Monday, December 7, 2009

BARUA YA WAZI KWA DADA YASINTA NGONYANI.....

Dada Yasinta Ngonyani

Kwako dada yangu mpendwa Yasinta Ngonyani mzaliwa wa Ruhuwiko Songea mkoani Ruvuma. Habari za siku nyingi na shikamoo zikufikie hapo ughaibuni ulipo, vipi kile kidole chako ulichijichoma na sindano ukishona nguo ya mwanano Camilla kinaendeleaje. Dada nilipokea taarifa za kujichoma kwako na sindano kwa masikitiko sana na sikuamini kuwa hata Ughaibuni mnatumia sindano za mkono kushona badala ya cherehani. Hata hivyo nakupa pole zako japo uliumia kwa uzembe mtupu.

Nashukuru barua yako uliyonitumia nimeipata jana ingawa mwandiko wako ulinipa shida sana kuusoma, na nimeshangaa sana kuwa hata watu walioko ughaibuni wanakuwaga na miandiko mibaya namna hii, usidhani nakukosea adabu dada yangu, naomba uniwie radhi kwani siwezi kuvumilia maudhaifu ya wengine na ndivyo nilivyoumbwa.

Dada dhumuni la barua hii nikutaka kujibu barua yako ya hivi karibuni ambayo ulinishauri eti niolewe kwa kuwa naanza kuzeeka sasa, dada katika barua yako hiyo umeeleza mengi sana juu ya faida za kuolewa. Umedai kuwa kuolewa ni kuondoa nuksi ili usife bila kuvaa pete ya ndoa, na pia ni fahari maana utakuwa huwajibiki kutunza familia hata kama unafanya kazi, kwani hiyo ni kazi ya mwanaume.

Umesema kuwa kwa mujibu wa mila na desturi tulizorithi kutoka kwa mababu na mabibi zetu ni kwamba wanaume ndio wanaowajibika kuwahudumia wake zao na watoto, yaani mwanamke hatakiwi kutoa hata senti tano kuchangia pato la familia kwa kuwa sio jukumu lake, kwani hilo ni jukumu la mume kwa maana yeye ndiye anayehakikisha familia yake inapata kila kitu, ikiwapo chakula, malazi, mavazi, na vipodozi kwa mkewe ili apendeze zaidi. Umesema kuwa kwa kawaida mwanamke ni pambo la nyumba kwa hiyo akibebana na majukumu ni saa ngapi atakuwa ni pambo la nyumba.

Pia umetoa sababu za kisayansi eti kwa jinsi mwanamke anavyozidi kuzeeka basi na mayai yake ya uzazi nayo yanazeeka kwa hiyo nikifikisha umri fulani nitakuwa sina uwezo wa kupata watoto wangu mwenyewe na kama nikibahatika kuwapata watakuwa mataahira au watumiaji wa mihadarati au Vibaka na wapiga debe.

Ukadai kuwa fahari ya ndoa ni watoto kwa hiyo kama nisipozaa ndoa yangu itaota mbawa, hata kama mume wangu atanipenda, mawifi na ndugu wa mume watachonga sana hadi niachike kwani katika ndoa za Kiafrika ndugu wana nguvu sana na wana uwezo wa kuamua hatima ya ndoa yenu watakavyo.

Ulitoa ushahidi mwingine kuwa wanaume wa siku hizi wanapenda kuona wanawake wanaowazidi umri kwa zaidi ya miaka 15 mpaka Ishirini kwa kuwa hao bado damu inachemka, kwa hiyo kwa jinsi ninavyozidi kuzeeka na ndivyo ninavyozidi kupoteza sifa ya kuolewa na kuwa disqualify kama ulivyosema mwenyewe kwa lugha ya kiingereza.

Niliisoma barua yako kwa makini sana na nilitafahari kwa kina, na ili kujiridhisha ikabidi na mimi nifanye utafiti wangu, unajua si vyema sana kuamini kila unaloambiwa hata kama ni kutoka kwa baba au mama yako mzazi. Dada sifa kubwa niliyo nayo ni kutokuwa dodoki kama alivyosema hayati mzee wa Mwitongo Mwalimu Nyerere.
Dada kuwa dodoki maana yake ni kubeba kila unaloambiwa bila kupima na kudadisi ili kujiridhisha, kama unavyojua dodoki ukilichovywa kwenye maji taka litatoka na kila aina ya uchafu, na ndio maana nikasema kuwa sitaki kuwa dodoki.

