Thursday, March 24, 2011

POLE DADA YASINTA KWA KUONDOKEWA NA DA’ MDOGO ASIFIWE

Asifiwe Ngonyani 26/11/1989-23/3/2011

Dada Yasinta,


Najua itakuwa ni vigumu kwako kusoma waraka huu kutokana na msiba mzito uliokupata, na ninaamini pia kuwa waraka wangu huu hutausoma kwa wakati, labda baada ya siku tatu nne hivi. Ingawa ninatamani sana kama ungeusoma leo sasa hivi, lakini hilo bado kwangu ni jambo la kufikirika, ninabaki kusema, labda, sijui au huenda, lakini naamini pia utanielewa japokuwa itakuwa ni too late.

Dada Naomba uamini kuwa msiba huu sio wakwako peke yako ni msiba wetu sote, yaani familia ya Mzee Ngonyani na ya Mzee Mkundi au pengine na Wanablog wote wa ndani na nje ya nchi.

Ni msiba wetu kwa sababu wengi wetu tulikufahamu wewe kupitia maandishi yako katika Blog ya Maisha na Mafanikio ambapo pia tukaifahamu familia yako na familia ya Mzee Ngonyani.

Umetushirikisha kwenye mambo yako mengi na hata yale yanayotokea katika familia yako, nakumbuka ulinijulisha juu ya ugonjwa wa mdogo wako Asifiwe mwanzoni tu nilipoanza kufahamiana na wewe mara baada ya kuanza kublog, mawasiliano yangu na wewe ya mara kwa mara yalitufanya tuwe karibu kiasi cha kutengeneza undugu. Umekuwa ni dada yangu mwema na umekuwa ukinifariji kwa kila jambo linalonitokea katika maisha yangu, tumekuwa tulishauriana kwa mambo mengi na kuwa karibu wakati wote.

Ingawa hatujawahi kuonana ana kwa ana, lakini ule ukaribu wetu umenifanya nijihisi kama tumeshawahi kuonana, Nilimpenda marehemu Asifiwe kama nilivyokupenda wewe, na nilimuona kama mdogo wangu, nakumbuka wakati akiwa amelazwa pale Muhimbili mwaka jana, nilikuwa niko Arusha, lakini nilikuwa nawasiliana naye kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani mara kwa mara. Nilijikuta nikiwa naye karibu kama mdogo wangu wa tumbo moja.


Dada yangu mpendwa, Ninavyoandika waraka huu, machozi yananilenga lenga kwa huzuni, kwa kuondokewa na mdogo wetu kipenzi Asifiwe. Ni mara nyingi tunapohudhuria misiba huwa wahubiri wanatufariji kwa mahubiri matamu kutoka katika vitabu vitakatifu, mahubiri hayo mara nyingi hutupa faraja na kukubaliana na yale yaliyotokea. Miongoni mwa wahubiri wa Kikristo hupenda sana kunukuu kitabu cha Ayubu katika Biblia, ambapo tunakumbushwa jinsi Ayubu alivyopitia mitihani migumu ambayo kwa kweli inatufanya tukubaliane na matakwa ya Mungu.

Kujadili kwa nini Asifiwe ametangulia akiwa na umri mdogo wa ubarubaru, ambapo alikuwa na matumaini ya kuendelea na elimu ili na yeye atimize ndoto zake itakuwa ni kumkufuru Mungu. Inatupasa tukubali kuwa Bwana aliumba, na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.

Nakuomba usikate tamaa, bado tupo sisi wadogo zako,dada zako na kaka zako na tutaendelea kushirikiana labda kuliko hapo kabla.


Mama yangu Namsifu Japhet Mkundi, Baba Mzee Japhet Mkundi, dada zangu, Rachel, Damari, Debra na kaka zangu pamoja na mdogo wetu Jarome wote wanakupa pole na wanaiombea familia ya Mzee Ngonyani iwe na ujasiri hasa katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa mdogo wetu Asifiwe.

