Tuesday, January 20, 2009

JE MSOMI HASA NI NANI?: MJADALA ULIOZUA UTATA MKUBWA.


Wakati nilipoanzisha huu mjadala sikujua kwamba unaweza kuwafikirisha wanazuoni kiasi hiki.

Maana hata mimi nilifika mahali nikajikuta nataka kuutelekeza msimamo wangu na kushika msimamo mwingine, kutokana na jinsi wasomaji walivyoweza kujenga hoja na kuzitetea kwa utaalamu wa hali ya juu.

Shukrani za pekee ziwandee, Kaka Evarist, Kaka Bwaya, Kaka Markus Mpangala, Kaka Mubelwa Bandio Mzee wa changamoto, Kaka Kamala Lutanisibwa, Kaka Kaluse Mzee wa Utambuzi, Kaka Mkodo Kitururu, Kaka Fadhy Mtanga, Kaka Egidio, bila kumsahau mwanablog mpya Mzee wa KISIMA, na wengineo wengi ambao walipitia blog hii na kusoma huu mjadala, na kwa njia moja ama nyingine uliweza kuwafikirisha japokuwa hawakupata fursa ya kutoa maoani yao. Pia wapo wale walionitumia email binafsi na kunipa maoni yao na chanagamoto zao, wote naheshimu maoni yenu na michango yenu iliyojaa uelewa mkubwa kabisa.

Naomba nikiri kwamba katika mijadala ambayo niliwahi kuiweka humu huu ndio uliosisimua zaidi, nadhani ni kwa sababu uligusa eneo ambalo ni nyeti sana yaani elimu.

Naomba leo nishereheshe mada hii, ili niweze kuweka wazi kile ninachokifahamu, kwa sababu wakati nawasilisha mada hii nilikuwa nimeiweka katika hali ya kuuliza swali, na nilikuwa nahitaji majibu.

Nashukuru kwamba majibu yalikuwa ni mengi na ya kutosha, lakini hayanifanyi nifunge mjadala, kwa sababu mjadala huu ni endelevu.

Kuna watu wengi miongoni mwetu ambao wanadai kwamba wamesoma sana, kwa hiyo wamejipa sifa ya usomi kama wanavyoamini wenyewe.

Lakini ukichunguza watu hawa wanaojiita wasomi wameshindwa hata kuleta mabadiliko katika maeneo yao ya kazi, wameshindwa kubuni na kuleta mabadiliko katika sekta wanazofanyia.

Kaka Evarist anadai nisiwahukumu wasomi.
Naomba nimnukuu:

Na kuhusu vigezo gani vinavyoweza kufanya mtu aitwe msomi,nadhani pia majibu yanaweza kutofautiana kati ya walio ndani ya fani flani na walio nje ya fani hiyo. Pia naomba nitofautiane kidogo nawe dada yangu katika hoja yako kwamba msomi lazima awe amebuni kitu.Nadhani usomi na ubunifu ni vitu viwili tofauti japo inatarajiwa msomi awe mbunifu ingawa si lazima awe mbunifu.Lakini pia kama unapozungumzia ubunifu unamaanisha kuja na kanuni (theory) mpya,then kuna mahala flani kitaaluma ni lazima uje na aidha theory mpya au uifanyie maboresho kwa iliyopo

Mwisho wa kunukuu.

Hapa mimi napata wasiwasi, Hivi kweli tunaweza kutofautisha usomi na ubunifu?
Sasa kama Msomi hawezi kubuni, Je thamani yake iko wapi?
Hivi BAKITA wako wapi, watuondolee huu utata.
Kaka Evarist, hatugombani, lakini naomba utafakari upya kauli yako. Binafsi siogopi kutofautiana bali nahitaji hoja yenye mashiko, ili niweze kukubaliana na wewe. La sivyo, kaka hapa tutakesha.

Naomba nikiri kwamba wengi wetu tunajua dhana na sio ukweli, kwani tumesoma dhana kwa miaka mingi na hatujagundua kwamba kujua ni zaidi ya kuwa na dhana, bali ni kuwa na uwezo wa kubuni na kuleta mabadiliko na hata wale waliokuzunguka wakiri hilo.

Hivi kwa nini hatushangai, kwamba tunao wataalamu wengi katika sekta za kilimo, mifugo, nishati na kila kitu lakini pamoja na rasilimali tulizobarikiwa hapa nchini, bado tumebaki kuwa masikini wa kutupwa. Wasomi hawa hawana ubunifu hata kidogo.

