Thursday, December 31, 2009

NIMETAFAKARI MAONI YENU, VUKANI KUENDELEA KUWA MTANDAONI.

Kazi na Dawa

Ni jambo la kujivunia, kung’amua kuwa kumbe blog ya Vukani iko juu na inapendwa. Kusema kweli sikuwahi kufahamu kuwa blog ya vukani inapendwa kiasi hiki na hilo limenifanya nifikirie upya uamuzi wangu.

Ulikuwa ni uamuzi mgumu sana, lakini nimeona ni vyema niheshimu maoni ya wasomaji wa blog hii na wanablog wenzangu na hivyo nitaendelelea kublog kama kawaida. Tarajieni mabadiliko makubwa katika blog hii kwani mwaka mpya na mambo mapya…au sio?

Natoa shukrani kwa wasomaji wote, mliotumia muda wenu kutoa maoni na wengine kuniandikia email binafsi, nawahakikishieni kuwa blog ya Vukani itaendelea kuwepo kama kawaida.

Sina mengi kwa leo ngoja nijiandae kwa ujio wa mwaka mpya wa 2010.

Ahsanteni sana.

Friday, December 25, 2009

BAADA YA KUTIMIZA MWAKA MMOJA LEO TANGU KUANZISHWA KWAKE BLOG YA VUKANI KUFUNGWA RASMI LEO

Kwa herini ya kuonana

Leo tarehe 25 December 2009 Blog hii ya VUKANI Inatimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake. Ni jambo la kujivunia kwamba ndani ya mwaka mmoja nimeweza kuweka makala 100 na nimemudu kuendelea kublog hata pamoja na majukumu mbalimbli ya kifamilia niliyokuwa nayo. Nilikuwa nikisafiri mara kwa mara lakini hata hivyo niliweza kuweke post kama kawaida ili wasomaji wa blog hii waendelee kusoma ujinga wangu.

Najua tangu nianze kublog kuna watu niliwakwaza na wengine niliwafurahisha na hata kuwafikirisha, lakini halikuwa lengo langu kumuumiza mtu kihisia kwa namna yoyote ile kwani lengo la blog hii ni kuelimisha, kufikirisha, na kufurahisha. Naamini malengo ya uwepo wa blog hii yalitimia kwa kiasi fulani.

Kama nilivyosema kuwa blog hii itakuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo, naamini yote hayo yalitimia na ndio maana leo natimiza mwaka mmoja nikijivunia kile nilichokifanya hadi leo.
Najua si rahisi kufanya tathmini na kujua kama ni wasomaji au wanablog wangapi ambao kwa njia moja ama nyingine wamejifunza au wamenufaika na huu ujinga wangu, ninaouweka humu lakini naamini kwa kiasi fulani kuna wengi wamejifunza na kunufaika na uwepo wa blog hii.

Kama kumbukumbu zenu haziko mbali, kwa wale wafuatiliaji wa blog hii watakumbuka kuwa, blog hii ilianza na misukosuko mingi, kwani karibu mara mbili nilipata shinikizo la wazazi wangu kuifunga na kuachana na mambo ya kublog, baada ya kuibua hoja ya kuhoji swala zima la nadharia ya hizi dini zetu za mapokeo, kama unataka kujikumbusha bofya hapa
NIMEANZA KUZISHITUKIA HIZI DINI. Mada hiyo iliwashitua sana wazazi wangu, ambapo walinitaka niache kublog kama sina mambo ya maana ya kuandika, swala la kuhoji uhalali wa dini likaonekana halina maana.

Nililazimika kuufunga ule mjadala ili kunusuru mahusiano yangu na wazazi wangu. Mara ya pili ni pale nilipopingana na wazazi wangu juu ya swala la kuendelea na elimu, baada ya kuacha chuo na kujikita kwenye biashara zaidi, hiyo nayo ilikuwa ni changamoto nyingine, lakini kutokana na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa blog hii nilimudu kuyamaliza na hivyo kuendelea kublog kama kawaida.

Naomba nikiri kwamba uwepo wa blog hii ni kutokana na kuvutiwa na blog ya MAISHA ya dada Yasinta Ngonyani, kwani ni yeye aliyenifanya nami nianze kublog na kwa msaada wa mdogo wangu Jerome kwa utundu wake aliweza kuifungua blog hii.

Pia siwezi kuepuka kumtaja kaka Markus Honorius Mpangala aka MCHARUKO kwani na yeye kwa upande wake alichangia kuifanya blog hii ionekane kama ilivyo leo. Pia siwezi kuepuka kumtaja kaka yangu mpendwa Mubelwa Bandio kwa kuwa karibu nami akinishauri hili na lile juu ya namna nzuri ya kublog, na pia amekuwa ni mhariri wangu mahiri akinisaidia kurekebisha lugha na namna nzuri ya kujenga hoja katika makala zangu.

Salaam kwako dada yangu Yasinta ngonyani, wewe ni dada yangu mpendwa, siwezi kuwataja dada zangu Debora Damari, na Rachel bila kukutaja wewe dada yangu mpendwa. Dada kwa kweli upendo wako ni wa ajabu kwangu umekuwa karibu nami na nimekuwa nikikufanyia masihara mengi na utani mwingi licha ya kwamba umenizidi sana umri. Umekuwa ni mshauri mwema kwangu juu ya mambo mengi yahusuyo maisha. Umechangia kwa kiasi kikubwa katika kunibadili kitabia kutokana na hekima zako, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa wema wako.

Kwako dada Subi, nawe kwa upande wako ninayo mengi ya kujivunia, umenifunza mengi na umenifanya nikue kifikra, wewe umekuwa mmoja kati ya dada zangu na nimekuwa nikijivunia sana kukufahamu, pokea salaam zangu.

Kaka yangu Mbwange Simon Mkodo Kitururu, Duh! Sina la kusema, kupitia blog yako na maoni yako nimejifunza mengi. Kwani kupitia blog yako ya Mawazoni nimejifunzza kuwa hakuna lugha ya matusi, bali kuna majina yanayowakilisha viungo vya mwili, miti, wanyama na vitendo, lakini kutokana na tafsiri tulizofundishwa tumekuwa tukiamini kuwa baadhi ya majina ya viungo vya mwili, wanyama miti na baadhi ya vitendo ni matusi.

Pia siwezi kumsahau kaka yangu wa kulikoni Ughaibuni Evarist Chahali, wewe ulikuwa ni msomaji mmojawapo uliyeweka changamoto zako humu na kuibua mijadala mikubwa na hata kuleta mgongano wa mawazo, najua ni siku nyingi hatujawasiliana lakini naamini unaikumbuka VUKANI.

Kaka yangu Profesa Matondo, sijui niseme nini, lakini wewe mwenyewe unajua ni kiasi gani umenisaidia kukua kifikra, ni jambo la kujivunia kuwa pamoja na Elimu yako na shughuli zako nyingi uliweza kurudi chini na kuweza kuzungumza nami kama vile kaka azungumzaye na mdogo wake tumbo moja. Umekuwa mshauri wangu katika masuala mbalimbali ya kielimu na kijamii, heshima kwako Profesa Matondo.

Kwako kaka Shabani Kaluse, aka baba Abraham, Mzee wa Utambuzi, naomba nikiri wazi kuwa kupitia kibaraza chako nimejifunza mambo mengi juu ya utambuzi na nimebadilika sana kitabia, umekuwa ukijibu email zangu binafsi na kunishauri mambo mengi sana juu ya maisha na mafanikio. Umekuwa mhariri wangu mzuri pale ninapotaka kuweka makala za kijamii umekuwa ukinishauri namna nzuri ya kujenga hoja. Nakushukuru sana kaka kwa wema wako.

Dada Schola Mbipa, heshima kwako dada, nakushukuru kwa ushauri mbalimbali uliokuwa ukinipa ili kuiboresha blog hii.

Uuuuwiiii!!!!! Jamani nusura nimsahau Kamala Lutatinisibwa, huyu naye kwa kweli amenifundisha mambo mengi sana juu ya Utambuzi, maoni yake yamekuwa yakileta changamoto katika blog zetu hizi na kuibua mijadala ya hapa na pale, huyu ni mdau mmojawapo ambaye amenifanya nisifikirie kuacha kublog.
Ngoja niwanong’oneze siri, kusema kweli kama nikiweka makala katika kibaraza hiki halafu Kamala asiweke maoni nahisi kama mada yangu haijakamilika….LOL, kwani ni mdau mmojawapo ambaye lazima akiweka maoni utapenda kuyarudia kuyasoma mara kadhaa, sio kwa kutokuelewa bali kwa kutafakari zaidi, maoni yake mara nyingi yanafikirisha.


Najua ni wengi, wengi sana waliojitokeza katika blog hii na kuweka maoni yao au kunitumia email binafsi wakinishauri hili na lile ili kuiboresha blog hii, pia wapo waliotaka mawasiliano nami ya karibu lakini kutokana na kutingwa nimeshindwa kutekeleza hilo, lakini naomba muamini kuwa tupo pamoja.

Kwa uchache niwataje hawa wafuatao ambao kwa njia moja ama nyingine wamekuwa ni chachu ya kufanikisha uwepo wa blog hii, kaka Damas Michael, Godwin Meghji, kaka Kisima, kaka Manento Kitururu, kaka James Jim, kaka Chib, Dada My Little World, kaka John Mwaipopo, kaka Edo Ndaki, Mummy Hery, Da' Mija na wengine wengi. Niliowasahau mtanisamehe jamani nafasi ni ndogo……LOL.

Sasa naomba mniruhusu kuifunga rasmi blog hii ili niweze kufanya mambo mengine ambayo naamini yatakuwa bora zaidi ya kublog.

Ahsanteni na kwaherini wote, tutawasiliana mungu akipenda.

Ahsanteni sana kwa ushirikiano wenu katika kipindi chote nilipokuwa nikiblog.
Nawapenda wote jamani, Mungu awe nanyi milele daima…..aaaaamen

Sunday, December 20, 2009

HIVI HUYU KIJANA NI NANI?

Picha kwa hisani yake mwenyewe
Ni kijana mdogo kwa umri lakini ni mkubwa kwa umbo.
Kijana huyu ni suriama aliyechanganya kati ya makabila mawili ya Mpare kutoka milima ya upareni na Mjita kutoka kule Musoma kusikoisha vita kati ya koo za Wanchori na Wanchoka.

Alifanikiwa kupata elimu yake kupitia shule kadhaa hapa nchini kabla hajakuwa mjanja na kutowekea Ughaibuni miaka kadhaa iliyopita, akiishi katika mojawapo ya nchi za Scandinavia.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa, wakati akiwa shuleni alikuwa na kipaji maalum cha sanaa na alikuwa ni bingwa wa kucheza na misamiati na nahau. Watu waliowahi kusoma naye wanakiri kuwa alikuwa na tatizo la kutomudu kutumia Tafsida pale alipotakiwa kutoa mada fulani katika midahalo ya shule.

Tatizo hilo lilikuwa likimletea matatizo na waalimu wake kwa kuwa alionekana kama vile hana adabu japokuwa ujumbe alioutoa ulikuwa na maana sana katika jamii na wenye kufundisha na kufikirisha pia. Hata hivyo wapo waliomuelewa na wengi walijifunza mengi kupitia hoja zake hizo zilizojaa vioja. Msome kwa kubofya hapa.

Pamoja na misukosuko aliyoipata kutoka kwa waalimu wake hakukata tamaa aliendeleza kipaji chake na baada ya kutowekea ughaibuni amekuwa muelimishaji mzuri kupitia kibaraza chake alichokipachika jina la Mawazoni.

Katika kibaraza hicho amekuwa akifikisha ujumbe wake wa kuielimisha jamii kwa kutumia misamiati nahau na tilalila zake anazozijua mwenyewe na kutokana na kutotumia Tafsida wengi wamekuwa hawamwelewi kwa kuwa wakisoma kichwa cha habari tu wanachoka na wanaacha, maana tafsiri inayokwenda akilini mwao ni kitu kingine badala ya kile kilichokusudiwa.

Tatizo ninaloliona katika makala zake si lugha iliyotumika bali ni tafsiri inayokwenda vichwani mwa wasomaji kwa kukimbilia kuhukumu kichwa cha habari badala ya kile kilichomo ndani ya hicho kichwa cha habari. Kwa mfano halisi unaweza kubofya hapa au hapa.

Ni mchangiaji mzuri sana katika vibaraza vya wengine na kwa kutumia staili hiyo hiyo ya Ant tafsida, amekuwa akiwachanganya wasomaji wengi na naomba nikiri kuwa hata mimi nilikuwa ni mmoja wapo wa wale waliokuwa hawamwelewi kabisa.

Ilinichukua muda kidogo kumwelewa na kwa kutumia kamusi ya Kiswahili na vitabu mbalimbali vya Kiswahili, kikiwamo kitabu kinachoitwa Titi la Mkwe na cha Jando na Unyago, nilimudu kumuelewa kijana huyu na makala zake zilizojaa nahau na upembuzi yakinifu.

