Friday, July 31, 2009

UFISADI: JE TANZANIA INAHITAJI YALIYOTOKEA GHANA 1979?

Ndugu wasomaji wa Blogu hii ya Vukani, leo nimeona niwawekee hii makala ambayo nimeidesa kutoka mtandao wa Jamii Forum.
Nilipousoma niliona ni vyema niwashirikishe wasomaji wa Vukani nao wapate kutafakari kama kuna haja ya kuwaiga wenzetu ili kutokomeza ufisadi hapa nchini.

Naomba kuwasilisha..................

Wale wanaoupinga ufisadi kwa dhati naomba mtafakari iwapo nchi yetu imefikia mahala ambapo pengine linahitajika tukio kama lile la Ghana la June 1979 ambalo kwa kiasi kikubwa limetokea kuwa ni fundisho kubwa kwa mafisadi na wale wanaowalinda. Mapema mwezi huu Rais Barack Obama alitembelea Ghana, nchi ya kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kupata heshima ya kutembelewa na kiongozi wa Marekani mwenye chimbuko la Bara hili.

Hakubahatisha katika kuichagua Ghana – na hasa kutokana na yale aliyoyatamka nchini humo kuhusu Afrika na viongozi wake. Aliwapasha kikweli kweli – kwamba wao ndio wahusika wa kwanza kwa yote yaliyo mabaya ndani ya tawala zao. Kwa hivyo asingeweza kutamka hayo kama angekuwa Tanzania, Nigeria au Kenya kwa mfano. Alichagua nchi angalau aliona inaweza kuwa mfano kwa wengine. Aliisifia sana Ghana kwa demokrasia iliyojijengea na inayoridhisha, uongozi mzuri na utawala bora, pamoja na udhati katika kupigana na ufisadi.

Lakini yote haya hayakuja bure, kwani ule msemo usemao “Usione vinaelea, vimeundwa” unaelezea vizuri sana hali hiyo ya sasa ya Ghana. Baada ya kupinduliwa kwa Kwame Nkrumah mwaka 1966, Ghana iliingia katika kipindi cha tawala za kijeshi na za dhulma. Hata ule wa kiraia uliokuwapo kwa muda mfupi (wa Dr Kofi Busia mwanzoni mwa miaka ya 70) ulikuwa hivyo hivyo -- ufisadi na kulindana ulikithiri kwa kiasi kikubwa sana – kama vile ilivyo hapa Tanzania. Hatimaye mwaka 1979 serikali ya kijeshi ya Jenerali Fred Akuffo iliamua kurudisha utawala wa kiraia.

Vyama vya siasa vikaruhusiwa, ikatayaarishwa katiba mpya na uchaguzi ukafanywa. Lakini kabla ya rais mpya wa kiraia, Hilla Liman kuapishwa, Luteni Jerry Rawlings wa kikosi cha Anga naye alifanya mapinduzi. Akawakamata majenerali wote waliokuwa wakipinduana huko nyuma, kuanzia Akwasi Afrifa, Ignatius Acheampong na Fred Akuffo na maafisa wengine watano. Mahakama maalum iliundwa, na kwa haraka haraka iliendesha kesi na kuwahukumu kuuawa kwa kupigwa risasi, tukio lililofanywa katika ufukwe wa Accra mapema June 16, 1979. Baada ya tukio hilo, tarehe 24 Septemba 1979 Rawlings aliruhusu utawala wa kiraia uendelee na hivyo Hilla Liman aliapishwa kuwa rais.

Rawlings alisema ilibidi majenerali hao wahukumiwe vile kwa sababu siyo tu waliipora nchi na kuifilisi huku wakilindana, lakini pia walishinikiza kuwepo kipengele cha “kinga” katika Katiba ya Kiraia waliyoiunda, kwamba wasiweze kushitakiwa kwa makosa yoyote – ya rushwa na utawala mbovu – walipokuwa madarakani. Rawlings alisema alijitolea kufanya hivyo kwa sababu, ungeingia tu utawala wa kiraia, watawala wale wa zamani wasingewajibishwa, kwa maana ya kushitakiwa, wangeendelea kutanua na mapesa na mali waliziowaibia wananchi.

