Saturday, April 24, 2010

TAFAKARI YA LEO: TUENDELEE NA SOMO LA IMANI

Kwa kauli tu Yesu aliweza kuukausha Mtini

Tafakari ya leo, ngoja tuendelee na somo la imani.
Hebu tuangalie mfano huu wa imani kwa kusoma katika kitabu cha Matayo 21:18-22, nitanuku,

“Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini aliona njaa. Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara. Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, jinsi gani mtini umenyauka mara? Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia mkiwa na IMANI, msipokuwa na SHAKA, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yoyote mtakayo yaomba katika SALA mkiamini, mtapokea’

Kuna watu ambao, kwa sababu ya kukosa kile ambacho jamii inakiona kuwa ndio ufunguo wa mafanikio, huwa wanaamini kwamba hawawezi kufanikiwa au kufanya vizuri maishani.

Kwa mfano, kwa kukosa elimu, ujuzi au utaalamu fulani, watu wengine hujihesabu kama wanyonge. Huchukulia kwamba ni wale tu wenye elimu, ujuzi na utaalamu fulani ndio wanaoweza au wanaotakiwa kufanikiwa.

Hivi ni nani asiyejua kuwa wale wanaoonekana kuwa wamefaniwa kimaisha na kumiliki ukwasi wa kutosha ni wale ambao hata hawakuwa na uwezo mkubwa darasani?

Hawa waliamini katika kufanikiwa huku wakitia shime katika kile wanachokifanya na wakiamini kuwa watafanikiwa. Sio kwamba watu hao walikuwa hawapati misukosuko, la hasha. Walikuwa wakipata misukosuko na wakati mwingine kurudi chini kabisa na kuanza upya lakini kwao hiyo ilikuwa ni changamotoa ambayo iliwazidishia moyo wa kujituma huku wakiamini kuwa watamudu na hakika kutokana imani waliyokuwa nayo waliweza kumudu na kuwa matajiri wakubwa hapa duniani.

Kama ukisoma habari za wale matajiri ambao utajiri wao umepatikana kwa njia ya halali, huenda ukashangazwa na simulizi zao. Utagundua kuwa juhudi, uvumilivu, subira na imani ndio silaha kuu iliyotumiwa na watu hao kufika hapo walipo.

Kuna wakati niliwahi kusoma kisa kimoja katika blog ya utambuzi na kujitambua ya kaka Kaluse, cha bwana mmoja aitwae Wiliam Mitchel, unaweza kubofya hapa kujikumbusha.

Bwana huyu awali alipata ajali ya pikipiki na kuungua karibu mwili wote, lakini baada ya kupona alirejea kwenye shughuli zake za kibiashara na kama kawaida, lakini katika hali pengine ya kushangaza alipata ajali nyingine ya ndege. Ajali hiyo ilimuacha akiwa na na ulemavu kuanzia kiunoni kwenda chini.

Bwana huyu hakukata tamaa. Alisema anataka kuishi na siyo kuishi tu bali kuishi kwa mafanikio. Alipopona alirudi katika biashara zake kama vile hakukuwa kumetokea jambo lolote baya au la kuvunja nguvu.Aliendelea kufanya biashara huku akiwa na makovu na ulemavu hadi akafanikiwa kuingia kwenye orodha ya mamilionea wa Marekani.Bila shaka umeshawahi kusikia au hata wewe mwenyewe kusema, “si wamesoma bwana, ndio wanaojaaliwa, sisi ambao hatuna shule kazi yetu itakuwa ni kuwatumikia”. Kauli kama hizi zina chimbuko lake mbali sana, pengine katika malezi yetu.

Wazazi walizoea au wamezoea kuwaambia watoto wao “Usiposoma, kazi yako itakuwa ni kuwabebea wenzako mizigo”. Kwa bahati mbaya mtoto aliyelishwa “sumu” hii anaposhindwa shule huamini kwamba yeye atabaki kuwatumikia wengine tu.

