Monday, March 30, 2009

KUTANA NA YASINTA, MJASIRIAMALI ALIYESEMA HAPANA KWA WANAUME WAKWARE

Nusura niwe mtoto wa mitaani

Juzi ijumaa nikiwa ofisini kwangu alipita binti mmoja akiwa na begi lake dogo kama yale yanayotumiwa na wanaume kubebea Lap Top.

Alinisalimia kwa uchangamfu na kujitambulisha kwangu kuwa anitwa Yasinta. Alionekana kuwa mchangamfu utadhani tunafahamiana siku nyingi, hata hivyo na mimi nilimchangamkia pia. Kumbe Yasinta ni mfanyabiashara wa kuuza viungo mbalimbali kama vile vya Pilau, viungo vya Chai, kwa kweli sikujua kama chai nayo ina viungo, pia alikuwa na viungo vya kupikia nyama , samaki au hata kuku na hasa kuku wa kienyeji na alitumia muda huo kunifundisha namna ya kutumia. Kwangu mimi hayo yalikuwa ni mapinduzi makubwa katika mapishi ya vyakula vya kiswahili

Yasinta Alionekana kuwa ni mdogo kiumri yaani ukimuangalia kwa haraka haraka anaonekana kuwa na umri wa kama miaka 18, hata hivyo sikukosea sana kwani nilipoomuliza umri wake aliniambi kuwa ana umri wa miaka 19 na mwishoni mwa mwaka huu ndio atatimiza umri wa miaka 20. Mara akaja jirani yangu mmoja ambaye ofisi zetu zinafuatana, alipomuona Yasinta alimshangilia sana na kuwaita wenzake na kuwajulisha ujio wa Yasinta, nilibaki nimeduwaa.

Baadae niliambiwa kuwa Yasinta alikuwa ni maarufu sana pale kwani alikuwa akiwauzia viungo vya mbalimbali na hivyo kufurahia mlo wao wa siku. Waliniambia kuwa walimfahamu Yasinta takribani miaka mitano iliyopita tangu alipoanza kuwapitishia ile biashara, wakati huo akiwa ni binti mdogo sana kwa umbo na umri.

Ni mwaka jana mwishoni alipowaaga kuwa anatarajia kufunga ndoa, na walimchangia fedha na zawadi nyingine. Tangu wakati huo Yasinta hakuonekana mpaka wakadhani labda ameamua kuachana na biashara hiyo, au mumewe amemkataza kuendele nayo.
Nilinunua viungo mbali mbali na niliamua kutumia fursa hiyo kufanya mazungumzo nae.
Yasinta alianza biashara hiyo mnamo mwaka 2005 Mara baada ya kumaliza darasa la saba mkoani Mbeya.

Je alifikaje mjini?

Yasinta alikuja mjini mwaka 2004 akiwa ndio amemaliza darasa la saba, baada ya kuwa hakufaulu na mama yake kutokuwa na uwezo wa kumuendeleza kielimu alichukuliwa na mama mmoja aliyekuwa akiishi maeneo ya Ilala hapa jijini Dar es salaam mwenyeji wa huko huko Mbeya ili kuja kufanya kazi za ndani.

Baba yake alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu wakati alipokuwa darasa la nne na kuanzia hapo majukumu ya kutunza familia aliyabeba mama yake pekee. Akiwa ni wa kwanza kuzaliwa na binti pekee kwa wazazi wake huku akifuatiwa na na wadogo zake wawili wa kiume, hakuwa na jinsi ilibidi aje mjini kufanya kazi za ndani ili aweze kumsaidia mama yake kuwatunza wadogo zake.

Alidumu na yule mama kwa mwaka mmoja. Lakini kutokana na mateso ilibidi atoroke na kujikuta akishia mtaani. Siku moja katika mizunguko yake ya kutafuta kazi alikutana na mabinti wa umri wake ambao walikuwa wakijiuza maeneo ya Buguruni na walimtaka ajiunge nao ili kujitafutia kipato, na walimuhakikishia kuwa shughuli ile ya kujiuza ina kipato kushinda hata ya kuajiriwa, hata hivyo Yasinta alikataa kata kata kujiunga nao, akamua kujichanganya na wale mama ntilie pale Buguruni CCM kwa kuwasaidia ili kujipatia kipato, hata hivyo mama mmoja allijitolea kumpa hifadhi.

Siku moja akiwa katika shughuli zake kama kawaida, alipita mama mmoja na kuagiza chakula, wakati akimuhudumia na kwa kuwa alikuwa ndie mteja pekee kwa wakati huo alianza kuzungumza nae. Katika mazungumzo yao yule mama alimjulisha juu ya biashara ya Viungo, mbalimbali vya mapishi ambayo ndio aliyokuwa akiifanya. Yasinta alivutiwa sana na ile biashara na kwa kuamini kuwa ule ulikuwa ndio wakati wa kuondokana na kazi za kutumwa, alimuomba yule mama amfundishe namna ya kufanya ile biashara.

