Thursday, April 29, 2010

ANAPOZUNGUMZA MWENDAWAZIMU…….

Mabinti wengi Vijijini hutumia fursa ya kwenda kisimani katika kufanya mambo yao

Kuna msemo mmoja walisema Wahenga wetu usemao, ‘anapozungumza mwendawazimu, anayesikiliza ni mtu na akili zake’

Wazee wetu wa zamani walikuwa na misemo mingi ambayo ilikuwa ikitumika katika kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa namna ambayo sio rahisi kumkwaza mtu.

Misemo hiyo ilitumika katika kuelimisha, kufundisha, kutoa ujumbe au kutoa tahadhari juu ya jambo fulani kulingana na suala husika. Wakati mwingine inakuwa ni vigumu kuelewa hadi pale atakapoelekezwa maana ya msemo huo.

Na mara nyingi misemo ya kale ilikuwa na ujumbe ambao huwezi kuupata endapo ni mvivu wa kufikiri. Inahitajika mtu awe na fikara jadidi au mwepesi wa kuchanganua mambo, vinginevyo atahangaika pasipo kupata ujumbe mahususi.

Bibi yangu ndiye mwenye jina hili la Koero naweza kumwita Ulamaa(kama wale watalamu wa mashairi) au nimwite mtu mwenye misemo mingi ya kale yenye mafunzo mengi ndani yake. Huwezi kukaa na bibi Koero kwa mazungumzo bila kukupa semi za kale ambazo aidha za mafumbo au methali. Nathubutu kumwita mkali wa tamathali za semi.

Wakati fulani nilipomtembelea kule kijijini, nakumbuka siku moja wakati tunaenda kisimani kuteka maji tuliwakuta mabinti kadhaa pale mtoni wakicheza na wavulana badala ya kuteka maji. Na hili kwa mabinti wa vijijini ni mwanya mzuri sana, na baadhi yetu unatukumbusha kisa cha Ngoswe;Penzi kitovu cha Uzembe. Tunakumbuka Ngoswe alitumia mwanya wa binti Mazoea kwenda kisimani kuteka maji ili amwage sera zake.

Sasa, Bibi yangu aliwakemea wale mabinti kwa kuwataka wateke maji na kupeleka makwao badala ya kucheza pale na wale wavulana, aliwakemea sana na kuwatahadharisha juu ya mchezo wao ule wa kukimbizana na wavulana kuwa hautakuwa na mwisho mzuri.

Lakini wale mabinti walimpuuza na kuendelea na mchezo wao huo, isipokuwa binti mmoja ambaye aliamua kuteka maji na kujitwisha na kuondoka zake akiwaacha wenzake ambao walikuwa wakimcheka, kwa kumwona muoga.

Hapo ndipo Bibi Koero akasema, “anapozungumza mwendawazimu anayesikiliza ni mtu na akili zake”. Kwa hakika ilinigusa sana, na nakiri sikumwelewa alimaanisha nini, sikuchoka kudadisi,.

Lakini baadaye tuliporudi nyumbani nilimuuliza juu ya msemo ule kwa hamasa ili nijue, huku akitabasamu alinimbia kuwa, ule msemo unaweza kuleta maana iwapo nitaugeuza kinyume chake, yaani badala ya “anapozungumza mwendwazimu anayesikiliza ni ni mtu na akili zake” utamkwe hivi “anapozungumza mtu na akili zake anayesikiliza ni mwendawazimu”. Hakika niliduwaa,nilihitaji maelezo zaidi.

Ndipo alinieleza kuwa msemo ule maana yake ulikuwa ni kufikisha ujumbe kwa namna ambayo haitawakera watu, kwa maana ya kuwaita wendawazimu bali kufikisha ujumbe kuwa mara nyingi watu na akili zao wanapozungumza ni vigumu sana watu kuwaelewa na ndio maana wanadharauliwa na kupuuzwa, mpaka kitambo kidogo ndipo watu wanapong’amua ukweli wa yale yaliyozungumzwa.

Maneno hayo yalinikumbusha gwiji wa sayansi Galileo Galilei ambaye alisema kuwa dunia hii haiko kama meza, kama watu wa enzi hizo walivyokuwa wameaminishwa. Bali dunia ni duara na inazunguka katika mhimili wake na kulizunguka jua, ndiyo maana tunapata usiku na mchana, lakini mwanasayansi huyo alipingwa vikali na watu akiwemo mfalme, ikabidi ajinyamazie.

Baada ya miaka kadhaa tangu atoe kauli ile, ilikuja kudhihirika kuwa utafiti wake ulikuwa ni sahihi. Na hapo ndipo msemo huo unapokuwa na maana kama ukiuzungumza kwa kinyume chake.

Kwa mfano yule binti kule mtoni ambaye alimsikiliza bibi Koero na kuamua kuteka maji na kuondoka huku akiwaacha wenzie wakimcheka, Je ni nani mjinga kati yake na wale wenzie? Kama bibi koero alikuwa ni mwendawazimu basi ni Yule binti pekee aliyekuwa na akili zake aliyeelewa na kufuata malekezo ya bibi Koero, na kuwaacha wnzie ambao walimuona bibi Koero kama ni mwendawazimu, wakati wao ndio wendawazimu kwa kushindwa kuelewa kile alichosema.

Nimekumbuka msemo huu baada ya kupitia blog kadhaa siku ya leo na kukutana na habari chungu mzima ambazo zimekuwa kama zimebeba fikra za mwendawazimu. Tumekuwa tukiandika mambo mengi sana tukijaribu kugusa kila nyanja katika jamii yetu lakini kumekuwa na watu wachache wenye akili zao ambao ndio walioweza kusikiliza na kuelewa na wengine kutoa maoni yao.

Kuna siku niliwahi kuweka porojo zangu hapa ambazo zilikuwa ni fikra zangu tu za kiwendawazimu lakini si haba niliwapata watu kadhaa wenye akili zao ambao walimudu kusoma ujinga wangu na kutoa maoni yao.

Miongoni mwao kuna maoni ya msomaji mmoja ambaye hakutaka kuweka utambulisho wake bayana, ambaye na yeye aliweka fikra zake za kiwendawazimu katika mada hiyo, ambapo nilivutiwa sana na mchango wake. Naomba uungane nami kwa kusoma maoni yake kama ifuatavyo hapo chini:

"Dada Koero, leo ni siku ya kwanza kukutembelea humu. Nimeipenda sana blog yako. Nimeona umeandika sana kuhusu madhira ya mama zetu. Dada Koero mimi nakuunga mkono, maana I have lived this life. So I know it. Swali langu kwako na wanawake wengine ni hili: Je ni kipi kifanyike KUPUNGUZA maana KUONDOA hii hali ni vigumu. Inaonekana wengi tunaliona tatizo na tumeishi na haya matatizo, lakini wote tunasema ni serikali ndo yenye jukumu! Mi nadhani we should be the change we seek!Tuanze na jukumu la kuchagua viongozi responsible na tuwawajibishe. Leo hii CCM akijua kwamba hana majority bungeni ya kupitisha sheria anazozitaka kwa manufaa yake......trust me ..atakuwa na adabu jinsi anavyotuongoza, perhaps hela za ufisadi angeziweka kwenye mipango ya kuwawezesha na si kuwasaidia hawa akina mama na wananchi kwa ujumla....Tatizo kubwa kwetu sisi waafrika popote tulipo...tunapenda kuwalaumu wengine kwa matatizo yetu. Ukiangalia kwa kiundani..hawa hawa unaowaonea huruma..ndo kesho utakuta wanaandamana kuipigia kura CCM! Sasa jamani..hivi mnategemea ukombozi wa mwafrika utatoka wapi? Mwenyezi MUNGU ALITUPA UTASHI lakini tunashindwa kuutumia. Do you really think Kikwete gives a damn to a dying villager down in Kwimba au Kigoma? only when he needs their votes!Hapa tutakuja na excuse kibao..kwamba watu tunachagua viongozi wabovu kwa sababu ya umasikini, lakini tunashindwa kugundua kwamba..Politics is everything! whether you are in America or in poverty stricken Tanzania.

Narudia tena, waafrika..viongozi wetu wanatuchukulia for granted. Na sisi tumeridhika na hii hali.Na sisi tumekubali.. Hata the so called "elites"..ndo wanatuangusha..maana wakisha "toka" imetoka hiyo.....Hawaangalii nyuma....zaidi ya "kuwaonea huruma" waliobaki huko nyuma...My take: Watanzania tuamke, tuchukue jukumu la maisha yetu. Tuache kumsingizia Mungu wala mwingine. HAITUSAIDII KULAUMU. Dada Koero, Trust me..leo hata ungeteua 70% ya wabunge wote wakawa wanawake...hali za mama zetu hazitabadilika! Tunahitaji kubadilisha mfumo wa jinsi tunavyojitawala au tunavyotawaliwa. Imagine...mpaka leo hatuna umeme wa kuaminika..lakini hebu jiulize..tangu JK aingie madarakani..tumelipa mabilion mangapi kwa makampuni ya umeme hewa? and guess what? Everybody is quite! and in October we will vote in masses for the same messy!Ofcourse, CCM siyo tatizo letu pekee..lakini..wakijua kwamba hata wananchi wanafikiria..hali itabadilika. For now..they know..they can do anything and go away with it. Mimi kiukweli...I get the feeling labda..ngoja umasikini uzidi kutuchapa weeeee (zaidi ya huu tulionao sijui itakuwaje ;-)...labda iko siku tutaamka na kuona kwamba we can influence things through the ballot!Waungwana naomba nisiwachoshe..lakini..mimi kiukweli nchi yangu na wananchi wenzangu wananisikitisha sana...Tunashindwa kufanya maamuzi magumu kwa manufaa yetu na watoto wetu. Umasikini na hali ngumu zinazowakabili mama na baba zetu utaendelea kudumu daima. Mpaka tutakapoamka na kusema INATOSHA!"
(Mwisho wa maoni yake)………..
Fikra za kiwendawazimu za msomaji huyu zilinivutia sana nikaona si vibaya nikiwashirikisha watu kadhaa wenye akili zao kutafakari kile alichokisema mwenzetu.

