Sunday, February 28, 2010

CHOZI LA MWANAMKE!

Kuzaa kwa shida

Kulea kwa shida

Kutafuta maji kilomita kadhaa tena ya kisima


Kutafuta kuni kilomita kadhaa

Kupikia familia zao

Kilio cha mwanamke wa Kiafrika ni nani akisikie!?

Ndugu wasomaji leo wakati natokea Karatu kuja Arusha mjini, njiani nilikutana na wanawake wakiwa katika shughuli zao za kila siku katika kuhudumia familia zao, nilikutana na wanawake wakitafuta kuni, wako waliokuwa wakitafuta maji tena umbali mrefu. hiyo ilinikumbusha madhila wayapatayo wanawake wa vijijini ambao wanaishi katika mazingira magumu ajabu, halafu tunaambiwa eti kuna usawa, utoke wapi?


Thursday, February 25, 2010

JAMANI HIVI HUWA NAELEWEKA?

Watoto huwa werevu kung'amua

Naamini wengi hamtanielewa kwa sababu hamjui leo ninataka kuandika nini. Hata wewe unayesoma hapa huenda ukasoma mwanzo mpaka mwisho lakini ukatoka kapa kwa kuwa najua utakua ni mmoja wa vilaza wa kusoma makala za kufikirika au kusadikika.

Nimekuwa nikijiuliza, hivi ni kwani nini watu huwa hawanielewi, nimekuwa nikijaribu kuandika kwa lugha nyepesi sana lakini sieleweki. Je uwezo wangu ni mdogo katika kueleza jambo likaeleweka au wale ninaowaandikia wana uelewa finyu wa kuelewa kile ninachomaanisha katika maandishi yangu.

Inashangaza sana kuona hata wale wanazuoni ninaowaamini nao pia wamekuwa ni wagumu kunielwa. Japokuwa ninatumia lugha nyepesi lakini bado wanashindwa kunielewa. Pamoja na kwamba leo hii nimejitahjidi sana kuandika kwa lugha nyepesi tena nimejitahidi kufafanua na kutoa mifano kadhaa, bado naona kuna ugumu watu kuelewea ujumbe wangu.

Wako wapi wanazuoni wenye ujuzi wa kusoma maandiko ya wengine na kuyatolea ufafanuzi hadi watu waelewe pasi na shaka?, wako wapi malenga wetu na wajuvi wa lugha wasaidie kutafsiri maandiko haya?

Hata wewe unayesoma hapa sasa hivi yawezekana usinielewe ninataka kuandika nini, lakini nakuomba usome maandiko haya kwa makini naamini utanielewa hapo baadae kuwa namaanisha nini.

Ni mara nyingi nimekuwa nikiandika juu ya kile niandikacho na nimekuwa nikiandika kwa lugha nyepesi sana lakini nasikitika kuwa wasomaji wengi hawanielewi kabisa. Labda leo niombe ushauri kwenu kuwa ni lugha gani nyepesi ambayo itakuwa ni rahisi kwenu kunielewa? Nikisema niandike Kiingereza naamini sitaeleweka maana nakijua kiingereza changu ni cha kuombea maji tu, nikisema niandike kipare lugha ya mama yangu ndio wee nitachemsha kabisa, na kichaga nacho lugha ya baba, lahaula, nitawachekesha walionuna.

Au nijaribu kuandika kwa Kiswidi, hapo itabidi niombe msaada kwa dada yangu Yasinta, lakini na yeye najua huenda hataeleweka kwa kuwa na yeye kajifunza lugha hiyo ukubwani. Au niandike kwa Kijapani, hapo itabidi niombe msaada kwa dada Mariam Yazawa. Mwe, mwenzenu nina kazi mimi, hata sijui nilitaka kuandika nini leo.

Hebu nikumbusheni, nilikuwa nataka kuandika nini vile?

Hata hivyo naamini mmenielewa japo kidogo, na asiyeelewa basi akaombe msaada pale TAASISI YA KUKUZA KISWAHILI CHUO KIKUU (TUKI)

Wednesday, February 24, 2010

TANZANIA INA NINI CHA KUJIVUNIA?

Je tumekosa viongozi wenye ubunifu?


Au tumekosa ardhi nzuri yenye rutuba na rasilimali?


