Niko Arusha kwa shughuli maalum ya kifamilia na Jumapili iliyopita nilikwenda kumtembelea rafiki yangu mpendwa Doreen niliyesoma nae huko Morogoro.
Doreen ni mwenyeji wa hapa hapa Arusha na anaishi na wazazi wake maeneo ya Unga Limited.
Niliamua kutumia usafiri wa daladala maarufu kama Vifodi, hapa Arusha kama vile na kule Nairobi nchini Kenya wanavyoita usafiri wao wa daladala matatuu.
Sikubeba simu, pochi wala sikuvaa saa niliepuka kubeba vitu vya thamani ambavyo vingewavutia vibaka.
Kwa wale msioujua mji wa Arusha na Vitongoji vyake, Unga Limited ni eneo hatari sana kwa Vibaka na wahuni hapa Arusha, huwezi kulitofautisha eneo hilo na eneo la Manzese pale jijini Dar Es Salaam au inawezekana Manzese ikawa na afadhali, au eneo la Kariobangi kwa kule Nairobi.
Niliondoka nyumbani kwa mjomba angu maeneo ya Njiro majira ya saa nne asubuhi kwa kuwa nilikuwa naenda eneo ambalo linasifika kwa uhalifu niliamua kuvaa mavazi ambayo hayatawavutia vibaka. Nilivaa Suruale yangu ya Jinz na jaketi, halafu nikavaa Kofia ya cap maarufu kama Kapelo na kisha nikavaa miwani yangu ya jua.
Kwa haraka haraka ukiniona utajua kabisa kuwa mimi ni mmojawapo wa wale wasichana walishindikana, yaani nilionekana kama muhuni fulani hivi na mvuta bhangi…
Hata Mjomba angu aliponiona alinishangaa sana, hata hivyo nilimjulisha madhumuni yangu ya kuvaa vile.
Unajua wakati mwingine unatakiwa uwe mjanja, unapoenda maeneo kama ya unga limited au maeneo mengine yanayofanana na hayo popote pale inabidi ujiweke katika mazingira ambayo hayatakutofautisha na wenyeji.
Nilifika stendi ya vifodi na kupanda basi la kuelekea mjini, maeneo ya stendi kuu, kwa hapa Arusha eneo ambalo huitwa mjini na ambalo ndipo vifodi vingi vinapogeuzia ni stendi, ambapo ndipo unapopatikana usafiri wa kwenda popote pale.
Nilifika Stendi na kupanda vifodi vya kwenda Unga Limited. Kama ilivyokuwa Dar, hata hapa Arusha abiria ni wa kugombea wakati mwingine ingawa pia nilikuta kuna utaratibu wa kupakia kwa zamu, lakini kuna wengine wanavunja huo utaratibu na hivyo kusababisha vurugu na fujo zisizo na msingi.
Nilipanda na kuchagua siti ya dirishani ili niweze kuyaona maeneo ya Unga Limited vizuri kwani ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kwenda huko.
Mwenyeji wangu aliniambia nishuke kituo cha soko mapunda kwani ana duka lake la biashara maeneo hayo na alinipa jina la hilo duka lake ambalo ni maarufu pale soko mapunda, nilimwambia Kondakta mapema kituo ninachoshuka kwani sikutaka kupitishwa kituo halafu nipotee. Kifodi chetu kilipojaa tuliondoka na ili kuhakikisha kuwa sipitishwi nilikuwa namkumbusha mara kwa mara mpaka mama mmoja alikaa jirani yangu ambaye kwa muonekano alionekana kuwa ni mbulu akanitoa wasiwasi kuwa tukifika kituo ninachoshuka atanijulisha, kuanzia hapo tukaanzisha mazungumzo nikawa namdadisi dadisi hili na lile kuhusu eneo hilo la Unga Limited.
Tulipofika eneo hilo la Soko Mapunda mwenyeji wangu huyo wa kwenye Kifodi akaniambia nishuke baada ya kumwambia Kondakta anishushe.
Nilishuka kituoni kisha nikasimama kwa nukta kadhaa nikiangaza macho yangu huku na kule ili niweze kusoma mazingira Nikavuta hatua kadhaa kuelekea kwenye duka moja mbapo nje walikaa vijana kadhaa huku wakila yale majani maarufu kama Mirungi ambayo serikali imeyapiga marufuku.