Kwa hivyo utawala bora uliopo Ghana sasa hivi umetokana na fundisho kubwa la kihistoria lisilosahaulika na limekuwa kama “onyo kali” (deterrent) kwa wengine. Ingawa Rawlings alirudi kuipindua tena serikali ya Liman, hiyo haikuondoa kile alichokifanya kwa nchi yake, kubadilisha mwelekeo wa nchi yake liyoonekana ikienda kusiko, na kikubwa ni kupiga rungu kubwa ufisadi kwa vitendo na siyo kwa maneno. Sisemi kama ufisadi hakuna Ghana, upo, lakini unashughulikiwa vilivyo kwa vyombo husika vilivyo huru, visivyoingiliwa na mamlaka za juu. Hivi majuzi waziri wa Nje wa zamani chini ya utawala wa Rais aliyeondoka John Kuffuor alikamatwa kwa rushwa kuhusiana na uagizaji wa mchele kutoka nje.

Alikamatwa kimya kimya bila hata ya umma kupiga kelele sana kwanza – kama ilivyo hapa kwetu. Kuna baadhi wanasema kitu kama hicho kingefaa pia hapa, kwani ufisadi umekithiri kupindukia, na kulindana kwa hali ya juu na kusafishana kwa wakubwa ndiyo umekuwa kitu cha kawaida na huku umma hauna nguvu zozote za kuweza kurekebisha mambo. Mimi naona tulijadili hili

Tuesday, July 28, 2009

HIVI VIONGOZI WETU HAWAIONI AIBU HII?

Hivi wenzetu wamewezaje kupendezesha miji yao?

Nimerudi Arusha baada ya kukaa Dar es salaam kwa takribani wiki mbili.Ama kweli ukikaa nje ya Dar es salaam unaweza kuona tofauti kubwa na mikoa mingine, nitatoa mfano.

Kusema ukweli kati ya miji inayovutia kwa usafi, ambayo nimewahi kuitembele Arusha na Moshi ndio miji misafi na ya kupigiwa mfano. Dar es salaam jiji ambalo Serikali yote iko hapo Kuanzia Rais mwenyewe na Baraza lake lote la mawaziri wakiwemo makatibu wakuu, na wakurugenzi wa sekta tofauti tofauti wanaishi hapo.

Cha kushangaza Dar es salaam ni jiji chafu ajabu sijapata kuona, hakuna eneo ambalo utatembelea uone kuna nafuu, ni uchafu uliokithiri, sijui hawa viongozi wetu ni vipofu au wamekosa uwezo wa kufikiri?

Ni jambo la kawaida kabisa kukuta watu, hasa wanaume wakitabawali pembeni ya barabara, bila hata ya wasiwasi, unaweza kukuta mtu kakwangua vocha kisha akaitupa baada ya kuitumia, mtu atanunu maji ya chupa na baada ya kumaliza kunywa hayo maji chupa itatupwa popote.

Naomba nikiri kwamba hata mimi nilikuwa naishi kwa mkabala huo, lakini tangu nihamie arusha, nimebadilika sana. Arusha na Moshi, hebu jaribu kukwangua Vocha kisha utupe ile karatasi baada ya kuitumia, utashangaa hata huyo mgambo katokea wapi, utasombwa msobe msobe na ukifikishwa mahakamani ni faini ya shilingi elfu 30 au jela miezi 6.

Kila mtu yuko makini katika kuzingatia swala la usafi na utunzaji wa mazingira tofauti na jiji la Dar es salaam ambalo limekithiri kwa uchafu wa kila aina kuanzia watoto wa mitaani, wasichana wanaojiuza na kila ghasia.
Askari wa jiji ambao wangetumika kukamata na kuwathibiti wale watu wanaotupa takataka ovyo mitaani wameachwa na kazi yao kubwa ni kukimbizana na wamachinaga na kinamama ntilie na kuwanyang’anya hata kile kidogo wanachodunduliza kwa ustawi wa famlia zao.