Naamini hanifahamu na mimi pia simfahamu ila kwa kupitia vibarazani mwetu tumetokea kufahamiana japo si kwa karibu sana. Pamoja na hayo bado najiuliza hivi huyu kijana ni nani?

Wednesday, December 16, 2009

BARUA YA SIRI NA USHAURI WA BURE KWA DADA SUBI

Dada Subi

Kwako dada Subi, ni matumani yangu kuwa umzima wa Afya na unaendelea na kazi zako za kila siku huko uliko. Utakapo kujua hali zetu huku nyumbani, wote hatujambo, Isipokuwa yule babu yako anayeishi kule bondeni karibu na ule muembe mkuubwa uliokuwa ukitumika kama maegesho ya baiskeli za kukodisha, anasumbuliwa sana na ile henia yake na anahitaji operesheni ya haraka. Dada unajua siku hizi sio baiskeli tena zinazoegeshwa kwenye ule muembe bali ni pikipiki maarufu kama Yeboyebo ndio zinaegeshwa na watu wanazikodisha kwa ajili ya kupelekwa wanakokwenda kwa gharama nafuu.

Lakini dada usafiri huo sio salama sana kwani kina mama na mabinti hubakwa na waendsha pikipiki wakware lakini, kesi hizi zimekuwa haziripotiwi Polisi kutokana na wanaofanyiwa vitendo hivyo kuona haya, unajua dada mtu kuwaambia Polisi wetu kuwa umebakwa ni kashfa na aibu kwani unaweza kujikuta ukizomewa mtaani baada ya polisi kuvujisha siri kuwa umeonjwa bila ridhaa yako.

Dada naona tuachane na hayo ya kubakwa, nikweleze madhumuni ya barua hii. Dada siku za hivi karibuni tumeanza kupata wageni hapa kijijini, wageni wenyewe ni wale waliokuja kijijini kwetu kwa unyenyekevu miaka mitano iliyopita wakitaka tuwape Kula ili wapate ridhaa ya kingia katika lile jumba kubwa kule Dodoma kwa ajili ya kusinzia na kujipatia posho mara mbili. Watu hao ambao wakati ule walikuja wakiwa slimu na sasa wana matumbo makubwa na mabodi gadi wa kuwalinda wamekuja na mikoba myeusi iliyosheheni vijisenti kwa ajili ya kutughilibu tena ili tuwape ridhaa nyingine ya kuendelea kula nchi ndani ya jumba kubwa kule Dodoma wakipigwa na viyoyozi.

Dada Subi kama unavyojua kuwa siku hizi mambo yemebadilika na sio kama wakati ule, wananchi wameerevuka na wanajua haki zao. Si unakumbuka jinsi viongozi wetu walivyokuwa wakipata wakati mgumu katika ziara zao kwa kupokelewa na mabango yenye ujumbe, wakati mwingine wa kejeli, na wengine kufikia kuzomewa majukwaani na wananchi tena wa kijijini ambapo awali viongozi wetu walidai kuwa watu wa vijijini ni watu wa “ndio mzee”, lakini sasa hivi wamewageuka na kuwazodoa hadharani baada ya kuchoshwa na longolongo zao.

Lakini wakazi wa Mbeya ndio walitia fora kwani wao walithubutu kupopoa mawe msafara wa mwenye nchi, ingawa hata hivyo walionja joto ya Dola, naamini unakumbuka kilichowapata masikini wale. Dada kuerevuka huko kwa wananchi kumetokana na kuangalia Luninga, si unajua Luninga ndio mwalimu mzuri wa kuelimisha jamii siku hizi. Nakumbuka matukio hayo tulizoea kuyasikia kwa majirani zetu tena kupitia redioni hasa idhaa ya Kiswahili ya BBC wakati ule wa Mwalimu, lakini siku hizi tunaona kupitia kwenye luninga zetu kila uchao, kwanini tusiige.

Kutokana na ugeni huo yule mzee Makalioni ambaye ndiye mwenyekiti wa wazee pale kijijini aliitisha kikao cha dharura ili kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuchaguliwa kwa huyo mwakilishi wetu huko mjengoni (kama yapo) ili kujua kama kuna haja ya kumpa ridhaa zetu tena.

Kwa kifupi kikao kilithibitisha kuwa kati ya yale yote yaliyoahidiwa na mwakilishi huyo kuwa atawafanyia, yaani kujenga mahosipitali kila mtaa, kujenga majosho ya ng’ombe, si unajua sisi ni wafugaji japo hatuko kama wamasai wanaohamahama, basi huyu mwakilishi aliahidi kujenga majosho ya ngombe kila kaya, kujenga barabara na vituo vya polisi kwa ajili ya usalama wetu. Pia aliahidi kutuletea wawekezaji watakaojenga viwanda na kuleta ajira kwa vijana pale kijijini ambao walikuwa wanategemea kupata kipato kwa kilimo cha jembe la mkono. Aliahidi kuleta Matrekta kwa kila mwanakijiji kama akipata ridhaa ya kuingia mjengoni.

Kikao kiligundua kuwa kati ya yote yaliyoahidiwa na mwakilishi huyo ni asilimia 0.006 tu ndiyo yaliyotekelezwa mengine yaliwekwa pending kwa ajili ya kuombea ridhaa nyingine ya kuingia mjengoni miaka mitano ijayo. Ili kutuhadaa mwakilishi huyo emekuja na Katapila na sasa linatimua mavumbi hapo kijijini kwa madai kuwa wanajenga barabara, lakini kwa bahati mbaya wanakijiji wameshitukia janja yake.

Dada katika kikao hicho wazee waliazimia kuwaita vijana wao walioko Ughaibuni ili warudi kugombea nafasi ya uwakilishi mjengoni na nafasi nyingine za uongozi hapa kijijini. Katika nafasi ya uwakilishi yalijitokeza majina matatu, jina la kwanza lilikuwa la kwako, la pili lilikuwa ni la yule mtoto wa katibu kata aliyekwenda Ughaibuni miaka kumi iliyopita na kupotelea huko na jina la tatu ni la yule kijana anayezaliwa na yule fundi maarufu wa baiskeli mwenye wake wawili…….yule anayeishi jirani na Mbuyu jirani na gulio la kijiji, inasemekana kijana wake alizamia meli mara baada ya kumaliza fom foo na kulowea huko. Baada ya wazee kuyatafakari majina yote matatu, jina lako lilionekana kung’aa, baada ya kupata kura nyingi za wazee ambao wamekubaliana kuwa uitwe ili uje kugombea nafasi hiyo ya uwakilishi wa mjengoni.

Sababu kubwa iliyowavutia ni tule tumisaada twa dawa za binadamu na madawa ya mifugo ulitotuleta wakati ule ulipokuja kuwaona. Unajua mara baada ya kumwaga madawa katika ile zahanati ya kijiji sifa zako zilivuma hadi vijiji vya jirani na hivyo ukapata umaarufu wa haraka kama ule wa Nyerere wakati ule wa kumpinga mkoloni.

Sifa nyingine iliyokufanya uwe maarufu hapa kijijini ni pale ulipotoa msaada wa dharura kwa kumzalisha yule binti wa mzee mkalimbembe ambaye alipata matatizo wakati wa kujifungua kwa mtoto wake kutanguliza mkono badala ya kichwa. Kwa Juhudi zako na kwa kushirikiana na wauguzi wa zahanati ya kijiji uliweza kumzalisha binti huyo.

Sifa hiyo imekujenga sana hapa kjijini na sasa wanataka uje ugombee uwakilishi mjengoni ili uwaletee maendeleo, wazee wanadai kwa kuwa umeishi ughaibuni, utakuwa huna tamaa za kifisadi na utakuwa umeridhika sana na maisha kutokana na kuishi na wazungu kwa miaka mingi sana.

Dada taarifa hizi ni za siri na nimekutumia kupitia njia za panya kwani yule mwakilishi akijua anaweza kukuhujumu usipate viza ya kuingia nchini. Kwa hiyo kwa taarifa hii inabidi ujiandae kwani utatumiwa ujumbe muda si mrefu.

Friday, December 11, 2009

KISA CHA BARUA YA WAZI KWA YASINTA.......

Barua yangu ya wazi kwa dada yangu wa hiyari, Yasinta Ngonyani iliwachanganya wasomaji wengi hadi wengine walinitumia email ya kutaka ufafanuzi kwamba kulikoni tena mambo ya binafsi kuwekwa kibarazani?

Nilijua hilo litatokea na kweli limetokea, nimepokea email kadhaa zikinitaka nifafanue kile nilichoandika.

Kwanza naomba nichukue nafasi hii kumshukukuru dada Yasinta kwa kuniruhusu kuweka ile barua ya wazi katika kibaraza hiki nikidai kuwa namuandikia yeye. Naomba niweke wazi kwamba ile barua ilikuwa haimuhusu yeye na wala hakuwahi kuniandikia barua yoyote. Ile barua haikuwa ni ya kweli na wala haihusiani na mimi, ila kuna rafiki yangu mmoja niliyewahi kusoma naye ambaye aliwahi kuolewa mara tu baada ya kumaliza kidato cha 4.

Nakumbuka kila tulipokutana alikuwa akiniuliza kama nitaolewa lini. Siku moja aliniambia maisha ya ndoa ni mazuri na asiyeolewa labda ana matatizo kwa kuwa anakosa tamu ya ndoa. Nilimsikiliza na kumpuuza kwa kuwa nafahamu kuwa maisha ya ndoa hayana formula, yaani yanaweza kuwa mazuri kwa huyu na yakawa mabaya kwa yule. Hivi karibuni nimepata taarifa kuwa ndoa yake imeota mbawa na aliyempora mume ni nyumba ndogo na ndio nikajikuta nakaa na kuandika ule ujinga na kuuweka hapa.

Sikuwa namsimanga yule shoga yangu bali nilitaka kufikisha ujumbe kwa watu wenye mtizamo kama wake.

Wednesday, December 9, 2009

UBUNIFU WA FULANA NA UJUMBE WA MIPASHOFulana zetu na ujumbe wa Mipasho

Kama ningekuwa nimelisema hili humu katika kibaraza hiki, naamini wengi mungeniita mtabiri, lakini bahati mbaya nilikuwa bado sijaanza kublog.

Nakumbuka wakati fulani niliwahi kuwaambia wanafunzi wenzangu wakati huo nikiwa shule kuwa, tunapoelekea si ajabu kukaibuka fulana zenye ujumbe wa maneno ya Kiswahili kama vile yale yanayopatikana kwenye khanga. Hilo nililisema baada ya mwanafunzi mwenzetu mmoja kuvaa fulana ambayo aliiandika maneno ya Kiswahili kwa kutumia Marker Pen ambapo aliandika “MTACHONGA SANA” nadhani labda alikuwa akipeleka ujumbe kwa mahasimu wake ambao alitofautiana nao.

Hilo naona sasa limetimia. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao wamekuwa wakichapisha fulana kwa maneno yenye ujumbe tofauti tofauti kulingana na mahitaji ya jamii kwa kipindi hicho. Zamani tulizoea kuwa wanawake ndio wanaozodoana kwa kutumia maneno ya kwenye Khanga.

Kwa mfano maneno kama, “Utakufa nacho kijiba cha roho” Chuki nichukie roho yangu niachie” “kama unaweza panda juu ukazibe” Nakadhalika, nakadhalika, yalikuwa ni maneno yanayopatikana kwenye khanga peke yake na hiyo ndio iliyokuwa silaha pekee inayotumika na wanawake katika mapambano miongoni mwao hasa katika maeneo ya uswahilini.

Kwa kawaida kama wanawake wametofautiana katika mambo fulani fulani, badala ya kugombana kwa kupigizana kelele ilikuwa mtu ananunua khanga yake yenye ujumbe anaoutaka umfikie mbaya wake na kivaa makusudi ili kufikisha ujumbe aliokusudia kwa mwenzake.
Niliwahi kusimuliwa wakati fulani kuwa hata wale wanawake wanaochukuliana mabwana, nao walikuwa wakipambana kwa kuvaliana khanga zenye ujumbe wa kuzodoana na wakati mwingine mtu anaweza kumchokonoa mwenzake kwa kuvaa khanga zenye ujumbe tofauti tofauti hata saba kwa siku na kujipitisha kwa mbaya wake ili kumpa ujumbe aliokusudia na mara nyingi ilikuwa ni kawaida kwa mahasimu hao kuanza kurushiana maneno na hata kupigana hadharani kutokana na mmoja kukerwa na maneno ya kwenye khanga alizovaa mwenzie.

Tofauti na zamani, siku hizi mambo yamebadilika, na sasa sio khanga pekee, bali hata fulana siku hizi zimekuwa zikibeba ujumbe tofauti tofauti ukiwemo wa maneno ya kuzodoana. Siku hizi kumeibuka wabunifu wa mavazi ambao huchapisha ujumbe wa maneno ambayo tulizoea kuyaona kwenye khanga na kuyaweka kwenye fulana na hata Blouse na watu wamekuwa wakizigombea.