Kwa bahati nzuri yule mama alimkubalia na na kuahidi kumpitia kesho ili wafuatane nae ili akamuoneshe mahali anaponunulia na kumuonesha namna ya kutayarisha.
Na kweli yule mama alimpitia kesho yake. Yasinta alimuaga yule mama aliyempokea pale Buguruni na kuondoka na yule mama kuelekea Kariakoo kufanya manunuzi.
Yule mama alijitolea kumpa hifadhi ya muda nyumbani kwake maeneo ya Vingunguti na kumfundisha namna ya kutengeneza viungo mbali mbali, Kutokakna na bidii aliyonayo ilimchukua Kiasi cha mwezi mmoja Yasinta kufudhu mafunzo hayo.

Yule mama alimkopesha Yasinta mtaji wa shilingi elfu kumi wa kuanzia.

Yasinta anakiri kuwa awali alikuwa na wakati mgumu sana kutokana na biashara kuwa ngumu lakini yule mama alimpa moyo wa subira.
Haikuchukuwa muda mrefu hali ilibadilika na biashara kumnyookea na kuweza kulipa mkopo aliokopeshwa na yule mama yake mlezi ambaye alimfanya kama mama yake mzazi kutokana na kumlea. Ilimchukuwa mwaka mmoja Yasinta kuhama na kupangisha chumba chake maeneo ya Buguruni na kuanza kujitegemea huku akiendelea na biashara yake hiyo ya viungo. Kuanzia hapo akawa anatuma hela kwa mama yake huko mbeya ili ziweze kumsaidia.

Mwaka mmoja baadae Yasinta alifanikiwa kununua kiwanja chenye ukubwa wa nusu eka maeneo ya Kinyerezi na ili iwe rahisi kwake kujenga. Ikabidi ahamie Segerea ili awe karibu na kiwanja chake. Taratibu alianza kujenga nyumba yake ya vyumba viwili. Ilimchukua mwaka mmoja na nusu kukamilisha nyumba yake ya vyumba viwili na kufanikiwa kuweka umeme na kuhamia nyumbani kwake. Lengo lake la kwanza likafanikiwa.

Yasinta alijiwekea malengo makuu matatu, wakati alipoanza biashara ya viungo.
Aliyataja malengo hayo kuwa ni kujenga nyumba yake mwenyewe, kukarabati nyumba ya mama yake kule Mbeya na kuwasomesha wadogo zake mpaka chuo kikuu.
Baada ya mdogo wake anayemfuatia kumaliza darasa la saba mwaka juzi akamleta na kumuandikisha katika shule ya sekondari ya binafsi iliyoko maeneo ya Ubungo na gharama za masomo analipa yeye kutokana na biashara yake ya viungo anayofanya.

Je Yasinta amemudu vipi kufikia hapo alipofikia na nini matarajio yake? Nilimuuliza.

Yasinta alikiri kuwa subira na uvumilivu ndio umemfikisha pale alipo sasa, kwani kuna wakati biashara ilikuwa haitoki kabisa mpaka anashindwa kulipa kodi ya nyumba, lakini kwa kuwa alikuwa amejiwekea malengo alihisi kuwa alikuwa na deni kubwa mbele yake na hiyo ilimpa hamasa ya kutokata tamaa na aliamini kuwa atafanikiwa.
Anasema aliponunua kiwanja alianza kuishi kwenye nyumayake kabla hata hajaijenga, kwani alikuwa akijiona kabisa kuwa amejenga na alikuwa akiiona nyumba yake ikiwa imekamilika kabisa, hakudhani kama atashindwa, aliamini tu kuwa ataweza.

Vipi kuhusu wanaume?
Nilimuuliza kwa kuwa yeye ni binti ambaye bado ni mbichi, kabla hajaolewa aliwezaje kukabiliana na vishawishi vya wanaume hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa akiishi peke yake na shughuli zake ni za kuzunguka maofisini?