Sio kwamba nawatetea Machinga au mama Ntilie kwani nao pia ni wachafuzi wa mazingira, lakini, hebu tujiulize, hivi hawa ndio wachafuzi wa mazingira pekee, vipi kuhusu gereji bubu zilizotapakaa kila mahali?

Kwanini wajasiriamali hawa wasitengewe maeneo mazuri na kuwekewa miundo mbinu ya kuvutia ili nao waweze kufanya biashara zao kwa ufanisi na utaratibu watakaowekewa?

Kwani Moshi na Arusha wamewezaje?

Ngoja niachane na hilo la uchafu maana linanitia hata kichefuchefu. Tatizo lingine nililoliona ni hili la foleni.......jamani yaani inaweza kukucukua zaidi ya masaa matatu kuingia mjini tu.
Najua watu watasema kuwa Arusha na Moshi hakuna magari mengi, naweza kukubaliana nao, lakini kama ikitokea mkoa unakuwa na watu wengi wenye kumiliki magari kwa maana ya kwamba baba, mama, na kila mtoto na gari lake ingawa wote wanaenda njia moja, lakini kila mtu anataka kuendesha gari ndio watu wakose ubunifu wa kupunguza foleni?
Binafsi nilishangazwa sana na ule uamuzi wa waziri mkuu wa wakati ule Shemeji yangu Mzee Lowasa alipoanzisha utaratibu wa njia tatu, kwangu mimi, mbinu ile haikuwa ni ufumbuzi badala yake ilkuwa ni ya kero na ilisababisha ajali na kupoteza maisha ya watu na wengine wakiachwa vilema.

Hivi sisi hatuna Vision wala Mission?
Yaani tupo tupo tu na mikakati ya zima moto, jambo halifanyiwi kazi, mpaka yatokee maafa?
Kama nikibahatika kupewa mamlaka ya kuongoza nchi hii, japo kwa mwezi mmoja tu ningefanya mampinduzi makubwa sana. Jambo la kwanza kabisa ningewanyang’anya wahandisi wote wa jiji la Dar es salaam vyeti vyao na kuwarudisha chuoni wakasome upya. Kwani wamesababisha nchi hii kuingia katika hasara kubwa. Badala ya kuboresha miradi ya maendeleo lakini kila siku ni kulipa watu fidia kwa kuwabomolea nyumba kutokana na ujenzi holela.
Utakuta watu wamejenga nyumba zao na mpaka umeme wameweka lakini kesho unasikia nyumba hizo zinabomolewa, kisa wamejenga katika maeneo yasiyopimwa.
Wakati wenzetu wataalamu wao wa uhandisi wanashindana kubuni miradi mikubwa yanye kupendezesha nchi zao na kuvutia watalii, lakini sisi tumekalia ubinafsi tu, hakuna ubunifu.

Kama watu wa ardhi wangekuwa wamepima Viwanja na kisha watu wakapewa bila urasimu na rushwa, haya yote yasingetokea. Kuna jinamizi kubwa la rushwa pale Ardhi, na wala serikali haijishughulishi, kuna watu wamegeuza mahali pale kama shamba lao la kuvuna pesa na hiyo hufanyika wazi wazi. Utafanya nini, ukienda Takukuru, nako mambo ni hayo hayo, nayo inahitaji kuchunguzwa.

Hatua ya pili baada ya kuwafukuza wahandisi wetu wazalendo wasio na hata chembe ya uzalendo, ningeomba msaada wa wataalamu kutoka kwa wenzetu waliofanikiwa kuitengeneza miji yao ikapendeza.
Kisha kwa ushirikiano na wataalamu hao nitajenga vituo vya kuegesha magari katika maeneo makuu manne yafuatayo, Kituo cha kwanza ningekiweka pale Moroco, kituo cha pili ningekiweka pale Magomeni, kituo cha tatu ningekiweka pale Kurasini na kituo cha nne ningekiweka pale Banda la ngozi barabara ya nyerere.

