ambao wanakutana kwa muda na kushirikiana katika mambo mengi kama vile wameoana, na kwa kawaida wanaume wakishafanikiwa kuupata mwili wa mwanamke, kupikiwa, na kufuliwa nguo huwa hawaoni tena sababu ya kuoa.

Na kwa kuwa kupenda kwa wanaume kunamaanisha pia tendo la ndoa hivyo upatikanaji wake unapokuwa rahisi wanakuwa hawaoni umuhimu wa kuoa.

Siku hizi wanawake wengi hawajali kuhusu miili yao, na kuigawa kirahisi kwa wanaume limekuwa ni jambo la kawaida kabisa. Na wengine hudhani kuigawa miili yao kirahisi kwa wanaume kunaweza kuwashawishi wanaume hao wawaoe, kumbe ndio kwanza wanaziba njia ya wao kuolewa.

Pia kuna dhana imejengeka miongoni mwa wanaume kwamba wanawake wa siku hizi hawaaminiki, hivyo wengi huona kwamba kuoa inaweza ikawa na maana ya usumbufu, na kwa bahati mbaya wanaume wanaamini kwamba siku hizi kumpata mwanamke wa maana ni jambo gumu sana. Kwa kufikiri hivyo, vijana wengi wa kiume huhangaika kutafuta mwanamke anayefaa bila mafanikio.

Wengi wanaamini kwamba kuna mwanamke mahali ambaye huyo hana kasoro na atakuja kukutana naye siku moja. Wengine wanahofia majukumu hasa ya kulea watoto, kwani huamini kwamba kulea ni jambo gumu sana. Pia wapo wengine wanaamini kwamba, hata mke anapaswa kulelewa kama mtoto, hivyo wanaamua kutafuta kwanza uwezo, ambao nao kuupata ni shughuli kubwa.

Wapo ambao wamefundishwa kwamba ni lazima wawe na nyumba kwanza ndio waoe, hivyo mpaka waje wapate uwezo wa kujenga wanakuwa wameshachelewa sana.

Kibaya zaidi, wapo baadhi ya wanaume, wanaona maisha bila ya ndoa ni bora kuliko yale ya ndoa.

Kwa mujibu wa baba yangu, aliwahi kunisimulia kwamba, zamani, kuoa ilikuwa kama vile ni jambo la lazima, na kijana yeyote ambaye angefikisha umri wa kuoa, halafu awe hajaoa, angelaaniwa sana na jamii, kwani angetafsiriwa kama ni mzinzi, lakini siku hizi swala hili limegeuka na kuwa ni la mtu binafsi na siyo la jamii tena.

Kwa hiyo ningependa kuwatahadharisha wasichana wenzangu kwamba wanapoingia kwenye uhusiano na wanaume wasitarajie sana kitu kinachoitwa ndoa kutoka kwa wanume hao.

Wasichana wenye hekima hawakubali kuonjwa na wanaume ili kulazimisha ndoa bali husubiri ndoa kwanza.







Sunday, January 25, 2009

NILISHINDWA KUMSAIDIA ZINDUNA!


Rafiki na ndugu yangu mpendwa.

Nilikuja nyumbani kwenu kama tulivyoahidiana ili nipate kukuaga lakini kwa bahati mbaya nimekukosa, nilikuja kukuaga kwa kuwa hutaniona tena kwani nasafiri safari ya mbali sana. Baada ya kusubiri sana nimeamua kurejea nyumbani na ilikufanikisha safari yangu, wakati nakuja kwenu nilipitia maduka kadhaa ya dawa na kununua vidonge vya klorokwini vipatavyo 40, naamini vidonge hivyo vitafanikisha safari yangu kwa amani, ili nipate kupumzika.

Naogopa na nahitaji mtu wa kuzungumza nae lakini simuoni, kwani nipo katika ulimwengu wa peke yangu na mbele yangu kuna giza nene, sijui msaada wangu utatoka wapi?Dada yangu mpendwa, wewe ndio rafiki yangu uliyekuwa karibu na mimi wakati wote, ukinipa moyo wa kuzikabili changamoto za maisha, lakini sasa naona imefikia tamati, sina budi kurejea kwa mola wangu.Najua ni dhambi kwa mwanaadamu kukatisha uhai wake kikatili namna hii, kama ulivyowahi kuniambia na kunisomea maandiko matakatifu katika biblia lakini kwa swala langu naamini hii ndio njia muafaka, naomba mungu anisamehe.

Naomba unisamehe kwa kukusababishia maumivu moyoni kwa kuondoka kwangu ghafla katika uso wa hii dunia, lakini sababu kubwa iliyosababisha hili litokee nadhani unaifahamu.Nasema unaifahamu kwa sababu umekuwa karibu na mimi kwa muda mrefu tangu tulipokutana sekondari tukiwa kidato cha kwanza mpaka tulipomaliza kidato cha nne.

Ulikuwa ni zaidi ya rafiki na ulitumia muda wako mwingi ukinifaariji na kunipa moyo hasa baada ya lile jaribio la kutaka kujiuwa la mwaka 2003 wakati tukiwa kidato cha tatu kushindikana.Ingawa naogopa lakini, nadhani hii ndio njia sahihi zaidi ili kuepuka haya maisha ninayoishi, maisha ya upweke yasiyo na hata chembe ya upendo, na hakuna hata mmoja zaidi yako wewe aliyejua upweke niliokuwa nao, hakuna hata mmoja miongoni mwa ndugu zangu aliyekuwa karibu yangu pale nilipohitaji masaada zaidi yako wewe, hakuna aliyewahi kunifuta machozi pale nilipokuwa nikilia kwa uchungu nikihitaji msaada zaidi yako wewe na kibaya zaidi hakuna hata aliyewahi kusikia kilio changu zaidi yako wewe.

Kwa muda mrefu nimekuwa nikipiga makelele ya kuomba msaada lakini sauti yangu imekuwa ikiishia mwituni, hakuna anayejali, na sasa nimeamua, ngoja niondoke labda watafurahi,maana wataishi kwa amani.Naamini hata kushindwa kwangu kuendelea na kidato cha tano ilichangiwa zaidi na matatizo ya kifamilia niliyokuwa nayo ambayo unayafahamu.

Dada yangu na rafiki yangu mpendwa tangu tulipoachana, mara baada ya kumaliza kidato cha nne na wewe kupangiwa kuendelea na kidato cha tano mkoani Morogoro, uliniacha na upweke mkubwa nisijue pa kukimbilia ili kupata faraja, kwani mateso yalizidi mno hapa nyumbani nilishindwa kujua mustakabali wa maisha yangu ya baadae na hakuna aliyeonesha kujali.

Nakushukuru sana kwa misaada uliyonipa wewe binafsi na ile niliyowahi kupewa na wazazi wako, naomba ufikishe shukrani zangu kwao, na waambie kwamba nawapenda sana.Naomba usinililie, na amini kuwa naondoka hapa duniani nikiwa nakupenda sana, na kwangu mimi utaendelea kubaki ndugu na rafiki yangu mpendwa.Nakutakia maisha mema hapa duniani na baki salama.

Ni mimi rafiki yako, ndugu yako na mdogo wako

Zinduna.(Sio jina lake halisi)

Jana tarehe 24/01/2009, imetimia miaka mitatu tangu rafiki yangu huyu roho yake iachane na mwili, baada ya kuamau kukatisha maisha yake. Alikuwa bado ni binti mbichi ambapo ndio kwanza alikuwa ametimiza miaka 20, lakini kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa mama yake wa kambo akishirikiana na baba yake mzazi aliamua kukatisha maisha yake.

Kwangu mimi huu ulikuwa ni msiba mkubwa kwani alikuwa ni zaidi ya rafiki.

Nakumbuka ndio nilikuwa nimerudi Dar es salaam, nikitokea Morogoro kuja kufanikisha mipango ya kuhamia katika shule moja ya binafsi iliyoko hapa jijini Dar es salaam.Siku mbili kabla ya rafiki yangu huyu kuutoa uhai wake, kama bahati nilikutana nae Kariakoo, lakini akiwa anaonekana kuwa mnyonge na asiye na furaha, alikuwa amefuatana na binti mmoja ambaye alinitambulisha kuwa ni mdogo wake.

Alinivuta pembeni na kuniambia kuwa ni bora tumeonana kwani anayo mazungumzo marefu na mimi hivyo alitaka kujua ratiba yangu ili aje nyumbani tuongee.Nilimwalika aje nyumbani siku mbili baadae yaani Jumanne ya tarehe 24/01/2006, ambayo ndio nitakuwa na nafasi ili tuongee, lakini kwa bahati mbaya siku hiyo nilikwenda Morogoro kupeleka fomu fulani kule shuleni nilikokuwa nasoma na ilikuwa nirudi siku hiyo hiyo.

Hivyo ilipofika siku hiyo kabla sijaondoka kuelekea Ubungo kupanda basi kuelekea Morogoro niliacha maagizo kwa mama kuwa rafiki yangu huyo akija anisubiri.Ni kweli alifika pale nyumbani majira ya saa nne asubuni hivi na baada ya kuambiwa nimeenda Morogoro, alikosa raha, hata hivyo mama alimshauri anisubiri kwa kuwa nitarudi siku hiyo hiyo. Kwa mujibu wa maelezo ya mama yangu, alikuwa akiuliza mara kwa mara kama nitarudi saa ngapi, mpaka mama yangu akawa na wasiwasi, ikabidi amuulize kama ana shida kubwa na mimi, ndipo akamjibu mama yangu kuwa amekuja kuaga kwani anasafiri kwa hivyo ameona ni vyema aje kuniaga mimi rafiki yake.

Mama yangu akamthibitishia kwamba ningerudi mapema,siku hiyo hiyo.Mpaka kufikia saa nane mchana nilikuwa bado sijarudi, akaomba apewe karatasi na kalamu ili aniachie ujumbe. Alipoletewa ndipo akaniachia huo ujumbe niliouandika hapo juu.Nakumbuka nilirudi Dar es salaam majira ya saa kumi na mbili jioni kwani siki hiyo usafiri wa kutoka huko Shuleni nilikokuwa nikisoma mpaka Morogoro mjini ulikuwa ni mgumu kidogo.

Nilipofika nyumbani mama alinipa ile barua aliyoacha rafiki yangu, na nilipoifungua na kuisoma sikuamini kile kilichoandikwa katika ile barua, nilishitukia napiga yowe kubwa, hadi mama akashituka.Niliongozana na mama hadi Temeke Mikoroshini alipokuwa akiishi huyo rafiki yangu, tulifika pale majira ya saa mbili usiku, na tulikuta umati mkubwa wa watu. Ni kweli rafiki yangu amekufa! Nilishikwa na butwaa.

Basi hivyo ndivyo alivyojitoa uhai rafiki yangu huyo. Msiba huo ulibaki kuwa kumbukumbu katika maisha yangu, kwa binti mdogo kiasi kile kujitoa uhai mapema namna ile.Kwa kifupi,nilifahamiana na Zinduna nilipojiunga na kidato cha kwanza, baada ya kufaulu darasa la saba.Tulitokea kuwa marafiki na nilimpeleka nyumbani na kumtambulisha kwa wazazi wangu, na kutokana nna kuniamini ndipo akanisimulia madhila aliyokuwa nayo.

Mama yake alifariki akiwa na umri wa miaka mitano na inasemekana mama yake alifariki kutokan na Depression (Naomba wataalamu munisaidia kutafsiri neno hili kwa Kiswahili) baada kuwa ameteswa sana na mumewe yaani baba yake.