Hata hivyo la kushangaza ndugu msomaji ni kwamba hapa Arusha watu wamekuwa wakitafuna majani haya hadharani na huku askari polisi wetu wakitazama tu, kwa Arusha na Moshi Mirungi ndio ulevi maarufu wanaotumia vijana wengi.
Niliamua kuwafuata wale vijana ili niwaulize kwa mwenyeji wangu. Nilipofika pale kwa lafudhi ya kuiga ya Kiarusha nikawawasalimia “Niaje machalii wangu” wote wakanijibu kwa pamoja “powa tu sister, mambo vipi” nami nikawajibu “Powa tu”
“Mbona mnasaga bila hata soda” niliwauliza, kwa utani, kwa kawaida walaji wa mirungi hawasemi kula mirungi bali husema kusaga mirungi au kusaga mbaga, Mirungi ina majina mengi sana, mengine hata siyafahamu.
“Duh! Sister hatuna chapaa (Pesa) tunaomba ututoe hata soda moja moja basi”
Alijibu mmoja wao, nikachomoa elfu mbili mfukoni nikawapa, walifurahi sana.
“Sasa Sister karibu tusage basi” alinikaribisha kijana mwingine niliyekuja kumfahamu baadae kuwa anaitwa Saiboko.
“Kwa leo sijisikii kusaga kabisa” nilimjibu.
Nilitumia muda huo kumuulizia mwenyeji wangu ambapo Saiboko alimuita kijana mmoja kwa jina la Nyoka aliyekuwa akicheza hapo jirani na dukani walipokaa na kumwambia anipeleke kwa mwenyeji wangu.
Kwa hapa Arusha, wale vijana wadogo wadogo huitwa nyoka, jina ambalo hutumika sana kule Mererani kuwatambulisha wale watoto wadogo wanaotumishwa kule katika migodi ya Tanzanite.
Yule mtoto alinipeleka mpaka kwa mwenyeji wangu, ambapo nilipokelewa kwa shangwe na mwenyeji wangu huyo.
Tulipoteana na Doreen kwa takribani miaka mitano tangu tulipoachana kule Morogoro baada ya kuhama na kurudi jijini Dar kuendelea na kidato cha sita, kwani mazingira ya pale shuleni Morogoro sikuyapenda kutokana na matatizo ya kiafya niliyokumbana nayo.
Mwenyeji wangu alifurahi sana kukutana na mimi, kwake yeye aliona kama ndoto, kwani nilipomtumia ujumbe wa simu ya mkononi kuwa nitakuwa mgeni wake alishangaa sana na hakuamini kabisa. Tulitumia muda huo kujibizana kwa ujumbe wa simu kwa kupeana michapo na kukumbushana mambo ya shuleni wakati huo.
Baaada ya kumaliza kidato cha sita Doreen hakubahatika kuendelea na chuo kikuu na ndipo alipoamua kuwa mjasiriamali akafungua duka lake kubwa akiuza bidhaa mbali mbali, pia alinijulisha kuwa ana vibanda viwili pale stendi kuu ambapo ameajiri wasichana wawili wanamuuzia, na pia analo duka la stationary jirani na shule ya msingi ya Naura.
Wakati tunaendelea kupeana michapo ya enzi hizo mara akaja msichana mmoja aliyeonekana kuwa dhaifu akiwa amembeba mtoto mdogo ambaye naye alionekana kuwa dhaifu vile vile, alipofika pale aliniomba hela ili akale, mwenyeji wangu alimfukuza kwa madai kuwa ananisumbua, nilimzuia asimfukuze, kwani nilitaka kuzungumza nae.
“Nawe Koero hujaacha tabia yako ya umama Theresa, achana nae huyo kazi kusumbua watu kwa kuomba omba tu hapa” aliniambia Doreen akinikataza nisiongee na yule binti.
Wakati nilipokuwa nikisoma Morogoro wanafunzi wenzangu walikuwa wakiniita mama Theresa, kutokana na tabia yangu ya kupenda kusaidia watu.
Nakumbuka siku moja tulikuwa tumeenda mjini siku ya Jumamosi mimi nilikwenda kanisani na wenzangu walikuwa wameenda kufanya manunuzi mbalimbali, tukakubaliana nikitoka kanisani tukutane stendi. Nilipotoka kanisani nikawafuata pale stendi nikawakuta wamekaa kwenye duka moja wakinywa soda, nilipofika niliungana nao nami nikaagiza soda yangu.