Magari yote ya watu binafsi yatakuwa yanaishia katika hivyo vituo ispokuwa ya mawaziri na makatibu wakuu na wakurugenzi na viongozi waandamizi wa serikali pekee tu ndio yatakayoruhusiwa kuingia maeneo ya kati kati ya mji.
Daladala kutoka maeneo mbali mbali ya nje ya mji yatakuwa yanaishia katika vituo hivyo, halafu kutakuwa na mabasi maalum makubwa yatakayo kuwa yanaanzia safari katika vituo hivyo kuingiza watu mjini tena kwa utaratibu maalum, kama kuna mtu anahitaji kuingia na gari lake binafsi maeneo ya mjini basi atalazimika kulipia gharama ya maegesho ya kiasi cha shilingi zisizopungua elfu 50 kwa siku.

Utaratibu huu utakuwa ukitumika siku za wiki tu, mwisho wa wiki yaani jumamosi kuanzia mchana na jumapili kutwa watu binafsi wataruhusiwa kuingia mjini na magari yao na watalipia ghrama ndogo tu za maegesho. Haihitaji kutumia akili ya kutengeneza Roketi ili kubuni mbinu hii.
Hii ni mbinu ambayo haihitaji gharama kubwa sana na italeta ufanisi kwani watu hawatachelewa makazini na kwenye shughuli zao.

Jamani huu ni mtazamo wangu tu na wala msinijengee chuki........

Wednesday, July 22, 2009

NI NANI ASIKIE KILIO CHAO?

Ndugu wasomaji na wanablog wenzangu, bado niko Dar, na kutokana na pilika pilika zilizonileta hapa kutokamilika, nitalazimika kukaa hapa kwa wiki moja zaidi.

Leo naomba nizungumzie wajane.
Nilipokuwa Arusha, nilishuhudia tukio ambalo mpaka leo limenikaa sana akilini, na linaniumiza roho sana.

Nilishuhudia mama mmoja mjane akinyang’anywa kila kitu na ndugu wa mumewe mara bada ya kutoka kumzika mumewe. Tukio hili la kuisikitisha lilitokea wiki moja baada ya mazishi ya mumewe mpendwa.

Nilisimuliwa kuwa mama huyu alikuwa akiishi na bwana huyo kinyumba, hawakuwahi kufunga ndoa kutokana na sababu za kidini, mume muislamu na mke mkiristo, lakini waliishi pamoja kwa takribani miaka sita na kujaaliwa kupata watoto wawili.

Inasemekana upande wa mume hawakumpenda yule mwanamke, kisa alikataa kubadili dini, na kuwa muislamu ili wafunge ndoa, hiyo ikawa ndio sababu ya kukataa asiolewe na ndugu yao. hata hivyo waliendelea kuishi pamoja na kwa mapenzi kama mume na mke hadi wakapata watoto wawili, wa kike na wa kiume.

Mara yule bwana akaanza kuugua ghafla, alipopelekwa hospitali haukuonekana ugonjwa na baaada ya siku tatu akafariki dunia.
Kasheshe lilianzia hapo ndugu wa marehemu wakadai kuwa yule mwanamke alimpa sumu ndugu yao ili arithi mali.
Kisa yule bwana alikuwa anamiliki miradi kadhaa na pia alikuwa na nyumba mbili hapo Arusha, moja akiwa ameipangisha na nyingine akiishi yeye na familia yake.

Mara baada ya mazishi yule mwanamke aliamriwa aondoke, mara moja na nyumba na miradi ya mumewe ikawa chini ya himaya ya ndugu wa mume.

Sina uhakika kama yule mwanamke anaweza kupata msaada wa kisheria kwani hakuwa ana ndoa na yule mume.
Sina uhakika hatima na yule mwanamke na wale watoto kwani wamenyang’anywa kila kitu.

Ndugu wasomaji na wanablog wenzangu, naamini kuwa hili sio jambo geni masikioni mwenu, inawezekana mliwahi kusikia au kushuhudia unyama wa aina hii.

Swali ninalijiuliza mpaka sasa, ni je hivi unyama huu wanaofanyiwa wajane, utaisha lini?
Jana nilikuwa nilikuwa nasoma Biblia na katika kusoma kwangu nikakutana na fungu moja la biblia lililonikumbusha tukio hili la Arusha na ndipo nikaona niwashirikishe wasomaji na wanablog wenzangu tutafakari kwa pamoja.