Mara baada ya mama yake kufariki, baba yake akaoa mke mwingine ambaye inasemekana kuwa ndiye aliyekuwa akimzuzua baba mpaka kufikia kumtesa mama yake. Huyo mama yake wa kambo alikuwa akimtesa sana kwani aligeuzwa kuwa mtumishi wa ndani pale nyumbani kwao na baba yake hakuonekana kujali sana kwani kwa kushirikiana na baba yake walikuwa wakimtesa na kumsimanga kuwa atakuwa Malaya kama mama yake, kitu ambacho si kweli, kwani hakuwahi kuwa na uhusiano na wanaume kama walivyokuwa wakimtuhumu.

Pamoja na mateso yote hayo lakini alijibidisha na masomo hadi akafaulu na kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule ya serikali, kitu ambacho hakikumfurahisha mama yake wa kambo.Kuanzia hapo mateso yalizidi na baba yake kama kawaida hakuonekana kujali.

Nakumbuka nilimsaidia sana katika kumfariji na kumpa moyo na hata pale baba yake alipokataa kumpa pesa za matumizi ya shule na mahitaji mengine, mama yangu alimpatia, hiyo ni baada ya kuwa nimemsimulia mama yangu juu ya mateso anayopata rafiki yangu huyo.

Hata nilipokuwa nikienda kwao kumtembelea mama yake hakuonekana kufurahia na muda mwingi alionekana kufoka foka bila sababu ya msingi.Kuna wakati mama yangu alimshauri ahamie kwetu ili kuepukajna na mateso yale lakini alikataa kata kata kwa madai kuwa baba yake atamuua.Habari za huyu binti ni ndefu sana na nikisema nisimulie nadhani nitawachosha.Hata hivyo bado ninayo maswali mengi sana juu ya lile tukio.

Hivi kama ningewahi kurudi si labda ningeweza kuokoa maisha ya rafiki yangu huyu?

Au kuchelewa kwangu kulikuwa ni kusudi maalum ili hilo tukio la rafiki yangu kujiua litokee?

Apumzike kwa amani na mwanga wa milele umwangazie.....................Aaaamen.

Habari hii itaendelea wiki ijayo......

Thursday, January 22, 2009

MUONGOZO WA WENYE NCHI UNAPOTUPWA KAPUNI.............

Leo naona nigeukie siasa kidogo, Jana wakati napekua pekua katika maktaba ya baba ili niweze kupata mada ya kuweka humu, basi nikakutana na kijitabu kidogo cha rangi ya kijani.
Kitabu hicho kimeandikwa “MWONGOZO WA CCM” ambacho kilichapwa mwaka 1981, na Printpak.

Wakati nakipitisha macho nikavutiwa sana na vifungu vilivyoandikwa ukurasa wa 77 na wa 80. Naomba ninukuu maneno hayo hapa chini.

Ukurasa wa 77.

(6)WIZI WA MALI YA UMMA , HUJUMA ZA KIUCHUMI, MAGENDO NA UJAMBAZI.

Kumekuwa na ongezeko kubwa la uhalifu wa aina mbalimbali nchini tangu tupate uhuru. Uhalifu wenye kutia wasiwasi maalum ni uhalifu wa kiuchumi. Wizi wa mali ya umma umeanza kuwa ni jambo la kawaida. Kumekuwa na matukio ya baadhi ya maafisa kuhusika na kuidhinisha mikataba na makampuni ya nchi za nje bila kujali maslahi ya Taifa. Wakati huo huo vipusa, dhahabu na mali mbali mbali a Taifa zinatoroshwa nje ya nchi kwa magendo na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa.

Ujambazi wa kutumia silaha nao umetumika ili kunyang’anya mali na kutisha wananchi.
Chama kitahakikisha kuwa Serikali inachukuwa hatua kali za kupambana na vitendo hivi vinavyodhoofisha uchumi wa Taifa. Iko haja pia kwa sasa ya kubuni sheria maalum zitakazoelekezwa kwenye vita dhidi ya uhalifu wa kiuchumi unaozidi kuongezeka”

Mwisho wa kunukuu kipengele hicho.

Halafu ukurasa wa 80, nao ulikuwa na maneno haya:

92. watu wameanza kuthamini zaidi vitu kuliko utu na tamaa ya kujipatia mali bila kuitolea jasho inaenea, matukio ya wizi wa mali ya umma yameongezeka. Lakini lililo baya zaidi ni kuwa mwizi wa aina hiyo anapogunduliwa, baadhi ya wananchi, badala ya kumfichua au kulaani kitendo chake, humsifu na kumhusudu. Wakati mwingine mvivu na mtegaji kazini hutetewa hata na vyombo vya chama vyenyewe. Wakati huo huo bado kuna mabaki ya tabia ya kupuuza elimu ya shule kwa watoto na badala yake kuna wazazi wanaopendelea watoto wao wachunge mifugo au hata kuolewa badala ya kuendelea na shule...........na blah blah blah blah blah nyingine zinaendelea..............................

Wasomaji wangu wapendwa mjumbe huwa hauwawi.

Mimi nimesoma tu nikaona ni vyema nikashirikisha wasomaji wangu kutafakari huo muongozo wa CCM, ulioandikwa hapo mnamo mwaka 1981, miaka minne kabla sijazaliwa.

Je mnayo maoni gani juu ya huo muongozo ulioandikwa na wenye nchi?

Naomba kuwasilisha.

Wednesday, January 21, 2009

KWA NINI NILIAMUA KUIITA BLOG YANGU, VUKANI?

Neno VUKANI nimelitohowa kutoka katika lugha ya mama yangu ya kipare.
Neno hili lina maana ya AMKENI, nadhani kaka Mkodo Kitururu atakuwa anafahamu vizuri kwa kuwa ni lugha yake.

Nakumbuka wakati fulani nilikwenda likizo kijijini huko upareni kuwasalimia bibi na babu yangu wanaomzaa mama yangu, basi kila siku asubuhi bibi alikuwa na kawaida ya kutuamsha ili tusali pamoja na alikuwa akitumia neno Vukani.

Nilipouliza maana yake nikaambiwa ni Amkeni au kwa msisitizo wa kiingereza WAKE UP.
Basi kuanzia siku hiyo nikatokea kulipenda sana hili neno, sijui ni kwa nini lakini lilikuwa linanihamasisha sana kuamka kifikra badala ya kuamka asubuhi tu.

Wakati nilipokuwa nafungua Blog yangu nilikuwa tayari nimeshachagua jina hili, na cha kushangaza nilipoliingiza kwenye mtandao nikagundua kwamba neno hili linatumiwa na makabila mawili ya Ki Zulu na Ki-Xhosa ya nchini Afrika ya Kusini, likiwa na maana moja, yaani Amkeni.

Si hivyo tu bali pia lipo gazeti moja maarufu nchini humo, linaloitwa Vukani.

Kwa maelezo zaidi bofya hapa.

Amkeni nionavyo mimi sio kuamka kutoka usingizini tu bali ni kuamka kifikra na kuhoji kila tulichofundishwa au kuambiwa kama kina ukweli kiasi gani?
Si hivyo tu bali pia ni kuamka na kuachana na ile tabia ya kufikiri kwa mazoea na kutenda kwa mazoea.
Kila jambo unalolifanya ujue sababu ya kufanya hivyo, sio eti kwa sababu, mama, baba, bibi, babu, mjomba, shangazi, na jamii iliwahi kufanya hivyo.

Nakumbuka wakati fulani nilihudhuria semina ya mambo ya uongozi, basi yule mwezeshaji kutoka nchini Marekani alitutolea mfano mmoja wakati alipokuwa akitufundisha namna ya kuepuka kufanya mambo kwa mazoea.

Kisa chenyewe ni hiki:

Kulikuwa na mama mmoja alikuwa na tabia, kila akitaka kuoka samaki ni lazima amkate mkia kabla ya kumuweka kwenye kikaango, ndio amuweke kwenye oven. Hata kama samaki mwenyewe ni mdogo.
Siku moja binti yake aliyekuwa na umri wa miaka 10 akamuuliza mama yake sababu ya kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka, mama yake akamjibu kuwa mama yake alikuwa na kawaida ya kufanya hivyo.
Alipomuuliza kama aliwahi kumuuliza mama yake sababu ya kufanya hivyo, mama yake akajibu kwamba hakuwahi kuuliza.

Basi wakati fulani bibi yake alipokwenda kuwatembelea, kama bahati mama yake alikuwa akiandaa samaki ili amuoke kama ilivyo kawaida akamkata mkia,
binti akaona huo ndio wakti muafaka wa kuujua ukweli maada bibi yupo. Ndipo akamuuliza sababu ya mama yake kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka.

Si mnaona watoto wa wenzetu walivyo wadadisi?

Bibi akamwambia akamuulize mama yake sababu ya kufanya hivyo, yule binti akamjibu bibi yake kwamba, mama yake alimwambia kuwa yeye yaani bibi, ndiye aliyemfundisha kukata mkia wa samakai kabla ya kumuoka.

Yule bibi akafikiria kidogo, kisha akamjibu, kwamba alikuwa akikata mkia wa samaki kwa sababu kikaango chake kilikuwa ni kidogo, hivyo ili samaki aweze kuenea kwenye kikaango alikuwa analazimika kukata mkia.

Yule binti akamwambia bibi yake, “Mbona sisi kikaango chetu ni kikubwa na isitoshe tunavyo vikaango vingi tu vya saizi tofauti tofauti, je kuna ulazima gani mama aendelee kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka?

Bibi akamjibu kwamba hakuna ulazima wowote.
Basi kuanzia siku hiyo yule mama akawa hakati tena mkia wa samaki.

Si mnaona jinsi mtoto huyu alivyokataa kulishwa kitu bila ya kijua sababu?
Naamini kwamba wote mtakubaliana na mimi kwamba sisi tumelelewa hivi, tunaambiwa tukate mikia ya samaki kabla ya kuwaoka na tunafuata, na wala hatuulizi sababu.

Kwa hiyo ninaposema VUKANI ninamaanisha AMKENI, ili muweze kuhoji baadhi ya mambo tunayofundishwa au kuambiwa ambayo hayana mantiki.



Tuesday, January 20, 2009

JE MSOMI HASA NI NANI?: MJADALA ULIOZUA UTATA MKUBWA.


Wakati nilipoanzisha huu mjadala sikujua kwamba unaweza kuwafikirisha wanazuoni kiasi hiki.

Maana hata mimi nilifika mahali nikajikuta nataka kuutelekeza msimamo wangu na kushika msimamo mwingine, kutokana na jinsi wasomaji walivyoweza kujenga hoja na kuzitetea kwa utaalamu wa hali ya juu.

Shukrani za pekee ziwandee, Kaka Evarist, Kaka Bwaya, Kaka Markus Mpangala, Kaka Mubelwa Bandio Mzee wa changamoto, Kaka Kamala Lutanisibwa, Kaka Kaluse Mzee wa Utambuzi, Kaka Mkodo Kitururu, Kaka Fadhy Mtanga, Kaka Egidio, bila kumsahau mwanablog mpya Mzee wa KISIMA, na wengineo wengi ambao walipitia blog hii na kusoma huu mjadala, na kwa njia moja ama nyingine uliweza kuwafikirisha japokuwa hawakupata fursa ya kutoa maoani yao. Pia wapo wale walionitumia email binafsi na kunipa maoni yao na chanagamoto zao, wote naheshimu maoni yenu na michango yenu iliyojaa uelewa mkubwa kabisa.