Hii nimeidesa kutoka katika mtandao wa jamii Forum, imeandikwa na Mdau mmoja anayejulikana kwa jina la Dalali.
Kutokana na kuvutiwa nayo, nimeona sio vibaya wasomaji wa Blog hii ya Vukani nao wakiweka changamoto zao hapa, kwani huenda kuna jambo tukajifunza wote.

Wana JF,

Wiki iliyopita nilipata mtihani mgumu baada ya mgeni wangu ambaye namuheshimu sana alipoamua kunitupia suala ambalo sikulitarajia. Sijui yalimjia mawazo gani lakini wakati tunakaribia kuagana ghafla aliniuliza kwa kizungu "Are you proud of your country?"

Nilishusha pumzi na kupepesapepesa macho nikijaribu kutafuta jibu la haraka nikashindwa.
Kwa vile ni mtu ninayemuhesimu sana, sikuweza kumtoa njiani au kumdanganya.
Nilijaribu kuwaza mambo ambayo naweza kuyaita yakujivunia nikashindwa.
Kila kilichokuwa kikija mawazoni mwangu kilikuwa si cha kujivunia bali cha kutia uchungu.
Mambo yaliyonijia haraka yalikuwa kama:-
rushwa iliyopindukia mipaka, - viongozi mafisadi, wezi waliojaa kila sekta na taasisi za serikali ambao hujitajirisha kwa kila nafasi anayoipata mtu,

- miaka karibu 50 ya uhuru hatuna hata umeme wa uhakika,
- watoto wanakaa chini mashuleni na hakuna kinachosomeshwa,
- mahospitali hayana madawa,
- barabara yo yote inayojengwa au kufanyiwa ukarabati basi ni kwa pesa ya msaada,

- tumeshindwa hata kujilisha licha ya kuwa na ardhi ya kutosha ambayo kama ikitumiwa kitaalamu tunaweza kulisha eneo kubwa la Afrika

- hata kuvua samaki tukala sisi wenyewe na kusafirisha tumeshindwa licha ya kua na eneo kubwa la bahari,

- hao tunaoambiwa ni wataalamu wetu hawana hata kitu kimoja walichovumbua,

- tumefanya mageuzi ya kutokana na udikteta wa chama kimoja tumeshidwa.Demokrasia imeshindwa kupiga hatua.Vyombo vyote vya dola vinafanya kazi na kutumikia chama tawala na hata uchaguzi ukifanyika ni mizengwe mitupu,
- hata kwenye mambo ya michezo ni aibu tupu. Tunashindwa hata kuingia kwenye mashindano ya kombe la Afrika.Mwisho ilibidi nimeze mate machungu nimjibu,
"NO, I'm ashamed".
Dalali

Friday, February 19, 2010

LEO TUJIFUNZE NAMNA YA KUOMBA MAJI KWA LUGHA ZA MAKABILA TOFAUTI TOFAUTI

Kina mama wakitoka kuteka maji kisimani

Ndugu wasomaji wa kibaraza hiki, leo nataka tujifunze namna ya kuomba maji kupitia lugha za makabila tofauti tofauti.

Hivi karibuni nilikwenda Wilayani Babati, kule nikakutana na watu wa kabila moja liitwalo Wasandawi, nilikuwa na kiu, lakini nilipata tabu sana kuomba maji maana lugha pekee ambayo nilitakiwa kuwasiliana nao ilikuwa ni Kisandawi, basi ilikuwa kaazi kweli kweli.

Kipare:
Nighenja mazi ya kunwa=Nisaidie maji ya kunywa

Kinyawezi:
Nalilomba minze kakunwa=Naomba maji ya kunywa

Kichaga:
Ngikundi Mringa= Naomba maji ya kunywa

Kingoni:
Nitangatilai manji mlongo wangu=Naomba maji ya kunywa ndugu yangu

Kimasai:
Njaaghe Ngare= Naomba maji ya kunywa

Kihehe:
Ndisuka Ululenga= Naomba maji ya kunywa

Kimeru:
Ngitelewa Mringa= Naomba maji ya kunywa

Kijaluo:
Miaa pi= Naomba maji ya kunywa

NIMEPATA MSAADA KWA MJUVI WA LUGHA YA KIJAPANI
Kijapani:
Kwanza inabidi useme:- 1. kao nodo itai - nina kiu

2. mizu nomu itai - nina hamu ya kunwya maji

Ukisha sema moja kati ya hayo hapo juu ndio unaunganisha na lingine kati ya haya hapa:-

1. omizu kudasai

2. omizu chodai

3. omizu onegai shmasu

Kihaya:
Ninshaba amaizi= Naomba maji ya kunywa

Haya wengine mtajazia hapo.

