Sunday, April 11, 2010

TAFAKARI YA LEO: IMANI KATIKA NENO TAKATIFU

Nabii Eliya katika maombi
Baada ya kutafakari kwa kina nimepata wazo la kuanzisha kipengele cha Tafakari ya Leo, ambacho kitakuwa kikuzungumzia neno takatifu la Mungu. Kipengele hiki kitakuwa kikiwajia kila siku ya Jumamosi ambapo ni siku yangu ya kupumzika na kumtumikia Mwenye enzi Mungu.

Katika kukumbushana huko, nitaelekeza fikra zangu juu ya maandiko matakatifu na hata nukuu mbalimbali kutoka kwa Wanafilosofia waliowahi kuishi hapa duniani wakiwemo Manabii.

Jana nilishindwa kuweka kipengele hiki kutokana na mtandao kupata kwikwi. Lakini kwa kuwa leo mtandao umetulia ninawaletea kipengele hiki kama ifuatavyo, naomba tutafakari kwa pamoja:

Leo ninaanza na somo la imani, hebu tuangalie 1Wafalme 18:42, nitanukuu,
“Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka ule, na unywe; kwani pana sauti ya mvua tele”

Mwisho wa kunukuu.
Kama tulivyosoma fungu hilo hapo juu, Nabii Eliya akimwambia Ahabu ainuke ale na anywe kwani pana sauti ya mvua tele.

Ukweli ni kwamba kulikuwa hakuna mvua, pia mawingu yalikuwa hayaashirii kuwepo kwa mvua, pia hata upepo ulikuwa hauvumi kuashiria kwamba kungenyesha mvua. Lakini Nabii huyu wa Mungu Eliya alisema, “Nasikia sauti ya mvua tele”

Kwa kauli hiyo ya Nabii Eliya inanionyesha kuwa katika swala la imani, kusikia ni dalili muhimu kabla ya kuona kile unachokitarajia.


Tatizo la kwa nini sisi tunakuwa na imani haba kiasi cha kutofanikiwa katika kila tulitendalo ni kutokana na kutaka kuona kile tunachokitarajia kabla ya kusikia kwanza.

Nabii Eliya Alisema kuna sauti ya mvua tele, hebu tuliangalie kwa makini neno “Sauti” kwa sababu neno sauti anazungumzia kelele na matokeo yake.


Pia ni vyema ukijua kwamba sauti aliyokuwa akiisikia sio halisi bali ilikuwa ni ya rohoni.
Katika biblia tunasoma kuwa Nabii Eliya alimwagiza mtumishi wake kwenda kuangalia iwapo kuna dalili ya mvua, na mtumishi huyo alikwenda mara sita kuangalia, lakini alirudi na jibu lile lile kuwa kulikuwa hakuna dalili ya mvua.

Labda wewe unayesoma hapa leo uko katika hali hiyo hiyo, umeshajaribu kila kitu na una imani katika kufikia malengo yako lakini imani yako imekuwa ni bure kabisa.


Hakuna kinachotokea na maisha yako yamekuwa ni yale yale, kama vile ilivyokuwa kwa mtumishi wa Nabii Eliya alivyokwenda kuangalia dalili ya mvua mara sita lakini akirudi na jibu lile lile la hakuna dalili ya mvua.

Labda kwa upande wako imekutokea katika kazi yako, biashara zako, ujuzi wako, elimu yako, na unaanza kupoteza imani kwa mungu au unafikiria kuachana na mungu na kutomwamini.

Nataka nikwambie leo hii kuwa kama imani yako ikisema ndio, hakika hata mungu hawezi kusema hapana.

Nabii Eliya alisema,… “Nasikia…” na hakusema….. “Naona….” Hii inaonyesha kuwa Nabii Eliya alikuwa anajua kanuni ya kuwa na imani.


Kwa hiyo na wewe ili dalili ya imani yako kufanya kazi ni lazima kwanza usikie ile dalili ya kupata majibu kutoka kwa mungu ni lazima ujiandae kuisikia dalili hiyo kutoka kwa mungu.

Lakini tatizo walilo nalo waumini wengi ni la kusikia. Katika biblia tunasoma katika Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”


Biblia haikusema kuwa “imani huja kwa kusikia neno” Kiasi gani utasikia inategemea na umbali unaoweza kuona.

Hebu tuangalie nyuma kidogo kwenye historia ya Abrahamu katika kitabu cha mwanzo 15:1. Mungu alimwambia Abrahamu “Usiogope Abrahamu, mimi ni ngao yako na thawabu yako kubwa sana”.

Lakini Abrahamu akamwambia mungu, “utanipa nini il hali sina hata mtoto”
Naamini kuwa tunafahamu kuwa hatimaye Abrahamu alikuja kupata mtoto.