Yasinta alikiri kuwa alikuwa akipata sana mitihani ya kutakwa na wanaume, wengine wakiwa ni wababa wazima wakuweza hata kumzaa mara tano lakini alikuwa amejiwekea nadhiri ya kutofanya mapenzi kabla ya ndoa, pia alikuwa amepanga kuwa hataolewa mpaka awe amejenga nyumba yake mwanyewe, kitu ambacho amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Je alimpataje Mwezi wake?
Yasinta alicheka kidogo, huku akiongea kwa aibu kidogo, alisema, “ Huyu mume niliyekuwa nae nilijuana nae miaka miwili iliyopita wakati akisoma sekondari wakti huo, tulikuwa tukikutana mara kwa mara kituoni tukisubiri usafiri wa daladala wa kwenda mjini. Kutokana na usafiri wa daladala Segerea kuwa ni mgumu tulikuwa tukigombea mabasi pamoja, siku moja akanilipia nauli, nilikataa kwa kuwa niliona kuwa yeye ni mwanafunzi, kwa hiyo haikuwa ni vyema anilipie nauli, lakini alisisitiza kunilipia na akakataa kupokea hela yake aliyomlipa kondakta wa daladala, na huo ukawa ndio mwanzo wa kufahamiana kwetu.
Baada ya kumaliza masomo alijunga na chuo kimoja mjini na kusomea mambo ya information Technology, na sasa ameajiriwa na kampuni moja binafsi akiwa ni mtaalamu wa kompyuta”.

Je mumeo anayo mikakati gani ya kukuendeleza kielimu, au ndio umeridhika na kiwango cha elimu ya darasa la saba ulicho nacho? Nilimuuliza.

Yasinta alisema kuwa ameanza kusoma masomo ya sekondari ya jioni katika shule moja ya binafsi iliyoko Tabata na ndio ameanza kidato cha kwanza ambapo itamchukua miaka miwili kumaliza kidato cha nne.

Ukweli ni kwamba nilifurahishwa sana na mazungmzo yangu na Yasinta, kwani ni miongoni mwa mabinti wachache hapa nchini wenye mtazamo chanya kuhusiana na maisha, na ameonesha kuwa, ukiamua unaweza, kwani hakuna kisichowezekana chini ya jua, kinachotakiwa ni kujiwekea malengo na kuwa na nia na dhamira ya kufikia malengo uliojiwekea. Kingine ni nidhamu katika kila jambo unalolifanya, kwani bila nidhamu hakuna kufanikiwa.

Hivi ni wasichana wangapi ambao wameshindwa kuendelea na masomo, na badala ya kujitafutia maendeleo kwa njia ya halali wamejikuta wakijiuza ili waweze kujikumu?
Ni wangapi wamekufa kwa ukumwi au wanaugua ukimwi sasa hivi baada ya kujiingiza katika vitendo vichafu vya kujiuza mwili?

Yasinta katuonesha njia kuwa tukiamua tunaweza.
Namtakia kila la heri katika ndoa yake, idumu na iwe na amani na upendo.

Wednesday, March 25, 2009

WENZETU WAMEWASHITUKIA SISI TUNAWAKARIBISHA

Wawekezaji wanaouza midoli
Soko la wahamiaji haramu wa kichina wanaoingia nchini Marekani linawaingizia mawakala wa biashara hii kiasi cha dola za Kimaekani bilioni 35 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa chapisho la Crime and illegal immigration lililotolewa hivi karibuni nchini Marekani imebainika kwamba mawakala hawa wa Kichina huingiza wahamiaji haramu wa Kichina kati ya 20,000 hadi 100,000 kwa mwaka, na kila mhamiaji anawajibika kuwalipa mawakala hawa haramu kati ya dola za Kimarekani 15,000 hadi 50,000 kama gharama ya kusafirishwa na kuingizwa nchini Marekani!

Wahamiaji hawa haramu hutakiwa kulipa malipo ya awali ambayo huweza kuwa robo au nusu ya malipo yote na kiasi kingine humaliziwa baada ya kufanikiwa kuingia nchini humo.
Chapisho hilo limelitaja jimbo la California kwamba ndilo lenye wahamiaji haramu wengi ukilinganisha na majimbo mengine.

Majimbo yanayofuatia ni Texas, New York, Florida na Illinois, Takwimu za hivi karbuni zinaonesha kwamba zaidi ya robo ya wahamiaji haramu wanaoishi nchini Marekani ni Wachina, ambapo inasemekana kuna wahamiaji haramu wapatao 1,321,000 wanaoishi nchini humo.

Jimbo la California lilitumia kiasi cha dola milioni 521 mwaka 1995 kuwaweka wahamiaji haramu gerezani, ambapo kiasi hicho kingeweza kujenga gereza lenye uwezo wa kuhifadhi wafungwa 2,300, kulipia gharama za askari wa doria wapatao 2,600, ambao wangeweza kufanya doria katika viunga vya California.

Baadhi ya wahamiaji haramu hujihusisha na vitendo vya uvunjaji wa sheria na hawa ndio wanaoigharimu serikali ya marekani. Ukweli ni kwamba waajiri wengi nchini Marekani wamenufaika sana na wahamiaji hawa haramu kwani huwafanyisha kazi kama vibarua kwa ujira mdogo sana ukilinganisha na ujira ambao wangemlipa raia wa Marekani.