Sio kwamba sifurahii ubunifu huo wa mavazi, bali ninachojaribu kutahadharisha hapa ni aina ya ujumbe unaowekwa kwenye hizo fulana, kuwa usije ukatufikisha mahali watu wakatumia nafasi hiyo kuweka ujumbe wa matusi au hata maneno ya uchochezi, kwani kuna uwezekano ukatufikisha mahali tusipopatarajia.

Naamini wengi mtakuwa ni mashahidi wa hizi fulana au blouse za mitumba zinazoingia kutoka katika nchi za Magharibi na Ulaya ambazo zina ujumbe wa maandishi au hata picha tofauti tofauti. Tumekuwa tukishuhudia ujumbe wa Matusi au hata uchochezi wa kiubaguzi kupitia fulana hizo, lakini kwa kuwa zimeandikwa kwa kiingereza au lugha zao inakuwa ni vigumu walio wengi kung’amua maana halisi ya ujumbe huo labda mpaka mtu aambiwe, wengi tunachojali ni uzuri wa fulana lakini sio ujumbe ulioko katika fulana hizo.

Monday, December 7, 2009

BARUA YA WAZI KWA DADA YASINTA NGONYANI.....

Dada Yasinta Ngonyani

Kwako dada yangu mpendwa Yasinta Ngonyani mzaliwa wa Ruhuwiko Songea mkoani Ruvuma. Habari za siku nyingi na shikamoo zikufikie hapo ughaibuni ulipo, vipi kile kidole chako ulichijichoma na sindano ukishona nguo ya mwanano Camilla kinaendeleaje. Dada nilipokea taarifa za kujichoma kwako na sindano kwa masikitiko sana na sikuamini kuwa hata Ughaibuni mnatumia sindano za mkono kushona badala ya cherehani. Hata hivyo nakupa pole zako japo uliumia kwa uzembe mtupu.

Nashukuru barua yako uliyonitumia nimeipata jana ingawa mwandiko wako ulinipa shida sana kuusoma, na nimeshangaa sana kuwa hata watu walioko ughaibuni wanakuwaga na miandiko mibaya namna hii, usidhani nakukosea adabu dada yangu, naomba uniwie radhi kwani siwezi kuvumilia maudhaifu ya wengine na ndivyo nilivyoumbwa.

Dada dhumuni la barua hii nikutaka kujibu barua yako ya hivi karibuni ambayo ulinishauri eti niolewe kwa kuwa naanza kuzeeka sasa, dada katika barua yako hiyo umeeleza mengi sana juu ya faida za kuolewa. Umedai kuwa kuolewa ni kuondoa nuksi ili usife bila kuvaa pete ya ndoa, na pia ni fahari maana utakuwa huwajibiki kutunza familia hata kama unafanya kazi, kwani hiyo ni kazi ya mwanaume.

Umesema kuwa kwa mujibu wa mila na desturi tulizorithi kutoka kwa mababu na mabibi zetu ni kwamba wanaume ndio wanaowajibika kuwahudumia wake zao na watoto, yaani mwanamke hatakiwi kutoa hata senti tano kuchangia pato la familia kwa kuwa sio jukumu lake, kwani hilo ni jukumu la mume kwa maana yeye ndiye anayehakikisha familia yake inapata kila kitu, ikiwapo chakula, malazi, mavazi, na vipodozi kwa mkewe ili apendeze zaidi. Umesema kuwa kwa kawaida mwanamke ni pambo la nyumba kwa hiyo akibebana na majukumu ni saa ngapi atakuwa ni pambo la nyumba.

Pia umetoa sababu za kisayansi eti kwa jinsi mwanamke anavyozidi kuzeeka basi na mayai yake ya uzazi nayo yanazeeka kwa hiyo nikifikisha umri fulani nitakuwa sina uwezo wa kupata watoto wangu mwenyewe na kama nikibahatika kuwapata watakuwa mataahira au watumiaji wa mihadarati au Vibaka na wapiga debe.

Ukadai kuwa fahari ya ndoa ni watoto kwa hiyo kama nisipozaa ndoa yangu itaota mbawa, hata kama mume wangu atanipenda, mawifi na ndugu wa mume watachonga sana hadi niachike kwani katika ndoa za Kiafrika ndugu wana nguvu sana na wana uwezo wa kuamua hatima ya ndoa yenu watakavyo.

Ulitoa ushahidi mwingine kuwa wanaume wa siku hizi wanapenda kuona wanawake wanaowazidi umri kwa zaidi ya miaka 15 mpaka Ishirini kwa kuwa hao bado damu inachemka, kwa hiyo kwa jinsi ninavyozidi kuzeeka na ndivyo ninavyozidi kupoteza sifa ya kuolewa na kuwa disqualify kama ulivyosema mwenyewe kwa lugha ya kiingereza.

Niliisoma barua yako kwa makini sana na nilitafahari kwa kina, na ili kujiridhisha ikabidi na mimi nifanye utafiti wangu, unajua si vyema sana kuamini kila unaloambiwa hata kama ni kutoka kwa baba au mama yako mzazi. Dada sifa kubwa niliyo nayo ni kutokuwa dodoki kama alivyosema hayati mzee wa Mwitongo Mwalimu Nyerere.
Dada kuwa dodoki maana yake ni kubeba kila unaloambiwa bila kupima na kudadisi ili kujiridhisha, kama unavyojua dodoki ukilichovywa kwenye maji taka litatoka na kila aina ya uchafu, na ndio maana nikasema kuwa sitaki kuwa dodoki.

Katika utafiti wangu dada nimegundua kuwa madai yako hayana ukweli, kwani wanawake wengi walioolewa wanajuta sana na watamani kuachika kutokana na manyanyaso ya wanaume.

Dada kwa mujibu takwimu za chama cha mambo ya wanawake, kuna wanawake wengi wamepeleka malalamiko yao huko wakitaka kuachika kutokana na manyanyaso kutoka kwa waume zao. Wanawake hao wanadai kuwa kigezo wanachotoa wanaume hao kuwanyanyasa ni mahari waliyolipa kwa wazazi wao.

Wanawake hao wanadai kuwa manyanyaso wanayopata yanategemea kiwango cha mahari waliyotozwa hao wanaume wao, kwa hiyo inakuwa ni vigumu kwa wale waliolipiwa mahari kubwa kudai talaka kwa kuwa wazazi washakula chao mapema kwa hiyo hawana uwezo wa kurudisha mahari ya watu na hivyo wanajaribu kutafuta wafadhili toka nje ili wawanasue katika ndoa hizo za mateso.

Wanawake hao wanatafuta uwezekano wa kubadili mila na desturi zetu ili wanawake ndio wawe wanaoa na kulipa mahari kama wahindi kwani kule India wenzetu wanawake ndio wenye sauti kuliko wanaume na ndio maana India na Pakistani zimewahi kutawaliwa na wanawake kama vile mama Indira Gandhi na Benaziri Bhuto ambao wote waliuwawa kwa husuda tu, na wale wanaume wanaotaka mfumo dume kama huu uliotamalaki huku kwetu

Dada kama wewe ni msomaji wa vitabu vitakatifu vya dini zetu hizi za mapokeo utakubaliana na mimi kuwa hata mwenyezi Mungu amewapendelea sana wanaume kiasi cha kuwapa kibri. Hebu soma maandiko matakatifu ya Biblia katika kitabu cha Waefeso 5, 22:24.

Dada maandiko hayo ndiyo yanawapa wanaume kibri kwa kudai kuwa wao ndio vichwa vyetu wakati vichwa vyetu tunavyo na tunatembea navyo.

Kwa hiyo dada ushauri wako kwangu nauona kama unataka kunipalia makaa ya moto ili tufanane wakati mie nimeshawashitukia wanaume zamani sana.
Najua utashangazwa na uamuzi wangu kwa kuwa ulitegemea nikubaliane na ushauri wako lakini napenda kukukatisha tamaa kuwa mie nimeshawashitukia wanaume siku nyingi.

Dada mimi ni mjanja………..LOL

Friday, December 4, 2009

MATEJA NA UTAMU WA TENDO LA KUJAMIIANA!


Mimi kwa kawaida ni mdadisi sana, na naomba nikiri kuwa udadisi wangu uliwahi kuniletea matatizo wakati fulani. nakumbuka nilikuwa naendesha gari katikati ya jiji, na wakati nimesimama kwenye taa za kuongozea magari,akaja mama mmoja ombaomba ambaye namkadiria kufikisha umri wa miaka 60 hivi.
Alionekana kuwa na afya njema tu. Alipofika pale nilipo aliniomba pesa, nilitoa kiasi cha fedha na kumpa, lakini nilimuuliza kwa upole kwamba kwa nini anaomba barabarani wakati afya yake ni nzuri tu. mama wee....alinishambulia kwa matusi na kama sio taa za barabarani kuniruhusu labda angenipasulia kioo cha gari langu, kwani nilimuona kupitia kioo cha pembeni akiokota kitu nadhani kwa ajili ya kunirushia, lakini alichelewa kwani nilishafika mbali. Tukio hilo lilinikumbusha tukio lililompata dada yangu Yasinta Ngonyani na mwendawazimu wa Ruhuwiko Songea.

Ngoja nirejee kwenye kile nilichotaka kusimulia leo. Nimesema kuwa mimi ni mdadisi sana, na udadisi wangu naona saa utaniletea matatizo, lakini sitaki kuacha na sijui ni kwanini. Juzi nikiwa kwenye Intenert Cafe moja iliyopo maeneo ya Mikocheni nilikutana na kaka mmoja ambaye ni mtumiaji wa madawa ya kulevya, maarufu kama Teja. Kijana huyo ambaye nilisoma naye shule moja akiwa amenitangulia darasa moja mbele, alikuwa akisifika sana kutokana na kuwa na akili sana darasani wenyewe tulikuwa tunaita akili za Nature, na mpaka tukawa tunamuita Nature kutokana na kuwa na akili ambazo sio za kawaida.

Alifanikiwa kufaulu na kuendela na masomo ya sekondari, nasikia alifaulu kidato cha nne na kuingia kidato cha tano na kupangiwa kwenda shule moja maarufu mkoani Tanga na huko ndipo alipojitumbukiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya na kuwa Teja kiasi cha kusababisha kufukuzwa shule na kurejea jijini na kuendela na tabia hiyo.

Nilipokutana naye pale cafe nilipiga naye stori mbili tatu na ndipo nikamuuliza swali, kwamba kwa nini amejiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya wakati alikuwa na maendeleo mazuri shuleni. Nilimuona akibadilika ghafla kama vile amekasirika, niliona mambo si shwari, ikabidi nimuwahi kumuomba radhi kwa swali langu la kijinga, lakini aliniambia kuwa hajakasirika, na kwa upole akaniuliza swali......

"Samahani Da' mdogo Koero, hivi unajua utamu wa tendo la kujamiiana?" Nilishangazwa la swali lile, lakini kwa kuwa niliyataka mwenyewe nikajikuta nikimjibu kuwa nafahamu. Kisha akaniuliza tena..... "Je Unajua utamu wa tendo la kujamiiana unadumu kwa muda gani katika ubongo wa binadamu?" Duh! hili lilikuwa ni swali gumu kwangu na nilijua sasa na mimi nimepatikana maana nilijifanya kuwa mdadisi, lakini sasa mambo yananigaeukia.

Nilijikakamua na kumjibu kwa kifupi. "Sijui maana sijawahi kufanya utafiti huo"
Yule kijana kwa upole akaniambia, "kwa kuwa umeuliza swali basi nitakujibu tena kwa ufasaha ili wakati mwingine usije ukauliza tena kwa mtu mwingine"

Aliniambia kuwa kwa mujibu wa tafiti mbalimbali imebainika kuwa utamu wa tendo la kujamiiana unadumu katika ubongo wa binadamu kwa sekunde tano tu, mtu anapofikia kileleni, lakini mtu anapotumia madawa ya kulevya, yaani pale anapojidunga dozi, ule utamu anaoupata ambao unafanana na utamu wa tendo la kujamiiana unadumu kwa dakika kumi na tano.
Kisha akaendelea kusema kuwa, kama utamu wa kujamiiana ambao hata hivyo unadumu kwa sekunde tano tu, lakini watu wanaupenda kupita kiasi huku wengine wakihatarisha maisha yao dhidi ya gonjwa la ukimwi na wengine wakitiana ngeu au hata kuuana kwa sababu ya utamu huo, kwa nini yeye asiamue kuwa Teja ambapo anaweza ku-enjoy kwa takribani dakika kumi na tano bila bughdha kwa kitu ambacho hakimpi usumbufu.

Wakati wote akinipa darasa hilo nilibaki nimemtumbulia macho kwa mshangao na nisiamini kile alichokuwa akinisimulia. Kusema kweli sikuwa na swali la nyongeza, nilimshukuru kwa majibu yake nikamuaga ili niondoke, lakini alinitaka nimuachie hela akapate kete yake ili apate stimu kwani nilimvurugia stimu yake kwa kumuuliza lile swali.

Sikutaka kugombana naye, nilitoa kiasi cha pesa na kumpa, kisha nikaondoka. Yaani kiranga kiliniisha, maana sikutegemea yale majibu ambayo yalikuwa na ushahidi wenye utafiti ambao hata sikujua kama utafiti ule una ukweli kiasi gani.

