Friday, December 25, 2009

BAADA YA KUTIMIZA MWAKA MMOJA LEO TANGU KUANZISHWA KWAKE BLOG YA VUKANI KUFUNGWA RASMI LEO

Kwa herini ya kuonana

Leo tarehe 25 December 2009 Blog hii ya VUKANI Inatimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake. Ni jambo la kujivunia kwamba ndani ya mwaka mmoja nimeweza kuweka makala 100 na nimemudu kuendelea kublog hata pamoja na majukumu mbalimbli ya kifamilia niliyokuwa nayo. Nilikuwa nikisafiri mara kwa mara lakini hata hivyo niliweza kuweke post kama kawaida ili wasomaji wa blog hii waendelee kusoma ujinga wangu.

Najua tangu nianze kublog kuna watu niliwakwaza na wengine niliwafurahisha na hata kuwafikirisha, lakini halikuwa lengo langu kumuumiza mtu kihisia kwa namna yoyote ile kwani lengo la blog hii ni kuelimisha, kufikirisha, na kufurahisha. Naamini malengo ya uwepo wa blog hii yalitimia kwa kiasi fulani.

Kama nilivyosema kuwa blog hii itakuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo, naamini yote hayo yalitimia na ndio maana leo natimiza mwaka mmoja nikijivunia kile nilichokifanya hadi leo.
Najua si rahisi kufanya tathmini na kujua kama ni wasomaji au wanablog wangapi ambao kwa njia moja ama nyingine wamejifunza au wamenufaika na huu ujinga wangu, ninaouweka humu lakini naamini kwa kiasi fulani kuna wengi wamejifunza na kunufaika na uwepo wa blog hii.

Kama kumbukumbu zenu haziko mbali, kwa wale wafuatiliaji wa blog hii watakumbuka kuwa, blog hii ilianza na misukosuko mingi, kwani karibu mara mbili nilipata shinikizo la wazazi wangu kuifunga na kuachana na mambo ya kublog, baada ya kuibua hoja ya kuhoji swala zima la nadharia ya hizi dini zetu za mapokeo, kama unataka kujikumbusha bofya hapa
NIMEANZA KUZISHITUKIA HIZI DINI. Mada hiyo iliwashitua sana wazazi wangu, ambapo walinitaka niache kublog kama sina mambo ya maana ya kuandika, swala la kuhoji uhalali wa dini likaonekana halina maana.

Nililazimika kuufunga ule mjadala ili kunusuru mahusiano yangu na wazazi wangu. Mara ya pili ni pale nilipopingana na wazazi wangu juu ya swala la kuendelea na elimu, baada ya kuacha chuo na kujikita kwenye biashara zaidi, hiyo nayo ilikuwa ni changamoto nyingine, lakini kutokana na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa blog hii nilimudu kuyamaliza na hivyo kuendelea kublog kama kawaida.

Naomba nikiri kwamba uwepo wa blog hii ni kutokana na kuvutiwa na blog ya MAISHA ya dada Yasinta Ngonyani, kwani ni yeye aliyenifanya nami nianze kublog na kwa msaada wa mdogo wangu Jerome kwa utundu wake aliweza kuifungua blog hii.

Pia siwezi kuepuka kumtaja kaka Markus Honorius Mpangala aka MCHARUKO kwani na yeye kwa upande wake alichangia kuifanya blog hii ionekane kama ilivyo leo. Pia siwezi kuepuka kumtaja kaka yangu mpendwa Mubelwa Bandio kwa kuwa karibu nami akinishauri hili na lile juu ya namna nzuri ya kublog, na pia amekuwa ni mhariri wangu mahiri akinisaidia kurekebisha lugha na namna nzuri ya kujenga hoja katika makala zangu.

