Thursday, March 24, 2011

PAMOJA NA MUNGU KUITENDEA FAMILIA YA MZEE NGONYANI MIUJIZA, ASIFIWE HATUNAYE TENA!


Mnamo siku ya Jumatano ya Machi 3, 2010, dada Yasinta aliweka makala pale kibarazani kwake akimshukuru Mungu kwa kuitendea familia yao miujiza.
Ni kweli Mungu aliitendea familia yao miujiza kwa kufanikisha upasuaji wa moyo wa mdogo wake Asifiwe pichani hapo juu. Walihangaika sana kutafuta tiba ya mdogo wake na hatimaye walijikuta wakiwa Muhimbili ambapo alitakiwa kufanyiwa upasuaji huo.
Ni katika kipindi hicho niliwasiliana sana na Yasinta pamoja na Asifiwe mwenyewe ambaye leo nimepata taarifa za kustusha na kusikitisha kuwa hatunaye tena.
Nimeona niweke makala hii ya dada Yasinta hapa kibarazani kwangu kama kumbukumbu ya msiba huu mzito ambao kwa kweli umeniacha mdomo wazi.


AHSANTE MUNGU KWA KUITENDEA FAMILIA YA MZEE NGONYANI MIUJIZA

Nakumbuka mwaka 1996, kuna tukio la kushangaza kidogo lililotokea katika tasnia ya Michezo kule nchini Italia na kuushangaza ulimwengu.
Tukio hilo lilimtokea mchezaji wa Kimataifa aitwae Nnwanko Kanu. Huyu alikuwa ni mchezaji wa Timu ya taifa ya Nigeria, ambaye alikuwa akichezea timu ya Ajax ya Uholanzi.

Ni baada ya Kuiwezesha nchi yake kutwaa kombe la Olympic, hapo mnamo mwaka 1996, ndipo alipopanda kilele cha mafanikio na kununuliwa na timu maarufu ya kule Italia inayoshiriki ligi ngumu ya almaarufu kama Serial A.

Mchezaji huyu alinunuliwa na timu ya Inter Milan na ni wakati alipokuwa akifanyiwa vipimo vya afya,(Medical Check Up) ndipo matokeo ya vipimo hivyo vilipoushangaza ulimwengu. Nnwanko Kanu aligundulika kuwa na matatizo ya moyo na alitakiwa kufanyiwa upasuaji haraka sana ili kunusuru afya yake.

Ikumbukwe kuwa mchezaji huyo tayari alikuwa akishiriki ligi za kimataifa, akichezea timu ya Ajax ya Uholanzi pamoja na kuchezea timu yake ya Taifa ya Nigeria na kuiwezesha kutwa kombe la Olympic, lakini katika kipindi chote hicho haikuwahi kugundulika kuwa na tatizo hilo. Hata hivyo kulikuwa na kupingana kwingi kitaalamu kati ya madaktari wagunduzi wa tatizo hilo na wale wa Uholanzi, lakini hatimaye alifanyiwa upasuaji na kurejea katika anga za michezo na kupata mafanikio makubwa.

Nimelikumbuka tukio hili kutokana na kile kilichomtokea mdogo wangu Asifiwe, huyu ni mdogo wetu wa mwisho kuzaliwa. Tukiwa tumezaliwa wanaume watano na wanawake wawili, yaani kati ya watoto saba wa Mzee Ngonyani na mama Ngonyani tuko watoto wakike wawili tu, yaani mimi na huyu mdogo wangu Asifiwe.

Akiwa darasa la sita ndipo alipoanza kuugua, ghafla, na tatizo kubwa lililokuwa likimsumbua ilikuwa ni tatizo la kukosa nguvu ghafla na kubanwa na kifua, lilikuwa ni tatizo ambalo kule Songea katika Hospitali ya Peramiho hawakuweza kugundua kuwa ni tatizo gani lakini kwa juhudi za madaktari aliweza kupewa tiba ambayo hata hivyo ilimletea nafuu badala ya kumponyesha.


Ni mwaka jana mwezi wa pili nilipokuwa nyumbani Tanzania ndipo nilipokata shauri tumpeleke katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya vipimo zaidi. Ni hapo ndipo tulipo shangawa na matokeo ya vipimo kuwa mdogo wetu Asifiwe anayo matatizo ya Moyo na anatakiwa kufanyiwa Upasuaji nchini India.

Naamini hata wewe unayesoma hapa unaweza kuhisi ni kwa kiasi gani nilikuwa naumia kwa kile kilichomtokea mdogo wetu.