Kudai kujua kile ambacho hunacho kimaisha, ni kujua tu dhana ya kitu hicho, wala sio kitu chenyewe. Unaweza kujua dhana kuhusu uzalishaji bora wa mali lakini wewe mwenyewe ukawa sio mzalishaji bora.

Kujua kitu ni kukifanyia kazi, kwa maana ya kwamba kama wewe ni mtaalamu wa uzalishaji bora, basi tuone huo uzalishaji bora kupitia kwako.

Kwa mfano tunalalamika kwamba nchi hii haina watalamu wa tiba, lakini ukienda pale wizara ya afya unakutana na wataalamu wa tiba wengi tu wa kutosha ambao wamegeuka kuwa watumishi wa maofisini, na huku wagonjwa wakikosa tiba.
Watu wamekimbia taaluma zao.

Wasomi wetu siku hizi wameamua kukimbilia kwenye siasa, maana huko ndiko kwenye tija.
Na hata wakipewa nafasi za kuongoza hawatengenezi mipango endelevu, bali huangalia zaidi kipindi watakachoongoza tu, kwa hiyo mipango ya maendeleo inazingatia kati ya miaka mitano au kumi.

Nadhani wakati umefika sasa wa jamii yetu kubadilika, kama tunataka dhana ya msomi ibebe maana iliyokusudiwa.

Inabidi tukague mfumo wetu wa elimu kama unamsaidia mwanafunzi kutumia elimu hiyo kubuni, kujiajiri na kumudu kubadili hali, iwe yake binafsi au ya wale waliomzunguka.

Lakini kama tutaendelea kukumbatia mfumo wa elimu tulionao unaomfundisha mwanafunzi kwamba kuna ajira baada ya kumaliza masomo yake, hiyo sio elimu.

Wengi wetu katika jamii hii ni wasomi wasio na tija hata kidogo, kwani tumekariri nadharia nyingi za marehemu wengu sana, ambazo zimetupa lundo la makaratasi yanayoitwa digrii.

Lakini ukweli wenye kuumiza ni kwamba hatujaelimika na wala hatuna maarifa.

Naomba kutoa hoja.


6 comments:

Unknown said...

Nadhani sasa huu mjadala hautakuwa na mwisho.

Dada Koero, unaonaje kama tukiomba msaada pale TUKI Chuo Kikuu, maana wale ndio watafiti waliopewa jukumu na serikali kukuza lugha ya kiswahili.

Nadhani wao wanaweza kuja na jibu muafaka.

Bado nasubiri jibu la Maana ya VUKANI

Christian Bwaya said...

Nafikiri, na nadhani ndivyo ilivyo, kwamba tatizo la elimu nchini linaweza kudhihirishwa na aina ya tafsiri ya msomi inayotolewa na wanajamii.

Nimependa mfano wako dada Koero kwamba kitendo cha 'wasomi' hawa kukimbilia siasa ni dalili tosha kwamba nchi yetu inatengeneza wasomaji.

Halafu Kaluse, TUKI wanaweza kutupa tafsiri, lakini si lazima itofautiane na mtazamo wa jamii nzima katika suala la usomi.

Tunahitaji mjadala mpana zaidi kukubaliana tafsiri ya kikwelii.

Unknown said...

Kaka Bwaya, Je wewe unashauri nini?
hebu angalia yale yanyotokea pale Mlimani,Je tunazalisha wasomi au watu wa aina gani?

Hivi tunaweza kupata wabunifu kweli kwa hali iliyopo pale chuo kikuu?

Umesema tunahitaji mjadala mpana kupitia njia gani maana hii ya blog wasomaji ni wachache na kama wako wengi hawataki kutoa maoani yao.

hebu tupe jibu.

Christian Bwaya said...

Kaluse,

Nadhani mipaka ya upana wa mjadala inategemeana na sisi wenyewe. Hatua kwa hatua tunaweza kuupanua mjadala huu kwa kiasi kinachowezekana. Madarasani. Vijiweni. Makazini. Kwenye vyombo vingine vya habari na kadhalika. Alimuradi kupata mawazo zaidi kuhusu jambo hili. Kwa upana zaidi.

Kuhusu vurugu la hawa wanaoitwa wasomi naomba msomaji aamue.

MARKUS MPANGALA said...

Haya nimetulia nduguzanguni, nawasabahi leo. maana nina kilio cha samaki moyoni.
sikiliza wimbo wake Thandiswa Madzwai akisema "siyo mwanzo"

Evarist Chahali said...

Dada Koero,nadhani katika comment yangu iliyopita nilikuomba utusaidie kutafuta KAMUSI YA KISWAHILI SANIFU na kufanya angalizo ya neno MSOMI.Hapo ndio utakuwa mwisho wa mjadala,unless kuwe na upinzani mwingine dhidi ya tafsiri hiyo ya kamusi.