Ni mimi mdogo wako


Koero Japhet Mkundi

PAMOJA NA MUNGU KUITENDEA FAMILIA YA MZEE NGONYANI MIUJIZA, ASIFIWE HATUNAYE TENA!


Mnamo siku ya Jumatano ya Machi 3, 2010, dada Yasinta aliweka makala pale kibarazani kwake akimshukuru Mungu kwa kuitendea familia yao miujiza.
Ni kweli Mungu aliitendea familia yao miujiza kwa kufanikisha upasuaji wa moyo wa mdogo wake Asifiwe pichani hapo juu. Walihangaika sana kutafuta tiba ya mdogo wake na hatimaye walijikuta wakiwa Muhimbili ambapo alitakiwa kufanyiwa upasuaji huo.
Ni katika kipindi hicho niliwasiliana sana na Yasinta pamoja na Asifiwe mwenyewe ambaye leo nimepata taarifa za kustusha na kusikitisha kuwa hatunaye tena.
Nimeona niweke makala hii ya dada Yasinta hapa kibarazani kwangu kama kumbukumbu ya msiba huu mzito ambao kwa kweli umeniacha mdomo wazi.


AHSANTE MUNGU KWA KUITENDEA FAMILIA YA MZEE NGONYANI MIUJIZA

Nakumbuka mwaka 1996, kuna tukio la kushangaza kidogo lililotokea katika tasnia ya Michezo kule nchini Italia na kuushangaza ulimwengu.
Tukio hilo lilimtokea mchezaji wa Kimataifa aitwae Nnwanko Kanu. Huyu alikuwa ni mchezaji wa Timu ya taifa ya Nigeria, ambaye alikuwa akichezea timu ya Ajax ya Uholanzi.

Ni baada ya Kuiwezesha nchi yake kutwaa kombe la Olympic, hapo mnamo mwaka 1996, ndipo alipopanda kilele cha mafanikio na kununuliwa na timu maarufu ya kule Italia inayoshiriki ligi ngumu ya almaarufu kama Serial A.

Mchezaji huyu alinunuliwa na timu ya Inter Milan na ni wakati alipokuwa akifanyiwa vipimo vya afya,(Medical Check Up) ndipo matokeo ya vipimo hivyo vilipoushangaza ulimwengu. Nnwanko Kanu aligundulika kuwa na matatizo ya moyo na alitakiwa kufanyiwa upasuaji haraka sana ili kunusuru afya yake.

Ikumbukwe kuwa mchezaji huyo tayari alikuwa akishiriki ligi za kimataifa, akichezea timu ya Ajax ya Uholanzi pamoja na kuchezea timu yake ya Taifa ya Nigeria na kuiwezesha kutwa kombe la Olympic, lakini katika kipindi chote hicho haikuwahi kugundulika kuwa na tatizo hilo. Hata hivyo kulikuwa na kupingana kwingi kitaalamu kati ya madaktari wagunduzi wa tatizo hilo na wale wa Uholanzi, lakini hatimaye alifanyiwa upasuaji na kurejea katika anga za michezo na kupata mafanikio makubwa.

Nimelikumbuka tukio hili kutokana na kile kilichomtokea mdogo wangu Asifiwe, huyu ni mdogo wetu wa mwisho kuzaliwa. Tukiwa tumezaliwa wanaume watano na wanawake wawili, yaani kati ya watoto saba wa Mzee Ngonyani na mama Ngonyani tuko watoto wakike wawili tu, yaani mimi na huyu mdogo wangu Asifiwe.

Akiwa darasa la sita ndipo alipoanza kuugua, ghafla, na tatizo kubwa lililokuwa likimsumbua ilikuwa ni tatizo la kukosa nguvu ghafla na kubanwa na kifua, lilikuwa ni tatizo ambalo kule Songea katika Hospitali ya Peramiho hawakuweza kugundua kuwa ni tatizo gani lakini kwa juhudi za madaktari aliweza kupewa tiba ambayo hata hivyo ilimletea nafuu badala ya kumponyesha.


