Thursday, January 22, 2009

MUONGOZO WA WENYE NCHI UNAPOTUPWA KAPUNI.............

Leo naona nigeukie siasa kidogo, Jana wakati napekua pekua katika maktaba ya baba ili niweze kupata mada ya kuweka humu, basi nikakutana na kijitabu kidogo cha rangi ya kijani.
Kitabu hicho kimeandikwa “MWONGOZO WA CCM” ambacho kilichapwa mwaka 1981, na Printpak.

Wakati nakipitisha macho nikavutiwa sana na vifungu vilivyoandikwa ukurasa wa 77 na wa 80. Naomba ninukuu maneno hayo hapa chini.

Ukurasa wa 77.

(6)WIZI WA MALI YA UMMA , HUJUMA ZA KIUCHUMI, MAGENDO NA UJAMBAZI.

Kumekuwa na ongezeko kubwa la uhalifu wa aina mbalimbali nchini tangu tupate uhuru. Uhalifu wenye kutia wasiwasi maalum ni uhalifu wa kiuchumi. Wizi wa mali ya umma umeanza kuwa ni jambo la kawaida. Kumekuwa na matukio ya baadhi ya maafisa kuhusika na kuidhinisha mikataba na makampuni ya nchi za nje bila kujali maslahi ya Taifa. Wakati huo huo vipusa, dhahabu na mali mbali mbali a Taifa zinatoroshwa nje ya nchi kwa magendo na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa.

Ujambazi wa kutumia silaha nao umetumika ili kunyang’anya mali na kutisha wananchi.
Chama kitahakikisha kuwa Serikali inachukuwa hatua kali za kupambana na vitendo hivi vinavyodhoofisha uchumi wa Taifa. Iko haja pia kwa sasa ya kubuni sheria maalum zitakazoelekezwa kwenye vita dhidi ya uhalifu wa kiuchumi unaozidi kuongezeka”

Mwisho wa kunukuu kipengele hicho.

Halafu ukurasa wa 80, nao ulikuwa na maneno haya:

92. watu wameanza kuthamini zaidi vitu kuliko utu na tamaa ya kujipatia mali bila kuitolea jasho inaenea, matukio ya wizi wa mali ya umma yameongezeka. Lakini lililo baya zaidi ni kuwa mwizi wa aina hiyo anapogunduliwa, baadhi ya wananchi, badala ya kumfichua au kulaani kitendo chake, humsifu na kumhusudu. Wakati mwingine mvivu na mtegaji kazini hutetewa hata na vyombo vya chama vyenyewe. Wakati huo huo bado kuna mabaki ya tabia ya kupuuza elimu ya shule kwa watoto na badala yake kuna wazazi wanaopendelea watoto wao wachunge mifugo au hata kuolewa badala ya kuendelea na shule...........na blah blah blah blah blah nyingine zinaendelea..............................

Wasomaji wangu wapendwa mjumbe huwa hauwawi.

Mimi nimesoma tu nikaona ni vyema nikashirikisha wasomaji wangu kutafakari huo muongozo wa CCM, ulioandikwa hapo mnamo mwaka 1981, miaka minne kabla sijazaliwa.

Je mnayo maoni gani juu ya huo muongozo ulioandikwa na wenye nchi?

Naomba kuwasilisha.

6 comments:

Unknown said...

Dada yangu, sasa huu upekuzi wako utakupeleka pabaya.
Angalia yasije yakakukuta ya akina Kubenea.
Mi yangu macho.

Simon Kitururu said...

Aliyeandika vifungu kama yuko hai na anashuhudia maprofesa wa UFISADI siku hizi, sijui atasemaje!:-(

Jaduong Metty said...

Koero,

Nadhani hiyo miongozo ya chama ilitolewa kabla ya Azimio la Z'Bar ambalo lilitoa rhuksa kwa kila kitu...

Lakini yote yanaonesha jinsi ambavyo Bongo imeshamiri kwa nadharia...soma MKUKUTA uone.

Subi Nukta said...

Nchi ya Tanzania imejaliwa kuwa na watu wenye kufikiri na kuandika maneno mengi na mazuri sana tangu enzi na enzi, tatizo ninaloliona katika kufanikisha malengo yetu lipo katika utendaji na uaminifu. Kila mtu aseme na agize, je, nani atende na kutimiza?
Iko shida. Lipo fundo mahali fulani. Linatakiwa litoke. Viongozi watambue kuwa vitendo ni bora zaidi ya maneno, tunayo ya kutosha, tuanze kuyafanyia kazi basi hayo tuliyonayo. Nani wa kutuongoza vyema katika kuyatekeleza hayo?

Albert Kissima said...

Viongozi wetu tangu enzi na enzi wamekuwa waongeaji tu. Kwa dhana ile ile ya kusoma ili kupata nafasi nzuri katika maofisi ,ndio hiyo hiyo inayotumika hata katika uongozi,yaani mtu akishapata uongozi anajali maslahi yake binafsi na kutokufikiria hata siku moja ni kitu gani ataweza kukifanya kwa jamii na kuwaletea maendeleo.

Kuna watu wa aina tatu "wale wafanyao mambo" wale wanaoongelea kuhusu kufanya mambo na kuna wale wanaokuwa wataalam kwa kukaa chini tu na kufikiria kuwa mambo yatafanyika vipi.Kwa mazingira yetu wale wanaoongelea kuhusu kufanya mambo na wale wanaokuwa wataalamu kwa kukaa chini na kufikiria tu(si kutenda) ni kwa namna gani mambo yatafanyika ndio wengi kabisa.Hali ambazo si nzuri hasa katika mazingira ya kusoma.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

i avoid politics. mijadala yote yenye harufu ya kisiasa, mimi huwa najaribu kukaa mbali nayo. kwa sababu likija suala la siasa, wengi hutafuta wa kumlaumu na huyo alaumiwaye, humlaumu mwingine pia. napenda utambuzi, wenye suruhisho la kutifua chanzo cha tatizo badala ya matawi