Kuhusu suala la uvumbuzi na usomi kuwa kitu kimoja,nadhani KAMUSI inaweza pia kuwa ya msaada zaidi.Binafsi naendelea kuamini kuwa nini tunachotaka kiwe sio lazima kiwe,na matarajio yetu kwamba wasomi wagfanye hiki au kile sio lazima iwe hivyo japo innastahili kuwa hivyo.Ndio hali halisi katika dunia.Tuna wabunge wanaopaswa kuwakilisha wapiga kura wao lakini baadhi yao huonekana majimboni wakati wa uchaguzi tu.Does that make them sio wabunge tena?Wanabaki kuwa wabunge lakini wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo.Wataalam wanaozembea maofisini wakati nchi inakwenda mrama wanaendelea kuwa wasomi japo usomi wao unakuwa hauna manufaa kwa jamii.Kwa upande mwingine,baadhi ya wasomi kutotumia usomi wao kwa manufaa ya nchi hakufanyi wasomi wote kuwa useless.Akina Shivji,late Chachage,Haroub Othman,late Cuthbert Omari,nk ni miongoni mwa wasomi walio/wanaojua matarajio ya jamii kwao na kwa kiasi kikubwa wamejitahidi kuihudumia jamii ipasavyo.

Pia ni rahisi kulaumu wasomi/wataalam wanaokaa tu maofisini pasipo kutumia ujuzi wao ipasavyo.Lakini unategemea nini katika mazingira ambayo usomi ni mithili ya "nuksi"?Mabosi wengi hawako comfortable na watu waliowapita japo kidato kimoja cha elimu,na si ajabu ushauri wa "msomi" ukapuuzwa kwa kigezo "eti huyu nae anajifanya mjuaji kwa ajili ya elimu yake" kana kwamba kujua wasichojua wengine ni dhambi au kosa la jinai.

Hivi unafahamu shauri ngapi za kitaaluma/kitaalam/kisomi zilipuuzwa na kutufikisha hapa tulipo?Unakumbuka ile benki ya kitapeli iliyofilisika Uganda ikaishia kupewa kibali Bongo japo wataalam walishaonya (nadhani Meridian Biao kama sijakosea),vipi kuhusu matapeli wa Richmond?Kuna wataalam waliofanya background check huko Houston,TX ilikodaiwa kuwa ndio hq ya Richmond ikagundulika kuwa ni mail-box company,wakashauri isipewe tenda,decision makers wakaamu vinginevyo.Sasa hapo kosa ni la wataalam au wafanya maamuzi?

Naomba kukunukuu "Inabidi tukague mfumo wetu wa elimu kama unamsaidia mwanafunzi kutumia elimu hiyo kubuni, kujiajiri na kumudu kubadili hali, iwe yake binafsi au ya wale waliomzunguka..."Japo naafikiana nawe kwamba ingependeza kuona wahitimu wakiweza kuitumia elimu yao watakavyo au pasipo kutegemea ajira,lakini hali halisi haiko hivyo.Wajiajiri wapi?Kwenye kilimo wanachoishia kukopwa na vyama vya ushirika kila kukicha?wageukie ujasiriamali ambao kabla hujakopeshwa na benki lazima umshikishe meneja wa benki chake ndipo atafakari kukupa mkopo?Unadhani wanufaika wakubwa wa mamilioni ya JK ni wahitimu waliokuwa na kiu ya kujiajiri wenyewe au mafisadi?Kumbuka kwamba kuajiriwa ni kufanya kazi kwa mujibu wa matakwa ya mwajiri (at least kwa tafsiri isiyo rasmi) na binadamu kwa asili si mpenda kufanysihwa mambo kwa mujibu wa matakwa ya flani (inherently deviant).Unadhani ingekuwa rahisi kama wishes zako zinavyoonyesha kungekuwa na watu huko TRL ambako mshahara mpaka Wahindi wapige mzinga serikalini?Au unadhani dada zetu wengine wangekuwa radhi kushushwa utu wao as barmaids kwa mshahara wa elfu 20 plus tips?Ni rahisi kuzungumzia KUJIAJIRI ukiwa kwenye comfort ya computer yako,lakini hali halisi huko kunakopaswa kuwafanya watu WAJIAJIRI ni mbaya.Let's be realistic!

Naomba kumalizia kwa kurejea ombi langu kwako dada Koero KUTAFUTA KAMUSI YA KISWAHILI SANIFU kisha kuangalia neno "msomi" HALAFU UTUWEKEE HAPA.Naamini hilo liko ndani ya uwezo wako.