Wednesday, February 17, 2010

KAMPENI YA ZINDUKA MALARIA HAIKUBALIKI: MHESHIMIWA RAISI ALITAKIWA KUIDHINISHA MATUMIZI YA DAWA YA DDT

Mheshimiwa Rais akizuindua kampeni za Zinduka malaria haikubaliki pale viwanja vya Leaders club

Niliwahi kuandika wakati fulani juu ya janga la malaria linavyowamaliza Watanzania, katika makala hiyo niliyoipa kichwa cha habari kisemacho ‘shiranga la ugonjwa wa malaria: bora tufe kuliko kuathiri mazingira!’ nilieleza mengi juu ya kukwama kwa makusudi dhamira ya kuutokomeza ugonjwa huo, kama ungependa kujikumbuasha bofya hapa.

Hivi karibuni katika kampeni ya Zinduka Maleria haikubaliki iliyozinduliwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alizungumzia jinsi malaria inavyowamaliza watanzania, wimbo ule ule ambao umekuwa ukiimbwa na wanasiasa kila uchao.

Naamini kila mtu anajua kuwa Malaria inaua wananchi wengi sana hapa nchini kuliko hata ugonjwa wa Ukimwi, lakini cha kushangaza mpaka leo hii hakuna hatua madhubuti ambayo imechukuliwa katika kuutokomeza ugonjwa huo.

Awali nilijua kuwa Raisi angetumia kampeni hizo kuidhinisha matumizi ya DDT, dawa ambayo imefaninkiwea kwa kiasi kikubwa kutokomeza ungonjwa wa malaria katika nchi ambazo zinatumia dawa hizo hususana Zanzibar.

Nilishangazwa na kauli ya Rais pale aliposema, naomba ninukuu, "Kila siku ya Mungu, hapa nchini, wanakufa watu hadi 291 kwa ugonjwa wa malaria. Kwa maneno mengine, kila saa inayopita, wanakufa watu zaidi ya 10 kwa ugonjwa wa malaria. Hawa ni watu wengi mno. Hivyo, malaria ni Janga la Taifa letu. Lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba malaria ni ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika. Ndiyo maana tumeamua kuwa wakati tunaendelea kushughulikia kutibu wagonjwa wa malaria, tuelekeze nguvu zetu katika kuzuia kwa kuanza juhudi za kutokomeza malaria nchini." Mwisho wa kunukuu,

Pia alibainisha njia kuu tatu za kupambana na kuushinda ugonjwa wa malaria, akisema kuwa njia ya kwanza ni kutumia dawa zenye nguvu na uwezo wa kutosha kuwatibia wale watakaokuwa wamepatwa na ugonjwa wa malaria.


Njia ya pili, alisema, ni kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuua mbu na akaelezea jitihada za Serikali yake juu ya kupatikana kwa vyandarua vya namna hiyo. Alisema kuwa mpaka sasa watoto wenye umri wa miaka mitano na kina mama waja wazito wanapewa vyandarua vya namna hiyo bure, lakini mipango inakamilika kuiwezesha kila kaya nchini kuwa na angalau vyandarua viwili vya namna hiyo.

Akasema kuwa njia ya tatu ni kuhakikisha kuwa mbu wanaobeba malaria hawazaliani na wanatokomezwa kabisa.
Kwa maneno yake mwenyeweRais Kikwete alisema, "Ni lazima tuhakikishe tunawamaliza mbu wanaoleta malaria kwenye mazalia yao. Tunaweza kabisa kuhahakisha kuwa sisi tunakuwa kizazi cha mwisho kufa kwa malaria. Nchi nyingine duniani zimeweza na naamini hata sisi tutaweza. Ndugu zetu wa Zanzibar wameweza na sisi wa Tanzania Bara tunaweza pia."