Tulipomaliza kunywa soda zetu kabla hatujaondoka kwenda kupanda basi nikakumbuka kuwa kuna dawa sijanunua, ikabidi niwaombe wenzangu wanisindikize kwenye duka la dawa lililokuwepo pale jirani nikanunue dawa zangu.
Tulipofia pale dukani, wakati nanunua dawa akaingia kaka mmoja alikuwa akitetemeka sana na alikuwa akionekana kuwa ni mgonjwa, ilibidi nimpishe kwanza anunue dawa kwani alionekana kuwa anaumwa hasa.
Alitoa cheti chake cha hospitalini kilichoandikwa dawa na kumpa yule muuzaji. Muuzaji alikiangalia kile cheti kisha akachukua Calculator na kupiga hesabu, kisha akamwambia yule mgonjwa kuwa dawa zake zitamgharimu shilingi elfu saba jumla, Yule kijana alikaa kimya, wote tukawa tunamuangalia tukisubiri atoe hela ili ahudumiwe ili na sisi tuhudumiwe, mara akaingiza mkono mfukoni na kutoa shilingi mia akamwambia muuzaji ampe panado, yule muuzaji akamwambia kuwa kwenye kile cheti hapakuandikwa panado, lakini yule kijana alisisitiza apewe panado kwanza na hizo dawa nyingine atakuja kununua siku nyingine.
Wote pale tulishikwa na butwaa ikiwa ni pamoja na yule muuzaji, lakini kama vile yule kijana alikuwa amesoma mawazo yetu, akamwambia yule muuzaji kuwa hana pesa kwa wakati ule na ndio sababu anataka apate japo panado kwanza za kupunguza maumivu halafu dawa atanunua siku nyingine akipata hela.
Nilijitolea na kumnunulia zile dawa na kuwaacha wanafunzi wenzangu na hata yule muuzaji vinywa wazi, sikushangaa sana kwani ni vigumu sana mwanafunzi kutoa kiasi kikubwa cha pesa vile kumsaidia mtu asiyemfahamu, ni ajabu eeh!
Yule kijana alinishukuru kweli nusura anilambe miguu, na alitaka kujua ninapoishi, lakini nikamwambia kuwa asijali na anione kama msamaria mwema yule aliyezungumziwa katika biblia.
Basi kuanzia siku hiyo wanafunzi wenzangu wakawa wananiita Mama Theresa, eti wakinifananisha na yule hayati mama Theresa wa Calcutta, sifa ambayo siistahili na wala siwezi kuifikia hata theluthi yake.
Sizungumzi habari hii ili kujisifu, bali nimekumbuka, baada ya Doreen kuniita hilo jina la Mama Theresa na ndipo nikakumbuka chanzo cha mimi kuitwa jina hilo.
Tuachane na habari za Morogoro, turejee Unga Limited kwa Doreen, basi nikampa yule binti kiasi cha hela ili akanunue maziwa fresh kwanza kwenye kibanda cha jirani ili mtoto anywe kwanza kwani alionekana kuwa na utapiamlo, kutokana na kukosa vyakula vyenye virurubisho na nywele za mtoto yule zilikuwa zimenyonyoka, sijui alikuwa na safura, (Mungu aepushie mbali)
Nilimchukua yule mtoto nakumpakata ili yule binti akanunue maziwa, wakati huo Doreen alikuwa ndani dukani kwake akihudumia wateja.
Yule binti ambaye alikuja kuniambia jina lake kuwa anaitwa Anita hakukawia alirudi akiwa na maziwa ya moto, niliyachukuwa na kisha nikampa kiasi kingine cha hela ili na yeye akapate chakula wakati namywesha mwanae maziwa.
Nilimuuliza jina la mtoto wake akaniambia kuwa anaitwa Elias, na alinijulisha kuwa ana umri wa miaka mitatu, ingawa alionekana kuwa na umri wa labda mwaka mmoja kutokana na kuwa nyondenyonde.
Nilimnywesha yule mtoto maziwa na kwa kuwa alikuwa na njaa aliyanywa kwa fujo na kuyamaliza, wakati wote namnywesha Eliasi maziwa, Doreen alikuwa akinitazama kwa mshangao.
