Saturday, September 19, 2009

HUYU NDIYE KAMALA LUTATINISIBWA

Kamala Lutatinisibwa,
Picha kwa hisani ya Blog ya Kijiwe cha Nyegerage.

Ni kijana wa kutoka kabila la Kihaya, na mzaliwa wa kule Bukoba mkoani Kagera. Alizaliwa miaka 28 iliyopita, tarehe 30 July.

Maisha yake ya udogoni hayakuwa mazuri sana kwani hakuwahi kufurahia upendo wa mama kwani inasemekana baba na mama walitengana mwaka mmoja tu baada ya yeye kuzaliwa akiwa ni mtoto wa mwisho hivyo akalelewa na bibi yake akishirikiana na shangazi zake kadhaa na binamu zake.

Binamu na baadhi ya ndugu alioishi nao kwa upendo na anaowakumbuka ni Jennifer Lukambuzi, Jovian na Elivida Binomutonzi, na dada yake Julieth na kaka yake Japhet ambao walikua pamoja wakicheza na kufurahia maisha ya utotoni. Alibatizwa tarehe 12/12/1982, rasmi bila ridhaa yake na kuwa mkirsto mfuasi wa ulutheri na kupewa jina la James.

Anakiri mwenyewe kuwa mpaka leo hajaweza kuelewa falsafa ya dhehebu hilo wala malengo yake na hivyo alibadili jina na kujiita Kamala Lutatinisibwa, na kubadili falsafa yake kutoka ile ya kimapokeo na kuhamia katika falsafa ya Spiritual yaani kujitambua.

Mwishoni mwa miaka ya 1980 kijana huyu akaanza shule ya awali maarufu kama vidudu au chekechea iliyokuwa ikimilikiwa na kanisa.

Anakiri kwamba hakuwa na mapenzi na shule hiyo ya awali kwani kuna wakati alikuwa akiishia njiani badala ya kwenda shuleni hivyo kuchapwa bakora kwa utoro. Alipokuwa darasa la tatu, alisomeshwa kipaimara na kuanza kula mkate kanisani ambao hujulikana kama kushiriki meza takatifu, ingawa hakuwahi kupenda kula mikate hiyo.

Kuna wakati alipenda mambo ya dini na kutaka kusomea uchungaji lakini baadaye alibadilisha uamuzi wake huo na kuamua kuishi kwa misingi ya falsaya ya Spiritual baada ya kuvutiwa na falsafa ya Budha na Osho.

Mnamo August 1, 1998 akiwa kidato cha pili kijana huyu alimpoteza baba yake mpendwa Omwami Ta Jasson Lutabwasibwa Kamala.

Baada ya kumaliza masomo yake ya Sekondari mnamo mwaka 2004 alihamia rasmi jijini Dar es salaam na kujiunga na vyuo mbalimbali ili kujifunza taaluma tofauti tofauti ambapo mpaka sasa ameweza kuwa mtaalamu wa Kompyuta, ingawa mwenyewe anakiri kuwa haipendi taaluma hiyo bali anapenda uandishi wa habari taaluma ambayo anaiendeleza kupitia kibaraza chake cha kublog akifundisha maarifa ya Utambuzi na stori za hapa na pale ili mradi maisha yanaendelea.

Ni mchangiaji mzuri katika blog za wengine ila msomaji asipokuwa makini anaweza kumuona kama mpotoshaj. Ni mkweli na hafichi kile anachokiamini bila kujali kama utakasirika au utafurahi.

Mara nyingi watu wasioelewa wanaweza kudhani labda ninapolumbana nae ninakuwa niko katika kiwango cha juu cha hasira, la hasha, ni katika kupendezesha mada husika na kuleta changamoto kuhusiana na mada hiyo.

Naomba nikiri kuwa Kamala ni mmoja kati ya wanablog ninaoheshimu sana misimamo yao, pamoja na kuonekana kuwa huwa natofautiana nae, lakini naomba nikiri kuwa sio kwamba nafanya hivyo kwa kuwa simpendi au sipendi misimamo yake. Ukweli ni kwamba napenda na ninaheshimu sana misimamo yake na maoni yake binafsi yawe ni mabaya au ni mazuri.

Hata hivyo naomba nikiri kuwa yapo mengi nimejifunza kutoka kwake na pia naamini kuwa

wasomaji wa blog hizi watakubaliana na mimi kuwa Kamala anao mchango mkubwa sana juu ya uwepo wa blog zetu kutokana na kutia hamasa kila achangiapo mada.

Naomba niishie hapa nisije nikatia chumvi sana na mchuzi ukachachuka.

Huyu ndiye Kamala Lutatinisibwa Omwami Ta Jasson Lutabwasibwa.

