Wednesday, July 8, 2009

YAKO WAPI MAHITAJI?

Leo nilikuwa napitia blog ya kaka yangu na mwanablog mwenzangu Mubelwa Bandio Mzee wa Changamoto, nikakutana na hii makala ambayo aliiandika hapo mnamo Juni 10, 2009.
Ukweli ni kwamba nimevutiwa sana na makala hii na ndio maana nikaona ni vyema niiweke hapa ili tuweze kuijadili kwa pamoja.

*********************************

Uchaguzi mkuu wa Tanzania unakaribia na kwa hesabu za haraka haraka, natumai vyama husika vimeshaanza kujipanga vema kwa ajili ya "msimu" huo wa kuonesha wanawajali wananchi na wako hapo kuwatetea, kuwahudumia na kuwatengenezea kaisha bora. Yale yale ya MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA. Katika pilika hizi za vyama, nina hakika moja ya hatua inayoendelea sasa ni kuandaa ILANI YA UCHAGUZI kwa kila chama ili kuweza "kuuza" sera zao.Kinachosikitisha sasa ni kuwa wapo waTanzania wengi ambao wana mahitaji mbalimbali muhimu na ambao maisha yao hayawezi kuwa sawa na wengine bila kuwezeshwa kwa namna fulani na ambao wameonekana kusahaulika lakini hawatumii muda huu kuweka mahitaji yao bayana ili yajumuishwe kwenye Ilani hizi.

Nazungumzia wenye mamlaka ya kuwasilisha na kuwakilisha wenye uhitaji ambao ni Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania ( SHIVYAWATA) linaloundwa na vyama mbalimbali ambavyo ni Chama cha Walemavu Tanzania ( CHAWATA), Chama cha Wasioona Tanzania ( TLB), Chama cha Viziwi Tanzania ( CHAVITA), Chama Cha Maalbino Tanzania ( CCMT) na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Akili (TAMH). , na vyama vingine mbalimbali venye kuwatetea wenye uhitaji ambavyo sasa ni wakati muafaka wa kukusanya maoni ya uhitaji toka kwa wanachama wao na kisha kuyaweka bayana kwa kila chama kuwa "wanachama wetu wanahitaji kiongozi ambaye atawajali katika mahitaji (watakayoyataja)" ili wagombea wajue namna ya kuyajumuisha kwenye mipango yao na pia kuweza "kujifunga" kwa jamii katika kutekeleza.

Kuna haki nyingi za msingi na lazima ambazo kwa namna moja ama nyingine wenzetu hawa wanawiwa vigumu kuzipata wanaposhindana na wasio na uhitaji, haki kama shule za kutosha kuwaelimisha, vifaa vya kuwawezesha kuelimika, vifaa vya kuwarahisishia maisha (hata kama ni vya kununua kwa gharama nafuu), maegesho, usafiri, uwezeshwaji wa kufika kwenye ofisi muhimu kwa urahisi (kama ilivyoelezwa HAPA). Natambua kuwa kuna viongozi wa vyama mbalimbali vinavyowakilisha wenye uhitaji mbalimbali, lakini nashangazwa na namna ambavyo hawatumii nafasi hizi kuwabana wagombea, bali wanasubiri mpaka wakati wanapotembelewa na viongozi (baada ya chaguzi) na kusoma risala kueleza matatizo yao ambayo wamekuwa nayo kwa muda mrefu.Ni muda wa kuwafanya wagombea KUELEWA UHITAJI WA WAHITAJI na kisha wajumuishe uhitaji huo katika sera zao ili wanapoingia madarakani wawe na "deni" la kuwatumikia wahitaji.

Lakini wenye mamlakahawafanyi hivyo, matokeo yake wanasiasa wetu wanachukua mwanya wa "kutojua" kujifanya wamesahau uhitaji wa wahitaji na kuanza / kuendelea kutumbua mali ilhali wahitaji wanaendelea kusota na kufa njaa. Ni swali ninaloendelea kujiuliza kuwa YAKO WAPI MAHITAJI YA WAHITAJI? Na ni lini viongozi wetu watayatatua bila "kushurutishwa?" Ni hakika kuwa viongozi wengi HAWANA UPENDO na ndio sababu wanatenda watendayo (kutowajali wahitaji).

Nasio alisema kuwa "them (they're) talking about this, them (they're) talking about that, poor people just a suffer (are suffering) while you live out fat...." " you living in the pride and luxuries, while needier are dying in their poverty. Lord know that they aint got no Love at all"

1 comment:

Mzee wa Changamoto said...

Asante kwa kukumbusha Dada. Nashukuru kwa ushirikiano wako na naamini tutaendelea kushirikiana namna hii.
Pamoja daima