Lakini hata hivyo kabla ya kupata mtoto, tuliona jinsi mungu alivyomchukuwa Abrahamu hadi ufukweni kuhesabu mchanga na pia alivyomchukuwa hadi nje wakati wa usiku na kumwambia ahesabu nyota. Unaweza kujiuliza kwa nini afanye yote hayo?

Naamini ni kwa sababu Mungu alitaka kubadili picha aliyokuwa nayo Abrahamu ya kutokuwa na mtoto.

Kwa somo hili naamini wote tumeona ni jinsi gani imani inavyoweza kufanya kazi iwapo tutafuata kanuni kama nilivyoeleza.

Tukutane Jumamosi ijayo……………

10 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hii itakuwa safi sana ni jambo zuru. Amina.

Mzee wa Changamoto said...

Dadaaaaaaaaaaaaaaaaa
Nashukuru na kufurahi kuona umeanza kuja na vipengele. Tlizungumzia hili saana na hatimaye limewadia.
Nashukuru kwa tafakari na kwa kutujulisha kuwa kila Jumamosi (kwa msaada wa Mungu na upatikanaji wa mtandao) tutakuwa tunapata TAFAKARI.
Niko nawe na naamini watambua hili
Much Luv Sis

MARKUS MPANGALA said...

Amina Mchungaji,
chunga kondooo kwa tafakari,

lakini nasikitika siku hizi huniamshi jumamsoi kwenda kusali Lol..
Tafakari msomaji wa TAFAKARI YA LEO

Faustine said...

...Sikujua mahubiri ni moja ya kipaji ulichonacho...Hongera!

Mzee wa Changamoto said...

Eti mtu anawaza kuwa maendeleo haya yanaweza kutuletea KANISA LA KWENYE BLOG.
Na anahisi ndio ushaanza hivyo.
Maana kuwa na Pastor Koero... Duh!!
Duh

Just joking Dear

John Mwaipopo said...

hapa tupo pamoja kama tunavyokuwa pamoja katika mengine, japo kwa macho na mitazamo tofauti. au?

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Aksante sana Dada Mchungaji. Sina hakika kama ni hivo kwani yawezekana ushafunga ndoa na Mt hivo ukawa Mama mchungaji :-)

Uloyasema ni ya msingi wa kila kitu... Nakusubiria hiyo jumamosi sabato...lol

Jacob Malihoja said...

Mungu akubariki sana! Nimefurahi sana kuona kuwa Koero umeona umuhimu wa kutafakari na kutambua Wwepo na Nguvu za Mungu katika maisha na harakati mbali mbali ambazo mwanadamu anaendelea nazo. Lakini pia napotafakari andiko hili ulilolitoa japokuwa mimi si mtaalamu wa maandiko, napata picha kuwa sauti ya mvua inasikika na tuinuke tule na tunywe, sijui katika lipi.. lakini kuna dalili njema hapa katika jambo fulani muda si mrefu! Na tuendelee kusali .. na tutume mtu aangalie kama mvua inanyesha … na tusubiri kufunuliwa.. ninaamini andiko hilo lina sababu ama ya wewe mwenywe Koero kuielewa ama umepewa kwa nguvu iliyo juu kutupa unabii fulani.. haya na tusubiri tu kuna jambo linakuja hapa, tutafunuliwa muda si mrefu.

Jacob Malihoja said...

Mh! Du! hapa sijui nichangie nini .. lakini nimepata cha kuchangia... Haya wote na tumwombe mungu awasaidie wote waliochoka kukaa peke yao .. wako wengi mno hao.. wenye kilio kama hicho!!!! wako ambao mpaka sasa bado .. na kila mmoja ana sababu tofauti .. wengine kwasababu ya masomo .. wengine kwasabbu ya kuzunguka nchi mbali mbali kusoma na kikzi.. wengine sijui kwasababu gani .. ila kimsingi wote wakati wao umekuwa bado.. wakati ukifika kila kitu kinafunguka.. wakati ukifika jiwe lililowekwa pale mlangoni litaondoka siku ya tatu na matumaini yatarudi upya! na hivi naamini wengi kwa andiko alilotoa Koero huenda wengine wameambiwa wainuke wale na wanywe sauti ya mvua inakuja!

Anonymous said...

Utukufu kwa Mungu,kwa yote unayofanya,swali kwa nini?nchi za kiafrika viongozi hawaaminiki?katika imani zao,Utajiri tulionao afrika imekuwa kama laana?tutategemea imani za kujenga afrika kutoka nje mpaka lini?mpaka bunge tunategemea wahisani au ndio imani yetu haiko kwa Mungu,au tunataka kuona kwa macho ya nyama?? from new enghland .