Thursday, December 31, 2009

NIMETAFAKARI MAONI YENU, VUKANI KUENDELEA KUWA MTANDAONI.

Kazi na Dawa

Ni jambo la kujivunia, kung’amua kuwa kumbe blog ya Vukani iko juu na inapendwa. Kusema kweli sikuwahi kufahamu kuwa blog ya vukani inapendwa kiasi hiki na hilo limenifanya nifikirie upya uamuzi wangu.

Ulikuwa ni uamuzi mgumu sana, lakini nimeona ni vyema niheshimu maoni ya wasomaji wa blog hii na wanablog wenzangu na hivyo nitaendelelea kublog kama kawaida. Tarajieni mabadiliko makubwa katika blog hii kwani mwaka mpya na mambo mapya…au sio?

Natoa shukrani kwa wasomaji wote, mliotumia muda wenu kutoa maoni na wengine kuniandikia email binafsi, nawahakikishieni kuwa blog ya Vukani itaendelea kuwepo kama kawaida.

Sina mengi kwa leo ngoja nijiandae kwa ujio wa mwaka mpya wa 2010.

Ahsanteni sana.

Friday, December 25, 2009

BAADA YA KUTIMIZA MWAKA MMOJA LEO TANGU KUANZISHWA KWAKE BLOG YA VUKANI KUFUNGWA RASMI LEO

Kwa herini ya kuonana

Leo tarehe 25 December 2009 Blog hii ya VUKANI Inatimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake. Ni jambo la kujivunia kwamba ndani ya mwaka mmoja nimeweza kuweka makala 100 na nimemudu kuendelea kublog hata pamoja na majukumu mbalimbli ya kifamilia niliyokuwa nayo. Nilikuwa nikisafiri mara kwa mara lakini hata hivyo niliweza kuweke post kama kawaida ili wasomaji wa blog hii waendelee kusoma ujinga wangu.

Najua tangu nianze kublog kuna watu niliwakwaza na wengine niliwafurahisha na hata kuwafikirisha, lakini halikuwa lengo langu kumuumiza mtu kihisia kwa namna yoyote ile kwani lengo la blog hii ni kuelimisha, kufikirisha, na kufurahisha. Naamini malengo ya uwepo wa blog hii yalitimia kwa kiasi fulani.

Kama nilivyosema kuwa blog hii itakuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo, naamini yote hayo yalitimia na ndio maana leo natimiza mwaka mmoja nikijivunia kile nilichokifanya hadi leo.
Najua si rahisi kufanya tathmini na kujua kama ni wasomaji au wanablog wangapi ambao kwa njia moja ama nyingine wamejifunza au wamenufaika na huu ujinga wangu, ninaouweka humu lakini naamini kwa kiasi fulani kuna wengi wamejifunza na kunufaika na uwepo wa blog hii.

Kama kumbukumbu zenu haziko mbali, kwa wale wafuatiliaji wa blog hii watakumbuka kuwa, blog hii ilianza na misukosuko mingi, kwani karibu mara mbili nilipata shinikizo la wazazi wangu kuifunga na kuachana na mambo ya kublog, baada ya kuibua hoja ya kuhoji swala zima la nadharia ya hizi dini zetu za mapokeo, kama unataka kujikumbusha bofya hapa
NIMEANZA KUZISHITUKIA HIZI DINI. Mada hiyo iliwashitua sana wazazi wangu, ambapo walinitaka niache kublog kama sina mambo ya maana ya kuandika, swala la kuhoji uhalali wa dini likaonekana halina maana.

Nililazimika kuufunga ule mjadala ili kunusuru mahusiano yangu na wazazi wangu. Mara ya pili ni pale nilipopingana na wazazi wangu juu ya swala la kuendelea na elimu, baada ya kuacha chuo na kujikita kwenye biashara zaidi, hiyo nayo ilikuwa ni changamoto nyingine, lakini kutokana na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa blog hii nilimudu kuyamaliza na hivyo kuendelea kublog kama kawaida.

Naomba nikiri kwamba uwepo wa blog hii ni kutokana na kuvutiwa na blog ya MAISHA ya dada Yasinta Ngonyani, kwani ni yeye aliyenifanya nami nianze kublog na kwa msaada wa mdogo wangu Jerome kwa utundu wake aliweza kuifungua blog hii.

Pia siwezi kuepuka kumtaja kaka Markus Honorius Mpangala aka MCHARUKO kwani na yeye kwa upande wake alichangia kuifanya blog hii ionekane kama ilivyo leo. Pia siwezi kuepuka kumtaja kaka yangu mpendwa Mubelwa Bandio kwa kuwa karibu nami akinishauri hili na lile juu ya namna nzuri ya kublog, na pia amekuwa ni mhariri wangu mahiri akinisaidia kurekebisha lugha na namna nzuri ya kujenga hoja katika makala zangu.