Hivi sasa mawakala hawa wamegeukia nchi za Kiafrika ambazo zimefungua milango kwa wawekezaji, Tanzania ikiwamo. Mbinu wanazotumia ni kuwaleta kupitia makampuni ya ujenzi na wawekezaji wadogo wadogo, Yaani hata muuza duka pale Karakoo ni Mchina.

Siku hizi Wachina hawa wanamiliki biashara ndogo ndogo na magereji ya mitaani ambayo yamesambaa hadi mikoani. Wachina hawa wamepanga hadi uswahilini na tunaombana nao chumvi kila siku, na wote hawa hawakutumia njia sahihi kuingia hapa nchini, bidhaa zao ni feki na hata uwepo wao hapa nchini ni feki pia.

Monday, March 23, 2009

HIVI SISI TUMELISHWA NINI?

Tumegeuka taifa la wachuuzi

Nimesoma kwa makini mjadala uliowekwa na dada Yasinta uliokuwa na kichwa cha habari kisemacho MISHAHARA HAITOSHI TUACHE UZEMBE KAZINI Mjadala huo umezua maswali mengi kuliko majibu hasa kutokana na maoni ya mchangiaji wa kwanza mwanablog na mwanautambuzi Kamala kuja na hoja ya kupinga kile kilichosemwa na Yasinta, ambaye hata yeye amekiri kuwa mjadala huo aliutoa kwa Profesa Mbele aliyeuweka pale kibarazani kwake, baada ya kuwa umemvutia sana.

Mimi naamini kuwa kila mtu anayo haki ya kuzungumza kile anachokiamini ilimradi kusiwe na kuvunjiana heshima na kukashifiana, kama alivyowahi kusema kaka Bwaya wakati fulani kuwa kutofautiana ndio kujifunza. Kilichonishangaza ni kuona mjadala huu umeanza kupogoka na kupoteza mwelekeo kwa baadhi ya wachangiaji kushambuliana bila kujenga hoja.

Nimevutiwa sana na maoni ya kaka Mubelwa, kaka Bwaya na Profesa Mbele, Maoni yao yamedhihirisha kuwa ni watu waliokomaa hasa katika kujenga hoja na kuheshimu maoni ya wengine.

Hivi kuna tatizo gani kuiga yale ya wenzetu yanayoweza kutufaa kuharakisha ukuaji wa uchumi hapa nchini? Mimi siamini kuwa hilo ni tatizo.

Ikumbukwe kwamba sheria inayozungumziwa, inatekelezwa katika nchi ambazo zimeshaendelea na zimepiga hatua kubwa sana kimaendendeleo. Hizi ni nchi ambazo tunazipigia magoti kuomba misaada mbalimbali ya kijamii. Je kuna tatizo gani kuwaiga kwa ustawi wa maisha yetu wenyewe?

Nchi zote duniani ambazo watu wake wanamaisha bora, hazikupata mafanikio hayo kwa kutegemea wafadhili au kusubiri wawekezaji kutoka nje ili wananchi wake wageuzwe vibarua kwenye ardhi yao wenyewe.
Nchi hizo zimeweza kufika hapo zilipofikia kwa sababu wananchi wake waliamua kufanya kazi. Kila mtu alizalisha na mwisho wa siku kukawa na ziada.

Iwapo nguvu kazi katika jamii haitatumika ipasavyo, ina maana kwamba watu wachache watazalisha kwa ajili ya wale wavivu wasiozalisha. Ni vigumu nchi kujiletea maendeleo.
Inaonekana mawazo yetu wote yamefungiwa mahali, kiasi kwamba tumefika mwisho wa kufikiri kwetu. Hivi bado tunaendelea kujidanganya kuwa tutapiga hatua katika kujiletea maendeleo?

Maendeleo gani hayo tunayozungumzia, ikiwa tu kupendekeza kuhusu watu kukatwa mishahara wakichelewa makazini au kusingizia kuwa wanaumwa kunazua mjadala mkubwa mpaka watu kutishiana kutoana macho. Wanaotetea wananufaika na nini?
Hivi mnadhani ni kitu gani kilichopelekea yule mkuu wa wilaya kule Bukoba kuwacharaza waalimu bakora? Si haya yanayosemwa? Eti watu wanalipwa mishahara midogo. Sasa hiyo ndiyo ihalalishe watu kuwa wazembe?