Ni mwaka jana mwezi wa pili nilipokuwa nyumbani Tanzania ndipo nilipokata shauri tumpeleke katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya vipimo zaidi. Ni hapo ndipo tulipo shangawa na matokeo ya vipimo kuwa mdogo wetu Asifiwe anayo matatizo ya Moyo na anatakiwa kufanyiwa Upasuaji nchini India.

Naamini hata wewe unayesoma hapa unaweza kuhisi ni kwa kiasi gani nilikuwa naumia kwa kile kilichomtokea mdogo wetu.

Hata hivyo baada ya kushauriana na madakatari alipangiwa kuwa awe anakuja pale Muhimbili kwa ajili ya matibabu yaani kliniki huku mchakato wa kufanyiwa upasuaji nchini India ukiendelea.

Kwa hiyo akawa anakuja Muhimbili na kurudi Songea (Ruhuwiko). Lakini mara hii ya mwisho yaani mwezi wa kwanza mwaka huu alipofika Kliniki aliandikiwa kufanyiwa upasuaji hapa hapa nchini na hivyo kulazwa pale Muhimbilli akisubiri kufanyiwa upasuaji.

Ni katika kipindi hicho sala na maombi vilifanyika kumuomba mungu afanikishe upasuaji huo ili mdogo wetu apone na kurejea shule kuendelea na masomo.
Mnamo tarehe 16/02/2010 mdogo wetu Asifiwe alifanyiwa upasuaji wa moyo na kwa uwezo wa Mwenye Enzi Mungu upasuaji ulikwenda vizuri na ijumaa tarehe 27/02/2010 ametolewa nyuzi zake na tarehe 01/03/2010 jumatatu ameruhusiwa.

Leo napenda kumshukuru Mwenye Enzi Mungu, Madaktari, Manesi na watu wote kwa Juhudi zao katika kumuhudumia mdogo wetu Asifiwe, sisi tunasema kwamba kwa uwezo wake ameweza kuisimamia kazi hiyo ya madaktari na kufanikisha upasuaji huo.Pia shukrani nyingi sana kwa daktari Mrs. Mushi wa kule Peramiho yeye ndiye aliyetupa ushauri wa kumpeleka Asifiwe, Kwanza katika kliniki moja hapa Dar ya Dr. Johnson M. Lwakatare. na ndipo tukapata rufaa ya kwenda Muhimbili .

Sisi tunaamini ni mungu pekee kwa kupitia mikono ya madaktari wale pamoja na manesi ameweza kufanikisha upasuaji huo. Nakumbuka siku tatu kabla ya kufanyiwa upasuaji huo nilizungumza na mdogo wangu, na kwa huzuni alinijulisha kuwa watoto wawili wa kike ambao walitangulia kufanyiwa upasuaji kabla yake wamepoteza maisha, ni watoto ambao walikuwa wana umri wa chini ya miaka 10, na walihitaji bado kuishi lakini Mwenye Enzi Mungu aliwapenda zaidi, na hivyo kuwatwaa. Ila namsifu Asifiwe, yeye hakuwa mwoga isipokuwa hakupenda kama ingetokea bahati mbaya kutuacha sisi nduguze.

Tulifanya maombi kwenye simu na nilimpa moyo mdogo wetu kuwa yote tumuachie Mungu kwani tunaamini atatenda miujiza. Lakini hata hivyo upasuaji uliahirisha tena kutokana na ziara ya ghafla ya mheshimiwa Raisi Jakaya Kikwete alipotembela hapo hospitali ya Muhimbili kuzungumza na madaktari.

Leo hii kwa niaba ya familia ya mzee Ngonyani napenda kuchukua nafasi hii kusema Ahsante Mungu kwa kuitendea familia ya Mzee Ngonyani Muujiza, Pia ningependa kuwashukuru wote mliokuwa nasi katika sala, katika kutupa moyo wakati tulipokuwa na mawazo. Na shukrani nyingi zimfikie kaka yetu Ngonyani na mkewe wa pale Kinondoni Kinondoni Mkwajuni kwa kuwa karibu nasi wakimhudumia mdogo wetu katika kipindi chote alipokuwa akija kliniki na hata wakati wa kufanyiwa upasuaji. Ninawashukuru kwa kuwa walitumia muda wao mwingi kwenda na kurudi Muhimbili ili kuhakikisha mdogo wetu Asifiwe hajisikii mpweke.
Na pia napenda kumpongeza yeye mwenyewe Asifiwe kwa kutoonyesha uoga.