Salaam kwako dada yangu Yasinta ngonyani, wewe ni dada yangu mpendwa, siwezi kuwataja dada zangu Debora Damari, na Rachel bila kukutaja wewe dada yangu mpendwa. Dada kwa kweli upendo wako ni wa ajabu kwangu umekuwa karibu nami na nimekuwa nikikufanyia masihara mengi na utani mwingi licha ya kwamba umenizidi sana umri. Umekuwa ni mshauri mwema kwangu juu ya mambo mengi yahusuyo maisha. Umechangia kwa kiasi kikubwa katika kunibadili kitabia kutokana na hekima zako, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa wema wako.

Kwako dada Subi, nawe kwa upande wako ninayo mengi ya kujivunia, umenifunza mengi na umenifanya nikue kifikra, wewe umekuwa mmoja kati ya dada zangu na nimekuwa nikijivunia sana kukufahamu, pokea salaam zangu.

Kaka yangu Mbwange Simon Mkodo Kitururu, Duh! Sina la kusema, kupitia blog yako na maoni yako nimejifunza mengi. Kwani kupitia blog yako ya Mawazoni nimejifunzza kuwa hakuna lugha ya matusi, bali kuna majina yanayowakilisha viungo vya mwili, miti, wanyama na vitendo, lakini kutokana na tafsiri tulizofundishwa tumekuwa tukiamini kuwa baadhi ya majina ya viungo vya mwili, wanyama miti na baadhi ya vitendo ni matusi.

Pia siwezi kumsahau kaka yangu wa kulikoni Ughaibuni Evarist Chahali, wewe ulikuwa ni msomaji mmojawapo uliyeweka changamoto zako humu na kuibua mijadala mikubwa na hata kuleta mgongano wa mawazo, najua ni siku nyingi hatujawasiliana lakini naamini unaikumbuka VUKANI.

Kaka yangu Profesa Matondo, sijui niseme nini, lakini wewe mwenyewe unajua ni kiasi gani umenisaidia kukua kifikra, ni jambo la kujivunia kuwa pamoja na Elimu yako na shughuli zako nyingi uliweza kurudi chini na kuweza kuzungumza nami kama vile kaka azungumzaye na mdogo wake tumbo moja. Umekuwa mshauri wangu katika masuala mbalimbali ya kielimu na kijamii, heshima kwako Profesa Matondo.

Kwako kaka Shabani Kaluse, aka baba Abraham, Mzee wa Utambuzi, naomba nikiri wazi kuwa kupitia kibaraza chako nimejifunza mambo mengi juu ya utambuzi na nimebadilika sana kitabia, umekuwa ukijibu email zangu binafsi na kunishauri mambo mengi sana juu ya maisha na mafanikio. Umekuwa mhariri wangu mzuri pale ninapotaka kuweka makala za kijamii umekuwa ukinishauri namna nzuri ya kujenga hoja. Nakushukuru sana kaka kwa wema wako.

Dada Schola Mbipa, heshima kwako dada, nakushukuru kwa ushauri mbalimbali uliokuwa ukinipa ili kuiboresha blog hii.

Uuuuwiiii!!!!! Jamani nusura nimsahau Kamala Lutatinisibwa, huyu naye kwa kweli amenifundisha mambo mengi sana juu ya Utambuzi, maoni yake yamekuwa yakileta changamoto katika blog zetu hizi na kuibua mijadala ya hapa na pale, huyu ni mdau mmojawapo ambaye amenifanya nisifikirie kuacha kublog.
Ngoja niwanong’oneze siri, kusema kweli kama nikiweka makala katika kibaraza hiki halafu Kamala asiweke maoni nahisi kama mada yangu haijakamilika….LOL, kwani ni mdau mmojawapo ambaye lazima akiweka maoni utapenda kuyarudia kuyasoma mara kadhaa, sio kwa kutokuelewa bali kwa kutafakari zaidi, maoni yake mara nyingi yanafikirisha.


Najua ni wengi, wengi sana waliojitokeza katika blog hii na kuweka maoni yao au kunitumia email binafsi wakinishauri hili na lile ili kuiboresha blog hii, pia wapo waliotaka mawasiliano nami ya karibu lakini kutokana na kutingwa nimeshindwa kutekeleza hilo, lakini naomba muamini kuwa tupo pamoja.

Kwa uchache niwataje hawa wafuatao ambao kwa njia moja ama nyingine wamekuwa ni chachu ya kufanikisha uwepo wa blog hii, kaka Damas Michael, Godwin Meghji, kaka Kisima, kaka Manento Kitururu, kaka James Jim, kaka Chib, Dada My Little World, kaka John Mwaipopo, kaka Edo Ndaki, Mummy Hery, Da' Mija na wengine wengi. Niliowasahau mtanisamehe jamani nafasi ni ndogo……LOL.

Sasa naomba mniruhusu kuifunga rasmi blog hii ili niweze kufanya mambo mengine ambayo naamini yatakuwa bora zaidi ya kublog.

Ahsanteni na kwaherini wote, tutawasiliana mungu akipenda.

Ahsanteni sana kwa ushirikiano wenu katika kipindi chote nilipokuwa nikiblog.
Nawapenda wote jamani, Mungu awe nanyi milele daima…..aaaaamen

Sunday, December 20, 2009

HIVI HUYU KIJANA NI NANI?