Bofya hapa kumsoma zaidi

22 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Koero hapa safi sana. Kamala anastahili haya yote uliyoyaandika ni kweli Kamala usipomzoea unaweza kulia na kusema huyu mtu vupi?
Lakini ukisha mzoea ni kweli Kamala ni mkweli na analeta changamoto sana katika blog zetu analepembesha mijadala.
Anasema kila kionekananacho na ni tabia nzuri nadhani wengi tunaogopa kusema ukweli ndo maana tunaona kama Kamala anadharua watu wengine LA HASHA ni kwamba ukweli unauma.

Kamala nona sasa tunazidi kukufahamu asante sana Da mdogo K. kazi nzuri sana.

Ramson said...

Dada Koero, inaonekana umeamua kutuwekea wasifu wa wanablog wetu, maana ulianza na dada Yasinta na sasa ni Kamala, naona uko makini na mambo ya Jinsia yaani hubagui...Hongera sana kwa hilo. nakumbuka Kamala alikushauri uandike wasifu wa Markus Mpangala Mzee wa Nyasa, lakini ukaona ni vyema ukaanza na yeye mwenyewe.

naomba nikiri kwamba mimi Nilikuwa simfahamu Kamala, ingawa alikuwa ni mwanafunzi mwenzangu pale katika madarasa yetu ya Utambuzi Kimara Rombo, nadhani anakumbuka wakati ule hayati Mwalimu wetu Munga alipokuwa akitujaza maarifa haya ya utambuzi kabla sijatimkia kusikijulikana. Ukweli ni kwamba sikubahatika kuupata wasifu wake kama huu uliotuwekea hapa leo, nashukuru kuwa sasa naweza kusema kuwa namfahamu Kamala tofauti na zamani.

Kuna sifa moja au mbili ambazo umezisahau ambazo mimi nazifahamu, kwanza ni ile ya kutokula Nyama, huyu bwana hapendi kabisa nyama, na sifa nyingine ni ile ya kupenda Meditation, huwa anapnda sana kufanya meditation.
Nimeona niziseme hizi sifa ili wasomaji wengine wafahamu, hasa dada Yasinta maana huyu bwana atakuwa amgeni wako, kwa hiyo kama huna matembele na michicha huko, basi iko kazi labda kama utamtengenezea mikate na asali....LOL

Haya dada yangu tunasubiri sasa wasifu wa mzee wa changamoto...LOL

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante Ramson! ni kweli ni vema nijiandaa ila matembele huku hakuna. Atakula spenachi, mchicha na mboga mabogo nilipanda na nimeweka akiba Karibu sana Kamala.

Unknown said...

Duh! sikujua kumbe Kamala alitamani kuwa Mchungaji, ina maan kama asingeshtuka saa hizi angekuwa anakemea MAPEPO.....kwa jina la Yesu Tokaaaaaaa....LOL..

Ahsante dada Koero kwa kupatia wasifu huu wa mwanablog mwenzetu, kwa kweli yapo mengi binafsi nilikuwa siyafahamu hamuhusuyo rafiki yangu huyu Kamala.

Dada Yasinta Ugeni huo unao,panda tu hizo spinachi na maboga jamaa atakula tu, labda kama atakuja hapa na kutuambia vinginevyo.

Nami naungana na kaka Ramson, nangojea wasifu wa mzee wa changamoto na Markus Mapangala....LOL

Mwanasosholojia said...

Ahsante dada Koero kwa kupanua wigo wa kufahamu wasifu wa wanajamii wetu...Kamala ni chachu miongoni mwa wanablogu, chachu ina raha yake na karaha zake hususani kwa anayeionja kwa mara ya kwanza...tuendeleze libeneke!

Mzee wa Changamoto said...

Nishabadili kwenye wasifu wangu nimeweka COPYRIGHT. Yaani ni mimi tu ninayeruhusiwa "kuwadanganya" kuhusu wasifu wangu. Lol
Nadhani tutaanza na wa Ramson kisha wa Mzee wa Utambuzi then Mwanasosholojia halafu Koero mwenyewe kisha mwana Lundunyasa na hapo ntakuwa nimeshapata "sifa" moja mbili za kuwekwa bloguni.
Lol
Asante Da'Mdogo

Mzee wa Changamoto said...

Nilisahau kuuliza. Sijasoma kuhusu LUBISI ina maana Kamala hapati hiyo kitu kabisa? Yaani kabla hajaamua "kujitambua" hakuwa akimung'unya hiyo kinywaji ya asili? ipi "akakonyagi"?
Anyway. Nasubiri wa Ramson

Ramson said...

