Tuesday, April 13, 2010

HIVI NAWAZA……AU NAOTA TU….!!!!!!????

Hebu nijipumzishe mie.....

Baba Kwembe?…….Baba Kwembe?……{Anaweka mzigo wa kuni upenuni mwa nyumba, kisha anatembea huku akiwa amejishika kiuno hadi chini ya mti ambapo mumewe alikuwa ameacha redio ikiwa imefunguliwa kwa sauti ya juu, anapunguza sauti na kuwa ya wastani}
Najua utakuwa na njaa mume wangu, lakini chakula kitakuwa tayari hivi punde…..{anaingia jikoni na anaweka chini kikapu kilichokuwa na mboga za majani alichokuwa amekibeba}…. Nimechelewa kidogo kurudi tangu uliponiacha shambani kwa sababu nilikuwa nakutafutia uyoga wako….si uliniambia kuwa leo una hamu na uyoga pori?………

Mwenzio leo nusura niumwe na nyoka uliponiacha shambani wakati natafuta kuni,..............Si nikaingi kwenye kile kijipori, pale karibu na shamba la mzee Ngabu, ……Hamadi nyoka huyu, tena Swila, kama si kumuwahi kumkata kichwa na panga angeniwahi wallahi…{ Anatoa mboga za majani na uyoga pori ndani ya kikapu na kuweka ndani ya sufuria ili kuosha}……Leo nimechoka ajabu na kesho natakiwa kliniki……si unajua kesho ndio siku yangu ya kwenda Ludewa Mission ili kusubiria siku yangu ya kujifungua…….

mume wangu,...... hivi umekumbuka kweli kupeleka baiskeli kwa fundi, sidhani kama nitaweza kutembea umbali wote ule kilomita tano!!!!.......Sitaweza…..nimechoka mwenzio ndio naingia mwezi wa tisa hivooo….. {anaosha mboga za majani kisha anamalizia kuosha uyoga. Anatoka nje kuchukua kuni huku akiwa amejishika kiuno kutokana na kuelemewa na ukubwa wa tumbo la ujauzito, anachukua kuni na kurejea jikoni na kukoka moto}……Nataka niwahi kupika kabla Kwembe hajarudi shule, maana najua akirudi atakuwa ana njaa ajabu….si unajua leo sikumfungashia viazi vyake vya kula shuleni….

Baba kwembe…. njoo basi huku jikoni uzungumze nami wakati napika……..tena kuna ndizi mbivu hapa waweza kutafuna kutuliza njaa wakati nakupikia mume wangu….. {Anainjika sufuria ya mboga za majani jikoni huku akaiendelea kukatakata nyanya na vitunguu}…..Miguu yangu imevimba ajabu…..hivi nitaweza kweli kutembea kesho kweli…….Basi nilitaka kusahau, wakati narudi njiani nimekutana na mzee Mwalyosi anadai kesho kuna kikao cha kujadili utaratibu wa kugawa pembejeo za kilimo…..kuna mgeni atakuja kutoka wilayani kuja kusikiliza kilio chetu baada ya kupata malalamiko juu ya uuzwaji wa vocha za pembejeo za kilimo kwa bei ya mchoromchoro….

{Anajimiminia togwa kwenye bilauri na kupiga funda kadhaa na kushusha pumzi…..Anaepua mboga baada ya kuiva na kuinjika uyoga jikoni}……Baba Kwembe, njoo basi unywe hata togwa basi kutuliza njaa……

Heeeee! {Anataharuki ghafla}……. Baba Kwembe si tulikubaliana kuwa uache kuvuta misigara yako, sasa huu mtemba hapa ni wa nani…{ Anauchukua ule mtemba na kutoka nao nje}…..Si ulishauriwa na Dakitari kuwa misigara yako itanidhuru mie na mtoto tumboni………hivi uko wapi wewe…. Mbona kama naongea peke yangu….

Mh..mhu..mhu….{inasikika sauti ya mwanaume akikohoa nyuma ya nyumba}…..niko huku narekebisha choo, kimebomoka…..
Njoo kwanza basi unywe togwa utulize njaa……{anareja jikoni na kuketi}

Jamani hii sio sinema, bali nilikuwa nawaza tu………………
TAMTHILIA HII ITAENDELEA.........

4 comments:

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

maisha halisi ya mama wa kitanzania!

nasubiria hiyo sehemu ya pili...

Yasinta Ngonyani said...

maisha haja jamani Koero usichelewa na huo mwendelezo....

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kawaida tu. hata maiwaifu anafanya

Koero Mkundi said...

Namnukuu Kamala hapa:

"kawaida tu. hata maiwaifu anafanya"

Kamala, laiti kama ungejua huo mwendelezo ukoje, usingethubutu kusema hayo....

Naomba usije ukafuta hayo maandishi maana yatakuumbua wallahi.....

Labda kama unazotabia kama za Baba Kwembe......Kumbuka kwamba hujamjua baba Kwembe ni nani?..LOL