Tunapoamini kwamba, kwa sababu hatuna elimu ya kutosha na pengine ujuzi au utaalamu fulani, hatuwezi kufika juu kwenye mafanikio, ni wazi hatutafika.

Moja ya vigezo muhimu vinavyoweza kutufikisha kwenye mafanikio ni kuamini kwetu kwamba tunaweza kufika huko, huku tukitia shime katika kile tunachokifanya kwa wakati huo. Tunapokuwa hatuna imani kwamba tunaweza kufika huko hata kama tufanye kazi usiku kucha bila kupumzika, hatutafika kamwe kwa kuwa tumejifungia njia wenyewe.

Yesu aliposema “Amin, nawaambia mkiwa na IMANI, msipokuwa na SHAKA, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yoyote mtakayo yaomba katika SALA mkiamini, mtapokea”

Hakuwa na maana nyingine bali ni kutuhakikishia kuwa kama tukitenda huku tukiomba na kuamini, hakuna lisilowezekana mbele ya Mungu, haijalishi una elimu au huna, kinachotakiwa ni sisi kutenda na kuamini tu, basi.

Kama kwa kuamini tu inawezekana kuuambia mlima, ung’oke, ukatupwe baharini, na ikawezekana, kwa nini isiwe kwenye kufanikiwa?

Naamini kila mtu anayo nafasi ya kufanikiwa na kupata kile anachokitaka na ambacho kitampa furaha, ni wajibu wake tu kuomba na kuamini.

*Tafakari ya leo kwa msaada wa Blog ya Utambuzi na Kujitambua*

Tukutane Jumamosi ijayo…………….

4 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kauli zetu zina nguvu sana japo sisi tumeegemea kutoa kauli hasi zaidi

hapa Yethu alikausha mti kwa sababu ulikuwa useless, hautoi matunda, kivuli wala majani ya kurutubisha ardhi, kwamba na sisi tujitahidini sana kuzaa matunda, mema

kwa mfano, kusaidiana, kupendena, kutendeana mema nk

tuzae matunda mema, Amina, Asante kwa kaujumbe

Anonymous said...

Koero;
Dini sasa ni biashara kubwa. Huwaoni akina Kakobe na akina Mwakasege walivyotajirika?

Ngoja mimi nikuoe halafu tufungue kanisa letu tuanze kuwatoa watu upepo. Tunaweza kuanza kuuza maji ya mibaraka kwa laki moja kamfuko kadogo. Wewe utakuwa ndiyo mchungaji na mimi nitakuwa mweka hazina.

UNASEMAJE? NIKO SERIOUS PLEASE NIJIBU kupitia mkanzabi2002@yahoo.com

Mzee wa Changamoto said...

Kipengele chako cha TAFAKARI YA LEO ni kati ya vipengele chanya zaidi hapa bloguni. Na hiki cha imani ni zaidi ya ninavyoweza sema.
Kaka Kamala ameongea la maana namna tusemavyo HASI na hili ni dhihirisho kuwa FIKRA huumba.
Linalonifurahisha zaidi ni namna ambavyo umeweza kushirikisha MAKALA NJEEMA SAANA ya kakangu Kaluse katika TAFAKARI.
NAWEKA OMBI KWA BLOGGERS WOOOTE kutumia makala zilizo makini na ambazo bado zina UHAI kwa jamii yetu na kuziunganisha na maisha ya sasa na makala zetu mpya. Haina maana kuandika mambo mapya kila siku iwapo yale tuliyoandika awali na ambayo ni suluhisho kwa jamii hayajatendewa kazi.
NIMEFURAHI SAAANA KUKUSOMA NA PIA KWA USHIRIKIANO WA KI-IMANI KATIKA BLOG.
Blessings

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

bila shaka Mzee wa Changamoto. Ujumbe umifika.

Aksante sana kwa makala hii Da Koero