Tuesday, July 28, 2009

HIVI VIONGOZI WETU HAWAIONI AIBU HII?

Hivi wenzetu wamewezaje kupendezesha miji yao?

Nimerudi Arusha baada ya kukaa Dar es salaam kwa takribani wiki mbili.Ama kweli ukikaa nje ya Dar es salaam unaweza kuona tofauti kubwa na mikoa mingine, nitatoa mfano.

Kusema ukweli kati ya miji inayovutia kwa usafi, ambayo nimewahi kuitembele Arusha na Moshi ndio miji misafi na ya kupigiwa mfano. Dar es salaam jiji ambalo Serikali yote iko hapo Kuanzia Rais mwenyewe na Baraza lake lote la mawaziri wakiwemo makatibu wakuu, na wakurugenzi wa sekta tofauti tofauti wanaishi hapo.

Cha kushangaza Dar es salaam ni jiji chafu ajabu sijapata kuona, hakuna eneo ambalo utatembelea uone kuna nafuu, ni uchafu uliokithiri, sijui hawa viongozi wetu ni vipofu au wamekosa uwezo wa kufikiri?

Ni jambo la kawaida kabisa kukuta watu, hasa wanaume wakitabawali pembeni ya barabara, bila hata ya wasiwasi, unaweza kukuta mtu kakwangua vocha kisha akaitupa baada ya kuitumia, mtu atanunu maji ya chupa na baada ya kumaliza kunywa hayo maji chupa itatupwa popote.

Naomba nikiri kwamba hata mimi nilikuwa naishi kwa mkabala huo, lakini tangu nihamie arusha, nimebadilika sana. Arusha na Moshi, hebu jaribu kukwangua Vocha kisha utupe ile karatasi baada ya kuitumia, utashangaa hata huyo mgambo katokea wapi, utasombwa msobe msobe na ukifikishwa mahakamani ni faini ya shilingi elfu 30 au jela miezi 6.

Kila mtu yuko makini katika kuzingatia swala la usafi na utunzaji wa mazingira tofauti na jiji la Dar es salaam ambalo limekithiri kwa uchafu wa kila aina kuanzia watoto wa mitaani, wasichana wanaojiuza na kila ghasia.
Askari wa jiji ambao wangetumika kukamata na kuwathibiti wale watu wanaotupa takataka ovyo mitaani wameachwa na kazi yao kubwa ni kukimbizana na wamachinaga na kinamama ntilie na kuwanyang’anya hata kile kidogo wanachodunduliza kwa ustawi wa famlia zao.

Sio kwamba nawatetea Machinga au mama Ntilie kwani nao pia ni wachafuzi wa mazingira, lakini, hebu tujiulize, hivi hawa ndio wachafuzi wa mazingira pekee, vipi kuhusu gereji bubu zilizotapakaa kila mahali?

Kwanini wajasiriamali hawa wasitengewe maeneo mazuri na kuwekewa miundo mbinu ya kuvutia ili nao waweze kufanya biashara zao kwa ufanisi na utaratibu watakaowekewa?

Kwani Moshi na Arusha wamewezaje?

Ngoja niachane na hilo la uchafu maana linanitia hata kichefuchefu. Tatizo lingine nililoliona ni hili la foleni.......jamani yaani inaweza kukucukua zaidi ya masaa matatu kuingia mjini tu.
Najua watu watasema kuwa Arusha na Moshi hakuna magari mengi, naweza kukubaliana nao, lakini kama ikitokea mkoa unakuwa na watu wengi wenye kumiliki magari kwa maana ya kwamba baba, mama, na kila mtoto na gari lake ingawa wote wanaenda njia moja, lakini kila mtu anataka kuendesha gari ndio watu wakose ubunifu wa kupunguza foleni?
Binafsi nilishangazwa sana na ule uamuzi wa waziri mkuu wa wakati ule Shemeji yangu Mzee Lowasa alipoanzisha utaratibu wa njia tatu, kwangu mimi, mbinu ile haikuwa ni ufumbuzi badala yake ilkuwa ni ya kero na ilisababisha ajali na kupoteza maisha ya watu na wengine wakiachwa vilema.

Hivi sisi hatuna Vision wala Mission?
Yaani tupo tupo tu na mikakati ya zima moto, jambo halifanyiwi kazi, mpaka yatokee maafa?
Kama nikibahatika kupewa mamlaka ya kuongoza nchi hii, japo kwa mwezi mmoja tu ningefanya mampinduzi makubwa sana. Jambo la kwanza kabisa ningewanyang’anya wahandisi wote wa jiji la Dar es salaam vyeti vyao na kuwarudisha chuoni wakasome upya. Kwani wamesababisha nchi hii kuingia katika hasara kubwa. Badala ya kuboresha miradi ya maendeleo lakini kila siku ni kulipa watu fidia kwa kuwabomolea nyumba kutokana na ujenzi holela.
Utakuta watu wamejenga nyumba zao na mpaka umeme wameweka lakini kesho unasikia nyumba hizo zinabomolewa, kisa wamejenga katika maeneo yasiyopimwa.
Wakati wenzetu wataalamu wao wa uhandisi wanashindana kubuni miradi mikubwa yanye kupendezesha nchi zao na kuvutia watalii, lakini sisi tumekalia ubinafsi tu, hakuna ubunifu.