“Hivi Koero ukiachiwa huyo mtoto utampeleka wapi?” Aliniuliza Doreen.
“Si namchukuwa na kuishi nae kwani kuna tatizo gani, si mtoto kama walivyo watoto wengine?” Nilimjibu.
Doreen alinijulisha kuwa yule binti anaishi ghetto na changu doa mmoja na kamfanya kama house girl wake na mlinzi wa chumba chake wakati akienda kwenye mishe mishe (Pilika pilika) zake za kujiuza.
Haikupita muda yule binti alirudi na nilipomdadisi ndipo aliponisimulia mkasa wake.
Anita ni mwenyeji wa Singida, na ni mtoto wa tatu kati ya watoto watano katika familia yao akiwa ndiye wa kwanza kuzaliwa huku akifuatiwa na kaka zake watatu na mdogo wake wa mwisho wa kike.
Alipomaliza darasa la saba alifaulu lakini baba yake alitaka kumuozesha badala ya kumuendeleza kielimu kwa madai kwamba watoto wa kike hawana faida hata wakisomeshwa kwa kuwa ni waolewaji, hivyo atakwenda kuwanufaisha familia ya mumewe.
Baada ya kuona baba yake ameshupalia aolewe ilibidi kwa kushirikiana na mama yake aende kushitaki kwa mwenyekiti wa kijiji ambaye kwa kushirikiana na mtendaji kata walimuita baba yake na kumuonya juu ya mpango wake huo na kumshinikiza ampeleke shule mwanae.
Baba yake Anita alikubali kwa shingo upande ikabidi auze ng’ombe zake mbili ili kumuwezesha Anita aende shule.
Alipofika kidato cha pili alijikuta anapata mimba ambayo nayo aliipata katika mazingira ya kutatanisha baada ya kulaghaiwa na mwanafunzi mwenzie waliekuwa wakisoma nae na kujikuta akipata ujauzito, cha kushangaza, yeye alirudishwa nyumbani lakini yule kijana aliachwa aendelee na masomo. Kama kawaida mfumo dume ukachukuwa nafasi yake.
Baada ya kurudishwa nyumbani baba yake alimpiga karibu amuue kama sio majirani kuingilia kati lakini hata hivyo alimfukuza na kumtaka asikanyage pale nyumbani kabisa na siku akikanyaga atamuua.
Anita alikimbilia Singida mjini kwa mama yake mdogo ambaye hakuwa na kazi maalum na kuishi nae hadi alipojifungua.
Hali ya maisha ilimuwia ngumu kwani hakupata masada wowote kutoka kwa mama yake mdogo, na ndipo alipokutana na huyo dada aliyemchukuwa kwa ahadi kuwa atamtafutia kazi huku Arusha, kumbe kazi yenyewe ni ya kulinda nyumba na kufanya kazi za ndani.
Maisha aliyokuwa anaisha ni ya kikatili sana kwani vijana wa kihuni walikuwa wakimuingilia usiku na kumbaka mara kadhaa pindi yule dada akishaondoka na alikuwa hampia hela kwa ajili ya maziwa ya mtoto wala mshahara na ndio sababau akawa anazunguka zunguka kwenye maduka na kwenye mabaa kuomba omba.
Habari ya Anita ni ya kusikitisha sana na nikisema niisimulie yote nitakuchosha. Kwa kifupi nilikubaliana na Anita kuwa nimpe nauli arudi Singida pamoja na mtaji wa biashara ili akirudi kule asikae bila kazi. Tulikubaliana kuwa ajiandae kwa safari Jumatatu asubuhi na ahakikishe hamwambii yule dada anayeishi naye ili kuepuka mpango mzima kuvurugika.
Doreen alizidi kunishangaa na kuonekana kama haamini juu ya kile nilichomuahidi Anita kwani alijua kuwa namdanganya tu binti wa watu. Hata hivyo siku iliyofuata yaani Jumatatu nilikwenda tena Unga Limited na kumkabidhi Anita kiasi cha pesa nilizomuahidi na ili kuhakikisha kuwa habaki pale kwa yule dada nilikodi Taxi na kuongozana naye tukiwa na mwenyeji wangu Doreeen hadi stendi na kumpakia kwenye basi la kwenda Singida na tulimkabidhi Kondakta wa basi lile kuwa ahakikishe kuwa yule binti anafika Singida na asiteremkie njiani.