Hata hivyo kwa umbeya wangu nimeona niiweke hii habari hapa kibarazani ili nilete changamoto toka kwa wadau na wasomaji wa blog hii.

Sunday, November 29, 2009

HE, ETI WAZEE HAWAPENDI KUVAA CONDOM!

Naomba muniwie radhi kwa kile nitakasimulia hapa leo, maana inawezekana nisiwafurahishe baadhi ya wasomaji wa blog hii au wanablog wenzangu. Ni jambo ambalo nililitafakari sana kabla hata sijaamua kuliweka humu nikaona ni bora niliweke ili niwashirikishe wadau wa blog hii.

Jana majira ya jioni nilitoka na shoga yangu kwende kupata mtori katika mgahawa ulioko jirani na nyumbani. Nakumbuka ilikuwa ni majira ya saa kumi mbili za jioni hivi. Wakati tunaendelea kula mtori wetu mara wakaja akina dada wawili ambapo walikaa katika meza iliyoko jirani na meza tuliyokaa.
Walikuwa wakicheka kwa furaha kuonesha kuwa ni marafiki ambao aidha walipoteana siku nyingi au walikuwa wanapeana habari kama ilivyo kawaida ya kina dada kila wakutanapo.

Hatukuwajali na tuliendelea na stori zetu, lakini nilijikuta nikivutiwa na mazungumzo yao. mmoja wa wale kina dada alikuwa akimasimulia mwenzake jambo fulani ambalo lilinivutia kulisikiliza. Hebu ngoja niwamegee kile nilichosikia kama kilivyo, sitapunguza wala kuongeza ili nisipunguze utamu maana kwangu mimi simulizi ile ilikuwa ngeni kwangu.

Yule dada alikuwa akimsimulia mwenzie juu mambo yaliyomkuta juma lililopita, na simulizi yake inaanza kama ifuatavyo:

Basi, mwenzangu huku kula kwangu vichwa, jana si yakanikuta ya kunikuta......
Hee! bibi wewe ni yapi hayo yaliyokukuta tena? Aliuliza mwenzake waliofuatana naye.
Yule dada akaendelea kusimulia mkasa wenyewe, Si unajua mishe mishe zangu za kutafuta mishiko {Nadhani Fedha} basi juzi mida ya usiku majira ya saa tatu nikazama zangu Club, na kwa kuwa nilipigika ile mbaya nilikuwa nimepania kuwa ni lazima nisitoke kapa, ile natia maguu tu maeneo ya viwanja mara ikasimama Toyota Hurrier moja nyeupe jirani na niliposimama kwenye kiosk kimoja ili kununua zana si uanjua huwezi kwenda vitani bila silaha...... mara kioo kikafunguliwa, na mzee mmoja hivi wa makamu ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha lile gari aliniita, nilisita kidogo, unajua mie siwahusudu sana mablakii wa kibongo kwa kuwa hawakati mshiko wa maana, nilijivuta hadi pale aliposimama yule mzee, aliniomba nipande kwenye gari ili tuzungumze, nilimuuliza tunaenda wapi, aliniambia kuwa tunakwenda kupata chakula cha usiku mahali kama kampani tu. "Sikiliza mzee mie niko kazini kama ni biashara sema una kiasi gani, sio mambo ya misosi, kwani mie nilikwambia nina njaa?" nilimwambia kisha nikaanza kuondoka kwa madaha, akaniomba nirudi tumalizane, na niliporudi akaniuliza nitahitaji kiasi gani, nikamtajia kiasi kikubwa cha hela nikidhani atashindwa, akaniambia powa twen zetu......basi tukaondoka zetu

Yule mzee alinimbia kuwa anayo nyumba yake maeneo ya mbezi beach na ndipo tunapokwenda kupumzika, alionekana ni mtu wa heshima na aliyekuwa akiongea kwa upole, aliendesha kwa kasi na alikuwa haongei alikuwa amefungulia muziki wa kizungu wa taratibu kwa sauti ya juu kidogo. tulipofika alipiga honi geti likafunguliwa na mlinzi, tukaingia ndani na kupaki gari kisha tukashuka na kuingia ndani, lilikuwa ni jumba la kifahari hasa. Tulipoingia pale sebuleni nilikuta kuna sofa nzuri za maana na kulikuwa na Bar, yule mzee aliingia pale Bar na kuchukua whisky na barafu na kujimiminia kisha akanimiminia na mimi, nilikataa na kumwambia kuw napendelea Ram badala yake, aliingia kwenye ile Bar na kunichukulia Bacard na Coke na glass ya barafu na kuniletea.

Yule mzee alikuwa akiifakamia ile Whisky kwa kasi ya ajabu kama vile alikuwa akiwahi mahali, anishika mkono na kuniingiza chumbani kwake, nilimuuliza kuwa mkewe yuko wapi, aliniambia kuwa hainihusu na nisitake kujua juu ya mkewe, alikuwa akiongea kwa hasira kama vile tumegombana vile, alinitupa kitandani na alinivamia kama nyati aliyejeruhiwa pale kitandani,.....nilianza kuogopa, nikamuomba atulie nivue mwenyewe...Shoga yangu wee kwani alinisikia, nilibaki kimya kusubiri kitakachotokea, lakini nilishtuka nikamuuliza kama anazo Condom, maana sikuwahi kujinunulia pale kwenye kiosk, akaniambia kuwa hana Condom na hayuko tayari kuvaa condom kwa kuwa sio utamaduni wake,

"Hee mwenzangu ulikuwa hujui...Wazee huwa hawapendi kuvaa condom, kwani hata mie yaliwahi kunikuta pia, tena mara tatu,mie sivitaki kabisa vizee," alidakia mwenzie.

Basi mwenzangu niliogoppa ile mbaya,ikabidi nimuombe anipa pesa yangu kabisa tuliyopatana, yule mzee akanyanyuka na kwenda kabatini, nikajua amefuata pesa, mara akarudi akiwa na Bastola mkononi, niliogopa nusura nizimie, kisha akaniambia kwa ukali. "Sikia wewe malaya, ukileta ubishi nitakuua na hakuna atakayeuona mzoga wako, usiniletee masihara kabisa, unasikia?" aliongea kwa ukali na alionesha kabisa alidhamiria kunifanyia unyama, nilitulia kama maji mtungini, kwanza sikujua nipo wapi na hata sijui akinitoa hapo nje nitaelekea wapi. Alinifanyia alivyotaka tena pekupeku, nakwambia, dada hakunibakisha si mbele wala nyuma, nilikuwa namuomba mungu amalize hamu yake anirudishe aliponitoa.

Alimaliza nakuniruhusu nikaoge kisha anirudishe aliponitoa, niliingia bafuni na kuoga harakaharaka ili niwahi kuondoka maana niliogopa asije akanirudia tena. Basi shosti nilipomaliza nilivaa haraka haraka bila hata kujipodoa na nilipotoka pale sebuleni nilimkuta ametulia akiangalia TV huku akiendelea kunywa whisky yake taratibu.

Tuliondoka pale na kunirudisha pale kijiweni kwangu, ambapo pia alinipa mshiko wangu kama tulivyopatana, yaani nakwambia hata sikuona kama ile hela ina maana kwangu, nilijuta na kujiona kama mjinga kumkubalia yule mzee, kwani sina uhakika kama hajaniachia miwaya, maana alikuwa hana wasiwasi wakati anajua wazi juu ya shughuli yangu ya kujiuza.

"Shoga sasa si ukapime ujue afya yako?" Alishauri mwenzie...
" Nyoo akapime nani? Mie? Thubutuu, haki ya nani sithubutu! ya nini nipime nijiuwe bure kwa presha".

Waliendelea kusimuliana uchafu wao na sie tukaondoka mahali pale, lakini moyoni nilikuwa na maswali kadhaa niliyokuwa nikijiuliza, juu ya ile shughuli waliyokuwa wakiifanya wale mabinti ambao kwa mtazamo wangu wangeweza kujiajiri na kujipatia kipato cha kuwawezesha kujikimu. Kingine ni kile walichodai kuwa wazee hawapendagi kuvaa condom, swali la kujiuliza, hivi wake wa wazee wenye tabia hizi ziko salama kweli? Na je ni wazee au hata vijana wangapi wenye tabia hizi ambao wamepoteza maisha na kusababisha mayatima na wajane kuongezeka na kuwa mzigo kwa jamii na serikali?

Kusema kweli nilivutiwa sana na simulizi ile ambayo kiukweli ilikuwa hainihusu, ila kutokana na umbeya wangu nimeona niwamegee wanablog na wasomaji wenzangu ili tutafakari kwa pamoja.

Thursday, November 26, 2009

NAJARIBU UPANDE WA PILI-VUKANI NDANI YA KWANZA JAMIII........

Wengi watanisoma humo

Rafiki yangu Markus Mpangala aliwahi kunishauri kuwa niwe muandishi wa habari, nikakataa wazo lake, lakini siku za hivi karibuni nimevutiwa sana na Gazeti la Kwanza Jamii na nimeona nitume Vijimakala vyangu humo, ili sauti yangu ya nyikani iwafikie wengi..........

Monday, November 23, 2009

TUMEMUENZI VIPI HAYATI HUKWE NZAWOSE?

Hayati Hukwe Nzawose

Ahsante kaka Mubelwa kwa kunipa Link ambayo imeeleza kwa muhtasari maisha hadi kifo cha msanii huyu Hukwe Nzawose.

Kusema ukweli sikufahamun kama Hukwe Nzawose amekwisha fariki siku nyingi kiasi hicho, sijui ni kutofuatilia kwangu habari, au msiba wake haukupewa uzito unaostahili kwenye vyombo vyetu vya habari.

Lakini nina maswali kadhaa ambayo ningependa kupata majibu:

Je Serikali yetu iliwahi kumtunukia nishani yoyote ya heshima Dr. Hukwe Nzawose, kabla na baada ya kifo chake?

Je kazi zake zinatumika vipi katika kutangaza utamaduni wetu hapa nchini na hata nje ya nchi?

Je kuna mnara wowote wa kumbukumbu ambao umejengwa kule Bagamoyo kuonyesha kuthamini mchango wake pale chuo cha sanaa Bagamoyo?

Mwisho naomba nitoe changamoto kwa wasomi wetu, kwamba kuna haja ya wao kukaa chini na kuandika historia ya mtu huyu ili iwe ni kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Saturday, November 21, 2009

ETI HUYU NI NANI?

Huyu ni nani?

Ndugu wasomaji, leo nilikuwa nachungulia mtandaoni nikajikuta nikivutiwa na hii picha ya huyu jamaa, naambiwa kuwa eti ni Mtanzania na anaishi ughaibuni. Mnaomfahahamu, naombeni mnijuze.....Huyu ni nani?

Wednesday, November 18, 2009

NIKAPIGIWA “EMCHEKU”

Usiku ndio muda muafaka

Ni usiku wa saa tatu hivi, niko kijijini kwa bibi Koero, na tuko jikoni tunaota moto, huku akinisimulia simulizi mbalimbali juu ya maisha. Bibi Koero ni hodari wa kutoa simulizi zenye kufundisha na za kusisimua.

Tukiwa katikati ya mzungumzo, mara tukasikia michakato ya miguu huko nje kuashiria kuwa kuna mtu huko, “Emcheku aha” ilikuwa ni sauti ya kiume kutoka nje, bibi aliniambia nitoke ili kuangalia kuwa ni nani.

Nilipotoka, kwa kuwa kulikuwa na giza, niliona kivuli cha mtu, lakini alikuwa na kurunzi yenye mwanga hafifu, na alikuwa akiiwasha na kuizima, nilirudi ndani kwa hofu na kumweleza bibi Koero mauzauza niliyokutana nayo huko nje.

Bibi Koero alicheka sana, na kuniambia kuwa, huyo ni mgeni wangu, kaja pale kuposa, na mlengwa ni mimi kwa kuwa hakuna binti mwingine pale nyumbani bali ni mimi.
Nililishangazwa na aina ule ya posa, kwangu mimi ile ilikuwa ni habari, na ili kujua mengi zaidi, nilimdadisi bibi Koero ili anisimulie juu ya utaratibu huo.

Bibi Koero anasimulia kuwa enzi zao, binti akivunja ungo, vijana huanza kufika pale mida ya usiku kupiga hiyo “Emcheku” inawezekana wakafika zaidi ya wavulana kumi kwa usiku mmoja kulingana na uzuri na tabia ya binti huyo.
Emcheku ni salaam ya heshima anayotoa mvulana anapokwenda kuchumbia.

Kwa kawaida wavulana hao wakifika kila mmoja kwa muda wake na kupiga hiyo Emcheku, Binti husika huambiawa atoke nje kuonana na mvulana huyo na kama hajampenda basi humweleza na huyo kijana huondoka zake, na akitokea mvulana anayempenda, basi hupewa ruhusa na binti huyo ili alete Posa na hapo ndio milango hufunguliwa kwa mvulana huyo kumtembela mchumba wake.