Kuna jambo moja ninajiuliza, hivi vyombo vyetu vya habari hususan magazeti na Redio haviwezi kweli kutengeneza vipindi hata vya nusu saa kusoma ujinga wetu huu katika blog zetu hizi?

Kusema kweli kuna ujinga mwingi sana unaoandikwa katika blog zetu hizi ambapo kama ungapewa nafasi katika vyombo vyetu vya habari vya magazeti na redio kwa kuwa vinawafikia wananchi wengi hapa nchini ukilinganisha na blog, naamini idadi ya watu wenye akili zao ambao ndio wanaoweza kuelewa kilichojificha ndani ya ujinga wetu huo ingeongezeka.

Hebu wewe unayesoma hapa, jaribu kumtembelea mzee wa changamoto Mubelwa Bandio kwa kubofya hapa usome ujinga wake au mzee wa Jielewa Christian Bwaya kwa kubofya hapa, pia ni vyema kusoma maisha na mafanikio kwa kumsoma dada Yasinta Ngonyani na ujinga wake kwa kubofya
hapa.

Nachelea kusahau ujinga wa Profesa Mbele ambapo unaweza kubofya hapa kumsoma, bila kumsahau kaka yangu Profresa Matondo naye kila kukicha hachoki kuandika fikra zake za kiwendawazimu kwa kutulisha chakula kichungu na kitamu ambapo ukipenda kukila waweza kubofya hapa.

Naogopa kupigwa mapanga shaaaaa na Chacha o'Wambura Ng'wanambiti kwa kusahau kuwakumbusha wasomaji kusoma ujinga wake na uwendawazimu wake kwa kubofya hapa, …Heeee nisimsahau mzee wa mitini, tena huyu kama hayuko mirembe ni bahati maana hata simuoni mjini siku hizi, naambiwa amekimbilia Karagwe baada ya kufulia na akiwa kule anaendeleza libeneka kwa kuandika ujinga wake kwenye kijiwe chake cha nyegerage, huyu ni Kamala, hebu bofya hapa kumsoma pia.

Kaka yangu wa kulikoni ughaibuni Evarist Chahali na yeye upuuzi wake upo hapa, kaka yangu Malkiory wa kule Ufini na yeye hayuko nyuma katika kuandika ujinga wake na kuweka hapa, kuna ndugu yangu mmoja siku hizi na yeye anajifanya kichaa kabisa, Fadhy Mtanga, yeye ameamua kuimba na mashairi ya ndoto za alinacha na kuyaweka hapa.

Mfumwa Kitururu, naambiwa karudi Bongo kimya kimya na kajichimbia Morogoro akitafakari juu ya namna ya kuendeleza stihizai zake pale mawazoni na kutufikirisha kwa lugha zake zilizojaa utata mtupu unaweza kubofya hapa kumsoma.

Kuna bwana mmoja mie napenda kumwita Mcharuko, maana kadata mpaka ameamua kutengeneza kurasa mbili ili kuendeleza libeneke la kuandika ujinga wake, huyu sio mwingine ni mzee wa Nyasa Markus Mpangala aka Paroko aliyestaafishwa kwa manufaa ya kanisa, ujinga wake uko
hapa
Ninaye dada yangu mpendwa, huyu alinibatiza jina la Binti Kipaji, sina uhakika kama nastahili jina hili, lakini kwa kuwa yeye ameona na kwa vigezo vyake ameniona nastahili, nasema shukrani dada yangu. Huyu ni dada Mija Sayi nasikia ni dada yake Profesa Matondo, na yeye anaandika ujanja wake hapa. Nisimsahau mdogo wangu my Little world, Faith Hillary, akiwa kule ughaibuni hachoki kuandika ujinga wake na kuuaweka hapa. Na pia nisingependa kumsahau kaka Jacob Malihoja, na mbwembwe zake katika kibaraza chake unaweza kubofya hapa kumsoma. Na kaka yangu kwa mama mwingine Ramadhani Msangi yeye anaweka ujinga wake hapa. Hupo kaka yangu mwenye Utambuzi na anayejitambua, yeye huwa anatushangaza katika kibaraza chake, unaweza kubofya hapa kumsoma. Yupo pia dada yangu Subi, mie wakati mwingine humwita Passions, naye mara nyingi anatufikirisha kwa tamathali zake za kiwendawazimu kupitia kibaraza chake kilichopo hapa

Kwa kweli, kuna wadau wengi katika tasnia hii ya blog ambao wanaandika ujinga wao lakini imekuwa kama kelele za mwana mpotevu nyikani. Kama kungekuwa na ushirikiano wa vyombo vya habari nilivyovitaja hapo juu kuchukua uamuzi wa kupitia blog hizi kwa minajili ya kuwafikishia Watanzania kile tuandikacho ingesaidia sana kuelimisha jamii kwa kiasi kikubwa.

Tujiulize mbona CNN ilifanikiwa sana kutumia blog kupata habari za chaguzi za Iran, Kenya na Zimbabwe kama njia mbadala ya kupata maarifa na habari anuwai? Huo ni mfano tu. Tunahitaji ushirikiano huu kwa vyombo vya habari kwa sababu wote tunajenga nyumba moja ambayo ni Tanzania, hatuna sababu ya kunyimana fito.

Naomba kuwasilisha

Sunday, April 25, 2010

WAZEE WETU NA ISHARA ZAO

Mzee akirudi kutoka safari

Kwa hapa mjini hulka hii haipo sana ukilinganisha na kule vijijini. Inawezekana ni kutokana na mazingira ya hapa mjini yalivyo, labda na muingiliano wa makabila.

Hapa nazungumzia jambo ambalo hata wewe unayesoma hapa huenda unalitenda au umelishuhudia likitendwa wakati wa makuzi yako kule kijijini.

Kuna hulka moja ambayo hutumiwa na wazazi wa kiume kutoa ishara kila wafikapo karibu na makazi yao mara warudipo kutoka iwe ni matembezini, kazini au hata safari. Ishara hiyo inaweza ikawa ni kikohozi, kupiga mluzi, chafya kumsalimu mtu kwa sauti ya juu.

Nakumbuka wakati fulani nilipokuwa kijijini alikozaliwa mama yangu, nilifikia kwa mjomba wangu. Naomba nikiri kuwa nimejifunza mambo mengi sana kuhusiana na maisha kupitia mjomba wangu huyu. Ni mtu mwenye hekima na busara na anayefuata mila na desturi za wazee wa kale na hajaathiriwa sana na tamaduni za magharibi.

Nilikuwa nimezoea kumsikia akikohoa kwa sauti kubwa kila anapokuwa akikaribia nyumbani. Na shangazi alikuwa amezoea kutuambia “mjomba wenu huyo” alikuwa akisema hivyo kama vile anatoa tahadhari hivi.

Siku moja nilishikwa na shauku ya kujua sababu ya yeye mjomba kufanya hivyo kila arudipo kutoka katika matembezi yake. Kwa bahati nzuri mjomba ananifahamu kuwa mimi ni mdadisi na kwa kulifahamu hilo, alikuwa amejenga tabia ya kunieleza jambo kwa kina na mifano ili nisije kumchosha na maswali, nilimpenda kwa hilo.

Mjomba aliniuliza swali moja kabla ya kujibu swali langu. Aliniuliza “hivi unaujua msemo mmoja unaosema paka akitoka?” nikamalizia kwa kujibu, “Panya hutawala” alinyamaza kwa muda, akakohoa kidogo ili kusafisha koo, kisha akaagiza aletewe maji. Mtoto mmoja aliinuka kwenda kumletea maji akanywa funda mbili tatu kisha akaendelea.

Alinimbia kuwa kwa kawaida mtu anapoweka sheria nyumbani kwake mara nyingi hazifuatwi mwenyewe akiwa hayupo, Kama ilivyo kwa panya kutawala pale paka anapokuwa hayupo, basi ndivyo inavyokuwa kwa watoto pale nyumbani, baba anapokuwa hayupo.

Aliendelea kusema kuwa wazee wetu wa zamani walikuwa na hekima sana, na ndio sababu ya kubuni namna ya kutoa taarifa kuwa wamefika nyumbani kwa ishara ili hata kama kuna jambo pale nyumbani haliko sawa mkewe aweze kuliweka sawa ili kuepusha mumewe kuona dosari.

Kwa mfano inaweza kutokea labda kuna kiti ambacho baba amezoea kukikalia kila awapo nyumbani na kwakuwa hayupo basi watoto wakawa wamekikalia kiti hicho, mama akisikia ishara ya mumewe kuwa anakuja, basi alikuwa akiwaeleza watoto kuwa baba ameshafika ili wakae kwa heshima na kama yuko aliyekalia kiti cha baba aondoke kumpisha baba.

Na ili kuonyesha kuwa wazee wetu wana busara, walikuwa hawafanyi papara kuingia ndani baada ya kutoa ishara. Wanachofanya ni aidha kumsemesha jirani kwa kumsalimia huku akiwa nje na kuzungumza naye mambo mawili matatu katika kupoteza muda au kuingia msalani hata kama hajisikii kwenda huko, ili mradi kupoteza muda japo kidogo ili kumpa mkewe muda kuweka mambo sawa.

Kama inatokea baba amesafiri kwa mfano, na kwa kuwa zamani kulikuwa hakuna mawasiliano ya simu za viganjani kama siku hizi, basi siku akirejea haendi nyumbani moja kwa moja anaweza kupitia kwa rafikiye au kwenye maeneo wakutanapo wazee kupiga soga na hapo mtoto yeyote atapewa mkoba kama alibeba mkoba na kama hakubeba mkoba atampa fimbo au bakora yake na kama hivyo vyote hana basi atampa koti au kofia aipeleke nyumbani, lengo ni kutoa tarifa kwa mkewe kuwa amerudi.

