Wednesday, December 16, 2009

BARUA YA SIRI NA USHAURI WA BURE KWA DADA SUBI

Dada Subi

Kwako dada Subi, ni matumani yangu kuwa umzima wa Afya na unaendelea na kazi zako za kila siku huko uliko. Utakapo kujua hali zetu huku nyumbani, wote hatujambo, Isipokuwa yule babu yako anayeishi kule bondeni karibu na ule muembe mkuubwa uliokuwa ukitumika kama maegesho ya baiskeli za kukodisha, anasumbuliwa sana na ile henia yake na anahitaji operesheni ya haraka. Dada unajua siku hizi sio baiskeli tena zinazoegeshwa kwenye ule muembe bali ni pikipiki maarufu kama Yeboyebo ndio zinaegeshwa na watu wanazikodisha kwa ajili ya kupelekwa wanakokwenda kwa gharama nafuu.

Lakini dada usafiri huo sio salama sana kwani kina mama na mabinti hubakwa na waendsha pikipiki wakware lakini, kesi hizi zimekuwa haziripotiwi Polisi kutokana na wanaofanyiwa vitendo hivyo kuona haya, unajua dada mtu kuwaambia Polisi wetu kuwa umebakwa ni kashfa na aibu kwani unaweza kujikuta ukizomewa mtaani baada ya polisi kuvujisha siri kuwa umeonjwa bila ridhaa yako.

Dada naona tuachane na hayo ya kubakwa, nikweleze madhumuni ya barua hii. Dada siku za hivi karibuni tumeanza kupata wageni hapa kijijini, wageni wenyewe ni wale waliokuja kijijini kwetu kwa unyenyekevu miaka mitano iliyopita wakitaka tuwape Kula ili wapate ridhaa ya kingia katika lile jumba kubwa kule Dodoma kwa ajili ya kusinzia na kujipatia posho mara mbili. Watu hao ambao wakati ule walikuja wakiwa slimu na sasa wana matumbo makubwa na mabodi gadi wa kuwalinda wamekuja na mikoba myeusi iliyosheheni vijisenti kwa ajili ya kutughilibu tena ili tuwape ridhaa nyingine ya kuendelea kula nchi ndani ya jumba kubwa kule Dodoma wakipigwa na viyoyozi.

Dada Subi kama unavyojua kuwa siku hizi mambo yemebadilika na sio kama wakati ule, wananchi wameerevuka na wanajua haki zao. Si unakumbuka jinsi viongozi wetu walivyokuwa wakipata wakati mgumu katika ziara zao kwa kupokelewa na mabango yenye ujumbe, wakati mwingine wa kejeli, na wengine kufikia kuzomewa majukwaani na wananchi tena wa kijijini ambapo awali viongozi wetu walidai kuwa watu wa vijijini ni watu wa “ndio mzee”, lakini sasa hivi wamewageuka na kuwazodoa hadharani baada ya kuchoshwa na longolongo zao.

Lakini wakazi wa Mbeya ndio walitia fora kwani wao walithubutu kupopoa mawe msafara wa mwenye nchi, ingawa hata hivyo walionja joto ya Dola, naamini unakumbuka kilichowapata masikini wale. Dada kuerevuka huko kwa wananchi kumetokana na kuangalia Luninga, si unajua Luninga ndio mwalimu mzuri wa kuelimisha jamii siku hizi. Nakumbuka matukio hayo tulizoea kuyasikia kwa majirani zetu tena kupitia redioni hasa idhaa ya Kiswahili ya BBC wakati ule wa Mwalimu, lakini siku hizi tunaona kupitia kwenye luninga zetu kila uchao, kwanini tusiige.

Kutokana na ugeni huo yule mzee Makalioni ambaye ndiye mwenyekiti wa wazee pale kijijini aliitisha kikao cha dharura ili kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuchaguliwa kwa huyo mwakilishi wetu huko mjengoni (kama yapo) ili kujua kama kuna haja ya kumpa ridhaa zetu tena.

Kwa kifupi kikao kilithibitisha kuwa kati ya yale yote yaliyoahidiwa na mwakilishi huyo kuwa atawafanyia, yaani kujenga mahosipitali kila mtaa, kujenga majosho ya ng’ombe, si unajua sisi ni wafugaji japo hatuko kama wamasai wanaohamahama, basi huyu mwakilishi aliahidi kujenga majosho ya ngombe kila kaya, kujenga barabara na vituo vya polisi kwa ajili ya usalama wetu. Pia aliahidi kutuletea wawekezaji watakaojenga viwanda na kuleta ajira kwa vijana pale kijijini ambao walikuwa wanategemea kupata kipato kwa kilimo cha jembe la mkono. Aliahidi kuleta Matrekta kwa kila mwanakijiji kama akipata ridhaa ya kuingia mjengoni.

Kikao kiligundua kuwa kati ya yote yaliyoahidiwa na mwakilishi huyo ni asilimia 0.006 tu ndiyo yaliyotekelezwa mengine yaliwekwa pending kwa ajili ya kuombea ridhaa nyingine ya kuingia mjengoni miaka mitano ijayo. Ili kutuhadaa mwakilishi huyo emekuja na Katapila na sasa linatimua mavumbi hapo kijijini kwa madai kuwa wanajenga barabara, lakini kwa bahati mbaya wanakijiji wameshitukia janja yake.

