Thursday, June 25, 2009

TAKWIMU HIZI ZINATISHA!!!

Hali huku ni mbaya zaidi

Usiku wa jana nilikuwa nikiangalia kipindi cha Bunge.
Kilichonisisimua ni hoja iliyotolewa na muheshimiwa Zito kabwe mbunge wa Kigoma kupitia tiketi ya Chadema.
Muheshimiwa Zito alitoa hoja hiyo wakati bunge lilipokaa kama Kamati, na kilichonivutia katika hoja yake hiyo ambayo mwenyewe aliita kuwa ni ya kisiasa zaidi ni takwimu kadhaa alizotoa zinazoainisha maeneo mbali mbali ya kijamii hususana kiafya na vifo.

Muheshimiwa Zito Kabwe alisema kwamba, kwa mujibu wa taarifa ya utafiti wa serikali iliyotolewa Novemba mwaka 2008 inaonyesha kwamba idadi ya Watanzania walio masikini iliongezeka kutoka 11 Milioni mwaka 2001 hadi 12.7 Milioni mwaka 2005na kwamba asilimia 75 ya watu hao masikini wanaishi vijijini.

Akiendelea kutoa hoja zake Muheshimiwa Zito alibainisha kwamba idadi ya watoto wanaokufa kwa mwaka inazidi kuongezeka na sasa kila mwaka watoto 800,000 ambayo ni sawa na idadi ya wakazi wa mkoa wa Lindi wanakufa.

Cha kusikitisha zaidi ni hili la wanawake 578 kati ya 100,000 wanaoenda kujifungua hupoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi.
Takwimu hizo zinabainisha kuwa kila baada ya dakika 60 Tanzania inapoteza mwanamke mmoja

Kwa kweli Takwimu hizi zinatisha, na sina uhakika kama kuna hatua zozote zilizoainishwa katika takwimu hizo japo kuonesha hatua zinazochukuliwa ili kupunguza au kuondoa tatizo hilo la njaa na vifo.

Wakati tulipokuwa tunaombwa kura tulibembelezwa sana na tuliahidiwa kuwa tutakuwa na maisha bora na ajira lukuki, lakini hata baada ya miaka takribani minne sasa hali inazidi kuwa mbaya kila uchao, na pengo kati ya matajiri na masikini linazidi kupanuka.

Kwa sasa niko Arusha, na mara nyingi nakuwa Karatu, kwa kweli hali ni mbaya na hasa baada ya uchumi wa dunia kuporomoka wakazi wa eneo hili wanakabiliwa na hali mbaya kutokana na kupungua kwa watalii.

Maeneo mengi ya hapa nchini yanakabiliwa na njaa na wananchi hawana hela kabisa.
Najua Mwakani watakuja tena na lugha tamu na vijizawadi wakitaka tuwape ridhaa ya kuendelea kutuogoza na kutokana na ufinyu wa uelewa hasa kwa watu wa vijijini, khanga na fulana vinatosha kabisa kupata ridhaa ya kuongoza halafu tunabaki tukiteseka kwa miaka mingine mitano………huu ni upuuzi kabisa

4 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

imeandikwa: mtu hataishi kwa mkate tu!

Mzee wa Changamoto said...

Hizi takwimu zinatisha japo sina hakika kama hata hizi zenyewe "hazijang'arishwa" ili zisikutishe. Tunajua kuwa ukusanyaji wa takwimu nyumbani ni wa hovyo hasa katika majanga na vitu kama maradhi na kifo. Sitashangaa kama idadi ya wanaoandikishwa ni nusu ya wanaofariki na hivyo kumaanisha kuwa idadi ya wafao ni mara mbili ya namba hizi. Ni nani anayeweza kuamini takwimu wanazopewa hawa viongozi ikiwa Mhe Rais alipewa takwimu za mwaka 1996 kama ilivyowahi kuripotiwa na Kaka Lukwangule hapa (http://lukwangule.blogspot.com/2008/12/i-am-back-kutoka-vijijini.html). Labda nikukaribishe na wewe Dadangu kwenye ulimwengu wa maudhi na kadhia kama nilivyomkaribisha Kaka Lukwangule baada ya post yake hiyo (Ingia http://changamotoyetu.blogspot.com/2008/12/welcome-back-lukwangule-welcome-to.html)
Haya tuyaonayo hapa ni upuuzi mkubwa kama ulivyosema lakini tukataka kumsaka mpuuzi tunaweza kujikuta kuwa sisi ndio wapuuzi zaidi ambao tunawaweza hawa wasio na fadhila kwenye nafasi ya kuendelea kutunyonya na ndio maana niliwahi kuandika kuhusu mzunguko kamili wa ujinga na namna tunavyouendeleza ale niliposema UJINGA 360 DEGREES, NI KAMA HADITHI YA KUKU NA YAI (http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/06/ujinga-360-degrees.html)
POLE SANA DADA

Yasinta Ngonyani said...

Hii mada ni ngumu kwangu kwa hiyo sina cha kuchangia ila nipo nawe.

Bennet said...

Hali ya nchi ni mbaya sana, kwa sisi tunaotembelea sana maeneo ya vijijini ndio tunaojionea hali hii maana umasikini ndio unaongezeka na hii inasababisha wana vijiji kuharibu mazingira kwa kukata miti na kuchoma mkaa ili angalau wapunguze makali ya maisha