Picha kwa hisani yake mwenyewe
Ni kijana mdogo kwa umri lakini ni mkubwa kwa umbo.
Kijana huyu ni suriama aliyechanganya kati ya makabila mawili ya Mpare kutoka milima ya upareni na Mjita kutoka kule Musoma kusikoisha vita kati ya koo za Wanchori na Wanchoka.

Alifanikiwa kupata elimu yake kupitia shule kadhaa hapa nchini kabla hajakuwa mjanja na kutowekea Ughaibuni miaka kadhaa iliyopita, akiishi katika mojawapo ya nchi za Scandinavia.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa, wakati akiwa shuleni alikuwa na kipaji maalum cha sanaa na alikuwa ni bingwa wa kucheza na misamiati na nahau. Watu waliowahi kusoma naye wanakiri kuwa alikuwa na tatizo la kutomudu kutumia Tafsida pale alipotakiwa kutoa mada fulani katika midahalo ya shule.

Tatizo hilo lilikuwa likimletea matatizo na waalimu wake kwa kuwa alionekana kama vile hana adabu japokuwa ujumbe alioutoa ulikuwa na maana sana katika jamii na wenye kufundisha na kufikirisha pia. Hata hivyo wapo waliomuelewa na wengi walijifunza mengi kupitia hoja zake hizo zilizojaa vioja. Msome kwa kubofya hapa.

Pamoja na misukosuko aliyoipata kutoka kwa waalimu wake hakukata tamaa aliendeleza kipaji chake na baada ya kutowekea ughaibuni amekuwa muelimishaji mzuri kupitia kibaraza chake alichokipachika jina la Mawazoni.

Katika kibaraza hicho amekuwa akifikisha ujumbe wake wa kuielimisha jamii kwa kutumia misamiati nahau na tilalila zake anazozijua mwenyewe na kutokana na kutotumia Tafsida wengi wamekuwa hawamwelewi kwa kuwa wakisoma kichwa cha habari tu wanachoka na wanaacha, maana tafsiri inayokwenda akilini mwao ni kitu kingine badala ya kile kilichokusudiwa.

Tatizo ninaloliona katika makala zake si lugha iliyotumika bali ni tafsiri inayokwenda vichwani mwa wasomaji kwa kukimbilia kuhukumu kichwa cha habari badala ya kile kilichomo ndani ya hicho kichwa cha habari. Kwa mfano halisi unaweza kubofya hapa au hapa.

Ni mchangiaji mzuri sana katika vibaraza vya wengine na kwa kutumia staili hiyo hiyo ya Ant tafsida, amekuwa akiwachanganya wasomaji wengi na naomba nikiri kuwa hata mimi nilikuwa ni mmoja wapo wa wale waliokuwa hawamwelewi kabisa.

Ilinichukua muda kidogo kumwelewa na kwa kutumia kamusi ya Kiswahili na vitabu mbalimbali vya Kiswahili, kikiwamo kitabu kinachoitwa Titi la Mkwe na cha Jando na Unyago, nilimudu kumuelewa kijana huyu na makala zake zilizojaa nahau na upembuzi yakinifu.

Naamini hanifahamu na mimi pia simfahamu ila kwa kupitia vibarazani mwetu tumetokea kufahamiana japo si kwa karibu sana. Pamoja na hayo bado najiuliza hivi huyu kijana ni nani?

Wednesday, December 16, 2009

BARUA YA SIRI NA USHAURI WA BURE KWA DADA SUBI

Dada Subi

Kwako dada Subi, ni matumani yangu kuwa umzima wa Afya na unaendelea na kazi zako za kila siku huko uliko. Utakapo kujua hali zetu huku nyumbani, wote hatujambo, Isipokuwa yule babu yako anayeishi kule bondeni karibu na ule muembe mkuubwa uliokuwa ukitumika kama maegesho ya baiskeli za kukodisha, anasumbuliwa sana na ile henia yake na anahitaji operesheni ya haraka. Dada unajua siku hizi sio baiskeli tena zinazoegeshwa kwenye ule muembe bali ni pikipiki maarufu kama Yeboyebo ndio zinaegeshwa na watu wanazikodisha kwa ajili ya kupelekwa wanakokwenda kwa gharama nafuu.

Lakini dada usafiri huo sio salama sana kwani kina mama na mabinti hubakwa na waendsha pikipiki wakware lakini, kesi hizi zimekuwa haziripotiwi Polisi kutokana na wanaofanyiwa vitendo hivyo kuona haya, unajua dada mtu kuwaambia Polisi wetu kuwa umebakwa ni kashfa na aibu kwani unaweza kujikuta ukizomewa mtaani baada ya polisi kuvujisha siri kuwa umeonjwa bila ridhaa yako.

