Saturday, March 14, 2009

VIBINTI NA MIMBA ZA UTOTONI!

Hawa ndio waathirika wa wanaume wakware

Juzi nilikwenda hospitalini kuchunguza afya yangu, sikuwa naumwa bali nimejiwekea utaratibu wa kufanya hivyo mara kwa mara ili kuuhami mwili wangu dhidi ya maradhi, kwani preventive is better than cure.

Nilipofika pale hospitalini wakati nikisubiri kumuona daktari alipita binti mmoja nadhani alikuwa na umri kama sikosei wa miaka 14 hivi, na alikuwa ni mjamzito.
Ukimuangalia umbo lake na ule ujauzito aliokuwa nao utaona kabisa unamuelemea, kwani hakustahili kwa umri aliokuwa nao kuwa na ule ujauzito. Alikuwa ameongozana na mama mmoja mtu mzima ambaye nilipomuangalia niligundua kuwa ni mama wa binti huyo kutokana na kufanana sana na mwanae.

Nilipata bahati ya kuzungumza na yule mama na kutokana na udadisi wangu niligundua kuwa yule binti alikuwa amepata ujauzito ule pindi tu aliomaliza darasa la saba mwaka jana.
Masikini yule mama hakuwa na uwezo wa kumuendeleza binti yake hivyo aliungana na mwanae katika biashara zake za mama ntilie, na hapo ndipo alipokutana na wanaume wakware wakamjaza ujauzito, na kibaya zaidi aliyefanya hivyo hajulikani alipo, katoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Niliondoka pale Hospitalini nikiwa na mwaswali mengi sana, hasa nilikuwa nikijiuliza mustakabali wa yule binti. Je maisha yake yatakuwaje? Hivi kama huyo aliyempa ujauzito ni muathirika wa ugonjwa wa ukimwi, ni nini hatma na majaaliwa ya huyu binti?

Miongoni mwa mambo yenye kuwatesa sana wazazi ni mimba za utotoni zinazowakumba watoto wao wa kike. Lakini sio wazazi tu bali huwasumbua zaidi wasichana wenyewe. Ni kwa nini baadhi ya wasichana wanamudu kupita vizuri kwenye umri wa miaka 13 hadi 19 bila matatizo, wakati wengine hukabiliwa na misukosuko mingi sana ya kiuhusiano, ikiwemo kubakwa kutokana na tamaa, mimba za utotoni, mapenzi ya kabla ya ndoa, kukataa shule kutokana na kujikita katika mapenzi na mengine mengi?

Ni kwa sababu wazazi wengi na hasa wale wa kike wamekuwa mfano mbaya kwa watoto wao. Wamekuwa mfano mbaya kwa njia mbalimbali, kuanzia kauli, vitendo na mitindo mingine ya maisha wanayoendesha. Wazazi wengine wamekosa kabisa muda wa kujadili na watoto wao chochote kuhusu uhusiano na maisha kwa ujumla. Mtu akichunguza kwa makini atabaini kwamba, famili ambazo wazazi wako huru sana kwa watoto, ambazo wazazi hawana muda wa kukaa na watoto na kuwapa nafasi ya kusema hisia na matarajio yao, ndizo ambazo zinasumbuliwa sana na watoto wao kuwa huru katika mapenzi na hata mimba za utotoni.

Akina mama ambao huwa karibu na watoto wao wa kike na kuzungumza nao kwa upendo kuhusu ubaya wa tendo la ndoa kabla ya ndoa huwa saidia sana watoto hao wa kike. Kwa kuwaonesha kwamba wanachukia kitendo cha mtoto wa kike kushiriki tendo la ndoa kabla ya muda huwasaidia weatoto wao kumudu kuchelewa kujihusisha na tendo la ndoa.

Ni wajibu wa wazazi kuhakikisha kwamba wanawasaidia watoto wao wa kike kukua katika mazingira ambayo yatawasaidia watoto hao. Hatua ya awali kabisa katikakuwasaidia ni ile ya kujadili masuala mbalimbali ya uhusiano, lakini kuwa mfano bora kwao kuhusiana na mambo hayo.
Hilo linaposhindikana mzazi hapaswi kumlaumu binti yake ambaye amepata ujauzito kabla ya muda muafaka.