Mzee wa changamoto, kwa bahati mbaya sana wasifu wangu haupatikani popote, kwani nilitokomea kusikojulikana siku nyingi na hata rafiki yangu Kamala ukimuuliza leo hii sidhani kama atanikumbuka ingawa mimi namkumbuka sana, hata hivyo nampa changamoto Dada Koero au hata Kamala mwenyewe, kama anaujua wasifu wangu, basi auweke kibarazani watu wanifahamu, kwani itakuwa ni vyema isiishie kuandikwa wasifu wa wanablog pekee, bali pia hata wasomaji na wachangiaji wa blog hizi wakiwekwa wasifu wao vibarazani mwenu, mtu kama Nuru Shaabani, rafiki yangu huyu ingekuwa ni vyema tukapata wasifu wake au rafiki yangu Chacha Wambura wa kule Musoma na yeye tukipata wasifu wake....bila kumsahau Mzee wa Changamoto pia.....Dada Koero kazi kwako...umelianzisha mwenyewe...LOL

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

haya., naendelea vizuri na maandalizi ya safari yangu ya kwa dada yasinta.

Ramson sikukumbuki wala nini lakini nakuhakikishia nitaupata wasifu wako na kuutundika au kumtumia dada koero. juu ya kula nyama na Meditation, umesema vyema

mzee wa c/moto lubisi???
kuna makala moja nilipokuwa migombani mwezi mei nililiongelea hilo. pekua kijiweni utaona na kupata jibu.

vinginevyo sina la kusema, nakaa kimya ili nizuie mimi mdogo 'ego' asichukue nafasi yangu ila nadhani ni ubunifu wa nguvu wa kumfanya mtu ajue asichokijua kuhusu yeye.

asante Koero binti

Ramson said...

Kamala nitashukuru sana iwapo utaupata wasifu wangu na kumpa dada Koero autundike hapa jamvini. kwani huenda ukawashangaza wengi....

Mzee wa changamoto usimtishe Da Koero na COPYRIGHT, Tunataka wasifu wa kila mtu uwekwe hapa ili tujuane, tena nimekumbuka, Pia usisahau wasifu wa Mzee wa JIELEWE, CHRISTIAN BWAYA....LOL

Albert Kissima said...

DU!


Dada Koerooooooo!Mimi nadhani ufuate wasifu wa Baba Mtakatifu Simon Kitururu.


DU!

Unknown said...

Bwana Kisima hapo umenena, baada ya wasifu wa Kamala, ufuate wasifu wa Ambiere Simon Mkodo Kitururu...
Tunaungoja kwa hamu sana....LOL

mumyhery said...

ha ha ha ha!!!!

Albert Kissima said...

Kaka Kaluse, naona umeshaanza kuuandika,
kumbe jina lake kamili ndilo hilo?


DUH!

Ramson said...

Eheee!! Nilisahau, Dada Koero usisahau wasifu wa Mummyhery na wa dada Schola Mbipa wa kibaraza cha Passion4Fasion......naamini patakuwa hapatoshi hapa kibarazani kwako.......LOL

Koero Mkundi said...

Jamani nimerudi, samahani nilikuwa safarini nje ya nchi kwa maswala ya kitabibu, na nimerudi jana usiku salama salimini na afya yangu imetengemaa sasa.

Kusema kweli sikupata fursa ya kupitia mtandao, nilikuwa na ratiba ngumu ajabau lakini leo asubuhi nimepitia maoani na mitazamo yenu, kwa kweli nimefarijika sana.

napenda nichukue fursa hii kumshukuru Rafiki yangu KAMALA, Mbunge Mtarajiwa, Msishangae ndugu zanguni hebu someni pale kwa kaka Maggid Mjengwa, na ndio mtaamini maneno yangu.

Kamala ndiye aliyefanikisha kupatikana kwa wasifu huu kupitia kibarazani kwake, lilikuwa ni swala la utundu tu katika kusherehesha kile alichowahi kutujuza kuhusu yeye, namshukuru sana, Pia ningependa kuwashukuru wachangiaji wote waliojitokeza kutoa maoni yao na mitazamo yao humu. Kwa wale waliotoa maombi ya kutaka kuandikwa kwa nyasifu za wanablog wengine kama vile wasifu wa Kaka Simon Mkodo Kitururu, Mzeee wa Changamoto, Kaka Kaluse Mzee wa Utambuzi, Kaka Bwaya, Kaka Markus Mpangala, Dada yangu, Schola Mbipa na dada yangu mwingine Mammyherry.....nawaomba mvute Subira, nitawawekea nyasifu zao na kila kitu kitajulikana kuhusu wao....LOL

Kwa wale waliotaka niweke nyasifu za kaka Ramson na Kaka Chacha Wambura wa kule Kinayantira Musoma, naomba munisamehe, kusema kweli sizifahamu nyasifu zao labda kama watanitumia ili niziweke hapa, nafasi iko wazi.

naomba ushirikianao wenu ili kufanikisha shughuli hii.....AHSANTENI SANA....