Mara nyingi matembezi hayo hufanywa usiku na mvulana akifika binti huruhusiwa na wazazi kutoka nje ili kuzungumza na mchumba wake, lakini walikuwa hawaruhusiwi kukutana kimwili au kuonjana mpaka utakapofika muda muafaka watakapofunga ndoa takatifu.

Tofauti na zamani, bibi Koero, anasimulia kuwa, siku hizi vijana wamebadilika sana na wengi wameuharibu utaratibu huo na kuugeuza kuwa kichaka cha kufanyia ngono. Wavulana siku hizi kama anamtaka binti, hupiga hiyo Emcheku na binti akiridhia, humhadaa, mpaka amuonje na akifanikiwa kuingia mitini na posa inaota mbawa.

Unaweza kukuta mvulana anawahadaa wasichana zaidi ya kumi lakini aisoe hata mmoja baada ya kuwaonja.

Wasichan nao wamekosa subira, kila wakisikia hiyo emcheku, wanajua kuwa ni bahati imewajia, kumbe hakuna lolote ni wavulana mafisadi tu wenye uchu wanataka kuwaonja na kisha kutoweka.

Sasa sijui na mimi nilipigiwa hiyo emcheku ili kuonjwa……LOL

Sunday, November 15, 2009

MUNGU ALINIONYESHA MSIBA ULE!


Kwanza ningependa kuchukua nafasi hii kuwashukuru wasomaji na wanablog wenzangu wote mlionipa pole kwa msiba uliotupata. Kusema kweli kama walivyosema baadhi ya wanablog kuwa ule ulikuwa ni msiba wa taifa kwani roho za watu zaidi ya 20 zimepotea wakiwemo watoto ambao bado walihitaji kuishi na kutimiza ndoto zao.

wakati mwingine unaweza kukufuru mungu kw kuhoji kile kilichotokea, lakini kama maandiko matakatifi katika vitabu vya dini hususana hizi dini zetu mbili ambazo ndizo dini kuu hapa nchi yaani ukristo na uislamu, vilivyoeleza kuwa yote mema na mabaya yanatoka kwake yeye na hatupaswi kuhoji mamlaka yake.
Lakini kama si hivyo naamini tungekuwa tunamlaani sana Mungu pale tunapoondokewa na wapendwa wetu.

Ukweli ni kwamba msiba ule uliotupata nilionyeshwa kabisa na mwenyezi Mungu katika njia ya ajabu sana. Ni kiasi cha wiki nilikuwa nasumbuliwa na malaria kiasi cha kulazwa Hospitalini na kutundikiwa Drip za Kwinini. Nakumbuka siku mbili kabla yakupata msiba ule niliota ndoto ya kustaajabisha sana, niliota kuwa nimeenda kijijini kwa bibi Koero kumtembelea na nilipofika kule kijijini nilipokewa na bibi Koero lakini hakuwa na furaha sana kama nilivyokuwa nimemzoea, nilipomdadisi sababu ya kutofurahishwa na ujio wangu, alinijibu kwa kifupi tu kuwa anajisikia vibaya.

Siku iliyofuata aliniomba nimsindikize shambani kwake ili akanioneshe mazao aliyolima, tulipofika shambani nilishangaa kukuta matuta mengi ya viazi vitamu yakiwa yamestawi barabara, niliruka kwa furaha, kwani mimi huwa napenda sana viazi vitamu, bibi alionekana kunishangaa, nilipomdadisi kuwa kwanini haonekani kufurahia mazao yake, aliniambia kuwa, sina haja ya kufurahia kustawi kwa vile viazi kwani havina ishara nzuri katika familia yetu. nilimdadisi anifafanulie maana ya kusema vile, aliniambia tukae chini anieleze.

Aliniambia kuwa hapo zamani enzi za mababu zao, ilikuwa kama mtu akilima viazi kisha vikastawi sana na kuonesha ishara ya mavuno ya kutosha, waliamini kuwa hiyo sio ishara nzuri katika familia husika, kwani ni lazima pangetokea maafa makubwa au kupata msiba wa mtu mzito katika familia, kwa hiyo hata yeye hawezi kufurahia kustawi kwa yale mazao kwani sio ishara nzuri katika ukoo wetu.

Nilijikuta nikilia kwa sauti, baada ya kusimuliwa habari ile na bibi Koero, nilishtuliwa na mama, alipokuja kuniamsha baada ya kusikia kilio changu. Ilikuwa ni saa kumi za alfajiri, nilimsimulia mama na bada ya kumweleza juu ya ile ndoto aliniambia kuwa sina haja ya kuamini kwani ni mambo ya kishetani, hata hivyo tulisali na mama kisha nikarudi kulala, lakini sikupata usingizi kutokana na kuogopa, ikabidi niamke na kuanza kusoma mtandao na baadae ndio nikaandika ile habari ya siku ya kufa kwangu, nilijikuta tu nikiandika na kuiweka hapa kibarazani kwangu.

Jioni nilipata email kutoka kwa kaka Shabani, Mzee wa Utambuzi. Email yake ilinifumbua macho na kuuona ukweli mpana zaidi, kwamba ile makala yangu haikuashiria jambo jema. kwani baada ya kusoma ile makala yangu niliyoipa kichwa cha habari kiisemacho SIKU YA KUFA KWANGU, kaka Shabani aliniandikia akiniambia kuwa ile makala imemtisha sana na aliniambia kuwa haiashirii jambo jema. Alitaka kujua zaidi hali yangu na pia kujua niliwaza nini mpaka kuandika makala ile.

Sikuweza kumjibu kutokana na kutingwa, lakini siku iliyofuata wakati najiandaa kumjibu na labda kumtaka ushauri juu ya ile ndoto niliyoota ndipo tukapokea taarifa za maafa yaliyotokea kijijini kwa mama ya kuporomoka kwa mlima kulikosababishwana mvua kubwa na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 20 wakiwemo shangazi na mjomba wake na mama pamoja na watoto wao.
Ulikuwa ni msiba mzito sana kwetu kwani alikuwa ndiye shangazi yake mama pekee aliyebaki, baada ya shangazi zake watatu kufariki miaka kumi iliyopita.

Safari yetu nayo ya kuelekea msibani iligubikwa na mauzauza mengi, kwani wakati tunakwenda, mimi ndiye niliyekuwa nikiendesha gari na tulipofika Korogwe kwenye kona za msambiazi niligonga Kondoo ambapo alikufa pale pale, nilibabaika kidogo ikabidi dada yangu anipokee na kuendesha yeye.

Leo wakati tunarudi tulisimama Korogwe ili kupata chakula cha mchana, na baada ya kupata chakula tukarejea kwenye gari ili kuendelea na safari, ni hapo ndipo tukagundua kuwa kitasa cha mlango kimevunjwa na mkoba wa mama uliokuwa na fedha, simu zake mbili za mkononi na Kamera umeibwa, tulijaribu kuwauliza watu waliokuwa jirani na gari letu, lakini hatukupata ushirikiano, tuliamua kuondoka lakini tulipofika ya maeneo ya Kwedikwazu, mdogo wangu Jarome ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha gari akagonga mnyama jamii ya kicheche au sijui ni fungo, hata sijui alikuwa ni mnyama gani maana alikuwa akiendesha kwa spidi kubwa kidogo. Ilibidi tumshauri apunguze mwendo hadi tukafika Dar.
Kilichotuuma ni kuibiwa kwa kamera ya mama ambayo ilikuwa na picha nyingi za kumbukumbu ya mazishi ya wale wahanga wa maporomoko ya mlima. Ni jambo ambalo lilitufadhaisha sana.
Tumerejea salama, na wote tuwazima wa afya

Wednesday, November 11, 2009

SIKU YA KUFA KWANGU!


Wengu tunaogopa kifo!

WAKATI NASOMA HIKI KISA KWA MARA YA KWANZA NILIOGOPA SANA, LAKINI KUNA KITU NILIJIFUNZA, HATA WEWE UNAWEZA KUJIFUNZA PIA.Naomba wakati unasoma hii habari uwe peke yako na uwe umetulia, bila kubughudhiwa.
Hakikisha hakuna unaloliwaza wakati unapoanza kusoma kwani hiyo itakusaidia kung’amua kile ninachomaanisha katika habari hii.


Naomba usiwe mwoga, kwani ni habari ambayo itakufunza jambo fulani katika maisha.
Haya ungana nami katika kusoma habari hii.


Katika akili yako hebu hisi kama vile unajiona, yaani tengeneza taswira kama vile unajiona ukiwa unaenda kuhudhuria mazishi ya mtu umpendae na unayemfahamu. Jione ukiwa unaendesha gari kuelekea kanisani ambapo ndipo mahali watu wanapokusanyika kuuaga mwili wa marehemu kabla ya mazishi.


Unapofika pale unapaki gari lako na kutoka kuelekea ndani ya kanisa, unapoingia ndani ya kanisa unaona kumepambwa na maua mazuri yenye kunukia na huku ukisikia ala za muziki mororo. Wakati ukielekea kwenye eneo ulilopangiwa kukaa unawapita ndugu, jamaa na marafiki wakiwa na nyuso zenye huzuni na majonzi yenye kuashiria kusikitishwa na kuondokewa na mtu waliyempenda sana.


Unapokaribia kufika kwenye nafasi uliyopangiwa kukaa, unapita karibu kabisa na sanduku lenye mwili wa marehemu na unapotazama mwili ulioko ndani ya sanduku hilo unastuka kuona mwili ulioko ndani ya sanduku hilo ni wa kwako!
Mara kuna sauti inakwambia "haya ni mazishi yako yatakavyokuwa miaka mitatu ijayo kuanzia sasa"


Watu wote walioko pale wamekuja kuonyesha mapenzi yao kwako na kukupa heshima kwa kuuaga mwili wako ili ukapumzike kwa amani.


Duh! Unashusha pumzi na kuketi, ili kusubiri ibada ianze. Unapoangalia ratiba ambayo ulipewa wakati unaingia pale kanisani unakuta wamepangwa wazungumzaji wanne, wazungumzaji wa kwanza wanatoka katika familia yako, mmoja wa watoto wako, mmoja wa kaka zako, dada zako, binamu, shangazi, mjomba, baba mdogo, mama mdogo, bibi, babu na ndugu wengine wa karibu ambao walisafiri maili nyingi ili kuja kushiriki mazishi yako.


Mzungumzaji wa pili ni mmoja wa marafiki zako ambaye mlishibana sana, mzungumzaji wa tatu ni kutoka katika mahali pako pa kazi na mzungumzaji wa nne ni kutoka katika kanisa unalo Sali au kutoka katika taasisi ya kijamii ambayo ulikuwa ukishiriki katika kuihudumia jamii baada ya muda wako wa kazi.


Sasa hebu fikiria kwa makini sana. Ungependa wazungumzaji hawa wazungumze nini juu ya maisha yako hapa duniani? Wewe ni mume, mke, baba au mama wa aina gani? Wewe ni mvulana, msichana, binamu, wa aina gani? Ni rafiki wa aina gani? Ushirikiano wako na wafanyakazi wenzako ulikuwaje?


Ungependa wakuzungumzieje? Ulikuwa ni mtu mwenye tabia gani kwa ujumla? Uliisaidiaje jamii, ulifanikiwa katika lipi? Ungependa wakukumbuke kwa lipi? Hebu waangalie kwa makini watu waliokuzunguka. Kama ungepewa nafasi, ungeyabadili vipi maisha yao?
Kama umesoma kwa makini habari hii naamini kuna jambo utakuwa umejifunza.
Nimegundua kuwa ili ujue kuwa wewe ni mtu wa namna gani ni vyema ukahudhuria mazishi yako mwenyewe………………


Tafakari…………….


Habari hii nimeitoa katika kitabu cha The 7 habits of highly effective people cha Stephen R Covey.

Saturday, November 7, 2009

MSIONE KIMYA......NAUMWA

Naikumbuka picha hii enzi hizo!

Ndugu zanguni, msione kimya, nimeshambuliwa na anofelesi na sasa najiuguza majeraha ya malaria yapata wiki sasa, nimepata tiba ipasayo lakini majaaliwa ya afya yangu hayaoneshi kutengemaa....nawashukuru sana kwa kunitembelea, na hapo nitakapopona nitarejea kwa kasi ya ajabu...

Nawapenda wote na mungu awabariki..

Saturday, October 31, 2009

LEO TUCHEMSHE BONGO KIDOGO.

Ndugu wasomaji wa blog hii takatifu, leo nataka nijaribu bongo za watu kama zinafanya kazi sawa sawa maana week end hii nimekosa hata cha kuandika kutokana na kuzidiwa na majukumu ya kifamilia.

Nimetenga zawadi za kuwatumia washindi watakaoshinda katika kujibu mafumbo haya yote. Zawadi ya kwanza itakuwa ni Picha yangu kubwa ya ukutani kwa wale walioko ughaibuni au mikoani, au kupata chakula cha usiku mimi na mshindi wa kwanza katika Hoteli maarufu jijini Dar kwa wale walioko hapa Dar. Zawadi ya pili ni kutumiwa zawadi ya kitabu cha The Secret kilichoko online na zawadi ya tatu ni kutumiwa picha ya familia ya mzee mkundi.

