Sunday, June 14, 2009

CHANGAMOTO YA MZEE WA CHANGAMOTO

Rais Mstaafu wa Ghana Jerry Rawlings: Alipofanya mapinduzi na kuingia madarakani wengi walimuita Dikteta.

Naomba nikiri kuwa siku hizi nimekuwa mtu wa Kudesa. Hii nayo kanipa kaka Mubelwa Bandio mzee wa Changamoto. Link ya makala hii ameiweka hapa kibarazani akitaka kusherehesha maoni yake katika mada nyingine niliyoidesa kutoka Jamii Forum iliyouliza “Laana yetu ni nini hasa?” nami kutokana na kuvutiwa na mada hii ya mzee wa changamoto nimeona si vibaya nikiiweka hapa kibarazani kwangu ili kupata mtazamo tofauti kutoka kwa wasomaji wa kibaraza hiki


Ninapoangalia namna "tunavyokaririshwa" maana za nani ni nani, na kwanini ni yeye na kwa manufaa ya nani na nani awe rafiki na nani awe adui yake nasikitika sana. Tumepangiwa kila kitu kwa tafsiri ya wenzetu ambayo kwa hakika ni kwa manufaa yao.Mandela alikuwa "mkorofi" ( na dikteta fulani hivi) kwa kudai uhuru ambao baada ya kutambulika sasa anaonekana ni shujaa japo hajabadili alichofanya, Saddam alikuwa shujaa aliposhirikiana na wao kisha akawa dikteta alipopingana nao.
Gadafi aliyekuwa dikteta na kuonekana kama asiyewajali wananchi wake sasa kawa shujaa na "kiongozi safi" kwa kuwaruhusu "wakuu" kuingia na kukagua silaha zake japo hakuna alichobadili kwa wananchi.Luciano aliwahi kuimba kuwa "they're trying to control our minds, and treating us like swine.
They telling us who to love or hate as if they're great"Najua akitokea mtu akalazimisha baadhi ya mambo ya maana kutendeka nyumbani basi ataitwa dikteta (na kwa bahati mbaya nasi tutashabikia hata kama si tafsiri yetu).
Najiuliza akitokea "kiongozi" akalazimisha kusimamishwa kwa mikataba yote ya madini ili ipitiwe upya hataonekana dikteta?
Je atakayelazimisha viongozi wakuu waliosababisha mabilioni ya hasara serikalini wachunguzwe licha ya katiba waliyoshindwa kuitii kutosema hivyo hataonekana dikteta?
Je atakayelazimisha wabunge kujenga ofisi na kutumia muda mwingi majimboni mwao kama walivyoahidi wakati wa kampeni hataonekana dikteta?
Atakayelazimisha utendaji wa mikoa kulingana na rasilimali zake kuwanufaisha wananchi wake na kisha nchi nzima huyo hataonekana dikteta?
Najua kuwa atakayewafikisha viongozi wakuu mahabusu ataitwa dikteta kwa kuwa amekwenda kinyume cha katiba, lakini sijui kwa nini katiba imlinde yule ambaye ameivunja kujilimbikizia mali na kuitia serikali hasara kubwa?
Kama huyu atakayetenda haya niliyosema hapo juu, atakayevunja mikataba ya ujenzi wa miundombinu yenye utata, atakayehakikisha ahadi za wananchi zinatekelezwa na waahidi hasa wabunge, atakayeshurutisha matumizi mazuri ya rasilimali za wananchi kwa manufaa ya sehemu husika, atakayeshinikiza malipo kwa wafanyakazi ambayo mpaka sasa haijajulikana kwanini hawajalipwa ilhali waheshimiwa wanapata pesa zao bila malimbikizo, atakayehakikisha kuwa mkulima wa anapata senti zake zote alizoikopesha serikali na ambazo anatumia pesa nyingi kufuatilia kuliko atakazolipwa, atakayesimamisha ziara za nje na ndani za viongozi (zisizo za lazima) na atakayeamua Tanzania iwe ya manufaa kwa wa Tanzania kwa kutumia kila kilichopo
Tanzania ataitwa DIKTETA, basi namuombea awepo. Aje atufanyie hayo na nadhani tunamhitaji na anaweza kuwa suluhisho la awali kwa yaliyopo.
Maana sasa imekuwa kama alivyosema Kaka Evarist kuwa HAKI IMEKUWA FADHILA na twahitaji atakayeangalia haki na kama haki.
Nionavyo ni kwamba mfumo unaotumika kumpata mtu atayewania uongozi unapita katika ngazi na misaada ambayo mpaka aje kupatikana mgombea anakuwa kashirikisha "wataalamu" wa ufujaji ambao akichukua madaraka hataweza kusema lolote juu yao.
Pengine nionavyo mimi ndilo tatizo, lakini kuna ukweli kuwa tafsiri nyingine zinatufanya tuwachukie wale ambao wanaweza kutuletea mabadiliko ya kweli na badala yake tunaendeleza "kubebana na kufichana" ambako kunaendelea kutuweka tulipo.
Ni Mtazamo wangu tu na naendelea kutunza haki ya kukosea na kukosolewa.

3 comments:

Evarist Chahali said...

Kwa kweli sasa Tanzania inahitaji dikteta wa kupigania wanyonge.

Albert Kissima said...

Mimi nadhani dicteta ni yeyote yule atakayekuwa mzalendo.
Hatujapata viongozi ambao ni wazalendo.
Kila mmoja wetu ni dicteta.
Wakenya walionyesha udicteta kwa kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi na hatimaye Raila Odinga alipata kuwa waziri mkuu,ambapo kulingana na matokeo ya uchaguzi alitakiwa kuwa raisi.

Kila mmoja wetu ni dikteta na udikteta huu tuuonyeshe kwenye uchaguzi wa mwaka kesho.Kabla hata ya matokeo kutangazwa itajulikana tu nani alipewa kura nyingi(hiki ndicho kilichowafanya wakenya waliowengi kutokukubaliana na matokeo)hivyo matokeo yakiwa tofauti itajulikana tu kuwa kulikuwa na hila ktk kuhesabu kura.
Tatizo na sisi wenyewe wananchi hatuna uzalendo.Maneno ya wengi haya hapa "mimi na maisha yangu bwana siasa itanisaidia nini"
"shauri yao, watajua wenyewe na siasa zao"
kwa maneno haya tutaweza kutetea haki zetu za msingi?




Changamoto:
Unafikiri yakitokea machafuko kama ya Kenya na Zimbabwe, sisi tutatatua vipi?
Itawezekana upinzani kuchukua nafasi nyeti ktk top layer ya serikali?

chib said...

Dikteta kwa spidi gavana labda, vinginevyo wabongo mtapukutika