Dada naona tuachane na hayo ya kubakwa, nikweleze madhumuni ya barua hii. Dada siku za hivi karibuni tumeanza kupata wageni hapa kijijini, wageni wenyewe ni wale waliokuja kijijini kwetu kwa unyenyekevu miaka mitano iliyopita wakitaka tuwape Kula ili wapate ridhaa ya kingia katika lile jumba kubwa kule Dodoma kwa ajili ya kusinzia na kujipatia posho mara mbili. Watu hao ambao wakati ule walikuja wakiwa slimu na sasa wana matumbo makubwa na mabodi gadi wa kuwalinda wamekuja na mikoba myeusi iliyosheheni vijisenti kwa ajili ya kutughilibu tena ili tuwape ridhaa nyingine ya kuendelea kula nchi ndani ya jumba kubwa kule Dodoma wakipigwa na viyoyozi.

Dada Subi kama unavyojua kuwa siku hizi mambo yemebadilika na sio kama wakati ule, wananchi wameerevuka na wanajua haki zao. Si unakumbuka jinsi viongozi wetu walivyokuwa wakipata wakati mgumu katika ziara zao kwa kupokelewa na mabango yenye ujumbe, wakati mwingine wa kejeli, na wengine kufikia kuzomewa majukwaani na wananchi tena wa kijijini ambapo awali viongozi wetu walidai kuwa watu wa vijijini ni watu wa “ndio mzee”, lakini sasa hivi wamewageuka na kuwazodoa hadharani baada ya kuchoshwa na longolongo zao.

Lakini wakazi wa Mbeya ndio walitia fora kwani wao walithubutu kupopoa mawe msafara wa mwenye nchi, ingawa hata hivyo walionja joto ya Dola, naamini unakumbuka kilichowapata masikini wale. Dada kuerevuka huko kwa wananchi kumetokana na kuangalia Luninga, si unajua Luninga ndio mwalimu mzuri wa kuelimisha jamii siku hizi. Nakumbuka matukio hayo tulizoea kuyasikia kwa majirani zetu tena kupitia redioni hasa idhaa ya Kiswahili ya BBC wakati ule wa Mwalimu, lakini siku hizi tunaona kupitia kwenye luninga zetu kila uchao, kwanini tusiige.

Kutokana na ugeni huo yule mzee Makalioni ambaye ndiye mwenyekiti wa wazee pale kijijini aliitisha kikao cha dharura ili kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuchaguliwa kwa huyo mwakilishi wetu huko mjengoni (kama yapo) ili kujua kama kuna haja ya kumpa ridhaa zetu tena.

Kwa kifupi kikao kilithibitisha kuwa kati ya yale yote yaliyoahidiwa na mwakilishi huyo kuwa atawafanyia, yaani kujenga mahosipitali kila mtaa, kujenga majosho ya ng’ombe, si unajua sisi ni wafugaji japo hatuko kama wamasai wanaohamahama, basi huyu mwakilishi aliahidi kujenga majosho ya ngombe kila kaya, kujenga barabara na vituo vya polisi kwa ajili ya usalama wetu. Pia aliahidi kutuletea wawekezaji watakaojenga viwanda na kuleta ajira kwa vijana pale kijijini ambao walikuwa wanategemea kupata kipato kwa kilimo cha jembe la mkono. Aliahidi kuleta Matrekta kwa kila mwanakijiji kama akipata ridhaa ya kuingia mjengoni.

Kikao kiligundua kuwa kati ya yote yaliyoahidiwa na mwakilishi huyo ni asilimia 0.006 tu ndiyo yaliyotekelezwa mengine yaliwekwa pending kwa ajili ya kuombea ridhaa nyingine ya kuingia mjengoni miaka mitano ijayo. Ili kutuhadaa mwakilishi huyo emekuja na Katapila na sasa linatimua mavumbi hapo kijijini kwa madai kuwa wanajenga barabara, lakini kwa bahati mbaya wanakijiji wameshitukia janja yake.

Dada katika kikao hicho wazee waliazimia kuwaita vijana wao walioko Ughaibuni ili warudi kugombea nafasi ya uwakilishi mjengoni na nafasi nyingine za uongozi hapa kijijini. Katika nafasi ya uwakilishi yalijitokeza majina matatu, jina la kwanza lilikuwa la kwako, la pili lilikuwa ni la yule mtoto wa katibu kata aliyekwenda Ughaibuni miaka kumi iliyopita na kupotelea huko na jina la tatu ni la yule kijana anayezaliwa na yule fundi maarufu wa baiskeli mwenye wake wawili…….yule anayeishi jirani na Mbuyu jirani na gulio la kijiji, inasemekana kijana wake alizamia meli mara baada ya kumaliza fom foo na kulowea huko. Baada ya wazee kuyatafakari majina yote matatu, jina lako lilionekana kung’aa, baada ya kupata kura nyingi za wazee ambao wamekubaliana kuwa uitwe ili uje kugombea nafasi hiyo ya uwakilishi wa mjengoni.

Sababu kubwa iliyowavutia ni tule tumisaada twa dawa za binadamu na madawa ya mifugo ulitotuleta wakati ule ulipokuja kuwaona. Unajua mara baada ya kumwaga madawa katika ile zahanati ya kijiji sifa zako zilivuma hadi vijiji vya jirani na hivyo ukapata umaarufu wa haraka kama ule wa Nyerere wakati ule wa kumpinga mkoloni.