Mara nyingi nirahisi kulaumu, lakini makosa kwa kiwango kikubwa ni ya wazazi zaidi kuliko watoto. Wengi wetu tuko kama tulivyo leo kutokana na jinsi wazazi wetu walivyotulea. Tulisikia, kuona au kuambiwa nini na wao, kwani maisha tunayoishi kwa kiasi kikubwa yameakisi malezi tuliyopewa na wazazi wetu.

Mzazi anataka mtoto wake awe au aje kuwa mtu wa aina gani, ni uamuzi wa mzazi huyo na sio uamuzi wa mtoto. Kwa hiyo kila mzazi anapaswa kujua anachagua nini kuwa na mtoto wa aina gani?

8 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nakubaliana nawe ni muhimu sana kwa kila mzazi kuchukua muda na kukaa china na kuongea na mtoto/watoto wetu. Haa kama ni dakika moja itasaidia kuliko kuwaacha wawe huru. Kwani mwisho wake ndio huo mimba na pia kutokuwa na adabu

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

wabongo mmnezowea kusikia mambo mmabaya. kwa nini unakwenda hosp? kwa sababu hujaambmiwa jambo baya kwamba unaumwa na inawezekana utakufa??

NATANIA, UKIMAINDI JIFUNGIE ULIE KISHA CHEKA SIKU ZIONGEZEKE!

ila uko sawa. sio kwa watoto wa kike tu bali wa kiume, wazazi vijana na kila mmoja. wote tunahitaji kujielewa na kujitambua vyema ili tuweze kuepuka sio mimba tu bali matokeo kibao ya kuongozwa ha hisia badala ya utu na fikra.

lazima tujitambue.
AMINA

Albert Kissima said...

Mtoto akikuzwa ktk mazingira ya kujielewa na kujiamini, atakuwa ktk nafasi nzuri sana ya kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali atakazokutana nazo ktk maisha zikiwemo mimba za utotoni hata na janga la ukimwi.

Kuna tatizo moja katika makuzi ya watoto.Mzazi/mlezi anafikiri kuwa mtoto akishakula,akivaa na akilala basi malezi ndio yanaishia hapo, kumbe mbali na hayo mtoto anatakiwa akuzwe kiakili na mambo mengine, hivyo elimu ya saikologia ni muhimu kwa wazazi/walezi.
Kati ya zawadi ya kipekee kabisa ya mzazi/mlezi kwa mtoto ni kumpa elimu ya kujitambua/kujielewa na kujiamini.

Kuna changamoto moja hapa, "kwa hali ya uchumi wa tanzania,wazazi wote wanalazimika kwenda kibaruani, watoto wanaachwa majumbani bila malezi ya wazazi" hili mwalionaje? Hakika ni tatizo,Nini suluhisho lake?

"jamii bila ukimwi inawezekana,tuanze na wazazi/walezi, wakuzeni watoto wenu ktk mazingira ya kujielewa na kujiamini"

Mzee wa Changamoto said...

Amani, Heshima na Upendo kwenu.
Da K asante kwa changamoto HALISI ya maisha yetu. Kikubwa kinachoonekana kuwakimbiza mabinti na hata vijana wadogo kwenye mahusiano ya ujanani ni kusaka "kijazio" cha furaha ambayo wanaikosa. Furaha ambayo wangestahili kuipata toka kwa watu wa karibu ambao wangestahili kuonesha wanawapenda, wanawajali na kuwasikiliza. Watu wanapokosa kutenda wale watendayo husababisha "madogo" hawa kukimbilia kusaka "raha na furaha" hizo nje ya nyumbani, nje ya ndugu na nje ya wale awafamuo na ambao mara nyingi huigiza kuwa na uwezo wa kuwajali na kuwapenda kuliko walivyowahi kudhania kuwa upendo upo na kisha kutumiwa saaaana na "waroho" hawa wa mapenzi. Tatizo ni kwamba kutumia kitu si lazima ukijali hasa ukitambua kuwa ni kwa kuwa kina shida na si wewe mwenye shida. Matokeo yake ni kuwa hakuna kumjali kwa afya wala mustakabali wake.
Na kwa vijana ama vibinti vidogo bado kale ka-imani kuwa "huyu ni mzima" kanakuwepo kutokana na kuonekana kama hajafanya saana mapenzi hivyo walafi wa ngono hufanya watakalo bila kujikinga wala kumkinga huyo kijana.
Na matokeo yake ni yale ambayo Koero umeyaona na pengine wengi wetu tumeshayashuhudia.
Wazazi nyumbani wamekosa upendo wa kweli kwa watoto. Kuna wanaodhani kuwa na mtoto ni kumvalisha, kumlisha, kumuandikisha shule anapotaka na kisha kusaidiwa kazi za nyumbani.