Wednesday, March 23, 2011

KWA HILI, WACHINA WANASTAHILI PONGEZI

Huwa tunawalaumu Wachina kutokana na bidhaa zao kuonekana hazina ubora lakini kwa upande wa Yebo Yebo nawafagilia, kwa mfano watoto hawa, wote wametinga Yebo Yebo na ambazo kwa kweli bei yake ni rahisi kuimudu hata kwa familia zenye kipato kidogo. Na zinasaidia sana kwa watoto kuchezea na kuepuka kuchomwa na miiba au kuingiwa na funza kwa wale wanaoishi maeneo yenye funza kama vile kule Sambaani Lushoto. Hapa watoto hawa wakiwa wamepozi kinamna
Na hapa wakifurahia MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA, ARI ZAIDI, NGUVU ZAIDI NA KASI ZAIDI……LOL

Saturday, March 19, 2011

UTABIRI LONGO LONGO!Aliyoyatabili Sheikh Yahaya 25/03 /2010 Haya hapa:Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mnajimu maarufu Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahaya Hussein, alisema

1......
.Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ataongezewa muda wa kuendelea na wadhifa huo.

2.......
Mchuano wa kugombea urais wa Zanzibar utakuwa na ushindani mkubwa kuliko miaka iliyopita.

3......
.Robo tatu ya wabunge walioko madarakani wataanguka na sura mpya zitakayoongezeka zitakuwa ni za wanawake.

4......
Hakutakuwa na uchaguzi mkuu kwa mwaka huu wala mpasuko ndani ya CCM.

5.....
.Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, ataendelea kushika wadhifa huo kwa kuwa nyota yake inang'aa vizuri.

6......
Viongozi wenye tuhuma kama Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, hawatang'aa kisiasa hadi mwaka 2015.

7......
Kutatokea harusi za viongozi pamoja na vifo vya watu maarufu, matatizo ya kifedha na kiuchumi, kulipuka kwa volcano, ukame na matetemeko ya ardhi.

8.....
(CCJ) kimetabiriwa kuwa hakitaweza kukibomoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kitendo cha viongozi wake wa muda kwenda kulilia kwenye kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kwamba sababu nyingine ya kukikwamisha ni jina walilolichagua.CCJ kingetumia jina la CCN.

CHANZO KILIKUWA: NIPASHE


Thursday, March 17, 2011

ETI NI MIPANGO YA MUNGU!?

Hivi ni mipango ya Mungu au ni kujitakia?

MJOMBA MASSAWE WA BUGURUNI ROZANA

Jana nilinunua Vocha hapa, nikavutiwa na Tangazo hili

Monday, March 14, 2011

BIASHARA KWELI NI MATANGAZO

Hii nimekutana nayo Jijini Arusha hivi karibuni!


Friday, March 4, 2011

Wednesday, March 2, 2011

KAKA MARKUS, UMESIKIA WENZETU WAMEWAKATAA BABA ZAO?


Kaka Markus Honorius Mpangala,

Kwanza shikamoo! Habari za siku,

Samahani sana kwa kutowasiliana na wewe kwa muda mrefu sana, kutokana na majukumu ya sasa. Majukumu hayo yananilazimisha mimi na ndugu zangu kuyabeba japo hali zetu kimaisha hazijatengemaa.

Kaka, nakuandikia waraka huu nikiwa natumia kibatari, kwa hiyo naomba usinilaumu kama utaona makosa ya herufi.

Kaka hali zetu ni mbaya sana! Kuna wakati mimi na ndugu zako wengine tunajiuliza ilikuwaje sisi kuzaliwa katika familia hii.