Na ikitokea amerudi usiku sana, basi anaweza kupitia kwa rafikie na kuomba kulala hapo na asubuhi kukipambazuka mtoto anapewa mkoba kuutanguliza nyumbani.

Mjomba alisema kuwa utaratibu huo ulikuwa unaepusha mambo mengi sana, kwa mfano kufumania. wazee wa zamani walikuwa wana utambuzi wa hali ya juu, kwa sababu walijua kuwa sisi binadamu ni dhaifu, walijua wazi kuwa inaweza kutokea ibilisi akampitia mkewe na kuingiza mwanaume ndani ya nyumba yeye akiwa amesafiri, hivyo kwa kutanguliza ishara kabla ya kufika nyumbani ni kutoa mwanya kwa mkewe kuweka mambo sawa ili kuepusha fumanizi.

Jambo lingine ni kuepusha baba kutoa maelekezo kila arudipo nyumbani, inaweza ikatokea labda hapendi redio au TV ikafunguliwa kwa sauti au watoto kupiga kelele, kwa hiyo akitoa ishara ina maana kama redio au TV imefunguliwa kwa sauti basi sauti itapunguzwa na watoto watapunguza kelele na kuka kwa heshima.

Toafauti na wazee wa zamani, siku hizi, mambo yamegeuka, vijana wa siku hizi hawatoi ishara tena, bali wanavizia lengo ni kutaka kuona makosa na kukemea kila kitu. Wakati wazee wa zamani walikuwa wanatoa ishara kuepusha ugoni, vijana wa siku hizi wanavizia na kutegeshea kabisa, tena ataweka na wapambe ili kuhakkisha anafuamania.

Na ndio maana ndoa nyingi siku hizi haziishi migogoro na mahusiano ya wanandoa wengi yako vululu vululu. Kila siku kelele na ghubu haliishi ndani ya nyumba, kitu ambacho kingeweza kuepushwa kama hulka hii ya kutoa ishara ingetumika.

Sishabikii wanawake kutoka nje ya ndoa, lakini hebu tuangalie faida nyingine kama za kuepeusha baba kukemea jambo moja kila mara. Kuna uwezekano mkubwa akapata msongo wa mawazo. Kuna mambo ambayo baba anaweza kusema yasifanyike pale nyumbani lakini yakawa yanafanyika kinyemela, si paka akitoka panya hutawala? sasa paka akirudi na kulia “nyau” ni wazi kuwa panya watarudi kwenye mashimo yao na kujificha, na ndivyo inavyokuwa kwa watoto pia.

Ni sawa na mzazi kumkuta binti yake uchochoroni mtaa wa saba akiwa na mwanaume, kwa baba mwenye busara pamoja na kumkemea bintiye lakini atajua kuwa binti yake kafanya heshima kwenda mbali na nyumbani kwao na kujificha uchochoroni asionekane na kama bahati mbaya mzazi yule akamuona. Lakini kama atamkuta nyuma ya nyumba yao, hapo ajue kwamba heshima hakuna tena hapo.

Lakini pia mambo yamegeuka, sio kama zamani, siku hizi kina Koero hatujifichi tena vichochoroni, ya nini kuliwa na mbu usiku au kukabwa na vibaka? Kama una mvulana wako unamleta nyumbani na kumtambulisha tu kwa wazazi bila wasiwasi, na sijui ni kutokana na huu utandawzi au sijui ni hizi TV, wazee nao kimya hawasemi hata.

Utakuta Koero kaja na mvulana wake Suruali iko mlegezo makalio yote nje,a kuwaambia wazazi wake, “huyu ni boy friend wangu” na wazazi nao bila aibu unawasikia, “Karibu sana kijana na ujisikie uko nyumbani” #$%^&$%^&*

Hicho ndicho kizazi chetu sie kina Koero na hakuna anayepiga kelele kukemea tabia hizi ilimradi kila mtu na lwake.

Saturday, April 24, 2010

TAFAKARI YA LEO: TUENDELEE NA SOMO LA IMANI

Kwa kauli tu Yesu aliweza kuukausha Mtini

Tafakari ya leo, ngoja tuendelee na somo la imani.
Hebu tuangalie mfano huu wa imani kwa kusoma katika kitabu cha Matayo 21:18-22, nitanuku,

“Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini aliona njaa. Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara. Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, jinsi gani mtini umenyauka mara? Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia mkiwa na IMANI, msipokuwa na SHAKA, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yoyote mtakayo yaomba katika SALA mkiamini, mtapokea’

Kuna watu ambao, kwa sababu ya kukosa kile ambacho jamii inakiona kuwa ndio ufunguo wa mafanikio, huwa wanaamini kwamba hawawezi kufanikiwa au kufanya vizuri maishani.

Kwa mfano, kwa kukosa elimu, ujuzi au utaalamu fulani, watu wengine hujihesabu kama wanyonge. Huchukulia kwamba ni wale tu wenye elimu, ujuzi na utaalamu fulani ndio wanaoweza au wanaotakiwa kufanikiwa.

Hivi ni nani asiyejua kuwa wale wanaoonekana kuwa wamefaniwa kimaisha na kumiliki ukwasi wa kutosha ni wale ambao hata hawakuwa na uwezo mkubwa darasani?

Hawa waliamini katika kufanikiwa huku wakitia shime katika kile wanachokifanya na wakiamini kuwa watafanikiwa. Sio kwamba watu hao walikuwa hawapati misukosuko, la hasha. Walikuwa wakipata misukosuko na wakati mwingine kurudi chini kabisa na kuanza upya lakini kwao hiyo ilikuwa ni changamotoa ambayo iliwazidishia moyo wa kujituma huku wakiamini kuwa watamudu na hakika kutokana imani waliyokuwa nayo waliweza kumudu na kuwa matajiri wakubwa hapa duniani.

Kama ukisoma habari za wale matajiri ambao utajiri wao umepatikana kwa njia ya halali, huenda ukashangazwa na simulizi zao. Utagundua kuwa juhudi, uvumilivu, subira na imani ndio silaha kuu iliyotumiwa na watu hao kufika hapo walipo.

Kuna wakati niliwahi kusoma kisa kimoja katika blog ya utambuzi na kujitambua ya kaka Kaluse, cha bwana mmoja aitwae Wiliam Mitchel, unaweza kubofya hapa kujikumbusha.

Bwana huyu awali alipata ajali ya pikipiki na kuungua karibu mwili wote, lakini baada ya kupona alirejea kwenye shughuli zake za kibiashara na kama kawaida, lakini katika hali pengine ya kushangaza alipata ajali nyingine ya ndege. Ajali hiyo ilimuacha akiwa na na ulemavu kuanzia kiunoni kwenda chini.

Bwana huyu hakukata tamaa. Alisema anataka kuishi na siyo kuishi tu bali kuishi kwa mafanikio. Alipopona alirudi katika biashara zake kama vile hakukuwa kumetokea jambo lolote baya au la kuvunja nguvu.Aliendelea kufanya biashara huku akiwa na makovu na ulemavu hadi akafanikiwa kuingia kwenye orodha ya mamilionea wa Marekani.Bila shaka umeshawahi kusikia au hata wewe mwenyewe kusema, “si wamesoma bwana, ndio wanaojaaliwa, sisi ambao hatuna shule kazi yetu itakuwa ni kuwatumikia”. Kauli kama hizi zina chimbuko lake mbali sana, pengine katika malezi yetu.

Wazazi walizoea au wamezoea kuwaambia watoto wao “Usiposoma, kazi yako itakuwa ni kuwabebea wenzako mizigo”. Kwa bahati mbaya mtoto aliyelishwa “sumu” hii anaposhindwa shule huamini kwamba yeye atabaki kuwatumikia wengine tu.

Tunapoamini kwamba, kwa sababu hatuna elimu ya kutosha na pengine ujuzi au utaalamu fulani, hatuwezi kufika juu kwenye mafanikio, ni wazi hatutafika.

Moja ya vigezo muhimu vinavyoweza kutufikisha kwenye mafanikio ni kuamini kwetu kwamba tunaweza kufika huko, huku tukitia shime katika kile tunachokifanya kwa wakati huo. Tunapokuwa hatuna imani kwamba tunaweza kufika huko hata kama tufanye kazi usiku kucha bila kupumzika, hatutafika kamwe kwa kuwa tumejifungia njia wenyewe.

Yesu aliposema “Amin, nawaambia mkiwa na IMANI, msipokuwa na SHAKA, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yoyote mtakayo yaomba katika SALA mkiamini, mtapokea”

Hakuwa na maana nyingine bali ni kutuhakikishia kuwa kama tukitenda huku tukiomba na kuamini, hakuna lisilowezekana mbele ya Mungu, haijalishi una elimu au huna, kinachotakiwa ni sisi kutenda na kuamini tu, basi.

Kama kwa kuamini tu inawezekana kuuambia mlima, ung’oke, ukatupwe baharini, na ikawezekana, kwa nini isiwe kwenye kufanikiwa?

Naamini kila mtu anayo nafasi ya kufanikiwa na kupata kile anachokitaka na ambacho kitampa furaha, ni wajibu wake tu kuomba na kuamini.

*Tafakari ya leo kwa msaada wa Blog ya Utambuzi na Kujitambua*

Tukutane Jumamosi ijayo…………….

Wednesday, April 21, 2010

HEBU SOMENI UTAFITI HUU!