Hata katika vitabu vya dini imesisitizwa sana kwamba kila mtu afanye kazi, katika Korani, kitabu cha kiislamu ipo aya inasema, “ Mkimaliza kuswali mtawanyike katika uso wa dunia ili kujitafutia ridhki” haikusemwa watu wakakae vijiweni na kupiga soga, na katika Biblia kuna andiko linasema “Asiyefanya kazi na asile chakula”

Kila mtu anapaswa kufanya kazi na kulipwa ujira kulingana na kazi yake, na kuna haja ya kutungwa sheria kali itakayomlazimu kila mtu kufanya kazi.
Kuna kundi kubwa la vijana limekaa bila kufanya kazi kutwa kwenye vituo vya mabasi wakivizia kuibia watu. Nguvu kazi inapotea bure, halafu tunapiga kelele kuwa kuwa nchi hii ni masikini. Mimi nasema umasikini uko vichwani mwetu, tukiweza kuuondoa, maendeleo ya uchumi yataonekana haraka sana.

Tusipotumia nguvu kazi yetu kwa kiwango chetu cha mwisho, tutakuwa tunapoteza muda bure, na tutaendelea kuwa watumwa wa wenzetu hadi mwisho.

Saturday, March 14, 2009

VIBINTI NA MIMBA ZA UTOTONI!

Hawa ndio waathirika wa wanaume wakware

Juzi nilikwenda hospitalini kuchunguza afya yangu, sikuwa naumwa bali nimejiwekea utaratibu wa kufanya hivyo mara kwa mara ili kuuhami mwili wangu dhidi ya maradhi, kwani preventive is better than cure.

Nilipofika pale hospitalini wakati nikisubiri kumuona daktari alipita binti mmoja nadhani alikuwa na umri kama sikosei wa miaka 14 hivi, na alikuwa ni mjamzito.
Ukimuangalia umbo lake na ule ujauzito aliokuwa nao utaona kabisa unamuelemea, kwani hakustahili kwa umri aliokuwa nao kuwa na ule ujauzito. Alikuwa ameongozana na mama mmoja mtu mzima ambaye nilipomuangalia niligundua kuwa ni mama wa binti huyo kutokana na kufanana sana na mwanae.

Nilipata bahati ya kuzungumza na yule mama na kutokana na udadisi wangu niligundua kuwa yule binti alikuwa amepata ujauzito ule pindi tu aliomaliza darasa la saba mwaka jana.
Masikini yule mama hakuwa na uwezo wa kumuendeleza binti yake hivyo aliungana na mwanae katika biashara zake za mama ntilie, na hapo ndipo alipokutana na wanaume wakware wakamjaza ujauzito, na kibaya zaidi aliyefanya hivyo hajulikani alipo, katoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Niliondoka pale Hospitalini nikiwa na mwaswali mengi sana, hasa nilikuwa nikijiuliza mustakabali wa yule binti. Je maisha yake yatakuwaje? Hivi kama huyo aliyempa ujauzito ni muathirika wa ugonjwa wa ukimwi, ni nini hatma na majaaliwa ya huyu binti?

Miongoni mwa mambo yenye kuwatesa sana wazazi ni mimba za utotoni zinazowakumba watoto wao wa kike. Lakini sio wazazi tu bali huwasumbua zaidi wasichana wenyewe. Ni kwa nini baadhi ya wasichana wanamudu kupita vizuri kwenye umri wa miaka 13 hadi 19 bila matatizo, wakati wengine hukabiliwa na misukosuko mingi sana ya kiuhusiano, ikiwemo kubakwa kutokana na tamaa, mimba za utotoni, mapenzi ya kabla ya ndoa, kukataa shule kutokana na kujikita katika mapenzi na mengine mengi?

Ni kwa sababu wazazi wengi na hasa wale wa kike wamekuwa mfano mbaya kwa watoto wao. Wamekuwa mfano mbaya kwa njia mbalimbali, kuanzia kauli, vitendo na mitindo mingine ya maisha wanayoendesha. Wazazi wengine wamekosa kabisa muda wa kujadili na watoto wao chochote kuhusu uhusiano na maisha kwa ujumla. Mtu akichunguza kwa makini atabaini kwamba, famili ambazo wazazi wako huru sana kwa watoto, ambazo wazazi hawana muda wa kukaa na watoto na kuwapa nafasi ya kusema hisia na matarajio yao, ndizo ambazo zinasumbuliwa sana na watoto wao kuwa huru katika mapenzi na hata mimba za utotoni.

Akina mama ambao huwa karibu na watoto wao wa kike na kuzungumza nao kwa upendo kuhusu ubaya wa tendo la ndoa kabla ya ndoa huwa saidia sana watoto hao wa kike. Kwa kuwaonesha kwamba wanachukia kitendo cha mtoto wa kike kushiriki tendo la ndoa kabla ya muda huwasaidia weatoto wao kumudu kuchelewa kujihusisha na tendo la ndoa.