Dada katika kikao hicho wazee waliazimia kuwaita vijana wao walioko Ughaibuni ili warudi kugombea nafasi ya uwakilishi mjengoni na nafasi nyingine za uongozi hapa kijijini. Katika nafasi ya uwakilishi yalijitokeza majina matatu, jina la kwanza lilikuwa la kwako, la pili lilikuwa ni la yule mtoto wa katibu kata aliyekwenda Ughaibuni miaka kumi iliyopita na kupotelea huko na jina la tatu ni la yule kijana anayezaliwa na yule fundi maarufu wa baiskeli mwenye wake wawili…….yule anayeishi jirani na Mbuyu jirani na gulio la kijiji, inasemekana kijana wake alizamia meli mara baada ya kumaliza fom foo na kulowea huko. Baada ya wazee kuyatafakari majina yote matatu, jina lako lilionekana kung’aa, baada ya kupata kura nyingi za wazee ambao wamekubaliana kuwa uitwe ili uje kugombea nafasi hiyo ya uwakilishi wa mjengoni.

Sababu kubwa iliyowavutia ni tule tumisaada twa dawa za binadamu na madawa ya mifugo ulitotuleta wakati ule ulipokuja kuwaona. Unajua mara baada ya kumwaga madawa katika ile zahanati ya kijiji sifa zako zilivuma hadi vijiji vya jirani na hivyo ukapata umaarufu wa haraka kama ule wa Nyerere wakati ule wa kumpinga mkoloni.

Sifa nyingine iliyokufanya uwe maarufu hapa kijijini ni pale ulipotoa msaada wa dharura kwa kumzalisha yule binti wa mzee mkalimbembe ambaye alipata matatizo wakati wa kujifungua kwa mtoto wake kutanguliza mkono badala ya kichwa. Kwa Juhudi zako na kwa kushirikiana na wauguzi wa zahanati ya kijiji uliweza kumzalisha binti huyo.

Sifa hiyo imekujenga sana hapa kjijini na sasa wanataka uje ugombee uwakilishi mjengoni ili uwaletee maendeleo, wazee wanadai kwa kuwa umeishi ughaibuni, utakuwa huna tamaa za kifisadi na utakuwa umeridhika sana na maisha kutokana na kuishi na wazungu kwa miaka mingi sana.

Dada taarifa hizi ni za siri na nimekutumia kupitia njia za panya kwani yule mwakilishi akijua anaweza kukuhujumu usipate viza ya kuingia nchini. Kwa hiyo kwa taarifa hii inabidi ujiandae kwani utatumiwa ujumbe muda si mrefu.

7 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Barua imetulia hiyo. Haya Da Subi zamu yako leo, kwa hiyo fanya haraka huko uliko jiandae ujembe ukifika tu unyanyuke. Lol

Markus Mpangala. said...

chagua moja

Faustine said...

Barua imeandikwa vizuri kwa kiswahili fasaha....Kazi nzuri...Hongera mwandishi

Faustine
drfaustine.blogspot.com

Candy1 said...

hahahahha! mie nazipenda hizi barua kweli yaani usipotoka na kitabu mwaka ujao dada Koreo yaani dah...anyway back to the letter, hawa viongozi wetu mmh...sijui tufanye nini... sasa dada Subi utagombea? hehehehe

SIMON KITURURU said...

Hivi kusoma barua za siri za watu wengine sio tabia mbaya?

Mzee wa Changamoto said...

Mie nimeisoma mara mbili na moja zaidi kisha nikafikiria mengi. Simfikirii Subi (maana sidhani kama atakuja abda wamwambie ataweza ku-access facebook huko. Si mwajua addiction yake)
Lakini nafikiria ukweli huu ulioelezwa kwa style ya kipekee ya kuburudisha. Ulilofanya Da Mdogo Koero ni kutueleza ukweli wa mambo katika mtiririko usiochosha maana ulishashitukia kuwa habari hizi za kisisasa ungeziweka katika mfumo wa "moja kwa moja" ungetusinziisha nayo.
Labda ninukuu kipande kilichonifurahisha na ambacho nawaza KWANINI HAWAFANYI HIVI?? Umesema "Kutokana na ugeni huo yule mzee Makalioni ambaye ndiye mwenyekiti wa wazee pale kijijini aliitisha kikao cha dharura ili kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuchaguliwa kwa huyo mwakilishi wetu huko mjengoni (kama yapo) ili kujua kama kuna haja ya kumpa ridhaa zetu tena."
Hili nimeliandika na kulilia saana./ Haya ndiyo wanayostahili kuyafanya watendaji wa vijiji na sio MAIGIZO YA RAIS. Watendaji wanastahili kukutana na kujadili kama aliye madarakani amewahudumia kwa manufaa ya wanakijiji kama alivyoahidi ama la, na kama hajafanya hivyo basi "apigwe chini kwa kauli moja". Tungekuwa na umoja wa hivyo wala tusingepata shari, kwani wagombea wngeanza kuhesabu kuwa kijiji hiki na hiki na hiki na kile sina changu. Ni bora nirejee kutekeleza ahadi, la sivyo huu ndio muhula wa mwisho kiyoyozini.
Asante kwa kutufikirisha. Asante kwa kutuchangamotoosha na kutupenda mpaka ukamtoa kafara Dadako pekee Subi, ili kila ampendaye asikose kusoma bali awe na hekima zaidi.
Luv ya Sis
Blessings

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___