Wednesday, December 9, 2009

UBUNIFU WA FULANA NA UJUMBE WA MIPASHOFulana zetu na ujumbe wa Mipasho

Kama ningekuwa nimelisema hili humu katika kibaraza hiki, naamini wengi mungeniita mtabiri, lakini bahati mbaya nilikuwa bado sijaanza kublog.

Nakumbuka wakati fulani niliwahi kuwaambia wanafunzi wenzangu wakati huo nikiwa shule kuwa, tunapoelekea si ajabu kukaibuka fulana zenye ujumbe wa maneno ya Kiswahili kama vile yale yanayopatikana kwenye khanga. Hilo nililisema baada ya mwanafunzi mwenzetu mmoja kuvaa fulana ambayo aliiandika maneno ya Kiswahili kwa kutumia Marker Pen ambapo aliandika “MTACHONGA SANA” nadhani labda alikuwa akipeleka ujumbe kwa mahasimu wake ambao alitofautiana nao.

Hilo naona sasa limetimia. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao wamekuwa wakichapisha fulana kwa maneno yenye ujumbe tofauti tofauti kulingana na mahitaji ya jamii kwa kipindi hicho. Zamani tulizoea kuwa wanawake ndio wanaozodoana kwa kutumia maneno ya kwenye Khanga.

Kwa mfano maneno kama, “Utakufa nacho kijiba cha roho” Chuki nichukie roho yangu niachie” “kama unaweza panda juu ukazibe” Nakadhalika, nakadhalika, yalikuwa ni maneno yanayopatikana kwenye khanga peke yake na hiyo ndio iliyokuwa silaha pekee inayotumika na wanawake katika mapambano miongoni mwao hasa katika maeneo ya uswahilini.

Kwa kawaida kama wanawake wametofautiana katika mambo fulani fulani, badala ya kugombana kwa kupigizana kelele ilikuwa mtu ananunua khanga yake yenye ujumbe anaoutaka umfikie mbaya wake na kivaa makusudi ili kufikisha ujumbe aliokusudia kwa mwenzake.
Niliwahi kusimuliwa wakati fulani kuwa hata wale wanawake wanaochukuliana mabwana, nao walikuwa wakipambana kwa kuvaliana khanga zenye ujumbe wa kuzodoana na wakati mwingine mtu anaweza kumchokonoa mwenzake kwa kuvaa khanga zenye ujumbe tofauti tofauti hata saba kwa siku na kujipitisha kwa mbaya wake ili kumpa ujumbe aliokusudia na mara nyingi ilikuwa ni kawaida kwa mahasimu hao kuanza kurushiana maneno na hata kupigana hadharani kutokana na mmoja kukerwa na maneno ya kwenye khanga alizovaa mwenzie.

Tofauti na zamani, siku hizi mambo yamebadilika, na sasa sio khanga pekee, bali hata fulana siku hizi zimekuwa zikibeba ujumbe tofauti tofauti ukiwemo wa maneno ya kuzodoana. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao huchapisha ujumbe wa maneno ambayo tulizoea kuyaona kwenye khanga na kuyaweka kwenye fulana na hata Blouse na watu wamekuwa wakizigombea.

Sio kwamba sifurahii ubunifu huo wa mavazi, bali ninachojaribu kutahadharisha hapa ni aina ya ujumbe unaowekwa kwenye hizo fulana, kuwa usije ukatufikisha mahali watu wakatumia nafasi hiyo kuweka ujumbe wa matusi au hata maneno ya uchochezi, kwani kuna uwezekano ukatufikisha mahali tusipopatarajia.

Naamini wengi mtakuwa ni mashahidi wa hizi fulana au blouse za mitumba zinazoingia kutoka katika nchi za Magharibi na Ulaya ambazo zina ujumbe wa maandishi au hata picha tofauti tofauti. Tumekuwa tukishuhudia ujumbe wa Matusi au hata uchochezi wa kiubaguzi kupitia fulana hizo, lakini kwa kuwa zimeandikwa kwa kiingereza au lugha zao inakuwa ni vigumu walio wengi kung’amua maana halisi ya ujumbe huo labda mpaka mtu aambiwe, wengi tunachojali ni uzuri wa fulana lakini sio ujumbe ulioko katika fulana hizo.

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Koero! Ahsante kwa ujumbe huu!

John Mwaipopo said...

shida yangu sio katika ujumbe ilimradi ujumbe huo hauiathiri jamii nzima. shida yangu ipo katika fulana, vitambaa, mabegi na kadhalika kuchorwa picha ya bange. ndio BANGE! halafu wazee wa maadili kama hawaoni. inaweza isiwe taabu sana kwani wao hawavuti lakini ninachojua mimi sifa ya tangazo ni kuendelea kukumbukika. sasa likirudiwarudiwa ndio mwake. hofu yangu sio vijana kuvutiwa na hatimaye kulivuta bange. hofu yangu ni kuwa mirembe kutawatosha? au tujenge limirembe kuuuubwa.

Ramson said...

Nahisi kama hii mada imechelewa....no no no...imekuja wakati muafaka,
Hongera dada yangu Koero kwa kuliona hili, mara nyingi huwa navutiwa sana na makala zako maana zinagusa mahali ambapo ni vigumu wengine kung'amua.
kaka Mwaipopo umenena kitu ni kweli hata Leso au handkachif nazo pia zina picha ya hiyo Mibange yao...
Ni mada nzuri...keep it up...da mdogo.....

Mzee wa Changamoto said...

Nakumbuka mwaka 96 nikiwa kule "kivulini" kwetu Bukoba kabla sijaja huku "juani" kuchuma niliingia nyimba ya ibada. Nikakuta jamaa amevaa fulana nzuri kwelikweli ya rangi ya bluu ilikuwa na ufito mzuri saana na kwa hakika ilionekana swafi.
Nilipokuja kumkaribia nikagundua kuwa mgongoni (sehemu ya shingo)kuna maneno yasemayo MORTUARY ATTENDANT.
Najua hakujua maana yake kwani hata lugha yetu ilimpa shida kuisoma na sina shaka kuwa alipoenda kununua aliuziwa kwa bei ya chini. Baada ya hapo nikaanza kuwa makini kuzisoma na iliyofuata (baada ya muda kadhaa ) niliiona ikiwa imevaliwa na kaka mmoja. Ilikuwa nzuri, kubwa ya pink na ilisema MY NEXT HUSBAND WILL BE NORMAL.
Mmmmmm!!!
Labda hawa hawakujua maana ya walichovaa, lakini hizi za hapo juu ni "custom made"
Nami ninazo zangu na huwa nazichapisha lakini si kwa ujumbe kama huu.
Kuhusu alilosema Kaka Mwaipopo.......No comment kwa leo.
Lol
Blessings

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___