Naomba nikiri kwamba katika mijadala ambayo niliwahi kuiweka humu huu ndio uliosisimua zaidi, nadhani ni kwa sababu uligusa eneo ambalo ni nyeti sana yaani elimu.

Naomba leo nishereheshe mada hii, ili niweze kuweka wazi kile ninachokifahamu, kwa sababu wakati nawasilisha mada hii nilikuwa nimeiweka katika hali ya kuuliza swali, na nilikuwa nahitaji majibu.

Nashukuru kwamba majibu yalikuwa ni mengi na ya kutosha, lakini hayanifanyi nifunge mjadala, kwa sababu mjadala huu ni endelevu.

Kuna watu wengi miongoni mwetu ambao wanadai kwamba wamesoma sana, kwa hiyo wamejipa sifa ya usomi kama wanavyoamini wenyewe.

Lakini ukichunguza watu hawa wanaojiita wasomi wameshindwa hata kuleta mabadiliko katika maeneo yao ya kazi, wameshindwa kubuni na kuleta mabadiliko katika sekta wanazofanyia.

Kaka Evarist anadai nisiwahukumu wasomi.
Naomba nimnukuu:

Na kuhusu vigezo gani vinavyoweza kufanya mtu aitwe msomi,nadhani pia majibu yanaweza kutofautiana kati ya walio ndani ya fani flani na walio nje ya fani hiyo. Pia naomba nitofautiane kidogo nawe dada yangu katika hoja yako kwamba msomi lazima awe amebuni kitu.Nadhani usomi na ubunifu ni vitu viwili tofauti japo inatarajiwa msomi awe mbunifu ingawa si lazima awe mbunifu.Lakini pia kama unapozungumzia ubunifu unamaanisha kuja na kanuni (theory) mpya,then kuna mahala flani kitaaluma ni lazima uje na aidha theory mpya au uifanyie maboresho kwa iliyopo

Mwisho wa kunukuu.

Hapa mimi napata wasiwasi, Hivi kweli tunaweza kutofautisha usomi na ubunifu?
Sasa kama Msomi hawezi kubuni, Je thamani yake iko wapi?
Hivi BAKITA wako wapi, watuondolee huu utata.
Kaka Evarist, hatugombani, lakini naomba utafakari upya kauli yako. Binafsi siogopi kutofautiana bali nahitaji hoja yenye mashiko, ili niweze kukubaliana na wewe. La sivyo, kaka hapa tutakesha.

Naomba nikiri kwamba wengi wetu tunajua dhana na sio ukweli, kwani tumesoma dhana kwa miaka mingi na hatujagundua kwamba kujua ni zaidi ya kuwa na dhana, bali ni kuwa na uwezo wa kubuni na kuleta mabadiliko na hata wale waliokuzunguka wakiri hilo.

Hivi kwa nini hatushangai, kwamba tunao wataalamu wengi katika sekta za kilimo, mifugo, nishati na kila kitu lakini pamoja na rasilimali tulizobarikiwa hapa nchini, bado tumebaki kuwa masikini wa kutupwa. Wasomi hawa hawana ubunifu hata kidogo.

Kudai kujua kile ambacho hunacho kimaisha, ni kujua tu dhana ya kitu hicho, wala sio kitu chenyewe. Unaweza kujua dhana kuhusu uzalishaji bora wa mali lakini wewe mwenyewe ukawa sio mzalishaji bora.

Kujua kitu ni kukifanyia kazi, kwa maana ya kwamba kama wewe ni mtaalamu wa uzalishaji bora, basi tuone huo uzalishaji bora kupitia kwako.

Kwa mfano tunalalamika kwamba nchi hii haina watalamu wa tiba, lakini ukienda pale wizara ya afya unakutana na wataalamu wa tiba wengi tu wa kutosha ambao wamegeuka kuwa watumishi wa maofisini, na huku wagonjwa wakikosa tiba.
Watu wamekimbia taaluma zao.

Wasomi wetu siku hizi wameamua kukimbilia kwenye siasa, maana huko ndiko kwenye tija.
Na hata wakipewa nafasi za kuongoza hawatengenezi mipango endelevu, bali huangalia zaidi kipindi watakachoongoza tu, kwa hiyo mipango ya maendeleo inazingatia kati ya miaka mitano au kumi.

Nadhani wakati umefika sasa wa jamii yetu kubadilika, kama tunataka dhana ya msomi ibebe maana iliyokusudiwa.

Inabidi tukague mfumo wetu wa elimu kama unamsaidia mwanafunzi kutumia elimu hiyo kubuni, kujiajiri na kumudu kubadili hali, iwe yake binafsi au ya wale waliomzunguka.

Lakini kama tutaendelea kukumbatia mfumo wa elimu tulionao unaomfundisha mwanafunzi kwamba kuna ajira baada ya kumaliza masomo yake, hiyo sio elimu.

Wengi wetu katika jamii hii ni wasomi wasio na tija hata kidogo, kwani tumekariri nadharia nyingi za marehemu wengu sana, ambazo zimetupa lundo la makaratasi yanayoitwa digrii.

Lakini ukweli wenye kuumiza ni kwamba hatujaelimika na wala hatuna maarifa.

Naomba kutoa hoja.


Sunday, January 18, 2009

MADA YA MSOMI HASA NI NANI? MAONI YA MARKUS MPANGALA

Wasomaji wangu wapendwa toka jana nilikuwa shamba na kule hakuna mtandao kabisa, ndio nimerejea na kukutana na maoni ya wasomaji wangu wapendwa, wakiendelea kutoa changamoto zao.
Miongoni mwa maoni niliyosoma, nimevutiwa sana na maoni ya kaka Markus Mpangala, naomba kwa ruksa yenu niyaweke hapa barazani bila kuhariri chochote.

Jamani kila nikitaka kuweka mada nyingine nakutana na changamoto zinazonivuta niendelee na hii mada, kaka Markus kauliza swali, nitamjibu.

Jumanne siku ambayo Rais mteule wa Marekani Bwana Barrack Obama ataapishwa nitaweka msimamo wangu juu ya hii mada, lakini sitaifunga.

Ujumbe maalum kwa mwana blog mpya KISIMA: Kaka juzi nilikutembelea nikataka kutoa maoni yangu lakini blog yako sijui umeiset vipi pale tunapoweka maoni, maana nimeandika maoni yangu nikashindwa kupost, naomba msaada tafadhali.

Sasa naomba musome haya maoni ya kaka Markus Mpangala hapa chini:

********************************************************************************************************************************************************
Hakuna matata mmepakua sana, sina nyongeza ngeni. Lakini mfano Jenerali Ulimwengu anahimiza kuhusu usomi wa wananchi katika mazingira yao, ni sawa na kile akisemacho Jean Jacques Rousseau kwamba kusoma ama kupata elimu lazima kuendane na mazingira. Kwanu naamini kwamba iwapo mtu akimaliza darasa la saba halafu akawa na ujuzi ambao nchi yake imetengenezea mazingira ya kuwa mjuzi zaidi wa kile akijuacho basi ataitwa msomi kwani tayari yupo katika utaalam/fani fulani. (soma UJAMAA NI IMANI cha J.K NYERERE). swali linabaki


USOMI ni nini hasa? hata kama mtu atakuwa kama kaka Everist na kupakua ujuzi ughaibuni, je dhana ya VX ni usomi au tafsiri juu ya mwonekano wa kisaikolojia kwamba aendeshaye hayo ni msomi? Huyu msomi ni yupi hasa? Ikiwa dhana ya usomi inaendana na kukaa darasani kisha ukaongeza ujuzi, vipi wale wasioingia darasani halafu wakawa na upeo mkubwa kuliko wasomi ambayo hutumia upeo wa wale wasioingia darasani? Sacrotes au?

Utakuta dhana hii ndiyo asemayo Nelson Mandela nataka kutambulika kama Mandela na siyo mtu aliyesoma na kujaza maktaba ya vitabu ambavyo vinamfanya aelewe kile anachokielewa bila kuwaelewesha wengine. Lakini swali hicho anachokielewa ni nini? Sawa twaweza kusema ni ujuzi wake wa fani fulani.

Mfano wapo wasomi wa masuala ya umeme lakini tuna mafundi wangapi wasiopita darasani kuongeza upeo? Je iwapo kutumia taaluma vibaya haina faida kwa jamii? kuna nadharia za faida ya uhalifu ya CRIMENOLOGY(nimesahau waandishi wake ila wapo wawili). Wao wanasema uhalifu ni jambo zuri sana kwani linaleta jamii yote pamoja na kushirikiana. Iwapo uhalifu unatokea katika jamii, kila kundi linatoa suluhisho kuhusu kukomesha uhalifu hata kama jamii hizo zinatofautiana ktk madaraka. Sasa mimi nauliza hivi, umewahi kusikia kitu kinaitwa WADAU? je hao ni nani? na ikiwa wasomi wanafanya utafiti wa jambo fulani, halafu wanawauliza wasio wasomi kupata mawazo yao na ufahamu wao kuhusu jambo wanalolichunguza. Mbona tunakuta kuna mambo wasomi hawayajui kabisa na wameyapata toka kwa wasiosoma.

Je msomi ni nani? katika uhai wake Sacrotes aliwahi kuwasha kurunzi(kama sijakosea) mchana na kuvinjari sokoni. walimcheka lakini akasema chekeni kuna watu wapo gizani ingawa mwaiona nuru. Je huyu alikuwa msomi kiasi gani wakati darasa halikufikia uzamili? Tunapotumia muda kublogu, wakati huohuo tunajuzwa kuna mtoto wa miaka kumi nchi afrika kusini anablogu; habari tamu hii, je utaalam wetu nao ni usomi?

Usomi ni ujuzi wa kitu fulani? sasa msomi huyu ni yupi? aliyekaa darasani na kuongeza ujuzi yule aliyebuni kitu bila kukaa darasani? Bado najifunza sijui msomi ni nani, ikiwa wasomi wenyewe wamekabidhiwa nchi kuongoza lakini wamekuwa vipofu waonao? Je hakuna anayejua kwamba tuna makatibu wa wizara wasomi halafu wanaingia mikataba ambayo asiyesoma kama Markus anahoji uelewa wa wasomi?

Je tutaendelea kupiga ramli kwamba msomi anayetegemewa kujaribu kuondoa umasikini lazima awe mjuzi wa kuandika mipango ya kuombea ngawira ughaibuni? Au msomi kama Profesa Ali Mazrui? Kumbe usomi hauna ubongo wala akili ya ziada bali ni kama nomino ya dhahani tu. Basi tukabli maneno ya kocha Jose Mourinho kwamba ukishindwa au kutojua jambo fulani basi jichukie.

Iweje wewe msomi mwenye Uporofesaaaaaa halafu utengenezewe simu na asiyesomea utengenezaji wa simu yenyewe, lakini unaamini ni mtaalam? Je utaalam na usomi ni tofauti?Koero swali hilo hapo: UTAALAMU WA JAMBO/FANI na USOMI ni tofauti? Je yule unayempelekea kutengeneza gari/baiskeli/simu n.k ni msomi kiasi gani? alikaa darasani?

Haya napumzika na wimbo wa miondoko ya KWAITO wake MANDOZA uitwao 'MYEKE BABA' unahusu usitumia nguvu kumpata mlimbwende panga hoja zenye mwitiko

January 17, 2009 10:55 AM

Thursday, January 15, 2009

MAONI YA WADAU JUU YA MADA YA "JE MSOMI HASA NI NANI?"