Ni wajibu wa wazazi kuhakikisha kwamba wanawasaidia watoto wao wa kike kukua katika mazingira ambayo yatawasaidia watoto hao. Hatua ya awali kabisa katikakuwasaidia ni ile ya kujadili masuala mbalimbali ya uhusiano, lakini kuwa mfano bora kwao kuhusiana na mambo hayo.
Hilo linaposhindikana mzazi hapaswi kumlaumu binti yake ambaye amepata ujauzito kabla ya muda muafaka.

Mara nyingi nirahisi kulaumu, lakini makosa kwa kiwango kikubwa ni ya wazazi zaidi kuliko watoto. Wengi wetu tuko kama tulivyo leo kutokana na jinsi wazazi wetu walivyotulea. Tulisikia, kuona au kuambiwa nini na wao, kwani maisha tunayoishi kwa kiasi kikubwa yameakisi malezi tuliyopewa na wazazi wetu.

Mzazi anataka mtoto wake awe au aje kuwa mtu wa aina gani, ni uamuzi wa mzazi huyo na sio uamuzi wa mtoto. Kwa hiyo kila mzazi anapaswa kujua anachagua nini kuwa na mtoto wa aina gani?

Wednesday, March 11, 2009

KIZUNGUMKUTI CHA NJAA NA UMASIKINI DUNIANI

Linapokuja swala la njaa na umasikini, hawa ndio wahanga.

Nilipokuwa Arusha, nilibahatika kupitia chapisho moja linalozungumzia hali ya umasikini na njaa hapa duniani. Katika chapisho hilo nimekutana na takwimu mbali mbali juu ya ongezeko la njaa duniani huku kukiwa na tahadhari kadhaa ili nadhani Dunia ijipange katika kukabiliana na hali hiyo.

Kwa mujibu wa chapisho hilo dunia imetakiwa kuchukuwa tahadhari kwa kuwa kuna mamilioni ya watu sasa hivi hapa duniani wanakabiliwa na tatizo la njaa, miongoni mwa watu hao kuna zaidi ya watoto milioni 250 wenye umri wa kwenda shule na kati ya hao zaidi ya watoto milioni 10 wanakabiliwa na tatizo la uzito mdogo kutokana na ukosefu wa vitamini kwa sababu ya kula vyakula visivyo na virutubishso.

Chapisho hilo lilizidi kubainisha kwamba inakadiriwa kuwa kila mwaka watu milioni 13 hufa kutokana na njaa au kwa sababu ya kutopata vyakula vyenye virutubisho, na mamilioni ya watoto pia nao hufa kila mwaka kutokana na tatizo hilo.

Pia ilibainika kwamba kati ya watu wanaokadiriwa kufikia zaidi bilioni 6 hapa duniani watu bilioni 1 wanakabiliwa na tatizo la kumiliki ardhi na hata rasilimali. Watu hawa wanaishi kwa dola moja kwa siku.

Hata hivyo inakisiwa na wataalamu hao walioandika chapisho hilo kuwa mpaka kufikia mwaka 2010 kuna uwezekano wa idadi ya watu hapa duniani kufikia bilioni 7 iwapo dunia haitachukuwa tahadhari kupunguza idadi ya watu, kwa maana ya watu kuzaa kwa mpango.

Ni hapo ndipo niliposhikwa na mshangao. Wataalamu hawa wanalamika kuwa watu wanakufa kwa njaa hapa dunianai na hapo hapo wanataka watu wazae kwa mpango ili kuthibiti idadi ya watu isiongezeke!

Wataalamu hao walitoa sababu ya kutaka dunia idhibiti idadi ya watu, walidai kwamba ongezeko la watu huchangia kwa kiasi kikubwa umasikini hapa duniani, kwani kila idadi ya watu inavyozidi kuongezeka na ndivyo uharibifu wa mazingira unavyozidi. Kwani kwa jinsi idadi ya watu inavyozidi hapa duniani na ndivyo mahitaji ya ardhi kwa kilimo na makazi navyoongezeka. Na pale mahitaji ya chakula yanavyozidi kuongeeka na ndivyo uharibifu wa mazingira unavyozidi kuongezeka pia.

Kwa nini ichukuliwe tahadhari ya kupunguza idadi ya watu?

Wataalamu hawa wanadai kwamba Umasikini na njaa unachangia sana watu kuzaana kwa wingi, kwani familia masikini zinategemea watoto kwa ajili ya kulima na shughuli nyingine za nyumbani kama vile kuchota maji na labda kuchunga mifugo kama ipo. Pia familia hizi huchukuwa tahadhari ya kujihakikishia usalama pindi wazazi wakizeeka ili watoto wapate kuwatunza.

Kwa kuwa umasikini unagharimu maisha ya watoto wengi kutokana na kufariki wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano, familia hizi huzaa watoto wengi kwa matumaini kwamba iwapo wapo watakaokufa basi wapo watakaoishi hadi kufikia utu uzima. Kwa hiyo watoto huchukuliwa na familia masikini kama njia ya kujihakikishia usalama.

