Sunday, April 25, 2010

WAZEE WETU NA ISHARA ZAO

Mzee akirudi kutoka safari

Kwa hapa mjini hulka hii haipo sana ukilinganisha na kule vijijini. Inawezekana ni kutokana na mazingira ya hapa mjini yalivyo, labda na muingiliano wa makabila.

Hapa nazungumzia jambo ambalo hata wewe unayesoma hapa huenda unalitenda au umelishuhudia likitendwa wakati wa makuzi yako kule kijijini.

Kuna hulka moja ambayo hutumiwa na wazazi wa kiume kutoa ishara kila wafikapo karibu na makazi yao mara warudipo kutoka iwe ni matembezini, kazini au hata safari. Ishara hiyo inaweza ikawa ni kikohozi, kupiga mluzi, chafya kumsalimu mtu kwa sauti ya juu.

Nakumbuka wakati fulani nilipokuwa kijijini alikozaliwa mama yangu, nilifikia kwa mjomba wangu. Naomba nikiri kuwa nimejifunza mambo mengi sana kuhusiana na maisha kupitia mjomba wangu huyu. Ni mtu mwenye hekima na busara na anayefuata mila na desturi za wazee wa kale na hajaathiriwa sana na tamaduni za magharibi.

Nilikuwa nimezoea kumsikia akikohoa kwa sauti kubwa kila anapokuwa akikaribia nyumbani. Na shangazi alikuwa amezoea kutuambia “mjomba wenu huyo” alikuwa akisema hivyo kama vile anatoa tahadhari hivi.

Siku moja nilishikwa na shauku ya kujua sababu ya yeye mjomba kufanya hivyo kila arudipo kutoka katika matembezi yake. Kwa bahati nzuri mjomba ananifahamu kuwa mimi ni mdadisi na kwa kulifahamu hilo, alikuwa amejenga tabia ya kunieleza jambo kwa kina na mifano ili nisije kumchosha na maswali, nilimpenda kwa hilo.

Mjomba aliniuliza swali moja kabla ya kujibu swali langu. Aliniuliza “hivi unaujua msemo mmoja unaosema paka akitoka?” nikamalizia kwa kujibu, “Panya hutawala” alinyamaza kwa muda, akakohoa kidogo ili kusafisha koo, kisha akaagiza aletewe maji. Mtoto mmoja aliinuka kwenda kumletea maji akanywa funda mbili tatu kisha akaendelea.

Alinimbia kuwa kwa kawaida mtu anapoweka sheria nyumbani kwake mara nyingi hazifuatwi mwenyewe akiwa hayupo, Kama ilivyo kwa panya kutawala pale paka anapokuwa hayupo, basi ndivyo inavyokuwa kwa watoto pale nyumbani, baba anapokuwa hayupo.

Aliendelea kusema kuwa wazee wetu wa zamani walikuwa na hekima sana, na ndio sababu ya kubuni namna ya kutoa taarifa kuwa wamefika nyumbani kwa ishara ili hata kama kuna jambo pale nyumbani haliko sawa mkewe aweze kuliweka sawa ili kuepusha mumewe kuona dosari.

Kwa mfano inaweza kutokea labda kuna kiti ambacho baba amezoea kukikalia kila awapo nyumbani na kwakuwa hayupo basi watoto wakawa wamekikalia kiti hicho, mama akisikia ishara ya mumewe kuwa anakuja, basi alikuwa akiwaeleza watoto kuwa baba ameshafika ili wakae kwa heshima na kama yuko aliyekalia kiti cha baba aondoke kumpisha baba.

Na ili kuonyesha kuwa wazee wetu wana busara, walikuwa hawafanyi papara kuingia ndani baada ya kutoa ishara. Wanachofanya ni aidha kumsemesha jirani kwa kumsalimia huku akiwa nje na kuzungumza naye mambo mawili matatu katika kupoteza muda au kuingia msalani hata kama hajisikii kwenda huko, ili mradi kupoteza muda japo kidogo ili kumpa mkewe muda kuweka mambo sawa.

Kama inatokea baba amesafiri kwa mfano, na kwa kuwa zamani kulikuwa hakuna mawasiliano ya simu za viganjani kama siku hizi, basi siku akirejea haendi nyumbani moja kwa moja anaweza kupitia kwa rafikiye au kwenye maeneo wakutanapo wazee kupiga soga na hapo mtoto yeyote atapewa mkoba kama alibeba mkoba na kama hakubeba mkoba atampa fimbo au bakora yake na kama hivyo vyote hana basi atampa koti au kofia aipeleke nyumbani, lengo ni kutoa tarifa kwa mkewe kuwa amerudi.

Na ikitokea amerudi usiku sana, basi anaweza kupitia kwa rafikie na kuomba kulala hapo na asubuhi kukipambazuka mtoto anapewa mkoba kuutanguliza nyumbani.