Haya tuanze kufumbua mafumbo yafuatayo:


Fumbo la Kwanza:

Mama Yasinta ana watoto watano, wa kwanza anaitwa Nana, wa pili anaitwa Nene, wa tatu anaitwa Nini, wa nne anaitwa Nono, Je wa tano ataitwa nani?

Fumbo la Pili:

Kuna mtu mmoja bubu alikwenda kununua miwani dukani, alipofika alimuonesha muuzaji ishara kama vile anavaa miwani yule muuzaji akamuelewa na kumpatia miwani akaondoka zake, mara akaja kipofu, Je unadhani ataonesha ishara gani ili apatiwe miwani?

Fumbo la Tatu:

Ninazo namba kumi zifuatazo: 1,3,5,7,9,11,13,15,17.19
Kama ukizijumlisha zote yaani 1+3+5+7+9+11+13+15+17+19 unapata 100.
Unachotakiwa kufanya ni kutafuta namba 5 miongoni mwa namba hizo ulizopewa hapo juu na ukizijumlisha unapata 50 yaani nusu ya 100.

Masharti:
Haitakiwa kurudia namba, kwa kuijumlisha mara mbili au kujumlisha namba pungufu ya namba tano zinazotakiwa. kwa mfano: 13+17+15+5 unapata 50. Sio sahihi kwa kuwa idadi ya namba zilizojumlishwa hazifiki 5.

Haya nasubiri majibu yenu…….

Friday, October 30, 2009

HUU NDIO WEMA!

Jirani kala nini?Huu ndio wema! Unapotenda wema usitegemee fadhila. Unapokuwa na marafiki, ndugu, na jamaa wa karibu, watendee wema bila kudhamiria kupata fadhila kutoka kwao. Ninapoongelea wema na kutoa ninamkumbuka mama Theresa wa Calcutta ambaye kwa umri na maisha yake angelikuwa Bilionea lakini kwa kujitolea kwake alikufa masikini, lakini akiwa ni tajiri wa nafsi. Nina maana alikufa akiwa na ridhiko, kwani kazi aliyotaka kuifanya aliifanya tena kwa kufaulu. Je wewe hufurahii kuwa kama yeye?

Kumbuka amri kuu isemayo “mpende jirani yako kama unavyojipenda” Je unapokula na kusaza huwa unajiuliza kuwa jirani kala nini?

Tafakari………

Wednesday, October 21, 2009

JAMANI HUU NI UTABIRI, UNAJIMU AU DHIHAKA?

Jamani mimi sio mpenzi au mshabiki wa mambo ya Nyota, kwangu mimi nachukulia kama huo ni ushirikina. Jana kuna mdau kanitumia huu utabiri au sijui niite unajimu, akinituhumu kuwa, kwa kuwa nimezaliwa mwezi wa Mei basi ninazo tabia hizi. Ukweli ni kwamba sina uhakika na hicho alichoandika, na siamini kabisa kama ninazo tabia hizo, ila waswahili wanasema Nyani haoni kundule. Kwa hiyo naomba wadau munisaidie kama unajimu huu unanihusu………….maana naona hii ni kaaaaaaaazi kweli kweli.

TABIA ZA WATU WALIOZALIWA MWEZI MEI…….HATA WEWE KOERO UMO

Mtu yeyote ambaye amezaliwa mwezi wa Mei mwaka wowote, anaweza kuwa na alama ya nyota ya Ng’ombe {Tauras} au Mapacha {Gemini}. Hapa sitazungumzia nyota moja moja, bali nitazungumzia mwezi ambao amezaliwa mtu. Kwa hiyo nitazungumzia waliozaliwa mwezi wa Mei ambapo wewe Koero ni mmoja wapo.

Watu waliozaliwa mwezi wa Mei ni wagumu, hawaambiliki wanapotaka kufanya jambo, wanapopania. Tunaweza kusema ni watu ving’ang’anizi. Lakini kwa bahati mbaya sana, kama wamempenda mtu, hakuna watu wanoporomoka kirahisi kama wao. Yaani kama wamempenda mtu wanashikwa kirahisi kuliko mtu mwingine yeyote.

Ni watu ambao wanaweza kuvumilia shida na suluba za maisha katika kiwango cha ajabu. Ni watu ambao wanamudu kuhimili misukosuko kimwili na kiakili, yaani hawachanganyikiwi kirahisikwenye misukosuko, hasa kama nia yao ya kung’ang’ania bado ipo.

Ni watu wenye uwezo mkubwa wa kumbukumbu. Kama ni uwezo wa kukariri masomo, basi ndiyo wenyewe. Lakini kwa bahati mbaya, wanapenda sana kujumuika na kujimwaga. Kwa hiyo wengi huwa hawafaidi matokeo ya vipaji vyao na wakati mwingine hata hivyo vipaji havionekani kwa sababu vinafungwa na kupenda kwao starehe.

Ni watu pia wanaofaa kwenye kazi kama zile za uhudumu katika ndege au hata mighahawani. Wana sifa ya kujua ladha ya chakula na wanamudu kutengeneza chakula kizuri sana nyumbani hata kama vifaa na fedha ni haba sana.

Ni watu ambao pia wana uwezo wa kuongoza kwenye mashirika au maeneo ya shughuli. Watu waliozaliwa Mei, inawezekana kwa nje wakaonekana kuwa na uwezo sana kuliko walionao kweli.

Hii ni kwa sababu wanajipenda sana, iwe kuvaa au hata kuwa na vitu vingine vya thamani vya nje. Mtu aliyezaliwa Mei anaweza kuwa na gari kubwa, lakini akiba ya shilingi elfu moja mfukoni hata nyumbani hana. Anaweza kuwa anavaa suti kila siku wakati hata godoro la kulalia hana.

Ni watu ambao wakipenda mtu wanakuwa kama vichaa, kwani watampa kila kitu. Kama nilivyosema, wanashikwa kabisa na kuwa kama mazuzu. Lakini wakimchukia mtu watapambana naye hadi waone kinaeleweka. Uzuri wao ni kwamba, wanapenda kukabiliana na mtu ana kwa ana, hawapendi mambo ya chini chini au njama. Wanapenda maisha ya wazi tu, hata kama ni ugomvi au uadui.

Watu waliozaliwa mwezi Mei iwe wanaume au wanawake hawatakiwi kuoa au kuolewa mapema. Hawatakiwi kufanya hivyo kwa sababu mara nyingi, kama sio zote ndoa zao za kwanza huwa wanakuwa wamekosea kuchagua. Labda ni kwa sababu wakishapenda wankuwa ni vipofu halisi. Ni watu ambao wanatakiwa wakitaka kutafakari na kuamua jambo wake wenyewe na kutafakari kimya. Hii ni kwa sababu wakiwa katika watu wengi, wantokea kuwaamini watu hao wengi na kuchukulia mawazo ya hao wengi kama yao. Ni watu ambao huchanganywa na kudanganywa kirahisi. Ni watu ambao wanapoingia kwenye hisia au upendo, hawana tena uwezo wa kufikiri vizuri.

Ni watu wenye wivu sana na mara nyingi wivu wao wa kimapenzi huwafanya kuleta vurugu au kusababisha machafuko ya wazi ya kiuhusiano. Lakini siku zote, baada ya vurugu hizo huhisi kushitakiwa na dhamira. Hujutia tabia zao za wivu lakini hawana uwezo wa kuzidhibiti kama wanavyoamini wao.

Kwenye uhusiano ukiacha wivu, ni waaminifu na wanyeyekevu kwa wapenzi wao. Wanafaa sana kuwa maafisa serikalini. Wauguzi na hata kufanya kazi za bustanini. Ni watu wazuti katika mashairi, muziki na sanaa kwa ujumla.

Kiafya ni watu wanaougua kirahisi maradhi yenye kuathiri koo, pua na mapafu pia. Kwa hiyo wantakiwa kuwa makini sana na mazingira ambayo yanaweza kudhuru koo, pua au mapafu yao. Vitu kama sigara, haviwafai watu waliozaliwa Mei

Sunday, October 18, 2009

KISA CHA SAIDI WA MBEKENYELA......!Nakumbuka alikuwa na kawaida ya kuja pale ofisini kwangu, maeneo ya mjini na kunisaidia shughuli za usafi na kumlipa ujira kidogo. Kama nilikuwa nataka kununua kitu nilikuwa namtuma. Ni kijana mchapa kazi kweli na mcheshi kupindukia.

Akiwa ni mzaliwa wa Lindi katika kijiji cha Mbekenyela, kijana huyu ambaye ningependa kumwita Saidi *{Sio jina lake halisi}hakubahatika kumuona mama yake. Anasimulia kuwa mama yake aliolewa akiwa na umri mdogo sana miaka 15 na mzee mmoja aliemzidi kwa miaka 50, aliolewa katika zile ndoa maarufu za Korosho. Ndoa ambazo hufanyika sana mara baada ya msimu wa korosho.

Anasema kuwa kule kwao Lindi, kila baada ya msimu wa korosho wazee wengi ambao wana mashamba makubwa ya Korosho hukimbilia kuoa vibinti vidogo kwa kuwa wanazo fedha za mauzo ya Korosho, kuna wakati watoto wa kike hulazimika kuachishwa shule ili kuozeshwa kwa vibabu hivyo visivyoisha tamaa, na mara nyingi ndoa hizo huwa hazidumu kwani fedha zikiisha na ndoa huingia katika misukosuko na hatimaye kuvunjika kutokana na vizee hivyo kushindwa kumudu gharama za malezi ya wake wawili au hata watatu.

Hali hiyo imesababisha familia nyingi mkoani humo kuwa na vijukuu baada ya mama zao kuachika na kurudishwa nyumbani, hivyo kufanya hali ya maisha katika familia nyingi kuwa ngumu.

Mama yake Saidi alifariki wakati akijifungua, hivyo saidi hakumjua mama yake na hivyo kulelewa na bibi yake. Alipokuwa darasa la tatu babu yake alifariki, na maisha pale nyumbani yakawa magumu kweli. Saidi aliamua kwenda kwa baba yake aliyekuwa akiishi kijiji cha jirani, kule alikutana na mateso ya ajabu kutoka kwa mama zake wakambo na hivyo kulazimika kurudi kwa bibi yake mzaa mama.

Hata hivyo alijitahidi kuendelea na masomo, huku akifanya vibarua vya hapa na pale ili kumsaidia bibi yake ambaye alishakuwa mzee kujikimu. Alilazimika kuacha shule na kukimbilia mjini Lindi ili kujitafutia kipato. Alipofika mjini alikuwa akiishi stendi huku akifanya vibarua vya kubeba mizigo ya abiria na shughuli nyingine za kuosha magari ili mradi mkono uende kinywani.

Siku moja alipata wazo aje Jijini Dar, hiyo ni baada ya kusikia sifa nyingi kuhusiana na jiji hili, kwa kuwa alikuwa na vijisenti vyake alivyojiwekea alikata tiketi na kuja mjini. Alipofika awali alifikia pale ubungo stendi na kama ilivyokuwa Lindi alijishughulisha na shughuli zile zile za kubeba mizigo ya abiria na kuosha magari, baadae alihamishia shughuli zake maeneo ya Posta. Kati kati ya mji, na hapo ndipo nilipotokea kufahamiana naye.

Ni kijana mwenye heshima na muaminifu, siku moja kama kawaida yangu nilianza kumdadisi kwani kutokana na umri wake niliona alistahili kuwepo shuleni, na ndipo aliponisimulia historia ya maisha yake. Ukweli ni kwamba nilishikwa na huzuni sana na wakati ananisimulia kuna wakati nilijikuta nikitokwa na machozi kutokana na kuguswa na maisha magumu aliyoapitia.
Nikisema nisimulie historia yake yote, nitakuchosha wewe msomaji lakini kwa kifupi ni kwamba, Saidi alipitia maisha magumu sana, na yanayosikitisha na kuhuzunisha. Baada ya kusikiliza simulizi yake juu ya maisha yake, nilikata shauri nimsaidie. Nakumbuka kipindi cha nyuma kuna wakati nilikwenda kwa mama yangu mdogo anayeishi maeneo ya Kigogo, pale jirani na anapoishi nilimkuta kijana mmoja anafunga vifuko vya karatasi kwa kutumia unga wa ngano. Alikuwa akitengeneza vifuko vya saizi tofauti tofauti kulingana na matumizi na kisha kuviuza katika maduka ya dawa na wakati mwingine maduka ya kawaida na hata kwa wale wauza CD za muziki kwa ajili ya kufungia bidhaa zao.

Kutokana na udadisi wangu kama kawaida niliweza kuongea na yule kijana mtengeneza mifuko, na ikatokea tukazoeana sana, na hapo ndipo nikajifunza kutengeneza hiyo mifuko, ingawa sikujua kama najifunza ili iweje.