Wataalamu hao wanashauri kuwa ili kupunguza idadi ya watu hapa duniani, ni vyema kwanza kupunguza umasikini na njaa, kwani hiyo itasaidia watu kuwa na mazingira mazuri ya kiafya na elimu na moja kwa moja idadi ya vifo itapungua, kwa hiyo haitakuwa na haja tena ya mtu kuzaa watoto wengi kama ya tahadhari ya kugawana na vifo.

Wadau naomba kuwasilisha

Baadae nikipata muda nitaandika kuhusu athari za uharibifu wa mazingira kwa mujibu wa chapisho hilo.

Monday, March 9, 2009

VACATION YA ARUSHA NA USHAURI WA ASIMWE WENYE UTATA

Hizi ndizo habari zinazonifaa
Habari za siku wapenzi wasomaji wa blog hii.
Samahani kwa ukimya wa siku kadhaa uliyosababishwa na misukosuko ya hapa na pale ya kimaisha. Wapenzi wasomaji yaliyopita si ndwele bali tuganga yajayo.

Vacation yangu ya Arusha ilikuwa ni nzuri kwani ilinikutanisha na ndugu zangu niliokuwa nimepoteana nao kwa takribani miaka mitatu, na pia nilibahatika kutembelea urithi wetu yaani mbuga ya wanyama ya ngorongoro pamoja na vivutio kadhaa yote hiyo ilikuwa ni kuupa mwili raha na kutuliza akili.

Pamoja na kwamba nilikuwa na fursa ya mtandao lakini sikuwa na muda wa kukaa na kuandika kwani sikutaka kuchanganya mambo.
Katika kipindi hicho nilichokuwa Arusha nilibahatika kuzitambaulisha Blog zetu hizi kwa ndugu jamaa na marafiki na nilitumia muda mwingi kueleza faida ya blog kwani wengi niliozungumza nao walidhani kuwa kumiliki Blog ni ujasiriamali kwa maana kupata ujira.

Na nilipowaeleza kuwa hakuna ujira wowote unaopatikana, walinishangaa sana na kunihoji kuwa ina maana gani kupoteza muda wangu kwa kitu kisicho na mshiko.
Nilitumia muda mwingi kuwaeleza faida za blog mpaka wakanielewa.

Jioni moja nilikaa na binamu yangu mtandaoni aitwae Asimwe, nilikuwa namfundisha mambo mbali mbali kuhusiana na mtandao. Asimwe ndio amemaliza kidato cha sita na sasa anasubiri majibu ya mitihani kama atabahatika kujiunga na chuo kikuu kwani hiyo ndio ndoto yake.
Nilitumia muda huo kumuonesha mijadala mbalimbali niliyowahi kuiweka katika blog yangu pamoja na maoni ya wachangiaji mbalimbali waliowahi kuchangia. Pamoja na kwamba alifurahi kusoma mijadala yangu na pia kupitia blog za wanablog wengine ambao nimewaunganisha na blog yangu lakini alikuja na ushauri.

Asimwe alinitaka nibadili namna ya uandishi wangu wa blog, alidai kuwa hafurahishwi na mijadala yangu, kwamba imekaa kisiasa zaidi kitu ambacho si kizuri sana kwa umri niliokuwa nao, hata hivyo kuna maeneo alikubaliana na mimi kimtazamo lakini alinishauri nianze kuandika habari za urembo na hasa zinazohusiana na mashindano ya urembo na mavazi au hata habari za mapambo ya nyumba na bustani za maua kwani hizo ndio habari za maana ambazo zitapata wasomaji wengi hasa wanawake.
Alidai kuwa mijadala ninayoiandika inafaa zaidi kama ikiandikwa na wanaume.

Nilimsikiza kwa makini sana binamu yangu huyo ambaye pia ni rafiki yangu mkubwa. Ukweli ni kwamba sikumpa jibu la moja kwa moja bali nilimwambia anipe muda nifikirie kwani hayo mambo anayotaka niandike sio sababu ya kuanzishwa kwa Blog hii ya VUKANI.
Kwa hiyo inabidi niwasilishe ushauri huu kwa wasomaji wangu ili nao watoe maamuzi kama nibadilishe sera na kuanza kuandika habari za urembo kama nilivyoshauriwa?