Salaam kwako dada yangu Yasinta ngonyani, wewe ni dada yangu mpendwa, siwezi kuwataja dada zangu Debora Damari, na Rachel bila kukutaja wewe dada yangu mpendwa. Dada kwa kweli upendo wako ni wa ajabu kwangu umekuwa karibu nami na nimekuwa nikikufanyia masihara mengi na utani mwingi licha ya kwamba umenizidi sana umri. Umekuwa ni mshauri mwema kwangu juu ya mambo mengi yahusuyo maisha. Umechangia kwa kiasi kikubwa katika kunibadili kitabia kutokana na hekima zako, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa wema wako.

Kwako dada Subi, nawe kwa upande wako ninayo mengi ya kujivunia, umenifunza mengi na umenifanya nikue kifikra, wewe umekuwa mmoja kati ya dada zangu na nimekuwa nikijivunia sana kukufahamu, pokea salaam zangu.

Kaka yangu Mbwange Simon Mkodo Kitururu, Duh! Sina la kusema, kupitia blog yako na maoni yako nimejifunza mengi. Kwani kupitia blog yako ya Mawazoni nimejifunzza kuwa hakuna lugha ya matusi, bali kuna majina yanayowakilisha viungo vya mwili, miti, wanyama na vitendo, lakini kutokana na tafsiri tulizofundishwa tumekuwa tukiamini kuwa baadhi ya majina ya viungo vya mwili, wanyama miti na baadhi ya vitendo ni matusi.

Pia siwezi kumsahau kaka yangu wa kulikoni Ughaibuni Evarist Chahali, wewe ulikuwa ni msomaji mmojawapo uliyeweka changamoto zako humu na kuibua mijadala mikubwa na hata kuleta mgongano wa mawazo, najua ni siku nyingi hatujawasiliana lakini naamini unaikumbuka VUKANI.

Kaka yangu Profesa Matondo, sijui niseme nini, lakini wewe mwenyewe unajua ni kiasi gani umenisaidia kukua kifikra, ni jambo la kujivunia kuwa pamoja na Elimu yako na shughuli zako nyingi uliweza kurudi chini na kuweza kuzungumza nami kama vile kaka azungumzaye na mdogo wake tumbo moja. Umekuwa mshauri wangu katika masuala mbalimbali ya kielimu na kijamii, heshima kwako Profesa Matondo.

Kwako kaka Shabani Kaluse, aka baba Abraham, Mzee wa Utambuzi, naomba nikiri wazi kuwa kupitia kibaraza chako nimejifunza mambo mengi juu ya utambuzi na nimebadilika sana kitabia, umekuwa ukijibu email zangu binafsi na kunishauri mambo mengi sana juu ya maisha na mafanikio. Umekuwa mhariri wangu mzuri pale ninapotaka kuweka makala za kijamii umekuwa ukinishauri namna nzuri ya kujenga hoja. Nakushukuru sana kaka kwa wema wako.

Dada Schola Mbipa, heshima kwako dada, nakushukuru kwa ushauri mbalimbali uliokuwa ukinipa ili kuiboresha blog hii.

Uuuuwiiii!!!!! Jamani nusura nimsahau Kamala Lutatinisibwa, huyu naye kwa kweli amenifundisha mambo mengi sana juu ya Utambuzi, maoni yake yamekuwa yakileta changamoto katika blog zetu hizi na kuibua mijadala ya hapa na pale, huyu ni mdau mmojawapo ambaye amenifanya nisifikirie kuacha kublog.
Ngoja niwanong’oneze siri, kusema kweli kama nikiweka makala katika kibaraza hiki halafu Kamala asiweke maoni nahisi kama mada yangu haijakamilika….LOL, kwani ni mdau mmojawapo ambaye lazima akiweka maoni utapenda kuyarudia kuyasoma mara kadhaa, sio kwa kutokuelewa bali kwa kutafakari zaidi, maoni yake mara nyingi yanafikirisha.