Leo nimepokea pendekezo kutoka kwa Kaka Mubelwa Bandio kwamba ikiwezekana maoni haya ya wadau wa blog hii niyaweke hapa barazani kwa sababu yamefikia kiwango cha kuwa kama vile ni uchambuzi juu ya mada yangu hiyo.

Naheshimu sana maoni na uchambuzi mbalimbali kutoka kwa wasomaji wangu, kwa kuwa wao ndio wanaonipa ari na mwamko wa kuketi katika kompyuta yangu na kuandika yale yanayowafikirisha.

Kwa hiyo kwa kuheshima ya Kaka Bandio nimeona ni vyema niyaweke maoni haya hapa barazani ili wasomaji wengine ambao hawakupata nafasi ya kusoma au kuchangia watoe mtazamo wao, maana nimeshauriwa na kaka Bwaya nisifunge huu mjadala.


kamala J Lutatinisibwa said...

tehe, tehe, tehe....

Msomi ni yare majamaa yanaoweza kuongea kiswahili kwa kuchanganya na kiingereza mbale ya watu ambao hawajasoma ili ionekane inavyojua kiingereza lakini isifikishe ujumbe husika ;-cheka-;hata mimi najiuliza msomi ni nani na kwa nini nisome zaidi ili iweje?

Nchi kama bongo inaongozwa na wasomi lukuki kama akina JK, MWinyi mkapa nk. ahaaa Labda msomi ni yule mwenye gari zuri na anayekaa ofisi ya kyoyozi na jumba lakifahali!??okey msomi na kama jenerali Ulimwengu yule jamaa anayeandika makala nzuri za kuwalalamiki viongozi ambao anajua hawawezi kubadilika badala ya kuelimisha jamii ili ijitambue na kujua nafasi yake (am very sory kutaja mtu kwa jina)

Lakini huo ndio ukweli kwamba kazi zake nzuri zinamfanya aonekane alivyokuwa na uelewa mpana lakini hauleti mabadiliko yoyote kwa walengwa zaidi ya kumsifia yeye) sio ulimwengu tu na wengine.na labda msomi ni yule jamaa anayekula na kunenepesha tumbo akiamini yuko fiti wakati ni ujinga mtupu.

msomi ni prof. mkandara anayewafukuza wanafuzi wote ili chuo kibaki chenyewe bila kujali ghrama.msomi ni wahubiri wanaotuhubilia vitu visivyoingia akilini na wasivyoweza kuvitenda wao. msomi ni yule jamaa anayemnyooshea mwenzie kidole na kumtusi ilia aachie nafasi na yeye ale.

Mimi namkubali msomi kama vile Bwaya, Kaluse, Kitururu, Koero nk. wanaotumia mida yao kublogu kwa kiswahili fasaha ili waeleweke, na wanaoheshimu uhuru wa maoni na labda watafungua tovuti na kuanzisha gazeti ili hoja zao ziwafikie wengi zaidi.

Namkubali marehemu Munga Tehenan kwa kutafuta elimu ya utambuzi kwa gharama kubwa na baada ya kujitambua akutugeia elimu hiyo bure na sisi tukaelimika bali kujali madarasa yetu.nimechoka kutaipu bwana ahaaa

January 9, 2009 11:48 AM

Mzee wa Changamoto said...

Kwenye Blog yangu kuna gadget ya PARADOX OF OUR TIME na naipenda saana licha ya kuwa nayo kwa miaka sasa, na baadhi ya sehemu zinasema

".We have more Degrees but less common sense; more knowledge but less judgment..We have more experts but more problems; more medicine but less wellness....We’ve learned how to make living, but not a life; we’ve added years to life not life to years..We have taller buildings, but shorter tempers; wider freeways but narrower viewpoint. .We’ve been all the way to the moon and back, but have trouble crossing the street to meet our neighbor..We’ve conquer outer space, but not inner space.These are the time for Fast food and slow digestion; tall men and short characters..More leisure but less fun; more kinds of food but less nutrition; two income but many divorces, fancier houses but broken homes.

Msomi wa sasa si kama yule ambaye hakuwa na "compass' lakini akaongoza mtumbwi toka Zanzibar mpaka Arabuni. Si yule ambaye angejua nyota ile ina maana gani na itamfikisha wapi na si yule aliyejua kuwa ukichoma majani haya na haya ukapata jivu litakusaidia kuua wadudu waharibuo mazao yako.

Wa sasa ni yule ambaye anaweza kurejea na kuremba kila ambacho alifundishwa kisha kukijengea hoja na ushawishi mnono wenye KUTAMANISHA hata kama hautekelezeki.Msomi ni nani? Nami nauliza maana hapa kuna mtazamo tofauti kulingana na tuonavyo Tatizo. Na mara zote NAMNA TUONAVYO TATIZO NDILO TATIZO

January 9, 2009 1:30 PM

Markus Mpangala said...

Msomi? Msomi?aisee labda ni mimi na wewe Koero! pengine sababu tunaweza kuandika bloguni? sijui pengine usomi anaosema Kalama wale jamaa wasiojua kiswahili wala kiingereza. Pengine kuamua kuwa mimi ni msomi tokana na kujua kwangu kusoma maandiko ya Kilatini! sijui labda kwakuwa mungu hakusema mimi ni msomi. Inawezekana kabisa nikawa msomi lakini sijitambui kama msomi sababu usomi ni swali gumu.

Naacha nimeshindwa vibaya sana, msomi ni yule aombaye pesa ughaibuni, yule fundi wa kuandika project za kuomba pesa kwa wafadhili au yule mpambe wa msomi ambaye anamsifia mwenzake msomi. heee usomi mbona hauna ubongo wa pekee? mbona wote tuna medulla oblangata,ubongo wa kati na mbele? usomi upo wapi? unarangi gani? usomi labda kujua kuongeza na nguruwe pori toka ulaya na marekani, wenye rangi zilizochubuliwa na makatambuga ya jua kali au baridi.LABDA msomi ni yule ajuaye UJINGA siyo usomi au yule ajuaye kwamba usomi siyo ujinga. LAKINI mbona kuna wajinga wasomi wasomao mpaka shahada za uzamili halafu wote wanasoma mistari ileile ya msomi aliyepita?

JIBU msomi ni yule atakaye anza kujitambua kama OSHO alivyowachapa bakora wanafunzi wake walipomwuliza watu wakiwauliza wao ni nani wajibu vipi! Lakini umewahi kusikia kuhusu FREEMASONS AU MASONIC, ndiyo maana dunia yote tunaweza kuwaza jambo moja ambalo wamepanga liwazwe, labda tujiulize Google Translator ni nini maana webmaster wote wanajua kiendeleacho ulimwenguni, wanajua ujinga wa wasomi. LAKINI msomi ni nani?Swali gumu naacha nimeshindwa, nangojea wengine wa utambuzi

January 9, 2009 1:37 PM

EVARIST said...

Kwa mtizamo wangu,nadhani pengine mtu HAJIITI msomi bali HUITWA msomi,na wanaomuita hivyo wana sababu zao za msingi (mara nyingi ni wana fani wenzie).Jamii ina uhuru wa kukubaliana na kikundi hicho cha wana fani au kukipuuza.Uluteni,kwa mfano, una mantiki zaidi jeshini kuliko uraiani ambako sanasana wanaofahamu kidogo watasema ni cheo cha nyota mbili.Lakini kijeshi uluteni ni zaidi ya hayo "mawe mawili",kuna uongozi wa moja ya vikundi vya kivita (platuni,kama sijakosea),nk.

Nadhani pia vyeti sio lazima vimaanishe usomi.Lakini again,wanaofahamu zaidi ni wale waliotunuku vyeti hivyo.Jumuiya ya wahadhiri inapoafikiana na kumteua mmoja wao kuwa profesa,kwa mfano,ina mantiki zaidi katika mazingira yao kuliko nje ya ulingo huo.Jinsi ya uprofesa huo utavyotumika ni suala jingine,na jamii ina uhuru wa kuuponda au kuuenzi uprofesa huo.

Na kuhusu vigezo gani vinavyoweza kufanya mtu aitwe msomi,nadhani pia majibu yanaweza kutofautiana kati ya walio ndani ya fani flani na walio nje ya fani hiyo.Pia naomba nitofautiane kidogo nawe dada yangu katika hoja yako kwamba msomi lazima awe amebuni kitu.Nadhani usomi na ubunifu ni vitu viwili tofauti japo inatarajiwa msomi awe mbunifu ingawa si lazima awe mbunifu.Lakini pia kama unapozungumzia ubunifu unamaanisha kuja na kanuni (theory) mpya,then kuna mahala flani kitaaluma ni lazima uje na aidha theory mpya au uifanyie maboresho kwa iliyopo.

Nje ya uwanja wa kitaaluma,huo unaweza usiitwe ubunifu lakini ndani ya ulingo huo,huo nao ni ubunifu.Pia naomba kutoafikiana nae kwamba kile unachokuja nacho wakati unaingia chuo kikuu kinaondolewa na KUWEKEWA UNACHOTAKIWA KUAMINI...Nani anayekutaka kuamini?Labda kwa wenzetu wa sayansi ambao nyakati nyingine X ni lazima iwe X,lakini mara nyingi (japo si mara zote)huko kwenye "ungwini" ni namna mwanafunzi anavyoweza kucheza na hoja zake.

Iwapo kuna mahala mwanafunzi analazimishwa kutetea hoja isiyo yake pasipo kuhoji basi hapo kuna kasoro.Kuhusu kukutana (naomba kukunukuu)"watu wengi ambao nawafahamu, ambao wamekariri sana elimu ya darasani, wanayo madigrii lakini ukizungumza nao, utafikiri umekutana na mtu ambaye hajawahi kutia mguu darasani hata siku moja" hudhani kwamba tatizo linaweza kuwa mnahukumiana ndivyo sivyo?

Yawezekana wao wanaamini mnaelewana katika mnachoongea lakini kumbe sivyo.Hudhani pia kwamba unaweza kuwa huwatendei haki kwa "kujipa mamlaka" (samahani kwa neno hilo) ya kuwahukumu?Au haiwezekani kwamba kwa vile hoja zao hazikuendana na matarajio yako ndio maana ukazihukumu kuwa ni kama za mtaani?

Mwisho,nadhani "makaratasi" (kwa maana ya vyeti) yataendelea kubaki na umuhimu wake hususan miongoni mwa wanafani husika.Kuwepo kwa vyeti feki hakuwezi kuondoa umuhimu wa vyeti halali just like kuwepo kwa noti feki kusivyoweza kuondoa umuhimu wa noti halisi.Jamii hailazimishwi kuthamini au kupuuza vyeti hivyo.

Elimu itaendelea kupatikana mtaani,madarasani,kwenye karakana,semina,nk...ni kutoka katika mazingira hayo ndio wahusika watampachika mwenzao/wenzao joho la usomi,umahiri,ujuzi,ubobeaji,ujanja,nk.Watakaotuzwa joho hilo nao hawawezi kuilazimisha jamii iwathamini/iwakubali,bali matokeo ya kazi zao yanaweza kufanya hivyo.

January 9, 2009 9:18 PM

Koero Mkundi said...