Naomba kuwasilisha

Monday, March 2, 2009

ALITAKA KUATHIRI SELF-ESTEEM YANGU

Ilibidi nikajichimbie Ngorongoro ili kupumzisha akili

Mtafaruku ulionitokea kwa kutofautiana na mama yangu uliniacha na majeraha mengi kiasi cha kuathiri self-esteem yangu
Kwa mujibu wa tafsiri niliyoipata katika makala ya kaka Bwaya aliyoipa kichwa cha habari kisemacho
Self-Esteem: Ni muhimu kwa mwanao

Bwaya aliliezea neno Self-Esteem kuwa ni ni jumla ya imani ama hisia tunazokuwanazo kuhusu nafsi zetu, ama kule kujielewa kibinafsi. Namna tunavyojielewa, huathiri kwa kiasi kikubwa dhamira ama mitizamo tuliyonayo ama tabia zetu na hivyo huathiri namna tunavyoweza kukabiliana na hisia mbalimbali.Aliendelea kusema Self-Esteem (fikra-chanya) pia huweza kufafanuliwa kama muunganiko wa uwezo binafsi pamoja na zile hisia za kujisikia kupendwa anazokuwa nazo mtu. Kwa hiyo, mtoto anayefurahia mafanikio yake lakini hajisikii kupendwa huweza kuishia kushindwa kujiamini (low self-esteemed). Vivyo hivyo, mtoto anayejisikia kupendwa lakini bado ana mashaka na uwezo wake katika kufanya mambo fulani fulani , naye hali kadhalika huishia kuwa kama yule wa kwanza. Hatojiamini.

Hali hiyo iliyoelezewa na kaka Bwaya ndiyo iliyonikumba baada ya ule mtafaruku, kwani mama alianza kuhoji uwezo wangu wa kuendesha biashara niliyoianzisha na pia alijaribu kunishusha sana kielimu kuwa kama nitaendelea kukataa kuendelea na masomo na kutaka kujikita kwenye biashara basi sitafika mbali nitashindwa vibaya, kwa kuwa nina elimu ndogo.

Nadhani kila mmoja wetu anafahamu kuwa kauli za wazazi zina nguvu sana, kwani tumejengewa kuamini kuwa analolisema mzazi ndilo sahihi hasa kama linahusu mustakabali wetu. Mpaka leo sijui ujasiri wa kupingana na mama niliutoa wapi, maana hata dada zangu walinishangaa sana kubishana na mama kiasi kile. Hata hivyo walimlaumu mama kuwa, eti ni yeye amenidekeza kwa sababu ni mtoto wa mwisho kwa watoto wake wa kike nikiwa nimepishana sana na dada zangu kiumri.

Kitendo cha mama kunikatisha tamaa juu ya biashara zangu kilinifanya nijenge fikra HASI na kuanza kuhisi kuwa labda alikuwa sahihi, kuwa sitaweza kusimama kibiashara kama nilivyokuwa nikiamini, na kuona kuwa sitafanikiwa kufikia malengo yangu.
Nilijikuta nikiwa njia panda, nisijue ni nini cha kufanya. Na ndipo nilipopatwa na msongo wa mawazo.

Iibidi nianze kupata ushauri nasaha ili nirejee katika hali yangu ya kawaida, kwani nilishapoteza mwelekeo na kujikuta nikiwa sijiamini kabisa kiasi cha kutaka kukaa tu bila kufanya chochote, kwamba bora nipoteze vyote yaani biashara na shule.

Baada ya kupata ushauri nasaha na kurudi katika hali yangu ya kawaida ikabidi nisafiri kidogo kwenda Arusha kwa mjomba angu kupumzisha akili na kujitafuta upya.
Nashukuru sasa nimepona na naamini malengo yangu yatatimia baada ya mama kunikubalia niendelee na biashara zangu.

Ukweli ni kwamba matatizo wanayoyapata vijana wengi wa umri wa utineja ni kuwa na kiwango kidogo cha fikra chanya (Low Self esteem) na inachangiwa sana na aina ya malezi tunayoyapata kutoka ama kwa wazazi wetu au walezi, na wakati mwingine hata waalimu.

Kwa kawaida mtu mwenye kiwango kidogo cha fikra chanya anakuwa karibu sana na matatizo ya kisaikolojia, hebu chunguza vijana wanaotumia madawa ya kulevya, pombe kupita kiasi, waliojiingiza kwenye vitendo vya kiuhalifu, umalaya, wanaopata mimba za utotoni na wale wanaoshindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kutokuwa na uwezo darasani, wote hawa kuna uwezekano mkubwa wakawa wanakabiliwa na tatizo la kuwa na fikra hasi zilizopandikizwa na wazazi au watu walioko karibu nao.

Watu wenye fikra Chanya (Self esteem) wanakuwa na mchango mkubwa katika jamii iliyowazunguka, wanakuwa ni watu wanaojiamini na wepesi kuthubutu katika biashara hata kama inahatarisha mitaji yao.

Kwa hiyo kufanikiwa kwetu katika kufikia malengo yetu inategemea zaidi aina ya malezi tunayoyapata kutoka kwa wazazi na walezi wetu.