Mimi nilitarajia kuwa huo ndio ulikuwa ni wakati muafaka wa yeye kutangaza rasmi matumizi ya dawa ya kuulia wadudu ya DDT, ambayo ndiyo inayotumiaka Zanzibar pia katika kuutokomeza ugonjwa huo.

Huwezi kuyataja mafanikio yaliyofikiwa na Wazanzibari katika kuutokomeza ugonjwa wa Malari bila kuitaja dawa ya DDT.

Binafsi naona kampeni hiyo ilikuwa na sura ya kisiasa zaidi kuliko kile ambacho kilitarajiwa na wananchi wengi, kwani hakuna jipya, hizo njia kuu tatu alizozitaja mheshimiwa raisi zimekuwa zikitajwa kila siku na wanasiasa na wataalamu wetu wa afya lakini hazijazaa matunda mpala leo na watu wanaendelea kuteketea.

Cha Kushangaza Kiwanda cha A to Z cha hapa Arusha ambacho ndio mtengenezaji mkuu wa vyandarua ni miongoni mwa wadhamini wakuu waliodhamini uzinduzi wa kampeni hiyo ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria, hii haiingii akilini, kwamba mtu anayetengeneza pato lake kwa kutegemea ugonjwa wa malaria akubali eti malaria iishe hapa nchini, kama sio siasa ni kitu gani, basi atakuwa ni mwenda wazimu.

Mimi naamini kuwa mheshimiwa Raisi anayo dhamira hasa ya kuutokomeza ugonjwa huu wa malaria, lakini wataalamu wetu wameshindwa kumshauri raisi wetu kufanikisha dhamira yake hiyo.

Bado nasisitiza kuwa kamwe hatuwezi kuutokomeza ugonjwa wa malaria kama hatutaruhusu matumizi ya dawa ya kuulia wadudu ya DDT.

Sunday, February 14, 2010

MSIONE KIMYA JAMANI NIKO HUKU ARUSHA..........

Katika pitapita zangu katika mji wa Arusha nikajikuta niko humu, jamani kublog Raha kweli

Jamani msione kimya niko huku Arusha nakula Valentine Day, niliondoka huko Dar, leo alfajiri na namshukuru mungu nimefika salama. Nitakaa huku kwa majuma kadhaa nikishughulika na masuala ya kifamilia, huenda nikaadimika mtandaoni, lakini nikipata muda nitatembelea Vibanda vya mtandao kuperuzi na kupata habari mbalimbali kupitia vibaraza vyenu na kama nitapata fursa nitaendeleza libeneka kama kawaida.


Basi mwenzanu nilijua huku hali ya hewa ni Baridi nikabeba nguo nzito, Duh, kuna joto bala kama Dar, hivi kesho lazima niamkie madukani kufanya manunuzi ya nguo za joto kabla ya kueleka Karatu kuchapa kazi, maana huku niko kwenye kampeni ya KILIMO KWANZA.

Sunday, February 7, 2010

WAALIMU WETU NA MAJINA YA KEJELI

Mwalimu akifundisha

Katika kusoma kwangu nimebahatika kusoma katika shule mbalimbali zikiwamo za hapa Jijini Dar na za mikoani.

Kusema kweli maisha ya shule ni kumbukumbu pekee ambayo kila mtu ambaye amebahatika kufuta ujinga anaweza kubaki nayo. Naam ni kipindi ambacho unakutana na watu kutoka katika mikoa mbalimbali na wenye tamaduni tofauti tofauti.

Nimegundua kuwa sekta ya ualimu ndiyo inayoongioza kwa waalimu kupewa majina ya utani na wanafunzi, na majina hayo yanaweza kuwa ni kutokana na tabia ya mwalimu, aina ya mavazi anayopenda kuvaa, kauli zake za mara kwa mara, matamshi na hata vituko anavyofanya, maana unaweza kukuta mwalimu ana vituko kama The Comedy.

Jana tulikuwa tunakumbushana mambo mbalimbali yaliyopita na dada zangu ambao walikuja kututembelea hapa nyumbani, na miogoni mwa kumbukumbu likajitokeza hilo la majina ya utani waliyokuwa wakiwapa waalimu wao.