Tafiti nyingi zilizofanywa kuhusiana na upotezaji muda unaofanywa na waajiriwa ni kwamba, wafanyakazi maofisini huwa wanapoteza saa tatu kila siku katika kufanya mambo ambayo hayana maana kwa mwajiri au kwa kazi zao. Kwa wale ambao wana mitandao ya intenet maofisini mwao na wanaweza kuangalia kwa kadiri wanavyopenda hutumia dakika 54 kwa siku kuangalia mitandao hiyo.

Watumishi wa maofisini hutumia dakika 18 kila siku kuchungulia madirishani. Hata wale ambao viti na meza zao katikati ya ofisi, huwa wanasimama na kwenda kuchungulia madirishani mara kwa mara. Kwa wastani hutumia dakika 18 kutwa.

Watumishi wa maofisini hutumia dakika 14 kwa kwenda kujisaidia au kwa wanawake kwenda kujipamba au kujipodoa upya bafuni au vyooni. Ile nenda rudi ya kujisaidia au kujipodoa upya huchukua wastani wa dakika 14 kila siku. Kumbuka, kuna watu hujisaidia haja kubwa hata kwa dakika kumi.

Watumishi wa maofisini yaani wale ambao hukaa ofisini, hutumia dakika 35 kila siku kupiga soga zisizohusiana na kazi na pengine zisizo na maan sana. Soga zinazohusu mpira, siasa, ufuska, majungu na umbeya mwingine hutawala.

Halafu hutumia dakika 17 katika kunywa kahawa au chai na pengine soda. Inaweza kuwa wananywea kwenye mighahawa ya kazini au pale ofisini walipo. Wengine wakati wakiwa wanakunywa kahawa au chai hawagusi kazi kabisa.

Siku hizi maofisini kuna mambo mengi ambayo yanaweza kuteka mawazo au akili ya watumishi. Vitu kama mitandao, kuchati na simu zao za viganjani, viriba vya chai na kahawa vya kujichotea na mengine mengi yanafanya kujikuta mtumishi ameacha kazi na kuingia katika kitu kingine.

Lakini watumishi wengi wa maofisini hasa wale ambao wanatumia muda mwingi ofisini,inadaiwa kwamba, hawafanyi mazoezi. Hii inasababisha watumishi wengi wa kazi za aina hiyo kufa au kustaafu mapema kutokana na ubovu wa afya.

Sunday, April 18, 2010

ULE MRADI WETU SASA UMEIVA………..

Dada Yasinta

Makao makuu ya NGO yetu

Kwako dada yangu mpendwa Yasinta Ngonyani, natumaini wewe na watoto wako pamoja na huyo shemeji yangu anayejifanya kutojibu salaam zangu muwazima wote. Unajua dada simlaumu sana huyo mumeo, maana najua alitishwa wakati anakuchumbia kuwa sisi Watanzania tuna shida sana, kwamba tukiona ndugu yetu kaolewa basi shida zetu zote zitaishia kwake. Naomba umtoe mashaka kwamba ukoo wa Ngonyani hatuka hivyo, yaani hatuko kama ule ukoo wa mzee Makalioni, yule anayependa kusingizia misiba kila uchao ili kujipatia ridhiki.

Mwambie kuwa ukoo wa Ngonyani ni Jiniazi na una watu makini sana na wenye akili za ziada, kwani haoni hao wanae wawili uliomtotolea baada ya kukumimbisha kuwa wana akili sana kama mama zao wadogo na wajomba zao.

Samahani dada ngoja niachane na hayo, unajua leo nimeamua kukuandikia waraka huu asubuhi huku nikinywa chai na mkate wa bofulo nilionunu hapo jirani kwa mpemba kwa sababu waraka huu ni muhimu sana, kwani unahusiana na lile dili nililokudokeza wakati ule ambalo limeanza kutema, kama yale machimbo ya Tanzanite kule Mererani.

Dada mimi sio mbinafsi na ndio maana nikaona nikushirikishe ili wote mimi na wewe na ukoo wote wa Ngonyani tuwe matajiri kama Bill Gate wa Sudani, yule anayetoa tunzo ya Raisi bora wa Afrika. Eti huyu jamaa amegundua kuwa maraisi wa Afrika kwetu wana njaa sana na ndio maana wanakuwa mafisadi na ili kuwatoa wasiwasi akaanzisha tunzo yenye mapesa mengi ili kuwaondolea tamaa ya wizi.

Naamini hata huyo mzungu wako ataamini kuwa ukoo wa ngonyani sio mchezo na una watu makini na mahiri katika kuzitafuta ngawira.

Dada huku nyumbani nimeanzisha mradi wa kuhamasisha ukimwi. Na nimeona nikushirikishe ili wote tuwe matajiri, lakini usidhani nakushirikisha bure, lazima utoe kamchango kako kama kianzio yaani utoe mtaji, kwani usione vinaelea vimeundwa. Sasa ili uwe na wewe ni mmiliki wa NGo yangu…….hapana yetu inabidi utumbukize kama Krona Milioni mia moja ili tuweze kuwavuta wafadhili kuwa NGo yetu sio ya kuganga njaa, dada naamini hizo pesa unazo kwani huyo mzungu wako hawezi kukosa pesa kidogo hivyo, maana hicho kiasi cha pesa ni kama vile anatoa hela ya kununulia Tooth Picks. Naomba hizo pesa uzitumbukize kwenye akaunti ya NGo yetu ambayo ni XXL 000055557788JK/KoeroNGo/Yasinta/Camilla/Eric.com hiyo ndiyo akaunti namba yetu.

Kama nilivyokwambia kuwa nimeanzisha huu mradi wa Ukimwi ambao nimeamua kuuita Intaneshino NGo for fool people of Ruhuwiko die because of ngono zembe. Na kama unavyoona hilo jina linatisha na kuvutia sana.

Dada huku ili uweze kuishi kwa amani na usalama ni lazima uwe mbunifu, ili uweze kuendesha gari linaloitwa Rav 4 au Toyota Haria ni lazima uwe na akili ya ziada ya kuwaona wengine ni wajinga na wewe ndiwe Generali Brigedia mwenye akili nyingi kuwazidi.

Mradi wetu wa ukimwi unaendeshwa kwa njia ambayo ni lazima tutapata fedha za wafadhili kwani tuna watu wanaoweza kubuni na wengine wanaoweza kutusaidia kuthibitishia dunia kwamba Tanzania inayo watu wanaoteketea kwa ukimwi hata kabla bwana hajarudi katika ule ujio uliotabiriwa kwenye kitabu kitakatifu cha biblia.

Kwanza tunajitahidi kuwasiliana na wafadhili na kuwaeleza kwamba huku nchini katika kila watu kumi unaokutana nao, basi kumi na moja wana virusi na kumi na mbili kati yao tayari wanaumwa mahututi. Na ili upate fedha za wafadhili haraka ni lazima takwimu zako ziwe zimechanganyikiwa kidogo kwani takwimu zikiwa sahihi wafadhili lazima wataingia mashaka au watakweri .

Sisi tuna mtaalamu wetu mmoja aitwae Chacha o’Wambura Ng’anambiti ambaye ni mwenyeji wa kule Kyabakari Barracks Musoma, Mara. Huyu kijana tumemuingiza katika mradi wetu kwa kuwa anajua kubuni na kutunga kiasi kwamba anaweza kukushawishi kwamba jina lako sio Yasinta bali unaitwa Jasimini na ukakubali.

Hata hivyo yuko kijana mwingine aitwae Kamala Lutatinisibwa, ambaye amelikimbia jiji la Dar Es Salaam na kwenda kuishi kule Karagwe kutokana na ukata, huyu ndio yuko kwenye mchakato wa usaili akiwania nafasi ya Meneja mahusiano katika NGo yetu. Unajua hii nafasi ya meneja mahusiano inahitaji watu makini na mahiri walio na utaalamu wa utambuzi. Kama atafauli katika usaili atatusaidia sana katika kupiga tiralila za propaganda kwa wafadhili pale watakapotaka kuthibitisha takwimu zetu.

Kwa upande wa huyu kijana Chacha o’Wambura Ng’wanambiti kazi yake ni kuandaa taarifa za kuombea pesa kwa mujibu wa matukio yaliyo katika jamii kwa wakati huo.

Kwa mfano hili tatizo la mafisadi lililoikumba nchi yetu, huyu mwenzetu amewaandikia wafadhili akiwambia kuwa Mafisadi na ukimwi ni ndugu kabisa kwani ukimwi unasambaa sana katika kipindi hiki ambacho mafisadi wameshika hatamu za nchi, kwa sababu mafisadi hao wamekwiba fedha za Richimondi ambazo zingesaidia mradi wa umeme vijijini na kwa kuwa mradi huo umekwama na kusababisha vijiji vyetu kama vile kule Ruhuwiko, Kashasha, Kyabakari, na kwingineko kukosa umeme, watu wanatumia fursa hiyo kuendelea kufanya ule mchezo mtamu gizani yaani ule mchezo ulikataliwa na mungu katika amri ya sita katika zile amri zake kumi.

Ameendelea kuwaeleza kuwa kwa kuwa huko vijijini bado wananchi wako gizani kutokana na kukosa umeme wanaume hawavalishi vilambio vyao vifanyio na inakuwa ni vigumu wanawake kug’amua janja yao kwa kuwa kuna giza totoro na hivyo kuambikizwa ukimwi kirahisi.

Kijana huyo ameendelea kuandika kwamba katika utafiti wetu tumegundua kuwa wakati mwingine hata wale wauza vifanyio huwauzia wateja vifuko vya ashikirimu wakidai ni vifanyio orijino kumbe ni feki, na hivyo vinashindwa kuhimili vishindo na kupasuka kiurahisi.

Kutokana na Write up hiyo Wafadhili wametujibu kwamba utafiti wetu ni wa kiwango cha juu na wameahidi kutupatia kiasi kikubwa cha pesa ili kudhibiti hali hii ya vijana kuendelea kuambukizana ukimwi ambapo unachagizwa na kupenda sana ngono.