Sifa nyingine iliyokufanya uwe maarufu hapa kijijini ni pale ulipotoa msaada wa dharura kwa kumzalisha yule binti wa mzee mkalimbembe ambaye alipata matatizo wakati wa kujifungua kwa mtoto wake kutanguliza mkono badala ya kichwa. Kwa Juhudi zako na kwa kushirikiana na wauguzi wa zahanati ya kijiji uliweza kumzalisha binti huyo.

Sifa hiyo imekujenga sana hapa kjijini na sasa wanataka uje ugombee uwakilishi mjengoni ili uwaletee maendeleo, wazee wanadai kwa kuwa umeishi ughaibuni, utakuwa huna tamaa za kifisadi na utakuwa umeridhika sana na maisha kutokana na kuishi na wazungu kwa miaka mingi sana.

Dada taarifa hizi ni za siri na nimekutumia kupitia njia za panya kwani yule mwakilishi akijua anaweza kukuhujumu usipate viza ya kuingia nchini. Kwa hiyo kwa taarifa hii inabidi ujiandae kwani utatumiwa ujumbe muda si mrefu.

Friday, December 11, 2009

KISA CHA BARUA YA WAZI KWA YASINTA.......

Barua yangu ya wazi kwa dada yangu wa hiyari, Yasinta Ngonyani iliwachanganya wasomaji wengi hadi wengine walinitumia email ya kutaka ufafanuzi kwamba kulikoni tena mambo ya binafsi kuwekwa kibarazani?

Nilijua hilo litatokea na kweli limetokea, nimepokea email kadhaa zikinitaka nifafanue kile nilichoandika.

Kwanza naomba nichukue nafasi hii kumshukukuru dada Yasinta kwa kuniruhusu kuweka ile barua ya wazi katika kibaraza hiki nikidai kuwa namuandikia yeye. Naomba niweke wazi kwamba ile barua ilikuwa haimuhusu yeye na wala hakuwahi kuniandikia barua yoyote. Ile barua haikuwa ni ya kweli na wala haihusiani na mimi, ila kuna rafiki yangu mmoja niliyewahi kusoma naye ambaye aliwahi kuolewa mara tu baada ya kumaliza kidato cha 4.

Nakumbuka kila tulipokutana alikuwa akiniuliza kama nitaolewa lini. Siku moja aliniambia maisha ya ndoa ni mazuri na asiyeolewa labda ana matatizo kwa kuwa anakosa tamu ya ndoa. Nilimsikiliza na kumpuuza kwa kuwa nafahamu kuwa maisha ya ndoa hayana formula, yaani yanaweza kuwa mazuri kwa huyu na yakawa mabaya kwa yule. Hivi karibuni nimepata taarifa kuwa ndoa yake imeota mbawa na aliyempora mume ni nyumba ndogo na ndio nikajikuta nakaa na kuandika ule ujinga na kuuweka hapa.

Sikuwa namsimanga yule shoga yangu bali nilitaka kufikisha ujumbe kwa watu wenye mtizamo kama wake.

Wednesday, December 9, 2009

UBUNIFU WA FULANA NA UJUMBE WA MIPASHO



Fulana zetu na ujumbe wa Mipasho

Kama ningekuwa nimelisema hili humu katika kibaraza hiki, naamini wengi mungeniita mtabiri, lakini bahati mbaya nilikuwa bado sijaanza kublog.

Nakumbuka wakati fulani niliwahi kuwaambia wanafunzi wenzangu wakati huo nikiwa shule kuwa, tunapoelekea si ajabu kukaibuka fulana zenye ujumbe wa maneno ya Kiswahili kama vile yale yanayopatikana kwenye khanga. Hilo nililisema baada ya mwanafunzi mwenzetu mmoja kuvaa fulana ambayo aliiandika maneno ya Kiswahili kwa kutumia Marker Pen ambapo aliandika “MTACHONGA SANA” nadhani labda alikuwa akipeleka ujumbe kwa mahasimu wake ambao alitofautiana nao.

Hilo naona sasa limetimia. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao wamekuwa wakichapisha fulana kwa maneno yenye ujumbe tofauti tofauti kulingana na mahitaji ya jamii kwa kipindi hicho. Zamani tulizoea kuwa wanawake ndio wanaozodoana kwa kutumia maneno ya kwenye Khanga.

Kwa mfano maneno kama, “Utakufa nacho kijiba cha roho” Chuki nichukie roho yangu niachie” “kama unaweza panda juu ukazibe” Nakadhalika, nakadhalika, yalikuwa ni maneno yanayopatikana kwenye khanga peke yake na hiyo ndio iliyokuwa silaha pekee inayotumika na wanawake katika mapambano miongoni mwao hasa katika maeneo ya uswahilini.