Ngoja nikukumbushe mazuri ya baba yetu mpendwa licha ya kumbukizi nyingine kutia simanzi. Baba yetu wa kutuzaa, ambaye alifariki miaka kumi na moja iliyopita (Mungu amrehemu) alitujengea misingi imara ya malezi na kutunza hazina zetu.

Baba alijaa upendo, aliona mengi na upendo wake kwetu ilibidi atutunzie hayo ili wanawe tunufaike. Kumbuka Baba alitunza mbuga za wanyama, madini, mito mabonde na milima, pia alihakikisha kuwa tunapata elimu bora kwa mustakabali wa maisha yetu na vizazi vyetu vijavyo. Yaani aliwakifikiria hadi wajukuu utadhani aliwaona au kujua watakuwa wangapi! Mweeeee!

Jamani, baba yetu mpendwa, alikuwa na uwezo mkubwa wa kuona mbali, kupambanua mambo na kutoa ushauri wa busara zilizotuongoza.

Kama ujuavyo katika mila zetu kuna wakati mtu anapoona umri umeenda huwa anaamua kupunguza majukumu yake ya kuongoza familia na kuteua mtoto mmoja mwenye kuonekana ana upeo na kwa kusaidiana na watoto wengine kubeba jukumu la kuongozi familia.

Mtoto huyu anakuwa ndiye kiongozi wa familia karibu kila kitu. Unakumbuka mzee mwenye mji akishachagua mtoto wa kuongoza familia hubaki mshauri. Basi hivyo ndiyo alivyofanya baba yetu.

Aliamua kupumzika na sio kupumzika tu, bali aliamua kurudi kijijini na kujishughulisha na kilimo, kwani aliwaacha baadhi ya vijana wake aliowaamini sana wamsaidie kuongoza familia yake.

Katika kipindi hicho pamoja na kuwa likuwa akiishi kijijini, lakini kaka na dada zetu wakubwa aliowapa jukumu la kuongoza familia walikuwa wakienda mara kwa mara kumuomba ushauri. Hata pale wasipofanya hivyo, akiona jambo limeenda kombo hakusita kulikemea hadharani.

Miaka kadhaa baadaye baba aliugua ghafla, pamoja na juhudi za matibabu ya hapa nchini na hata huko ughaibuni hayakufua dafu, baba alifariki dunia, huo ndio ukawa mwisho wake hapa duniani! Aah! Chozi linanitoka kaka yangu.

Baada ya kifo cha baba, ndugu zetu waliopewa mamlaka ya kuongoza familia yetu wakiongozwa na kiranja mkuu, walitutoa wasiwasi kuwa tusiwe na shaka kwani baba ametuachia misingi imara na familia hivyo haitatetereka.

Tulipewa ahadi kemkem, harara zikatushika kwamba aah! Mambo poa kabisa! Nakwambia tukajifariji, nyoyo zikapoa kwa matumaini ya kiongozi wa familia, maneno yake yalikuwa kama nyama ya ulimi, nasi tukahadaika. Maana tuliahidiwa hali bora za kimaisha, kumbe ilikuwa ghiliba.

Kaka tangu baba afariki, mambo yalibadilika, maadui zetu aliotutahadharisha baba kuwa macho nao tuliwaona wakipigana vikumbo kuja katika familia yetu na kumlaghai kiranja mkuu na ghafla tukaanza kuona wakikabidhiwa hazina zetu waziendesha na nyingine wakiuziwa kabisa.

Tunashuhudia hazina zetu zinavyotafunwa waziwazi, huku sisi wanafamilia tukibaki mikono mitupu, na tukithubutu kuhoji tunaambiwa kuwa tuna wivu wa kike, eti tule nyasi na hatujasoma.

Utaratibu aliotuachia marehemu baba ilikuwa imeamuliwa kuwa kila kiranja aliyeteuliwa kuongoza familia anatakiwa aongoze kwa miaka mitano kisha tunachagua kiranja mwingine na wasaidizi wake.