Sisulu said...

naona mkutano wa wana blog umeanza tayari!

Simon Kitururu said...

MmmmH!

Minatoka nje na kupendekeza pia tuwekewe wasifu wa Miungu ya Kitanzania a.k.a Mrungu kwa Wapare , e.t.c

Maana wasifu wa Mungu huyu wa mapoke bado unanichanganya laba kwa sababu sijui kwa undani Miungu ya kabla ya GOD na Allah ilikuwa inaletaje za kuleta:-(

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Kamala Lutatinisibwa Omwami Ta Jasson Lutabwasibwa - ni mmoja kati ya watu wachache ambao hawasiti kuita "spade a spade". Kwa vile wengi wetu tumezoea kupakana/kupakwa mafuta mgongo wa chupa, tabia hii akivu ya Kamala Lutatinisibwa Omwami Ta Jasson Lutabwasibwa kidogo inatushangaza na wengine wanakwazika. Mimi mwenyewe ni lazima nikiri kwamba ilinichukua muda kidogo kumtambua Kamala. Na sasa naweza kusema ni rafiki yangu ingawa bado tunagongana katika mijadala hapa na pale. Lakini kwa sisi tulio katika taaluma tunaamini kwamba mijadala-kinzani ndiyo hasa inayosukuma mbele maarifa. Na ukimsikiliza vizuri Kamala utaelewa anachokisema hata kama ikiwa ni lazima uende maktabani na kupekua upya vitabu vya kifalsafa na kisaikolojia ili hatimaye uweze kufikia majumuisho (generalizations) chanya.

Tuendeleeni kuelimishana na kuipigania jamii yetu. Mimi mwenyewe nadhani nimebadilika (kwa wema) tangu nianze kublogu - na hili ni jambo jema. Na kwa sasa nawaona wanablogu wote kama ndugu. Ndiyo maana siku nikienda kwenye mkutano Uswisi sitakuwa na shida ya kukaa hotelini kama mkutano utakuwa unafanyikia karibu na aliko Mwanafalsafa Kitururu au Dada Yasinta. Nina marafiki duniani kote!

Kamala Lutatinisibwa Omwami Ta Jasson Lutabwasibwa - wewe usibadili msimamo wako. Tunakuhitaji katika dunia ya blogu hivyo hivyo ulivyo!

Si vibaya dada Koero akiendelea kutuletea wasifu wa wanablogu mbalimbali.

MARKUS MPANGALA said...

Waam, hiki sio kma wala kioja ni ukweli mtupu.. Lol.... nipo sana tena saaaannnaa. Lakini naona hapo dada Keoro kanisema mimi.......samahani najihisi tu lakini kweli nina tabia mbaya siku hizi hata kaka Kaluse alisema bwana vipi usiache kutoa maoni.... mmmmh pale Kamala anawsifu kwa kutoa maoni katika blogu zetu.... hongera ila kweli ngoja nijisahihishe jamani lakini shule jamani shule shule....
Wasifu wa mzee wa nyasa?? Mi nimekubali sana wasifu wa Kamala manake naona salamu yake ya kwanza kwangu ilikuwa Haloo Maggid Mjengwa ni ndugu yako? Heee nikashangaa sana manake swali hilo lilikwisha kuulizwa na mzee wangu Fredy Macha... Lol ikabidi nijisaili je nafanana na Maggid? Lol.....mambo matamu sana haya Koero unatuchangamsha kwayo.

Kamala naona maenyoa ndevu zake katika hii picha manake ile tabia ya kukuna ndevu zake anapotaka kutoa hoja ilinikuna sana Lol..... mchungaji Kamala L, NAKUSALIMIA KAKA UPO????
Nasubiri wasifu wa Mzee wa changamoto bila kujali hakimiliki yake......tena hilo tutakupiga mawe

MARKUS MPANGALA said...

Nilisahau tunaomba wasifu wa Edo Ndaki na mzee wa uskochi kaka Chahali

John Mwaipopo said...

Nzuzulima umenena, tena umeninenea. Koero nakusifu kwa kuweza kusanifu wasifu huu. umetulia. huyu jamaa ni wa pekee. kigeni kwake ni msimamo na kuamini lile analokiamini. Nilimwelewa sana alipochangia-ga kwa yasinta kuhusu kufiwa na mama. kama hukutulia ungedhani anamkashifu yasinta, la hasha. tena nadhani sifa hii ya kusimama kwenya msimamo thabiti ina makandokando ya uongozi vile? sijui.