Dada namuona Chidakwa, huyu binti wa mzee Makalioni anakuja kwa kasi sijui baba yake kabuni msiba mwingine ili tumpe michango ya rambirambi, hebu ngoja nifiche huu waraka maana akiuona atakwenda kumwambia baba yake ili na yeye aanzishe NGo yake na kujipatia fedha…….unajua dada ukiwa na aidia zilizokwenda shule inabidi ufanye siri maana kuna wezi wa aidia ile mbaya, unaweza kushangaa wenzako wamekupiku……hebu ngoja nimsikilize…..nitakumalizia hii habari wakati mwingine…LOL

Saturday, April 17, 2010

TAFAKARI YA LEO: IMANI INA NGUVU KIASI GANI?

Nikiyagusa mavazi yake tu nitapona

Tafakari ya leo tuangalie mfano huu wa imani kwa kusoma habari hii ya mwanamke aliyekuwa akitokwa na damu, katika kitabu cha Marko 5:25-34.

Nitanukuu kutoka katika Biblia Takatifu:


“Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na mbili na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa na vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya. Aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka , naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je! Wawaona makutano wanavyokusonga-songa , nawe wasema , Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo, Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.”

Huyu mwanamke alikuwa na hili tatizo kwa miaka 12, ambayo kwa kweli ni miaka mingi sana kuishi na ugonjwa. Na alijaribu kila njia, akitafuta tiba lakini hakuweza kupona.

Hata hivyo kitu kimoja kilichonivutia ni kwamba, pamoja na kuhangaika kwa miaka yote hiyo akitafuta tiba lakini hakukata tamaa, na baada ya kusikia habari za Yesu akaona ni vyema ajaribu huenda atapona, na hakika kutokana na imani aliyokuwa nayo akapona. Bwana yesu asifiwe!

Watu wengi wanadhani kuwa imani ni kama mazingaombwe kwamba unaamini tu halafu imani yako inakuletea kila kitu unachohitaji mikononi mwako .
Hii haiwezekani. Iwapo fikra hasi, au matamshi yako ni ya kukata tamaa na hujiamini, imani haiwezi kufanya kazi kwa mtu wa namna hiyo.

Kwa nini?

Ni kwa sababu Imani sio kitu kinachofanya kazi papo kwa hapo, bali inahitaji mchakato fulani huku ikirutubishwa na fikra chanya.

Ili imani iweze kufanya kazi ni lazima ipitie katika mchakato ufuatao ndio ufanye kazi:


Uamuzi: Kumbuka kwamba huyu mwanamke alikuwa amejaribu tiba kadhaa wakiwemo madaktari bingwa na maarufu, hakuweza kupona, lakini aliposikia habari za Yesu akafanya uamuzi katika moyo wake kwamba kupitia Yesu Kristo atapona. Huo ni mchakato wake wa kwanza kabisa kuelekea katika kupona.

Imani: katika Marko 5:28 yule mwanamke alisema “Nikiyagusa mavazi yake tu nitapona” Ile kauli ya kusema “Nitapona” ni kauli chanya na yenye nguvu na kama tulivyoona kuwa inatoka kwa mwanamke ambaye alikuwa amejaribu tiba kadhaa kwa miaka 12 bila kupona.
Ni katika Matayo 9:20:22 tunaposoma kuwa alijisemea kauli hiyo kutoka moyoni mwake. Hapo ndipo tunapoona kuwa ni kwa jinsi gani imani inavyokuwa na nguvu hata kwa kujisemea moyoni tu, inatosha kufanya jambo liwe.

Kutenda: Katika Marko 5:27, tunasoma kuhusu, mwanamke huyo Alivyopenya katika kundi la watu na kwenda kugusa mavazi ya Yesu Kristo.
Ni kitu gani kilimsukuma hadi akaamua kujipenyeza katikati ya kundi la watu ili tu kugusa mavazi ya Yesu?
Ni kwa sababu aliamini neno la mungu na ndio sababu ya yeye kuchukuwa uamuzi.
Kutenda kile unachokiamini ndio njia sahihi ya wewe kuelekea katika kufanikiwa, haitakiwi kusema tu, hiyo haitoshi.

Ili imani iweze kufanya kazi ni lazima upitie katika mchakato huo ndipo imani iweze kufanya kazi.


Tukutane Jumamosi ijayo.........

Friday, April 16, 2010

UNAPOSUBIRI KUSIFIWA!


Unapofanya jambo lolote, fanya tu kama nafsi yako inakubali na inafurahia jambo hilo.
Usifanye jambo kwa kutegemea kusifiwa. Kumbuka usiposifiwa itakuuma sana, lakini ukisifiwa bila kutegemea sifa hiyo, utajisikia furaha sana.

Bila shaka utakubaliana na mimi kuwa Binadamu ni kiumbe anayependa kusifiwa, lakini ikitokea ukawa na kiu kubwa ya kupenda kusifiwa , basi inabidi ujiulize, ni wapi pana kasoro kwenye fikra zako.

Haiyumkini katika malezi yako hukuwahi kusifiwa kamwe na maisha yako yalitawaliwa na kulaumiwa kwingi na kukosolewa, hivyo ukajikuta ukihitaji kukamilishwa.

Haya burudika na shairi hili la Malenga wa Mvita.

UWATAPO HAKI YAKO


Namba nawe mlimwengu, pulikiza matamko
Nikweleze neno langu, uzinduwe bongo lako
Nayo nda M'ngu si yangu, na ayani haya yako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni


Simama uitete, usivikhofu vituko
Aliyo nayo mwendee, akupe kilicho chako
Akipinga mlemee, mwandame kulla endako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni


Amkani mulolala,na wenye sikio koko
Isiwe mato kulola,natutizame twendako
Tuwate na kuduwala,usingizi si mashiko
Uwatapo haki yako,utaingiya motoni


Teteya kwa kula hali, usiche misukosuko
Siche wingi wala mali,sabilisha roho yako
Unyonge usikubali, ukaonewa kwa chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni



Siche kifaru na ndovu, wangazidi nguvu zako
Wapempe kwa uwekevu, unusuru haki yako
Siandame wapumbavu,kilicho chako ni chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni


Cha mtu hakifitiki,kikafungiwa kiliko
Huzuka kikawa hiki,kazana utwae chako
Uwatapo yako haki,fahamu ni dhara kwako
Leo na kwa Mola wako,utaingiya motoni



Fumbuwa unyang'arize, uone duniya yako
Bure sijiangamize,kuangalia wendako
Utatupa upoteze,wende ambapo si pako
Uwatapo haki yako,utaingiya motoni


Kadhalika nako pia,huko ambako sikwako
Huwezi kujitetea,wala huwi na mashiko
Basi iwaze duniya,kwani ya kale hayako
Uwatapo haki yako ,utaingiya motoni


Kadi tamati shairi,sitii la ongezeko
Mwanati iwa tayari, utete haki yako
Unyonge usiukiri,Jifunge ufe kwa chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

Shairi hili limetungwa na Ahmad Nassir wa Malenga wa Mvita

Thursday, April 15, 2010

KILA MWELEKWA NA TEMBO…..