Yaani ilikuwa kuchagua kwa njia ya kugombea katika makundi, (baba aliruhusu katika familia kuwa na makundi mbalimbali na kila kundi lilitoa mwongozo wake kwa wanafamilia wa jinsi watakavyoongoza wakipewa ridhaa na wanafamilia)

Kutokana na utaratibu huo, tumejikuta tunayo makundi kadhaa lakini yenye nguvu ni mawili tu ambayo yalikuwa yamepania hasa mwaka uliopita kumuondoa kiranja mkuu na kundi lake kutokana kuiyumbisha familia na kutusababishia maisha magumu.

Mwaka jana kulikuwa na kitimtim, na ilibaki almanusura kiranja mkuu abwagwe, kama sio hila zao angengolewa. Lakini kaka hali imezidi kuwa mbaya sasa tumejikuta tunaogopa kuhoji na kuikemea hali hiyo kwa sababu tunatishiwa kuwa tutaivuruga familia na kusababisha machafuko.

Ninavyokuandikia waraka huu, kila kitu kimepanda bei, umeme wa mgao na hauna uhakika, halafu tunaambiwa kuwa kuna jamaa anatakiwa tumlipe fidia kwa kukatisha mkataba wa kutuuzia umeme, wakati mtu mwenyewe alirithi mkataba wa kilaghai kutoka kwa mtu mwingine aliyetutapeli awali na mpaka sasa shauri lake liko kwa mlao.

Mmmh! Kaka naona unataka kuniuliza huyu Mlao ni nani. Nisikilize kwanza, Mlao ni yule mtu anayesikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi. Haya naona umeelewa ila usicheke!

Kaka, wenzetu katika familia nyingine wameanza kuwashitukia viranja wao, kwa siku za hivi karibuni tumeshuhudia viranja hao wakizikimbia familia zao na kwenda uhamishoni baada ya wanafamilia kuwakataa hadharani.

Kama ulivyosikia walianza wanafamilia wa mzee Tusitusi, wao walimkataa kiranja wao hadharani kwa kuingia mitaani hadi akakimbilia uhamishoni kutokana na nguvu ya wanafamilia.

Nimeambiwa sababu kubwa ni kutokana na mkate kupanda bei, ukosefu wa mashamba ya kilimo na fursa za ajira kwa wale waliokwenda shule.

Baada ya tukio hilo la familia ya Mzee Tusitusi, wanafamilia wengine wa mzee Msisiri nao wakaja juu, kisa gharama za maisha zimepanda. Nao walichachamaa mpaka kiranja wao akakimbilia uhamishoni pia.

Kaka umesikia yaliyotokea kwa mzee Libelibe? Mmmh! Makubwa haya jamani! Wanafamilia wa mzee Libelibe familia yao ina neema za kila aina wakipewa kila kitu bure na kiranja wao, kama vile elimu, matibabu na huduma nyingine muhimu za kijamii, lakini wamemkataa kweupeee!!

Nao wameingia mitaani hawamtaki na wataka aondoke……, mmmh! lakini hata hivyo kiranja wao amewaua wanafamilia wengi kwa silaha za moto kwa sababu ya uasi, na amekuwa akisingizia kuwa uchochezi huo unatoka katika familia nyingine kitu ambacho si kweli kwa huyo kiranja wao kakaa muda mrefu katika uongozi wa familia takribani miaka 40, na sasa amechokwa.

Wakati wenzetu wakisema basi kwa viranja wao, sisi huku pamoja na hali ngumu ya maisha, na wizi wa waziwazi wa hazina zetu unaofanywa na kiranja wetu akishirikiana na wageni lakini sisi huku tunasema hewala baba.

Kaka hali inatisha, lakini nimeona wanafamilia wameanza kushtuka kama wanaibiwa na kutokana na kundi moja lililojaribu kugombea kushika hatamu za uongozi wa kuongoza familia likashindwa, Kwahiyo wanapita kwa wanafamilia kuwaelimisha na kuwaeleza kuwa kiranja anatupeleka kubaya, nimeona dalili za wanafamilia kuzinduka na siku si nyingi, tutashuhudia yanayotokea kwa majirani zetu.

Kaka kwa leo naomba niishie hapa

Nitakuandikia kwa kirefu wakati mwingine.