Kama kungekuwa na sensa tungeona ni wangapi wanapata muda wa kuwasikiliza wanawao na kuongea nao mazuri na mabaya ya ulimwengu. Ni wangapi wanakuwa kimbilio la awali pale watoto wao wanapokuwa na shida?
Ni wangapi wako huru kuongea hisia zao hata kama zinaweza kuwakwaza watoto wao lakini ni kwa manufaa ya watoto wao?
Ni wangapi wanaweza kukiri kuwa wamekosea katika baadhi ya maamuzi waliyowahi kufanya kwa watoto wao?
Ni wangapi wanaweza kuwaambia watoto wao kuwa tabia mbaya (addiction) walizonazo si njema na japo wanazo lakini ni vibaya kuwa nazo?
Ni wangapi wanaweza kuwaeleza watoto wao walivyoweza kujiepusha na tamaa za mwili?
Ni wangapi wanajiona kama vile wanaakisiwa maisha na tabia zao na watoto wao?

Na pengine mwisho wazazi wangejiuliza kama WANAJUA NAFASI YAO YA KUWAFANYA WATOTO WAO WAWE KAMA WATAKAVYOKUWA?
Baraka kwenu

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kissima kufanya kazi kwa baba na mama sio ugumu wa uchumi kama tunavyodhani ila ni pamoja na ujinga wa haki sawa kwamba kwa kuwa mume anafanyakaizi basi na mke afanye ili kuwa sawa na mke. tunasahau ukweli kwamba mama anahitajika zaidi kwa mtoto na kulea.

mzee wa chang.....
furaha ya kweli umeisahau. imo ndani mwetu. ni lazima tufundishwe jinsi ya kuipata ndipo mambo mengine yafuate.

baba / mama wasio na furaha ni vigumu nao kutoa furaha kwa watoto wao.

ngono ni muhimu na ni tamu endapo itafanyika kwa wakati muafaka na mazingira sahihi vinginevyo ni kifo na kusaga meno

Christian Bwaya said...

Ukitaka kumfaham vizuri mzazi, tizama wanae. Sababu anaowazaa ni kopi/taswira yake yeye mwenyewe.
Wawe wazuri ama wabaya kitabia, hicho ndicho kipimo cha malezi na hata tabia ya mzazi husika.

Tulivyo, ni tafsiri ya malezi ya wazazi wetu.

Leo hii mimba zimekuwa nyingi. Sababu hasa ni ngono inayoanzwa mapema mno siku hizi. Miaka 15 watoto wameshaunga msururu wa 'wapenzi' na wameachika mara kadhaa.

Yote haya kama ilivyoelezwa vizuri na Mubelwa na wachangiaji wengine, yanatokana na ukosefu wa mahusiano ya karibu katika ngazi ya familia.

Wazazi wanatafuta hela. Wako bize. Wanadhani inatosha kumpa mtoto mahitaji ya kimwili kama chakula, mavazi, malazi na shule za 'watakatifu'. Wanawaacha watoto wao kwa mahausigeli, ambao pamoja na kutokuwajua ndio wanageuka wahandisi wa tabia za mtoto. Wanasahau kuwa kulea ni project inayogharimu zaidi ya makaratasi yanayoitwa hela. Kulea ni pamoja na kujali mahitaji ya ki-hisia na ki-akili.