Najua ni wengi, wengi sana waliojitokeza katika blog hii na kuweka maoni yao au kunitumia email binafsi wakinishauri hili na lile ili kuiboresha blog hii, pia wapo waliotaka mawasiliano nami ya karibu lakini kutokana na kutingwa nimeshindwa kutekeleza hilo, lakini naomba muamini kuwa tupo pamoja.

Kwa uchache niwataje hawa wafuatao ambao kwa njia moja ama nyingine wamekuwa ni chachu ya kufanikisha uwepo wa blog hii, kaka Damas Michael, Godwin Meghji, kaka Kisima, kaka Manento Kitururu, kaka James Jim, kaka Chib, Dada My Little World, kaka John Mwaipopo, kaka Edo Ndaki, Mummy Hery, Da' Mija na wengine wengi. Niliowasahau mtanisamehe jamani nafasi ni ndogo……LOL.

Sasa naomba mniruhusu kuifunga rasmi blog hii ili niweze kufanya mambo mengine ambayo naamini yatakuwa bora zaidi ya kublog.

Ahsanteni na kwaherini wote, tutawasiliana mungu akipenda.

Ahsanteni sana kwa ushirikiano wenu katika kipindi chote nilipokuwa nikiblog.
Nawapenda wote jamani, Mungu awe nanyi milele daima…..aaaaamen

17 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Kuukubali ukweli wa kukuruhusu wewe kuacha ku-blog ni jambo lisilo la mzaha. Ni ngumu kukuacha uende ilhali kila siku umekuwa ukiibua mijadala, habari, maswali na maandiko yaliyonifanya niendelee kujivunia uwepo wako kama nijivuniao wa wengi
Lakini nakubaliana nawe katika hili kwa kuwa umeomba na hapa nanukuu "kufanya mambo mengine ambayo naamini yatakuwa bora zaidi ya kublog"
Mara zote nimekuwa nikikutakia lililo jema na sitasita kufanya hivyo
Na kama ufanyalo ni jema zaidi ya ku-blog, sina ninalokuombea zaidi ya mafanikio huko uhamishiako juhudi.
Bado ntaendelea kutembelea na kujikumbusha mijadala mbalimbali, kui-desa na kupata mawazo ya kile niwezacho kuandika
MWISHO najua kuwa HUJAACHA KU-BLOG bali utakapopata hili na lile la kutushirikisha utafanya hivyo. Ni kuwa hatutakutegemea kubandika maandiko kila siku ila twajua mara chache chache utakuwa nasi.
UNAPENDWA KAMA ILIVYO SIKU ZOTE NA NAJIVUNIA KUKUFAHAMU
Blessings

Yasinta Ngonyani said...

NO, NO, NO, Koero napenda kuamini katika nafsi yangu kuwa unatania tu hapa. Kuacha kublog? Koero nashindwa la kusema na nahisi natokwa na machozi kwani mada zako, mijadala yako vimekuwa ni vya kuelimisha na umekuwa iunainua mijadala sasa leo nini. Kwa kweli kwa mimi hili ni pigo haswa.

Ila kama kweli umeamua hivyo basi ni uamuzi wako. Kwa sababu kila binadamu anajua napoamua kitu anafanya nini. Koero nakutakia kila jema na lolote utakalofanya na pia unajua ni vipi najisikia NAKUPENDA SANA MDOGO WANGU nadhani unajua.

Candy1 said...

Blog inafungwa?...are you kidding me?...Sorry just somehow siwezi kuamini ila naona habari ndio hiyo.

Anyway japo nimeingia kijijini kwa miezi kadhaa or niseme muda mfupi, ila nime-enjoy kila post iwekwayo hapa. Post zako zilikuwa zinanifundisha, kunipa fikira na kunichekesha pia. It was such an entertainment to me that I can't believe you are actually closing it :-(.Ila ndio uamuzi wako dada.

Mungu awe nawe pia dada na baraka zake zote! Nitaku"miss" kweli yaani!!! dah!

SIMON KITURURU said...

:-(

Godwin Habib Meghji said...