Wadau naomba nisifunge huu mjadala, maana naona changamoto ya kaka Evarist imenitoa jasho.
Lakini siamini kama nimepata majibu sahihi kulingana na hoja yangu ya kutaka kujua kwamba msomi hasa ni mtu wa namna gani?

Nadhani mada hii ni pana sana, na inahitaji tafakuri kubwa. Sikuandika mada hii ili kubeza elimu au kuwabeza wasomi wetu hapa nchini, bali nikuwa najaribu kuangalia jambo hili katika mkabala tofauti, kwa hiyo kutofautiana kimawazo ndio njia sahihi ya kujifunza na kuyajua mambo kwa upana wake.

Bado niko kwenye utafiti, na nikirejea chuoni nitaendelea na utafiti huu, halafu nitaweka majibu yangu humu. Bado nakaribisha maoni zaidi kutoka kwa wadau mbali mbali.Ahsanteni sana.

January 10, 2009 9:11 AM

Bwaya said...

Sikuwa ulingoni kwa siku kadhaa hivi. Nimependa utaratibu wa kibaraza hiki wa kutokulifunga 'jalada' kwa faida ya wasomaji ambao, kwa sababu moja ama nyingine, tunakutana na hoja ikiwa kabatini.Kuhusu usomi.

Nadhani hatuwezi kuwa na majibu yanayofanana. Pengine hata namna tunavyoutazama usomi wenyewe inatofautiana baina ya fani na fani, mtu na mtu, na kadhani.Hata hivyo nionavyo mimi, ni kwamba kinachofanyika madarasani si kutufanya tuwe wasomi. Kumbi za mihadhara, maktaba na vyumba vya maabara vinatupanua ufahamu. Kutufanya tupate mitazamo ya watu wengine waliotutangulia.

Kutujulisha maarifa yaliyopo. Huu kwangu si usomi.Tukifikia mahala pa kuweza kuyatumia maarifa hayo ili kujua namna ya kutatua changamoto zinazotukabili sisi wenyewe pamoja na jamii kwa ujumla, hapo tunaweza kuwa wasomi.Kwa mipaka ya tafsiri yangu, msomi ni mtu yoyote, bila kujali idadi ya madarasa aliyokanyaga, awezaye kuyatumia maarifa yake kuzikabili changamoto za maisha kiufanisi. Alikoyatoa maarifa haya si jambo la msingi.

Daktari wa SUA aliyechaifua kila aina ya kitabu cha kilimo, lakini asiweze kutusaidia kuyakabili matatizo ya kilimo nchini, kwa kisingizio kwamba eti alivyonavyo kichwani havishabihiani na changamoto za kilimo chetu, huyu si msomi. Ni sawa kompyuta isiyoweza kuzitambua data zenye format tofauti.Nani mpimaji wa usomi wa mtu? Nadhanijamii katika upana wake.

Watu wa kawaida kabisa, hao ndio wenye vigezo vya kweli vya usomi. Sababu ni kwamba utumiwaji wa maarifa hutafsirika katika maisha ya watu. Watu wa kawaida wanaangalia namna elimu ya watu inavyowaletea unafuu wa changamoto za maisha yao.Sikubaliani na utaratibu wa genge la mabwanyenye wa madarasa yetu wanaoiamulia jamii nani yu msomi na yupi siye.

Kwa sababu ni wazi kwamba 'wasomi' hawa ni mabingwa wa kurudufu maarifa ya wenzao ambayo kwa bahati mbaya hayaleti yoyote katika jamii. Profesa anaweza kujua vitu vingi sana katika fani husika, na ndivyo ilivyo, lakini si lazima awe msomi hata kama anaheshimika na maprofesa wenzake wanaotumia vigezo vinavyoandikika. Kama mtu hawezi kutafsiri viandikwa vyake katika maisha ya kawaida kwa maana ya kuifaidia jamii, sidhani kama ana sifa za kuitwa msomi.

Profesa anayepika tafiti zake kwa manufaa ya mafisadi, je naye ni msomi? Profesa asiye na lugha inayoeleweka na watu wanaoitwa wa kawaida, anayejijengea ukuta kati yake na jamii yake inayemhitaji, naye ni msomi? Mashaka yangu ni haya. Ninawafahamu wanasayansi wengi waliokimbia umande, ama kushindwa mitihani, ambao maarifa yao yanaheshimika mpaka leo.

Je, hawa si wasomi hata kama hawana vyeti? Hawakuwahi kuitwa madokta wala maprofesa, lakini waliweza kuyatumia maarifa yao wenyewe ambayo wasomi wa enzi hizo hawakuwa nayo!Shule, nadhani, ingeleta maana kama utaratibu wa kupimana uelewa kwa mitihani ili kupeana vyeti hautauawa.Albert Einstein, mwanafizikia mashuhuri aliwahi kusema, '...elimu ni kile kinachobaki, baada ya kusahau vyote ulivyofundishwa madarasani...'. Msomaji amue hekima ya maneno haya.

January 12, 2009 6:04 PM

Koero Mkundi said...

Binafsi nilishtushwa na ukimya wako kaka Bwaya, nikajiuliza kulikoni? Unajua nimesoma maoni ya wachangiaji wangu wote, ukabaki wewe tu. Ahsante sana kwa mtazamo wako na ahsante sana kwa kunitembelea.

Bado nasubiri maoni ya wasomaji wengine........

January 12, 2009 6:18 PM

Bwaya said...

Asante sana Koero. Haraka mtandaoni, kwa hofu ya kuishiwa muda hutufanya tuandike kwa mcharazo.

Naomba nihariri:...shule, nadhani ingeleta maana kama utaratibu wa kupimana uelewa kwa kutumia mitihani kwa minajili ya kupeana vyeti, ungeuawa...'

January 12, 2009 6:25 PM

Koero Mkundi said...

Nilikuelewa.Hata hivyo ahsante kwa ufafanuzi ili wasomaji wengine wasije potea.

January 12, 2009 6:32 PM

EVARIST said...

Naomba kuchangia tena.Nadhani kuna tofauti ya maana ya kitu na namna kitu hicho kinavyopaswa kuwa.

Daktari wa SUA aliebukua na kupata udaktari ni msomi.Jamii ipende isipende,ili kuwa na ujuzi alofikia muungwana huyo lazima hatua flani zipitiwe,ikiwa ni pamoja na kuingia darasani,kutoa mihadhara,nk.Hizo ni taratibu za kuingia daraja la usomi.

Usomi wa Msomi usipoweza kuisaidia jamii,au kutokuwa na manufaa kwa jamii,inapelekea kushuka thamani kwa usomi huo,lakini hakuondoi usomi.Kitakachotengua usomi wa mhusika ni kukiuka kanuni na taratibu za fani husika,na sio flani anapenda au flani hapendi.Ikumbukwe,walomwingiza katika daraja hilo sio jamii bali WASOMI wenzie.Wanaweza kuwa mabwanyenye wanaofikiria maslahi yao binafsi,lakini huo ndio ukweli mchungu wa maisha.

Kwa mfano, Tuna viongozi wabovu,lakini kwa vile wamechaguliwa (wakati mwingine kwa kununua kura) wanaendelea kuitwa viongozi.Je wabunge wasiowakilisha VEMA wananchi wao hatuendelei kuwaita WABUNGE?Nadhani kisifa (adjective) USOMI inatokana na kitenzi (verb) SOMA au KUSOMA.Kwa mantiki hiyo,USOMI unahusiana na KUSOMA,na nomino MSOMI ni MTU ALIESOMA.Wakati mwingine maneno ya kiswahili yanaleta maana flani yanapoelekwa kwenye lugha nyingine.

Kwenye Swahili-english dictionary,ukisaka maana ya neno MSOMI kwa Kiingereza inakupa majibu yafuatayo:
msomi , pl wasomi { English: intellectual }noun msomi , pl wasomi { English: learned person , pl learned people }noun msomi , pl wasomi { English: lecturer , pl lecturers } [derived: soma V]noun msomi , pl wasomi { English: reader } [derived: soma V]noun ,msomi , pl wasomi { English: scholar , pl scholars } [derived: Swahili -soma]noun 5 distinct results returned (chanzo:THE KAMUSI PROJECT)

Kwa mtizamo wangu unaoweza kuwa sio sahihi,nadhani kuna umuhimu wa kutofautisha MATARAJIO YA JAMII KWA "WASOMI" na MAANA YA NENO "MSOMI".Bwaya anahoji iwapo Profesa anayepika tafiti zake kwa manufaa ya mafisadi, je naye ni msomi?Yes,ni MSOMI,lakini ANAYEKIUKA KANUNI,TARATIBU NA SHERIA ZINAZOONGOZA FANI YAKE.

Kuna baadhi ya sifa ambazo mtu akishafanikiwa kuzipata hubaki nazo kwa muda mrefu kama sio milele. Ni mithili ya ualimu,jina linaendelea kubaki MWALIMU hata pale mtu anapostaafu au kufukuzwa kazi. Naomba kunukuu hoja nzito ya Bwaya kwamba "....Ninawafahamu wanasayansi wengi waliokimbia umande, ama kushindwa mitihani, ambao maarifa yao yanaheshimika mpaka leo. Je, hawa si wasomi hata kama hawana vyeti?

Hawakuwahi kuitwa madokta wala maprofesa, lakini waliweza kuyatumia maarifa yao wenyewe ambayo wasomi wa enzi hizo hawakuwa nayo!" Binafsi,nadhani mwanzoni mwa mjadala niligusia juu ya umuhimu wa vyeti KAMA KITAMBULISHO lakini haimaanishi kwamba kutokuwa na cheti kunamuondolea mtu umahiri wake katika fani husika.

Pia ili mtu aitwe msomi si lazima awe dokta au profesa LAKINI LAZIMA ASOME,iwe nyumbani,darasani au kwa njia ya posta au kujielimisha kwa elimu vitendo.HUWEZI KUWA MSOMI PASIPO KUSOMA.Utawezaje kuwa mwanasayansi kama hujasoma sayansi?Mwisho,wakati JAMII INATARAJIA wasomi wafanye vitu kwa manufaa kwa jamii,kutakuwa na wasomi watakaotimiza matarajio hayo,na kuna wengine ambao hawatatimiza.

Wote wataendelea kuitwa wasomi.Kitakachozidi au kupungua ni heshima yao kwa jamii na wanafani wenzao.Kinyume cha matarajio ya jamii kuhusu kinachotarajiwa kutoka kwa anayeitwa MSOMI hakibadili maana ya neno MSOMI...just like UONGOZI MBOVU usivyoweza kuondoa maana ya neno UONGOZI (bali kuathiri TASWIRA ya uongozi).Swali,je kuna neno MBADALA kwa mtu aliyesoma sana lakini kusoma huko hakuinufaishi jamii?

January 13, 2009 4:32 AM

Koero Mkundi said...

Leo nimeamka alfajiri majira ya saa kumi na moja na nusu hivi na kukutana na maoni ya kaka Evarist, ambayo yamenisisimua sana.
Labda nikuulize kaka Evarist,Je wale wanaotunukiwa digrii za heshima, nao tuwaiteje?

Je wanayo sifa ya kuitwa wasomi?

Je Jamii iwatambueje?

Kuhusu jina mbadala la msomi ambaye hana tija katika jamii labda tuwaulize watu wa BAKITA, nadhani hii ni changamoto kwao na kwa wadau wengine.

Lakini hata hivyo tukishindwa tunaweza kutohowa kutoka katika lugha nyingine kama wenzetu watakuwa walipambazukiwa mapema na kuwatenganisha watu wenye sifa hizi.