Matokeo yake, watoto hawajisikii kupendwa. Matokeo yake, watoto wanajikuta wakithamini watu wengine na yale wanayosema kuliko wazazi wao.
Kwa hiyo wanaamini zaidi taarifa potofu za marafiki-rika kuliko hata wazazi. Mzazi anaonekana mshamba hata kama anachosema ni ukweli. Lakini kwa sababu haaminiki, basi hata anachosema kinapuuzika kyepesi. Wanaonekana 'wanoko'.

Tufanyeje basi? Wazazi wawekeze kwa watoto. Wayachukulie malezi kama uwekezaji. Watumie muda mwingi na watoto tangu wakiwa wadogo. Haifai kuzaa na kumwachia hausigeli makujumu yako.
[Ulizaa ulee!]

Ni katika ukaribu huo, wajitahidi kujiaminisha kwa watoto wao. Waaminike kiasi kwamba hata wanachokisema kiaminiwe na watoto.

Vinginevyo, hata kama wangefundisha sana, bado wataonekana watu wasio na taarifa za kutosha waliopitwa na wakati.

Ikiwa hivyo, marafiki watachukua jukumu. Hiyo itamaanisha ngono kuwa kimbilio rahisi la kutafuta 'upendo'. Ikifikia hapo mimba si ajabu, na ikiwezekana na UKIMWI. Na wakulaumiwa ni mzazi aliyedhani hela ndio jibu la 'malezi' yote.

Simon Kitururu said...

Pamoja na yote tukumbuke tu kisaikolojia kuna miaka fulani watoto kibaiolojia ya mwili wanahasi au kuwa kichwa ngumu kutokana na homones na mambo mengi ya ukuaji.

Kifupi najaribu kusema kuwa;

Tusilaumu kupita kiasi wazazi na kusahau vikorombwezo vingine visivyo wazazi vichangiavyo toto dogo ghafla kujisikia kubwa na hata ukilipeleka kanisani badala ya kusikiliza mahubiri linavutiwa na matako ya yule muimbisha kwaya.

Na sasa hivi na hizi technolojia ambazo ni watoto wenye muda wakuzifahamu kuliko wazazi. Mzazi unaweza ukawa unashindana na blog ya VUKANI na video game isiyo VUKANI katika kumuelimisha mtoto wako umchungaye.

Come 'n See said...

kwa kweli hiyo swala la mimba za utotoni linakera. Nimekuwa nikisoma na kufuatilia kwa muda kidogo ripoti zinazotolewa kwenye vyombo vya habari juu ya mada hiyo. cha kushangaza sana hakuna mtu hata moja aliyoko kwenye nafasi za kutatua tatizo hiyo anatoa tamko kwa jinsi gani anavyokerwa na swali hiyo. wasemaji wamekuwa wakitoa tishio tu bila kutoa mwongozo juu ya nini kifanyike ili kunusuru watoto wa kike kutoka kwa tamaa za wanaume kujifurahisha nafasi zao bila hata basi kuchukua hatua za muhimu kama kuvaa kondomu au basi kama alishindwa kijikinga japo basi akubali jukumu la kulea mtoto na mama yake bila kusingizia kwamba ni aibu kwake kukubali lawama.
Aidha, mimi ninakubaliana na hoja ya wachangia mada wengine waliopendekeza wazazi na walezi wachukua muda na kuongea na watoto juu ya maswala ya ngono na ujinsia kwa udani.
Eti, sisi tunatumia muda mrefu sana tu kukaa kwenye vikao na kujadili au kutoa ushauri kutatua matatizo ya watu wengine lakini ya watoto tunalisahau.
Pia ingefaa basi hata hawa wenzetu wa serikali na NGOs basi waelimisha umma juu ya madhara, wajibu wa umma katika kutokomeza tabia hii ya kuwadanganya watoto wa kike au "explotating" shida na tamaa za watoto wa kike.
kama mtu ni mwanaume kweli basi si ajitose na kutongoza mwanamke anayelingana na shida yake za nyege.