Fungu lenyewe ni Kutoka 22: 22-24, linasema:
Nitanukuu, “Usimtese mjane yeyote aliyefiwa na mumewe wala mtoto yatima, ukiwatesa watu hao katika neno lolote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto nami nitawauwa ninyi kwa upanga na wake wenu watakuwa wajane na watoto wenu mayatima”
Mwisho wa kunukuu.

Friday, July 17, 2009

KOERO SAFARINI DAR!!!!


Wasomaji na wanablog wenzangu, leo saa nne asubuhi hii naondoka hapa Arusha nikielekea Dar Es Salaam, kwa ajili ya kuwaona wazazi wangu na mambo mengine madogo madogo.

Nitakuwepo Dar Es Salaam kwa muda wa siku tano, kwani Jumatano narudi arusha kuendelea na majukumu yangu yaliyonihamishia Arusha.

Kama mnavyojua kuwa safari ni hatua na hivi vyombo tunavyosafiri navyo vinatengenezwa kwa mikono ya wanaadamu, namuomba mungu anifikishe salama.
Naomba mniombee safari njema na nitakapofika nitawajuza kupitia humu katika blog yenu ya VUKANI.
Nawapenda wote……………..

Sunday, July 12, 2009

WANAWAKE HUPOTEZA MUDA MWINGI SANA KUCHAGUA NGUO YA KUVAA!!!

Hii nimeidesa kutoka katika mtandao wa Jamii Forum, nimeona niwashirikishe wasomaji wa blog hii ya VUKANI na wanablog wenzangu ili kupata ukweli juu ya hili.........

Matokeo ya utafiti uliofanywa nchini Uingereza umeonyesha kuwa wanawake hutumia muda mwingi sana katika maisha yao kuchambua makabati yao kutafuta nguo ipi ya kuvaa wakati wanapotoka majumbani mwao.

Kwa mujibu wa utafiti huo wanawake hutumia muda mwingi sana katika maisha yao wakitafakari nguo ipi ya kuvaa wakati wanapoenda makazini, kwenda 'Out', kwenye vakesheni au shughuli zao za kawaida za kila siku. Utafiti huo uliofanywa na kampuni kubwa ya maduka ya nguo ya Matalan ya nchini Uingereza ulishirikisha wanawake 2,491.

Utafiti huo ulifanywa kwa wanawake wenye umri kati ya miaka 16 na 60 ulionyesha kuwa wanawake hutumia takribani dakika 20 kutoa uamuzi wa nguo ipi wavae kabla ya kutoka kwenda kujirusha mwishoni mwa wiki. Wanawake hutumia dakika 52 kutoa uamuzi wa nguo zipi za kuchukua wakati wanapoenda vakesheni.

Wakati wanapokuwa vakesheni wanawake hutumia dakika 10 wanapoamka asubuhi kuamua nguo ipi ya kushinda nayo mchana na nyakati za usiku hutumia dakika 10 nyingine kuamua kivazi kipi cha usiku cha kuvaa. Utafiti huo ulionyesha pia kuwa wanawake hutumia dakika 36 kuchagua nguo ya kuvaa wakati wa kujiandaa kwenda kwenye sherehe na maharusi. "Kwa wastani wanawake karibia wote hujaribu nguo zaidi ya mbili kila siku asubuhi kabla ya kufikia uamuzi nguo ipi ya kuvaa" ulisema utafiti huo.

Wanawake wanaofanya kazi nao hutumia takribani dakika 15 usiku wa kuamkia siku ya kazi kuchagua nguo ya kuvaa wakati wanapoenda makazini, ulimalizia utafiti huo.

Wednesday, July 8, 2009

YAKO WAPI MAHITAJI?

Leo nilikuwa napitia blog ya kaka yangu na mwanablog mwenzangu Mubelwa Bandio Mzee wa Changamoto, nikakutana na hii makala ambayo aliiandika hapo mnamo Juni 10, 2009.
Ukweli ni kwamba nimevutiwa sana na makala hii na ndio maana nikaona ni vyema niiweke hapa ili tuweze kuijadili kwa pamoja.