Mjomba alisema kuwa utaratibu huo ulikuwa unaepusha mambo mengi sana, kwa mfano kufumania. wazee wa zamani walikuwa wana utambuzi wa hali ya juu, kwa sababu walijua kuwa sisi binadamu ni dhaifu, walijua wazi kuwa inaweza kutokea ibilisi akampitia mkewe na kuingiza mwanaume ndani ya nyumba yeye akiwa amesafiri, hivyo kwa kutanguliza ishara kabla ya kufika nyumbani ni kutoa mwanya kwa mkewe kuweka mambo sawa ili kuepusha fumanizi.

Jambo lingine ni kuepusha baba kutoa maelekezo kila arudipo nyumbani, inaweza ikatokea labda hapendi redio au TV ikafunguliwa kwa sauti au watoto kupiga kelele, kwa hiyo akitoa ishara ina maana kama redio au TV imefunguliwa kwa sauti basi sauti itapunguzwa na watoto watapunguza kelele na kuka kwa heshima.

Toafauti na wazee wa zamani, siku hizi, mambo yamegeuka, vijana wa siku hizi hawatoi ishara tena, bali wanavizia lengo ni kutaka kuona makosa na kukemea kila kitu. Wakati wazee wa zamani walikuwa wanatoa ishara kuepusha ugoni, vijana wa siku hizi wanavizia na kutegeshea kabisa, tena ataweka na wapambe ili kuhakkisha anafuamania.

Na ndio maana ndoa nyingi siku hizi haziishi migogoro na mahusiano ya wanandoa wengi yako vululu vululu. Kila siku kelele na ghubu haliishi ndani ya nyumba, kitu ambacho kingeweza kuepushwa kama hulka hii ya kutoa ishara ingetumika.

Sishabikii wanawake kutoka nje ya ndoa, lakini hebu tuangalie faida nyingine kama za kuepeusha baba kukemea jambo moja kila mara. Kuna uwezekano mkubwa akapata msongo wa mawazo. Kuna mambo ambayo baba anaweza kusema yasifanyike pale nyumbani lakini yakawa yanafanyika kinyemela, si paka akitoka panya hutawala? sasa paka akirudi na kulia “nyau” ni wazi kuwa panya watarudi kwenye mashimo yao na kujificha, na ndivyo inavyokuwa kwa watoto pia.

Ni sawa na mzazi kumkuta binti yake uchochoroni mtaa wa saba akiwa na mwanaume, kwa baba mwenye busara pamoja na kumkemea bintiye lakini atajua kuwa binti yake kafanya heshima kwenda mbali na nyumbani kwao na kujificha uchochoroni asionekane na kama bahati mbaya mzazi yule akamuona. Lakini kama atamkuta nyuma ya nyumba yao, hapo ajue kwamba heshima hakuna tena hapo.

Lakini pia mambo yamegeuka, sio kama zamani, siku hizi kina Koero hatujifichi tena vichochoroni, ya nini kuliwa na mbu usiku au kukabwa na vibaka? Kama una mvulana wako unamleta nyumbani na kumtambulisha tu kwa wazazi bila wasiwasi, na sijui ni kutokana na huu utandawzi au sijui ni hizi TV, wazee nao kimya hawasemi hata.

Utakuta Koero kaja na mvulana wake Suruali iko mlegezo makalio yote nje,a kuwaambia wazazi wake, “huyu ni boy friend wangu” na wazazi nao bila aibu unawasikia, “Karibu sana kijana na ujisikie uko nyumbani” #$%^&$%^&*

Hicho ndicho kizazi chetu sie kina Koero na hakuna anayepiga kelele kukemea tabia hizi ilimradi kila mtu na lwake.

3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Zamani naipenda zamani!! Hivi kwa nini ya zamani ni mazuri kuliko ya sasa. Sijui nimepatwa na jini au vipi maana ukilinganisha sasa na zamani utakuta kila kitu ni tafauri watu, matendo nk. Watoto siku hizi hawasikii na hizo ishara ndo kabisa hazieleweki kabisa.

Anonymous said...

na ishara nyingine ni hii, wazazi walipotaka kufanya mambo ya baba na mama, walihakikisha watoto wamelala. Sasa walihakikisha vipi kama hao jamaa wamelala? basi walianza kumuita mmoja baada ya mwingine, wakiona kimya wanajua wamelala. Kwa mfano walikuwa wanaita; Koero, Koero, asipojibu walijua keshalala huyo, halafu wakamwita Yasinta, Yasinta, kama kimya basi walijua na huyo pia kalala, wakaendelea mpaka mtoto wa mwisho. Na kama ilitokea mmoja akaitika, basi aliombwa apeleke maji ya kunywa, halafu akasisitizwa akalale ili kesho awahi shule. zamani bwana!!!

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Anony: safi sana hiyo ni dhamani!

Siku hizi mwalimu wetu ni TV. Mabusu njenje si kwa baba/mama (wazazi) bali hata kwa watoto

uzungu umetamalaki. ngoja tuone utakapotufikisha :-(