Waelekwa na Tembo

Upo msemo mmoja kwa watu wa Pwani usemao Kila mwelekwa na Tembo haachi kugea kani. Huu ni moja ya misemo mingi katika jamii zetu. Je msemo huu una maana gani?
Msemo huu unamaanisha kwamba yule abebwaye na Tembo haachi madaha au maringo.
Katika familia zetu hizi za Kiafrika, sina uhakika sana na za wenzetu huko Ughaibuni, na ndio maana ningependa kuzungumzia zaidi familia za Kiafrika kwa kuwa ndizo ninazozifahamu zaidi.
Katika malezi ya familia zetu hizi za Kiafrika, huwa inatokea mtoto mmoja akawa ni kipenzi cha wazazi yaani baba na mama ukilinganisha na watoto wengine.
Hii haijalishi mtoto huyu anacho kipato au hana, anaweza akawa ni mkorofi na asiyejali wazazi au hata kujijali yeye mwenyewe.
Lakini kama bahati ya kupendwa imemdondokea hakuna wa kupinga. Nasikitika kwamba bahati hii sikuipata mimi katika familia ya mzee Japheti Kisarika Mkundi na mama Namsifu Kiangi Mkundi.
Hata hivyo sina maana kuwa sikitiko hilo ni lawama, la hasha, bali ni namna wazazi wetu wanavyowapenda zaidi baadhi ya watoto wao.
Watoto wa aina hii mara nyingi nao hawaishiwi vituko, ninaamini ni kutokana na kutambua kwao wao ni Kipenzi cha wazazi.
Inaweza ikatokea labda watoto mnaishi huko mjini na mkaamua kuwapelekea wazazi fedha za matumizi,na nguo. Lakini unaweza kushangaa kukuta pesa kapewa kiasi na nguo vile vile.
Wakati mwingine unaweza kukuta wazee wanavaa nguo zenye viraka, chafu na hazistahili kuitwa nguo kwa kiasi fulani, lakini mtoto wao huyo mpendwa kapewa nguo ambazo mlitaka wazazi wajisitiri.
Wazazi hawa hawajijali wao kwanza, bali humwangalia kipenzi chao, na kufanya mambo ambayo yatampendeza. Tena mambo yenyewe ni upendeleo, na yenye kila dalili za kumjali zaidi mtoto huyo kuliko wenyewe.
Na ikitokea mtoto huyo anasababisha vurugu au ugomvi katika familia au kwa watu wengine, kisha walalamikaji wakayafikisha kwa wazazi wake. Utashangazwa licha ya ushahidi wa wazi kuonyesha mtoto wao ni mkorofi, lakini wazazi watamtetea.
Hivyo ndivyo ilivyo katika baadhi ya familia zetu hizi, na watu tumeyakuta hayo na tumeyazoea na pengine na sisi tunayatumia katika familia zetu au tutayatumia huko siku za usoni.
Jambo hili lipo ni katika familia, lakini pia hata katika masuala ya uongozi shiranga hilo lipo. Iwe ni kwenye uongozi katika sehemu za kazi au hata katika uongozi wa kisiasa.
Ni rahisi kujionea upendeleo wa wazi kabisa na wakati mwingine unazusha malumbano miongoni mwa viongozi wenyewe.
Leo ningependa kuzungumzia uongozi wa nchi, na hapa nataka kuzungumzia mamlaka ya juu kabisa ya nchi yetu hii.
Niliwahi kusimuliwa kuwa hata enzi za Hayati baba wa taifa Mwalimu J.K Nyerere, kulikuwa na baadhi ya viongozi ambao walikuwa wakigea kani.
Ilikuwa hata wafanye makosa ya wazi lakini mzee wa Mwitongo huko Mara alikuwa akiwahamisha kutoka sehemu hizo na kuwapeleka sehemu nyingine na huko pia waliendelea kuvurunda.
Lakini aliwavumilia tu, mpaka alipong’atuka madarakani na kujipumzikia hadi kifo chake kilipomkuta. Mungu amlaze mahali pema.
Zilipita awamu mbili baada ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Awamu ya pili ya Rais Mstaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Naye alikuwa na watu wake waliokula Tende na Halua, akaja Rais wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamini Mkapa, na yeye alikuwa ana wapendwa wake ambao walikunywa Asali na Maziwa.
Sasa tuko kwenye awamu ya nne ya mheshimiwa Jakaya Kikwete, hapa ndipo ninapopata kizunguzungu kabisa na mambo kuwa vululuvululu.
Maana hao waliopata bahati ya kuelekwa na Tembo siyo kwamba wana gea kani tu bali pia wanadhulumu kila kitu na kuwaacha wanyonge wakiteseka, wasijue la kufanya.
Awali kulikuwa na taarifa zilizotolewa na wapinzani pale Temeke Mwembe Yanga kuwa kuna mabilioni ya fedha yametafunwa, lakini wenye mamlaka wakayapuuza madai hayo, na kuonekana kama vile ni uzushi.
Na wengine wakatuhabarisha wanakwenda mahakamani kumshtaki Dr Slaa, lakini mtu mmoja tu alihoji busara za hao wanaotaka kwenda mahakamani naye ni waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba.
Mzee huyu alisema waziwazi kuwa endapo watakwenda mahakamani, wataumbuka na yatazuka mambo ambayo wenyewe wanadhani hayajulikani kwa baadhi ya watu. Ngebe zao ziliishi na hawakwenda mahakamani, ingawaje hawakukoma kuchokonoa.
Sasa baada ya kuchokonoana kwa muda mrefu ndipo kukazuka songombingo la kutajana miongoni mwao, sababu wapinzani walisema kama mhusika hakufanya basi kwa mamlaka yake aliachia suala hilo lifanyike, hivyo awajibike.
Na la maana zaidi, bila shaka sote ni mashahidi wa kile kilichotokea baadaye. Nina hakika baada ya watunga sheria wa chama tawala kule Mjengoni, na pengine ni kutokana na kuchoshwa na vitendo hivyo au ni kutokana na kutoswa na kunyimwa mgawo, wakachachamaa.
Mpaka mwenye mamlaka ya kuiongoza nchi akaridhia wateule wale warejeshe ile akiba waliojichotea ghalani la sivyo wasije wakamlaumu………Ebo! mtu ajichotee tule tuakiba twetu ghalani bila ya ruksa yetu halafu anaambiwa tena kwa kubembelezwa kuwa arejeshe mwenyewe kwa hiyari yake la sivyo asije akalaumu…….
Kimya kimya tukasikia magwiji kukwiba wamerejesha mkwanja na ili kutufumba macho wakakamatwa wachuja nafaka kadhaa na kufikishwa kwa Pilato.
Pamoja na kukamatwa kwao kuna kiini macho huko mpaka leo kuna tamthiliya inaendelea huko ikisubiri oktoba uchaguzi upite mambo yaishe kimya kimya…..ni nani asiyetujua kwa kusahau, na mwanzo wake wameenza na kuzusha mijadala mingine ili kufunika funiko la chuma kwa wachotaji wale.
Hivi sasa, kumeibuka mengine tena, kuwa waelekwa na tembo wamechota ile akiba walioirejesha, kule kwenye ghala letu kuu, wakisingizia Kilimo kwanza.
Hivi inakuwaje mambo haya lakini, mbona kwa wenzetu wako macho, na hawakubali ujinga huu?
Hivi karibuni tumeshuhudia kule Kazykhstan, Rais aliyekuwepo madarakani ambaye hata hivyo walimchagua wenyewe kwa kura nyingi tu lakini wamemtoa madarakani na kinga ya kumlinda kisheria imeondolewa.
Si hivyo tu kule Thailand tumeshuhudia wananchi wakivunja uzio wa jengo la Bunge na kulivamia Bunge kiasi cha kusababisha Waziri mkuu na wabunge kuondolewa kwa Helikopta.
Kwa Thailand kila mmoja anaelewe kile kilichomkuta Thaksin Shinewatra. Alipoondolewa kwa madai ya rushwa na ubadhirifu alipigiwa kelele, lakini leo wananchi walewale waliompigia kelele walipochagua serikali nyingine kumbe nayo ni yaleyale.
Sasa wanamgeukia Shinewatra, na ndiyo maana wakaamua kuvamia mjengoni ili kieleweke maana iliwachosha kuona wadokozi wakiendelea kumaliza ghala yao.
Namini hata sisi tunaweza kukataa ujinga huu, kama wao wameelekwa na Tembo na sisi tumeelekwa na Mungu tuone ni nani mjanja.
Hebu tujiulizeni wote hivi mambo haya mpaka lini, tunahitaji kuamka na kusema basi imetosha.
Nchi haina huduma muhimu za kijamii, hospitali huko vijijini hakuna, na kama zipo hazina dawa, wananchi wanalazimika kutembea umbali wa kilomita kadhaa kufuata huduma hizi huku watu wakiwapoteza wake zao na watoto kutokana na vifo wakati wa kujifungua kutokana na huduma duni.
Huduma ya maji ni duni wakati tuna mito na maziwa nchi nzima, achilia mbali huduma za barabara, kuna mikoa mingine haifikiki kutokana na miundombinu duni.
Fedha hizi licha ya kusaidia kilimo kwanza lakini pia zingeweza kuboresha huduma za kijamii hapa nchini.
Angalia watu katika Kilimo Kwanza wanachota Viatirifu,vocha za pembejeo na kadhalika. Hawa wanajulikana, lakini hawachukuliwi hatua zozote.
Halafu hivi sasa ndio kwanza wameshaanza kuzindua mpango wao wa kuwakamua wananchi hawa masikini kwa njia ya mtandao, tena uzinduzi wenyewe umefanywa kwa mbwembwe na shajara iliyogharimu fedha za walipa kodi.
Yaani kwa sasa tumekuwa tukichotewa ghala yetu halafu tunageukiwa hata ghala za majumbani mwetu zichotwe. Hivi sisi ni watu wa aina gani tusiotambua maana ya maendeleo?
Au maendeleo ni hizo kamari za kuchangia chama ili kiendelee kutuchotea ghala yetu ibakie tupu? Wakati wachotaji na waidhinishaji uchotaji wapo tena walikaa meza za mbele kabisa kuchangishana, na hawajashukuliwa hatua zozote.
Wapare wanayo methali moja inasema "Mshughu kurughe" yaani ni kama M’baazi kujipika, kwamba unaweza kuvuna mbaazi na kisha shina lake likatumika kama kuni na kuzipika mbaazi hizo.
Na ndicho tunachokishuhudia sasa, wananchi kukaangwa na fedha zao, tuchange fedha ziwawezeshe kuingia madarakani kisha tukione cha mtema kuni.
Ndugu zangu, tusipotatua kero ya leo, itakuwa kero ya kesho, na tusipotatua kero ya kesho itakuwa kero ya leo.
Together we can…………..

Tuesday, April 13, 2010

HIVI NAWAZA……AU NAOTA TU….!!!!!!????

Hebu nijipumzishe mie.....

Baba Kwembe?…….Baba Kwembe?……{Anaweka mzigo wa kuni upenuni mwa nyumba, kisha anatembea huku akiwa amejishika kiuno hadi chini ya mti ambapo mumewe alikuwa ameacha redio ikiwa imefunguliwa kwa sauti ya juu, anapunguza sauti na kuwa ya wastani}
Najua utakuwa na njaa mume wangu, lakini chakula kitakuwa tayari hivi punde…..{anaingia jikoni na anaweka chini kikapu kilichokuwa na mboga za majani alichokuwa amekibeba}…. Nimechelewa kidogo kurudi tangu uliponiacha shambani kwa sababu nilikuwa nakutafutia uyoga wako….si uliniambia kuwa leo una hamu na uyoga pori?………

Mwenzio leo nusura niumwe na nyoka uliponiacha shambani wakati natafuta kuni,..............Si nikaingi kwenye kile kijipori, pale karibu na shamba la mzee Ngabu, ……Hamadi nyoka huyu, tena Swila, kama si kumuwahi kumkata kichwa na panga angeniwahi wallahi…{ Anatoa mboga za majani na uyoga pori ndani ya kikapu na kuweka ndani ya sufuria ili kuosha}……Leo nimechoka ajabu na kesho natakiwa kliniki……si unajua kesho ndio siku yangu ya kwenda Ludewa Mission ili kusubiria siku yangu ya kujifungua…….

mume wangu,...... hivi umekumbuka kweli kupeleka baiskeli kwa fundi, sidhani kama nitaweza kutembea umbali wote ule kilomita tano!!!!.......Sitaweza…..nimechoka mwenzio ndio naingia mwezi wa tisa hivooo….. {anaosha mboga za majani kisha anamalizia kuosha uyoga. Anatoka nje kuchukua kuni huku akiwa amejishika kiuno kutokana na kuelemewa na ukubwa wa tumbo la ujauzito, anachukua kuni na kurejea jikoni na kukoka moto}……Nataka niwahi kupika kabla Kwembe hajarudi shule, maana najua akirudi atakuwa ana njaa ajabu….si unajua leo sikumfungashia viazi vyake vya kula shuleni….