Katika utafiti wangu dada nimegundua kuwa madai yako hayana ukweli, kwani wanawake wengi walioolewa wanajuta sana na watamani kuachika kutokana na manyanyaso ya wanaume.

Dada kwa mujibu takwimu za chama cha mambo ya wanawake, kuna wanawake wengi wamepeleka malalamiko yao huko wakitaka kuachika kutokana na manyanyaso kutoka kwa waume zao. Wanawake hao wanadai kuwa kigezo wanachotoa wanaume hao kuwanyanyasa ni mahari waliyolipa kwa wazazi wao.

Wanawake hao wanadai kuwa manyanyaso wanayopata yanategemea kiwango cha mahari waliyotozwa hao wanaume wao, kwa hiyo inakuwa ni vigumu kwa wale waliolipiwa mahari kubwa kudai talaka kwa kuwa wazazi washakula chao mapema kwa hiyo hawana uwezo wa kurudisha mahari ya watu na hivyo wanajaribu kutafuta wafadhili toka nje ili wawanasue katika ndoa hizo za mateso.

Wanawake hao wanatafuta uwezekano wa kubadili mila na desturi zetu ili wanawake ndio wawe wanaoa na kulipa mahari kama wahindi kwani kule India wenzetu wanawake ndio wenye sauti kuliko wanaume na ndio maana India na Pakistani zimewahi kutawaliwa na wanawake kama vile mama Indira Gandhi na Benaziri Bhuto ambao wote waliuwawa kwa husuda tu, na wale wanaume wanaotaka mfumo dume kama huu uliotamalaki huku kwetu

Dada kama wewe ni msomaji wa vitabu vitakatifu vya dini zetu hizi za mapokeo utakubaliana na mimi kuwa hata mwenyezi Mungu amewapendelea sana wanaume kiasi cha kuwapa kibri. Hebu soma maandiko matakatifu ya Biblia katika kitabu cha Waefeso 5, 22:24.

Dada maandiko hayo ndiyo yanawapa wanaume kibri kwa kudai kuwa wao ndio vichwa vyetu wakati vichwa vyetu tunavyo na tunatembea navyo.

Kwa hiyo dada ushauri wako kwangu nauona kama unataka kunipalia makaa ya moto ili tufanane wakati mie nimeshawashitukia wanaume zamani sana.
Najua utashangazwa na uamuzi wangu kwa kuwa ulitegemea nikubaliane na ushauri wako lakini napenda kukukatisha tamaa kuwa mie nimeshawashitukia wanaume siku nyingi.

Dada mimi ni mjanja………..LOL

6 comments:

Fadhy Mtanga said...

Barua nimesoma japo ni ya da Yasinta. Wala sijui nichangie nini. Ila hakya Mungu vijeba tumepigwa vijembe humu hapana wesa sema.

Mija Shija Sayi said...

Haya da'Yasinta umemuanza mwenyewe...

Nice post.

Bennet said...

Keoro kama unataka kutoa mahari njoo kwetu, Mama yangu atapokea halafu tuoane (LOL)ukiwa tayari tuwasiliane nikuelekeze hahahahah au unaogopa kuoana na mkulima

Markus Mpangala said...

Kufumbua macho siyo kuamka jamani ipo kazi.....au akupigaye ngumi ya jicho nawe mpige ngumi ya sikio.... akikuuliza unaonaje....nawe muulize unajiskiaje
LABDA):
Siyo kila NDIYO inandiyo KIUNDANI, ila kuna NDIYO ambazo huambana na UTANI.....lol....

kama kule INDIA? tena wanaruhusu mwanamke hata kuoa wanaume wawili kwa wakati mmoja(someni kitabu CIVICS FORM 1).

Kaka Fadhy umenichekesha sana ha ha ha ha ha ha ha ha ha unaogopa hata kunywa MCHUZI KWA BAMIA????

ha ha ha ha ha kaka BENNET ha ha ha ha ha nadhani wewe ni mkristo bila shaka.... nadhani nabii wenu Yesu/ISSA alisema ukitaka kuishi kama yeye haina noma..... KUPANGA NI KUCHAGUA.
NAKUSIHI MSIKILIZE LUCKY DUBE katika IT'S NOT EASY.

Candy1 said...

Mmh...mie sijaolewa lakini naangalia kitu pande mbili, upande wake mzuri na mbaya pia (advantages and disadvantages). Nimeona mifano mingi tu ya ndoa na hakuna ambayo iliyoenda mfano wa zile bembea za ku "slide" na hakuna lisilowezekana (pambio?)...sisemi mengi namsubiri Dada Yasinta...ila mmh

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___