*********************************

Uchaguzi mkuu wa Tanzania unakaribia na kwa hesabu za haraka haraka, natumai vyama husika vimeshaanza kujipanga vema kwa ajili ya "msimu" huo wa kuonesha wanawajali wananchi na wako hapo kuwatetea, kuwahudumia na kuwatengenezea kaisha bora. Yale yale ya MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA. Katika pilika hizi za vyama, nina hakika moja ya hatua inayoendelea sasa ni kuandaa ILANI YA UCHAGUZI kwa kila chama ili kuweza "kuuza" sera zao.Kinachosikitisha sasa ni kuwa wapo waTanzania wengi ambao wana mahitaji mbalimbali muhimu na ambao maisha yao hayawezi kuwa sawa na wengine bila kuwezeshwa kwa namna fulani na ambao wameonekana kusahaulika lakini hawatumii muda huu kuweka mahitaji yao bayana ili yajumuishwe kwenye Ilani hizi.

Nazungumzia wenye mamlaka ya kuwasilisha na kuwakilisha wenye uhitaji ambao ni Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania ( SHIVYAWATA) linaloundwa na vyama mbalimbali ambavyo ni Chama cha Walemavu Tanzania ( CHAWATA), Chama cha Wasioona Tanzania ( TLB), Chama cha Viziwi Tanzania ( CHAVITA), Chama Cha Maalbino Tanzania ( CCMT) na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Akili (TAMH). , na vyama vingine mbalimbali venye kuwatetea wenye uhitaji ambavyo sasa ni wakati muafaka wa kukusanya maoni ya uhitaji toka kwa wanachama wao na kisha kuyaweka bayana kwa kila chama kuwa "wanachama wetu wanahitaji kiongozi ambaye atawajali katika mahitaji (watakayoyataja)" ili wagombea wajue namna ya kuyajumuisha kwenye mipango yao na pia kuweza "kujifunga" kwa jamii katika kutekeleza.

Kuna haki nyingi za msingi na lazima ambazo kwa namna moja ama nyingine wenzetu hawa wanawiwa vigumu kuzipata wanaposhindana na wasio na uhitaji, haki kama shule za kutosha kuwaelimisha, vifaa vya kuwawezesha kuelimika, vifaa vya kuwarahisishia maisha (hata kama ni vya kununua kwa gharama nafuu), maegesho, usafiri, uwezeshwaji wa kufika kwenye ofisi muhimu kwa urahisi (kama ilivyoelezwa HAPA). Natambua kuwa kuna viongozi wa vyama mbalimbali vinavyowakilisha wenye uhitaji mbalimbali, lakini nashangazwa na namna ambavyo hawatumii nafasi hizi kuwabana wagombea, bali wanasubiri mpaka wakati wanapotembelewa na viongozi (baada ya chaguzi) na kusoma risala kueleza matatizo yao ambayo wamekuwa nayo kwa muda mrefu.Ni muda wa kuwafanya wagombea KUELEWA UHITAJI WA WAHITAJI na kisha wajumuishe uhitaji huo katika sera zao ili wanapoingia madarakani wawe na "deni" la kuwatumikia wahitaji.

Lakini wenye mamlakahawafanyi hivyo, matokeo yake wanasiasa wetu wanachukua mwanya wa "kutojua" kujifanya wamesahau uhitaji wa wahitaji na kuanza / kuendelea kutumbua mali ilhali wahitaji wanaendelea kusota na kufa njaa. Ni swali ninaloendelea kujiuliza kuwa YAKO WAPI MAHITAJI YA WAHITAJI? Na ni lini viongozi wetu watayatatua bila "kushurutishwa?" Ni hakika kuwa viongozi wengi HAWANA UPENDO na ndio sababu wanatenda watendayo (kutowajali wahitaji).

Nasio alisema kuwa "them (they're) talking about this, them (they're) talking about that, poor people just a suffer (are suffering) while you live out fat...." " you living in the pride and luxuries, while needier are dying in their poverty. Lord know that they aint got no Love at all"