Je wadau wengine mnasemaje?

January 13, 2009 6:09 AM

Bwaya said...

Nimesoma kwa makini maoni ya kaka yangu Evarist. Nimevutiwa na mchango wake.Nisirudie alichosema mwongoza mjadala dada Koero. Pengine wakati tukiwasubiri BAKITA tuseme, aliyepita darasani tumwite msomaji, maana hana tofauti na msoma novo, hata kama yeye anaonekana kuchemsha ubongo zaidi.

Akiweza kutumia maarifa yake kwa tija aitwe msomi.Kwa kuzingatia mchango wa kaka yangu Evarist, naomba niulize: Hivi 'shule' zilianza -anzaje? Ni akina nani hasa walianzisha shule kama usomi hauwezekaniki bila shule? Maana yangu ni kwamba, ikiwa shule ndizo zinatengeneza wasomi, yaani haiwezekani kuwa msomi bila shule, na ikiwa pasipo shule hapana msomi, je shule hizi zilikujaje bila wasomi wasioenda shule?

Labda nisemee eneo la sayansi ninalolifahamu fahamu. Wanasayansi wengi walifanya tafiti zao kwa akili zao wenyewe bila kulazimika kufuata mwongozo wa yeyote. Inashangaza. Na si kwamba walisoma sana viandikwa na hivyo kupata ujanja wa kurekebisha nadharia zilizokuwepo. Hapana.

Walitumia vipaji vyao wenyewe kuisoma nature. Hawa hawakuwa wasoma makarabrasha tu (ya wenzao), bali walitumia muda mwingi kuzisoma hali fulani , kuzifanyia kazi na mwishowe walikuja na siri zinazojadilika. Na ndio maana chuo kikuu enzi hizo kilimaanisha eneo ambalo watu wenye 'siri' hukutana kwa mijadala.Ndio maana bado siamini kabisa kwamba kinachofanyika siku hizi si usanii maana kinaishia maili nyingi kabla ya usomi.

January 13, 2009 6:41 PM

Koero Mkundi said...

Haya tumsubiri kaka Evarist tumsikie atasemaje?

Nilijua mapema kabisa kwamba mada hii ni ya moto,na niliamua makusudi kuiandika ili kuwafikirisha wasomaji wangu.

Basi kuna rafiki yangu mmoja kanipigia simu leo na kunishutumu juu ya mada yangu hii, kwanza nilishangaa, maana najua kwamba hapendi kusoma blog,

Eti ananilaumu kuwa nawapoteza watu. Anasema, mimi nasoma chuo kikuu halafu nawaambia watu kuwa hakuna wasomi, au sitaki watu waerevuke?

Nikashikwa na mshangao, hivi kumbe watu wanasoma ili waerevuke?

Kwa hiyo wale wasiosoma hawajaerevuka!

Hiyo ilikuwa ni changamoto nyingine. Hata hivyo nilimshauri siku nyingine aweke maoni yake humu ili wasomaji wengine wasome mtazamo wake.

Sijafunga mjadala.

January 13, 2009 7:51 PM

EVARIST said...

Dada Koero,nadhani kabla ya kujibu kuhusu wanaotunukiwa shahada za heshima ni muhimu kufahamu kwanini wanapewa shahada za heshima.

Kwa uelewa wangu mdogo,shahada za heshima hutolewa na taasisi husika (mara nyingi ni za kitaaluma) kwa kutambua mchango wa mtunukiwa katika jambo fulani.Nadhani PhD ya heshima alopewa JK huko Kenya inatoa mfano mzuri.Uamuzi wa kuwaita wasomi au la hao walopewa honorary degree nadhani unategemea zaidi suala la taaluma.

Kuhusu jamii itawatambuaje,hilo linarudi tena kwenye hoja yangu ya msingi kwamba matarajio ya watoa shahada (eg chuo) na mpokea shahada (kwa upande mmoja) na jamii (kwa upande mwingine)yanaweza yasifanane.Ndugu yangu Bwaya,naomba nifafanue tena kwamba kwa mtazamo wangu (unaoweza kuwa sahihi) usomi unaendana na kusoma.

Shule ni moja tu ya mahala pa kupata fursa ya kusoma.Kuhusu shule zilianzaje,binafsi sina jibu kwa vile sijawahi kusoma historia ya shule.Lakini lililo dhahiri ni kwamba anayekwenda shule hawezi kufundishwa na mwenzie ambaye nae hajui kitu.Ni dhahiri kuwa shule ni miongoni mwa vyanzo vya wasomi. Bwaya,nadhani huwatendei haki wasomi kwa kuwaita wasomaji japo naheshimu mtizamo wako.

Nadhani msomaji ni yule ambaye halazimiki sana kuingia ndani zaidi ya anachokisoma,kutengeneza hoja za kuunga mkono au kupinga au kutahiniwa (eg kusoma gazeti,kwa mfano).Kuhusu "usanii" wa kazi nyingi za wasomi kuihsia kwenye mafaili,nadhani wanaopaswa kulaumiwa zaidi sio wanataaluma bali wale wanaotakiwa kufanyia kazi mapendekezo ya kitaaluma.

Ikumbukwe,kazi nyingi za kisomi huishia tu kutoa mapendekezo na ni juu ya watengeneza sera kuamua kufuata mapendekezo hayo au kuyapuuza. Usomi sio udikteta kwamba kwa vile nimetafiti kitu flani na kuthibitisha kwa findings zangu basi lazima kikubalike.Dada Koero, nadhani kilichomshangaza huyo mwanafunzi mwenzio ni nini basi kimewapeleka chuoni...maana kwa tafsiri ya mtaani ukiwa mwanafunzi unaitwa msomi(naomba nisijifanye nafahamu mawazo yake,ni hisia tu).

Nimalizie kwa kusema kuwa binafsi naendelea kuamini kuwa ili mtu awe msomi ni lazima asome.Kuhusu asome wapi,hilo ni swala jingine.Asome nini,inaweza kuwa elimu nadharia au elimu vitendo.Kiasi gani cha elimu kinastahili kumfanya mtu aitwe msomi,nadhani suala si cheti au idadi ya digrii bali content ya kile kinachompa sifa ya usomi.

January 13, 2009 10:59 PM

Koero Mkundi said...

Haya kaka Bwaya, umeona hoja nzito hiyo kutoka kwa kaka Evarist?

Labda niweke wazi kwamba, mimi sikwenda chuoni, ili niwe msomi, kwa sababu siamini kabisa kwamba kwenda kwangu chuoni kutanifanya niwe msomi.

Kwangu mimi namuona msomi ni yule aliyejitambua, na jamiii ikamkubali.watu kama Gautama Sidharata, Osho, Mama Theresa, Lenin, Dalai Lama na wengine wanaofanana na hao, naweza nikawaita kuwa ni wasomi kwa sababu walijitambua na kutumia vipaji vyao kwa manufaa ya watu wengine.

Tunapokuwa chuo kikuu tunafundishwa kuhusu utandawazi, ujamaa, ubepari, na nadharia nyingine chungu mzima halafu tunaambiwa tuchague nadharia yoyote ile kati ya hizo ili tuitee, hatuambiwi tutafute nadharia zetu na kuzitetea,la hasha.

Nadhani sisi tumefungwa na tafsiri kuliko uhalisia. Kwenda chuo kikuu hakumfanyi mtu kuwa na sifa ya kuwa msomi, bali kuondoa kile alichokuwa nacho na kupewa kingine.

Kaka Evarist kumbuka kwamba kila mtu kazaliwa akiwa na kipaji chake, kinachotakiwa ni njia sahihi ya kumuwezesha mtu kukuza kipaji chake na kufikia malengo yake.Lakini hilo halipo.Na ndio maana siku hizi watu wanakimbilia kusomea taaluma zenye masilahi, kinachoangaliwa ni mshiko sio kipaji alicho nacho mtu.

Utakuta mtu anakwambia "Wewe unasomea Sayansi ya jamii, itakusaidia nini? Si bora ungesomea sheria, udaktari au uhasibu"Kwa nini? Kwa sababu taaluma hizo zina mshiko, na ndio zenye maslahi.Mimi naona hapa ndipo dhana ya usomi inapoingia mushkeli, labda tutafute neno jingine mbadala. Naomba Nikiri kwamba, nakubaliana na Kaka Bwaya kwa mtazamo wake.kama kuna mwenye mtazamo tofauti atuwekee hapa.

January 14, 2009 6:31 AM

Bwaya said...

Ndio.

Wakati tunawasubiri wasomaji wengine, naomba nirudi tena. Ninukuu maneno ya Evarest aliposema "...Kuhusu 'usanii' wa kazi nyingi za wasomi kuishia kwenye mafaili,nadhani wanaopaswa kulaumiwa zaidi sio wanataaluma bali wale wanaotakiwa kufanyia kazi mapendekezo ya kitaaluma...

"Hapa ningependa kuuliza.

Hivi kazi ya msomi ni ipi? Kupendekeza ama kufanyia kazi kile alichonacho? Kwa nini asubiri wengine kumfanyia kazi mapendekezo yake? Kama kweli anakiamini alichonacho, na kama ni kweli hafanyi usanii wa kitaaluma, kwa nini asichukue hatua yeye mwenyewe?

Kwa sababu, nionavyo mimi ni kwamba wasomi wa ukwelii, pamoja na kukubalika kwenye jumuiya zao za kitaaluma, wanajipenyeza katika jamii kuuza mawazo yao kwa namna yoyote iliyo halali!Mfano rahisi.

Evarest mwenyewe. Ni watu wachache wa namna yake, wamethubutu kujadiliana na watu wa kawaida kama sisi. Evarest amekuwa akitumia maarifa yake ya sayansi ya siasa, kutuchambulia mambo tusiyoyajua. Ametumia muda wake mwingi kuandika kwenye magezeti kadhaa, hata kama mara nyingine ameibua mambo yanayowakwaza hao anaotuambia wanapaswa kutekeleza mapendekezo ya wasomi.

Lakini hajasita kutoa mchango wake kwa jamii yake. Hakusubiri watu wengine watumie maarifa yake kufanya utekelezaji. Sasa kwangu, huo ndio usomi. Matumizi ya elimu.Hata kama inakuwa kama siwatendei haki, ni kweli kwamba hao wengine ni wasomaji.

Kwa sababu hata kwenye magazeti, msomaji makini ni yule ambaye huingia ndani zaidi ya anachokisoma,kutengeneza hoja za kuunga mkono au kupinga hata kama hatahiniwi. Ikumbukwe kutahiniwa si sifa ya msingi sana ya elimu. Kutahiniwa ni kama vile mtahini anasema najua hutasoma bila mtihani, ngoja nikupe mtihani ili usome. Kwa hiyo kwa mfano wa msoma gazeti, mimi naona ikiwa anaweza kusoma bila shuruti (wakati akijua kabisa hana mtihani) maana yake huyo ni msomi kuliko yule mwingine wa darasani amabye akiwa na hakika hakuna mtihani hawezi kusoma asilani.

Ushahidi wa wazi. Wanafunzi wengi wa Vyuo Vikuu wakishapewa makaratasi yao, hawakumbuki tena kama kuna kitu kinaitwa kusoma. Kumbe hawa jamaa walikuwa wanasoma sana kwa sababu gani? Kwa kuhitimisha, nitumie maneno ya Evarest kwamba "shule ni moja tu ya mahala pa kupata fursa ya kusoma".