Kwa kawaida kama wanawake wametofautiana katika mambo fulani fulani, badala ya kugombana kwa kupigizana kelele ilikuwa mtu ananunua khanga yake yenye ujumbe anaoutaka umfikie mbaya wake na kivaa makusudi ili kufikisha ujumbe aliokusudia kwa mwenzake.
Niliwahi kusimuliwa wakati fulani kuwa hata wale wanawake wanaochukuliana mabwana, nao walikuwa wakipambana kwa kuvaliana khanga zenye ujumbe wa kuzodoana na wakati mwingine mtu anaweza kumchokonoa mwenzake kwa kuvaa khanga zenye ujumbe tofauti tofauti hata saba kwa siku na kujipitisha kwa mbaya wake ili kumpa ujumbe aliokusudia na mara nyingi ilikuwa ni kawaida kwa mahasimu hao kuanza kurushiana maneno na hata kupigana hadharani kutokana na mmoja kukerwa na maneno ya kwenye khanga alizovaa mwenzie.

Tofauti na zamani, siku hizi mambo yamebadilika, na sasa sio khanga pekee, bali hata fulana siku hizi zimekuwa zikibeba ujumbe tofauti tofauti ukiwemo wa maneno ya kuzodoana. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao huchapisha ujumbe wa maneno ambayo tulizoea kuyaona kwenye khanga na kuyaweka kwenye fulana na hata Blouse na watu wamekuwa wakizigombea.

Sio kwamba sifurahii ubunifu huo wa mavazi, bali ninachojaribu kutahadharisha hapa ni aina ya ujumbe unaowekwa kwenye hizo fulana, kuwa usije ukatufikisha mahali watu wakatumia nafasi hiyo kuweka ujumbe wa matusi au hata maneno ya uchochezi, kwani kuna uwezekano ukatufikisha mahali tusipopatarajia.

Naamini wengi mtakuwa ni mashahidi wa hizi fulana au blouse za mitumba zinazoingia kutoka katika nchi za Magharibi na Ulaya ambazo zina ujumbe wa maandishi au hata picha tofauti tofauti. Tumekuwa tukishuhudia ujumbe wa Matusi au hata uchochezi wa kiubaguzi kupitia fulana hizo, lakini kwa kuwa zimeandikwa kwa kiingereza au lugha zao inakuwa ni vigumu walio wengi kung’amua maana halisi ya ujumbe huo labda mpaka mtu aambiwe, wengi tunachojali ni uzuri wa fulana lakini sio ujumbe ulioko katika fulana hizo.

Monday, December 7, 2009

BARUA YA WAZI KWA DADA YASINTA NGONYANI.....

Dada Yasinta Ngonyani

Kwako dada yangu mpendwa Yasinta Ngonyani mzaliwa wa Ruhuwiko Songea mkoani Ruvuma. Habari za siku nyingi na shikamoo zikufikie hapo ughaibuni ulipo, vipi kile kidole chako ulichijichoma na sindano ukishona nguo ya mwanano Camilla kinaendeleaje. Dada nilipokea taarifa za kujichoma kwako na sindano kwa masikitiko sana na sikuamini kuwa hata Ughaibuni mnatumia sindano za mkono kushona badala ya cherehani. Hata hivyo nakupa pole zako japo uliumia kwa uzembe mtupu.

Nashukuru barua yako uliyonitumia nimeipata jana ingawa mwandiko wako ulinipa shida sana kuusoma, na nimeshangaa sana kuwa hata watu walioko ughaibuni wanakuwaga na miandiko mibaya namna hii, usidhani nakukosea adabu dada yangu, naomba uniwie radhi kwani siwezi kuvumilia maudhaifu ya wengine na ndivyo nilivyoumbwa.

Dada dhumuni la barua hii nikutaka kujibu barua yako ya hivi karibuni ambayo ulinishauri eti niolewe kwa kuwa naanza kuzeeka sasa, dada katika barua yako hiyo umeeleza mengi sana juu ya faida za kuolewa. Umedai kuwa kuolewa ni kuondoa nuksi ili usife bila kuvaa pete ya ndoa, na pia ni fahari maana utakuwa huwajibiki kutunza familia hata kama unafanya kazi, kwani hiyo ni kazi ya mwanaume.

Umesema kuwa kwa mujibu wa mila na desturi tulizorithi kutoka kwa mababu na mabibi zetu ni kwamba wanaume ndio wanaowajibika kuwahudumia wake zao na watoto, yaani mwanamke hatakiwi kutoa hata senti tano kuchangia pato la familia kwa kuwa sio jukumu lake, kwani hilo ni jukumu la mume kwa maana yeye ndiye anayehakikisha familia yake inapata kila kitu, ikiwapo chakula, malazi, mavazi, na vipodozi kwa mkewe ili apendeze zaidi. Umesema kuwa kwa kawaida mwanamke ni pambo la nyumba kwa hiyo akibebana na majukumu ni saa ngapi atakuwa ni pambo la nyumba.