Baba kwembe…. njoo basi huku jikoni uzungumze nami wakati napika……..tena kuna ndizi mbivu hapa waweza kutafuna kutuliza njaa wakati nakupikia mume wangu….. {Anainjika sufuria ya mboga za majani jikoni huku akaiendelea kukatakata nyanya na vitunguu}…..Miguu yangu imevimba ajabu…..hivi nitaweza kweli kutembea kesho kweli…….Basi nilitaka kusahau, wakati narudi njiani nimekutana na mzee Mwalyosi anadai kesho kuna kikao cha kujadili utaratibu wa kugawa pembejeo za kilimo…..kuna mgeni atakuja kutoka wilayani kuja kusikiliza kilio chetu baada ya kupata malalamiko juu ya uuzwaji wa vocha za pembejeo za kilimo kwa bei ya mchoromchoro….

{Anajimiminia togwa kwenye bilauri na kupiga funda kadhaa na kushusha pumzi…..Anaepua mboga baada ya kuiva na kuinjika uyoga jikoni}……Baba Kwembe, njoo basi unywe hata togwa basi kutuliza njaa……

Heeeee! {Anataharuki ghafla}……. Baba Kwembe si tulikubaliana kuwa uache kuvuta misigara yako, sasa huu mtemba hapa ni wa nani…{ Anauchukua ule mtemba na kutoka nao nje}…..Si ulishauriwa na Dakitari kuwa misigara yako itanidhuru mie na mtoto tumboni………hivi uko wapi wewe…. Mbona kama naongea peke yangu….

Mh..mhu..mhu….{inasikika sauti ya mwanaume akikohoa nyuma ya nyumba}…..niko huku narekebisha choo, kimebomoka…..
Njoo kwanza basi unywe togwa utulize njaa……{anareja jikoni na kuketi}

Jamani hii sio sinema, bali nilikuwa nawaza tu………………
TAMTHILIA HII ITAENDELEA.........

Sunday, April 11, 2010

TAFAKARI YA LEO: IMANI KATIKA NENO TAKATIFU

Nabii Eliya katika maombi
Baada ya kutafakari kwa kina nimepata wazo la kuanzisha kipengele cha Tafakari ya Leo, ambacho kitakuwa kikuzungumzia neno takatifu la Mungu. Kipengele hiki kitakuwa kikiwajia kila siku ya Jumamosi ambapo ni siku yangu ya kupumzika na kumtumikia Mwenye enzi Mungu.

Katika kukumbushana huko, nitaelekeza fikra zangu juu ya maandiko matakatifu na hata nukuu mbalimbali kutoka kwa Wanafilosofia waliowahi kuishi hapa duniani wakiwemo Manabii.

Jana nilishindwa kuweka kipengele hiki kutokana na mtandao kupata kwikwi. Lakini kwa kuwa leo mtandao umetulia ninawaletea kipengele hiki kama ifuatavyo, naomba tutafakari kwa pamoja:

Leo ninaanza na somo la imani, hebu tuangalie 1Wafalme 18:42, nitanukuu,
“Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka ule, na unywe; kwani pana sauti ya mvua tele”

Mwisho wa kunukuu.
Kama tulivyosoma fungu hilo hapo juu, Nabii Eliya akimwambia Ahabu ainuke ale na anywe kwani pana sauti ya mvua tele.

Ukweli ni kwamba kulikuwa hakuna mvua, pia mawingu yalikuwa hayaashirii kuwepo kwa mvua, pia hata upepo ulikuwa hauvumi kuashiria kwamba kungenyesha mvua. Lakini Nabii huyu wa Mungu Eliya alisema, “Nasikia sauti ya mvua tele”

Kwa kauli hiyo ya Nabii Eliya inanionyesha kuwa katika swala la imani, kusikia ni dalili muhimu kabla ya kuona kile unachokitarajia.


Tatizo la kwa nini sisi tunakuwa na imani haba kiasi cha kutofanikiwa katika kila tulitendalo ni kutokana na kutaka kuona kile tunachokitarajia kabla ya kusikia kwanza.

Nabii Eliya Alisema kuna sauti ya mvua tele, hebu tuliangalie kwa makini neno “Sauti” kwa sababu neno sauti anazungumzia kelele na matokeo yake.


Pia ni vyema ukijua kwamba sauti aliyokuwa akiisikia sio halisi bali ilikuwa ni ya rohoni.
Katika biblia tunasoma kuwa Nabii Eliya alimwagiza mtumishi wake kwenda kuangalia iwapo kuna dalili ya mvua, na mtumishi huyo alikwenda mara sita kuangalia, lakini alirudi na jibu lile lile kuwa kulikuwa hakuna dalili ya mvua.

Labda wewe unayesoma hapa leo uko katika hali hiyo hiyo, umeshajaribu kila kitu na una imani katika kufikia malengo yako lakini imani yako imekuwa ni bure kabisa.


Hakuna kinachotokea na maisha yako yamekuwa ni yale yale, kama vile ilivyokuwa kwa mtumishi wa Nabii Eliya alivyokwenda kuangalia dalili ya mvua mara sita lakini akirudi na jibu lile lile la hakuna dalili ya mvua.

Labda kwa upande wako imekutokea katika kazi yako, biashara zako, ujuzi wako, elimu yako, na unaanza kupoteza imani kwa mungu au unafikiria kuachana na mungu na kutomwamini.

Nataka nikwambie leo hii kuwa kama imani yako ikisema ndio, hakika hata mungu hawezi kusema hapana.

Nabii Eliya alisema,… “Nasikia…” na hakusema….. “Naona….” Hii inaonyesha kuwa Nabii Eliya alikuwa anajua kanuni ya kuwa na imani.


Kwa hiyo na wewe ili dalili ya imani yako kufanya kazi ni lazima kwanza usikie ile dalili ya kupata majibu kutoka kwa mungu ni lazima ujiandae kuisikia dalili hiyo kutoka kwa mungu.

Lakini tatizo walilo nalo waumini wengi ni la kusikia. Katika biblia tunasoma katika Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”


Biblia haikusema kuwa “imani huja kwa kusikia neno” Kiasi gani utasikia inategemea na umbali unaoweza kuona.

Hebu tuangalie nyuma kidogo kwenye historia ya Abrahamu katika kitabu cha mwanzo 15:1. Mungu alimwambia Abrahamu “Usiogope Abrahamu, mimi ni ngao yako na thawabu yako kubwa sana”.

Lakini Abrahamu akamwambia mungu, “utanipa nini il hali sina hata mtoto”
Naamini kuwa tunafahamu kuwa hatimaye Abrahamu alikuja kupata mtoto.


Lakini hata hivyo kabla ya kupata mtoto, tuliona jinsi mungu alivyomchukuwa Abrahamu hadi ufukweni kuhesabu mchanga na pia alivyomchukuwa hadi nje wakati wa usiku na kumwambia ahesabu nyota. Unaweza kujiuliza kwa nini afanye yote hayo?

Naamini ni kwa sababu Mungu alitaka kubadili picha aliyokuwa nayo Abrahamu ya kutokuwa na mtoto.

Kwa somo hili naamini wote tumeona ni jinsi gani imani inavyoweza kufanya kazi iwapo tutafuata kanuni kama nilivyoeleza.

Tukutane Jumamosi ijayo……………

Friday, April 9, 2010

ASILIMIA 90 YA UCHUMI WA TANZANIA INAMILIKIWA NA WAGENI!

Tumebaki kuwa wachuuzi tu.

ZAIDI ya asilimia 90 ya uchumi wa Tanzania unaendelea kumilikiwa watu wenye asili ya Asia na Ulaya, takwimu zinaonyesha.

Takwimu hizo zimetolewa huku kukiwa na kilio kikubwa cha Watanzania wazawa, kutaka wajengewe mazingira mazuri ya uwezeshaji ili kumiliki uchumi wa nchi kupitia migodi mikubwa ya madini na maeneo nyeti ya kiuchumi.

Lakini wakati kilio hicho kikiwa hakijapata ufumbuzi, Taarifa ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, iliyowasilishwa katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi jana, ilisema watu wenye asili ya mabara ya nje wanaomiliki uchumi wa Tanzania ni sawa na asilimia moja ya Watanzania.

Takwimu hizo zilifafanua kwamba, asilimia hiyo 90 ya uchumi wa nchi umeshikwa na watu wenye asili ya Asia na Ulaya, wakati asilimia 99 ya Watanzania wazawa, hawana kitu.
Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizowasilishwa katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Omar Yusuph Mzee, tatizo la Watanzania weupe kumiliki uchumi, lilianza tangu wakati wa ukoloni.

"Wakati wa enzi za ukoloni na hata baada ya uhuru Watanzania wengi hawakuwa wakishiriki kikamilifu katika kumiliki uchumi wa nchi yao. Uchumi wa nchi umeendelea kutawaliwa na wageni wakishirikiana na Watanzania wachache," inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasema "asilimia 99 ya wananchi ni Watanzania weusi na asilimia 1 iliyobaki inajumuisha Waasia na Wazungu ambao wana miliki zaidi ya asilimia 90 ya uchumi wa nchi hii (Msambichaka, 2008).