Ni kweli. Maana sikusema kwamba wanaoenda shule hawawezi kuwa wasomi, ila nilihoji pia kwamba upo uwezekano wa mtu kuwa msomi bila shule na kwamba kwenda shule peke yake hakutoshi kumfanya mtu awe msomi. Kwa hiyo hapo nadhani tumekubaliana na Evarest kimsingi. Usomi na shule vinahusiana, ila pia vinaweza kuwa vitu viwili tofauti.

January 14, 2009 1:12 PM

Mzee wa Changamoto said...

Sasa natamani maoni yangekuwa yanaandikwa "barazani" maana naona huu ni zaidi ya uchambuzi. Nawashukuruni saaaaana saaana

January 15, 2009 5:14 AM

JE MSOMI HASA NI NANI?

Hivi karibuni nilikuwa na mjadala mzito na baba yangu kuhusiana na dhana nzima ya mtu kujiita kuwa ni msomi.Chanzo cha mjadala huo ilikuwa ni pale aliponitaka niachane na biashara niliyoianzisha ili niendelee na elimu ya juu, kwani hapendi kuwa na mtoto ambaye sio msomi.

Basi hapo ndipo nilipoanzisha mjadala wa kutaka kujua kwamba msomi ni mtu wa namna gani? Au je mtu anaweza kupimwa kwa vigezo gani ili aitwe kuwa ni msomi?Mjadala huo ulikuwa ni mzito na uliochangamsha pale nyumbani kwani kila mtu alipata nafasi ya kuchangia kwa mtazamo wake, na kutokana na mjadala huo nimejifunza mambo mengi sana kuhusiana na hii dhana ya mtu kuitwa kuwa ni msomi.

Hebu niwaulize wasomaji na wanablog wenzangu, hivi msomi ni nani?Kama mtu amesomea taaluma fulani labda tuseme, udaktari, uhandisi au udaktari wa falsafa, Je huyu anaweza kujiita kuwa ni msomi?Nimeuliza hivyo kwa sababu kama mtu ni msomi kwa maana ya dhana ya usomi tunayoifahamu, basi atakuwa anajua kile alichofundishwa na kukaririshwa tu akiwa darasani, lakini yeye mwenyewe hajawahi kuwa na kitu chochote kipya alichobuni.Kama ni hivyo basi sioni kama kuna mtu anayeweza kujivuna kuwa yeye ni msomi.Atajiitaje kuwa ni msomi wakati amekaririshwa nadharia za wengine pasipo kubuni kitu chake mwenyewe?

Nadhani hiyo inatosha kuvunja dhana ya watu kujiita wasomi.Hivi ni nini tofauti kati ya msomi na yule ambaye hakuwahi kuingia darasani hata siku moja?Kwangu mimi tofauti iliyopo labda ni kwamba, mmoja ametembea sana kutoka nyumbani hadi darasani na mwingine hajawahi kufanya hivyo hata siku moja.Huyu aliyetembea sana kwenda darasani kutafua elimu, amevuliwa akili yake na kupewa akili ambayo ni nadharia za watu wengine, zikiwemo zile sahihi na zisizofaa hata kuzitazama. Lakini amezikubali hizo nadharia na hivyo anaitwa kuwa ni msomi.

Kwa mfano ukienda chuo kikuu unafundishwa hata namna ya kulitazama jambo na kulihukumu kwa kutumia akili za watu wengine. Kile ulichokuja nacho, yaani imani na ufahamu wako kuhusu maisha, uchumi na siasa vinaondolewa na kuwekewa ambacho unatakiwa ukiamini na kukitetea kwa nguvu zako zote bila kuhoji, na hiyo itakufanya uitwe labda daktari wa falsafa na kutunukiwa digrii yako ya tatu, na kuanzia hapo utaitwa msomi!Kumbuka kwamba digrii ni karatasi zaidi kuliko maarifa, ndio maana dunia nzima inasumbuliwa na wimbi la digrii feki.

Ninachojua mimi ni kwamba wasomi wengi wa vyuo vikuu na madigrii yao ni wajinga sana kwenye maeneo mengine ya maisha.Na jambo lingine ambalo linanishangaza, ni dunia hii kuendelea kukumbatia karatasi kama kipimo cha usomi. Unaweza kukuta mtu hajui chochote, lakini kwa sababu ana makaratasi yake yanayosema amesomea Shahada ya Uchumi, basi atapewa nafasi kubwa. Kisa ni karatasi!Halafu baadae mnashangaa, kwa sababu hana anachozalisha.

Sasa usomi ni kitu gani, ni karatasi, ni kukariri nadharia za watu wengine, ni kujua jambo kwa undani au ni kujiuliza na kutafuta jibu?Kuna watu wengi ambao nawafahamu, ambao wamekariri sana elimu ya darasani, wanayo madigrii lakini ukizungumza nao, utafikiri umekutana na mtu ambaye hajawahi kutia mguu darasani hata siku moja. Na wangine wako mitaani hawana kitu,na wamekata tamaa na maisha, kisa hakuna ajira.Kwa kuamini kwamba karatasi ndizo zinazomfanya mtu kuwa msomi ndio maana sisi vijana wengi huko mashuleni na vyuoni tunajitahidi kushindana kukariri ili tufaulu sana na kupata digrii za viwango vya juu.

Tunachotaka ni karatasi ili tupate ajira na wala sio maarifa. Tunapomaliza masomo tunatoka kama tulivyoingia na pengine tukiwa tumechuja zaidi kiufahamu.Nimewahi kujiuliza swali hili, hivi watu kama Arstotle Sophocles, na wale wajuvi wa kwanza kwanza duniani, walifundishwa na nani, walikaa darasa lipi na kupewa vyeti gani?Hawa hawakukaa darasani, bali walizalisha maarifa baada ya tafakari kubwa na ya muda mrefu. Walijiuliza maswali ili kupata majibu, waweze kuisaidia jamii hapa duniani.

Kwa mtazamo wangu hawa ndio wasomi, kwa sababu utafiti wao unagusa kila eneo la maarifa bila kujali kama ni sayansi, biashara, tiba au sanaa.Msomi ni mtu aliye huru kutafuta maswali kuhusu maisha yetu ya kila siku katika nyanja tofautu tofauti na kuyapatia majibu.Msomi hatembei na takwimu za watu, bali anatafuta zake na kwa njia zake. Msomi ni mtu aliyekomaa, sio kasuku aliyekariri nadharia lukuki za wengine ambazo hajawahi kuzifanyia kazi.Bado nauliza msomi hasa ni nani?

posted by Koero Mkundi at 7:55 AM on Jan 9, 2009

Tuesday, January 13, 2009

HAKUNA MAFISADI TANZANIA!!!!!!!

Sasa hivi neno Mafisadi limetamalaki katika midomo ya watanzania wengi, wakizungumzia ubadhirifu wa viongozi wetu waliowahi kushika madaraka makubwa au walioko madarakani.

Ni kweli kuna hali kama hiyo, lakini kwa kuangalia viongozi wa nchi duniani, hatuwezi kujifananisha na nchi za Asia, Latin Amerika au Ulaya, kwani nchi hizo nazo zimewahi kuwa na viongozi wabadhirifu, wala rushwa na mafisadi, huku Afrika ikiwa na viongozi wawili tu kati ya viongozi kumi waliotajwa.

Kwa kuangalia kiwango cha fedha ambazo viongozi wameiba au kuchukua kwa njia zisizo halali anayeongoza kwa fedha nyingi haramu ni aliyekuwa Rais wa Indonesia,
Suharto, ambaye aliiba kiasi cha dola za marekani kati ya Bilioni 15 mpaka 35.

Wa pili ni
Ferdinand Marcos wa Phillipines ambaye aliiba kiasi cha dola za Marekani kati ya Bilioni 5 hadi 10.

Mobutu Sese seko wa iliyokuwa Zaire ambayo sasa hivi inajulikana kama Congo DRC, huyu anashika nafasi ya tatu kwa viongozi wabadhirifu duniani.
Huyu alikomba kiasi cha dola za Marekani Bilioni 5.

Sani Abacha wa Nigeria naye alikomba kiasi cha dola za Marekani kati ya 2 hadi 5.

Slobodan Milosevic wa Serbia na Montenegro alijitwalia kiasi cha dola za Kiamrekani bilioni 1.

J C Duvalier wa Haiti alijichukulia dola za Marekani milioni 300 hadi 800.

Albert Fujimori wa Peru alikwiba dola za Marekani milioni 600. Pavlo Lazarenko alijichotea dola za Marekani kati ya milioni 114 hadi 200

Arnoldo Aleman wa Nicaragua alihamisha dola za Marekani milioni 100, na Joseph Estrada alichukuwa dola za Marekani kati ya milioni 78 hadi 80.

Kwa hiyo sio kweli kwamba Afrika ikiwemo Tanzania ndio tu inayonuka kwa ufisadi.

Je wadau mnasemaje?

Saturday, January 10, 2009

DINI ZINAPOTUMIKA KAMA KITEGA UCHUMI.......

Niliwahi kuandika makala nikizungumzia kuhusu kuzishitukia dini lakini nikapata changamoto kutoka kwa wazazi wangu.
Ilibidi nifunge mjadala ili nijipange upya kwani niligundua kwamba ile mada sikuiandika katika wakati muafaka.

Siku hizi kila kona ya hapa nchini kuna sauti nyingi zenye kumtaja Yesu, si kwa nia ya kumtukuza bali kwa kumkashifu na kumbeza.
Dini siku hizi zinatumika kama kitega uchumi, kama mwamvuli wa uovu, kama kimbilio la walioshindwa kujisaidia na kama kimbilio la waovu ambao wanataka kuonekana kama kondoo kwa ngozi wakati ni chui.

Imani ni nguvu na imani ni ukombozi, lakini ni utumwa na adhabu pia. Kila mtu mwenye imani kubwa juu ya kitu fulani ni lazima maisha yake kwa kiasi kikubwa yatafungwa na imani hiyo. Imani zetu ndizo zinazotufanya au kutuwezesha kuona kile tunachotaka maishani kinatutokea.

Imani zetu ndizo zinazotufanya kusali, kuomba kunyenyekea, kwa jina la mungu au chochote ambacho tunaamini kwamba ndicho kikubwa zaidi na kinachoratibu na kushikilia sehemu ya maisha ambayo sisi hatuna uwezo wa kuyadhibiti au kuyaratibu.

Kwa sababu hiyo kuna wenzetu ambao wamegeuza nguvu hiyo kuwa kifaa cha kujinufaisha wakati sisi tukiumia. Ni wengi hivi sasa ambao ni watumwa halisi wa hawa wachungaji na manabii. Kuna wachungaji na manabii wa uongo ambao hutumia nguvu za giza kufanikisha malengo yao.

Hali mbaya ya uchumi imewafanya wananchi walio wengi kugeukia dini kama suluhisho.
Kuna idadi kubwa kuliko wewe unavyojua ambayo huamini kwamba wanaweza kuondoa matatizo yao kupitia wachungaji.
Wanaamini pia kwamba matatizo yanayowakabili ni matokeo ya wachawi, mapepo au laana fulani.
Katika hali kama hiyo hawa wachungaji huwanasa kirahisi watu wenye imani za kishirikina kwanza halafu huwanasa wale wasiojua kwamba nao ni binadamu kama hao wachungaji. Hii ikiwa na maana kwamba nao wanaweza kujiombea na kujitafutia nafuu kwenye maisha.