Hata hivyo baada ya kushauriana na madakatari alipangiwa kuwa awe anakuja pale Muhimbili kwa ajili ya matibabu yaani kliniki huku mchakato wa kufanyiwa upasuaji nchini India ukiendelea.

Kwa hiyo akawa anakuja Muhimbili na kurudi Songea (Ruhuwiko). Lakini mara hii ya mwisho yaani mwezi wa kwanza mwaka huu alipofika Kliniki aliandikiwa kufanyiwa upasuaji hapa hapa nchini na hivyo kulazwa pale Muhimbilli akisubiri kufanyiwa upasuaji.

Ni katika kipindi hicho sala na maombi vilifanyika kumuomba mungu afanikishe upasuaji huo ili mdogo wetu apone na kurejea shule kuendelea na masomo.
Mnamo tarehe 16/02/2010 mdogo wetu Asifiwe alifanyiwa upasuaji wa moyo na kwa uwezo wa Mwenye Enzi Mungu upasuaji ulikwenda vizuri na ijumaa tarehe 27/02/2010 ametolewa nyuzi zake na tarehe 01/03/2010 jumatatu ameruhusiwa.

Leo napenda kumshukuru Mwenye Enzi Mungu, Madaktari, Manesi na watu wote kwa Juhudi zao katika kumuhudumia mdogo wetu Asifiwe, sisi tunasema kwamba kwa uwezo wake ameweza kuisimamia kazi hiyo ya madaktari na kufanikisha upasuaji huo.Pia shukrani nyingi sana kwa daktari Mrs. Mushi wa kule Peramiho yeye ndiye aliyetupa ushauri wa kumpeleka Asifiwe, Kwanza katika kliniki moja hapa Dar ya Dr. Johnson M. Lwakatare. na ndipo tukapata rufaa ya kwenda Muhimbili .

Sisi tunaamini ni mungu pekee kwa kupitia mikono ya madaktari wale pamoja na manesi ameweza kufanikisha upasuaji huo. Nakumbuka siku tatu kabla ya kufanyiwa upasuaji huo nilizungumza na mdogo wangu, na kwa huzuni alinijulisha kuwa watoto wawili wa kike ambao walitangulia kufanyiwa upasuaji kabla yake wamepoteza maisha, ni watoto ambao walikuwa wana umri wa chini ya miaka 10, na walihitaji bado kuishi lakini Mwenye Enzi Mungu aliwapenda zaidi, na hivyo kuwatwaa. Ila namsifu Asifiwe, yeye hakuwa mwoga isipokuwa hakupenda kama ingetokea bahati mbaya kutuacha sisi nduguze.

Tulifanya maombi kwenye simu na nilimpa moyo mdogo wetu kuwa yote tumuachie Mungu kwani tunaamini atatenda miujiza. Lakini hata hivyo upasuaji uliahirisha tena kutokana na ziara ya ghafla ya mheshimiwa Raisi Jakaya Kikwete alipotembela hapo hospitali ya Muhimbili kuzungumza na madaktari.

Leo hii kwa niaba ya familia ya mzee Ngonyani napenda kuchukua nafasi hii kusema Ahsante Mungu kwa kuitendea familia ya Mzee Ngonyani Muujiza, Pia ningependa kuwashukuru wote mliokuwa nasi katika sala, katika kutupa moyo wakati tulipokuwa na mawazo. Na shukrani nyingi zimfikie kaka yetu Ngonyani na mkewe wa pale Kinondoni Kinondoni Mkwajuni kwa kuwa karibu nasi wakimhudumia mdogo wetu katika kipindi chote alipokuwa akija kliniki na hata wakati wa kufanyiwa upasuaji. Ninawashukuru kwa kuwa walitumia muda wao mwingi kwenda na kurudi Muhimbili ili kuhakikisha mdogo wetu Asifiwe hajisikii mpweke.
Na pia napenda kumpongeza yeye mwenyewe Asifiwe kwa kutoonyesha uoga.

2 comments:

Fadhy Mtanga said...

ni vigumu kuamini.
Naiombea faraja familia ya Ngonyani katika kipindi hiki kigumu.

Pia namwomba Mwenyezi Mungu aipokee roho ya Asifiwe na kuihifadhi pahala pema.

Amen.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Hizi ni habari mbaya sana.

Mungu Akupumzishe salama Asifiwe kwani umetangulia tu. Na poleni sana wafiwa. Mungu Awashike mkono na kuwatia nguvu katika kipindi hiki kigumu.