SITAKI KUAMINI.... NA ITANICHUKUA MUDA KUKUBALI.
Inawezekana una sababu nzito za kufanya hivyo...
MIMI BADO NINA AMINI KUBLOG NI SEHEMU YAKO YA MAISHA, NI KARAMA NA KIPAJI ULICHOPEWA NA MOLA. KWA KUTOENDELEA KUKITUMIA, UTAKUWA HUJATUNDENDEA HAKI WAPENZI WA BLOG HII.

kwa imani hiyo niliyokuwa nayo(KUBLOG NI SEHEMU YA MAISHA YAKO) naamini huwezi kuacha moja kwa moja...( NIMEJISHTUKIA NAJIFARIJI...)

Nikutakie tu mafanikio mema kwenye hizo shughuli zilizo muhimu kuliko kublog...

Fadhy Mtanga said...

Is it?

Markus Mpangala said...

..............

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Koero anatania tu. Naamini NIKO SAHIHI!

PASSION4FASHION.TZ said...

OMG....Kulikoni???
Jamani mbona nashindwa kuamini? katika blog nazopenda kusoma hii ni mojawapo,sasa tutapata wapi hadithi na mafundisho ya bibi Koero? Emcheku!!!

Mmmh! ni ngumu lakini inabidi tueshimu maamuzi yako au Emcheku ya kwa bibi Koero ilijibu? tuambie ili tuanze kujiandaa kuja kucheza mduara hahahhaaa! au umejiingiza kwenye siasa weye?? maana kampeni ndio zilisha anza..LOL

Sio rahisi kuamini kama kweli leo ndio mwisho lakini usiache kututembelea vibarazani kwetu upatapo nafasi,hata kama ni kampeni za uchaguzi usisite kutushirikisha tukupigie debe...hahahahhahaa!

Merry xmas and happy new year naomba ukienda kwa bibi Koero au hata kama ukiongea nae kwenye simu mpe salamu zangu japokua ndio hatutapata tena simulizi zake.
much love.xx

Mzee wa Changamoto said...

Dada Koero
Kwa niaba ya familia yangu na wapenda mema wote nakutakia kila lililo jema wakati huu wa sikukuu na usalama kuelekea mwaka mpya
Baraka kwako

Kissima said...

Dada, ni vigumu kuamini, lakini kama ndivyo, nakutakia kila lenye Heri, mafanikio tele kwa kila jema ulifanyalo.
Naamini bado tupo pamoja kwani kama hutofundishia kwenye darasa lako basi elimu utaitoa kwa kupitia madarasa ya wengine. Binafsi nimekuwa nikiifurahia saaaaana blog yako kwani sikuwa natamani chochote ukiandikacho kinipite,japokuwa nimekuwa nikiweka maoni yangu mara chache.

Da! Lakini hapana, ni kweli dada au watania tu? Hebu tusubirie tuone ni kwa namna gani utafunga mjadala huu. Pengine watuweka tumbo joto tu.

mumyhery said...

ndio imekuwa hivyo tena?

Mija Shija Sayi said...

Ngoja nilie, nikishamaliza ndo ntarudi kujua kulikoni?!!!!!

Markus Mpangala. said...

?????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????????

Markus Mpangala. said...

Leo nimepata angalau neno la kuandika hapa tokana na hii habari. Daima nilikuwa kimya.

UKWELI WANGU.
Sijanyoa msiba, ila nipo katika maombezi na maombolezo. Walau nijifariji kwakuwa naweza kujifariji.

HATA HIVYO

NAMHITAJI SANA DADA ASIMWE, ni 'WANTED' sana, mmesahahu wanablogu??????????????

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

Chenye mwanzo kina mwisho. kutengnana siku zoote huwa ni kugumu sana. vitu vyote, huishia kwa kutengana. ila ni muhimu kutengana ili tujekukutana tena na kuwa pamoja!!!!

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___