Pia umetoa sababu za kisayansi eti kwa jinsi mwanamke anavyozidi kuzeeka basi na mayai yake ya uzazi nayo yanazeeka kwa hiyo nikifikisha umri fulani nitakuwa sina uwezo wa kupata watoto wangu mwenyewe na kama nikibahatika kuwapata watakuwa mataahira au watumiaji wa mihadarati au Vibaka na wapiga debe.

Ukadai kuwa fahari ya ndoa ni watoto kwa hiyo kama nisipozaa ndoa yangu itaota mbawa, hata kama mume wangu atanipenda, mawifi na ndugu wa mume watachonga sana hadi niachike kwani katika ndoa za Kiafrika ndugu wana nguvu sana na wana uwezo wa kuamua hatima ya ndoa yenu watakavyo.

Ulitoa ushahidi mwingine kuwa wanaume wa siku hizi wanapenda kuona wanawake wanaowazidi umri kwa zaidi ya miaka 15 mpaka Ishirini kwa kuwa hao bado damu inachemka, kwa hiyo kwa jinsi ninavyozidi kuzeeka na ndivyo ninavyozidi kupoteza sifa ya kuolewa na kuwa disqualify kama ulivyosema mwenyewe kwa lugha ya kiingereza.

Niliisoma barua yako kwa makini sana na nilitafahari kwa kina, na ili kujiridhisha ikabidi na mimi nifanye utafiti wangu, unajua si vyema sana kuamini kila unaloambiwa hata kama ni kutoka kwa baba au mama yako mzazi. Dada sifa kubwa niliyo nayo ni kutokuwa dodoki kama alivyosema hayati mzee wa Mwitongo Mwalimu Nyerere.
Dada kuwa dodoki maana yake ni kubeba kila unaloambiwa bila kupima na kudadisi ili kujiridhisha, kama unavyojua dodoki ukilichovywa kwenye maji taka litatoka na kila aina ya uchafu, na ndio maana nikasema kuwa sitaki kuwa dodoki.

Katika utafiti wangu dada nimegundua kuwa madai yako hayana ukweli, kwani wanawake wengi walioolewa wanajuta sana na watamani kuachika kutokana na manyanyaso ya wanaume.

Dada kwa mujibu takwimu za chama cha mambo ya wanawake, kuna wanawake wengi wamepeleka malalamiko yao huko wakitaka kuachika kutokana na manyanyaso kutoka kwa waume zao. Wanawake hao wanadai kuwa kigezo wanachotoa wanaume hao kuwanyanyasa ni mahari waliyolipa kwa wazazi wao.

Wanawake hao wanadai kuwa manyanyaso wanayopata yanategemea kiwango cha mahari waliyotozwa hao wanaume wao, kwa hiyo inakuwa ni vigumu kwa wale waliolipiwa mahari kubwa kudai talaka kwa kuwa wazazi washakula chao mapema kwa hiyo hawana uwezo wa kurudisha mahari ya watu na hivyo wanajaribu kutafuta wafadhili toka nje ili wawanasue katika ndoa hizo za mateso.

Wanawake hao wanatafuta uwezekano wa kubadili mila na desturi zetu ili wanawake ndio wawe wanaoa na kulipa mahari kama wahindi kwani kule India wenzetu wanawake ndio wenye sauti kuliko wanaume na ndio maana India na Pakistani zimewahi kutawaliwa na wanawake kama vile mama Indira Gandhi na Benaziri Bhuto ambao wote waliuwawa kwa husuda tu, na wale wanaume wanaotaka mfumo dume kama huu uliotamalaki huku kwetu

Dada kama wewe ni msomaji wa vitabu vitakatifu vya dini zetu hizi za mapokeo utakubaliana na mimi kuwa hata mwenyezi Mungu amewapendelea sana wanaume kiasi cha kuwapa kibri. Hebu soma maandiko matakatifu ya Biblia katika kitabu cha Waefeso 5, 22:24.

Dada maandiko hayo ndiyo yanawapa wanaume kibri kwa kudai kuwa wao ndio vichwa vyetu wakati vichwa vyetu tunavyo na tunatembea navyo.

Kwa hiyo dada ushauri wako kwangu nauona kama unataka kunipalia makaa ya moto ili tufanane wakati mie nimeshawashitukia wanaume zamani sana.
Najua utashangazwa na uamuzi wangu kwa kuwa ulitegemea nikubaliane na ushauri wako lakini napenda kukukatisha tamaa kuwa mie nimeshawashitukia wanaume siku nyingi.

Dada mimi ni mjanja………..LOL

Friday, December 4, 2009

MATEJA NA UTAMU WA TENDO LA KUJAMIIANA!


