Wednesday, March 11, 2009

KIZUNGUMKUTI CHA NJAA NA UMASIKINI DUNIANI

Linapokuja swala la njaa na umasikini, hawa ndio wahanga.

Nilipokuwa Arusha, nilibahatika kupitia chapisho moja linalozungumzia hali ya umasikini na njaa hapa duniani. Katika chapisho hilo nimekutana na takwimu mbali mbali juu ya ongezeko la njaa duniani huku kukiwa na tahadhari kadhaa ili nadhani Dunia ijipange katika kukabiliana na hali hiyo.

Kwa mujibu wa chapisho hilo dunia imetakiwa kuchukuwa tahadhari kwa kuwa kuna mamilioni ya watu sasa hivi hapa duniani wanakabiliwa na tatizo la njaa, miongoni mwa watu hao kuna zaidi ya watoto milioni 250 wenye umri wa kwenda shule na kati ya hao zaidi ya watoto milioni 10 wanakabiliwa na tatizo la uzito mdogo kutokana na ukosefu wa vitamini kwa sababu ya kula vyakula visivyo na virutubishso.

Chapisho hilo lilizidi kubainisha kwamba inakadiriwa kuwa kila mwaka watu milioni 13 hufa kutokana na njaa au kwa sababu ya kutopata vyakula vyenye virutubisho, na mamilioni ya watoto pia nao hufa kila mwaka kutokana na tatizo hilo.

Pia ilibainika kwamba kati ya watu wanaokadiriwa kufikia zaidi bilioni 6 hapa duniani watu bilioni 1 wanakabiliwa na tatizo la kumiliki ardhi na hata rasilimali. Watu hawa wanaishi kwa dola moja kwa siku.

Hata hivyo inakisiwa na wataalamu hao walioandika chapisho hilo kuwa mpaka kufikia mwaka 2010 kuna uwezekano wa idadi ya watu hapa duniani kufikia bilioni 7 iwapo dunia haitachukuwa tahadhari kupunguza idadi ya watu, kwa maana ya watu kuzaa kwa mpango.

Ni hapo ndipo niliposhikwa na mshangao. Wataalamu hawa wanalamika kuwa watu wanakufa kwa njaa hapa dunianai na hapo hapo wanataka watu wazae kwa mpango ili kuthibiti idadi ya watu isiongezeke!

Wataalamu hao walitoa sababu ya kutaka dunia idhibiti idadi ya watu, walidai kwamba ongezeko la watu huchangia kwa kiasi kikubwa umasikini hapa duniani, kwani kila idadi ya watu inavyozidi kuongezeka na ndivyo uharibifu wa mazingira unavyozidi. Kwani kwa jinsi idadi ya watu inavyozidi hapa duniani na ndivyo mahitaji ya ardhi kwa kilimo na makazi navyoongezeka. Na pale mahitaji ya chakula yanavyozidi kuongeeka na ndivyo uharibifu wa mazingira unavyozidi kuongezeka pia.

Kwa nini ichukuliwe tahadhari ya kupunguza idadi ya watu?

Wataalamu hawa wanadai kwamba Umasikini na njaa unachangia sana watu kuzaana kwa wingi, kwani familia masikini zinategemea watoto kwa ajili ya kulima na shughuli nyingine za nyumbani kama vile kuchota maji na labda kuchunga mifugo kama ipo. Pia familia hizi huchukuwa tahadhari ya kujihakikishia usalama pindi wazazi wakizeeka ili watoto wapate kuwatunza.

Kwa kuwa umasikini unagharimu maisha ya watoto wengi kutokana na kufariki wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano, familia hizi huzaa watoto wengi kwa matumaini kwamba iwapo wapo watakaokufa basi wapo watakaoishi hadi kufikia utu uzima. Kwa hiyo watoto huchukuliwa na familia masikini kama njia ya kujihakikishia usalama.

Wataalamu hao wanashauri kuwa ili kupunguza idadi ya watu hapa duniani, ni vyema kwanza kupunguza umasikini na njaa, kwani hiyo itasaidia watu kuwa na mazingira mazuri ya kiafya na elimu na moja kwa moja idadi ya vifo itapungua, kwa hiyo haitakuwa na haja tena ya mtu kuzaa watoto wengi kama ya tahadhari ya kugawana na vifo.

Wadau naomba kuwasilisha

Baadae nikipata muda nitaandika kuhusu athari za uharibifu wa mazingira kwa mujibu wa chapisho hilo.

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Mmh Koero mchozi unanidondoka kwani niwaonapo hao watoto kama mzazi roho inauma sana nashindwa hata kufikiri. Ngoja labda nikae vizuri kwanza nitarudi

Mzee wa Changamoto said...

VUKANI (Amkeni)

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

aisee sasa sisi huku njaa si tumeizowea na ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku? au

Ansbert Ngurumo said...

Koero, Asante kwa changamoto hii. Tuendelee kuwa pamoja.

Simon Kitururu said...

Mmh!