Ilikuwa ni kumbukumbu nzuri ambazo ziliifanya siku yangu ya jana niione nzuri ajabu. Nami nimeona niwashirikishe wasomaji wa kibaraza hiki juu ya kumbukumbu hizi. Hata hivyo naamini kuwa miongoni mwa wasomaji wa kibaraza hiki wapo waalimu ambao nao huenda walikuwa au ni miongoni mwa watu ambao walikutana na kisirani hiki cha kupewa majina ya utani na wanafunzi.

Naamini sio vibaya kama nao wataweka changamoto zao walizowahi kukutana nazo au wanazokutana nazo katika taaluma zao hizo.

Binafsi nakumbuka kuna mwalimu tulikuwa tunamwita darubini, huyu alikuwa ana macho makali, kwa mfano unaweza kuwa kwenye chimbo (Chimbo ni eneo la kujificha) na kama akipita eneo hilo ukawahi kukimbia, utashangaa siku ya pili mkiwa kwenye gwaride akikuita kwa jina kuwa upite mbele, na hapo ni lazima upate bakora.

Kingine ni pale ambao umejificha mahali, halafu ukawa unachungulia kwenye kona ya ukuta, akiona jicho tu utashangaa akikuita kwa jina na hapo pia utachezea bakora, alikuwa na kipaji cha kukariri majina na sura za wanafunzi wake, huyu alikuwa ni mwalimu wa nidhamu na mara nyingi waalimu wa nidhamu ndio wanaokutana na adha hii ya kupewa majina ya ajabu.

Mwalimu mwingine tulikuwa tunamuita Pindipo. Huyu alipenda sana kutumia neno la ‘Pindipo utakapobainika’ pale ambapo anatahadharisha juu ya jambo fulani. Kama kawaida wanafunzi wakampachika jina la Pindipo.

Mwalimu mwingine ninayemkumbuka tulikuwa tunamwita ‘Kala nini’ huyu naye kama umefanya makosa na amekasirika sana, alikuwa akipenda kusema ‘binti reo utaniereza nimekura nini usiku wa jana’ huyu alikuwa anatokea kule kwa akina Chacha Wambura. Na ndipo wanafunzi wakamwita Mwalimu Kala nini.

Huko Sekondari napo nikakutana na vituko hivyo, kuna mwalimu wetu wa Biology tulikuwa tunamwita mwalimu Mandible, Mandible ni zile antenna za Panzi, sasa yeye alikuwa akipenda kulitamka hilo neno mpaka tukamwita hilo jina la mwalimu Mandible.

Mwalimu mwingine alikuwa ni mwalimu wa Kiswahili huyu tulimwita jina la Ngoswe, kama mnakumbuka kile kitabu cha Ngoswe, Penzi kitovu cha uzembe.

Mwalimu mwingine alikuwa akiitwa ‘However,’ huyu, hawezi kusema maneno matatu ya kiingereza bila kutamka hili neno la However, na hapo wanafunzi wakampa jina la However.

Kwa kweli ni majina mengi mno na kama nikisema niyataje hapa, basi nitawachosha, ngoja niwaachie na wasomaji wengine watoe kumbukumbu zao.

Wednesday, February 3, 2010

KWA NINI IWE NI WANAUME TU WANAONUNUA MKUYATI?

Jamaa akinunua Mkuyati

Kuna wakati wanaume wanaweza kuwa na ugumu wa kujua kwamba wake au wapenzi wao hawaridhiki kimapenzi. Hiyo inatokana na uwelewa mdogo waliokuwa nao wanaume juu ya tofauti kubwa iliyopo kati ya wanawake na wanaume kuhusiana swala zima la hisia za kimapenzi.

Wanawake wana matarajio makubwa sana katika kila eneo linalohusu maisha yao, lakini linapokuja swala la tendo la ndoa mambo ni tofauti sana. Kwa kawaida wanawake wengi ambao hawaridhishwi na tendo la ndoa kwenye uhusiano wao huwa wanafanya siri.

Bila kujali kama tatizo liko kwao au kwa waume zao, wanawake hufanya siri kutoridhika kwao kimapenzi, na huweka siri kwa waume zao na hata kwa madaktari. Na ndio maana sishangai kuona kwamba wateja wa wauza dawa zinazohusiana na kuongeza hamu ya tendo la ndoa yaani Mkuyati ni wanaume.