Mimi kwa kawaida ni mdadisi sana, na naomba nikiri kuwa udadisi wangu uliwahi kuniletea matatizo wakati fulani. nakumbuka nilikuwa naendesha gari katikati ya jiji, na wakati nimesimama kwenye taa za kuongozea magari,akaja mama mmoja ombaomba ambaye namkadiria kufikisha umri wa miaka 60 hivi.
Alionekana kuwa na afya njema tu. Alipofika pale nilipo aliniomba pesa, nilitoa kiasi cha fedha na kumpa, lakini nilimuuliza kwa upole kwamba kwa nini anaomba barabarani wakati afya yake ni nzuri tu. mama wee....alinishambulia kwa matusi na kama sio taa za barabarani kuniruhusu labda angenipasulia kioo cha gari langu, kwani nilimuona kupitia kioo cha pembeni akiokota kitu nadhani kwa ajili ya kunirushia, lakini alichelewa kwani nilishafika mbali. Tukio hilo lilinikumbusha tukio lililompata dada yangu Yasinta Ngonyani na mwendawazimu wa Ruhuwiko Songea.

Ngoja nirejee kwenye kile nilichotaka kusimulia leo. Nimesema kuwa mimi ni mdadisi sana, na udadisi wangu naona saa utaniletea matatizo, lakini sitaki kuacha na sijui ni kwanini. Juzi nikiwa kwenye Intenert Cafe moja iliyopo maeneo ya Mikocheni nilikutana na kaka mmoja ambaye ni mtumiaji wa madawa ya kulevya, maarufu kama Teja. Kijana huyo ambaye nilisoma naye shule moja akiwa amenitangulia darasa moja mbele, alikuwa akisifika sana kutokana na kuwa na akili sana darasani wenyewe tulikuwa tunaita akili za Nature, na mpaka tukawa tunamuita Nature kutokana na kuwa na akili ambazo sio za kawaida.

Alifanikiwa kufaulu na kuendela na masomo ya sekondari, nasikia alifaulu kidato cha nne na kuingia kidato cha tano na kupangiwa kwenda shule moja maarufu mkoani Tanga na huko ndipo alipojitumbukiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na kuwa Teja kiasi cha kusababisha kufukuzwa shule na kurejea jijini na kuendela na tabia hiyo.

Nilipokutana naye pale cafe nilipiga naye stori mbili tatu na ndipo nikamuuliza swali, kwamba kwa nini amejiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya wakati alikuwa na maendeleo mazuri shuleni. Nilimuona akibadilika ghafla kama vile amekasirika, niliona mambo si shwari, ikabidi nimuwahi kumuomba radhi kwa swali langu la kijinga, lakini aliniambia kuwa hajakasirika, na kwa upole akaniuliza swali......

"Samahani Da' mdogo Koero, hivi unajua utamu wa tendo la kujamiiana?" Nilishangazwa la swali lile, lakini kwa kuwa niliyataka mwenyewe nikajikuta nikimjibu kuwa nafahamu. Kisha akaniuliza tena..... "Je Unajua utamu wa tendo la kujamiiana unadumu kwa muda gani katika ubongo wa binadamu?" Duh! hili lilikuwa ni swali gumu kwangu na nilijua sasa na mimi nimepatikana maana nilijifanya kuwa mdadisi, lakini sasa mambo yananigaeukia.

Nilijikakamua na kumjibu kwa kifupi. "Sijui maana sijawahi kufanya utafiti huo"
Yule kijana kwa upole akaniambia, "kwa kuwa umeuliza swali basi nitakujibu tena kwa ufasaha ili wakati mwingine usije ukauliza tena kwa mtu mwingine"

Aliniambia kuwa kwa mujibu wa tafiti mbalimbali imebainika kuwa utamu wa tendo la kujamiiana unadumu katika ubongo wa binadamu kwa sekunde tano tu, mtu anapofikia kileleni, lakini mtu anapotumia madawa ya kulevya, yaani pale anapojidunga dozi, ule utamu anaoupata ambao unafanana na utamu wa tendo la kujamiiana unadumu kwa dakika kumi na tano.
Kisha akaendelea kusema kuwa, kama utamu wa kujamiiana ambao hata hivyo unadumu kwa sekunde tano tu, lakini watu wanaupenda kupita kiasi huku wengine wakihatarisha maisha yao dhidi ya gonjwa la ukimwi na wengine wakitiana ngeu au hata kuuana kwa sababu ya utamu huo, kwa nini yeye asiamue kuwa Teja ambapo anaweza ku-enjoy kwa takribani dakika kumi na tano bila bughdha kwa kitu ambacho hakimpi usumbufu.

Wakati wote akinipa darasa hilo nilibaki nimemtumbulia macho kwa mshangao na nisiamini kile alichokuwa akinisimulia. Kusema kweli sikuwa na swali la nyongeza, nilimshukuru kwa majibu yake nikamuaga ili niondoke, lakini alinitaka nimuachie hela akapate kete yake ili apate stimu kwani nilimvurugia stimu yake kwa kumuuliza lile swali.

Sikutaka kugombana naye, nilitoa kiasi cha pesa na kumpa, kisha nikaondoka. Yaani kiranga kiliniisha, maana sikutegemea yale majibu ambayo yalikuwa na ushahidi wenye utafiti ambao hata sikujua kama utafiti ule una ukweli kiasi gani.

Hata hivyo kwa umbeya wangu nimeona niiweke hii habari hapa kibarazani ili nilete changamoto toka kwa wadau na wasomaji wa blog hii.