Baada ya kuongea na saidi nilipata wazo la kumfundisha ile kazi yakutengeneza mifuko ya karatasi, na baada ya kumweleza alifurahi sana. Kazi yenyewe haikuhitaji mtaji mkubwa, hivyo nilimpa kazi ya kupita katika maduka ya stationary na kuokota makaratasi na kisha aniletee. Na mimi nilipita pia kwenye maduka ya aina hiyo ambayo yalikuwa jirani na ofisi yangu na kuwaomba wawe wananihifadhia makaratasi wasiyoyatumia kwa kuwa nilikuwa na shida nayo, kwa kweli walinipa ushirikiano, kwani mpaka jioni nilikuwana lundo la makaratasi, naye Saidi kwa upande wake aliweza kukusanya makaratasi mengi sana, hatua ya kwanza ikawa imekamilika.

Tulipanga siku inayofuata ndio darasa letu lianze. Na siku iliyofuata nilinunua unga wangu wa ngano katika duka moja la jirani kule nyumbani kiasi cha kilo moja hivi, niliona hiyo ingetosha kuanzia, na nilipofika ofisini nilimkuta saidi ameshafika na kuanza shughuli zake za usafi kama kawaida, ila siku hiyo alikuwa ni mchangamfu sana. Baada ya kumaliza shughuli za usafi nilikaa naye na kuanza kumfundisha hatua kwa hatua mpaka akamudu kutengeneza mfuko, nilimuacha akiendelea kutengeneza mifuko yake na mimi nikawa naendelea na bishara zangu pale ofisini lakini nilikuwa naikagua kazi yake mara kwa mara na kuitoa makosa madogo madogo, na hatimaye alimudu.

Mpaka kufikia jioni alikuwa ametengeneza mifuko inayofikia mia sita ya saizi tofauti tofauti na huwezi kuamini ndugu msomaji, wateja alianza kuwapatia pale pale. Na huo ndio ukawa ndio mwanzo wa Saidi kuinuka.

Nililazimika kuibinafsisha ofisi yangu kwa kumuachia rafiki yangu aiendeshe na mimi kuhamia Arusha kwa muda katika kutekeleza majukumu ya kifamilia. Hivi karibuni nilitembelea ofisi yangu, nilipofika pale nilipata ujumbe kuwa Saidi ananitafuta sana na aliacha namba yake ili nikipita pale nimpigie, kwa kuwa sikuwa na simu rafiki yangu alimpigia na kumjulisha kuwa niko pale, Saidi aliniomba nimsubiri kwani alikuwa maeneo ya Kariakoo, niliamua kumsubiri kwa shauku ili kujua sababu ya kunitafuta.

Hata hivyo yule rafiki yang alinijulisha kwamba Saidi mambo yake sio mabaya kwani amenenepa na ana pesa sana simu hizi, kwanza simuamini nikajua ananitania. Haikupita muda Saidi alifika mahali pale, awali sikumjua kabisa mpaka alikiniita kwa jina langu huku akicheka kama kawaida yake. Alinieleza mengi kuhusu maisha yake, baada ya kuwa nimemuanzishia ile biashara. Aliniambia kuwa, ile biashara ilimnyookea na mpaka kufikia wakati ule alikuwa amemudu kufungua duka lake la kuuza CD maeneo ya Tandika na duka lingine la vitenge, khanga na vitambaa vya magauni hapo hapo Tandika pia ameoa na ana mtoto mmoja na amefanikiwa kununua shamba la eka mbili maneno ya Mkuranga, nilimdadisi kama ameanza ujenzi, akanijibu kuwa hajaanza bado lakini yuko kwenye harakati za kuanza, nilimuahidi kumnunulia mifuko kumi ya cement ili aweze kuanza hata msingi, alifurahi sana.

Akisimulia namna alivyomudu, anasema kuwa, kutokana na biashara hiyo ya mifuko kumpatia faida kubwa, rafiki yake mmoja alimshauri aweke fedha zake Saccos, ili akuze mtaji, alianza kuweka kila siku shilingi elfu kumi, na baada ya mwaka mmoja alikuwa amejikusanyia kiasi cha shilingi 3,650,000 kiasi ambacho hakuwahi kuota kuwa nacho.

Mpaka kufikia hapo alikuwa na uwezo wa kukopa shilingi milioni tisa na ushee, lakini hakuwa na dhamana kulingana na mkopo wa kiasi hicho, hivyo alianza na shilingi milioni moja ambapo alianza kwa kufungua biashara ya kuuza kanza na CD kule Tandika na baadae aliweza kuanzisha biashara nyingine ya kuuza vitenge na khanga hapo hapo Tandika. Hata hivyo Saidi anasema kwamba hajaacha biashara ya kuuza mifuko, anaendelea nayo kwani ndio iliyomuwezesha kufikia hapo alipo.

Nilizungumza na Saidi mambo mengi na kusema kweli alionekana kuwa na matarajio makubwa sana, hata mimi alinishangaza sana.

Mafanikio ya Saidi siwezi kujivunia kama sitamtaja yule kijana wa Kigogo ambaye ndiye aliyenifundisha kazi hiyo. Lakini kuna jambo moja najiuliza, hivi kuna watoto wangapi walioko mitaani leo wanaoshi katika mazingira magumu? Bila shaka ni wengi sana, Hivi si tunalo shirika letu la SIDO? Nazungumzia shirika la viwanda vidogovidogo. Hivi hawa wameshindwa kabisa kubuni miradi itakayowawezeka hawa vijana wa mitaani kujiajiri na kumudu maisha ya kujitegemea na hata kuchangia pato la Taifa badala ya kuiacha nguvu kazi hii ikipotea bure.
Tukumbuke kwamba hawa ndio kesho wana Graduate na kuwa vibaka na hata majambazi ambao huishia kupora na kudhulumu roho za watu. Watashindwaje kufanya hivyo ili hali tumewatelekeza watoto hawa. Jamii imewatelekeza, na hata serikali yao imewatelekeza, kwa nini tunakosa ubunifu.

Naomba tutafakari………….

Tuesday, October 13, 2009

HEBU TUTAFAKARI JUU YA KAULI HII!


Bado niko Dar, na huenda wiki ijayo nikarejea Arusha kuendelea na shughuli za kilimo.

Wakati tunaelekea kuadhimisha miaka kumi ya kifo cha muasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hapo kesho, leo nimeona niweke kipande hiki cha mazungumzo yake juu ya kuuvunja Muungano wakati alipokuwa akiongea na Klabu ya Waandishi wa habari Tanzania.

Zanzibar wanaweza wakajitenga hivi, kwa ujinga, kwa ulevi, lakini kwa ujinga, hasa wa viongozi wao. Wanaweza wakjitenga hivi na Watanganyika wakbaki wameduwaa tu. Lo! Wazanzibari hawa wamefanyaje? Wanatuacha wenzetu hawa: wanatuacha jamani! Wanakwenda zao wenzetu!” Wakawaacha Watanganyika wameduwaa hivi. Watanganyika walioachwa wameduwaa kwa kitendo cha wazanzibari kuwakimbia, watbaki wamoja, hawataparaganyika. Narudia, Wazanzibari wanaweza wakatoka wakajitenga wenyewe tu: “Wengine wan bendera sisi hatuna; wengine wan wimbo wa Taifa sisi hatuna. Kwa nini? “Basi halafu, watajitenga watawaacha Watanganyika wameduwaa. “Hivi kweli wenzetu wametuacha!”. Wakiwaacha Watanganyika katika hali hiyo. Watanganyika wanaowashangaa wazanzibari katika kuwaacha, Watanganyika hawa watakuwa Salama

Watanganyika wakiwakataa wazanzibari kwa tendo la dhambi ile ile ya “sisi Watanganyika”, “waoWazanzibari, wakautukuza “usisi Tanganyika” na, kwa ajili hiyo wakwafukuza wazanzibari , hawatabaki salama. Hapatakuwa na Tanganyika. Wakishakujitenga tu Watanganyika hawatabaki salama. Hapatakuwa na Tanganyika. Wakishajitenga tu, Wazanzibari wako kando hivi, mmewafukuza mnajidai wakubwa ninyi: “ hawa nani hawa, wao wan rais sisi hatuna raisi kwa nini? Watimuee” Mnawatimua. Mkampata Yelstin wenu hapa akawatimua. Hambaki. Kwani mtasemaje? Mtakuwa mmeshasema sababu ya kuwafanya ya “wale ni wao” na “ninyi ni ninyi” “wao” vipi wazanzibari; halafu mbaki ninyi?’.

Maana kama leo wapo kabila la wazanzibari, mmewabagua mtaanza vijumba vya wapemba, vipo vijumba vya wapemba humu. Basi watakimbia Wapemba. Baadhi yao wamo waliokimbia wakati ule wa zamani, Vijumba vya kwanza, mtasema ‘Wapemba, Wapemba’ mtamaliza za Wapemba halafu mtajikuta mliokuwa mnajiita ‘sisi Watanganyika’ mtakapoanza kuchoma nyumba za Wapemba. Mnazichoma moto zile, mnakuta eh! Sisi wote sio wamoja. Mbona za Wapemba tulizichoma moto, za Wachaga hatuchomi kwa nini? Maana Wachaga si wazawa bwana!Hapa kuna wazawa, sasamnachoma za Wapemba tu za Wachaga mnaacha..! Mtakuta hakuna watu wanitwa Watanganyika. Mtakuta mnajidanganya tu. Mnadhani kuan watu wanitwa Watanganyika. Hakuna! Kuna Wagogo, Wanyamwezi, Wasukuma,Wazanaki, Wakuria, Wamwera, eh! Wengi sanasiwezi kuwataja wote. Mtakuna hakuna hiki kitu kizima hivi kinaitwa ‘sisi Watanganyika’

Na madhali mmwfanya dhambi ya kusema ‘wao Wazanzibari’ si wenzetu, dhambi ile itawatafuna ninyi. Na mimi nasema, Mwenyezi Mungu anisamehe, mnastahili iwatafune. Hamwezi kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabuna adhabu zingine zimo mle mle ndani ya kitendo: hasisubiri. Kwa hiyo la kwanza nimesema tunao ufa wa muungano. Ufa wa kwanza kabisa’

Nimekiweka kipande hiki makusudi kutokana na hali jinsi ilivyokuwa tete kule Zanzibar, Serikali yetu kwa bahati mbaya imejitia hamnazo na inaonekana kupuuzia mgogoro ulioko pale kisiwani lakini kama kuna watabiri naomba watujuze, maana mie naona kabisa tunapoelekea si kuzuri hata kidogo, na litakalotokea pale kisiwani amini nawaambia huku Bara hatutakuwa salama hata kidogo, Tumeona wenzetu wameshaanza kulipuana kwa mabomu, tusijidanganye, vita hiyo itahamia huku, kwani moto mkubwa huanza na cheche ndogo sana.

Mimi naona kabisa kuna dalili za wazi za Rais Kikwete kufunika komba ili mwanaharamu apite, yaani amalize kipindi chake cha uongozi akajipumzishe zake huko Msoga, ili hilo balaa limuangukie mwingine. Hivi viongozi wetu walijisikiaje Rais wa Marekani Barack Obama alipotunukiwa Tunzo ya amani ya Nobel, si ni kutokana na juhudi za kuleta amani, kwanini sisi tunashindwa jambo hili? Tukumbuke kuwa kama ikitokea vita wenzetu hawa wanauwezo wa kukimbilia katika nchi zenye usalama na familia zao na kutuachia sisi balaa huku nyuma, kama tulivyoona huko Somalia, Sudan na kwingineko, wale wanaopiganisha vita katika nchi hizo familia zao ziko salama kabisa katika nchi za ugenini, zikiishi maisha ya kifahari na wengine wakiwa humu humu nchini. Wanaokufa kule ni masikini na familia zao ambao hawana masilahi kabisa na vita hivyo.

Naona sasa wakati umefika kwa wananchi wa kada mbalimbali, wasomi na viongozi wa dini kukutana kwa pamoja na kuiambia serikali, sasa imetosha, tunahitaji amani ya kudumu kisiwani pale, na kama wameshindwa basi waondoke waje viongozi makini na wenye uwezo wa kumaliza mgogoro ule.

Akilihutubia Bunge mara baada ya kupata ushindi wa kishindo, Raisi Kikwete alitoa ahadi kem kem ikiwemo hii ya kumaliza mgogoro wa kisiasa kule Zanzibar. Leo miaka mitano imepita hatuoni juhudi zozote makini za kumaliza mgogoro ule, zimebaki porojo tu,…. Hivi kwa nini lakini!!!!!????

Thursday, October 8, 2009

TUMESHINDWA KUANDIKA HISTORIA YETU WENYEWE?


Hivi karibuni niliomba msaada hapa katika kibarazani, nikiomba kuelekezwa mahali vinapopatikana vitabu mbalimbali vilivyokuwa vikitumika mashuleni miaka ya 1980.

Kutokana na ushirikiano mzuri wa wasomaji wa kibaraza hiki na wanablog wenzangu, nilielekezwa maeneo kadhaa ambapo niliambiwa nikajaribu huko, kwamba huenda nikavipata vitabu hivyo.