Nilipokuwa nyumbani Tanzania, jijini Dar Es Salaamu nilishangaa sana kuona katika magazeti maarufu ya Udaku, {Tabloids} matangazo mengi ya biashara yanayotawala katika magazeti hayo ni ya kuuza dawa za kuongeza nguvu za kiume au hamu ya tendo la ndoa kwa wanaume na nyingine zilikuwa ni za kuongeza ukubwa wa maumbile ya kiume, dawa kama Mkuyati, Mzakaru, Super Shaft, Kifaru, Sekwa na nyingine chungu nzima ni maarufu sana jijini Dar Es Salaam.

Sio kwamba wanawake hawana matatizo ya tendo la ndoa, la hasha. Wanawake wanayo matatizo hayo ya tendo la ndoa lakini kwao hiyo siyo agenda, yaani si kitu cha kuwaumiza sana kichwa. Lakini kwa wanaume ni tofauti sana, wanapokuwa na tatizo la kukosa ufanisi katika tendo la ndoa huo utakuwa ni mgogoro mkubwa sana, kwani kwao hili ni jambo linalopewa kipaumbele kuliko mambo yote.Kwa wanaume kukimbilia hospitalini au kwa mganga wa jadi na kusema “nina tatizo kubwa” ni jambo la kawaida kabisa….

Lakini wanawake hawafanyi hivyo, Badala ya kulifanya tatizo hili ni mgogoro halisi, huwekwa chini kabisa kwenye orodha ya matatizo yao, huwekwa kiporo na litashughulikiwa kwa wakati atakapojisikia kufanya hivyo kwa wakati wake.Wanawake wanaweza kwenda kuomba ushauri au kuwasimulia mashoga zao, kuhusu matatizo ya ndoa.

Lakini ni hadi wachokozwe ndipo wanapoweza kusema kwamba maisha yao ya tendo la ndoa na waume zao hayako sawasawa. Hilo halipewi uzito wa juu au naweza pia kusema hufanywa siri.Wanawake hawaridhishwi na tendo la ndoa kwa sababu mbali mbali. Lakini bila kujali sababu hizo, kwao ni vigumu sana kusema kuhusu kutoridhishwa kwao.

Ukiona mwanamke anatangaza sana kuhusu kutoridhishwa kwake na tendo la ndoa, basi ujue huyo na mumewe wako kwenye uhusiano mbaya sana. Kwani atakuwa anatumia maelezo ya kutoridhika kwake kama adhabu ya kumkomoa mumewe kwa kumuaibisha.

Lakini wale walioko kwenye ndoa imara ni vigumu kuwasikia wakilalamika kwamba hawaridhiki na tendo la ndoa. Inawezekana kutoridhika kwake kunatokana na yeye mwenyewe, yaani labda hana hamu au hafiki kileleni kutokana na matatizo mbali mbali yakiwemo ya kisaikolojia au matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango, lakini bado sehemu kubwa wanaume huchangia. Hata hivyo pamoja na sababu hizo, mwanamke hayuko tayari kusema kuhusu kutoridhika kwake.

Kushindwa huko kunatokana na jinsi jamii ilivyomfunga mwanamke, kutoonesha kuhitaji tendo la ndoa. Akionesha kutoridhika na tendo la ndoa huonekana ni Malaya, kwa hiyo hukaa kimya na kuonesha kutojali. Lakini bila shaka nadhani umefika muda wa wanawake kuwa huru kuhusu tendo la ndoa na kusema hisia zao wazi wazi bila kuogopa jamii itawaonaje, kwani jamii imekandamiza haki yao ya kuzungumzia tendo la ndoa kwa muda mrefu sasa.

Wanaume nao wanapaswa kujua kwamba wanawake hawapendi au hawawezi kuzungumzia kutoridhishwa kwao na tendo la ndoa, hivyo kutosema kwao kusitafsiriwe kuwa ndio wanawaridhisha, ni vyema kutoa ushirikiano kwa wake au wapenzi wao na kutafuta kujua kama wanawaridhisha.

Ni jambo la busara kama mwanaume atadadisi kwa upendo na lugha ya upendo na kuonesha kama yuko tayari kutoa ushirikiano pale ambapo mke au mpenzi ataonesha kutoridhishwa na tendo la ndoa.

Mada hii nimeichukua kutoka kwenye kibaraza cha MAISHA, cha dada Yasinta, nami nimevutiwa nayo nikaona sio vibaya kuirejea ili kujikumbusha.