"Hii ina maana asilimia 99 ya Watanzania halisi wanamiliki asilimia 10 tu ya uchumi wa taifa lao," inasisitiza ripoti.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kurekebisha kasoro zilizoko, ikiwa ni pamoja na kuanzisha (lililokuwa) Azimio la Arusha, Vijiji vya Ujamaa, Elimu ya Kujitegemea, Serikali za Mitaa, Vyama vya Ushirika, Sera ya Uwekezaji na Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma.
Inasema hata hivyo,juhudi hizo hazijazaa matunda yaliyotarajiwa na kwamba na kwamba kushindikana kwa juhudi za kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi yao, ndilo chimbuko la kubuniwa kwa mkakati wa kuwawezesha wananchi kiuchumi, katika ilani ya CCM ya mwaka 2000."

Habari hii imendikwa katika Gazeti la Mwananchi la tarehe 8/4/2010 na mwandishi Ramadhan Semtawa, nami nimeona niiweke hapa ili tujadili kwa pamoja.

Wednesday, April 7, 2010

MKE ASIYE NA MUME, AKAMCHUMBIE NANI?


Niolewe na nani mie!
Isingekuwa vigeni, mwanamke kuchumbia
Ningepita mitaani, mume kujitafutia,
Nisimuudhi Manani, ndio nimejizuia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Ndege maingainga, si jambo la kujitakia,
Mume mwema natamani, vipi tajitafutia?
Na mwanamume haini, sitaki kunichumbia,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Nimetulia nyumbani, sina mume kunioa,
Wanifuatao ndani, si wachumba wa kuoa,
Hutaka kunirubuni, maasini kunitia,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Ndege maingainga, si kosa langu sikia,
Niliolewa zamani na mume mwenye udhia,
Kanitia kilabuni, pombe kumchuuzia
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Mimi nikamuamini, huku machozi nalia,
Mume hii kazi gani, alokataza jalia?
Kheri tukate kuni, mimi nitakuuzia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Akapanda hasirani, na maneno akafyoa:
Mke wee mke gani, dini lini ulijua!
Alipozidisha kani, ndoaye nikajivua.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?

Wako mabwana wa shani, ningependa kunioa,
Hawamtii shetani, Munguamewaongoa,
Nao wamomashakani, kwa mabibi walooa,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?


Tu wema hatujuani, wake na waume pia,
Twaingia mashakani, kwa wenzi waso murua,
Namlilia Manani, mume mwema kunioa,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?



Nawe muombe, ndoa yenu kutulia,
Tusikuone mwakani, viragoumepania,
Mke na mume nyumbani, mumche Mola Jalia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?





Shairi hili limetungwa na Sheikh Amri Abedi, nami limenivutia nikaona niliweke hapa ili tujifunze kwa pamoja

Saturday, April 3, 2010

WAMALAWI NA NDOA ZA VIBINTI!

Mmoja wa wa waathirika wa ndoa hizo

Binti huyu naye ni miongoni mwa waathirika wa ndoa hizi za vibinti

Huyu sio babu na mjukuu wake bali ni mtu na mkewe

“Baba yangu wa kambo aliniamuru niache shule ili niolewe na mzee wa umri wa miaka 77, kwa madai kuwa umri wangu ni mkubwa ukilinganisha na darasa ninalosoma, kwani wakati huo ndio nilikuwa niko darasa la nne. Nilimkatalia na kumweleza wazi kuwa ningependa kuendelea na masomo”. Hivyo ndivyo alivyoanza simulizi yake binti huyu Balita Simpokolwe.

lakini hata hivyo kukataa kwake hakukuweza kumsaidia.

Kwani baba yake alianza kumtuma sokoni kuchukua fedha kwa mtu mmoja mzee hivi, ambaye alikuwa hamfahamu, ambapo alikuwa akipewa kiasi cha kati ya dola 5 mpaka 10, kiasi ambacho alitakiwa anunulie chakula na kiasi kinachobaki alikuwa kimpa baba yake huyo wa kambo.

Balita anakiri kwamba hakuweza kuhisi jambo lolole kuhusiana na zile pesa alizokuwa akipewa na yule mzee kwa kuwa aliamini kuwa yule alikuwa ni rafiki wa karibu wa baba yake wa kambo. Lakini wiki tatu baadae tangu awe anakwenda kuchukua fedha kwa mzee yule, alishangaa kumuona akija nyumbani kwao na jembe dogo la kulimia bustani. ( kwa mila za watu waishio Malawi Kaskazini hususan katika wilaya ya Nsanje jembe dogo la kulimia bustani inatumika kama ishara ya mahari)

“Nilishtuka sana, baada ya baba yangu wa kambo kunitaka nipokee jembe lile la bustani kutoka kwa yule mzee.(Kwa mila zao, binti kupokea jembe kutoka kwa mwanaume ni ishara kuwa amekubali kuolewa na mume huyo). Lakini huku nikiwa imechanganyikiwa, nilikataa kupokea jembe lile.”

Hata hivo mama yake aliungana naye kupinga binti huyo kuolewa kwa kuwa bado alikuwa ni mdogo, “baba yangu wa kambo alikuja juu akidai kuwa atampa talaka mama yangu iwapo atapinga mimi kuolewa na mzee huyo, na cha kusikitisha zaidi alidai kuwa haiwezekani nisiolewe na mzee huyo kwa kuwa tumeshakula fedha zake.” Alisema bintin huyo kwa masikitiko.

Hivyo alilazimishwa kuolewa na mzee huyo, lakini baada ya wiki mbili tangu aolewe kikundi kimoja cha kutetea unyanyasaji wa wanawake na watoto kiitwacho Chitipa Women’s Forum kilimuokoa kutoka katika ndoa hiyo baada ya kuwashwishi wazazi wa binti huyo wamrejeshe shuleni.

Belita Simpokolwe, sasa anaishi na mmoja wa baba zake wadogo, amefurahi sana baada ya kurejea shule kuendelea na masomo yake. Tukio hili ambalo lilimpata Belita Disemba mwaka 2008 lilimuacha akiwa na amesathirika kisaikolojia.

Kwa mujibu wa mwalimu anayemfundisha alikiri kuwa kuna wakati alikuwa anashindwa kuzingatia masomo yake pale kumbukumbu za tukio lile la kutolewa shuleni na kuozeshwa kwa nguvu linapomjia, lakini binti huyo ambaye alikuwa na miaka 13 wakati huo akiozeshwa, amemudu kuendelea na masomo yake ambapo anataka kutimiza ndoto zake za kuwa muuguzi hapo atakapomaliza masomo.

“Kinachoniuma ni kwamba nimekuwa ni muathirika wa ndoa ya utotoni baada ya wale niliowaamini kuwa watanitunza na kunilinda kunitoa kafara kiasi cha kutaka nisitimize ndoto yangu” alisema binti huyo aliyekuwa akisoma shule ya msingi Kawale kaskazini mwa Malawi, akiwa yuko darasa la sita wakati huo.

Belita ni mmoja kati yan mabinti walioathiriwa na mila marufu kama Kupimbira, ambapo mabinti hulazimishwa kuacha shule na kuozeshwa kwa wazee ili kujipatia mahari, na hii hufanyika bila hata ya binti kufahamishwa.

Wakati mwingine wazazi hulazimika kuwaozesha mabinti zao ili kulipa madeni.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na tasisi ya Chipita Women’s Forum inaonyesha kwamba ,taktibani asilimia 17 ya mabinti huachishwa shule na kuozeshwa kwa wazee, huku wengine wakilazimika kuacha shule wenyewe kutokana na unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na waalimu wa kiume na wanaume wakware wenye uchu wa kufanya mapenzi na vibinti.

Akizungumzia mila zinazotumika kuwakandamiza watoto wa kike na kuwakatisha shule Mwenyekiti wa Chipita Women’s Forum, Bi Ruth Mbale alizitaja mila kama ‘Kupimbira’, ambapo mabinti hulazimishwa kuacha shule na kuozeshwa kwa wazee ili kujipatia mahari, ‘Nhlanzi’ ambapo familia ya mke huozesha binti mwingine kwa mume wa binti yao kama zawadi kutokana na kuitendea wema familia husika, ‘Kulowa kufa’ mwanamke aliyefiwa na mume kuingiliwa kimwili na mwanaume mwingine ili kuondoa mkosi wa vifo kijijini, kwa kawaida shughuli hiyo hufanywa na mwanamume maalum wa kufanya shughuli hiyo. Mila hii pia inasemekana inafanyika hapa nchini hususana wilayani Ukerewe ambapo hujulikana kama ‘Kusomboka’, hii kwa hapa nchini hufanywa na wanaume na wanawake. Bi Mbale pia aliitaja mila ya ‘Fisi’ ambapo mume ambaye hana nguvu za kiume anamkodisha mwanume wa nje ili amuingilie mkewe kwa ajili ya kumpa ujauzito, lengo kuu ni kujipatia watoto.

Bi Mbale alikiri kupata ugumu katika kupiga vita mila hizi kutokana na usiri mkubwa uliokuwepo katika jamii hiyo ya watu waishio Kaskazini mwa Malawi.

Akizungumzia idadi ya mabinti waliiokolewa na taasisi yao tangu walipoanza kampeni ya kuwaokoa wanafunzi walioozwa kabla ya kumaliza masomo, Bi Mbale alisema kuwa wamefanikiwa kuwaokoa mabinti 40 waliokuwa na umri kati ya miaka 7 hadi 16 ambapo walirejeshwa shule na kuendelea na masomo.

Alisema kuwa, ingawa inakuwa ni vigumu kwa mabinti hao kurejea katika hali yao ya kawaida kabla hawajaolewa lakini huwapa ushauri nasaha hadi warejee kwenye hali zao za kawaida na kuendelea na masomo yao.

Habari hii nimeitoa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari ukiwemo mtandao wa inteneti