Ukweli ni kwamba sijavipata vitabu hivyo, lakini katika juhudi zangu za kutafuta vitabu hivyo nilipita katika taasisi ya kiswahili pale chuo kikuu mlimani {TUKI} na katika jengo la Quality Plaza lililoko Nyerere Road, pale kuna duka moja, nadhani linaitwa Mkuki na Nyota kama sikosei.
Nilikutana na vitabu vingi sana katika maeneo hayo, kwa mfano katika duka la vitabu lililopo pale Quality Plaza, nilikutana na vitabu vya elfu lela ulela, visa vya Sindbad baharia, na vingine vingi tu, hivyo hivyo pale Mlimani nilikutana na kazi nyingi za tafiti zinazozungumzia historia za makabila yetu, mila desturi na historia ya nchi yetu, bara la Afrika kwa ujumla na kadhalika na kadhalika.

Nilivutiwa na vitabu kadhaa ambavyo nilivinunua, lakini kilichonishangaza sana ni kukuta vitabu vingi vinavyoelezeza historia ya nchi yetu, makabila yetu na hata mila na desturi zetu vimetungwa na Wazungu.

Yaani nilishangaa sana kuona kwamba wazungu ndio wanaotufahamu zaidi kuliko sisi wenyewe. Pamoja na kuwa na wasomi wengi tena wa kutosha, lakini bado tumeshindwa kuandika historia ya nchi yetu, makabila yetu na mila na desturi zetu mpaka wazungu waje watuandikie?

Ina maana maisha ya mkazi wa pale Rufiji au Kipatimo kule Kilwa anayajua mzungiu kuliko Mtanzania mwenyewe? Au maisha ya mkazi wa kule Katerero Bukoba, Ruhuwiko Songea, Manyoni Singida, Mlima Kilimanjaro kule Moshi, Kyela kule Mbeya, au Kibaigwa kule Dodoma, wasomi wetu wameshindwa kufanya tafiti za makabila na mila na desturi za wakazi wa huko mpaka wazungu waje watusaidie kuandika?

Inashangaza kuona kuwa waliondika historia ya nchi yetu ni wazungu wengi sana ukilinganisha na sisi wenyewe.
Hata hivyo nilijaribu kumuuliza yule muuzaji wa vitabu na jibu lake lilikuwa ni rahisi sana, eti alidai kuwa wazungu wanazo fedha za kuendeshea tafiti mbalimbali ukilinganisha na sisi wenyewe. Ujinga gani huu..

Sina uhakika sana kama kilichoandikwa katika vitabu vyao kuwa ni sahihi kwani, habari zinazopendwa na hawa wenzetu ni zile zilizopotoshwa na kutiwa chumvi nyingi ili zivutie, hakuna habari inayohusu Bara la Afrika itakayoandikwa kwa usahihi kama ilivyo bila kutiwa chumvi. Lakini cha kushangaza huko mashuleni na vyuoni tunaambiwa tuvisome vitabu hivyo ili kuja kuvifanyia mitihani.
Hivi wasomi wetu wako wapi? Wanafanya nini? Na tafiti zao juu ya nchi yetu, makabila, mila na desturi zetu ziko wapi?

Friday, October 2, 2009

JE VITABU HIVI VINAPATIKANA WAPI?

Wasomaji wapendwa na wanablog wenzangu, baba yangu Mzee Mkundi anaomba msaada wa kutaka kujua vinapopatikana vitabu vya DARUBINI, yaani vile vitabu vilivyokuwa vimeandikwa UJINGA WA MUAFRIKA, anakumbuka baadhi ya hadithi zinazopatikana humo kama vile:

KAUTIPE NA UTUMBO WA KUKU

UREMBO WA NDONYA

KAWAMBWA NA KAPU LA KARANGA

CHAI YA DC

Pia anatafuta vitabu vya KISWAHILI vya darasa la nne, la tano na la sita, vya miaka ya 1980 anakumbuka hadithi zinazopatikana humo kama vile:

BROWN ASHIKA TAMA,

KAPULYA MDADISI

KIBANGA AMPIGA MKOLONI

MWEKA NADHIRI NA SHETANI

NUNDA MLA WATU

CHILUNDA APAMBANA NA CHUI

Mwenya kujua vinapopatikana vitabu hivi anijuze, baba anataka kuweka maktaba yake vizuri kwa ajili ya wajukuu zake………

Sunday, September 27, 2009

VUA NGUO NIKUPE UTAMU!!!!!!!!

Jamani hii sio falsafa ya kaka yangu Simon Mkodo wa Kitururu, kwa hiyo naomba msistushwe na kichwa cha habari hapo juu. Jana nikiwa nimejipumzisha nyumbani baada ya kutoka kanisani, niliamua kufungulia redio ili kusikiliza habari mbali mbali.

Nilipofunga redio nilikutana na kipindi cha watoto kilichokuwa kikirushwa hewani na Redio One, wakati huo ilikuwa ni wakati wa vitendawili, nilijikuta nikivutiwa na kile kipindi kwani kilinikumbusha enzi zile nikiwa mwanafunzi, nilitulia kwenye kiti na kusikiliza kipindi kile.

Mara mwanafunzi mmoja aliyetakiwa kutoa kitendawili chake akasema ‘Kitendawili’
Wenzake wakajibu ‘tega’, na ndipo akasema ‘Vua nguo nikupe utamu’
Yule mwendesha kipindi ambaye alikuwa ni miongoni mwa wale wanafunzi alimkata yule mwanafunzi kalma, na kumuonya yule mwanafunzi, kwa maneno yake mwenyewe alisema, ‘Jamani hivyo vitendawili haviruhusiwi, kwa nini huwaulizi wenzio, muwe mnawaelimisha wenzenu’

Akamchagua mwanfunzi mwingine na kipindi kikawa kinaendelea. Hata hivyo mimi bado nilibaki na swali, Je yule mwanafunzi alimaanisha nini katika kitendawili chake?
Kwa nini hakupewa nafasi ya japo kutoa jibu akiwa Off Air na kisha muongoza kipindi akatoa ufafanuzi? Je watoto walioko majumbani ambao walikuwa wakisikiliza kile kipindi watakuwa na picha gani juu ya kile kitendawili?

Unajua siku hizi kiswahili kimegeuzwa sana kiasi kwamba kila neno siku hizi limegeuka kuwa matusi.

Kwa kawaida watoto ni wadadisi sana na hicho kitendawili huenda watoto wengine waliokuwa kwenye kipindi na wale waliokuwa wakisikiliza majumbani mwao wamewauliza wazazi wao, na kwa bahati mbaya sana mwenye jibu la kitendawili kile alinyimwa haki ya kutoa jibu, Je wazazi watajibu nini?

Mpaka leo bado natafuta jibu la kitendawili kile, mwenye nalo anisaidie……

Saturday, September 19, 2009

HUYU NDIYE KAMALA LUTATINISIBWA

Kamala Lutatinisibwa,
Picha kwa hisani ya Blog ya Kijiwe cha Nyegerage.

Ni kijana wa kutoka kabila la Kihaya, na mzaliwa wa kule Bukoba mkoani Kagera. Alizaliwa miaka 28 iliyopita, tarehe 30 July.

Maisha yake ya udogoni hayakuwa mazuri sana kwani hakuwahi kufurahia upendo wa mama kwani inasemekana baba na mama walitengana mwaka mmoja tu baada ya yeye kuzaliwa akiwa ni mtoto wa mwisho hivyo akalelewa na bibi yake akishirikiana na shangazi zake kadhaa na binamu zake.

Binamu na baadhi ya ndugu alioishi nao kwa upendo na anaowakumbuka ni Jennifer Lukambuzi, Jovian na Elivida Binomutonzi, na dada yake Julieth na kaka yake Japhet ambao walikua pamoja wakicheza na kufurahia maisha ya utotoni. Alibatizwa tarehe 12/12/1982, rasmi bila ridhaa yake na kuwa mkirsto mfuasi wa ulutheri na kupewa jina la James.

Anakiri mwenyewe kuwa mpaka leo hajaweza kuelewa falsafa ya dhehebu hilo wala malengo yake na hivyo alibadili jina na kujiita Kamala Lutatinisibwa, na kubadili falsafa yake kutoka ile ya kimapokeo na kuhamia katika falsafa ya Spiritual yaani kujitambua.

Mwishoni mwa miaka ya 1980 kijana huyu akaanza shule ya awali maarufu kama vidudu au chekechea iliyokuwa ikimilikiwa na kanisa.

Anakiri kwamba hakuwa na mapenzi na shule hiyo ya awali kwani kuna wakati alikuwa akiishia njiani badala ya kwenda shuleni hivyo kuchapwa bakora kwa utoro. Alipokuwa darasa la tatu, alisomeshwa kipaimara na kuanza kula mkate kanisani ambao hujulikana kama kushiriki meza takatifu, ingawa hakuwahi kupenda kula mikate hiyo.

Kuna wakati alipenda mambo ya dini na kutaka kusomea uchungaji lakini baadaye alibadilisha uamuzi wake huo na kuamua kuishi kwa misingi ya falsaya ya Spiritual baada ya kuvutiwa na falsafa ya Budha na Osho.

Mnamo August 1, 1998 akiwa kidato cha pili kijana huyu alimpoteza baba yake mpendwa Omwami Ta Jasson Lutabwasibwa Kamala.

Baada ya kumaliza masomo yake ya Sekondari mnamo mwaka 2004 alihamia rasmi jijini Dar es salaam na kujiunga na vyuo mbalimbali ili kujifunza taaluma tofauti tofauti ambapo mpaka sasa ameweza kuwa mtaalamu wa Kompyuta, ingawa mwenyewe anakiri kuwa haipendi taaluma hiyo bali anapenda uandishi wa habari taaluma ambayo anaiendeleza kupitia kibaraza chake cha kublog akifundisha maarifa ya Utambuzi na stori za hapa na pale ili mradi maisha yanaendelea.

Ni mchangiaji mzuri katika blog za wengine ila msomaji asipokuwa makini anaweza kumuona kama mpotoshaj. Ni mkweli na hafichi kile anachokiamini bila kujali kama utakasirika au utafurahi.

Mara nyingi watu wasioelewa wanaweza kudhani labda ninapolumbana nae ninakuwa niko katika kiwango cha juu cha hasira, la hasha, ni katika kupendezesha mada husika na kuleta changamoto kuhusiana na mada hiyo.

Naomba nikiri kuwa Kamala ni mmoja kati ya wanablog ninaoheshimu sana misimamo yao, pamoja na kuonekana kuwa huwa natofautiana nae, lakini naomba nikiri kuwa sio kwamba nafanya hivyo kwa kuwa simpendi au sipendi misimamo yake. Ukweli ni kwamba napenda na ninaheshimu sana misimamo yake na maoni yake binafsi yawe ni mabaya au ni mazuri.

Hata hivyo naomba nikiri kuwa yapo mengi nimejifunza kutoka kwake na pia naamini kuwa

wasomaji wa blog hizi watakubaliana na mimi kuwa Kamala anao mchango mkubwa sana juu ya uwepo wa blog zetu kutokana na kutia hamasa kila achangiapo mada.

Naomba niishie hapa nisije nikatia chumvi sana na mchuzi ukachachuka.

Huyu ndiye Kamala Lutatinisibwa Omwami Ta Jasson Lutabwasibwa.

Bofya hapa kumsoma zaidi

Friday, September 18, 2009

SALAAM ZA MAKABILA YETU

Kijijini kwetu

Wasomaji wapendwa wa blog hii isiyoisha vituko, Kwa sasa niko jijini Dar es salaam nimerejea kimya kimya na leo nilikuwa najaribu kufanya utafiti wa lugha za makabila yetu hapa nchini. Kwa mujibu wa tafiti inasemekana kuna makabila zaidi ya 120 hapa nchini.Niliamua kuangalia zaidi salaam, hususan za asubuhi, Kutokana na utafiti wangu nimepitia makabila kadhaa na kukutana na maneno yanayotumiaka katika salaam za asubuhi ambayo yanafanana kidogo, hebu tuone maneno hayo ni yapi:


KINGONI: Uyimwiki = Habari za asubuhi

KIZIGUA: Kugona vihi = Habari za asubuhi

KINYAKYUSA: Ughonile = Habari za asubuhi

KIYAO: kwimukaga = Habari za asubuhi

KIPARE: Murevuka = Habari za asubuhi

KIUNGUJA: wambaje = Habari za asubuhi

KISAMBAA: Onga makeo = Habari za asubuhi

KIANGAZA: Mwalamtse = Habari za asubuhi

KINYAMWEZI: Mwangaluka = Habari za asubuhi

KICHAGA: Shimbonyi = Habari za asubuhi

KIMERU: Konumbware = Habari za asubuhi

KIMASAI: Sopai = Habari za asubuhi

KISUKUMA: Mwadila = Habari za asubuhi

KIHEHE: Kamwene = Habari za asubuhi

KIBENA: Kamwene = Habari za asubuhi

KIKINGA: Ulamwihe = Habari za asubuhi

KINYIRAMBA: Ulalaliani = Habari za asubuhi

KIHAYA: Wabonaki = Habari za asubuhi


Kwa leo naishia hapa mwenye nyongeza anaweza kuongeza ili tujifunze pamoja.
Tukutane wakati ujao