Nilichukuwa muda huo kumueleimisha Doreen juu ya umuhimu wa kuwasaidia wenye shida.
Ni vyema kutoa misaada kwa wenye shida, pale unapoona kuwa kuna mtu anahitaji msaada na kama uwezo unao.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa safari yangu nilipomtembelea rafiki yangu Doreen, siku ya Jumapili.
Hapo nyuma niliwahi kuandika tatizo la mimba mashuleni, wiki ijayo nikipata nafasi nitalieleza tatizo hili kwa kina na namna tunavyoweza kuliepuka.
{Anita sio jina lake halisi}
KASESELA MBUNGE, DIWANI UKISHINDWA UCHAGUZI JILAUMU MWENYEWE
-
*Mjumbe wa Halmshauri kuu ya chama cha Mapinduzi (CCM) taifa (MNEC) Richard
Kasesela akisisitiza mambo mazuri aliyoyafanya Rais Dkt samia Suluhu Hassan
k...
20 minutes ago
7 comments:
Suala la kuhitaji msaada ni la kila mtu. Naweza kusema mengi kuhusu misaada niliyoweza kupata toka kwa nisiyemjua wakati nikiihitaji zaidi ilinishangaza hata mimi mwenyewe. Labda mfano mmoja ni msaada niliopata toka kwa Dada Renatha Benedicto wakati nilipopata ajali na ambaye mpaka wakati huo sikuwa nikimjua wala yeye kumjua, bado unaendelea kuugusa sana moyo wangu.
Unawekeza Dada. Shukrani yako yaja na itakujia wakati wa uhitaji kama ambavyo umekuwa kwa hao, japo katika kiwango na aina tofauti ya uhitaji.
Asante kwa kuwa ulivyo.
Blessings
Koero hiii habari ni habari ya kusikitisha na habari ya kufurahisha. Kuona jinsi unavyoweza kuwasaidia watu. Naweza nikasema kweli Mungu kakupa kipaji ambacho si wengi wanacho. Nakuomba uwe hivvyo hivyo kama ulivyo ipo siku utaipata thawabu yako. Mungu akubariki sana kwa kujali wenye shida.
Koero kwa nini usiandike kitabu cha simulizi hizi.
Nimerudi tena nilisahau kusema hili:- kuhusu watoto wa kike wasipelekwe shule. Hii ni upuuzi wa bure Kwa sababu gani msichana anapopata mimba yeye tu anafukuzwa shule na yule aliympa anabaki kuendelea na masomo. Hili jambo linanipa kero sana. Najua wazazi wanakata tamaa kutusomesha watoto wa kike kwa mtindo huu. Lakini tukumbuke kuwa mimi sijapata mimba kwa uwezo wa roho mtakatifu. Hapa cha msingi ilibidi wote wafukuzwe au kwa nini kusiwe na shule watu wanaweza kusoma hata wakiwa na mimba. Kwani mimba ni ugonjwa. Na pia kwa nini kusiwe na shule ambayo wasichana baada ya kujifungua wanasoma. Na hapo hapo pawe na chekechea kwa ajili ya watoto wao. Kwa sababu mara nyingi hasa hizi sekondari zisizo za serikali wanawakataa wasichana waliozaa kuendelea na masomo. Kusema kweli sielewi kabisa wanawaza nini. Mimi naenda shuleni kuusoma tena wao wanasema hawanipokei kwa vile nimezaa. Kwani ni kuwa sista. KWA KWELI NINASIKITISHA SANA NA INAKATISHA TAMAA. Lilikuwa hili nilitaka kusema.
msaada na usio msaada. duniani hakuna msaada wa kumsaidi mtu kwani umsaidiapo mtu umejisaidia wewe mwenyewe.!
Hongera Koero dadangu
Endelea hivyo ndugu yangu
Hii ni dunia mwenzangu
Hatujui tuendako mpendwa'ngu
Wote tungekuwa kama Keoro nadhani tungeweza kukwamuana kiuchumi na kuwasaidia wale wasio na uwezo ili wapate kujitegemea
Hongera kwa moyo wako wa huruma kwa jamii Mungu akuzidishie na wale unaowasaidia waweze kuwasaidia na wengine
Post a Comment