Kama watu wa ardhi wangekuwa wamepima Viwanja na kisha watu wakapewa bila urasimu na rushwa, haya yote yasingetokea. Kuna jinamizi kubwa la rushwa pale Ardhi, na wala serikali haijishughulishi, kuna watu wamegeuza mahali pale kama shamba lao la kuvuna pesa na hiyo hufanyika wazi wazi. Utafanya nini, ukienda Takukuru, nako mambo ni hayo hayo, nayo inahitaji kuchunguzwa.

Hatua ya pili baada ya kuwafukuza wahandisi wetu wazalendo wasio na hata chembe ya uzalendo, ningeomba msaada wa wataalamu kutoka kwa wenzetu waliofanikiwa kuitengeneza miji yao ikapendeza.
Kisha kwa ushirikiano na wataalamu hao nitajenga vituo vya kuegesha magari katika maeneo makuu manne yafuatayo, Kituo cha kwanza ningekiweka pale Moroco, kituo cha pili ningekiweka pale Magomeni, kituo cha tatu ningekiweka pale Kurasini na kituo cha nne ningekiweka pale Banda la ngozi barabara ya nyerere.

Magari yote ya watu binafsi yatakuwa yanaishia katika hivyo vituo ispokuwa ya mawaziri na makatibu wakuu na wakurugenzi na viongozi waandamizi wa serikali pekee tu ndio yatakayoruhusiwa kuingia maeneo ya kati kati ya mji.
Daladala kutoka maeneo mbali mbali ya nje ya mji yatakuwa yanaishia katika vituo hivyo, halafu kutakuwa na mabasi maalum makubwa yatakayo kuwa yanaanzia safari katika vituo hivyo kuingiza watu mjini tena kwa utaratibu maalum, kama kuna mtu anahitaji kuingia na gari lake binafsi maeneo ya mjini basi atalazimika kulipia gharama ya maegesho ya kiasi cha shilingi zisizopungua elfu 50 kwa siku.

Utaratibu huu utakuwa ukitumika siku za wiki tu, mwisho wa wiki yaani jumamosi kuanzia mchana na jumapili kutwa watu binafsi wataruhusiwa kuingia mjini na magari yao na watalipia ghrama ndogo tu za maegesho. Haihitaji kutumia akili ya kutengeneza Roketi ili kubuni mbinu hii.
Hii ni mbinu ambayo haihitaji gharama kubwa sana na italeta ufanisi kwani watu hawatachelewa makazini na kwenye shughuli zao.

Jamani huu ni mtazamo wangu tu na wala msinijengee chuki........

6 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Koero mada ya leo imekaa safi sana nimeipenda sana:- Haya mambo ya usafi kwa kweli yanaleta aibu sana kama ulivyosema kula na kutupa tu. Kuna siku Rafiki yangu mmoja mswidi atulikuwa Dara na alikuala ndizi na baadaye alitembea na lile ganda kutafuta sehemu ya kutupa yaani kama vile pipa.Lakini hata hivyo sasa hivi kuna sehemu kuna mapipa ya kutupa taka lakini watu wanachafua tu mazingira. Hii pia ni moja ya sababu kuna kuwa na kipindupindu mara kwa mara.

Tuje kwenye jambo hili la foleni:- Nimeyapenda mawazo yako ya kupunguza foleni kwa kweli huwa inakatisha tamaa ukiwa Dar kama kweli utafika huko uendako?
Na pale wakati wa foleni ndio muda ambao wizi mwingi hutokea.

Kwa hiyo mdogo wangu Koero nakuunga mkono 100% kwamba daladala zote zingetolewa na kuwekwa mabasi makubwa tu. Na labda kuwe na vituo ambavyo viwe vimeanzia mbali kidogo na pia vituo vya kuegesha magari viwe vingi zaidi kingine kiwa labda pale mwengi...maana pale kaazi kwelikweli. Na pia bila kusahau kuwe na ratiba ionyeshayo basi linaondoka saa ngapi. Tupo Pamoja.

Mzee wa Changamoto said...

Da' Koero. Mie "NIMESHIBA NJAA" maana nimesema na kuandika na kisha kuandika na kusema na sasa nahisi nashiba njaa. Sijui nani wa kumlaumu nani lakini naomba nikubaliane nawe katika mengi uliyosema (maana ni ukweli) na nikumbushe haka ka-kipengele nilikowahi kutoa. Ilikuwa ni sehemu ya kwanza ya "Ni kama hadithi ya Kuku na Yai". Iangalie hapa unisaidie kuunganisha mawazo http://changamotoyetu.blogspot.com/2008/12/ni-kama-hadithi-ya-kuku-na-yai.html
Lakini bado swali labaki kuwa liule lile kuwa tuendako kupiga kura na kuwapa dhamana hawa "watawala", "TUNACHAGUA KWA UTASHI AMA UHITAJI?" (http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/07/tunachagua-kwa-utashi-ama-uhitaji.html)
HESHIMA KWAKO

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

mamammmaaa

SIMON KITURURU said...

MmmH!

Egidio Ndabagoye said...

Karibu sana A Town na K'njaro.

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___