Mawindo rahisi ya wachungaji na manabii matapeli ni wale watu wenye hofu, wasiojiamini, walio katika matatizo ambayo wameshindwa kuyapatia ufumbuzi, na wale ambao wanakabiliwa na hitilafu za kiakili, kama vile sononi, msongo, na fadhaa.

Kwa kuwa na hofu na shida zao wanakosa uwezo wa kujiuliza maswali na hivyo hutumika kama vitendea kazi vya wachungaji na manabii hawa ambao kati yao kuna wanotumia nguvu za giza kuwahujuma.

Mimi nimekulia katika dini ya Kikristo tena nilikuwa nasali katika dhehebu la wasabato, lakini siku hizi naomba nikiri wazi kwamba siendi tena kanisani.

Kwa nini?

Kwa sababu naamini kwamba naweza kuwa na imani yangu binafsi bila kuwa na dini na nikafika huko wanakopaita mbinguni.
Swala la msingi hapa ni uhusiano wangu na Mungu, je ni imara kiasi gani?
Kama uhusiano wangu na mungu ni imara, kwa maana ya kwamba namuamini na ninafanya yale yaliyo mema na sio lazima yawe ni yale yaliyoandikwa katika vitabu vya dini, basi hata dini haina maana kwangu.
Nasema haina maana kwangu kwa sababu siamini kwamba binadamu mwenzangu anaweza kuwa na uwezo wa kimungu na anaweza kubadili maisha yangu.

Huwezi kuamini, kuna watu hawajiamini kabisa na wamekuwa dhalili kwa hawa wachungaji kiasi kwamba wanaamini kuwa hawawezi kubadili maisha yao wenyewe isipokuwa hawa wachungaji.

Kumbuka kwamba sisi tumeumbwa na mwenye enzi mungu kwa mfano wake, sio kwa sura bali kwa uwezo wake, kama yeye aliumba basi na sisi tunaweza kuumba, ni kiasi cha kutumia akili tu katika kufikiri kwatu. Kama ukiiweka rehani akili yako kwa mchungaji utaumba nini?
Kwa hiyo kama bado unategemea mchungaji akuamulie kuhusu maisha yako, basi ujue kwamba unayo matatizo makubwa ya kiakili na labda unahitajika upelekwe Mirembe kwenye hospitali ya wendawazimu.

Kama unawashangaa na kuwacheka wale wanaoamini waganga na uchawi basi ujue kwamba huna tofauti nao, kwa hiyo huna sababu ya kuwacheka.

Siku hizi kuna wachungaji hewa wanoibuka kila uchao na mazingaombwe yao, mtu anajifunza viini macho na uchawi halafu anaingia nao katika nyumba ya ibada na kuuonesha halafu anaita ni muujiza wa mwenye enzi mungu! Ama kweli wajinga ndio waliwao.

Kuibuka na kuongezeka kwa wachungaji hawa matapeli, inaonesha ni kwa kiasi gani watu wasiotaka kutumia akili zao wanavyoongezeka hapa duniani.
Ukweli ambao haukanushiki ni kwamba miujiza mingi inayofanywa na hawa wanojiita wachungaji au manabii iwe ni kwenye nyumba za ibada au hata huko mitaani ni miongoni mwa nguvu ambazo binadamu anazo au amejifunza na kufuzu kuwa nazo.
Wanaodanganywa na miujiza hii ni wale ambao bado wako kwenye giza la ujinga.

Hivi kweli tunahitaji miujiza ili tuweze kuomba na kusikilizwa na mungu?
Binafsi sidhani kama tunahitaji hiyo miujiza ili maombi yetu yasikilizwe na mungu, kwani miujiza haina maana yoyote kwa mungu.
Kama swala ni miujiza mbona hata shetani alifanya na anendelea kufanya miujiza.
Kwangu mimi miujiza ni mbinu inayotumiwa na watu hawa ili kunasa akili zetu, ili tuwaamini na tusionae uovu wao.

Kuongezeka kwa umasikini, kukata tamaa, watu kutojua malengo yao katika maisha, migogoro ya ndoa na familia, na kadhalika, ndio chimbuko la kuongezeka kwa wachungaji hawa na manabii matapeli, kwani hayo ndiyo mawindo rahisi kwao.

Binafsi naamini kwamba mchungaji, kiongozi wa dini au nabii ni yule anayemsaidia muumini au mwanaadamu kujua malengo yake ya kuwepo hapa duniani, kumsaidia muumini kuondoka katika hofu, na kuwaonesha namna bora ya kutenda mambo mema katika maisha, na hawawafungi na kuwafanya waone kwamba bila wao, yaani wachungaji, basi maisha yao hapa duniani hayana maana.
Kwa bahati mbaya viongozi wa dini wa aina hii ni adimu sana kupatikana.

Wachungaji na viongozi wa dini hatari wa kuogopwa ni wale ambao wanatumia nguvu ambazo sio za mungu bali za giza,
Kundi hili ni kubwa na linatawala katika nyumba za ibada, na linazaa viongozi na waumini kwa kasi ya ajabu.
Utakuta nyumba ya ibada inaanzishwa leo kesho imefurika waumini wengi mpaka unajiuliza watu hawa wamelishwa nini?

Na cha kushangaza miongoni mwa waumini hao, wapo wanaopoteza kazi, wanaopoteza ndoa zao, na wanaopoteza uwezo wa kufikiri na hatimaye wanakuwa mandondocha wasio na akili

Kumbuka kwamba wewe unaweza kusali na mungu akakusikia, unachotakiwa kufanya ni kuomba mungu na kuamini kwamba yupo na maombi yako yatakubaliwa, huhitaji kiongozi wa dini akusemee au akuombee kwa mungu kwani yeye ni binaadamu tu kama ulivyo wewe.


Friday, January 9, 2009

HIVI MSOMI HASA NI NANI?

Hivi karibuni nilikuwa na mjadala mzito na baba yangu kuhusiana na dhana nzima ya mtu kujiita kuwa ni msomi.Chanzo cha mjadala huo ilikuwa ni pale aliponitaka niachane na biashara niliyoianzisha ili niendelee na elimu ya juu, kwani hapendi kuwa na mtoto ambaye sio msomi. Basi hapo ndipo nilipoanzisha mjadala wa kutaka kujua kwamba msomi ni mtu wa namna gani? Au je mtu anaweza kupimwa kwa vigezo gani ili aitwe kuwa ni msomi?

Mjadala huo ulikuwa ni mzito na uliochangamsha pale nyumbani kwani kila mtu alipata nafasi ya kuchangia kwa mtazamo wake, na kutokana na mjadala huo nimejifunza mambo mengi sana kuhusiana na hii dhana ya mtu kuitwa kuwa ni msomi.

Hebu niwaulize wasomaji na wanablog wenzangu, hivi msomi ni nani?Kama mtu amesomea taaluma fulani labda tuseme, udaktari, uhandisi au udaktari wa falsafa, Je huyu anaweza kujiita kuwa ni msomi?

Nimeuliza hivyo kwa sababu kama mtu ni msomi kwa maana ya dhana ya usomi tunayoifahamu, basi atakuwa anajua kile alichofundishwa na kukaririshwa tu akiwa darasani, lakini yeye mwenyewe hajawahi kuwa na kitu chochote kipya alichobuni.

Kama ni hivyo basi sioni kama kuna mtu anayeweza kujivuna kuwa yeye ni msomi.Atajiitaje kuwa ni msomi wakati amekaririshwa nadharia za wengine pasipo kubuni kitu chake mwenyewe?Nadhani hiyo inatosha kuvunja dhana ya watu kujiita wasomi.

Hivi ni nini tofauti kati ya msomi na yule ambaye hakuwahi kuingia darasani hata siku moja?


Kwangu mimi tofauti iliyopo labda ni kwamba, mmoja ametembea sana kutoka nyumbani hadi darasani na mwingine hajawahi kufanya hivyo hata siku moja.Huyu aliyetembea sana kwenda darasani kutafua elimu, amevuliwa akili yake na kupewa akili ambayo ni nadharia za watu wengine, zikiwemo zile sahihi na zisizofaa hata kuzitazama. Lakini amezikubali hizo nadharia na hivyo anaitwa kuwa ni msomi.

Kwa mfano ukienda chuo kikuu unafundishwa hata namna ya kulitazama jambo na kulihukumu kwa kutumia akili za watu wengine. Kile ulichokuja nacho, yaani imani na ufahamu wako kuhusu maisha, uchumi na siasa vinaondolewa na kuwekewa ambacho unatakiwa ukiamini na kukitetea kwa nguvu zako zote bila kuhoji, na hiyo itakufanya uitwe labda daktari wa falsafa na kutunukiwa digrii yako ya tatu, na kuanzia hapo utaitwa msomi!


Kumbuka kwamba digrii ni karatasi zaidi kuliko maarifa, ndio maana dunia nzima inasumbuliwa na wimbi la digrii feki.Ninachojua mimi ni kwamba wasomi wengi wa vyuo vikuu na madigrii yao ni wajinga sana kwenye maeneo mengine ya maisha.

Na jambo lingine ambalo linanishangaza, ni dunia hii kuendelea kukumbatia karatasi kama kipimo cha usomi. Unaweza kukuta mtu hajui chochote, lakini kwa sababu ana makaratasi yake yanayosema amesomea Shahada ya Uchumi, basi atapewa nafasi kubwa. Kisa ni karatasi!Halafu baadae mnashangaa, kwa sababu hana anachozalisha.Sasa usomi ni kitu gani, ni karatasi, ni kukariri nadharia za watu wengine, ni kujua jambo kwa undani au ni kujiuliza na kutafuta jibu?

Kuna watu wengi ambao nawafahamu, ambao wamekariri sana elimu ya darasani, wanayo madigrii lakini ukizungumza nao, utafikiri umekutana na mtu ambaye hajawahi kutia mguu darasani hata siku moja. Na wangine wako mitaani hawana kitu,na wamekata tamaa na maisha, kisa hakuna ajira.

Kwa kuamini kwamba karatasi ndizo zinazomfanya mtu kuwa msomi ndio maana sisi vijana wengi huko mashuleni na vyuoni tunajitahidi kushindana kukariri ili tufaulu sana na kupata digrii za viwango vya juu.Tunachotaka ni karatasi ili tupate ajira na wala sio maarifa. Tunapomaliza masomo tunatoka kama tulivyoingia na pengine tukiwa tumechuja zaidi kiufahamu.

Nimewahi kujiuliza swali hili, hivi watu kama Arstotle Sophocles, na wale wajuvi wa kwanza kwanza duniani, walifundishwa na nani, walikaa darasa lipi na kupewa vyeti gani?
Hawa hawakukaa darasani, bali walizalisha maarifa baada ya tafakari kubwa na ya muda mrefu. Walijiuliza maswali ili kupata majibu, waweze kuisaidia jamii hapa duniani.

Kwa mtazamo wangu hawa ndio wasomi, kwa sababu utafiti wao unagusa kila eneo la maarifa bila kujali kama ni sayansi, biashara, tiba au sanaa.
Msomi ni mtu aliye huru kutafuta maswali kuhusu maisha yetu ya kila siku katika nyanja tofautu tofauti na kuyapatia majibu.Msomi hatembei na takwimu za watu, bali anatafuta zake na kwa njia zake. Msomi ni mtu aliyekomaa, sio kasuku aliyekariri nadharia lukuki za wengine ambazo hajawahi kuzifanyia kazi.

Bado nauliza msomi hasa ni nani?